Wednesday, November 16, 2016

Rais wa Congo Joseph Kabila atangaza kutokuwania Urais tena



Rais wa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo Joseph Kabila, amelihutubia Bunge la Taifa jana na kuwahkikishia wananchi kuwa hatogombea tena Urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Rai Kabila amesema anaiheshimu katiba ya nchi yake na kwamba ataifuata huku akisisitiza kuwepo kwa amani na utulivu.

“Jahmuri ya Kidemorisia ya Congo ni nchi inayoongozwa na katiba, hatujakiuka katiba na tutaendelea kuiheshimu. Kwa mda huu kilicho muhimu ni kuangalia maisha ya wakongo,” alisema Kabila.

Hata hivyo, juzi waziri mkuu Augustina Matata Ponyoa alijiuzulu kutoa nafasi wadhifa huo kuchukuliwa na upinzani kwenye utawala wa mpito.

Hatua hii ni ya kutuliza vurugu za kisiasa nchini humo baada ya vyama vikuu vya kisiasa kususia mazungumzo ya kitaifa.

Awali Kamisheni ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iliahirisha uchaguzi wa rais uliokuwa umepangwa kufanyika mwaka huu hadi mwezi Julai mwakani.

Pia, Mahakama ya juu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilitangaza kuwa iwapo serikali ya Rais Joseph Kabila haitaweza kuandaa uchaguzi wa rais katika wakati ulioainishwa basi kiongozi huyo anaweza kubakia madarakani.

Kabila alishika hatamu za kuiongoza Congo mwaka 2001 baada ya mauaji ya baba yake, Laurent Kabila, na kisha akashinda uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka 2006.
 
 

Wednesday, November 16, 2016

Vyeti FEKI vya vifo Vyatumika Kupata mikopo Elimu ya Juu


Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imebaini kuwepo kwa baadhi ya wanafunzi ambao wamewasilisha vyeti feki vya vifo vya wazazi wao ili waonekane kama ni watoto yatima; hivyo wapewe kipaumbele cha kupatiwa mkopo.

Kuwepo kwa vyeti hivyo vya bandia kumegunduliwa na bodi hiyo baada ya kupeleka nakala za vyeti vyote vya vifo ofisi ya Msajili wa Vizazi na Vifo (Rita) kwa ajili ya uthibitisho ndipo ikagundulika kuwepo kwa kasoro hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul- Razaq Badru, amesema  kuwa wahusika wote ambao wamewasilisha vyeti hivyo feki suala lao limekabidhiwa kwa mamlaka zinazoshughulika na makosa ya jinai.

Hata hivyo, Badru hakutaka kuingia kwa undani kuhusu suala hilo kwa maelezo kuwa bado wanaendelea na ukaguzi.

“Bado tunaendelea kuchunguza na idadi yao hapa sina, tukikamilisha tutawaita kuwaambia idadi yao,” alisema Badru na kuongeza kuwa kutokana na kasoro hizo, ndio maana kuna baadhi ya watu wanaolalamika kuwa ni yatima, lakini hawakupata mkopo. 

“Hayo malalamiko ya kwamba kuna yatima wamekosa mikopo tumeyasikia, lakini na sisi tunajiridhisha kuwa huyu ni yatima baada ya kupata uthibitisho wa vyeti vya vifo kutoka Rita,” alisema Badru.

Aliongeza kuwa hata wale ambao ni wanafunzi wenye ulemavu, bodi hiyo haiwezi kuwaamini kama ni walemavu, bali hadi wapate uthibitisho kutoka kwa daktari wa wilaya (DMO) kuthibitisha ulemavu wa mwombaji.

Alisema baadhi ya wanafunzi ambao wanalalamika kuwa wamekosa mikopo ni wale ambao maombi yao yalikaguliwa na kukutwa na dosari kadhaa, na wakaombwa wazirekebishe kasoro hizo, lakini baadhi yao hawakufanya hivyo.

Badru alisema bodi yake baada ya kuchambua maombi ya waombaji wote; hadi sasa imeshatoa mikopo kwa wanafunzi wote wanaostahili wakiwemo yatima, walemavu, wanafunzi wanaosoma kozi za kipaumbele na wahitaji wanaosoma kozi zingine.

Akizungumzia suala la baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambao wamekosa mikopo na kulazimika kurudi makwao, Badru alisema wanafunzi hao yawezekana ni miongoni mwa wale ambao hawakukidhi vigezo vya kuweza kupewa mkopo.

“Pale Dodoma tumetoa mkopo kwa wanafunzi wapya takribani 3,000, hivyo hao wanaoondoka kurudi nyumbani yawezekana wako kwenye kundi la wanafunzi ambao hawakukidhi vigezo vya kupewa mkopo,” alisema Badru.

Alisema sio rahisi kutoa mkopo kwa wanafunzi wote, kwani Serikal inaendeshwa kwa bajeti na mwaka huu wamechagua kusomesha wanafunzi 25,000 kulingana na bajeti iliyopo pamoja na kulingana na mahitaji ya wataalamu wanaotakiwa na kutokana na vipaumbele vyake.

Alisema anatambua kuna wanafunzi zaidi ya 10,000 ambao wamekosa mikopo na kuongeza; “lakini bajeti ya mwaka huu imeishia hapo, mwaka kesho tunaweza kuishauri Serikali iongeze fedha baada ya kuwa tumefanya tathmini uhitaji wa mikopo hiyo.”

Hata hivyo, Badru alisema kuna wanafunzi ambao wanasoma kozi za kipaumbele, lakini wazazi wao wana uwezo, hao nao hawakupatiwa mikopo licha ya kuwa kwenye kundi la wanaostahili mkopo.

“Kuna mtu anasomea udaktari, lakini wazazi wake wana uwezo, na kuna mwanafunzi anasomea sayansi ya jamii na wazazi wake ni watu wasio na uwezo, hapo lazima tuangalie mhitaji ni yupi kati ya hao wawili na ndiye tunampatia mkopo,” alisema Badru.

Alisema kuna wanafunzi wanasoma kozi za kipaumbele baadhi yao hawakupata mkopo kabisa na baadhi yao wamepatiwa mkopo kidogo baada ya bodi hiyo kufanya tathmini ya hali ya uchumi ya wazazi au walezi wa mwombaji.
 
 

Wednesday, November 16, 2016

Waziri wa Ujenzi Prof. Mbarawa atoa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi Mkuu wa ATCL kufanya mabadiliko ya menejimenti ya Shirika hilo


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kufanya mabadiliko katika menejimenti ya Shirika hilo ili kuongeza ufanisi na kuboresha utendaji kazi.

Ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza katika mkutano wa Menejimenti pamoja na wafanyakazi wa Shirika hilo na kuwataka kutoa huduma bora ili kulifanya Shirika hilo kuwa miongoni mwa mashirika bora ya ndege barani Afrika.

“Nataka ndani ya mwezi mmoja uwe umeshafanya mabadiliko katika menejimenti, mabadiliko lazima yaanzie juu kwanza kwa watoa maamuzi na ishuke hadi kwa wafanyakazi wazembe na wasio waadilifu,” amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Mbarawa amepinga nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi wa Shirika hilo hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali ipo katika juhudi za kulifufua na kuliimarisha Shirika hilo.

Aidha Waziri Mbarawa ameitaka Idara ya Masoko ya shirika hilo kuzunguka katika taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake na kuzishawishi kuweza kutumia huduma za usafiri wa anga wa ATCL.

“Serikali imekamilisha upande wake wa ununuzi wa ndege, sasa kazi inabaki kwenu, sitaki watu wa masoko kukaa ofisini”, amesema Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa wafanyakazi wa ATC wanatakiwa kujipanga kutoa huduma iliyotukuka kwa wateja wake ili kuweza kuhimili ushindani uliopo katika mashirika ya ndege nchini.

“Inabidi tofauti kubwa ionekane kati yenu na mashirika mengine, yeyote ambaye anaona hawezi kutoa huduma bora kwa mteja atafute sehemu nyingine kwani hapa hatufai ”, amesisitiza Waziri Mbarawa.

Profesa Mbarawa amelitaka shirika hilo kutumia mfumo wa kisasa wa kukata tiketi kwa njia ya simu na kompyuta ili kuwarahishia watumiaji wa shirika hilo kuweza kupata tiketi kwa haraka na urahisi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Eng. Ladislaus Matindi amemhakikishia Waziri Mbarawa kufanyia kazi maagizo aliyotoa na kuahidi kuboresha utendaji kazi wa shirika hilo kwa lengo la kuteka soko la ushindani wa usafiri wa anga nchini.

“Kwa sasa tumeanza vizuri na naamini uwezo wa kuzalisha faida zaidi tunao, tunaahidi kuboresha utendaji kazi ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Serikali ya Awamu ya Tano,” amesema Eng. Matindi.\
 
 

Wednesday, November 16, 2016

Dr. Shein Atia Saini Sheria ya Gesi na Mafuta.....Asema Wanaoikosoa ni Wachoyo na Hawana Nia Njema na Zanzibar


Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, jana amesaini sheria ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ya Zanzibar.

Mbali ya kusaini sheria hiyo, amewapiga kijembe wanaoikosoa sheria hiyo kuwa ni wachoyo na wasioitakia mema Zanzibar.

Dk. Shein aliwaambia viongozi na waandishi wa habari kuwa sheria hiyo namba 6 ya mwaka 2016, inaipa Zanzibar mamlaka ya kisheria ya kuendeleza rasilimali ya mafuta na gesi asilia.

Alisema kitendo cha kutia saini sheria hiyo, hakijavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano kama baadhi ya watu wanavyodai.

“Hakuna aliyevunja sheria, anayevunja sheria wala atakayevunja sheria. Lakini kama wao wanadai kutia saini sheria hii ni kuvunja sheria, basi watafute suluhisho la kisheria,” alisema.

Aliwashauri wenye mawazo hayo wakasome vizuri Sheria ya Mafuta Namba 21 ya 2015 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo imeweka msingi imara wa kisheria wa kutambua rasilimali ya mafuta na gesi asilia ni miongoni mwa mambo yaliyoorodheshwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo yanahitaji usimamizi bora na imara wa kisheria.

Alisema sheria hiyo imeainisha mambo makuu matatu ambayo kwanza ni kuwa shughuli zote za mafuta na gesi asilia kwa upande wa Tanzania Bara zitasimamiwa na taasisi zilizoanzishwa ndani ya sheria namba 21 ya 2015.

Sheria hiyo inatamka pia kuwa shughuli zote za mafuta na gesi asilia kwa upande wa Tanzania Zanzibar zitafanywa na taasisi zitakazoanzishwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania Zanzibar.

Kuhusu mapato yatokanayo na shughuli hizo, Dk. Shein alisema sheria inatamka upande wa Tanzania Bara mapato yatatumiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa faida ya Tanzania Bara wakati kwa upande wa Tanzania Zanzibar yatatumiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa faida ya Zanzibar.

“Kila upande ulishiriki kikamilifu katika mchakato huu. Tulishauriana kwa kina viongozi na tukapata ushauri wa kutosha kutoka kwa wanasheria wetu wakuu hadi kufika bungeni,” alisema Dk. Shein.

Alisema anatambua sheria hiyo ni mpya na anaelewa changamoto ambazo zinaweza kutokea, lakini akatoa wito kwa wananchi kuiunga mkono na kushirikiana na Serikali.

“Mafuta ni jambo kubwa katika maendeleo, pia yasipotumika vyema yanaweza kuitikisa nchi,” alisema Dk. Shein.

Aliwatahadharisha wananchi kutegemea mafanikio ya haraka kutoka sekta hiyo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akionesha hati muswada wa sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi asilia ya mwaka 2016,baada ya kusaini hati hiyo katika hafla iliyofanyika jana ukumbi wa Ikulu Mjini Unguja,ambapo Viongozi mbali mbali wa Serikali na vyama vya Siasa walihudhuria hafkla hiyo,[Picha na Ikulu.]
Viongozi Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama Zanzibar wakiwa katika hafla ya utiaji saini muswada wa sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi asilia ya mwaka 2016,uliotiwa jana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein katika ukumbi wa Ikulu Mjini Unguja
Baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi na Viongozi mbali mbali wakiwa katika hafla ya utiaji saini muswada wa sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi asilia ya mwaka 2016,uliotiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein katika ukumbi wa Ikulu Mjini Unguja jana
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe,Zubeir Ali Maulid (kulia) na Waziri wa Nishati na Madini Mhe,Profesa Sospiter Muhongo,wakiwa katika hafla ya Utiaji wa saini muswada wa sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi asilia ya mwaka 2016,uliotiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,katika ukumbi wa Ikulu Mjini Unguja jana.
 
 

Wednesday, November 16, 2016

Meya wa West Virginia ajiuzulu baada ya kufurahia andiko lililomfananisha mke wa Obama na Nyani


Meya wa mji wa Clay nchini Marekani, Beverly Whaling amejiuzulu wadhifa huo  baada ya kuunga mkono maandishi yenye ubaguzi wa rangi kwenye facebook dhidi ya mke wa Rais Barack Obama, Michelle Obama.

Meya huyo aliingia matatani na kuamua kujiuzulu nafasi yake baada ya kuonesha kufurahishwa na ‘post’ ya kibaguzi iliyoandikwa na Mkurugenzi wa shirika moja la kutoa misaada, Pamela Taylor aliyelenga kubainisha tofauti kati ya mke wa Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump, Melania na mama Michelle Obama.

Taylor alimtusi Michelle akimfananisha na sokwe huku akimpamba Melania kuwa ni mrembo.

Meya huyo aliandika chini ya ujumbe huo wa kibaguzi, “Just made my day Pam.”

Zaidi ya watu 200,000 wamejiandikisha mtandaoni ndani ya muda mfupi kupinga ubaguzi huo na kuwataka Whaling na Taylor kujiwajibisha haraka.

Vitendo vya kibaguzi vimeripotiwa kuongezeka nchini humo tangu Trump alipotangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais.

Ingawa kauli zake wakati wa kampeni zilikuwa na matamko tata, Trump amewataka wafuasi wake kuacha mara moja vitendo vyovyote vya kibaguzi akisisitiza kuwa yeye atakuwa rais wa Wamarekani wote.
Reviewed by RICH VOICE on Novemba 16, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...