HABARI ZA JUUMATANO HII

..

...

.

PLAZA.jpg

JEMBE1.jpg

MKEKA.jpg

Wednesday, January 4, 2017


Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumatano Ya January 4



 

Wednesday, January 4, 2017

Ziara Ya Rais Magufuli Kagera Yatumbua Watatu

Baada  ya Rais Dk. John Magufuli kuagiza watumishi wote wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera waliohusika katika ukarabati wa majengo ya Shule ya Sekondari Omumwani ambayo yameonekana kutoendana na thamani ya fedha zilizotumika wachunguzwe, watumishi watatu wa manispaa hiyo wamesimamishwa kazi.

Watumishi hao walisimamishwa jana na Katibu Tawala, Mkoa wa Kagera, Diwani Athumani, baada ya kufanya ukaguzi wa miundombinu ya maji iliyomo katika majengo ya shule hiyo.

Shule hiyo ilikarabatiwa kuwapa hifadhi ya muda wanafunzi wa shule za sekondari Ihungo na Nyakato zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera, Septemba 10, mwaka jana.

Baada ya ukaguzi huo, Athumani alimtaka Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Chibunu Lukiko, kumtajia majina ya watumishi waliohusika moja kwa moja katika usimamizi wa kila siku wa shughuli hiyo.

Katika maelezo yake, Athuman alisema aligundua ukarabati uliofanywa ulikuwa chini ya kiwango na hauendani na thamani ya Sh milioni 119 zilizotolewa na Serikali.

“Kwanini wakurugenzi hampendi kufuatilia miradi iliyo katika maeneo yenu? Kama mngefuatilia mapema, mngegundua ubadhilifu uliofanyika hapa na kuchukua hatua mapema.

“Kwa hiyo, naagiza kuanzia leo Januari 3 (jana), mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba uwasimamishe watumishi wote waliohusika ambao ni Mhandisi Kitengo cha Ujenzi wa Manispaa ya Bukoba, Andondile Mwakitalu, Mhandisi Msaidizi, Costane Felix na fundi Charles Kafumu.

“Hawa lazima wasimamishwe ili kupisha uchunguzi utakaofanyika kwa ajili ya kulinganisha kazi iliyofanywa na kiasi cha fedha kilichotumika kama vinaendana.

“Tatizo jingine nililoligundua ni kutokuwapo kwa usimamizi mzuri wa mradi huo kutoka kwa watumishi wa manispaa. Hao nao uchunguzi dhidi yao utafanyika kwa uwazi na ukweli na hatutamwonea mtu.

“Sitaki kusikia shughuli hii inasimama eti kwa sababu ya hawa watu wamesimamishwa, fanya makabidhiano na wale watakaokuwapo.

“Kaimu mkurugenzi hakikisha mnakabidhiana kila kitu, hata msumari usibaki na uchague watu wengine wa kuendelea na kazi ya kusimamia mradi huu ili ukamilike kwa muda uliopangwa,” alisema.

Naye Mhandisi Mwakitalu aliyesimamishwa, alisema majengo hayo yalikuwa katika hali mbaya na kwamba ukarabati wake unahitaji fedha nyingi ili yarudi katika hali yake ya kawaida.

Wednesday, January 4, 2017

Ningekuwa Diamond nisingejiita simba – Darassa

Hit maker wa wimbo ‘Muziki’ Darassa ameweka wazi maana ya ule mstari wake wa “sio simba, sio chui, sio mamba” kwa kusema Diamond hakupaswa kujiita simba kwani simba ni mnyama ambaye anaweza kuuliwa anapozidiwa nguvu.

Darasa amedai Diamond ni msanii ambaye amehangaika sana kutoka kimuziki hivyo mafanikio yake na uwezo wake wa muziki alitakiwa ajiite jina lingine kwa kuwa Daimondi ni zaidi ya Simba kwa sasa kwani ni zaidi ya mnyama Simba.

“Ningekuwa Diamond nisingejiita simba,” Darassa alikiambia kipindi cha Enewz cha EATV. “Ninavyomuona Diamond ni zaidi ya Simba, kuna watu wanaua simba, simba, kajichanganya, kaingia kijijini kapotea, Diamond kwa kitu anachofanya ni zaidi ya simba, angeweza kujiita jina lingine lolote kubwa, kafanya vitu vingi sana,”

Pia rapper huyo alidai wanyama wote ambao amewataja katika wimbo wake hawaogopi kwa kuwa ana kitu kikubwa ndani yake na yeye ni mwanaume na anajiamini kwa muziki wake anaofanya.

“Kwa upande wangu nimesema siyo simba, siyo chui siyo mamba, mamba ni mnyama anayetisha sana kwenye maji, simba anatisha sana porini, chui ni hunter mzuri, so katika vitu vyote ambavyo viko humo, mimi humo kote simo, ninacho kitu ambacho kinaweza kunifanya nikwambie aaaaah”. Amemalizia Darassa

Wednesday, January 4, 2017

Waziri Mkuu Aagiza Umeme Wa Uhakika Kisarawe II

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuhakikisha eneo la Kisarawe II linakuwa na umeme wa uhakika ili kuwezesha viwanda na wananchi wa eneo hilo kupata nishati hiyo.

Alitoa agizo hilo jana jioni (Jumanne, Januari 3, 2017) wakati alipotembelea kiwanda cha Milkcom kinachozalisha bidhaa za maziwa na kiwanda cha Watercom kinachozalisha maji vilivyoko katika kata ya Kisarawe II wilayani Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi.

“Waziri wa Nishati ahakikishe eneo hili linapata umeme wa uhakika ili kuviwezesha viwanda hivi kufanyakazi vizuri jambo litakaloongeza uzalishaji. Pia wananchi wanaoishi katika maeneo haya nao watanufaika na upatikanaji wa nishati hiyo,” alisema.

Waziri Mkuu alisema amefarijika na jitihada za muwekezaji huyo za kuunga mkono mkakati wa Serikali ya awamu ya Tano wa kuifanya Tanzania kujenga uchumi wa viwanda utakaoliwezesha Taifa kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Awali, Msemaji wa Viwanda hivyo, Aboubakar Faraj akisoma taarifa ya viwanda hivyo kwa Waziri Mkuu alisema moja ya changamoto zinazowakabili ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika jambo linasababisha kupanda kwa gharama za uzalishaji.

“Punde umeme unapokatika tunalazimika kutumia majenereta kwa muda mrefu. Hii husababisha ongezeko la gharama za uzalishaji ambazo huumiza kiwanda kwa sababu haiwezekani kumtwisha mzigo huu mlaji,” alisema.

Faraji alisema changamoto nyingine ni miundombinu ya barabara ambayo usababisha wateja wengi kushindwa kufika kwenye viwanda hivyo kwa urahisi, hivyo aliiomba Serikali kuwatatulia kero hilo.

Aliongeza kuwa kwa sasa viwanda hivyo vimeajiri watu zaidi ya 1,800, ambapo alisema endapo Serikali itawahakikishia upatikanaji wa umeme na barabara wataongeza ajira kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2018.

Mapema Waziri Mkuu alizindua wodi ya wazazi katika Zahanati ya Kisarawe II iliyojengwa kwa ufadhili wa kampuni ya mafuta ya Oilcom. Wodi hiyo yenye vyumba vitatu itawapunguzia akinamama kusafiri umbali mrefu kutuata huduma hiyo.

Wednesday, January 4, 2017

Majaliwa Akagua Maghala Ya Hifadhi Ya Chakula Chang'ombe Dar Es Salaam

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na  Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Deusdedit Mpazi wakati alipotembelea  maghala ya NFRA, Chang'ombe jijini Dar es salaam Januari 4, 2017.


 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mhahindi wakati alipotembelea magahala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) , Chang'ombe jijini Dar es salaam Januari  4, 2017.  Kulia kwake ni  Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Deusdedit Mpazi. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mhahindi wakati alipotembelea magahala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) , Chang'ombe jijini Dar es salaam Januari  4, 2017.  Kulia kwake ni  Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Deusdedit Mpazi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Wednesday, January 4, 2017

UVCCM Wampongeza Rais Magufuli Kwa Kumtumbua Mkurugenzi Mtendaji TANESCO



Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umesema kuwa umefurahishwa na kitendo cha Rais Magufuli cha kupigania maslahi ya wanyonge na kuzuia kupandisha bei ya umeme nchini.

Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka wakati wa kikao cha watumishi wa umoja huo wa kutathmini utendaji kazi wa mwaka 2016 na kuweka utendaji wa mwaka huu.

Shaka amesema kitendo cha Rais Magufuli kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), Mhandisi Felchesm Mramba, ameonyesha uzalendo, ujasiri na upendo kwa wananchi ambao walimpa dhamana ya kuongoza nchi.

“UVCCM tunaunga mkono uamuzi wa Rais wa kuzuia kupanda kwa bei ya umeme na ametazama maslahi ya wananchi waliomchagua kuingia madarakani,”amesema Shaka.

Hata hivyo, amesema kuwa Tanesco kupitia kwa Mkurugenzi wake Mramba aliyetumbuliwa na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo waliwaahidi wananchi kutopandisha bei ya umeme.

Wednesday, January 4, 2017

Mkuu Wa Jeshi La Polisi Nchini, Igp Ernest Mangu Atuma Timu Ya Maofisa Wa Jeshi La Polisi Kwenda Zanzibar Kuchunguza Vitendo Vya Udhalilishaji


Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu ametuma timu ya Maofisa  wa Polisi ikiongozwa na Kamishna wa Polisi Jamii Mussa Alli Mussa kwenda Zanzibar kushughulikia kero na malalamiko ya wananchi juu ya vitendo vya udhalilishaji na ukatili kwa watoto/wanawake ambavyo vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara.

Timu hiyo imepewa jukumu la kuchunguza vitendo hivyo vya udhalilishaji na kiini chake na hatimaye kuja na mpango mkakati wa kuzuia vitendo hivyo ikiwemo kuwakamata  wahusika na kuwafikisha mahakamani.

IGP Mangu amewataka wananchi wa Zanzibar, Taasisi za kiserikali na Taasisi za kiraia zilizopo Zanzibar kutoa ushirikiano kwa timu hiyo ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na maadili ya Watanzania.

Imetolewa na:
Advera John Bulimba - ACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.

Wednesday, January 4, 2017

Anaswa na polisi akifukua kaburi la albino

Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za kufukua kaburi la marehemu ambaye likuwa ni mlemavu wa ngozi (Albino) aliyefariki mwaka 2010 kwa lengo la kuchukua viungo vyake.

Taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa na Kamanda a Polisi Mkoani Mbeya DCP Dhahiri Kidavashari inasema kuwa mnamo tarehe 03.01.2017 majira ya saa 01:00 usiku katika Kijiji cha Mumba kilichopo Kata ya Ilembo, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la JONAS JOHN mkazi wa Chapakazi alikamatwa na askari Polisi akiwa na wenzake wawili wakifukua kaburi la marehemu SISTER OSISARA aliyekuwa mlemavu wa ngozi (ALBINO)

Inadaiwa kuwa marehemu alifariki dunia mwaka 2010 kwa ugonjwa wa homa na kuzikwa katika makaburi ya Kijiji cha Mumba.

Mtuhumiwa alikutwa na majembe na makoleo ambayo walikuwa wakiyatumia kufukuria kaburi hilo. Baada ya mahojiano mtuhumwa huyo aliwataja washirika wenzake wawili ambao walikimbia baada ya kuwaona askari.

Jeshi hilo linaendelea na msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa .

Katika tukio lingine Mnamo tarehe 03.01.2017 majira ya saa 3:30 usiku katika kata ya Makongolosi wilayani Chunya, mkoa wa Mbeya, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la KELVIN KUBANDA mkazi wa Kahama alikamatwa akiwa na bhangi kete 10 sawa na uzito wa gramu 55.

Mtuhumiwa alikamatwa akiwa katika kijiwe cha kuvutia Bhangi. Upelelezi unaendelea.

Jumatano, 4 Januari 2017

VIJANA ASPIRE KWENDA SENEGAL, VIPAJI VINGINE VYATAFUTWA

MWANAJESHI WA ISRAEL ATIWA HATIANI KWA KOSA LA MAUAJI BILA YA KUKUSUDIA

BALOZI SEIF AZINDUA NYUMBA ZA KUISHI MAAFISA NA ASKARI WA UHAMIAJI, PEMBA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilikagua Jengo la Gorofa Mbili litakalobeba Familia Sita za Maafisa na Askari wa Uhamiaji baada ya kulizindua rasmi hapo Mtaa wa Mtukitu Chake chake Kisiwani Pemba ikiwa ni sherehe za kutimia Miaka 53 ya Mapinduzi Zanzibar.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi, Maafisa wa Uhamiaji na Wizara ya Mambo ya Ndani walioshuhudia ufunguzi wa Jengo la Makaazi ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji chake chake Pemba. Kulia ya Balozi Seif ni Kamishna wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar Johari Msoud Sururu,Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani Meja Gneral Projestus Rwegasira na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh., Mohamed Aboud Mohamed. Kushoto ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mh. Mwnajuma Majid,Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiam Iddi na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga.
Muonekano wa Haiba ya Jengo Jipya la Makaazi ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji liliopo katika Mtaa wa Mtukitu Chake Chake Kisiwani Pemba.
Kamishna wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar Johari Masoud Sururu akitoa Taarifa ya ujenzi wa jengo la Makaazi ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji wakati wa hafla ya kulizindua rasmi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Meja General Projestus Rwegasira akitoa salamu katika hafla ya uzinduzi wa jengo la Makaazi ya Askari wa Uhamiaji Chake chake Pemba.
Kikundi cha Utamaduni cha Mkuta Ngoma cha Mkoa wa Kusini Pemba kikitumbuiza kwenye hafla ya ufunguzi wa Jengo la Makaazi ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji Chake Chakle Pemba.

BALOZI DR. KAMALA ATEMBELEA KISIMA CHA MAJI CHA KATA MABALE AMBACHO KIMEACHA KUTOA MAJI

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AWASILI MKOANI RUVUMA KWAZIARA YA KIKAZI

UVCCM LONGIDO YATOA MSAADA KWA WATOTO YATIMA

Kushoto ni Katibu wa UVCCM wilaya ya Longido Isaya Karakara, Katibu Hamasa wa UVCCM mkoa wa Arusha Neema Emmanuel na Mjumbe Baraza Kuu UVCCM Mkoa wa Arusha Robert Kaseko w akikabidhi msaada kwa Mmiliki wa kituo cha kulelea Watoto yatima cha Masai Foundation Joyce Kabati
Kushoto ni Katibu wa UVCCM wilaya ya Longido Isaya Karakara, Katibu Hamasa wa UVCCM mkoa wa Arusha Neema Emmanuel na Mjumbe Baraza Kuu UVCCM Mkoa wa Arusha Robert Kaseko w akikabidhi msaada kwa Mmiliki wa kituo cha kulelea Watoto yatima cha Masai Foundation Joyce Kabati

                                                                      Habari picha na Woinde Shizza,Arusha.

Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Longido umetembelea kituo cha Watoto yatima na Wanaoishi katika mazingira magumu cha Masai Foundation kilichopo mji mdogo wa Namanga na kutoa msaada wa vyakula pamoja na vifaa mbalimbali.

Mjumbe Baraza Kuu UVCCM Mkoa wa Arusha Robert Kaseko Amesema kuwa wameamua kushirikiana na jamii katika kusaidia watoto ikiwa ni moja kati ya michango wanayoitoa ili kutosheleza mahitaji muhimu yanayohitajika katika kituo hicho.

Robert Amesema kuwa jukumu la kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu ni la kila mwanajamii hivyo jamii inapaswa kujitoa kusaidia watoto hao.

Katibu Hamasa wa CCM mkoa wa Arusha Neema Emmanuel amesema kuwa vijana hao wameamua kujitoa kutoa msaada kwa jamii ili kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu hivyo ameiomba jamii kujitokeza kwa wingi kuwasaidia watoto hao.

“Hawa ni watoto wetu sote kila mtu anapaswa kuona kuwa ana jukumu la kuwasaidia hawa watoto ili waweze kufanikisha ndoto zao” Neema

Katibu wa UVCCM wilaya ya Londigo Isaya Karakara na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya Tulli Lemanga aliyejitolea kuwakatia bima ya afya watoto wanaolelewa katika kituo hicho wamesema kuwa vijana hao wataendelea na utamaduni huo mara kwa mara katika kuunga mkono juhudi za serikali katika kutatua changamoto za watoto.
 
Mmiliki wa kituo hicho Joyce Kabati amewashukuru vijana hao kwa kutembelea watoto hao jambo ambalo linaleta faraja kwa watoto hao ambao na wanamahitaji mbalimbali ambayo yamewasilishwa na vijana hao.


Mbunge Lwakatare wa CHADEMA Ammwagia Sifa Rais Magufuli






Serikali Yafuta Posho Za Vitafunwa, Mazingira Magumu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya posho mbalimbali zisizokuwa za kisheria zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Ametia agizo hilo leo (Jumanne, Januari 3, 20017) wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi.

“Kuanzia sasa marufuku Wakurugenzi kutoa posho zisizotambulika kisheria zikiwemo za mazingira magumu, kujenga uwezo na vitafunwa katika halmashauri zenu na badala yake fedha hizo zitumike kwenye miradi ya maendeleo,” amesema.

Agizo hilo litawezesha Jiji la Dar es Salaam kuokoa sh bilioni 130 zilizokuwa zitumike na Halmashauri na Manispaa za jiji hilo, ambazo kwa sasa zitaingizwa kwenye miradi na shughuli za maendeleo.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma nchini kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuacha kutumia fedha kinyume cha utaratibu na watakaobainika Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali za kisheria.

“Katika halmashauri zetu kila mtumishi anashiriki katika ukusanyaji wa mapato hadi walinzi, lakini mwisho wa siku vitafunwa huliwa na wachache wanaojiita wakubwa huku wengine wakisikilizia kwa nje. Jambo hili haliwezekani,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesisitiza kwamba Mkurugenzi yeyote atakayebainika kulipa posho hizo baada ya siku ya leo atakuwa amejifukuzisha kazi.

Aidha, ameagiza fedha zilizokuwa zikitolewa kwa madiwani kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo zisitolewe moja kwa moja kwa madiwani na badala yake zipelekwe kwenye kata husika na zifuatiliwe matumizi yake.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amezionya halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa kila fedha zinayopelekwa kwenye halmashauri hizo inatumika kama ilivyokusudiwa na atakayebainika kutumia kinyume hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Pia amewataka watumishi wote wa umma nchini kuwajibika ipasavyo na kuhakikisha wanawatumikia vyema mwananchi ikiwa ni pamoja na kuepuka vishawishi na kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na ufisadi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa siku tatu kwa watumishi 10 wa halmashauri hiyo ambao wamehamishiwa kutoka wilaya ya Temeke wawe wameripoti katika Manispaa hiyo, vinginevyo watakuwa wamejifukuzisha kazi.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Bw. Hashim Mgandilwa wakati akiwasilisha taarifa ya wilaya hiyo kwa Waziri Mkuu, alisema hadi sasa asilimia 98 ya watumishi waliotakiwa kuhamia kwenye halmashauri hiyo wameripoti isipokuwa 10 na hakuna taarifa zozote juu yao.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


EWURA yatangaza bei mpya za mafuta

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (EWURA)  imetangaza bei mpya za nishati ya mafuta zitakazoanza kutumika kesho Jumatano huku bei ya mafuta ya taa na dizeli ikiwa imeshuka kwa wastani wa shilingi 66 kwa lita.

Taarifa iliyotolewa na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Felix Ngamlagosi inaonesha kuwa kwa wastani kumekuwa na ongezeko dogo sana la bei ya mafuta ya petroli ambayo kwa jiji la Dar es Salaam bado itauzwa kwa bei ile ile ilivyokuwa mwezi uliopita.

Hata hivyo, taarifa hiyo imetoa ruhusa kwa wauzaji wa jumla na rejareja wa mafuta nchini kuuza bidhaa hiyo kwa bei ndogo chini ya bei elekezi iliyotangazwa na mamlaka hiyo kama njia ya kuchochea ushindani baina ya wauzaji wa mafuta nchini.


Utata Wagubika Mauaji ya Afisa Mtendaji Mbeya

Mwili wa ofisa mtendaji wa mtaa wa Kabwe, katika kata ya Iyela jijini Mbeya Clementine Enock (34) umekutwa ukiwa umetelekezwa katika eneo la Airport ya zamani baada ya kuuawa na watu wasiofahamika kwa kubanwa pumzi.

Kamanda wa polisi mkoani Mbeya Dhahiri Kidavashari alisema jana kuwa walibaini kuwepo kwa mwili huo Januari mbili, mwaka huu majira ya saa moja asubuhi baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Kidavashari alifafanua kuwa kabla ya tukio hilo marehemu aliondoka nyumbani kwao siku ya Mwaka mpya  na kuaga kuwa anakwenda Airport kwenye sherehe ya rafiki yake huku akiwa na gari yenye namba za usajili T234 DJM aina ya Toyota Spacio.

Alisema kuwa ndugu wa marehemu walipata hofu mara baada ya ndugu yao kuchelewa kurudi nyumbani na ndipo wakaanza kumpigia simu bila mafanikio mpaka usiku wa manane.

“Marehemu aliaga nyumbani kwao Uyole ya Kati alikokuwa akiishi majira ya saa kumi jioni siku ya tarehe moja kwa madai anaenda kwenye sherehe ya rafiki yake akiwa na usafiri wa gari lake, ambapo mpaka kufika usiku wa manane hakukuwa na taarifa yeyote ndipo hofu ikatanda kwa familia ambapo walipiga simu kwa ndugu jamaa na marafiki na kueleza kuwa hawajui alipo,” alisema Kidavashari.


Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari siku iliyofuata majira ya saa moja asubuhi mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umetupwa katika eneo la wazi jirani na Shule ya Sekondari ya Samora ambapo uchunguzi wa awali unaonesha kifo chake kilitokana na kubanwa pumzi na watu wasiofahamika.

Alisema mazingira ya kifo yanaonyesha wazi kuwa marehemu aliuawa na mtu wa karibu yake huku akisema tukio hilo lilifanywa ndani ya nyumba ya mtu.

TCRA Yatishia Kuzifutia Leseni Kampuni za Simu


Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) imetishia kusitisha kwa muda au kufuta kabisa leseni ya biashara kwa kampuni zote za mawasiliano nchini, zitakazoshindwa kujisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE)

Hatua hiyo ni kulingana na sheria mpya ya fedha ambayo imetoa ukomo wa hadi Desemba 31 mwaka jana kampuni hizo ziwe zimejisajili katika soko hilo.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam hii leo; Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Mhandisi James Kilaba amesema kwa sasa wanasubiri maelezo kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana  (CMSA) kuhusu idadi ya kampuni za mawasiliano zilizokidhi sifa za kusajiliwa katika soko la hisa kwa ajili ya kuchukua hatua kwa zile zilizokaidi kutekeleza agizo hilo la kisheria.

Mhandisi Kilaba amesema TCRA imeikabidhi CMSA orodha ya kampuni zaidi ya 80 za mawasiliano, orodha ambayo CMSA itaipitia kwa lengo la kuchuja na kupata kampuni ambazo zinastahili kujisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Kauli ya Mhandisi Kilaba imekuja huku taarifa kutoka soko la Hisa la Dar es Salaam zikionesha kuwa ni kampuni tatu pekee ndizo zimejisajili katika soko hilo, licha ya muda wa kufanya hivyo kufikia ukomo wake Jumamosi ya Desemba 31 mwaka jana.

Serikali kuajiri walimu 4000 wa masomo ya Sayansi na Hisabati.........Wale wa Maomo Mengine Watulie Maana Hakuna Uhaba Kwa Sasa

Serikali imesema ipo kwenye mchakato wa kuajiri walimu 4000 wa masomo ya Sayansi na Hisabati.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwa katika ziara yake ya kutembela wilaya mpya za jiji hilo, akianzia na Kigamboni siku ya leo.

Majaliwa amesema mchakato wa ajira hizo unaendelea chini ya Ofisi ya Rais Utumishi, na muda wowote kutoka sasa mchakato huo utakapokamilika, majina yatatolewa na walimu hao kuajiriwa.

Kuhusu walimu wa masomo mengine, Waziri Mkuu amesema walimu wa masomo mengine hususani ya sanaa wapo wa kutosha na kwamba wanapaswa kusubiri kwakuwa wao wako wengi zaidi na hakuna uhaba na uhitaji wa walimu hao wa masomo ya sanaa.

Hivi karibuni, Wizara ya Elimu iliwataka wahitimu wa ualimu katika masomo ya sayansi na hisabati kutuma taarifa (CV) zao ili izihakiki kabla ya ajira, mchakato ambao tayari umekamilika na majina yalitumwa katika wizara ya utumishi.

Naibu Waziri wa Elimu, Mhandisi Stella Manyanya wiki mbili zilizopita wakati akiongea na kituo cha EATV alisema kuwa kazi ya wizara yake ilikuwa ni kuhakiki taarifa za wahitimu hao, na si kuajiri, huku akibainisha kuwa zoezi hilo limekamilika na majina yako utumishi ambao ndiyo watahusika na kuajiri.

Pia alisisitiza kuwa kama wizara ya elimu waliomba kupewa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati haraka kwa kuwa uhitaji wao ni mkubwa zaidi na kuwataka wahitimu wote waliotuma taarifa zao, wasubiri watapata majibu muda si mrefu.

Wednesday, January 4, 2017

Polisi kufukua kaburi la binti aliyezikwa kwa siri Arusha

Familia moja  jijini Arusha inadaiwa kumzika kwa siri mtoto wao mdogo wa kike wa miaka mitatu katika kaburi lililofichwa, huku majirani wakidanganywa kuwa binti huyo yupo hai.

Taarifa za kisa hicho cha kusikitisha zimevifikia vyombo vya usalama. Kwa sasa kuna mipango ya kuhakikisha kuwa mwili wa binti huyo, Nuru Losipha aliyezikwa kwa siri na familia yake, unafukuliwa kwa uchunguzi zaidi.

Inadaiwa kuwa Losipha alipoteza maisha wakati akifanyiwa tohara au ukeketaji na ngariba, ambaye jina lake halikufahamika mara moja, huku familia yake ikishuhudia.

Kitendo hicho kilifanyika katika kijiji cha Engutoto Kata ya Mwandeti wilayani Arumeru Desemba 28, mwaka jana, zikiwa zimebaki takriban siku tatu tu, kabla ya mtoto huyo aliyekuwa na umri wa miaka mitatu tu, hajaingia mwaka mpya wa 2017.

Mtendaji wa Kata ya Mwandeti, Njivaini Kivuyo awali alikuwa amepitwa na taarifa hizo hadi vyombo vya habari vilipotinga kijijini hapo kwa uchunguzi na ndipo alipolazimika kwenda kuripoti tukio hilo kwenye kituo cha Polisi cha Ngaramtoni.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Charles Mkumbo aliapa kuwa liwalo na liwe na kwamba ikiwezekana kaburi litafukuliwa ili mwili wa malaika huyo asiye na hatia, uchunguzwe upya.

“Ndio kwanza nazipata hizi taarifa, na kama polisi tutaomba kibali cha mahakama ili twende kulifukua kaburi husika tujiridhishe kama kweli mtoto huyo amezikwa humo na iwapo tutaukuta huo mwili, basi tutaanza uchunguzi juu ya kifo chake,” alisema Kamanda arles Mkumbo.

Baba wa marehemu, Losipha Kaiser anadai kuwa mtoto wake alifariki kutokana na ugonjwa wa baridi yabisi na kwamba aliugua kwa kipindi kirefu kabla ya kupoteza maisha Desemba 28, mwaka jana. Lakini madai yake hayo yanapingana na ripoti ya muuguzi katika duka la dawa lililopo kijiji cha jirani cha Kidali, anayeitwa Jane Andrew.

“Walimleta mtoto hapa walitaka nimsaidie tiba, lakini tayari huyo binti alikuwa amezimia na kutokwa na damu nyingi,” alidai.

Muuguzi huyo aliwahimiza wamkimbize mtoto hospitali, na hakufahamu nini kiliendelea hadi ripoti za kifo zilipomfikia.

Huku serikali ikipiga marufuku vitendo vya ukeketaji kwa wasichana, bado kuna familia nyingi kwenye mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa, zinaendeleza mila hiyo kwa siri.

Kwa sasa familia hizo zimegundua mbinu mpya ya kuwatahiri watoto wa kike wakiwa wadogo sana, kuepuka kukamatwa.

Ngariba wanaotumika kukeketa watoto, mara nyingi ni akina mama vikongwe wasiokuwa na ujuzi, taaluma za afya na hutumia vifaa butu, ambazo husababisha uvujaji mwingi wa damu na kuwa chanzo cha maambukizi ya magonjwa mengine.

Wednesday, January 4, 2017

Mlinzi mwingine auawa Geita....Aliyepigwa na wafugaji Morogoro Afariki Dunia

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi
 Mauaji ya walinzi mkoani Geita yamendelea kuwa tishio kwa usalama wao baada ya mlinzi mwingine aliyekuwa akilinda maduka yapatayo 15, kuuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani. 

Mauaji ya mlinzi huyo Kisusi Iddy (40) aliyekuwa akilinda maduka hayo kwenye Mtaa wa Mwatulole, ni muendelezo wa matukio ya kuuawa walinzi wa maduka na mali mbalimbali kwani katika kipindi cha miaka miwili  jumla ya walinzi 20 wameuawa. 

Taarifa zilizopatikana jana kuhusu mauaji ya mlinzi huyo na kuthibitishwa na mwenyekiti wa mtaa huo, Fikiri Toi zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Januari Mosi na wauaji hao hawakuiba kitu chochote. 

Mwili wa Iddy ulikutwa umefunikwa kwa shuka lake alilokuwa akilitumia lindoni, huku likiwa limetapakaa damu. 

Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama amefuta vibali vyote vya waganga wa tiba za asili kwa madai wao ni moja ya chanzo cha imani za kishirikina zinazosababisha mauaji hayo.

 Alisema kutokana na kukithiri kwa mauaji hayo, mamlaka yake inakusudia kufufua Jeshi la Jadi (Sungusungu) ili kusaidia kuyadhibiti. 

Hata hivyo, Kapufi alisema uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa wakati wa uhai wake, Iddy alikuwa analinda maduka ya wafanyabiashara yanayofikia 15 na kwamba baada ya kufuatilia, hakuwa na mafunzo yoyote ya ulinzi.

 Aliyepigwa na wafugaji Moro afariki 
Fabian Bago (21) anayedaiwa kushambuliwa na wafugaji katika Kijiji cha Kolelo, Morogoro, amefariki dunia katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro alikokuwa akipatiwa matibabu. 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Frank Jacob alisema kijana huyo alifariki dunia saa 11 jioni jana akiwa kwenye wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu na kwamba mwili wake umehifadhiwa kusubiri taratibu nyingine za kipolisi.

 Dk Jacob alisema mara baada ya kufikishwa hospitalini hapo, kijana huyo alifanyiwa vipimo na matibabu lakini alifariki dunia kutokana na majeraha makubwa kichwani yaliyoharibu sehemu ya ubongo. 

Baba mzazi wa kijana huyo, Alan Bago alisema ameshatoa taarifa polisi kuhusina na kifo cha kijana wake na sasa anasubiri maelekezo ya polisi ili aweze kuendelea na taratibu za mazishi. 

Wednesday, January 4, 2017

Zitto Kabwe Adai Kuna Uhaba Mkubwa wa Chakula Nchini.........Waziri wa Kilimo Ampinga

Wakati Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe akidai kuwa hali ya chakula nchini siyo nzuri kutokana na uhifadhi mbaya, Serikali imesema hali ni shwari licha ya baadhi ya maeneo kutopata mvua za wastani. 

Zitto alidai jana kuwa Ghala la Taifa la Chakula (SGR) lina hifadhi ya chakula kinachotosha kwa siku nane tu wakati Novemba 2015 kulikuwa na chakula cha kutosha miezi miwili. 

Kwa mujibu wa Zitto, taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Novemba inaonyesha kuwa Mamlaka ya Taifa ya Hifadhi ya Chakula (NFRA), imebaki na tani 90,476 tu za chakula ambacho amedai ni cha kutosholeza siku nane.

 Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alijibu madai hayo ya Zitto akisema nchi ina chakula cha kutosha wala siyo cha siku nane wala mwezi pekee, bali zaidi. 
Dk Tizeba alisema NFRA inakuwa na akiba ndogo kwa kuwa mwaka 2016 ndiyo ambao nchi ilipata mavuno makubwa ya tani milioni 16 ambazo hazikuwahi kutokea, hivyo maghala ya watu bado yana akiba kubwa ya chakula hivyo wakala haukununua chakula kingi. 

“NFRA inanunua chakula kwa kuangalia mahitaji kwa mwaka huo ukoje, watu wakivuna sana maghala yao yanakuwa yamejaa na mahitaji ya chakula yanakuwa madogo ndiyo maana Serikali hainunui chakula kingi. Miaka miwili iliyopita Serikali ilinunua mahindi kwa wingi lakini yaliishia kuharibika,” alisema Dk Tizeba. 

Aliongeza kuwa Serikali sasa ina mradi wa kujenga ghala jingine lenye uwezo wa kuhifadhi tani 260,000 ili likiungana na la sasa lenye uwezo wa tani 246,000 nchi iwe na uwezo wa kuhifadhi tani zaidi ya 500,000. 

“Kuna maeneo mahindi yameanza kukomaa na wakulima wa huko watavuna kama kawaida, tunachokifanya tutadhibiti uuzaji wa chakula nje ya nchi bila vibali ili chakula kisambae zaidi kwa Watanzania. Japo siwezi kutaja kiasi cha chakula kilichopo kwa sababu za kiusalama, ila kinatosha siyo kwa siku nane wala mwezi mmoja bali ni zaidi,” alisema Tizeba. 

Juzi wakati akihutubia mkutano wa kampeni za udiwani katika kata ya Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, Zitto alisema kauli ya Rais John Magufuli kwa wananachi wa Mkoa wa Kagera kwamba Serikali haina shamba ni kuficha uamuzi unaosababisha kukosekana kwa akiba ya chakula ya kutosha. 

Alidai kuwa hali ya chakula nchini si nzuri, wananchi wanashuhudia namna bei za vyakula zinavyopanda kila siku akidai kuwa bei ya sembe na mchele zimekuwa juu na gharama za maisha zitaendelea kupanda kutokana na uhaba wa chakula kuwa mkubwa.

 “Hali ya chakula inazidi kuwa mbaya kwa sababu ya maamuzi mabovu ya Serikali kuhusu hifadhi ya chakula. Serikali zote zilizopita huko nyuma zilikuwa zinanunua chakula cha akiba ili wakati wa ukame kama sasa chakula hicho kiingie sokoni, hivyo kushusha bei na kuwezesha wananchi kumudu gharama za chakula,” alisema Zitto. 

Aliongeza kuwa mpaka sasa NFRA ina tani 90,476 za chakula wakati kipindi kama hicho mwaka 2015 ghala la chakula lilikuwa na tani 459,561. 

Takwimu alizozitoa Zitto Kabwe alizinukuu katika ripoti ya BoT ya Novemba mwaka jana ambayo inaonyesha kuwa tangu Januari 2016 hadi Julai 2016, akiba ya chakula ilipungua kutoka tani 125,668 hadi 49,632, lakini hadi Oktoba mwaka huo iliongezeka hadi 90,476. 

Ripoti hiyo inaonyesha tofauti ya uhifadhi wa chakula kwa mwaka jana na miaka mingine miwili iliyotangulia kwani mwaka 2014 Januari, kulikuwa na tani 235,309 na Desemba, tani 466,583 huku mwaka mwaka 2015 Januari kukiwa na tani 459,561 na Desemba 180,746. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata), Steven Ruvuga alisema hali halisi kwa wakulima siyo nzuri kwa kuwa mvua zilinyesha chini ya kiwango, hivyo kuna hofu ya ukosefu wa chakula cha kutosha baadaye. 

“Sasa hivi nipo Kiteto na kwa kawaida mahindi yalipaswa kuwa tayari yameinuka kufikia walau mabega ya mtu mzima, lakini nikiyatizama sasa bado yako chini. 

"Mwaka huu kuna hatari ya ukosefu wa chakula na naishukuru Serikali kwa kuwa imeanza kuchukua hatua katika maeneo yenye uhitaji,” alisema Ruvuga. 

Aliongeza kuwa Ghala la Taifa linapaswa kuwa na wastani wa tani 300,000 za akiba lakini kama sasa zipo 90,476 zinaweza zisikidhi mahitaji ya kila mtu hivyo ni vyema ikabuni mpango mbadala.
 
HABARI ZA JUUMATANO HII HABARI ZA JUUMATANO HII Reviewed by RICH VOICE on Januari 04, 2017 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...