Wananchi wa Jimbo la Igunga wametakiwa kutumia Zana za kisasa za kilimo ili kuendana na soko la Mazao la kimataifa.




Ushauri huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Igunga Ndugu Nicholaus Ngassa alipokua akizungumza na Wadau wa Kilimo na Wanahabari katika ofisi yake Jimboni hapo.


Aidha Bwana Ngassa aliwaeleza faida za kutumia zana hizo ambazo ni pamoja na kupata mazao mengi pasi na upotevu wakati wa ulimaji na hata uvunaji.


"Tunapotumia Zana hizi tunasaidia kupata mazao mengi kama unavyojua sisi ni wakulima wa awamu nyingi na mazao mbalimbali, tunalima Mahindi, Ufuta, Choroko na hata Mpunga hivyo tutapata kwa wingi na tutainyanyua Igunga", Alisema Bwana Ngassa


Bwana Ngassa alizungumzia kuhusu zana za kilimo zinazotolewa kwa mikopo na Mfuko wa pembejeo wa Taifa yakiwamo matrekta, pawa tila na mitambo ya umwagiliaji na kuwa Igunga wamepata fursa hiyo na wanatakiwa kuifangia kazi.


"Nimezungumza na Ofisi ya Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo na wameahidi kutusaidia kwa kutupa zana kwa mikopo na hata kama una keshi nayo sio mbaya hivyo tuitumie hii fursa wazee wangu", Alieleza Bwana Ngassa


Pia aliwakumbusha hasara za wakulima wanaolima pembezoni mwa vyanzo vya maji hasa katika bwawa la Mwanzugi jambo ambalo linachangia kupungua kwa kina cha bwawa hilo kwa mujibu wa wataalamu wa Halmashauri ya Igunga.


Kwa niaba ya Wananchi na wadau wa kilimo, Bwana Madede alimshukuru Mbunge huyo kwa kasi anayokuja nayo kwa upande wa kilimo maana ndio kazi kubwa ya Wanaigunga walio wengi.


"Tulisubiri siku nyingi kupata Mbunge wa namna hii maana tumeteseka sana, huyu ni kijana wetu ila kasi anayokuja nayo kwenye kilimo nampongeza sana mdogo wangu Ngassa", alisema Madede.


Nae Muwakilishi wa Madiwani wa Viti maalumu Bi Kulwa Kagolo alisema mikopo hii inatija kwa wanawake na watanyanyuka kiuchumi maana wao ndio wakulima wa mashamba madogo madogo.

"Wanawake tunasahaulika sana kwenye swala la kilimo ila kwa mikopo hii tutanufaika sana sababu sie ndo wakulima wa vishamba vyetu vidogo vidogo vya mboga na mahindi",


Igunga ni Wilaya inayoongoza katika kilimo cha Mpunga Mkoani Tabora na pia ni shamba la mbegu za pamba nchini Tanzania.

Wananchi wa Jimbo la Igunga wametakiwa kutumia Zana za kisasa za kilimo ili kuendana na soko la Mazao la kimataifa.  Wananchi wa Jimbo la Igunga wametakiwa kutumia Zana za kisasa za kilimo ili kuendana na soko la Mazao la kimataifa. Reviewed by RICH VOICE on Desemba 12, 2020 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...