HABARI ZA JUMAMOSI NZURI YA LEO 07/01/2017

Saturday, January 7, 2017

 

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumamosi Ya January 7

Magari yenye taa za mwanga mkali yapigwa marufuku

POLISI Kikosi cha Usalama Barabarani kimesema kitaanza kukamata magari yote ambayo yamewekwa taa zenye mwanga mkali (spotlights) kwa kuwa uwekaji wa taa hizo, ni kinyume na sheria ya usalama barabarani.

Uwekaji wa taa hizo zenye mwanga mkali, umezuka kwa kasi katika maeneo mbalimbali nchini, jambo ambalo limetajwa linaweza kusababisha ajali kwa dereva atakayemulikwa na taa hizo.

Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Kikosi hicho, Naibu Kamisha Mohammed Mpinga ofisi kwake jijini Dar es Salaam, ambapo alisema ukamataji wa magari hayo utaanza rasmi wiki ijayo.

Mpinga alisema wameshatoa maelekezo kwa askari wa usalama barabarani, kuhakikisha wanakamata magari, pikipiki na malori makubwa ambayo yamewekwa taa hizo.

“Ziko taa za aina fulani zinazowekwa kwenye magari na hata ukitembea usiku utaona mwingine ameweka taa moja mwingine anaweka nyingi sana, kiasi ambacho zimeleta matatizo kwa madereva wengine,” alisema Kamanda Mpinga.

Aidha, alisema kwenye barabara kuu kuna mtindo wa madereva wa magari makubwa, kuweka taa kubwa ambazo zinawekwa juu na kumulika mwanga mkali, kiasi ambacho dereva anayemulikwa anapata upofu wa muda na kushindwa kudhibiti chombo chake.

Kamanda Mpinga alisema kuwa walishatoa muda wa kutosha kwa wamiliki wote wa magari, walioweka taa hizo kuziondoa, hivyo kwa sasa wataanza kuwachukulia hatua wote ambao watakuwa hawajaziondoa.

Alifafanua kuwa uwekaji wa taa hizo ni kinyume cha Sheria ya Usalama Barabarani Kifungu cha 39 Sura ya 168, ambacho kinaeleza matumizi ya taa. Mpinga pia alisema magari yatakayokamatwa ni yale ambayo yameongezewa taa hizo.

Alisema magari ambayo yametoka kiwandani yakiwa na taa hizo, hayatahusika.

“Hapa nazungumzia taa za kuongeza. Lakini pia kuna magari kwa ajili ya uwindaji huwa yanawekwa taa, lakini wanachotakiwa kufanya waweke kava, wakati wote ziwe na kava,” alisema.

Alisema wamiliki wa magari hayo ya kuwindia, wanatakiwa kuondoa kava hizo wanapokuwa porini tu na kuongeza kuwa mtindo wa wamiliki wa magari makubwa kuweka taa nyuma ya magari ambayo inamulika, matokeo yake mtu anayemfuata anafikiri gari anakuja kumbe inakwenda mbele.
 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Atembelea Mgodi Wa Makaa Ya Mawe Ya Ngaka.....Anusa Madudu, Aahidi kutuma Gavana, CAG, Msajili wa Hazina kufanya ukaguzi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa atamtuma mara moja Msajili wa Hazina aende kufanya uchunguzi wa kina na wa kijinai (forensic investigation) ili kijiridhisha kama mapato na matumizi ya kampuni ya TANCOAL ni halali.

Ametoa kauli hiyo jana  mchana (Ijumaa, Januari 6, 2017) mara baada ya kupokea taarifa na kutembelea mgodi huo ili kuona shughuli za uzalishaji zikoje.

Waziri Mkuu amesema atamwagiza pia mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili apitie mahesabu ya kampuni tangu mwaka 2011 walipoanza uzalishaji. 

“Mbali na CAG, itabidi Gavana wa Benki Kuu naye aangalie utumaji wa fedha uliokuwa ukifanywa kama ulifanyika kwa halali,” alisema.

Katika maswali aliyoyauliza Waziri Mkuu, alitaka kujua ni kwa nini kampuni hiyo haijalipa gawio kwa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ambao ni mbia (asilimia 30) na kampuni ya Intra Energy Limited (asilimia 70) licha ya kuwa imekuwa ikifanya uzalishaji wa makaa ya mawe na kuyasafirisha kwenye viwanda hapa nchini na nje ya nchi.
 
“Taarifa zenu zinaonyesha kuwa mmepata kila mwaka lakini rekodi nilizonazo zinanionyesha kuwa mwaka 2013 mlipanga kuzalisha tani 50,000 na mkauza zaidi ya hapo. Mkaguzi wa hesabu anasema kampuni imepata hasara, hii itawezekanaje?” alisema wakati akimhoji Mkurugenzi Mtendaji wa NDC, Bw. Mlingi Mkucha.
 
“Desemba 2013 mliuza tani 39,000 kwa wamiliki wa viwanda vya nguo, pia mliuza tani 2,000 kwa kampuni ya saruji ya Zambia, Novemba 2013 mliingia makubaliano ya kuuza tani 165,000 kwa kampuni ya saruji ya Kitanzania na ziliuzwa. Mbona financial statement zenu zinasema mwaka huo nao mlipata hasara?”
 
“Mnasema gawio (dividend) hutolewa baada ya mtu kutangaza faida. Mbona mlivuka lengo lakini mkatangaza kuwa kampuni imepata hasara katika mwaka huo wa fedha?”
 
Waziri Mkuu alimbana Bw. Mkucha aeleze ni kwa nini akiwa mwanasheria wa NDC aliruhusu kuwepo kwa mkataba unaotoa mwanya kwa kampuni ya TANCOAL kulipia gharama za menejimenti kwa wakurugenzi ambao wako Australia wakati hawahusiki na utendaji wa kila siku wa TANCOAL hapa nchini.
 
Pia alihoji ni kwa nini aliyekuwa Mkurugenzi wa NDC, Bw. Gideon Nassari alikuwa ni mjumbe wa Bodi ya TANCOAL na mjumbe wa Bodi ya Intra Energy Corporation ya Australia huku akiwa ni Mtendaji Mkuu wa NDC. 
“Wewe ulikuwa mwanasheria wa NDC na ulilijua hilo lakini hukuona taabu ya kiutendaji katika hilo? Au ulishindwa kusema kwa sababu alikuwa ni bosi wako?”
 
Waziri Mkuu amemtaka Bw. Mkucha aupeleke mikataba huo kwa Mwanasheri Mkuu wa Serikali ili aupitie upya na hasa kipengele cha kufungua akaunti za NDC kwa kutumia kanuni za Australia na suala la utaratibu wa gawio kwa wanahisa ambapo kifungu kilichopo kinaipa Bodi ya TANCOAL mamlaka ya kuamua kutoa au kutokutoa kwa wanahisa.

“Kipengele kama hiki kwenye mikataba kinazuia ninyi kupata gawio, na ndiyo maana hesabu zao kila mwaka zimekuwa zinasoma hasara na ninyi mnaona sawa tu huku Serikali ikiendelea kukosa mapato yake,” alisema.

Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa kampuni ya TANCOAL uongeze uzalishaji ili iweze kukidhi mahitaji ya ndani kwani makampuni mengi yamebaini gharama kubwa iliyopo kwenye matumizi ya mafuta ya dizeli na sasa yanahitaji makaa ya mawe kwa uzalishaji.
 
“Nimetembelea mgodi na kujiridhisha kuwa makaa ya mawe yapo ya kutosha. Uongozi wa kampuni mmesema mashine ziko bandarini Mtwara, lipieni mkamilishe taratibu ili mashine na mitambo yenu vije kusaidia kuongeza uzalishaji,” alisema.
 
“Nirudie wito wa Serikali kuwa hatutaruhusu uagizaji wa makaa ya mawe kutoka nje ya nchi na kwa maana nyingine tumewaongezea wigo wa soko lakini ninyi mnakosa teknolojia ya uchimbaji makaa kwa wingi. Fanyeni haraka kuleta hivyo vifaa vilivyoko bandarini,” alisisitiza.
 
Akiwa kwenye mgodi huo, Waziri Mkuu alielezwa kuwa kampuni hiyo imepanga kuongeza uzalishaji na kufikia tani 60,000 kutoka tani 2,500 za sasa. Hivi sasa, uchimbaji kwenye mgodi wa Ngaka unafanyika kwenye eneo la Mbalawala na Mbuyura ambayo yana mashapo (deposits) ya tani milioni 423.
 
IMETOLEWA NA

Tanzania Yapata Fursa Kubwa ya Biashara....Yaingizwa Katika Mpango Mkubwa wa Biashara na China

Jitihada za Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan za kuiingiza Tanzania katika mpango mkubwa wa biashara kwenye Bara la Asia, Mashariki ya Kati, Ulaya na Afrika, umefanikiwa.

Ni baada ya Tanzania kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi saba zilizoingizwa katika mpango, unaojulikana kama ‘China One Belt, One Road Stratergy’. Nchi nyingine ambazo zimechaguliwa na kuingizwa kwenye mpango huo ni Malaysia, Sri Lanka, Nepal, Bangladesh, Pakistan na Thailand.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, jana, ilisema baada ya Tanzania kuingizwa rasmi katika mpango huo, Makamu wa Rais, Samia ambaye pia mjumbe katika jopo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa la Kumuwezesha Mwanamke Kiuchumi, akiwakilisha nchi za Ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika, alikutana na watendaji kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Biashara (TCCIA) na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), kuwaeleza kuhusu muhimu wa Tanzania kuingizwa kwenye mpango huo.

Makamu wa Rais alisema Tanzania imepata uanachama ndani ya mpango huo, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na mfanyabiashara wa madini na vito kutoka China, Dk Helen Lau kuhusu manufaa ya mpango huo.

Alisema alimuomba mfanyabiashara huyo, kuisaidia Tanzania kuingia kwenye mpango wa China One Belt, One Road Stratergy, jambo ambalo limefanikiwa.

Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa mwezi Septemba mwaka 2016, ulifanyika mkutano Guangdong nchini China kujadili maombi ya kujiunga na mpango huo, ambapo Makamu wa Rais alimuomba Dk Helen, kwa niaba ya Tanzania, awasilishe maombi ya kutaka kujiunga.

Kwa bahati nzuri, ombi la Tanzania lilikubaliwa na kupata uanachama katika mpango huo mkubwa wa China One Belt, One Road Stratergy.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makamu wa Rais alisema kuwa moja ya fursa zinazotolewa na Serikali ya China katika mpango huo, kila nchi mwanachama hupewa vyumba vya ofisi katika jengo linaloitwa 21st Century Maritime Silk Road Expo bila kulipa kodi ya pango kwa miaka mitatu.

Baadhi ya vyumba vya jengo hilo, vitatumiwa na nchi husika kuonesha na kutangaza bidhaa zao. Kufutia Tanzania kuingizwa kwenye mpango huo, Samia aliwaagiza watendaji wa sekta binafsi aliokutana nao Ikulu jijini Dar es Salaam, wajipange na kuweka mikakati ya namna ya kunufaika na mpango huo haraka iwezekanavyo.

Alibainisha kuwa mpango huo wa China One Belt, One Road Stratergy, ulibuniwa na serikali ya China kwa dhamira ya kuzikutanisha jumuiya za wafanyabiashara za Mashariki mwa Bara Asia, Mashariki ya Kati, Ulaya na Afrika ili wabadilishane mawazo, kuonesha njia na kupeana ushauri wa jinsi ya kukuza biashara kati ya nchi wanachama wa mpango huo ili kuiwezesha sekta ya biashara, kuchangia vyema kwenye uchumi wa mataifa yao.

Makamu wa Rais alisema baada ya Tanzania kuingia kwenye mpango huo, itanufaika na fedha za mfuko kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu, ambazo zinatolewa kwa nchi zilizojiunga na mpango huo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TPSF, Godfrey Simbeye na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar, Taufik Turki walimuahidi Makamu wa Rais kuwa watatumia fursa hiyo ipasavyo ili kukuza biashara kati ya Tanzania na nchi wanachama wa mpango huo.
OFISI YA WAZIRI MKUU

 

Zitto Kabwe Aitaka Serikali Itangaze Balaa la Njaa

Kiongozi wa Chama cha ACT –Wazalendo, Zitto Kabwe ameitaka Serikali kutangaza rasmi baa la njaa kwa mujibu wa sheria kutokana na hali ya chakula kuwa mbaya nchini.

Kauli ya Zitto imetolewa wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisisitiza utunzaji wa chakula baada ya kukagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Kanda ya Songea.

Agizo la Majaliwa pia limetolewa siku mbili baada ya Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba kutofautiana na Zitto kuhusu hali ya chakula ambapo Waziri huyo alisema hali ya chakula nchini ni shwari huku Mbunge huyo wa Kigoma Mjini akisema ni mbaya.

Jana, mbunge huyo akihutubia mkutano wa kampeni ya kumnadi mgombea udiwani Kata ya Nkome, Geita aliendelea kupigilia msumari kauli yake akisema, “Hali ya chakula ni mbaya, ni mbaya, ni mbaya.”

Alisema baada ya ziara ya Waziri Mkuu kwenye maghala ya Taifa na kujionea hali ya chakula nchini, ni vyema Serikali ikachukua hatua.

“Ninapendekeza Serikali ichukue hatua muhimu ya kisheria ya kutangaza baa la njaa nchini. Tamko la baa la njaa litaisaidia Serikali kupata bajeti ya dharura ya kununua chakula na kutoa uhuru kwa wakuu wa wilaya kutangaza bila woga kuwa maeneo yao yana njaa,” alisema Zitto huku akimpongeza Majaliwa kwa ziara hiyo.

Lowassa, Maalim Seif Kutikisa Zanzibar Kesho

Wanasiasa wakongwe nchini, Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Edward Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika, kesho wanatarajia kuungana kwa mara ya kwanza jukwaani tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Vigogo hao wa vyama vya CUF (Maalim Seif) na Chadema (Lowassa) wataunguruma katika viwanja vya Skuli ya Fuoni visiwani Zanzibar kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Dimani kwa tiketi ya CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhani, katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Januri 22 kuziba nafasi ya aliyekua mbunge wa jimbo hilo, Hafidh Ally Tahir aliyefariki dunia Novemba 11  mwaka jana.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu  amesema kuwa chama chake kimemua kuungana na CUF katika uchaguzi huo ili kuhakikisha mshirika wake huyo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) anamshinda mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aidha, Mwalimu aliongeza kuwa baada ya Lowassa kushiriki uzinduzi wa kampeni hizo kesho, viongozi wengine wa Chadema watafuata kwa kufanya mikutano mbalimbali jimboni humo. Alisema kuwa baada ya Lowassa atafuata Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe pamoja Tundu Lissu kwa nyakati tofauti, kisha wengine wataendelea hadi mwisho wa kampeni hizo.

Akizungumzia uamuzi huo wa Chadema, Mkurugenzi wa Habari,Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, Salim Bimani alieleza kufurahishwa na uamuzi huo wa Chadema na kueleza kuwa hatua ya Lowassa kuhudhuria uzinduzi huo itaongeza hamasa kubwa kwa wapenzi wa chama hicho.

“Umenambia hadi Lowassa atakuwepo? Ni furaha iliyoje, Wanzibari wana shauku kumuona. Siku ya kampeni patakuwa hapatoshi Skuli ya Fuoni, hapa Simba (Maalim Seif) kule Lowassa kipenzi kingine cha Wazanzibar,” Bimani anakaririwa na Mwananchi.

Aliongeza kuwa kama Lowassa atahudhuria mkutano huo atakuwa na mambo mawili makubwa ya kufanya, la kwanza likiwa kuwashukuru Wazanzibar kwa kura walizompa katika uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Na la pili litakuwa kumpigia kampeni mgombea wa CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhani.

Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, wataingia katika jimbo hilo ikiwa ni siku chache baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kufanya uzinduzi wa kampeni hizo akiambatana na viongozi wengine wa kitaifa wa chama hicho.

Hivyo, kwa muktadha wa kisiasa, vigogo hao wa Ukawa wana kazi ya kusawazisha matuta yaliyowekwa na timu ya chama tawala iliyoongozwa na Kinana
\ ..............

Wafugaji 50 Wala Kinyesi, Damu na Mkojo Kunusuru Maisha Yao

Watu 50 wakiwa na watoto wadogo wamenusurika kufa, baada ya kupotea ndani ya Pori la Akiba la Selous kwa siku saba; huku wakikosa chakula na maji na kulazimika kula kinyesi cha ng’ombe, damu na mikojo ya binadamu.

Watu hao ambao ni wafugaji, walikuwa wakihama na mifugo yao inayokadiriwa kufikia 1,780 kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, yakiwemo Chumvi na Muhoro waliekea Morogoro, ambako walidai ndiko yalipo makazi yao.

Tukio hilo ambalo si la kawaida kutokea katika pori hilo, lilianzia Jumatano iliyopita wakati wafugaji hao, walipoanza safari ya kuelekea Malinyi mkoani Morogoro, wakiongozwa na mwenyeji wao, waliyemtaja kwa jina la Mzee Mzigua, ambaye hata hivyo wanadai aliwalaghai na kuwatelekeza.

Wafugaji hao walisema walitembea kwa siku tano ndani ya pori hilo, wakitarajia kufika Malinyi, yaliko makazi yao. Lakini hali ilikuwa tofauti, baada ya mwenyeji wao huyo, kuwalaghai kwa kuwapitisha njia sisizo sahihi.

Walisema waliishiwa chakula na maji ya akiba na mwisho walijikuta wanatokea ndani ya Pori la Akiba la Selous; huku hali zao zikiwa zimedhoofu kutokana na njaa na kiu cha maji. Wakiwa safarini, mwenyeji wao huyo, aliwataka kila mmoja alipe fedha ikiwa ni ujira wake kwa kuwaonyesha njia. Walidai kuwa walimlipa fedha nyingi.

Wengine walimlipa Sh milioni mbili, Sh milioni moja na wengine Sh 500,000, wakitarajia angewasaidia. Walitembea usiku na mchana ndani ya pori hilo, wakipishana na wanyama wakali kama simba na nyati, hivyo kuhatarisha usalama wa maisha yao na watoto wao.

Hali ilizidi kuwa mbaya zaidi, baada ya kutimia siku ya tano wakiwa ndani ya pori hilo, pale walipoishiwa chakula na maji, hivyo kuwalazimu kuanza kuchinja ng’ombe na kunywa damu kwaajili ya kukata kiu. Pia walikula kinyesi chao ili kupunguza njaa. Yule mwenyeji wao aliwatelekeza baada ya kuona hali zao zimekuwa mbaya.

Alitokomea kusikojulikana, akiwaacha wasijue pa kwenda, hivyo kulazimika kutelekeza mifugo yao ili kunusuru kwanza maisha yao. Halikadhalika, wengine walilazimika kunywa mikojo yao na mingine kuwanywesha watoto wao kunusuru maisha yao, hali iliyowafanya kuathirika kiafya na kushindwa kuendelea na safari.

Wengine walianguka na kupoteza fahamu. “Sisi tulikuwa tunataka turudi nyumbani kwetu Morogoro. Huku tulikuja wakati wa operesheni ya Morogoro, huku tulikuja kununua ng’ombe lakini miji yetu ipo kule Morogoro. Tukaambatana na huyo mwenyeji wetu aliyejitambulisha kwa jina la Mzee Mzigua na mtoto wake.Lakini tunajua mpaka nyumbani kwake”alisema Kiongozi wa msafara wa wafugaji hao, aliyejitambulisha kwa jina la Lisesi Cherahani Bela na kuendelea;
 “Zilitimia kama siku nne tukiwa hatujanywa maji, jua lilikuwa linawaka, tukaanza kuanguka, tukaanza kuchinja ng’ombe na kunywa damu, tulijaribisha kula kinyesi cha ng’ombe, tulikuwa tunakojoa mkojo tunanywesha hata watoto. Mimi nilikunywa mkojo lita moja, ikaniathiri hapa kifuani, kumbe mkojo ni kitu kibaya.”

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika eneo hilo, kiongozi huyo alisema baada ya kuona hali inakuwa mbaya zaidi, alitafuta eneo ambalo lina mtandao wa simu na kufanya mawasiliano na watu mbalimbali, ambapo alifanikiwa kuwasiliana na watu wa Kigoma na kuomba msaada wao.

Alisema kuwa watu hao, waliwasiliana na wahifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na kuwasiliana na wahifadhi wa Pori hilo la Selous, ambao walianza kazi ya kuwasaka na hatimaye kuwakuta katika eneo la Mlima Luhombelo, lililopo katikati ya Pori hilo wakiwa tayari wameshadhoofika kiafya.

Askari hao wa wanyamapori wa Pori hilo, waliwapatia uji na maji na kuwapa huduma ya kwanza wale wengine ambao walikuwa na hali mbaya.

Baada ya taarifa hizo za kupotea kwa wafugaji hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Gaudence Milanzi alifika katika eneo hilo juzi, akiambatana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Martin Leibooki, Meneja wa Pori la Akiba la Selous, Henock Msocha na maofisa wengine wa wizara na pori hilo.

Milanzi alisema Serikali inaangalia namna ya kuwasaidia wafugaji hao, kurejea katika hali zao kiafya pamoja na kuwasaidia kutafuta mifugo yao ili waweze kurejea katika makazi yao na kuendelea na shughuli zao.

“Kwa upande wa Serikali kama Wizara hatuchukulii kama hawa wameingia kwenye hifadhi hapana, muhimu kwanza ni kuokoa maisha ya binadamu, na hicho ndicho tunategemea kukifanya sasa hivi, na baada ya hapo kutakuwa na masuala ya kutafuta hiyo mifugo, kwa sababu wamepata hasara kubwa”alisema Katibu Mkuu huyo.

Aliutaka uongozi wa wilaya ya Rufiji, kutoa ushirikiano na wizara ili kuwabaini waliowadanganya wafugaji hao, kwa kuwaingiza kwenye pori hilo na kuwatapeli kiasi hicho kikubwa cha fedha.

“Hawa waliowadanganya na kupita huko ndani ya pori kwa kweli tutaendelea kuwatafuta na tutaomba tuwe na ushirikiano na uongozi wa Wilaya kwa sababu inaelekea kuna watu kazi yao ndo hiyo, ukiangalia pesa walizowapa ni nyingi sana, sasa watu wamechukua pesa zote na wamewaacha katika hali kama hii, wengine wana watoto wadogo, kwa hiyo tutahakikisha tunashirikiana kuwatafuta ili tukomeshe hili tatizo moja kwa moja”alisema.

Katibu Mkuu huyo alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TAWA na Mhifadhi Selous kwa juhudi za haraka walizochukua. Alisema wizara yake itaendelea kushirikiana na Mamlaka mbalimbali, kutoa misaada ya haraka, endapo yatatokea tena matukio ya aina hiyo.

Kwa upande wake, Leibooki alisema TAWA ambao ndiyo wamiliki wa hifadhi zote za wanyamapori nchini, haitawachukulia hatua za kisheria wafugaji hao, kwa kuwa waliingia ndani ya pori kwa kudanganywa na watu wenye nia mbaya.

Lakini, alisisitiza kuwa mamlaka yake, itawashughulikia kisheria wawindaji haramu na wafugaji wanaoingiza mifugo yao ndani ya hifadhi zilizo chini ya Mamlaka yake.

Pia alisema Mamlaka yake, inaendelea na utaratibu wa kushirikiana na wananchi waishio pembezeni mwa hifadhi zote, kwa kuwapa elimu ya ufugaji bora kwa kushirikiana na wizara zinazohusika na kuendeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo miundombinu ya maji.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafugaji chini (CCWT), Magembe Makoye aliwataka viongozi wa Halmashauri mbalimbali nchini, kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji mahali walipo, bila ya kuondoa watu wengine.

Alisema kuwa wao kama chama, wamesikitishwa na tukio la kuondolewa kwa wafugaji hao katika bonde hilo la Rufiji, kwa kuwaambia warudi walipotoka. Alisema tamko hilo lilitolewa na uongozi wa Halmashauri hiyo na ndilo lililosababisha matatizo hayo.

Makoye alisema kufanya hivyo, hakuondoi migogoro ya wafugaji na wakulima, badala yake ni kuendelea kuzalisha migogoro hiyo katika maeneo mengine, ambayo wafugaji watahamia.

“Tunalaani kweli vitendo hivi vya viongozi na watendaji wengine wa Halmashauri kuwafukuza wafugaji, tena wakati mwingine kwa kuwatisha na matokeo yake wananchi hawa 50 wangepoteza maisha, kama isingekuwa bahati ya mtu mmoja kuwa na simu kati yao” alisema Katibu Mkuu huyo.

“Kwa kweli kwa niaba ya wafugaji wote wa Tanzania naishukuru sana Wizara ya Maliasili kupitia kwa Katibu Mkuu, Gaudence Milanzi.” alisema Katibu huyo.

Alisema kuwa kungeweza kutokea majanga makubwa zaidi kwa kuwa kuwa wafugaji hao walikuwa wakisafiri na watoto wao wadogo katika mazingira hatarishi katikati ya pori hilo, ambalo lina wanyama wakali.

“Kwa kweli ni mazingira ya kusikitisha. Lakini niishukuru sana Serikali kwa maana ya Wizara ya Maliasili na Utalii, wamefanya kazi yao kwa namna ambavyo mimi ninawiwa kuwashukuru. Tangu jana tumewasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara, leo watu wote wameweza kupatikana, kumefanyika doria ya ndege, doria za magari, doria kwa miguu, wamewatafuta hawa watu, wamewaokoa, wamewaleta kwenye huduma za afya, wamewapa chakula, wamewahifadhi, hawajawadhuru” alisema.

Aliiomba Serikali kuhakikisha tatizo la wafugaji nchini, linatafutiwa ufumbuzi wa kudumu, kwani jamii haiwezi kuendelea kubaki na tatizo hilo kwa miaka yote. Alitaka wafugaji watafutiwe maeneo ya kudumu ya kufugia, ikiwa ni pamoja na kupimiwa maeneo yao, badala ya hali ilivyo sasa kuafukuza kila kukicha.
Baadhi ya Mzoga wa ngombe uliopatikana ndani ya Pori la Akiba la Selous,  Kanda ya Kaskazini Mashariki  Kingupira  baada ya Wafugaji 50  waliotelekezwa kwa muda wa  siku tano na mtu mmoja waliyemtaja kwa  jina maarufu la Mzigua aliyewarubuni kwa kuwaonyesha njia za mkato ndani ya Pori hilo na kisha kuwakimbia( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na Utalii)
Mmoja wa  wafugaji aliyepotea na  kutelekezwa ndani ya Pori la Akiba la Selous,  Bw. Lisesi Cherehani aliyekuwa na ng’ombe 180 na punda mmoja akiangalia mmoja wa ng'ombe wake aliyekufa kwa kukosa  maji ya kunywa kwa muda  wa siku tano kwenye Kanda ya Kaskazini Mashariki katika Pori la Akiba la Selous ( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na Utalii)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence  Milanzi (katikati) akipata taarifa kutoka kwa  Meneja wa Mradi wa Pori la Akiba la Selous    Bw. Enock Msocha (wa tatu kushoto)  mara baada ya  kuwasili kwa ajili ya kuwatembelea  Wafugaji 50 waliokolewa na Askari wanyamapori baada ya kutelekezwa  na mtu mmoja waliyemtaja kwa  jina maarufu la Mzigua aliyewarubuni kwa kuwaonyesha njia ya mkato ndani ya Pori hilo na kisha kuwakimbia ( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na Utalii)
 

Uzinduzi wa Kampeni: Kinana Arusha Kombora Zito Kwa Maalim Seif na CUF

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amerusha kombora zito kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, huku akimwita mgombea wa urais wa kudumu aliyekata tamaa.

Pamoja na hayo, Kinana amewataka Wazanzibari kuachana na maneno ya mitaani kwani Uchaguzi Mkuu ulishamalizika na Dk. Ali Mohamed Shein ameshaapishwa kuwa rais kwa mujibu wa sheria.

Kauli hiyo aliitoa jana katika uzinduzi wa kampeni za chama hicho za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Dimani zilizofanyika Maungani, nje kidogo ya mji wa Unguja.

Alisema CCM itaendelea kuchaguliwa na wananchi kwa sababu inatimiza wajibu wa kuwatumikia wananchi, kutimiza matakwa na sera kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Kinana alishangazwa na CUF kushindwa kutanua wigo wa demokrasia ndani ya chama hicho na kuendelea kumshikilia mgombea urais mmoja wa kudumu kwa zaidi ya miongo minne.

“Kuna mgombea mmoja hapa Zanzibar ameanza kugombea urais tokea akiwa na miaka 30 na sasa ana miaka 80, toka akiwa bado kijana mbichi, sasa amekuwa kikongwe na kupinda mgongo ila bado ana tamaa ya kuwania urais.

“Demokrasia ndani ya chama chetu ni ya aina yake na kwamba kukubalika kwetu mbele ya wananchi kunatokana na misimamo yetu inayotetea masilahi ya umma. Hata demokrasia yetu ndani ya CCM kamwe haifanani na vyama vingine,” alisema Kinana huku akishangiliwa.

Kinana alisema CCM ina umoja imara na katu hazuiwi mwanachama kuwania nafasi ya uongozi na haina sifa ya kuwa na wagombea wa kudumu kama ilivyo CUF ambayo tangu ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 hadi sasa, Katibu Mkuu wake Maalim Seif amekuwa mgombea wa kudumu.

Alisema ushiriki wa wana CCM 25 ndani ya chama kuwania nafasi ya uteuzi wa ubunge Jimbo la Dimani ni kielelezo tosha cha kuimarika kwa demkorasi, na mgombea aliyepatikana anaungwa mkono na wanachama wote.

Alieleza kuwa vikao vya CCM vya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati Kuu (CC) vilikutana na kupitisha jina la mgombea aliyeshinda kura za maoni, huku CUF ikiwa kimya, ikishindwa hata kufanya vikao vyake kwa mujibu wa katiba ya chama chao.

Akizumgumzia kupwaya kwa dhana na misingi ya demokrasia ndani ya CUF, Kinana alisema hivi sasa chama hicho kina wenyeviti watatu, ambao mmoja ni wa muda, mwingine wa mpito na aliyebaki ni wa zamani

Aidha Kinana aliwashangaa wanachama wa CUF ambao wanakubali kudanganywa kirahisi kila siku na kuaminishwa ipo siku mgombea wao wa urais aliyeshindwa uchaguzi atatangazwa na Umoja wa Mataifa (UN) kuwa Rais wa Zanzibar.

“Tuliambiwa hapa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar utafutwa, watakuja watu toka UN, mara tukaelezwa wangekuja   Jumuiya ya Ulaya, wakaambiwa washone nguo mpya kusherehekea ushindi, huku siku zikitaradadi hakuna kinachotokea,” alisema.

Kinana alisema viongozi wa CUF hawana uwezo wowote wa kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo kwani walibahatika kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini bado hakuna walichofanya.

“Kama ni mkate CUF walipata nusu na CCM nusu, wakashika wizara makini za Biashara na Viwanda, Katiba na Sheria, Habari na Utamaduni, Mawasiliano na Miundombinu, lakini kutokana na wao kuwa dhaifu, hawakumudu hata kujenga kiwanda kidogo,” alisema.

Kinana aliwaomba wananchi wa Dimani kumchagua mgombea ubunge wa CCM, Juma Ali Juma kwa sababu ni makini, mchapakazi na mwepesi wa kuwatumikia wananchi.

Akihutubia katika mkutamo huo wa uzinduzi wa kampeni, mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Balozi Seif Ali Idd, aliwaeleza wananchi wa Dimani kuwa si sifa ya wagombea wa CUF kuwatumikia wananchi na mfano mzuri ni katika majimbo ya Pemba.

Vigogo Wengine Kutumbuliwa TANESCO.....Lengo ni kuimarisha utendaji wa Shirika Hilo

Siku moja baada ya vigogo watatu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kushushwa vyeo, uongozi wa shirika hilo umesema utaendelea na fagio hilo kama njia ya kuongeza ufanisi kwenye utendaji.

Vigogo hao wa ngazi za juu ambao ni wakurugenzi, wamehamishiwa Chuo cha Mafunzo cha Tanesco (TSS) kwa madai kuwa shirika linaboresha ufanisi wake.

Walioshushwa vyeo ni pamoja na Declan Mhaiki aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji anayeshughulikia usambazaji wa umeme.

Wengine ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji na Huduma kwa Mteja, Mhandisi Sophia Mgonja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji Umeme, Nazir Kachwamba.

Wakati hao wakipitiwa na panga hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali Watu, Watson Mwakyusa, aliamua kuandika barua kuacha kazi mwenyewe.

Juzi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka, alisema jana wangetoa taarifa kuhusu hamisha hamisha hiyo.

Jana mchana Idara ya Kitengo cha Mahusiano cha Shirika hilo, kilitoa taarifa na kusema kuwa wataendelea na hatua mbalimbali za mabadiliko ya uongozi kwa lengo la kuongeza ufanisi zaidi wa kiutendaji.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa mabadiliko yanayoendelea ndani ya Tanesco yatawekwa wazi wakati mwafaka kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za shirika kupitia vyombo vya habari.

Kitengo hicho kilieleza kuwa kwa sasa bado wanaendelea na panga pangua na endapo watakamilisha watatoa taarifa kwa umma.

“Tunaomba vyombo vya habari vitoe fursa kwa mamlaka husika kuendelea kukamilisha zoezi hili muhimu kwa maendeleo ya Shirika na Taifa kwa ujumla na taarifa rasmi itatolewa baada ya zoezi kukamilika,’’ ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Januari Mosi, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli alimteua Dk. Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, baada ya kumng’oa aliyekuwa mkurugenzi wa shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba.

Mramba alitenguliwa uteuzi wake siku mbili baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kutangaza kuridhia ombi la Tanesco la kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 kutoka 18 waliyoomba.

Kabla ya uteuzi huo, Dk. Mwinuka alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akiwa mjini Bukoba kwenye ibada ya Mwaka Mpya, Rais Magufuli alisema amekerwa na kusikitishwa na vitendo vya baadhi ya watumishi wa umma kujitokeza hadharani na kutangaza au kuzungumzia mambo ya kitaifa kama uamuzi wa Serikali bila kushirikisha viongozi wao wa ngazi za juu.

Kutokana na hali hiyo, alisema watendaji hao ni miongoni mwa majipu yanayostahili kutumbuliwa.
 

Waziri Nchemba: Hatutamhukumu mtu kwa kazi anayoifanya, tutamhukumu kwa kosa analolifanya

Ikiwa imepita siku moja tangu waziri wa mambo ya ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba kusema kuwa watakaofanya unyama wa kuua au kuchinja watu au wanyama kwa mapanga na sime wataona chamoto, bado kauli hiyo imekaidiwa kwa baadhi ya watu wanaosadikika kuwa ni wa jamii ya kifugaji baada ya kumjeruhia kichwani kwa sime Rajabu Ayub (36) mkazi wa kijiji cha Mbigiri wilayani kilosa, akiwa shambani kwake na kumsababishia maumivu.

Polisi mkoani Morogoro mpaka sasa inawashikilia watu 24 kwa mahojiano zaidi kuhusu tukio hilo. Waziri Mwigulu Nchemba ameagiza nguvu zaidi ya dola iongozwe katika maeneo hayo mpaka mhusika wa tukio hilo atakapopatikana.

Hili ni tukio la pili tangu Waziri Mwigulu awepo mkoani Morogoro la kwanza likiwa la Fabiano Bago mkazi wa kolelo wilaya ya Morogoro ambaye alijeruhiwa maeneo ya kichwani kwa sime na watu wa jamii ya kifugaji mara baada ya kumuona akiongea na simu wakidhani anawataarifu polisi na Fabian alifariki dunia kutokana na majeraha aliyopata
 

Marekani kumsaka mtoto wa Osama Bin Laden Aliyeapa Kulipa Kisasi

Marekani imesema kuwa imemuorodhesha mtoto  wa mwisho wa Osama Bin Laden, Hamza, katika orodha ya magaidi wanaosakwa na taifa hilo.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema kuwa Hamza Bin Laden ameanza kushiriki katika maswala ya kundi la al Qaeda, kundi la jihad lililofadhiliwa na babake.

Hamza amesema kuwa atalipiza kisasi mauaji ya babake yaliotekelezwa na kikosi maalum cha Marekani kwa kutekeleza mashambulizi dhidi ya Wamarekani.

Hamza amepigwa marufuku  kufanya biashara na raia wa Marekani huku mali zake zikizuiliwa pia.

Mamake Hamza ni Khairiah Sabar, mmoja wa wake za Osama aliyekamatwa wakati wa shambulio la wanajeshi wa Marekani kwenye maficho ya Osama mjini Abbotabad nchini Pakistan mwaka 2011.

Mkuu wa kitengo cha usalama cha kundi la al-Qaeda Ibrahim al-Banna pia ameongezwa katika orodha hiyo .

Marekani imetoa kitita cha dola milioni 5 kwa mtu yeyote atakayemkamata al-Banna.

Hamza bin Laden alitambuliwa kuwa mmoja wa viongozi wa al-Qaeda mwaka 2015 na baadaye akaapa kulipiza kisasi mauaji ya babake mwezi Julai mwaka uliopita.
 
Katika ujumbe wa sauti wa dakika 21 wenye kichwa "We Are All Osama," (Sote ni Osama), na uliochapishwa katika mitandao, aliapa lazima angelipiza kisasi mauaji ya babake mwaka 2011 nchini Pakistan.

''Tutaendelea kuwasaka na kuwapiga popote pale mtakapokuwa mmejificha ati nyuma ya pazia za usalama kwa maovu mnayoyaendeleza ,Palestina, Afghanistan, Syria, Iraq, Yemen, Somalia na kote kwenye ardhi ya waislamu mnayokalia,'' shirika la habari la Reuters lilimnukuu.

''Na kwa wale wanaodhania kuwa tutakuwa tukilipiza kisasi mauaji ya Osama ole wenu, kwanini sisi tutakuwa tukilinda dini ya kiislamu'' alisema Hamza.

Hamza, kulingana na wachanganuzi, alitambulishwa na kiongozi wa kidini wa kundi la al-Qaeda Ayman al-Zawahiri katika ujumbe huo uliolenga kuwavutia vijana ambao kwa sasa wamejiunga kwa wingi na kundi la Islamic state.

Hamza sasa anaungana na nduguye wa kambo, Saad, kuwa miongoni mwa watu wa jamii ya Osama walioorodheshwa kuwa magaidi.

Chanzo: BBC
 

Serikali yapiga marufuku ununuzi wa sare za jeshi la zima moto na uhamiaji toka taasisi binafsi

Naibu waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mhandisi Hamad Yusuph Masaun amepiga marufuku ununuzi wa sare za jeshi la zima moto na uhamiaji kwa taasisi binafsi na badala yake ameagiza sare hizo zizalishwe katika viwanda vya jeshi la magereza nchini.

Mhandisi Masauni ameyasema hayo baada ya kutembelea kiwanda cha jeshi la magereza kilichopo Ukonga kinachoendeshwa kwa nguvu kazi ya wafungwa ikiwa ni ufuatiliaji, utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania la kulitaka jeshi hilo liwasimamie wafungwa katika uzalishaji wa sare.

“Kuanzia leo uhamiaji,zima moto wote washone nguo, kama ambavyo magereza wanashona katika kile kiwanda, kwamba dhamira ya mheshimiwa rais ya kutoa maelekezo ambayo yamefuatilia utendaji kazi wake nimeridhika, kwamba ni marufuku kama alivyosema mheshimiwa rais kwa askari Magereza na askari wote wa vyombo vya usalama nchini kununua uniform kwa raia, jeshi la magereza linatengeza furniture zenye ubora wa hali ya juu,” alisema Mhandisi Masauni.
 

Lowassa Atajwa Kusababisha Deni la Milioni 1

Jina la waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa limetajwa na mkaazi mmoja wa Mbeya mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla kuwa sababu ya deni la shilingi milioni moja kutokana na mapenzi ya wafuasi wake.

Mkaazi huyo wa kata ya Ruanda Nzovwe aliyejitambulisha kwa jina la Amos Mwakyambiki alidai kuwa wafuasi wa Chadema waliharibu paa la nyumba yake walipopanda kwa lengo la kufuatilia mkutano wa Lowassa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana, na kwamba chama hicho kilimuahidi kumlipa fidia ya shilingi milioni moja lakini hadi sasa ahadi hiyo haijatekelezwa.

Alimueleza mkuu wa mkoa huo kuwa kutokana na uharibifu huo mkubwa uliofanyika, wapangaji wake waliamua kuhama nyumba yake hivyo kukosa kipato.

“Naomba Serikali ya Mkoa inisaidie kuzungumza na meya (wa Chadema) ili niweze kulipwa stahiki zangu kwani sasa sijui hatma yangu. Kuku niliokuwa nauza kwa ajili ya kupata nauli kwenda ofisi za jiji wamekwisha,” Mkaazi huyo anakaririwa.

Kutokana na madai hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya alimuagiza Mkuu wa Wilaya kufuatilia suala hilo huku akitahadharisha wananchi kuhusu matumizi ya nyumba zao wakati wa kampeni.

“Lakini na nyie wananchi msikubali nyumba zenu zibadilishwe kuwa viwanja vya siasa,” alisema Makalla.

Akizungumzia taarifa hizo, Mkuu wa Idara ya Habari ya Chadema, Tumaini Makele alisema kuwa chama hicho kitafuatilia kuona ni nani aliyetoa ahadi hiyo kwa mwananchi huyo na ilikuwa katika mazingira gani ili walifanyie kazi ipasavyo.

Picha 8: Muonekano wa sasa wa Jennifer na Patrick walioibuliwa na marehemu Steven Kanumba

Watu wengi watawakumbuka Jennifer na Patrick kwa jinsi walivyoweza kutikisa tansia ya filamu Tanzania kipindi cha nyuma walipoibuliwa na marehemu Steven Kanumba.

Watoto hawa wawili walicheza kwa ustadi mkubwa katika filamu za Uncle JJ na This is It zote za marehemu Kanumba.

Kwa sasa Hanifa Daud ‘Jennifer’ na Othman Njaidi ‘Patrick’ si watoto tena. Wawili hawa hawajaonekana sana kwenye filamu baada ya Steven Kanumba aliyewatoa kufariki.

Jennifer ambaye amehitimu kidato cha nne mwaka jana mara ya mwisho alionekana kwenye filamu ya Zena na Betina ya Salma Jabu a.k.a Nisha mwaka 2014. Kwa upande wake Patrick, yeye alisema kuwa hana shauku ya kuigiza tena kama ilivyokuwa awali.
Credit: Bongo5 
 
 

Saturday, January 7, 2017

Picha: Billicanas Ya Mbowe Yabomolewa Rasmi

Shirika  la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza kubomoa jengo la iliyokuwa Klabu Bilicanas na ofisi za Free Media inayomiliki gazeti la Tanzania Daima zinazomilikiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe, lililopo makutano ya barabara ya Mkwepu na Indira Gandhi lenye kitalu namba 725-726/24 na hati namba C. T No. 186018/15 and C. T No. 186018/10.

Ubomoaji huo ulioanza jana unafanyika wakati Mbowe ameingia katika mgogoro na NHC baada ya kampuni ya udalali ya Poster and General Traders kumtolea vyombo nje mwanzoni mwa Septemba, mwaka jana kwa kudaiwa Sh bilioni 1.2 ambayo ni deni la pango ya miaka 20.

Mwanzoni mwa Septemba, mwaka jana NHC kwa kushirikiana na Kampuni ya Poster and General Traders, ilifika katika jengo hilo kwa maelekezo ya kutoa  thamani mbalimbali zilizokuwa katika ofisi za jengo hilo na kumpa Mbowe siku 14  kulipa deni analodaiwa na kuweza kugomboa mali hizo.

Mpango huo ulisimamiwa na Meneja wa Ukusanyaji Madeni wa NHC, Japhet Mwanasenga na alisema Mbowe alikuwa na muda wa wiki mbili kwa wakati huo kulipa fedha hizo kabla ya vifaa vyake kupigwa mnada.

Mwanasenga alisema taratibu zote zilifuatwa kabla ya kumwondoa mteja huyo ikiwamo notisi na kwamba vifaa hivyo vitashikiliwa kwa muda huo na endapo akishindwa kulipa jengo hilo atapangishwa mtu mwingine.

Alisema shirika hilo linahitaji fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa majengo yake hivyo mteja anayedaiwa ajiandae kuondolewa wakati wowote huku baadhi ya watu wakilihusisha tukio la Mbowe kuondolewa katika ofisi hizo na masuala ya siasa.

Hata hivyo, Mwanasenga, alisema uamuzi wa kumwondoa katika ofisi hizo hauna uhusiano na masuala ya siasa.

Kutokana na hali hiyo, Mbowe kupitia Mawakili wake, John Malya na Peter Kibatala, walifungua shauri la kupinga kuondolewa katika jengo hilo Mahakama Kuu ya Tanzania na kutaka kurudishwa katika jengo hilo.

Hata hivyo, maombi hayo yalitupiliwa mbali Oktoba 17, mwaka jana na Jaji Sivangilwa Mwangesi na kusema kuwa mahakama hiyo imechukua uamuzi huo baada ya kujiridhisha na hoja kuu tatu kuwa hakuna mkataba wa ubia uliopo baina ya NHC na Mbowe Hotels Limited na kuwa uhusiano pekee uliosalia ni wa mpangaji na mpangishaji.

Pia Jaji Mwangesi alisema mahakama imejiridhisha kuwa NHC imefuata taratibu zote katika kuiondoa Mbowe Hotels Limited kwa kutoa ilani ya siku 30 na baadaye siku 14 kabla ya kumtoa mteja wao huyo.

Kuhusu kusajiliwa au kutosajiliwa kama dalali rasmi wa mahakama wa kuendesha mchakato wa kumhamisha Mbowe katika jengo hilo, alisema hiyo nayo haikuwa hoja yenye mashiko na kwamba waombaji walitakiwa kuwasiliana na Msajili wa Mabaraza ya Ardhi.

Katika shauri hilo, NHC iliongozwa na Wakili Kiongozi, Aloyce Sekule na Ipilinga Panya na mawakili wake wengine waliojikita katika kujibu hoja zilizokuwa zikitolewa na wateja wao.

HABARI ZA JUMAMOSI NZURI YA LEO 07/01/2017 HABARI ZA JUMAMOSI NZURI YA LEO 07/01/2017 Reviewed by RICH VOICE on Januari 07, 2017 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...