Uteuzi Wa Wagombea Ubunge Katika Jimbo La Liwale Na Udiwani Katika Kata 37
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza tarehe 13 Septemba 2018 kuwa siku ya uteuzi wa wagombea Ubunge katika jimbo la Liwale Mkoani Lindi na tarehe 21 Septemba 2018 kuwa siku ya uteuzi kwa wagombea Udiwani katika kata 37 zilizopo katika Hamashauri ishirini na saba na mikoa kumi na tatu ya Tanzania Bara.
Hata hivyo, baada ya uteuzi huo Tume imepokea malalamiko kupita vyanzo mbalimbali juu ya kutotendewa haki kwa baadhi ya wagombea Udiwani katika baadhi ya maeneo yenye chaguzi hizo.
Tume, imefanya ufuatiliaji na kupokea taarifa za awali kutoka kwa baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi kwenye maeneo yanayolalamikiwa.
Kwa mujibu wa maelezo ya wasimamizi hao wagombea ambao hawakuteuliwa ni kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuwekewa pingamizi, kutorejesha fomu siku ya uteuzi, kujitoa baada ya kuteuliwa na baadhi kutotimiza masharti ya uteuzi ambayo ni ujazaji wa fomu za uteuzi kikamilifu na kutotimiza idadi ya wadhamini inayokubaliwa kisheria.
Maeneo ambayo wagombea wake wamewekewe Pingamizi na wagombea wenzao ni pamoja na kata ya Kibutuka Halmshauri ya wilaya ya Liwale, Kata ya Ruvu Halmashauri ya Wilaya Kibaha, Kata ya Njianne Halmasahuri ya wilaya Mkuranga, Kata ya Jibondo na Kilindoni Mafia na Kata ya Ikwiriri Halmashauri ya Rufiji, ambapo ni Wagombea wa CUF waliowekewa Pingamizi.
Aidha, katika Halmashauri zote ambazo wagombea wa CHADEMA walichukua fomu kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya udiwani hawakurejesha fomu hizo kwa ajili ya uteuzi.
Vile vile, Baadhi ya wagombea mfano Mgombea wa CUF kata ya Ruaruke, Wagombea ACT WAZALENDO na CUF katika kata ya Mailimoja na Mgombea wa ACT WAZALENDO katika kata ya Mbwawa zote kutoka Halmashauri ya Mji wa Kibaha hawakuteuliwa kwa sababu hawakurejesha fomu za uteuzi.
Wengine ambao hawakurejesha fomu ni mgombea wa CUF kata ya Kisiju Halmshauri ya Mkuranga, mgombea wa CUF na mgombea TLP kata ya Mjimwema Halmashauri ya Kigamboni.
Aidha, katika kata ya Kagando wagombea wa CUF,TLP NCCR-MAGEUZI na ACT WAZALENDO na Kata ya Hamugembe Mgombea wa CUF wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba hawakurejesha fomu ili wateuliwe.
Vile vile, katika Halmashauri ya Kakonko kata ya Rugenge mgombea wa CUF hakurejesha fomu na mgombea wa NCCR-MAGEUZI Katika Halmashauri ya Sumbawanga kata ya Ikozi hakurejesha fomu pia.
Katika Halmashauri ya wilaya ya Geita wagombea wa Vyama CCK na ADC hawakurejesha Fomu kwa Msimamizi wa Uchaguzi kata ya Nyankumbu, wakati huo huo wagombea wa CUF na NCCR-MAGEUZI kata ya QURUS hawakurejesha fomu za uteuzi. Wakati katika Halmashauri ya Monduli Mji mgombea wa ACT WAZALENDO hakurejesha Fomu.
Baadhi ya wagombea hawakuteuliwa kwa kuwa hawakujaza fomu za uteuzi kikamilifu ikiwemo kutotimiza idadi ya wadhamini na wengine kutodhaminiwa na Vyama vyao vya Siasa. Mfano; Wagombea wa CUF katika kata za Jibondo na Kilindoni Halmashauri ya wilaya Mafia, wagombea wa CUF na ACT WAZALENDO Kata ya Mabatini Halmashauri ya Nyamagana hawakuteuliwa kutoka na mapungufu haya.
Vile vile, kuna baadhi ya wagombea waliojitoa baada ya uteuzi, hili limejitokeza katika Halmashauri ya Babati mji ambapo mgombea wa CUF kata ya Sigino alijitoa baada ya kurejesha fomu kabla ya muda wa uteuzi kumalizika, na pia Halmashauri ya Geita Mji kata ya Nyankumbu ambapo wagombea wa ACT WAZALENDO na CUF walijitoa pia baada ya kuteuliwa.
Kwa ujumla hiyo ni taarifa ya awali katika zoezi la uteuzi wa wagombea Ubunge na Udiwani katika kata 37 uliofanyika katika maeneo mbalimbali yenye uchaguzi. Katika Uchaguzi huu vyama vya ACT WAZALENDO, CCM, CUF, DP, NCCR –MAGEUZI, NRA na SAU vitashiriki kwa kuwa vimesimamisha wagombea.
Taarifa kamili kuhusu zoezi la uteuzi ikiwemo matokeo ya rufaa itatolewa hapo baada mchakato wote kukmilika.
Imetolewa na,
Mkurugenzi wa Habari na Elimu kwa Umma Tume ya Taifa ya uchaguzi
23 Septemba 2018
Uteuzi Wa Wagombea Ubunge Katika Jimbo La Liwale Na Udiwani Katika Kata 37
Reviewed by RICH VOICE
on
Septemba 24, 2018
Rating:
Hakuna maoni