Wednesday, November 9, 2016

Treni Yanusurika Kuchomwa Moto na Wananchi....Vioo 30 vya Mabehewa Vyapasuliwa, 17 Watiwa Mbaroni


TRENI ya abiria  inayofanya safari zake kati ya Kituo Kikuu  cha Reli na maeneo ya Pugu  Dar es Salaam maarufu kama ‘Treni ya Mwakyembe’ nusura ichomwe moto juzi, baada ya wananchi   kudai kuchoshwa na usumbufu wa shirika hilo.


Wananchi hao walitaka warudishiwe nauli zao  kwa kile walichodai Shirika   la Reli Tanzania (TRL)  limeshindwa kuwa na ratiba inayoeleweka.


Tukio hilo lilitokea juzi  saa 3:00 usiku eneo la Majumbasita, baada ya treni hiyo kukaa kituoni hapo kwa muda mrefu bila kuambiwa kuambiwa chochote.


Hali hiyo iliwafanya abiria  kuvamia kituo kidogo cha mawasiliano kilichopo eneo hilo wakitaka warejeshewe  nauli zao vinginevyo wangekichoma moto pamoja na mabehewa ya treni hiyo.


Mwandishi aliwashuhudia abiria   wakitaka kuingia ndani ya kituo hicho huku wakiwalazimisha wafanyakazi waliokuwapo wawarudishie fedha zao za nauli.


Purukushani hiyo iliyodumu kwa takribani saa  mbili  ilimalizika kwa abiria hao kuvunja vioo vya mabahewa ya treni vipatavyo 30.


Wafanyakazi kuona hivyo walijifungia ndani ya kituo hicho  huku  polisi  waliokuwa wakisindikiza treni hiyo  wakitimua mbio   kunusuru  maisha yao.


Baadhi ya abiria walisema   tangu Ijumaa   iliyopita wamekuwa wakipata usumbufu kwa kukatishiwa tiketi huku treni  ikichelewa na wakati mwingine kutoonekana  kabisa.


Walisema  jambo hilo  limekuwa likiwasababishia hasara na kuwalazimu  kutafuta usafiri mwingine na   kuchelewa kufika  kwenye  majukumu yao.


Kufuatia kukithiri vitendo vya uharibifu wa miundombinu ya reli na treni vinavyofanywa na baadhi ya wananchi, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kupitia  kwa Mkurugenzi Mtendaji , Masanja Kadogosa imetoa onyo kwa wananchi kutofanya vitendo hivyo.

“Tukio hili si mara ya kwanza kujitokeza, lilijitokeza tarehe 24, 26 na 28 mwezi wa 10 na Novemba 7 Katika matukio hayo kulitokea uharibifu wa miundombonu na kujeruhi baadhi ya wafanyakazi wa TRL akiwemo Mustapha Omary ambaye ameshonwa nyuzi 8 katika hospitali ya mnazi mmoja,” amesema.

Amesema kutokana na uharibifu huo, watuhumiwa 17 wanashikiliwa na jeshi la polisi na kwamba upepelezi ukikamilika watachukuliwa hatua za kisheria.

Kadogosa amedai kuwa, wahusika wa fujo na uharibifu huo ni makondakta wa dalala kwa lengo la kutisha wananchi kutoutumia usafiri wa treni.

“Kuna watu wa daladala wanafikiri wataendelea kufanya fujo ili wananchi waone kuwa usafiri wa treni si salama wapande magari yao, sisi hatulazimishi wananchi kuutumia usafiri wetu ila kutokana na ubora wa huduma zetu wanakuja wenyewe. Pia hatusitishi kutoa huduma kwa sababu ya fujo zao sababu tutawatesa abiria wetu zaidi ya 21,000,”

Naibu Kamishna wa Polisi na Kamanda wa Reli, Simon Chillery amesema jeshi la polisi linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini wengine waliohusika.
 

 

 

Wednesday, November 9, 2016

Rais Barack Obama ampongeza Rais Mteule, Donald Trump na kumualika Ikulu kujadiliana juu makabidhiano ya ofisi.


Rais Barack Obama wa Marekani  amempongeza Rais Mteule wa taifa hilo, Donald Trump na kumualika Ikulu kujadiliana juu makabidhiano ya ofisi.


Wednesday, November 9, 2016

Msajili wa vyama vya siasa Tanzania, avifutia usajili Vyama Vitatu

SeeBait

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania Jaji Francis Mutungi ametangaza kuvifutia usajili vyama vitatu baada ya kubainika kukiuka sheria ya usajili wa vyama.


Vyama hivyo ni pamoja na CHAUSTA kilichopata usajili wa kudumu tarehe 5 Novemba 2001, The African Progressive Party of Tanzania ( APPT-Maendeleo) kilichopata usajili wa kudumu terehe 4 Machi 2003 na Chama cha Jahazi Asilia kilichopata usajili wa kudumu tarehe 17 Novemba 2004.


Jaji Mutungi amesema kuwa mchakato wa kufuta usajili wa vyama hivyo umetokana na zoezi la uhakiki wa utekelezaji wa masharti ya usajili na matakwa mengine ya sheria ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu lililofanyika kuanzia tarehe 26 Juni hadi 26 Julai 2016.


Amesema katika zoezi hilo uhakiki ulibaini kuwa vyama hivyo vimepoteza sifa za usajili wa kudumu kwa kukiuka masharti ya sheria ya vyama vya siasa, na kwamba kila chama kilipewa ya nia ya msajili kufuta usajili wake, lakini vikashindwa kutoa utetezi wa kuridhisha ili visifutiwe usajili.


Kufuatia uamuzi huo, Msajili amewataka waliokuwa wanachama wote wa vyama hivyo kutojiuhusisha na shughuli yoyote kwa majina ya vyama hivyo, na kwamba kufanya hivyo ni kuvunja sheria, huku akiviasa vyama vingine kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria.


Wednesday, November 9, 2016

Breaking News: Donald Trump Ndo Mshindi wa Kiti cha Urais wa Marekani

SeeBait

Mgombea wa Chama cha Republican, Donald Trump ameshinda uchaguzi mkuu wa Marekani baada ya kufikisha kura 276 huku Hillary Clinton akiwa na kura 218.

Hillary Clinton amempigia simu Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump na kumpongeza kufuatia ushindia huo alioupata.

Akizungumza na wafuasi wake baada ya kutangazwa mshindi, Trump amewataka raia wote wa Marekani, waliomchagua na ambao hawakumchagua kuungana na kuanza kuijenga nchi yao kwani muda wa kampeni na siasa za kugawanyika umekwisha.


 

Wednesday, November 9, 2016

Rais Magufuli Ampongeza Donald Trump Kwa Kushinda Kiti cha Urais Wa Marekani

SeeBait

Leo November 9, 2016 Marekani imeweka historia nyingine baada Donald Trump wa chama cha Republican kutangazwa mshindi wa kiti cha Urais, na tayari ameanza kupokea pongezi kutoka kwa viongozi wa nchi mbalimbali ikiwemo Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli.


Rais Magufuli ametoa pongezi zake kwa Rais Donald Trump kupitia ukurasa wake Twitter

Wednesday, November 9, 2016

Ratiba ya Mazishi ya Spika Mstaafu, Samwel John Sitta


Mwili wa aliyekuwa spika wa bunge,  Samuel Sitta unatarajia kuwasili nchini siku ya Alhamis ukitokea nchini Ujerumani ambapo alipokuwa akipatiwa matibabu.


Taarifa hiyo imetolewa na Gerald Mongela ambaye ni msemaji wa familia.  

Amesema mara baada ya mwili huo kuwasili nchini utapelekwa nyumbani kwa marehemu Masaki jijini Dar es Salaam na siku ya Ijumaa shughuli za kuaga zitafanyika katika viwanja vya Karimjee kisha kupelekwa bungeni mjini Dodoma.


“Mwili wa mpendwa wetu mheshimiwa Samuel Sitta utawasili na ndege ya Emirates siku ya Alhamis saa tisa na nusu alasiri na baada ya hapo mwili tutauleta hapa nyumbani kwaajili ya kukaa nao na kupumzika kusubiri ratiba ya Ijumaa,”alisema Mongela.


Mazishi ya Marehemu Samwel John Sitta yatafanyika siku ya Jumamosi Urambo mkoani Tabora. 

 

 

Wednesday, November 9, 2016

Serikali: Ukosefu wa ajira kwa vijana umepungua

SeeBait

Serikali ya Tanzania imesema kwamba kulingana na takwimu inaonesha kuwa  ukosefu wa ajira kwa vijana nchini Tanzania umepungua kwa asilimia mbili, kutoka asilimia 13.7 mwaka 2012 mpaka asilimia 11.7 mwaka huu.


Akizungumza jana bungeni, mjini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali na majibu Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu Mhe. Anthony Mavunde,  alisema licha ya kupungua huko kwa ukosefu wa ajira, serikali imeweka mipango ya kuwawezesha vijana kuwa na wigo mpana wa ajira nchini.


  Mhe. Mavunde alisema kuwa kwa takwimu hizo Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kutoa ajira kwa vijana wengi zaidi kushinda baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya na Uganda.

Wednesday, November 9, 2016

TRA Yakusanya Shilingi Trilioni 1.15 Mwezi Oktoba

SeeBait

Na Ally Daud-MAELEZO.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikia kukusanya shilingi trilioni 1.15 kwa mwezi Oktoba ikiwa ni kukamilisha malengo waliyojiwekea katika ukusanyaji wa mapato.


Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi Bw. Richard Kayombo wakati wa mkutano  na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu  hali ya makusanyo na zoezi la uhakiki wa namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN)linaloendelea hivi sasa.


“Tumefanikiwa kukusanya shilingi Trilioni 1.15 kwa mwezi Oktoba mwaka huu ikiwa ni kufanikisha malengo ya ukusanyaji kodi nchini ili kukuza uchumi wa nchi pamoja kusaidia Serikali kuendeleza huduma za jamii nchini” alisema Bw. Kayombo.


Aidha Bw. Kayombo amesema kuwa mapato hayo yametokana na mikakati thabiti iliyowekwa na mamlaka hiyo katika ukusanyaji kodi hapa nchini ili kuweza kusaidia ongezeko la pato la Taifa .


Katika hatua nyingine TRA imefanikiwa kushinda kesi 9 kati ya 10 zilizokuwa zikiendelea katika mahakama mbalimbali nchini dhidi ya walipa kodi wake na kufanikiwa kupata kiasi cha takribani Bilioni 16.9 .


“Tumefanikiwa kushinda kesi 9 kati ya 10 ambazo zilifikishwa mahakamani dhidi ya walipa kodi na kupata kiasi cha shilingi bilioni 16.9 hivyo kufanya juhudi zetu za kukusanya mapato mengi zaidi” aliongeza Bw. Kayombo.


Mbali na hayo Bw. Kayombo amesema kuwa zoezi la uhakiki wa namba za utambulisho wa mlipa kodi ambalo limeanza hivi karibuni linaendelea na litafikia tamati Novemba 30 mwaka huu kwa mkoa Dar es salaam hivyo wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya uhakiki huo.


Aidha Bw. Kayombo ameongeza kuwa  kila mwenye namba ya utambulisho wa mlipa kodi anatakiwa akahakiki kwa ajili ya kupata taarifa sahihi za mlipa kodi ili kuepuka kufutwa kwa  namba yake ya utambulisho baada ya zoezi hilo kumalizika kwa mkoa husika.


HABARI ZA KIMATAIFAA


Habari | 09.11.2016 | 16:16

Rais Barack Obama wa Marekani amemwalika ikulu hapo kesho alkhamisi mshindi wa uchaguzi wa rais Donald Trump. Msemaji wa ikulu ya Marekani,Josh Earnest amesema rais Obama anapanga kumueleza Trump kuhusu kipindi cha mpito kilichoandaliwa na washirika wake.Tajiri huyo asiyekuwa na maarifa yoyote ya kisiasa ameshinda kwa mshangao wa wengi,uchaguzi wa rais na ataingia ikulu ya White House january 20 kama rais wa 45 wa Marekani. Katika hotuba yake ya ushindi mara baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa,Trump amesema atakuwa rais wa kila mmarekani. Kuhusu siasa ya nje,ameahidi kushirikiana na mataifa yote yatakayokuwa tayari kufanya hivyo. Chama cha Trump,Republican kinashikilia pia wingi wa viti katika mabaraza yote mawili ya bunge la Marekani-Congress

 

 

 

Kansela Angela Merkel amempongeza rais mteule wa Marekani Donald Trump.Akizungumza mjini Berlin kansela Angela Merkel amekumbusha uhusiano wa dhati kati ya nchi hizi mbili na kusema:"Ujerumani na Marekani zinashikamana chini ya misingi ya Demokrasia,uhuru,kuheshimu haki na hadhi ya binaadamu bila ya kujali asili yake,rangi yake ya ngozi,dini,jinsia wala mwelekeo wake kijinsia au kisiasa. Natangaza utayarifu wa kushirikiana na Trump chini ya misingi hiyo ya maadili."Wanasiasa nchini Ujerumani wamepigwa na mshangao kutokana na ushindi wa Donald Trump. Mambo hayatakuwa rahisi,yatakuwa magumu zaidi amesema waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinemeier huku waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen akiutaja ushindi wa Donald trump kuwa ni mshituko mkubwa.

 

 

 

Mwenyekiti wa baraza la Ulaya,Donald Tusk na mwenzake wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya,Jean-Claude Juncker wanapanga kuandaa haraka iwezekanavyo mkutano wa kilele pamoja na rais mteule wa Marekani Donald Trump. Katika risala yao ya pongezi,viongozi hao wa Umoja wa ulaya wamemwalika Trump aitembelee Ulaya."Wakati huu ni muhimu kuliko wakati wowote ule mwengine kuimarisha uhusiano miongoni mwa nchi zinazopakana na bahari ya Atlantik,wamesema katika risala yao ya pongezi,wakizingatia masuala kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi,mapambano dhidi ya ugaidi,wakimbizi na mzozo wa Ukraine. Mkutano wa kilele kati ya Umoja wa ulaya na Marekani utafungua njia ya kusawazisha mambo kwa kipindi cha miaka minne inayokuja. Nae waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amependekeza uitishwe mkutano wa mawaziri wa nchi za nje wa nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani. Mkutano huo ungepaswa kuitishwa jumamosi ijayo mjini Luxemburg,siku moja kabla ya kikao cha kawaida cha mawaziri wa nchi 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya.Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May anasema nchi yake na Marekani ni washirika wakubwa wa biashara,usalama na ulinzi na hali hiyo haitobadilika. Na waziri mkuu wa Italy pia,Matteo Renzi amempongeza Trump na kusema ana hakika uhusiano wa kirafiki kati ya Italy na Marekani utaendelea kuwa madhubuti.

 

 

Maandamano dhidi ya Trump yameripotiwa karibu na pwani ya California,baada ya mgombea wa chama cha Republican kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais-Habari hizo zimetangazwa na maripota wa shirika la habari la Reuters na wa vyombo vyengine vya habari vya eneo hilo. Waandamanaji wametia moto sanamu la Trump,wamevunja maduka na madirisha na kutia moto taka taka na mipira ya magari katika eneo la Oakland,katika pwani ya San Franasisco. Masafa machache kutoka hapo,katika chuo kikuu cha California,wanafunzi wa Berkley pia waliandamana katika uwanja wa chuo kikuu. Maandamano yameripotiwa pia katika eneo jengine la chuo kikuu cha California-Davis ambako wanafunzi waliweka vizuwizi majiani,na kuongozana huku wakiimba nyimbo dhidi ya Donald Trump. Mwanaharakati mmoja aligongwa na gari huko Oakland alipokuwa anaweka vizuwizi katika njia kuu.

Reviewed by RICH VOICE on Novemba 09, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...