Saturday, August 27, 2016

Waziri Mkuu: Tanzania Iko Tayari Kujifunza Kutoka Nchi Nyingine.

SeeBait
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania iko tayari kujifunza kutoka kwa nchi nyingine ambazo ni wanachama wa Mpango wa Kujitathmni Kiutawala Bora barani Afrika (APRM) ili iweze kuboresha hatua ilizofikia kwenye mpango huo.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Agosti 26, 2016) wakati akichangia mada katika Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Mpango wa Kujitathmni Kiutawala Bora barani Afrika (APRM Forum) uliofanyika kwenye hoteli ya InterContinental jijini Nairobi, Kenya.

“Nitumie fursa hii kukiarifu kikao chako kwamba Tanzania imeshaanza kutekeleza mpango kazi wa Kitaifa ambao umejikita kutatua changamoto katika sekta za maji, elimu, kilimo, nishati na miundombinu kama zilivyoainishwa kwenye kikao cha APRM,” alisema.

“Ili kuhakikisha kuwa zinafanyiwa kazi haraka, changamoto hizi za kisekta zimepewa kipaumbele kwenye Mpango wetu wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano wa 2016-2021 ambao umejikita zaidi kwenye viwanda,” aliongeza.

Tanzania ilifanyiwa tathmini yake Januari, 2013 kwenye kikao cha Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika kilichofanyika Addis Ababa, Ethiopia.

Mapema, akifungua mkutano huo, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema viongozi wa Afrika hawana budi kukubaliana na kuungana kutafuta suluhisho katika ushindani wa kibiashara.

Alisema nchi wanachama wa mpango huo hawana budi kujenga umoja kama njia ya muafaka ya kufikia makubaliano hayo.

Wakati huohuo, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alisema bara la Afrika linakabiliwa na changamoto 11 (strategic bottlenecks) ambazo zinakwamisha maendeleo ya bara hilo na akataka zitafutiwe ufumbuzi ili kuzisaidia nchi nyingi barani humo. 

Akiwasilisha mada binafsi katika mkutano huo, Rais Museveni alisema kwa zaidi ya miaka 50, amekuwa kiongozi katika sehemu kadhaa na kwamba amebaini kuwa changamoto hizo zimezuia ukuaji wa uchumi barani Afrika pamoja na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
 
Alisema asilimia kubwa ya changamoto hizo haikupata ufumbuzi hata wakati malengo ya maendeleo ya milenia (MDGs) yalipokuwa yanatekelezwa.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni mikanganyiko ya kiitikadi ambayo huzaa ubinafsi na maslahi binafsi; kuwepo kwa mataifa dhaifu (weak states); nguvukazi duni (kitaaluma na kiafya), uduni wa miundombinu (barabara, maji, umeme, tehama) ambao unashindwa kuvutia uwekezaji; uhaba wa viwanda unaolazimisha nchi kusafirisha mali ghafi na uhaba wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa barani Afrika.

Changamoto nyingine ni uduni wa huduma za kijamii unaosababisha huduma mbovu kwenye maeneo ya utalii, mabenki na mahoteli; kilimo duni kisichotumia mbolea, dawa za kuua wadudu, mbegu za kisasa au njia za umwagiliaji; makosa ya kisera kama vile ubinafishaji au utaifishaji mali zinazomilikiwa na sekta binafsi; ukandamijazi wa demokrasia na ukosefu wa maadili miongoni mwa watumishi wa umma.

Naye Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alisema kwa vile changamoto hizo zinagusa nchi nyingi za Afrika, ni vema iundwe timu ya wataalamu watakazipitia zote na kuainisha zipi zinafaa kufanyiwa kazi na kisha taarifa yao iwasilishwe kwenye kikao kijacho cha Wakuu wa Nchi wanachama.

Akifunga mkutano huo, Rais Kenyatta aliitaka sekretarieti ya APRM ipitie changaoto hizo na kuziwakilisha kwenye kikao chao kijacho ambacho alisema kitafanyika Januari 2017, mjini Addis Ababa, Ethiopia katika tarehe itakayopangwa baadaye. 
 
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, AGOSTI 27, 2016
                                  ,,,,,,,,,,,,,,,,,
                                   

Saturday, August 27, 2016

JWTZ Lawatoa Hofu Wananchi.......Lasema Septemba 1 Litasherehekea Miaka 52 kwa Kufanya Usafi Mtaani

SeeBait
Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) leo linaanza shamrashamra za maandalizi kuelekea siku ya maadhimisho ya 52 ya majeshi inayotarajiwa kufanyika Septemba Mosi mwaka huu kwa kufanya usafi na upandaji miti katika kambi za jeshi na baadhi ya taasisi nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, Msemaji wa JWTZ Kanali Ngemela Lubinga aliwatoa hofu wananchi kuwa wasitishike pindi watakapoona wanajeshi katika maeneo ya karibu na makazi yao.

“Kesho (leo) tuaanza kufanya usafi kuanzia maeneo ya Kawe hadi karibu na kambi ya Lugalo, na kwamba niwatoe hofu wananchi pindi watakapoona wanajeshi wengi mitaani kwa kuwa hatuna nia mbaya hivyo wasitufikilie vibaya,” alisema.

Alisema jeshi hilo litafanya usafi pamoja na upandaji miti katika baadhi ya maeneo nchini hadi siku ya kilele cha maadhimisho hayo. Pia wanajeshi watajitolea damu salama katika hospitali za kambi za jeshi.

“Siku kuu ya majeshi itaadhimishwa pamoja na wanajeshi kujitolea damu kwenye vituo maalumu vya kutolea damu salama mikoani, katika hospitali zetu za kanda,” alisema na kuongeza.

“Sanjari na utoaji damu, madaktari wetu JWTZ watatoa huduma za tiba bure kama upimaji wa virusi vya Ukimwi, kisukari, na upimaji wa shinikizo la damu. “

“Kama ilivyo mila na desturi ya majeshi kufanya usafi na utunzaji wa mazingira, kuelekea siku ya maadhimisho tutafanya usafi na kupanda miti maeneo ya jirani na kambi na kwenye taasisi za kiraia kadri mahusiano yatakavyofanyika na taasisi hizo, ” alisema.

Pia alisema siku hiyo ya maadhimisho itaadhimishwa kwa kuienzi michezo na kudumisha urafiki baina ya JWTZ, wananchi, na Taasisi na kwamba mashindano mbalimbali yatafanyika.
Tarehe hiyo hiyo  ya Septemba 1 , Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetengaza kufanya maandamano na mikutano nchi nzima ili kulaani kile wanachokiita udikteta unaofanywa na serikali ya awamu ya tano.

Tayari tangazo hilo la Chadema limepingwa vikali na Rais John Magufuli, Waziri Mkuu Majaliwa Kassim, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani na Nsato Marijani, Kamishina wa Jeshi la Polisi, Operesheni na Mafunzo huku chama hicho kikiendelea kusisitiza azma yake.
                                                               ,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,

Saturday, August 27, 2016

Viongozi Mbalimbali wa Chadema Waendelea Kutiwa Mbaroni Kwa Uchochezi.......Wabunge CUF Waunga Mkono UKUTA

SeeBait
Zikiwa zimesalia siku nne kabla ya maandamano yanayodaiwa yatafanywa na Chadema, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amekuwa kiongozi wa 26 wa chama hicho kukamatwa na polisi kwa tuhuma za uchochezi ndani ya kipindi kifupi. 

Kukamatwa kwa viongozi hao kunatokana na kauli zao zinazosisitiza kufanyika kwa maandamano yaliyopewa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), yaliyopangwa kufanyika nchi nzima Septemba Mosi. 

Hata hivyo, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imezuia maandamano hayo na mikusanyiko yoyote ya kisiasa hadi mwaka 2020 kwa lengo la kuipa nafasi Serikali iliyopo madarakani kuwaletea wananchi maendeleo. 

Baadhi ya viongozi wa Chadema waliokamatwa na kuhojiwa mpaka sasa ni Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Visiwani, Salum Mwalimu, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye kesi yake iko mahakamani. 

Lissu alikamatwa Agosti 3, mkoani Singida baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Ikungi uliopo jimboni kwake kwa tuhuma za uchochezi. 

Agosti Mosi, Mbowe alijisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam na kuhojiwa kwa saa tatu. Kiongozi huyo aliitwa kwa mahojiano maalumu kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kauli za chama hicho kukinzana na agizo la Rais John Magufuli la kuzuia shughuli zozote za kisiasa ikiwapo mikutano kufanyika nchini. 

Lema alikamatwa juzi alfajiri nyumbani kwake Njiro kwa Msola na makachero wa polisi kwa tuhuma za uchochezi ikiwa ni siku moja tangu kuachiwa kwa dhamana Diwani wa Chadema wa Kata ya Sombetini, Ally Benanga aliyefunguliwa mashtaka ya uchochezi mahakamani. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo jana alithibitisha kukamatwa kwa Lema na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea wa tuhuma za kutoa lugha za uchochezi mitandaoni. 

Alisema mbunge huyo alitoa kauli za uchochezi na kuzisambaza kwenye mitandao, mapema wiki hii. 

Polisi walisema ujumbe wa Lema kwenye mtandao ulisisitiza wito wa kufanyika mikutano na maandamano ya Ukuta, kwamba Mkoa wa Arusha umejiandaa kwa lolote na yeye atakuwa mstari wa mbele. 

Meya wa jiji la Arusha, Calist Lazaro alithibitisha kukamatwa kwa Lema na kueleza kuwa bado walikuwa hawajajua tuhuma zake. 

“Ni kweli mbunge anashikiliwa na tunaendelea kuhangaika apate dhamana leo (jana), ama afikishwe mahakamani,” alisema.

Salum Mwalimu na wenzake 17 watiwa mbaroni
Wakati Lema anakamatwa Arusha, Naibu Katibu Mkuu Visiwani, Salum Mwalimu na wenzake 17 walikamatwa wakati wakijiandaa kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mwandoya wilayani Meatu Mkoa wa Simiyu. 

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Onesmo Lyanga alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 25, saa 10 jioni katika kijiji hicho. 

Lyanga alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa wanajiandaa kufanya mikutano ya hadhara yenye lengo la uchochezi. 

Alisema baada ya kupata taarifa kutoka katika vyanzo vyao, walifika eneo la tukio na kuwakamata kwa kuwa hata kibali cha kufanya mkutano hawakuwa nacho.

Jana, Mwalimu na wenzake walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bariadi na kusomewa mashtaka ya kuwashawishi wananchi kufanya vitendo viovu na uchochezi. 

 Viongozi hao walinyimwa dhamana na kurudishwa rumande hadi Agosti 30. 

Agosti 23, Diwani wa Chadema, Kata ya Sombetini, Ally Bananga (40), alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha kujibu tuhuma za kuhamasisha uchochezi. 

Akisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi Augustino Rwezire, diwani huyo alidaiwa kuhamasisha wananchi kufanya maandamano yasiyo halali, Septemba Mosi. 

Diwani huyo alifikishwa mahakamani hapo Agosti 23, ambapo Wakili wa Serikali Charles Kagirwa, alidai alitenda kosa hilo Agosti 13, wilayani Karatu Mkoa wa Arusha. 

Pia, alisema kuwa siku ya tukio Bananga akiwahutubia wananchi katika mkutano wa wazi uliofanyika eneo la Hosteli ya Karatu, aliwahamasisha wananchi hao washiriki katika kusanyiko lisilo halali Septemba Mosi. 

Agosti 25, viongozi wengine wanne wa Chadema Jimbo la Kigoma Mjini, walikamatwa na polisi wakidaiwa kujihusisha na vitendo vya uchochezi. 

Waliokamatwa ni mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Kigoma, Ally Kisala, Katibu wa Baraza la Vijana Chadema Mkoa (Bavicha), Omary Gindi, Katibu wa chama jimbo la Kigoma mjini, Frank Ruhasha na Mwenyekiti wa mtaa wa sokoni katika Kata ya Katubuka, Moses Bilantanye. 

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (DCP), Ferdinand Mtui alikiri viongozi hao wanne kushikiliwa kituoni hapo kwa muda lakini walipata dhamana, hivyo kuruhusiwa kuondoka na kutakiwa kuripoti kituoni hapo jana. 

Katibu wa Chadema Mkoa wa Kigoma, Shaaban Madede aliwaomba Polisi kwamba chama hicho kimejipanga kuandamana kwa amani na kufanya mikutano kila pembe ya mkoa, lengo ikiwa ni kufikisha ujumbe kwa wananchi juu ya kilio chao dhidi ya Serikali kukandamiza demokrasia. 

Wabunge CUF  Waunga Mkono UKUTA
Wakati wabunge wa Chadema wakikamatwa, wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), wamesema wanaunga mkono Ukuta, kwa sababu imelenga kupambana na uvunjaji wa demokrasia unaodaiwa kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. 

Msimamo huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Wabunge wa CUF, Riziki Mngwali alipozungumza na wanahabari kufuatia taarifa zilizosambaa kuwa wabunge hao wanapinga Ukuta. 

Riziki ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani, alisema wabunge wa chama hicho hawana tatizo na Ukuta na wanaunga mkono, hivyo tofauti na propaganda zinazoenezwa kuwa wanaupinga. 

“Chadema ni washirika wetu kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hivyo hatuna sababu ya kutowaunga mkono. 

 “Tunachosubiria ni taratibu za uongozi wa juu kukamilika kisha watupe mwongozo nini cha kufanya kwenye Ukuta. Lakini wabunge tupo pamoja na operesheni hii, hatuipingi kwa sababu ina lengo ya kudai haki na demokrasia inayominywa,” alisema Riziki. 
,,,,,,,,,,,

Saturday, August 27, 2016

Waziri Simbachawene Aagiza Machinga waondolewe Kariakoo....Asema Rais hakumaanisha warudi

SeeBait

Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwaondoa wafanyabiashara wadogo maarufu kama Machinga katika maeneo ya soko la Kariakoo na barabarani, hususan karibu na barabara za mabasi ya mwendo kasi.

Akizungumza jana na Kamati ya Bunge, Waziri huyo wa TAMISEMI alisema kuwa kurejea kwa wafanyabiashara hao katika maeneo hayo kumeleta usumbufu mkubwa na uchafu wa mazingira katika maeneo ya jiji.

“Namuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam awaondoe na asilegeze kamba,” alisema Waziri Simbachawene.

Alisema kuwa hali hiyo imetokana na tafsiri isiyo sahihi ya agizo la Rais John Magufuli alipokuwa ziarani Mkoani Mwanza.

“Wala agizo  la Mheshimiwa Rais halikumaanisha hicho. Mheshimiwa Rais alisema tuwatafutie maeneo mbadala ambao wapo maeneo kama ya Mwanza na walikuwa wanafanya biashara ya kuuza nguo, akizungumzia wale particular group walioko pale Mwanza. Kwa Dar es Salaam tulishamaliza huko,” alisema.

Aidha, alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha hakuna hata machinga mmoja atakayeonekana akifanya biashara katika maeneo ya barabara za mabasi yaendayo kasi.

Aigizo hilo la Waziri Simbachawene liliungwa Mkono na wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge ambao walisema kuwa hali ya soko la Kariakoo imekuwa mbaya kutokana na kuzagaa kwa machinga.
 
 

Saturday, August 27, 2016

Polisi Mwingine Auawa Kwenye Mapambano Makali na Majambazi Huko Mkuranga

SeeBait
Ilikuwa ni kama filamu ya askari na maadui wakati askari wa Jeshi la Polisi walipopambana na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi kwenye nyumba iliyo eneo la Vikindu wilayani Mkuranga.

Taarifa ambazo zimepatikana kutoka kwa watu waliokuwa karibu na operesheni hiyo na ambazo hazijathibitishwa na mamlaka rasmi, zinasema kamishna wa Kitengo cha Kuzuia Ujambazi, ASP Thomas Njuki aliuawa kwa kupigwa risasi kichwani. 
Taarifa hizo zilisema kuwa jambazi mmoja aliuawa ingawa idadi ya waliokamatwa haikufahamika mara moja kutokana na mashuhuda kutoa takwimu tofauti. 
Kamanda wa Polisi wa Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema ataongea na waandishi wa habari leo saa 4:00 asubuhi kuzungumzia tukio hilo. 
Tukio hilo limetokea siku chache baada ya askari wanne wa Jeshi la Polisi kuuawa wakati wakibadilishana lindo kwenye tawi la benki ya CRDB lililoko Mbande jijini Dar es Salaam. 
Watu hao, waliofika wakiwa wamepanda pikipiki, walipora silaha na kutoweka nazo. Katika tukio la jana, askari wa Jeshi la Polisi walikuwa na nia ya kuwakamata watu waliowashuku kuwa ni majambazi. 
Kwa mujibu wa watu wanaoishi karibu na nyumba hiyo, mpambano kati ya polisi na majambazi hao ulianza saa 7:30 usiku baada ya polisi kuvamia nyumba walimopanga majambazi hayo. 
Tukio lilivyotokea 
Chanzo kimoja cha habari kimeeleza kuwa baada ya polisi kufuatilia nyendo za wakazi wa nyumba hiyo walianza upelelezi na kubaini kuwa huenda wanahusika na matukio kadhaa ya uhalifu, likiwamo la uvamizi wa kituo cha polisi cha Stakishari na lile la tawi la CRDB Mbande mkoani Pwani. 
Mpashaji huyo alisema kuwa jana saa saba usiku, polisi walifika kwenye nyumba hiyo iliyo Mtaa wa Vikindu Mashariki ambayo ina maduka upande wa mbele, ikipakana na nyumbani nyingine mbili pembeni na nyuma zikiwa umbali usiozidi hatua nne. 
Habari hizo zinasema askari hao kwanza walimtuma mwenyekiti wa serikali ya mtaa kwenda kuwasihi wafungue mlango na walipokataa ndipo walipoenda kugonga, wakiwaamrisha watu hao wafungue mlango. 
“Baada ya kuona hawatii amri ya kufungua mlango, polisi waliamua kuvunja vitasa kwa kutumia bastola, ndipo risasi zikaanza kurushwa,” alisema mpashaji habari huyo. 
 “Kwa kuwa mkuu alikuwa mbele, wahalifu walimpiga risasi kichwani na alikufa palepale.” 
Mtu huyo alisema kuwa baada ya Kamishna Njuki kufariki, askari wengine walirudi nyuma kujihami zaidi. 

Baada ya hapo polisi waliendelea kupiga risasi kuelekea maeneo mbalimbali ya nyumba hiyo na wahalifu hao kujibu mashambulizi. 

“Kila chumba ambacho polisi walikuwa wakijaribu kurusha risasi, zilijibiwa. Inaelekea kila chumba kilikuwa na mtu mwenye silaha,” alisema shuhuda mwingine wa tukio hilo. 

Habari kutoka kwa majirani zinasema hadi saa 2:45 asubuhi, milio ya risasi iliendelea kurindima katika eneo hilo. 
Baadaye polisi waliomba kuongezewa nguvu na Jeshi la Wananchi (JWTZ) ambao walifika na kuendeleza mapambano hayo. 

 Mtoto ataja alipojificha baba
Wakati mapambano yakiendelea, sauti za watoto waliokuwa wakilia zilisikika na ndipo askari wa JWTZ waliamuru watu hao wawatoe nje. 
“Watoto walipotoka nje, polisi waliwauliza baba yupo wapi, mtoto mmoja akajibu yupo darini,” alisema

Baada ya polisi kusikia hivyo, walielekeza mashambulizi yao darini na kufanikiwa kumjeruhi mtu aliyejificha darini ambaye alishuka. 

Wakati polisi wakishinikiza atoke ndani ili kujisalimisha, mtu huyo alijipiga risasi mara baada ya kutoka na kufariki dunia.
Wakazi Vikindu wahaha!
Kutokana na tukio hilo, taharuki ilitanda kwa wakazi wa Vikindu na biashara zote zilifungwa eneo hilo huku wananchi wakiwa na chupa za maji kutokana na mabomu ya machozi yaliyokuwa yakipigwa kila mara. 
Wakazi wa eneo ambalo lipo karibu na maegesho ya magari ya Farid Seif, hawakuruhusiwa kutoka ndani na waliofanikiwa kutoka usiku hawakuingia hadi jana saa 7.00 mchana wakati hali ilipotulia. 
Kutokana na majibizano ya risasi, watu wanaofanya kazi jijini Dar es Salaam ambao wanaishi vijiji vya Melela, Vianzi, Pemba Mnazi na Mfuru hawakwenda kazini kutokana na barabara inayotoka Vikindu kufungwa hadi saa 7.00 mchana. 
Tukio hilo lilisababisha umati wa watu kukusanyika kushuhudia mapambano hayo, lakini hakuna raia aliyeruhusiwa kuvuka mita 150 kwenda eneo la tukio. 
Nyumba waliokuwa Wanaishi hao Majambazi
        KATKA HABARI ZA MICHEZO 

RIPOTI SPESHO

KIRAFIKI ITALY v FRANCE SEP 1 KUTUMIWA KUJARIBU VIDEO KUSAIDIA MAREFA!


FIFA-VARS2MFUMO wa Video kusaidia maamuzi ya Marefa Uwanjani, VARS [Video Assistant Referes] utatumika kwa mara ya kwanza katika Mechi ya Kimataifa hapo Septemba 1 wakati Italy ikicheza na France huko Bari.
Habari hizi zimetangazwa na FIFA hapo Jana.
Kwenye Mfumo huo wa Video, Refa Msaidizi atakuwepo pembeni mwa Uwanja na atakuwa na Mawasiliano na Refa wa Mechi wakati wote wa Mechi hiyo akipitia Video bila kusitisha Mechi.
Ikiwa litatokea tukio ambalo Refa Msaidizi ameliona atamtonya Refa wa Mechi ambae ana rulsa ya kuukubali ushauri huo au au akaamua mwenyewe kwenda pembeni kuliptia na kutoa uamuzi wake.
Ama Refa anaweza kumuomba Refa Msaidizi kulipitia tukio ili ampe ushauri.
VARs imekuwa ikitumika kwa Majaribio huko USA kwenye Ligi Daraja la 3 na sasa FIFA, ikishirikiana na IFAB, ambacho ndicho chombo pekee kinachoweza kubadili Sheria za Soka, vimeafika Majaribio hayo na sasa yameingia hatua mpya ya Majaribio kwenye Mechi za Kimataifa.
Mechi hiyo ya Italy na France pia itahudhuriwa na Rais wa FIFA, Gianni Infantino na Makamu Katibu Mkuu wa FIFA General Zvonimir Boban.
Hivi sasa, kwenye Soka, inatumika Teknloji ya Kuamua kama Mpira umevuka Mstari wa Goli, GLT [Goal Line Technology] ambayo humsaidia Refa kuamua kama ni Goli au si Goli.
...........
 

WENGER ANYAKUA WAWILI WA LA LIGA!


WENGER-NA-WAPYABEKI wa Germany Shkodran Mustafi na Straika wa Spain Lucas Perez Jana walitarajiwa kukamilisha upimwaji wao wa Afya zao ili kusaini Mkataba na Arsenal.
Arsenal walishaafikiana na Valencia ili kumnunua Mustafi, mwenye Miaka 24, kwa Dau la Pauni Milioni 35 na ushei huku pia wakikubaliana na Deportivo La Coruna kumchukua Perez, 27, ambae akifunga Bao 17 katika Gemu 37 Msimu uliopita.
Dau la Perez limetajwa kuwa ni Pauni Milioni 17.1.
Wachezaji hao wanaungana na Wapya Viungo Granit Xhaka na Kelechi Nwakali, na Fowadi Takuma Asano.
Kwa kuwachota Mustafi na Perez, Meneja wa Arsenal Arsene Wenger sasa ameelekea kujibu mapigo ya kwamba yu mgumu kutoa Fedha kununua Wachezaji Wapya.
Akiongea hapo Jana, Wenger alisema Klabu yao ipo kwenye mazungumzo na ana Imani watafanikiwa kuzikamilisha Dili hizo kabla Dirisha la Uhamisho kufungwa Agosti 31 Saa 7 Usiku, Saa za Bongo.
Wenger ameeleza: “Safari hii ni Dirisha la Uhamisho la ajabu. Nilidhani litakuwa rahisi lakini ni gumu kupita yote ya nyuma!”
Kati ya Wapya wao, Mchezaji wa Japan Asano Takuma, alienunuliwa kutoka Sanfrecce Hiroshima Mwezi Julai, atajiunga kwa mkopo huko Bundesliga kuichezea Stuttgart kwa Msimu Mmoja.
,,,,,,,,,,,,,,,,

EPL: LEO KUANZA SPURS-LIVERPOOL, KWISHA HULL-MAN UNITED!


LIGI KUU ENGLAND
Ratiba:
**Saa za Bongo
Jumamosi Agosti 27
1430 Tottenham v Liverpool                 
1700 Chelsea v Burnley              
1700 Crystal Palace v Bournemouth                
1700 Everton v Stoke                 
1700 Leicester v Swansea           
1700 Southampton v Sunderland          
1700 Watford v Arsenal              
1930 Hull City v Man United       
+++++++++++++++++++++++++++      
EPL-2016-2017Ligi Kuu England, EPL, Leo inaingia Wikiendi yake ya mwisho kabla kupisha Mechi za Kimataifa kwa Wiki 2 na hii Leo zipo Mechi 8 na ya mwanzo kabia ni ile ya White Hart Lane Jijini London kati ya Tottenham Hotspur na Liverpool nay a mwisho hu huko huko KCOM Stadium ambako Hull City watacheza na Manchester United.
Katikati ya Mechi hizo mbili, huko Stamford Bridge, Chelsea watacheza na Burnley, Crystal Palace kuivaa Bournemouth, Everton na Stoke City, Southampton na Sunderland na Watford kuikaribisha Arsenal.
+++++++++++++++++++++++++++
JE WAJUA?
-Safari hii Ligi hii ya England haina tena Jina la Mdhamini na itajulikana rasmi kama Ligi Kuu tofauti na Msimu uliopita ilipoitwa Barclays Premier League kutokana na udhamini wa Barclays.
+++++++++++++++++++++++++++
Hadi sasa, baada ya Mechi 2 kwa kila Timu za juu 4 ni Man City, Man United, Hull City na Chelsea ambao EPL-TEBOwameshinda Mechi zao zote.
Jumapili zipo Mechi 2 tu,
IGI KUU ENGLAND
Msimu Mpya 2016/17
Ratiba:
**Saa za Bongo
Jumapili Agosti 28
1530 West Brom v Middlesbrough
1800 Man City v West Ham         
Jumamosi Septemba 10
1430 Man United v Man City                
1700 Arsenal v Southampton                
1700 Bournemouth v West Brom           
1700 Burnley v Hull          
1700 Middlesbrough v Crystal Palace               
1700 Stoke v Tottenham             
1700 West Ham v Watford          
1930 Liverpool v Leicester          
Jumapili Septemba 11
1800 Swansea v Chelsea   
Jumatatu Septemba 12
2200 Sunderland v Everton  
 
SHUKRANI ZANGU ZA DHATI NI KWA MPEKUZI PAMOJA NA SOKA IN BONGO  
Reviewed by RICH VOICE on Agosti 27, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...