JUMATANO 31/08/2016

Wednesday, August 31, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumatano ya Agosti 31

SeeBait


Wednesday, August 31, 2016

Lowassa Aandika Waraka Mzito Kuhusu Oparesheni UKUTA.....Asimulia Kilichomfanya Akutane na Rais Magufuli

SeeBait
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa ameandika barua kuhusu operesheni ya chama chake iliyopewa jina la Ukuta na jinsi ambavyo jeshi la Polisi na Serikali lilivyopanga ‘kuubomoa’.

Katika waraka huo, Lowassa ameeleza kuwa ameamua kushika kalamu na kuandika masikitiko yake kuhusu hali ya amani nchini akidai Serikali imekata mkono wa amani.

Ameeleza kuwa Serikali imekandamiza upinzani na demokrasia na ndio chanzo cha wao kuanzisha UKUTA kupinga ukandamizaji huo.

“Binafsi nafurahishwa na kutiwa moyo na jinsi watanzania walivyoipokea Operesheni hii, pamoja na vitisho vya dola,” ameandika. “Siku zote sisi Chadema na Ukawa kwa ujumla ni wenye kulitakia amani na utulivu Taifa letu. Maandamano haya ya Septemba 1 ni ya amani, lakini vitendo vya jeshi la polisi vimewapa wasiwasi Watanzania,” Lowassa ameongeza.

Katika andiko hilo, Lowassa amedai kuwa amekuwa akipigiwa simu na viongozi wastaafu pamoja na watu mashuhuri wakimshauri kushawishi wakae na Serikali kuzungumza ili kuepusha taifa kujiingiza katika machafuko. Aliongeza kuwa kukutana na Rais John Magufuli katika Jubilee ya miaka 50 ya ndoa ya Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa ni sehemu ya juhudi hizo.

“Nyote ni mashahidi wa tukio la kukutana na Rais Magufuli katika Jubilei ya miaka 50 ya ndoa ya mzee Mkapa. Ulikuwa ni mwanzo wa juhudi zetu za kuwanyooshea mkono wa amani. Lakini tunashangazwa wenzetu hawako tayari kuupokea mkono huo,” ameandika.

Aliongeza kuwa katika kikao cha juzi cha ndani cha chama hicho kilichofanyika katika Hotel ya Giraffe jijini Dar es Salaam walipanga kuzungumzia jinsi ya kuunyosha zaidi mkono wa amani lakini Jeshi la Polisi ‘liliukata’.

“Kitendo kile kwangu binafsi kimezidi kuniimarisha na kunipa nguvu zaidi ya kudai demokrasia na kuheshimu katiba ambayo viongozi wetu waliapa kuifuata na kuitetea,” unasomeka waraka wa Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa.

Wednesday, August 31, 2016

Makusanyo Kodi za Simu Yapanda Maradufu

SeeBait
Sheria ya Fedha ya Mwaka 2016 iliyopitishwa kuhusu utozaji ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha kwenye miamala ya benki na simu, imeanza kuzaa matunda kutokana na ongezeko la mapato lililoanza kushuhudiwa kutoka kampuni za simu.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyokutana jana na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), iliambiwa kutokana na sheria hiyo iliyopitishwa Bunge baada ya kupitisha bajeti ya mwaka huu, mwezi uliopita serikali imeshuhudia ongezeko kubwa la mapato, yaliyotolewa na kampuni za simu.

Taarifa hiyo ilitolewa jana kwenye Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, imeonesha Kampuni ya Vodacom ilikuwa ikitoa kodi ya ushuru wa bidhaa kwa fedha zinazotumwa kwa wastani wa Sh milioni 360 kwa mwezi, lakini baada ya mabadiliko ya sheria, Julai pekee mwaka huu imelipa Sh bilioni 1.9.

Mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Godwin Barongo aliiambia kamati hiyo kuwa kwa upande wa Kampuni ya Tigo, walikuwa wanatoa wastani wa Sh milioni 250 kwa mwezi, lakini sasa wametoa Sh bilioni 1.48.

Barongo ambaye ni Meneja Msaidizi, Kitengo cha Walipa Kodi Wakubwa TRA alikuwa akizungumzia namna Mtambo Maalumu wa Kusimamia Mawasiliano na Udhibiti wa Mapato yatokanayo na Simu (TTMS) unaosimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ulivyowezesha kufanikisha ukusanyaji mapato.

“Pamoja na mabadiliko ya sheria yaliyoanza mwezi Julai mwaka huu, kampuni za simu zilikuwa zikitoza transfer, lakini sheria ilikuwa haigusi kwenye kutoa, Baada ya hiyo, tuligundua kuwa sasa kamisheni nyingi zilipelekwa kwenye kutoa kwa sababu hakuna tozo na kwenye transfer zinapungua,” alisema Barongo.

Aliendelea kusema, “Kwa hiyo mabadiliko haya ya sheria ya sasa hivi ambayo tunatoza kwenye kuweka na kutoa, yametusaidia.” 
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso alisisitiza kuwa wabunge wanategemea Wizara ya Miundombinu kupitia sekta ya mawasiliano, ichangie mapato mengi kwa serikali.

Baada ya Bunge kupitisha mabadiliko ya sheria ya fedha yaliyopitisha utozaji kodi ya ushuru wa bidhaa katika miamala ya benki na simu za mkononi, ulijitokeza mjadala ambao baadhi ya watu walidai ushuru huo utaathiri wateja wa kampuni za simu na benki.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alifafanua kwamba serikali imeamua kutoza ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha au vyote kwa kadri itakavyotozwa akisisitiza kwamba utalipwa na benki na kampuni na si mtumiaji au mpokeaji wa fedha katika miamala itakayofanyika.
 
 

Wednesday, August 31, 2016

Ndege za Kivita Kutawala Anga la Dar Septemba 1

SeeBait
Septemba mosi mwaka huu inataraji kuingia katika histori ya Tanzania kutokana na matukio ambayo yanataraji kufanyika siku hiyo, matukio hayo ni pamoja na sherehe za miaka 52 ya Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ), maandamano ambayo yamepangwa kufanywa ya UKUTA na tukio la kupatwa kwa jua.

Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati alipokutana na Maafisa wa Jeshi la JWTZ Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema JWTZ inapotimiza miaka 52 ni fahari kubwa hivyo tunapaswa kuwapongeza kwa kudumisha amani na mshikamano.

Alisema Jeshi hilo limejipanga kurusha angani ndege zake za kivita katika anga la Dar es Salaam, Septemba 1 mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 52 ya kuanzishwa kwake.

Makonda aliwataka wananchi kutokuwa na hofu wanaposikia ngurumo za ndege hizo bali wafurahie kwani ni ndege zao.

“Mnaposikia milio ya ndege zetu mbalimbali, mfurahie kwa sababu hizo ni ndege za wananchi. Usisikie muungurumo ukashtuka. Hakuna jambo lolote lile zaidi ya kuonesha vifaa vyetu na jinsi ambavyo wanajeshi wetu kwa miaka 52 wamaeendelea kuwa imara na vifaa vizuri,” alisema Makonda.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa waliwataka wananchi waliojipanga katika vikundi mbalimbali kuripoti kwa wakuu wao wa wilaya kujiandikisha ili waweze kushiriki pamoja na Jeshi hilo katika zoezi la usafi jijini humo.

Aliwataka wakazi wa mkoa huo pia kujitokeza kuchangia damu katika vituo mbalimbali ambavyo vimeanishwa ili kuunga mkono juhudi za uchangiaji damu zitakazofanywa na wanajeshi wa JWTZ.

“Hii ni sehemu ya amani, tufanye usafi kwa amani. Tujitolee damu zetu kwa amani na mwisho wa siku tuwaenzi na kuwapongeza wanajeshi wetu kwa kazi kubwa wanayoifanya,” Makonda alieleza.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa aliendelea kutoa onyo kwa watu watakaotaka kufanya maandamano yaliyopigwa marufuku ya oparesheni UKUTA akiwataka kutii sheria.

“Mimi ninavyojua UKUTA ni kuwa mtu amefika mwisho wa kufikiri sasa kama watakuwa wamefika mwisho wa kufikiria basi sisi tutawasaidia … watu wapo wanapanga kufanya mambo ya kusaidia jamii wao wanapanga maandamano nawashauri wananchi waungane na Polisi,” alisema Makonda.
 
 

Wednesday, August 31, 2016

Lowassa, Mbowe Watakiwa Kuripoti Polisi Keshoi Septemba 1

SeeBait
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama hicho, Edward Lowassa na viongozi wengine waandamizi wameitwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwenda kuripoti kesho Septemba Mosi.

Hatua hiyo inatokana na viongozi hao kukamatwa juzi, baada ya kufanya mkutano maalumu wa ndani wa Kamati Kuu, na walipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda hiyo na kuhojiwa kabla ya kuachiwa.

Mbali na Mbowe na Lowassa, viongozi wengine wa Chadema waliokamatwa na kutakiwa kwenda Polisi kesho ni Katibu Mkuu, Vincent Mashinji, Naibu wake, John Mnyika na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Said Issa Mohammed.

“Wameitwa Polisi waende Septemba mosi kuripoti baada ya jana kukamatwa na kuhojiwa wakituhumiwa kukiuka maagizo ya Polisi,” alisema Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene na kufafanua:

“Lakini wanaweza kwenda au wakaanzia kwenye maandamano kisha wakaenda Polisi kuripoti.”

Alisema maandamano hayo yatakuwapo kama yalivyopangwa kwani maandalizi yake yamekamilika.

Habari zaidi zilieleza, kwamba jana mchana viongozi hao walikuwa wakifanya kikao Makao Makuu ya chama hicho Kinondoni Dar es Salaam, ambapo pia walikutana na wabunge wote wa chama hicho kwa makundi tofauti.

Kwa mujibu wa mtoa habari ndani ya Chadema makao makuu katika kikao hicho walijadili mambo mengi ikiwa ni pamoja na suala la utekelezaji wa Ukuta kesho.

Mmoja wa wabunge wa Chadema alisemai kwamba walikuwa wakiwekana sawa kuhusu maandamano yao.

Alibainisha kwamba katika mkutano huo ambao Mbowe hakuwepo pia walijadili maombi ya viongozi wa dini kuwataka kusitisha maandamano hayo Septemba mosi.

“Viongozi wa dini wamekuwa wakituomba tusitishe maandamano ya Ukuta Septemba mosi, tusubiri hadi baada ya mkutano wa vyama vya siasa Septemba tatu,” alisema Mbunge huyo wa Kanda ya Ziwa.

Aliongeza: Katika mkutano huo, Lowassa na viongozi wengine walijadili hayo na ikikubalika kwa heshima ya viongozi wa dini maandamano ya Ukuta yafanyike baada ya Septemba tatu.”

Hata hivyo, mwandishi alishuhudia wabunge wengi wa chama hicho wakitoka katika mkutano huo kimya kimya bila kutaka kuzungumza na kabla muda uliopangwa kwisha, huku taarifa zikieleza kwamba mkutano huo uliahirishwa baada ya kuwepo taarifa za kutaka kuvamiwa na Polisi.

“Tumeambiwa tusambaratike, tutajulishwa wapi tutakutana tena, kama hapa au wapi,” alidokeza mmoja wa wabunge hao.

Baada ya mkutano huo kuahirishwa, Lowassa alitoka eneo hilo huku taarifa zikieleza alikuwa akielekea kwenye moja ya hoteli jijini humo kuungana na Mbowe ambapo walikuwa na mazungumzo na baadhi ya viongozi wa dini. 
 
 

Wednesday, August 31, 2016

Taarifa Toka IKULU : Rais Magufuli atengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha.

SeeBait
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 31 Agosti, 2016 amemteua Bw. Doto M. James kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Kabla ya uteuzi huo Bw. Doto M. James alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango (Sera).

Bw. Doto M. James ataapishwa kesho tarehe 01 Septemba, 2016 saa 2:45 Asubuhi Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Kufuatia uteuzi huo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile atapangiwa kazi nyingine.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
31 Agosti, 2016
 

Wednesday, August 31, 2016

Breaking News: Mbowe Atangaza Kuahirisha Maandamano ya Oparesheni UKUTA Yaliyokuwa Yamepangwa Kufanyika Kesho

SeeBait
Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo,Freeman Mbowe  ametangaza kusitishwa kwa maandamano ya Oparesheni UKUTA yaliyokuwa yamepangwa kufanyika kesho nchi nzima hadi tarehe moja Octoba.

Akizungumza na wanahabari leo, makao makuu ya chama hicho, Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Mbowe amesema, Chadema inalazimika kuahirisha maandamano na mikutano ya kesho kutokana na kuheshimu wito wa viongozi wa dini zote waliowaomba.

“Viongozi wa dini zote hapa nchini kuanzia, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Mkuu wa Kanisa la Kianglikana Tanzania, Rais wa Baraza la Maaskofu (TEC), Katibu Mkuu wa Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), Mkuu wa Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT), Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste (CPCT), Mufti Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) na Mufti Mkuu wa Zanzibar, wametusihi tuahirishe ili wao wazungumze na Rais John Magufuli kutafutia suluhu suala hili,”
amesema Mbowe.

Mbowe amezitaja taasisi na watu wengine wenye heshima kubwa ndani na nje ya nchi waliokiomba chama hicho kuahirisha maandamano na mikutano hiyo kuwa ni Mzee Joseph Butiku ambaye ni Mwenyekiti wa Tasisi ya Mwalimu Nyerere, Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA),  Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) pamoja na mjane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mama Maria Nyerere ambaye alizungumza na Edward Lowassa kwa niaba ya chama hicho.

“Kwa heshima ya viongozi wetu wa dini na taasisi hizi, tunawatangazia wanachama wetu kote nchini kuwa tunaahirisha maandamano hayo kwa muda wa mwezi mmoja ili kuwapa nafasi viongozi hawa waonane na Rais Magufuli na kama asipowaelewa hata hao, sisi tusilaumiwe,” amesisitiza Mbowe.



 
 

Reviewed by RICH VOICE on Agosti 31, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...