Mo Dewji: Visa 10 vya utekaji nyara vilivyoishangaza dunia



Mo DewjiHaki miliki ya pichaAFP/GETTY IMAGES

Kisa cha kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania Mo Dewji kimewashangaza wengi, huku polisi wakiendelea kumtafuta.
Katika historia, vimetekelezwa visa vingi vya kutekwa kwa watu maarufu vilivyoushangaza ulimwengu.
Hapa, tunakusimulia kumi vilivyoshangaza zaidi.

John Paul Getty III

Kisa hiki hukumbukwa na wengi baadhi wakidai ni mfano wa madhara ya mtu kuwa bahili.
Mwaka 1973, wahalifu walimteka mjukuu wa tajiri wa mafuta Jean Paul Getty, kwa jina John Paul Getty III ambaye alikuwa na miaka 16 wakati huo.
Alitekwa akiwa katika jumba la Piazza Farnese jijini Roma, Italia.
Watekaji nyara walidai kikombozi cha $17 milioni ambazo ukilinganisha na utajiri wa babu yake, zilikuwa pesa kidogo.
Lakini mzee huyo mpango wake ulikuwa vingine.
Isitoshe, mjukuu huyo alikuwa mtukutu na mara kadha alikuwa anawatania watu kwamba anaweza hata kujiteka nyara.
Alipopewa ujumbe wa kudai kikombozi, babu yake aliupuuza.
Isitoshe, aliamini kwamba kama angelipa pesa hizo basi angewaweka hatarini jamaa zake wengine kwani watekaji wanyewalenga na kudai fedha. Akaamua hatoi chochote.

Mo DewjiHaki miliki ya pichaAFP
Image captionMo Dewji alitekwa hotelini eneo la Oyster Bay alikokuwa ameenda kwa mazoezi

Watekaji nyara walipoona wataondoka mikono mitupu, waliamua kumtumia ujumbe.
Walimkata mvulana huyo sikio na kuutma kipande chake pamoja na fungu la nywele kwa gazeti moja, na ujumbe kwamba iwapo pesa hazingelipwa, wangekuwa wakikata kipande kila wakati na kutuma hadi walipwe pesa hizo.
Maskini wa watu alilazimika kulipa na mvulana huyo akarejeshwa, lakini tukio hilo liliathiri sana maisha yake.
Kufikia wakati wa kulipa, watekaji walikuwa wamepunguza kikombozi walichodai hadi $3 milioni, ambazo ndizo zilizolipwa.
Babu huyo alilipa $2.2 milioni mwenyewe - kiasi cha juu zaidi ambacho aligundua kwamba angelipa bila kutozwa kodi. Kiasi kilichosalia kikilipwa na mwanawe (babake mtoto).

Ivan Kaspersky

Iwapo unafahamu mambo ya kompyuta na mitandao, basi itakuwa ajabu iwapo jina la Kaspersky haujawahi kulisikia.
Ivan Kaspersky ni mwana wa Eugene Kaspersky tajiri mtengenezaji wa programu za kompyuta na programu za kupambana na virusi vya kompyuta na kupambana pia na wadukuzi.
Mwaka 2011, genge la watekaji nyara lilifanikiwa kumteka mtoto wake aliyekuwa na umri wa miaka 20 wakati huo. Alizuiliwa mjini Moscow na watekaji nyara wakaitisha kikombozi.
Lakini hawakumakinika sana na walifanya makosa yaliyowasaidia wapelelezi kujua walikuwa wanamzuilia wapi.
Polisi walifuatilia mawimbi ya moja ya simu waliyotumia kumpigia babake kijana huyo wakidai kikombozi.
Eugene Kaspersky utajiri wake unakadiriwa na jarida la Forbes kuwa $1.4B, karibia sawa na Mo Dewji. Ana watoto wanne.

Patty Hearst

Patty Hearst ni mjukuu wa tajiri mmiliki wa kampuni ya uchapishaji magazeti William Randolph Hearst.
Umaarufu wake ulimuweka hatarini.

Mo Dewji

Mwaka 1974, akiwa na miaka 19 alipokuwa alishambuliwa, akapigwa hadi akapoteza fahamu na kutekwa kutoka nyumbani kwake California.
Kundi la siasa za mlengo wa kushoto kwa jina SLA, ambalo lilikuwa linaelekezwa na profesa wa Chuo Kikuu cha California, lilidai kuhusika.
Sharti lao lilikuwa kwamba familia ya Hearst itoe chakula cha thamani ya $70 kwa kila familia maskini jimbo la California. Kwa jumla, hizo zingekuwa $400 milioni.
Babaye Patty alichukua mkopo na akapanga kutoa chakula cha thamani ya $2 milioni ambacho kiliangushwa katika eneo la Bay Area kwa ajili ya kutumiwa na jamii maskini.
Hilo halikuwaridhisha watekaji.
Ili kujiokoa, Patty alilazimika mwenyewe kukubali kuwa mwanachama cha SLA na baadaye akashiriki shughuli zao ambapo miongoni mwa mengine walitekeleza wizi.
Alikamatwa mwishowe na kufungwa jela miaka 35 kwa kosa la wizi wa benki.

Walter Kwok

Mwaka 1990, Walter Kwok na ndugu zake wawili walirithi mali ya kampuni tajiri zaidi katika biashara ya ardhi na majumba jijini Hogn Kong Sun Hung Kai Properties pamoja na mali ya baba yao Kwok Tak Seng.
Mara moja, wakawa kwenye orodha ya Forbes ya watu tajiri zaidi duniani.
Wapenda vya bure wakawa wanamezea mate utajiri wao. Mwaka 1997 Kwok alitekwa na jambazi maarufu Cheung Tze-keung, maarufu zaidi kwa jina 'Big Spender'.
Mke wake Kwok, Wendy alifanikiwa kushauriana nao na kufanikisha uhuru wake bila kuwashirikisha polisi.
Ingawa hakukuwa na taarifa yoyote rasmi kuhusu kiasi cha kikombozi kilicholipwa na kumkomboa, Tze-keung alidai kwamba alilipwa $600 milioni kumwachilia Kwok.
Alikamatwa baadaye kwa makosa mbalimbali, na akauawa nchini China 16 Desemba 1998 baada ya kuhukumiwa kifo.

Aldo Moro

Aldo Moro alikuwa mwanasiasa maarufu nchini Italia aliyependwa sana na raia. Alikuwa amehudumu kama Waziri Mkuu kati ya 1963-1968.
Moro alikuwa ndiye waziri mkuu aliyekuwa amehudumu muda mrefu zaidi tangu wakati wa vita vikuu vya dunia.
Lakini umaarufu wake na kupendwa kwake na watu pengine vilimharibia mambo.

Fedha
Image captionFedha

Machi 1978, wanachama wa kundi la wanamgambo wa Red Brigades, waliwaua walinzi wake watano na kumteka kutoka kwenye barabara moja Roma.
Waliitisha kuachiliwa huru kwa wenzao 16 waliokuwa wanazuiliwa na serikali ndipo waruhusu kumwachilia huyu Moro.
Serikali ilikataa.
Alipigwa risasi mara kumi akiwa kwenye gari na kuachwa akiwa marehemu baada ya kuzuiliwa kwa siku 55.

Frank Sinatra Jr

Mwana wa mwanamuziki maarufu Frank Sinatra na mkewe Nancy, Frank alikuwa na miaka 19 alipotekwa 1968.
Kijana huyo alitekwa na wanaume watatu Barry Keenan, Johnny Irwin na Joe Amster, kwenye chumba nambari 417 katika hoteli ya Harrah ufuo wa Ziwa Tahoe.
Babake Frank Sr alilipa kikombozi cha $240,000. Baada ya kuzuiliwa kwa siku mbili, aliachiliwa huru.
Kisa hicho kilizua utata, baadhi wakifikiri pengine mwanamuziki huyo alikuwa anajitafutia njia ya kufufua umaarufu wake, siku hizi utasema pengine alikuwa 'anajitafutia kiki'.
Wahusika, wanaume hao watatu walikamatwa baadaye na kupatikana na hatia, ingawa aliyepanga utekaji nyara huo, Keenan, baadaye alitangazwa kisheria kuwa mwenye akili punguani.

Charles Lindbergh Jr.

Kilikuwa kisa kilichoishangaza na kuisikitisha dunia mwaka 1932.
Charles Lindbergh Jr alikuwa mwana wa rubani maarufu wa ndege Charles Lindbergh ambaye alikuwa pia mwandishi maarufu. Alikuwa anatazamwa na wengi kama 'Shujaa wa Marekani' baada ya kuwa wa kwanza kufanikiwa kuvuka bahari ya Atlantiki akiwa kwenye ndege peke yake.
Mtoto huyo alikuwa na miezi 20 alipotekwa akiwa analala nyumbani kwao New Jersey.
Mtekaji nyara aliacha ujumbe uliokuwa na makosa mengi ya kisarufi, akidai kikombozi cha $50,000, na hata kueleza kikombozi kingelipwa kwa sarafu za thamani gani.
Alitahadharisha pia dhidi ya kutangazwa kwa kisa hicho na kuhusishwa kwa polisi. Taarifa hata hivyo zilienea haraka.
Licha ya hakikisha kwamba mtoto wao angekuwa salama baada ya kikombozi kulipwa, mwili wa mtoto huo ulipatikana vichakani miezi miwili baada yake kutekwa.
Polisi walifanikiwa kumtafuta mtekaji nyara kwa kufuata nambari za usajili za dola zilizotumiwa kulipa kikombozi.
Richard Hauptmann alikamatwa na kupatikana na hatia ya utekaji nyara na mauaji. Aliuawa 1936 kwa umeme.

Kim Kardashian


Kim Kardashian na mumewe Kanye WestHaki miliki ya pichaOTHER
Image captionKim Kardashian na mumewe Kanye West

Hiki zaidi hakikuwa kisa cha utekaji nyara, lakini nyota wa uigizaji wa maisha ya uhalisia kwenye runinga Kim Kardashian alivamiwa na majambazi Oktoba 2016 akiwa jijini Paris.
Waliingia kwenye chumba chake wakiwa wamevalia kama maafisa wa polisi na wakamzuilia kwa muda wakiwa na bunduki.
Alikuwa amelala wakati huo na walimfunga mikono na kumuacha kwenye hodhi la bafu.
Walipora vitu vya thamani alivyokuwa navyo, ambavyo vinakadiriwa kuwa vya thamani ya
$10 milioni.
Katika mahojiano ya baadaye, Kim alieleza alivyowasihi wasimuue, akiwaambia kwamba alikuwa na familia.
Ni kisa kilichomfanya kubadilisha jinsi anavyochapisha picha na maelezo kuhusu safari na maisha yake kwenye mitandao ya kijamii.

George Clooney

Mwigizaji George Clooney alikuwa Darfur, Sudan akiwa na babake akiigiza filamu ya
A Journey to Darfur (Safari ya Darfur) pale kundi la watoto waliokuwa na bunduki aina ya AK47 walipowashambulia.
Walishambuliwa wakivuka kwenye kizuizi cha barabarani.
Genge la vijana lilipora kila kitu kwenye gari lao.
Clooney anasema aliingiwa na wasiwasi sana kutokana na kisa hicho.
Baadaye hata hivyo alifanya mzaha na kusema huenda watoto hao hawakufahamu yeye alikuwa nani.
"Bila shaka huwa hawana televisheni huko," alisema.

Familia ya Jennifer Hudson


Jennifer Hudson akitumbuiza New York Oktoba 11, 2018Haki miliki ya pichaAFP/GETTY
Image captionJennifer Hudson akitumbuiza New York Oktoba 11, 2018

Jennifer Hudson alipata umaarufu aliposhiriki katika kipindi cha American Idol mwaka 2004. Ingawa alimaliza akiwa was aba, nyota huyo alipata umaarufu kutokana na kipaji chake.
Mwaka 2008, alipata pigo kubwa pale mamake wa miaka 57 Darnell, ndugu yake Jason, 29, na binamu yake Julian, 7, walipozuiliwa mateka na kisha kuuawa kwa kupigwa risasi.
Mshambuliaji alikuwa anawafahamu vyema.
William Belfour alikuwa mume wa zamani wa dadake. Alikamatwa na kushtakiwa mauaji na uvamizi na akahkumiwa vifungo vitatu vya maisha na miaka mingine 120.
CHANZO BBC SWAHILI
Hudson na jamaa zake, wakitafuta kitu cha kuwapa matumaini baada ya kisa hicho, walianzisha wakfu wa Hudson-King wa familia za jamaa za watu waliouawa.
Mo Dewji: Visa 10 vya utekaji nyara vilivyoishangaza dunia Mo Dewji: Visa 10 vya utekaji nyara vilivyoishangaza dunia Reviewed by RICH VOICE on Oktoba 13, 2018 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...