Sethi Agoma Kuvuliwa Madaraka IPTL
Siku
chache baada ya kuondolewa katika Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya
Kufua Umeme ya IPTL, mfanyabiashara Herbinder Sethi ameeleza
kusikitishwa kwake na hatua hiyo, huku akisema hautambui uongozi mpya
uliowekwa madarakani.
Uamuzi
wa kumwondoa Sethi katika bodi ya wakurugenzi ambayo pia ilimvua
uenyekiti wa IPTL, ulifikiwa baada ya kushindwa kushiriki na kuhudhuria
mikutano ya bodi kwa miezi sita mfululizo bila ruhusa, tangu Juni 19,
2017 alipokamatwa na kushtakiwa.
Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimsomea Sethi mashtaka 12 ya uhujumu uchumi,
utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Dola 22.198
milioni za Marekani (Sh309.5 bilioni).
Hata
hivyo, taarifa kutoka kwa wakili wake, Hajra Mungula iliyotolewa jana
kupitia mitandao ya jamii ilisema Sethi hatambui mabadiliko ya uongozi
uliowekwa na kwamba yeye ni mmiliki halali wa IPTL ambayo kimsingi
inamilikiwa na kampuni anayoimiliki ya Pan African Power Solutions
(PAP).
“Pamoja
na kuagiza wanasheria wake kuchukua hatua za haraka za kisheria,
Mwenyekiti Sethi pia hana taarifa zozote juu ya mabadiliko hivyo
anapenda kuutaarifu umma wazipuuze taarifa hizo kwa kuwa hazitokani na
mamlaka halali ya kisheria ya kampuni hiyo,” ilisema taarifa ya Mungula
Mungula
alisema mabadiliko hayo yamekwenda kinyume na notisi ya katazo la
Mwanasheria Mkuu wa Serikali la Februari 12, 2018 lenye kumbukumbu Na.
AGS234 lililozuia aina yoyote ya uhamishaji wa mali na umiliki wa mali
za IPTL.
“Kimsingi mabadiliko hayo batili yanaathiri na kwenda kinyume na maelekezo ya Serikali.
“Pamoja
na kwamba Mwenyekiti bado yuko mahabusu akituhumiwa kwa mashtaka kadhaa
ya jinai, hiyo haiondoi ukweli kuwa IPTL ni kampuni binafsi yenye
wamiliki halali wenye hisa halali, hivyo haiwezekani kwa mtu asiyehusika
na asiye mwanahisa kutangaza mabadiliko ya uongozi bila kufuata
taratibu zilizopo kisheria,” alisema Mungula.
Alisisitiza
kwamba licha ya Sethi kuwa na mashtaka ya jinai yanayomkabili, lakini
Watanzania wajue bado kampuni hiyo iko chini ya usimamizi salama wa PAP
na kwamba madeni yote, madai ya mali na stahiki zote zinazohusiana na
kampuni hiyo zipo katika mikono salama.
Sethi Agoma Kuvuliwa Madaraka IPTL
Reviewed by RICH VOICE
on
Mei 18, 2018
Rating:
Hakuna maoni