SUNDAY NEWS 01/01/2017

SHEREHE ZA MWAKA MPYA ZAFANA JIJINI LONDON

Sherehe za kuukaribisha mwaka mpya jijini London zimefana na kupambwa na fataki za rangi tofauti, wakati watu katika sehemu mbalimbali duniani wakifurahia mwaka mpya.

Watu milioni moja walikusanyika Jijini London kushuhudia fataki zenye rangi tofauti zikiupamba mji huo mkuu wa Uingereza.
Jumla ya fataki 12,000 zilipamba anga la London, ambapo mwaka mpya ulichelewa kuingia kwa sekunde moja kutokana na kupungua kwa kasi ya mzunguko wa dunia.
Watu waliokuwa wamekusanyika Jijini London kungojea kuukaribisha mwaka mpya

Jumapili, 1 Januari 2017

RAIS DKT. MAGUFULI ASHIRIKI IBADA YA JUMAPILI YA MWAKA MPYA KATIKA KANISA KUU JIMBO KATOLIKI LA BUKOBA MKOANI KAGERA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba Desiderius Rwoma mara baada ya kuwasili katika Kanisa Kuu la Jimbo katoliki Bukoba mkoani Kagera.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akibusu mkono wa Askofu Msaidizi Jimbo Katoliki la Bukoba Askofu Methodius Kilaini mara baada ya kuwasili katika Kanisa Kuu la Jimbo katoliki Bukoba mkoani Kagera kwa ajili ya Ibada.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akielekea katika katika Kanisa Kuu la Jimbo katoliki Bukoba mkoani Kagera mara baada ya kuwasili na kupokewa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba Desiderius Rwoma (katikati) pamoja na Askofu Msaidizi Jimbo Katoliki la Bukoba Askofu Methodius Kilaini wa kwanza (kulia)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika ibada ya mwaka mpya katika Kanisa Kuu la Jimbo katoliki Bukoba mkoani Kagera.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika ibada ya mwaka mpya katika Kanisa Kuu la Jimbo katoliki Bukoba mkoani Kagera.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba Desiderius Rwoma mara baada ya Ibada.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na waumini wa Kanisa Kuu la Jimbo katoliki Bukoba mkoani Kagera mara baada ya Ibada.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisali katika kaburi la Marehemu Kadinali Rugambwa mara baada ya Ibada kanisani hapo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimshukuru Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba Desiderius Rwoma mara baada ya kushiriki Misa ya Mwaka mpya kanisani hapo. Katikati ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba Askofu Methodius Kilaini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisaini kitabu cha Wageni Kanisani hapo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba Desiderius Rwoma kushoto pamoja na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba Askofu Methodius Kilaini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na masista kanisani hapo mara baada ya Ibada. PICHA NA IKULU 
 

Jumapili, 1 Januari 2017

BALOZI SEIF AUKARIBISHA MWAKA MPYA 2017 KWA KUITAKA JAMII KUENDELEA KUSHIRIKIANA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akijumuika pamoja na baadhi ya Viongozi na watendaji wa Ofisi yake kwenye chakula alichokiandaa nyumbani kwake hapo Mtaa wa Kama kwa ajili ya kuuaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka Mpya wa 2017.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akijichagulia mlo kwenye tafrija ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2017.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mahsriki, Kikanda na Kimataifa Balozi Ramadhan Muombwa naye hakuwa nyuma kushiriki kwenye tafrija hiyo.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Idara zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakitunisha misuli katika tafrija hiyo ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2017.
Wa kwanza kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa shughuli za SMZ na SMT Nd. Khalid Bakari Amrani, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Nd. Ali Juma Hamad na Mkurugenzi wa Idara ya Sherehe na maadhimisho ya Kitaifa Bibi Riziki Daniel Yussuf.

Baadhi ya washiriki wa hafla hiyo wakifurahia chakula kitamu kilichotayarishwa kwenye Tafrija hiyo ya usiku.
Familia ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ikionekana kupozi kwenye tafrija hiyo wakifuatilia muziki laini uliokuwa ukitumbuiza katika Tafrija hiyo.
Balozi Seif Ali Iddi, Mkewe pamoja na Familia yao wakisakata rumba kwenye tafrija ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2017 nyumbani kwao Mtaa wa Kama.
Olaaaaaaaa. Ndii. Ni wakati wa kuingia saa 6 na dakika moja ya usiku wa kuingia mwaka mpya wa 2017 washiriki wa tafrija hiyo wakijimwaga uwanjani kuukaribisha mwaka huo.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma Nhunga akitoa shukrani kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa washiriki wa Tafrija ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2017.

                                                                                                    Picha na – OMPR – ZNZ.
 

Jamii imeaswa kuendelea kushirikiana katika harakati zao za kila siku za kimaisha na Kifamilia ili kukifanya kizazi chao kukua katika maadili na utamaduni unaokubalika kidini na kidunia jambo ambalo litatoa faraja kwa wazazi, walezi pamoja na Viongozi wa Kitaifa.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma Nhunga wakati wa hafla maalum ya kuuaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka Mpya wa 2017.

Mh. Mihayo alisema hayo kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyeandaa hafla hiyo Nyumbani kwake Mtaa wa Kama nje kidogo ya Kaskazini Magharibi ya Mji wa Zanzibar akiwashukuru baadhi ya Viongozi na Wafanyakazi wa Ofisi hiyo pamoja na Familia zao walioshiriki katika kuukaribisha mwaka mpya.

Katika kuuaga mwaka 2016 uliobeba matukio mbali mbali yakiwemo mengi ya udhalilishaji wa Kijinsia ya yale yaliyopoteza maisha ya Wananchi wengi kutokana na ajali za bara barani, Naibu Waziri Mihayo alisema suala la kupendana miongoni mwa Jamii ndani ya mwaka mpya wa 2017 linafaa kufanywa kuwa jambo la msingi.

Kupitia hafla hiyo ya chakula cha usiku Mhe. Mihayo Juma Nhunga kwa Niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwatakia kheir ya mwaka Mpya Wananchi wote wa Zanzibar na kuwataka wale waliokoseana ndani ya mwaka uliopita wasameheane.

Alisema Mwaka mpya unahitaji zaidi mambo mapya na ya msingi ili kulifanya Taifa na wananchi wake waelekee kwenye maendeleo yatakayoleta faida na kustawisha maisha yao ya kila siku.

Hafla hiyo ya chakula cha usiku uliyowakutanisha baadhi ya Viongozi na watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Familia zao iliambatana na muziki laini uliotoa burdani safi kwa washiriki hao walioshindwa kukaa kwenye viti vyao na kuonekana wakianza kuserebuka.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar 
1/1/2017.  
 

Jumapili, 1 Januari 2017

ASKOFU MOKIWA AWAONGOZA WAUMINI WAKE KUTOA MSAADA NA KUFANYA USAFI HOSPITALI YA MWANANYAMALA JIJINI DAR ES SALAAM

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dk.Valentino Mokiwa (katikati), akiwaongoza waumini wa kanisa hilo Archidikonari ya Kinondoni kufanya usafi katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala Dar es Salaam leo asubuhi wakati kanisa hilo lilipotoa msaada wa vitanda na magodoro katika hospitali hiyo vyote vikiwa na thamani ya sh.milioni 12.
                                           Waumini wa kanisa hilo wakiendelea na kufanya usafi.
                                                                       Takataka zikipelekwa eneo maalumu.
                                                                                    Takataka zikipelekwa kutupwa.
                      Waumini wa kanisa hilo wakipiga picha mbalimbali za tukio hilo.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk.Valentino Mokiwa (kulia), akipanda mti nje ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala, wakati alipowaongoza waumini wa kanisa hilo kutoa msaada wa magodoro na vitanda vya wagonjwa pamoja na kufanya usafi wa mazingira Dar es Salaam leo asubuhi. Kushoto anayemsaidia kupanda mti ni Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dk.Daniel Nkungu na wengine ni waumini wa kanisa hilo.
 Kiongozi wa kanisa hilo wilaya ya Kinondoni Achidikin Con Mathew Maigwa (kulia), akipanda mti.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dk. Daniel Nkungu (kulia), akipanda mti.
 Ofisa Afya wa Hospitali hiyo, Amina Pole (kushoto),
akipanda mti.
 Waumini wa kanisa hilo na viongozi wao wakiwa kwenye
tukio hilo.
 Askofu Dk. Valentino Mokiwa akimkabidhi moja ya kitanda kati ya 15, Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Daniel Nkungu.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Daniel Nkungu akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Serikali baada ya kupokea msaada huo.
                                                                                                           Na Dotto Mwaibale

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Angilikana Tanzania, Dk Valentino Mokiwa amesema migogoro ya kisiasa inayoibuka hivi sasa inaweza kuhatarisha
hali ya amani nchini.

Dk. Mokiwa ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam leo wakati akiwaongoza waumini wa kanisa hilo Archidikonari ya Kinondoni kutoa misaada ya vifaa tiba na kufanya usafi wa mazingira katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala.

“Migogoro ya kisiasa ambayo imeanza kuzuka hivi sasa inaweza kuhatarisha amani ya nchi ni vizuri viongozi wanaovutana wakutana na kuweka mambo sawa” alisema Mokiwa.

Alisema migogoro ya kisiasa inayoendelea inaweza kusababisha kutoweka kwa amani hivyo ni jukumu la viongozi husika kuliangalia jambo hilo kwa karibu na kulitafutia ufumbuzi.

Alisema nchi yetu inahitaji amani na utulivu na kuondokana na matukio ya kuogopesha akitolea mfano miili ya watu saba iliyokutwa ndani ya viroba vilivyotupwa mto Ruvu Bagamoyo mkoani Pwani.

Alisema matukio kama hayo yanaweza kuwafanya wananchi kukimbia nchi yao kwa hofu hivyo inatakiwa kila mmoja wetu kuwa na hofu ya mungu.
 

Akizungumzia msaada uliotolewa na kanisa hilo katika hospitali hiyo ambao ni vitanda 15,magodoro 20, mashuka 40 na viatu vya tahadhri jozi 30 vyenye thamani ya Sh12 milioni alisema kanisa hilo kwa muda mrefu limekuwa likifanya maombi ya kuwaombea viongozi wa nchi na kutoa misaada ya kijamii hususan katika sekta ya afya, elimu na maeneo mengine.
Mokiwa alisema wananchi wanapokuwa katika afya bora ndipo wanapoweza kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo hivyo kuinua uchumi wao na
taifa kwa ujumla.

Mkuu wa kanisa hilo wilaya ya Kinondoni Achidikin Con Mathew Maigwa alitoa mwito kwa wadau wa maendeleo kote nchini kuwa na moyo wa kusaidia watu wenye uhitaji kama wanavyotoa michango ya harusi na sherehe nyingine.

Alisema ni jukumu la kima mmoja wetu wa kusaidia jamii na si
kuiachia serikali pekee na ndio maana kanisa hilo limekuwa likifanya hivyo kama neno la mungu linavyoelekeza kuwa tupendane kwani unapokwenda kumfariji mgonjwa inasaidia kumpa hali ya unafuu.

Akizungumza kwa niaba ya serikali na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dk. Daniel Nkungu alilishukuru
kanisa hilo kwa msaada huo na kusema inazidisha ari ya kazi kwa wafanyakazi na kuwafariji wagonjwa ikiwa na kuwafanya wapate nafuu na kupona haraka.

(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com)
 
 

Jumapili, 1 Januari 2017

UONGOZI WA SERIKALI YA MTAA WA MARUZUKU BUGURUNI JIJINI DAR ES SALAAM WATOA SARE ZA SHULE KWA WATOTO 200

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Maruzuku katika Kata ya Mnyamani Buguruni Manispaa ya Ilala, kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Jabiri Sanze (kulia), akimkabidhi sare za shule mtoto, Hamad Ali Dar es Salaamleo, ambaye ataanza darasa la kwanza mwezi huu. Serikali ya mtaa huo imetoa sare za shule, daftari na penseli kwa watoto 200 watakaoanza darasa la kwanza mwaka huu wa 2017. Katikati ni mama wa mtoto huyo, Farida Rashid.
Mtoto Issa Athumani akipokea msaada huo. Katikati mama yake Halima Issa.
Mtoto Asnat Mashaka akipokea msaada huo. Nyuma yake ni mama yake, Arat Hamisi
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mnyamani Jafari Mrisho (kushoto), akizungumza kwenye tukio hilo.
Katibu Kata wa Kata ya Mnyamani (CUF), Omari Simba (kulia), akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo.
        Wazazi na walezi wakiwa na watoto wao wakisubiri kupokea msaada huo.
                                              Vifaa hivyo vikiandaliwa kabla ya kukabidhiwa watoto.
                                                                   wazazi na walezi wakiwa kwenye hafla hiyo.
                                                                    wazazi na walezi wakiwa kwenye hafla hiyo.
Watoto na wazazi wao wakisubiri msaada huo.
                                                                                                          Na Dotto Mwaibale

SERIKALI ya Mtaa wa Maruzuku katika Kata ya Mnyamani Buguruni Manispaa ya Ilala kupitia Chama cha Wananchi (CUF), imetoa sare za shule kwa watoto 200 wanakaoanza darasa la kwanza mwezi Januari ili kuleta msukumo wa masomo katika mtaa huo.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa mtaa huo, Jabiri Sanze alisema wanaziunga mkono jitihada za Rais Dk.John Magufuli za kuhakikisha kila mwanafunzi anapata elimu bure na katika mazingira bora.

“Tumeamua kutoa msaada huu mdogo kwa watoto 200 waliopo katika mtaa wetu ili kutoa hamasa kwa wazazi na walezi kwani kipindi hiki cha mwezi Januari kinachangamoto kubwa na mahitaji mengi ya shule kwa wanafunzi” alisema Sanze.

Sanze alitaja msaada huo kuwa ni mashati ya shule, madaftari na penseli za kuandikia ambapo aliwaomba wazazi wasaidie eneo la sketi, kaputura, viatu na mabegi.

Alisema watoto walionufaika na msaada huo ni wavulana 86 na wasichana 114 wote kutoka katika mtaa wa Maruzuku.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mnyamani Jafari Mrisho aliupengeza uongozi wa mtaa huo kwa mpango huo wa kuwasaidia watoto hao wanaotarajia kuanza darasa la kwanza na akawaomba wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kusaidia ili kuwafikia watoto wote wa mitaa mitatu ya kata hiyo ambayo ni Mji Mpya, Mbarouk na Mnyamani.

Mjumbe wa mtaa huo Haroub Mussa aliwataka wazazi wa watoto waliopata msaada huo kutunza sare hizo na kuwa serikali ya mtaa itaendelea kushirikiana na wananchi na kuhakikisha watoto wote wanaopaswa kuanza darasa la kwanza wanakwenda shuleni.

                                  (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com)
 

Jumapili, 1 Januari 2017

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MWANDISHI WA HABARI KUFIKISHWA MAHAKAMANI KWA AGIZO LA DC KAHAMA

TAARIFA KWA UMMA

UONGOZI wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga (SPC),na baadhi ya waandishi wa habari wilayani Kahama,wamekutana na mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu ili kupata muafaka wa tatizo la kukamatwa na kufikishwa mahakamani mwandishi wa habari wa kujitegemea Paul Kayanda.

Kikao hicho cha usuluhishi kilichofanyika leo Jumamosi Desemba 31,2016 katika ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo,kimehudhuriwa pia na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Kahama.
 

Kayanda alikamatwa jana Desemba 30,2016 na kufikishwa mahakamani kwa agizo la Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu akimtuhumu kuandika habari za kumdhalilisha na kuzisambaza kwenye barua pepe mbalimbali za vyombo vya habari.

Katika kikao ,Uongozi wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga ,ulimuomba mkuu wa wilaya Nkurlu kutaka kufahamu kilichomsukuma kuchukua maamuzi hayo,na nini ushauri wake juu ya suala hilo lakini pia kumsikiliza mwandishi Paul Kayanda.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili,kikao kilibaini kuwepo kwa mapungufu katika habari iliyoandikwa na Kayanda kuhusu habari ya laptop mbili zilizoibiwa nyumbani kwa mkuu huyo wa wilaya.

Mkuu huyo wa wilaya alikiri kuwepo kwa tukio la wizi nyumbani kwake lakini mwandishi huyo aliandika habari kwa kuingilia uhuru binafsi wa kiongozi huyo akielezea watu wanaoingia na kutoka nyumbani kwake lakini maisha anayoishi na kijana wake.

Kwa kuangalia maslahi mapana ya umma kutokana na kutegemeana katika kusukuma maendeleo ya jamii baina ya uongozi wa serikali na waandishi wa habari ,kikao kimemtaka Kayanda kumwomba radhi mkuu huyo wa wilaya kwa kuingilia uhuru wake binafsi na kuuhusisha na habari ya wizi wa laptop badala ya kujikita kwenye tukio la wizi wa laptop pekee.

Kikao pia kimebaini kuwa pamoja na mapungufu ya mwandishi, ni ukweli ulio wazi kuwa mkuu huyo wa wilaya aliibiwa kompyuta mpakato (lap top) mbili nyumbani kwake na kuagiza vijana watatu wakamatwe kwa mahojiano polisi akiwemo mmoja anayeishi nyumbani kwake japo ameelezea kuwa hakujua walishikiliwa kwa siku ngapi.

Mkuu huyo wa wilaya pia alieleza kukerwa na ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia simu ya mkononi (sms) alizodai kutumiwa na Kayanda kwa kutumia simu nyingine (tofauti na anayotumia) zenye lugha ya kumtuhumu na kumdhalilisha.

Hata hivyo kikao hakikuona kuwepo kwa ushahidi wa moja kwa moja kuthibitisha kama ni za mwandishi huyo kweli au la huku kikao kikiomba sms hizo zifuatiliwe ili wamiliki wa namba hizo wajulikane .

Baada ya kujadiliana kwa kina katika kikao hicho kilichodumu kwa muda wa saa mbili,Kayanda amemwomba mkuu wa wilaya msamaha kwa mapungufu yaliyojitokeza katika habari hiyo aliyoiandika, na mkuu wa wilaya ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Kahama amekubali kumsamehe mwandishi huyo akiahidi kufuata taratibu zingine kuondoa kesi mahakamani na kutaka kusafishwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ilikoandikwa habari hiyo.

Nkurlu amesema anatambua kazi nzuri inayofanywa na waandishi wa habari wilaya ya Kahama na mkoa wa Shinyanga kwa ujumla katika kuandika habari zinazohusu serikali na akaomba kudumishwa kwa ushirikiano uliopo baina ya viongozi wa serikali na waandishi wa habari ili kusaidia kuharakisha maendeleo ya wananchi huku akiwasisitiza waandishi wa habari kuzingatia weledi katika kazi zao.

Aidha Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga imewasisitiza waandishi wa habari kuzingatia weledi na kufuata maadili katika kutekeleza majukumu yao ili kuepuka migongano isiyokuwa na tija kwa umma.

Pia tunawashauri wadau wote wa habari pindi inapotokea kuingia katika mgogoro wowote ama na waandishi wa habari au chombo cha habari si vyema kwenda mahakamani moja kwa moja bali wawasiliane na viongozi wa klabu za waandishi wa habari katika mkoa husika ili kusuluhishana na kuwekana sawa.

Imetolewa na

Kadama Malunde

MWENYEKITI –SPC


Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu,waandishi wa habari na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Kahama wakiwa katika kikao cha usuluhishi
Waandishi wa habari wakiwa katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kahama
Kikao kinaendelea
Waandishi wa habari wakiondoka katika ofisi ya mkuu wa wilaya baada ya kikao kumalizika
CHANZO NI RWEYUNGA BLOG

Agizo la Waziri Mkuu kwa walimu wanaoishi mbali na shule zao

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza walimu wanaishi mbali na shule wakati shule zao zina majengo wahame mara moja na warudi kuishi kwenye nyumba za shule.

Amesema haifai kuacha walimu waishi mbali na maeneo ya shule kwani hali hiyo inachangia uchelewaji kazini na inapunguza muda wa kuwasimamia wanafunzi au kuwasaidia jioni pale wanapohitajika kufanya hivyo.

Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Chingumbwa, kata ya Mbekenyera, wilayani Ruangwa Ijumaa, Desemba 30, 2016 kwenye mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi kijijini hapo.

“Nimeambiwa kuwa walimu wako wachache kwa sababu hapa shuleni hakuna nyumba za kuishi walimu. Mbona wanakaa Mbekenyera? Watawezaje kuwahi kazini asubuhi wakati hawana magari? Mvua ikinyesha watafikaje shuleni? Kuanzia leo, walimu wote warudi mara moja na waje kupanga hapa kijijini kwa sababu nyumba zipo,” alisisitiza.

“Uamuzi wa walimu kuishi jirani na shule ulifikiwa ili mwalimu awepo na kuwasimamia wanafunzi wakati wakifanya usafi na wakati mwingine aweze kutoa msaada kwa wanafunzi wanaojisomea jioni pindi wakihitaji msaada au ufafanuzi,” alisema.

Pia Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea Chezue asimamie zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anapunguza walimu walioko Ruangwa mjini na kuwahamishia shule za vijijini ambako kuna upungufu wa walimu.

Alisema ili kusaidia juhudi za Serikali za kuboresha elimu nchini, ni vema kila kijiji kikaweka utaratibu wa kuchangia matofali ili iwe rahisi kuanza ujenzi wa nyumba za walimu.

Akiwa katika kijiji cha Mkutingome, Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa aliwahamasisha wakazi wa kijiji hicho wachangie matofali 100 kutoka kila kaya ili yapatikane matofali 40,000 yatakayotumika kujenga zahanati ya kijiji hicho.

Yeye aliahidi kuwachangia mabati 150 ambayo kati yake, mabati 100 yatatumika kuezekea zahanati ya kijiji na mengine 50 yatatumika kukamilisha nyumba ya Mwalimu ambayo imekaa kwa muda mrefu bila kumaliziwa.

Katika kuhakikisha ujenzi wa zahanati hiyo unaanza mara moja, Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Wanyumbani Construction, Bw. Fakihi J. Bakili alichangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo ya kijiji cha Mkutingome. Nao Umoja wa Wachimbaji Wadogo katika mgodi wa Namungo ambao uko jirani na kijiji hicho waliahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
 

Sunday, January 1, 2017

Waziri Nchemba akutana na Mama wa Chid Benz.....Aeleza Alivyosikitishwa na Hali yake

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ameguswa na hali ya uathirika wa matumizi ya dawa za kulevya inayomtesa rapa Chid Benz na kulazimika kufika nyumbani kwao kuzungumza na mama yake mzazi.

Chidi Benz anayemiliki tuzo kadhaa za muziki alijikuta amenasa kwenye mtego wa matumizi ya dawa za kulevya ambao sio tu ulimuondoa kwenye maisha ya muziki bali pia uliidhoofisha afya yake na kuuondoa kabisa mwili wake wa ‘chuma’.

Kupitia akaunti yake ya Instagram, Waziri Nchemba ameeleza kusikitishwa na hali ya Chidi Benz na kutumia nafasi hiyo kuwataka wale wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kuacha mara moja kwani Serikali ya Awamu ya Tano imeazimia kupambana nao.

Hivi ndivyo alivyoandika:
Nimekutana na kufanya mazungumzo na mama wa msanii Rashid Makwilo “Chid Benz” ambaye kwasasa amepatwa na tatizo la Dawa za kulevya.Inasikitisha na haivumiliki kuona nguvu kazi ya Taifa inapotea huku wauzaji wakinufaika kwa pesa haramu.Ifahamike wazi vita ya serikali dhidi ya magenge, wauzaji na wasambazaji wa madawa ya kulevya imeongezeka hasa katika awamu hii ya tano chini ya Mh.Rais J.P.Magufuli,hivyo anayejihusisha kwa namna yoyote ni vema akaamua kuachana nayo kabla hajakutwa na mkono wa dola.

Mbali ya vyanzo vya taarifa tulivyonavyo,ni wajibu wa kila aliye RAIA MWEMA kutoa taarifa zitakazo saidia kuangamiza biashara haramu ya madawa ya kulevya.

Naishukuru familia ya Chid Benz kwa jitihada wanazozifanya kuhakikisha kijana mwenzetu anarejea katika hali yake ya kawaida.

Unaweza kuimba,unaweza kufanikiwa,unaweza kutatua matatizo yako bila kutumia madawa ya kulevya.
 
 

Sunday, January 1, 2017

Lowassa, Sumaye Wamtembelea Lema Gerezani

Maziri  wakuu wa zamani ambao ni wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa na Fredrick Sumaye, jana wamemtembelea Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema katika Gereza Kuu la Kisongo mjini Arusha.

Lowassa akiongozana na Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro ambaye pia ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, ndiye aliyekuwa wa kwanza kufika katika gereza hilo.

Calist alisema Lowassa alifika gerezani hapo saa tano asubuhi huku Sumaye aliyeongozana na Naibu Meya wa Arusha, Viola Lazaro akifika baadaye saa saba mchana.

Calist alisema Lowassa akizungumza na Lema, alimwambia kuwa mahakama ndiyo chombo pekee kinachoaminiwa na wananchi, hivyo kinapaswa kutenda haki kwa watu wote.

Alisema Lowassa aliridhishwa na afya ya Lema na kumtaka awe mvumilivu, hasa katika kipindi hiki anachokabiliwa na kesi na aliwataka wananchi wa Arusha Mjini kumwombea kiongozi huyo.

“Watanzania wana matumaini makubwa sana na mahakama, wanaamini chombo hiki pekee ndicho kitakachowapa haki yao, hivyo kwa mwaka 2017 mahakama itoe haki na kuendesha kesi bila upendeleo kwa sababu ndiyo sauti ya wanyonge, nakutakia amani na mwaka mpya mwema,” Calist alimnukuu Lowassa.

Kwa upande wake, Sumaye alisema kuwa alimtaka mbunge huyo kuwa jasiri katika kipindi hiki kwa sababu suala linalomkabili litafika mwisho.

“Mimi nilikuja tu kumsalimia, kumjulia hali ya afya yake kwa sababu Lema tangu amekaa huku gerezani nilikuwa sijapata nafasi ya kuja kumtembelea, kwa vile wakati huu niko katika maeneo haya ya Kaskazini, nikasema nije kumsalimia, afya yake nzuri na nimemuona hana wasiwasi, naona kabisa amekaa vizuri, ameelewa hiyo hali na amepokea, hana uso wa kusononeka na hilo limenipa moyo.

“Nimemwachia ujumbe ‘just be strong’ (awe jasiri), haya yote yatapita muda wake ukifika, suala lake liko mahakamani sio la kisiasa, hata kama lililomleta huku linahusiana na siasa, suala la dhamana tunatarajia litafika mwisho wake, lakini nimemwambia hata kama dhamana ikikosekana, bado kesi ya msingi itafika mwisho wake, asiwe na wasiwasi wala hamaki, awe jasiri asikate tamaa,” alisema.

Desemba 11, mwaka jana, Katibu wa Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, alimtembelea Lema katika gereza hilo na alimtia moyo aendelee na mapambano na kumtaka asikate tamaa ya kupigania haki za Watanzania.

Lema alikamatwa Novemba 2, mwaka jana akiwa nje ya Viwanja vya Bunge mjini Dodoma na kufikishwa mahakamani Novemba 11, mwaka jana akikabiliwa na kesi za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli na hadi wakati huo bado anashikikiwa mahabusu katika gereza hilo.

Januari 4, mwaka huu Mahakama Kuu Kanda ya Arusha inatarajia kutoa uamuzi wa rufaa namba 135 ya mawakili wa Serikali waliyokata kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha uliompa Lema dhamana, hata hivyo uamuzi huo haukuweza kutekelezwa kwa sababu ya nia ya kukata rufaa waliyoitoa mawakili hao wa Serikali.

Sunday, January 1, 2017

Waziri Muhongo Azuia Bei Mpya Ya Umeme

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kusitisha bei mpya ya umeme iliyotangazwa juzi na Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Felix Ngamlamgosi.

Taarifa ya kusitisha kwa bei hiyo ilitolewa jana na Profesa Muhongo kupitia barua yake kwa Ewura.

Muhongo amesema  kuwa amesitisha bei hiyo mpya kwa sababu nne, ikiwamo kutoshirikishwa katika mchakato huo akiwa ni waziri mwenye dhamana.

“Ewura walipokwenda mikoani Watanzania wote walipinga bei kupanda, wao wametumia kigezo kipi cha kupandisha? Pili taratibu zilizopo ni kwamba Tanesco wanapeleka maombi Ewura, kisha Ewura wanafanya zoezi hilo la kuuliza wahusika watumiaji wa umeme, baada ya hapo wanatengeneza ripoti wanaileta wizarani, na ningaliipata hiyo ripoti.

“Hivi tunavyoongea sijaipata mkononi, nikiipata nitaiita Ewura na Tanesco tunajadili na baada ya hapo ndipo wanaenda kutangaza. Wao wametangaza hata mimi taarifa nazipata kama wewe,” alisema Profesa Muhongo.

Katika sababu ya tatu ya kusitisha bei hiyo, Profesa Muhongo alisema hakuna ukweli kuwa kupandisha bei ya umeme kutasababisha Tanesco imalize matatizo yake kifedha.

“Tanesco kila mwaka inapandisha bei, mbona hawajajikwamua? Mbona madeni yanazidi kuongezeka? Nyingine ni kwamba tunakopa fedha kutoka nje ya nchi na watakaolipa hilo deni ni Watanzania wote, sasa hatuwezi kukopa kulipa madeni ya Tanesco halafu shukrani tutakayoipata ni kupandishiwa bei ya umeme tena.

“Nyingine nenda ufuatilie Tanesco wana matumizi mabaya ya fedha, nimesitisha zoezi lao, sijui kama hizo fedha wamerudisha, unajua wanapeana wale walioko juu bonasi kati ya Sh milioni 40 na milioni 60 kwa mwaka,” alisema Profesa Muhongo.

Alisema Ewura wanapaswa kupeleka ripoti ijadiliwe, kwani haiwezi kuwa Serikali ndani ya Serikali na haiwezi kupandisha bei bila waziri mwenye dhamana kujua kwa kuwa inapata bajeti kutoka bungeni.

Sunday, January 1, 2017

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumapili ya January 1, 2017


 
HABARI ZA KIMATAIFA
Polisi mjini Istanbul wameeleza kwamba idadi ya watu waliouwawa kwenye klabu moja ya usiku katika mji mkuu wa Uturuki, Istanbul imeongezeka. Hadi kufikia sasa watu 39 wameuwawa na wengine 70 wamejeruhiwa katika shambulizi liliyofanyika wakati wa mkesha wa mwaka mpya kwenye klabu maarufu ya mjini Istanbul inayoitwa Reina. Gavana Vasip Sahin amesema mshambuliaji mmoja aliingia ndani ya klabu hiyo baada ya kuwauwa kwa kuwapiga risasi polisi mmoja na raia mmoja waliokuwa mlangoni na hatimae akaanza kuwafyatulia risasi watu waliokuwa ndani ya klabu hiyo. Gavana huyo amesema analichukulia shambulio hilo kuwa ni la kigaidi. Hata hivyo baadhi ya vyombo vya habari nchini Uturuki vinaripoti juu ya watu zaidi ya mmoja ambao huenda wakawa wamehusika na shambulio hilo ambalo chanzo chake bado hakijajulikana. Uturuki inakabiliwa na visa vya mashambulizi kutokea mwaka uliopita. Serikali ya nchi hiyo imekuwa ikielekeza lawama zake kwa wafuasi wa Fethullah Gülen mpinzani wa rais Recep Tayyip Erdogan aliyeko uhamishoni. Makundi yenye msimamo mkali ya Kikurdi na vile vile kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS pia yanalaumiwa kuhusika na mashambulio nchini Uturuki.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja azimio la kuunga mkono juhudi za Urusi na Uturuki za kumaliza mgogoro wa Syria. Wajumbe wa baraza hilo wanaunga mkono juhudi za Moscow na Ankara za kutafuta amani kwa mujibu wa azimio lililopitishwa mjini New York na ambalo liliwasilishwa na Urusi. Mpango huo wa Urusi na Uturuki unatoa nafasi ya kufanyika mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Syria na wawakilishi wa makundi ya upinzani yaliyopangwa kufanyika katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana. Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa limetoa mwito wa kuharakisha ugawaji wa misaada ya kiutu na kwa watu wa Syria.
\
Waziri wa mazingira wa Burundi ameuwawa kwa kupigwa risasi. Waziri Emmanuel Niyonkuru aliyekuwa na umri wa miaka 54 alishambuliwa na mtu asiyejulikana wakati ambapo alikuwa akielekea nyumbani. Mauaji hayo yametokea kwenye maeneo ya Rohero katika mji mkuu wa Bujumbura. Msemaji wa polisi Pierre Nkurikiye ameeleza kwamba wanamshikilia mwanamke mmoja kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo. Mauaji hayo ni ya kwanza kutokea yanayomuhusisha mtu mwenye wadhfa wa juu serikalini katika muda wa miaka miwili wa machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini Burundi.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ametoa mwito kwa raia wa Ujerumani kuingia katika mwaka huu wa 2017 wakiwa na matumaini pamoja na ari ya kuushinda ugaidi. Hata hivyo Kansela Merkel amesema hatua za kiusalama ni za lazima. Katika hotuba yake ya mwaka mpya Kansela Angela Merkel alisema hakuna mashaka kuwa ugaidi unaofanywa na makundi ya watu wenye itikadi kali ni jaribio gumu kabisa kwa Wajerumani Merkel amesema serikali yake itaanzisha sheria zitakazolenga kurekebisha maswala ya usalama baada ya shambulio lililotokea kabla ya Krismasi katika mji wa Berlin.
 
Wawakilishi wa serikali na wa vyama vya upinzani katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametia saini makubaliano ya kutatua mzozo wa kisiasa yaliyosimamiwa na kanisa katoliki. Rais Joseph Kabila anatakiwa kuondoka madarakani baada ya uchaguzi utakaofanyika mwaka huu wa 2017. Kamati ya kijamii ya kanisa katoliki iliyoongoza mazungumzo hayo imethibitisha kufikiwa kwa mapatano hayo. Uchaguzi wa urais umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu na sio mwaka ujao wa 2018. Muhula wa pili wa rais Kabila ulimalizika tangu tarehe 20 mwezi Desemba mwaka 2016 uliomalizika hapo jana. Maandamano yaliyofanyika awali ya kumtaka rais kabila ajiuzulu yalizusha vurugu ambapo baadhi ya waandamanaji waliuwawa.


Italia inapanga kuwachukulia hatua kali zaidi wahamiaji ambao wamenyimwa kibali cha makaazi na wale waliofukuzwa. Mbali na vizuizi vinne vikuu Italia inapendekeza kujengwa vizuizi vingine 16 hayo ni kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani ya Rome. Aidha mkuu wa polisi Franco Gabrielli amewataka maafisa wa polisi waongeze jitihada za kuwasaka wahamiaji waliokataliwa hifadhi. Serikali mpya ya waziri mkuu Paolo Gentiloni inapanga kuanzisha sheria kali kuliko zilizowekwa na mztangulizi wake Matteo Renzi. Jumla ya wahamiaji elfu 27 walitakiwa waondoke nchini Italia lakini ni idadi ndogo ya chini ya wahamiaji 5,000 waliondolewa kwa mujibu wa idara inayosimamia takwimu za uhamijai Eurostat. Hadi kufikia mwaka jana wa 2016 zaidi ya wahamiaji laki moja na elfu themanini na moja waliingia Italia kupitia kwenye bahari ya Mediteranian.
 
Rais Mteule wa Marekani Donald Trump hajaondoa uwezekano wa kukutana na Rais wa Taiwan Tsai Ing-Wen iwapo atazuru nchini humo baada ya Trump kuapishwa Januari 20. Trump ameyasema hayo wakati wa mkesha wa mwaka mpya akiwa mapumzikoni mjini Florida ambapo pia aliendelea kuonyesha mashaka yake iwapo Urusi ilihusika na mashambulizi ya mtandaoni dhidi ya maafisa wa chama cha Democratic wakati wa mchakato wa uchaguzi wa mwaka jana.
CHANZO NI DW. 
SUNDAY NEWS 01/01/2017 SUNDAY NEWS 01/01/2017 Reviewed by RICH VOICE on Januari 01, 2017 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...