Friday, November 11, 2016
Rais Magufuli aongoza mamia ya Watanzania kuaga mwili wa Samuel Sitta
Mwili
wa aliyekuwa spika wa bunge la Tanzania, Samuel Sitta umeagwa katika
viwanja vya Karimjee na mamia ya watanzania wakiongozwa na Rais wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Makamu wa Rais mama Samia Suluhu.
Wengine ni Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Dk. Gharib Bilal.Baada ya kuagwa Dar, mwili wake utapelekewa Dodoma kwa ajili ya wabunge kutoa saamu za mwisho kisha kupelekwa Urambo, Tabora.
Friday, November 11, 2016
Agizo la Serikali kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha sita mwezi Mei mwaka huu Ambao Hawakujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)
Serikali
amewaagiza wote waliohitimu kidato cha sita Mei mwaka huu na ambao
hawajajiunga na vyuo vya elimu ya juu, wakaripoti katika kambi za Jeshi
la Kujenga Taifa (JKT) Desemba Mosi, mwaka huu.
Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi ametoa agizo
hilo mjini Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa
Habari wa Bunge.
Dk
Mwinyi alisema Mei na Juni mwaka huu, JKT iliwafanyia usaili vijana wa
kujiunga na JKT kwa kujitolea. Alisema usaili huo ulifanyika kwa
kushirikiana na kamati za ulinzi za wilaya na mikoa.
“Wizara
ya Ulinzi na JKT inapenda kuwatangazia vijana wote waliosailiwa Juni
mwaka huu, kujiunga na JKT kwa kujitolea, waripoti kwenye kambi
walizopangiwa ifikapo Desemba Mosi mwaka huu kwa nauli zao,” amesema Dk Mwinyi.
Dk Mwinyi amesema mafunzo hayo ni ya miezi mitatu kwa mafunzo yenye utaratibu wa kawaida na miaka miwili kwa wa kujitolea.
Ili
kufanikisha hilo, Wizara ilimuagiza Mkuu wa JKT kufufua kambi ya
Makuyuni JKT iwe miongoni mwa kambi kuanzia Desemba mwaka huu.
Aliagiza kambi za Luwa na Milundikwa za mkoani Rukwa, zirejeshwe kwa shughuli za JKT za kilimo na ufugaji.
Dk
Mwinyi alimuagiza Mkuu huyo wa JKT pia kambi ya Mpwapwa irejeshwe kwa
ajili ya kuendesha mafunzo ya kilimo na ufugaji ndani ya JKT.
Friday, November 11, 2016
Mahakama Yampa Siku 7 Profesa Lipumba na Msajili wa Vyama Kujibu Hoja za CUF
Mahakama
Kuu imewapa siku saba Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis
Mutungi na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake kujibu
madai ya chama hicho.
Msajili,
Lipumba na wenzake walipewa muda huo jana na Jaji Sekieti Kihiyo
kutokana na kesi ya madai iliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa CUF
mahakamani hapo.
Katika
kesi hiyo namba 23 ya mwaka 2016, bodi ya wadhamini CUF inaiomba
mahakama itoe amri ya kubatilisha barua ya Msajili inayomtambua Profesa
Lipumba kuwa ndiye mwenyekiti wa chama hicho.
Pia,
wanaiomba mahakama itoe amri ya kumzuia Msajili kufanya kazi nje ya
mipaka yake ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yake na pia itoe
amri ya kumzuia Msajili kuingilia masuala ya kiutawala ndani ya chama
hicho.
Mbali
na Msajili na Profesa Lipumba, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wanachama wengine tisa
waliosimamishwa uanachama wa chama hicho, akiwamo Naibu Katibu Mkuu Bara
ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua (Tabora), Magdalena Sakaya.
Kesi
hiyo ilitajwa jana mahakamani hapo kwa mara ya kwanza tangu
ilipofunguliwa Oktoba 19, mwaka huu na mahakama ikataka wadaiwa
kuwasilisha majibu ya madai hayo ya CUF, Novemba 17, mwaka huu.
Pia,
Mahakama ilielekeza upande wa Maalim Seif kuwasilisha majibu ya hoja za
wadaiwa Novemba 23 na ikapanga kesi hiyo itajwe tena Novemba 24, kwa
ajili ya kuendelea na hatua nyingine.
Wadai
katika kesi hiyo wanawakilishwa na mawakili Juma Nassoro na Halfani
Daim wakati Msajili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wanawakilishwa na
Wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Obadia Kameya na Lipumba na wenzake
wakiwakilishwa na Mashaka Ngole.
Katika
hati ya Kiapo kinachounga mkono maombi hayo, Maalim Seif anadai kuwa
Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka ya kuingilia utendaji wa ndani
wa Vyama vya Siasa.
Anadai
kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya nchi haimpi mamlaka Msajili
wa Vyama vya Siasa kuwa chombo cha rufaa wala kurejea mambo ya utawala
ndani ya chama cha siasa.
Badala
yake anadai mamlaka hayo yako kwa vyombo vya juu vya chama na Mahakama
na kwamba jukumu la Msajili ni kusajili vyama na kuweka kumbukumbu za
vyama hivyo.
CUF
kimekuwa na mgogoro wa kiuongozi baada ya Profesa Lipumba kuandika
barua ya kutengua uamuzi wake wa awali wa kujiuzulu ambao Msajili
alikubaliana naye na alikiandikia barua chama kuendelea kumtambua
mwenyekiti huyo. Hata hivyo, CUF ilimfukuza uanachama Lipumba.
Friday, November 11, 2016
Misiba Yasitisha Mkutano wa Bunge Mjini Dodoma Leo
Mkutano wa Tano wa Bunge umeahirishwa kwa namna yake baada ya muhimili huo wa dola kupata misiba mikubwa miwili.
Misiba
hiyo ni wa Spika Mstaafu, Samuel Sitta aliyefariki nchini Ujerumani na
Mbunge wa Dimani(CCM) Hafidh Ally ambaye alifariki dunia usiku wa
kuamkia leo (Ijumaa) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Dodoma.
Mara
baada ya kutangaza kifo cha Hafidh Spika wa Bunge, Job Ndugai
alimtaka Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge, Ajira, Kazi,
Vijana Jenista kutengua kanuni ili kuwezesha mambo vote kufanyika.
Spika
alimtaka Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo Ndogo, Andrew
Chenge kuhitimisha hoja yake ya taarifa ya Kamati iliyowasilishwa juzi
bila kujadiliwa na wabunge ili Serikali yaweze kufanyia kazi.
Baada ya kufanya hiyo, Spika ameahirisha bunge hadi saa 8.30 mchana kwa ajili ya kikao maalum cha Bunge.
Amesema
mara baada kikao maalum cha bunge kumuaga Sitta basi Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa atatoa hoja yake kuahirisha Bunge kwa kifupi sana
tofauti na wakati mwingine.
Friday, November 11, 2016
LIVE: Fuatilia Hapa Zoezi la Kuuaga Mwili wa Samwel Sitta ambalo Linaongozwa na Rais Magufuli
Leo
kuna shughuli ya kuaga mwili wa aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia Spika wa Bunge Maalum la
Katiba(BMK), Marehemu Samwel Sitta.
Rais Magufuli ataongoza waombolezaji kuuaga mwili wa Marehemu Sitta katika Viwanja vya Karimjee.
Friday, November 11, 2016
BOT Yasitisha Kuweka Dhahabu Kama Hazina Ya Rasilimali Za Kigeni
Benki
Kuu ya Tanzania (BOT) imesitisha kuweka dhahabu kama hazina ya
rasilimali za kigeni kwa sababu ya kuyumba kwa bei ya madini hayo katika
soko la dunia na kusababisha uwezekano wa kupunguza thamani ya hazina
ya rasilimali ya nchi.
Kauli
hiyo imetolewa jana mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Igunga Mhe.
Dalaly Kafumu aliyehitaji kufahamu sababu za Serikali kukataa kutunza
dhahabu safi katika Benki Kuu wakati Tanzania ni nchi mojawapo
inayozalisha dhahabu safi.
Mhe.
Kijaji alisema kuwa jukumu la msingi la Benki Kuu ni kuandaa na
kutekeleza Sera ya Fedha inayolenga kuwa na utulivu wa bei kwa ajili ya
ukuaji endelevu wa uchumi wa Taifa hivyo ili kufanikisha azma hiyo Benki
Kuu inadhibiti ongezeko la ujazi wa fedha kwa kutumia nyenzo mbalimbali
zikiwemo za kuuza dhamana na hati fungani za Serikali pamoja na
kushiriki katika soko la jumla la fedha za kigeni kati ya mabenki.
“Katika
kutekeleza jukumu lake la msingi, Benki Kuu hutunza hazina ya
rasilimali za kigeni zinazotosha kuagiza bidhaa nje kwa kipindi
kisichopungua miezi minne lakini kwa muda mrefu sasa Benki Kuu ya
Tanzania haiweki dhahabu kama sehemu ya rasilimali hizo kutokana na
kuyumba kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia”, alisema Mhe. Kijaji.
Naibu
Waziri huyo alitoa mfano wa kushuka kwa bei ya dhahabu katika soko la
Dunia ambapo dhahabu ilishuka kutoka dola 1,745 za kimarekani katika
mwezi Septemba 2012 hadi dola za kimarekani 1,068 kufikia mwezi Desemba
2015.
Mhe.
Kijaji alifafanua kuwa hazina ya rasilimali za kigeni zinaweza kuwa
dhahabu – fedha (monetary gold) au fedha za kigeni ambapo uamuzi kuhusu
hazina itunzwe vipi unazingatia vigezo mbalimbali vikiwemo vile vya
kudumisha thamani, wepesi wa kubadilisha pamoja na faida inayopatikana
kwa kuwekeza hazina hiyo.
Aidha,
Mhe. Kijazi alisema kuwa ununuzi na uuzaji wa madini ya dhahabu
unahitaji ujuzi maalum ambapo kwa kuzingatia jukumu la msingi la Benki
Kuu inaonyesha dhahiri kuwa Benki hiyo haijajijengea uwezo katika eneo
la biashara ya madini hayo.
Friday, November 11, 2016
TANZIA: Mbunge Hafidh Ali Tahir Afariki Dunia Alfajiri ya Leo Akiwa Mjini Dodoma
Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia, Job Ndugai (Mb) anasikitika
kuwatangazia kuwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani, Zanzibar, Hafidh
Ali Tahir amefariki dunia leo saa 9 alfajiri katika Hospitali ya
General mkoani Dodoma.
Spika anaungana na Wabunge wote katika kuomboleza msiba huu.
Awali
Marehemu pia alikuwa mwalimu wa soka kwenye timu ya Bunge Sports Club
na mpaka usiku wa Novemba 10 alikuwa pamoja na Wabunge katika vikao
mpaka saa 2.45 usiku.
Friday, November 11, 2016
Picha 5: Mwili wa Spika Mstaafu Samwel Sitta Uliyopokelewa Airport Jijini Dar es Salaam
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan jana aliongoza
viongozi na wananchi katika mapokezi ya Mwili wa Spika Mstaafu Samuel
Sitta katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere
Jijini Dar es Salaam ukitokea nchini Ujerumani alipofariki wakati
anapatiwa matibabu.
Akizungumzia jinsi anavyomfahamu Samuel Sitta katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alisema Taifa limeondokewa kiongozi mwadilifu,mzalendo, mchapakazi na mtetezi wa wanyonge hivyo taifa litaendelea kuumuenzi utendaji wake.
Viongozi
mbalimbali waliojumuika na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Samia Suluhu Hassan katika mapokezi ya mwili wa Spika Mstaafu
Samweli Sitta kweye Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere ni
pamoja na Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Seif Ali
Iddi, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika, Kikanda na
Kimataifa Dkt Augustine Mahiga na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul
Makonda.
Baada ya Mwili wa Spika Mstaafu Samuel Sitta kuwasili nchini jana mchana alipelekwa nyumbani kwake Masaki jijini Dar es Salaam ambapo leo asubuhi viongozi na wananchi watatoa heshima zao ya mwisho za kuuaga mwili wa marehemu katika viwanja wa Karimjee jijini.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
akimpokea mjane wa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Waziri Mwandamizi Mstafu Marehemu Samuel Sitta, Mama
Margaret Sitta (kushoto) mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege
wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
akiwaongoza viongozi mbali mbali wakati wa mapokezi ya mwili wa Spika
Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri Mwandamizi
Mstafu Marehemu Samuel Sitta
Friday, November 11, 2016
Reli ya Standard Gauge kutoka Dar-Mwanza kuanza kujengwa Disemba, 6 mwaka huu
Hatua
ya kwanza ya maandalizi ya ujenzi wa reli ya Standard Gauge imeshaanza
ambapo awamu ya kwanza ya ujenzi huo kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza
itaanza rasmi Disemba 6, 2016.
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania
(RAHCO) Masanja Kadogosa amesema serikali imetenga trilioni 1 kwa ajili
ya ujenzi huo.
“Ujenzi wa reli ya standard gauge umeshaanza lakini hatua iliyokuwepo haionekani, tenda zimeshaanza kutangazwa,” alisema Kadogosa wakati akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.
Alisema
ujenzi huo utaanza kwa awamu na kwamba awamu ya kwanza inatarajiwa
kuanzwa Disemba 6, 2016 wakati ya pili itaanza Februari 15, 2016.
“Ujenzi
huo utachukua miaka mitatu kukamlika, ambapo utaleta manufaa kwa kizazi
cha sasa na kijacho. Pia utarahisisha usafirishaji wa mizigo kutokana
na kwamba litakuwa na mabehewa yenye kilomita 2 ambayo sawa na ukubwa wa
maroli 300,” alisema.
Alisema wamiliki wa majengo yatakayo athiriwa na ujenzi huo watalipwa fidia.
“Hifadhi
ya reli ina maana kwamba kila upande inaachwa mita 30, hivyo kama kuna
nyumba zitakazokuwa nje ya mita hizo zitatakiwa kubolewa wamiliki
watalipwa fidia,” alisema.
Aidha, Kadogosa alisema
kuna miradi mingine midogo ya ujenzi na ukarabati itafanyika ikiwemo ya
ujenzi wa reli mpya ya Dar es Salaam ambayo itatumiwa kwa ajili ya
usafiri kwa wakazi wa jiji hilo.
“Kuna
Mradi wa kujenga reli mpya katika jiji la Dar es Salaam na viunga vyake
kwa ajili ya treni za abiria ili kupunguza msongamano wa abiria na
magari. Mradi huu uko katika hatua ya upembuzi yakinifu na usanifu wa
awali chini ya kampuni ya ushauri ya GIBB Engineering ya Afrika Kusini
na kwamba inatarajiwa kukamilika Disemba 2016,” alisema.
Friday, November 11, 2016
Picha: Rais Magufuli Alivyoongoza wananchi wa Dar kuaga mwili wa Marehemu Joseph Mungai
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, jana tarehe 10 Novemba, 2016 aliwaongoza
viongozi na wananchi wa Dar es Salaam kuuaga mwili wa Waziri na mbunge
Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Joseph James Mungai katika
ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na Rais Magufuli Viongozi wengine waliofika kuuaga mwili wa Marehemu Mungai ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, Makamu wa Rais Mstaafu, Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba, Waziri Mkuu Mstaafu. Frederick Tluway Sumaye, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi na Viongozi wengine mbalimbali wa Serikali na Siasa.
Joseph
James Mungai alifariki dunia tarehe 08 Novemba, 2016 katika hospitali
ya Taifa Muhimbili baada ya kuugua ghafla na mwili wake utasafirishwa leo Ijumaa kwenda Mafinga Mkoani Iringa kwa Mazishi
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na waombolezaji waliofika kuaga mwili wa Marehemu Joseph
Muungai katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam Novemba 10,2016
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Rais
Mstaafu awamu ya tatu Benjamin Mkapa pamoja na waombolezaji wengine
walipofika kuaga mwili wa Marehemu Joseph Muungai katika Ukumbi wa
Karimjee jijini Dar es salaam Novemba 10,2016
Reviewed by RICH VOICE
on
Novemba 11, 2016
Rating:
Hakuna maoni