Thursday, November 10, 2016

Wanafunzi hewa 65,198 wabainika shule za msingi, sekondari nchini

SeeBait
Jumla  ya wanafunzi hewa 65,198 wamegundulika kuwepo katika shule za msingi na sekondari nchini, ambako idadi ya wanafunzi hao isingebainika kiasi cha Sh milioni 931.3 zingepelekwa shuleni kuhudumia wanafunzi hewa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Katika mkutano na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alisema kati ya wanafunzi hao wa shule za msingi ni 52,783 na sekondari ni 12,415.

Simbachawene alisema kazi ya uhakiki wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari ilifanyika mikoa yote nchini kutokana na agizo la Ofisi ya Rais, Tamisemi kwa makatibu tawala wa mikoa yote ya Tanzania Bara.

Alisema waliagizwa kuhakiki idadi ya wanafunzi katika shule zote za msingi na sekondari kwa kulinganisha taarifa ilivyokuwa Machi mwaka huu wakati wa ujazaji wa madodoso ya takwimu za shule za awali, takwimu za shule za msingi, sekondari na nyaraka za mahudhurio ya wanafunzi.

Alieleza kuwa taarifa za idadi ya wanafunzi kabla ya kuhakiki Machi 2016, zilionesha kulikuwa na wanafunzi 9,746,534 wa shule za msingi na wanafunzi 1,483,872 wa shule za sekondari.

“Baada ya uhakiki tuliofanya Septemba mwaka huu, inaonesha kuwepo wanafunzi 9,690,038 wa shule za msingi na wanafunzi 1,429,314 wa shule za sekondari,” alieleza na kuongeza kuwa uchambuzi umeonesha kuwa wanafunzi 52,783 wa shule za msingi na wanafunzi 12,415 wa sekondari hawakutolewa maelezo ya uwepo wao shuleni.

Alisema kwa tafsiri rahisi hao ni wanafunzi hewa kwa shule za msingi na sekondari nchini, ambao idadi hiyo ya wanafunzi hewa kama isingebainika kwenye uhakiki huo na kupelekwa fedha, Sh milioni 931.3 zingepelekwa shuleni kuhudumia wanafunzi hewa katika mwaka wa fedha 2016/2017.

Alisema kati ya fedha hizo Sh milioni 527.8 ni kwa shule za msingi na Sh milioni 403.4 ni kwa shule za sekondari.

Aliitaja mikoa inayoongoza kuwa na wanafunzi hewa ni Tabora (12,112), Ruvuma (7,743), Mwanza (7,349), Dar es Salaam (4,096), Kagera (4,763), Rukwa (4,054), Singida (3,239), Kilimanjaro (2,594), Kigoma (2,323), Njombe (2,307), Simiyu (2,081) na Arusha (1,923).

Mikoa mingine ni Mara (1,855), Tanga (1,378), Geita (1,281), Morogoro (1,172), Mtwara (882), Mbeya (786), Shinyanga (695), Songwe (512), Manyara (330), Dodoma (284), Lindi (281), Pwani (187), Iringa (161) na Katavi (0).

Waziri huyo alisema wanafunzi hewa walianza wakati serikali ilipoanza kupeleka fedha shuleni kama ruzuku.

Alisema Sh bilioni 27 zimekuwa zikipelekwa kila mwezi kama ruzuku ya uendeshaji shule za msingi na sekondari na posho ya madaraka kwa ajili ya wakuu wa shule na walimu wakuu, lakini baadhi ya walimu waliamua kuongeza idadi ya wanafunzi ili wapate fedha zaidi.

“Huu ujinga unaweza kufanywa hata katika ngazi ya wizara ni jambo la uchunguzi, zile fedha hazipiti Tamisemi zinakwenda moja kwa moja shuleni,” alieleza na kuongeza kuwa hatua za kinidhamu zinaendelea kuchukuliwa kwa wale wote waliosababisha uwepo wa wanafunzi hewa na Tamisemi inaendelea kuhakiki takwimu zilizowasilishwa.

“Serikali haitegemei tena kuwepo suala la wanafunzi hewa. Naagiza makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa na wakuu wa shule kuhakikisha suala la wanafunzi hewa halijitokezi tena katika shule zote za msingi na sekondari,” alibainisha Simbachawene.

Thursday, November 10, 2016

Joseph Mungai Kuwagwa Leo Dar..........Mwili wa Samwel Sitta Kuwasili Leo


Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Elimu, Joseph Mungai unatarajiwa kuagwa   Dar es Salaam leo katika viwanja vya Karimjee.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, mtoto wa marehemu, William Mungai alisema ibada ya kuuaga mwili huo itafanyika katika viwanja hivyo saa 5.00 asubuhi.

Hata hivyo mtoto huyo wa marehemu hakutaka kuingia kwa undani kuhusu chanzo cha kifo cha baba yake, badala yake alisema familia iachwe iendelee kushauriana na daktari.

Alisema pamoja na hayo, kifo hicho kimewashtua kwa vile  kimetokea ghafla na kwamba baada ya kuisha kwa ibada ya kuaga mwili huo, utasafirishwa hadi Mafinga, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa kwa mazishi.

“Hadi sasa familia tunajua kwamba marehemu aliugua tumbo la kawaida na tulimpeleka hospitalini ambako alifariki dunia, tunaomba familia iachwe, kwa sababu  bado tunashauriana na daktari wake.

“Tumekubaliana mwili wake uagwe kesho (leo) saa tano Viwanja vya Karimjee ambako pia historia yake yote na familia itasomwa,” alisema William.

Kifo cha Mungai kilitokea juzi jioni katika kile kilichoelezwa kuwa   alianza kujisikia vibaya baada ya kunywa kiywaji katika   hoteli moja iliyopo Msasani, ambayo aliizoea.

Mmoja wa waombelezaji waliofika nyumbani kwa marehemu jana ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)- Zanzibar, Salum Mwalimu ambaye alimwelezea Mungai kuwa aliunga mkono  mabadiliko ya siasa.

“Hakuwa na kadi ya Chadema lakini alipenda mabadiliko, mwanaye William aligombea ubunge wa Mafinga kupitia  Chadema na baba yake alimuunga mkono,” alisema.

Mbunge wa zamani wa Kwela, Chrisant Mzindakaya alisema amesikitishwa na kifo hicho ikizingatiwa wiki iliyopita walikuwa pamoja na walizungumza mambo mengi ya siasa.

“Hakuwa na kesho katika maisha yake, alilokuwa na uwezo wa kulifanya alilifanya siku hiyo hiyo, alikuwa na msimamo, hakukubali kuyumbishwa,” alisema Mzindakaya.

Wakati huohuo, mwili wa aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta unatarajiwa kuwasili leo ukitokea  Ujerumani ambako alikuwa akitibiwa hadi mauti yalipomfika.

Taarifa zilizotolewa na msemaji wa familia ya marehemu, Gerald Mongella, zinasema  mwili huo utawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 9.00 mchana na kupelekwa nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam.

“Ijumaa(kesho) saa tatu asubuhi ibada ya kuuaga mwili huo itafanyika katika viwanja vya Karimjee ambako ndugu na wakazi wa   Dar es Salaam watapata fursa ya kuaga,” alisema Mongella.

Mwili wa Sitta utasafirishwa hadi Dodoma ambako utaagwa na wabunge na baadaye utasafirishwa kwenda Urambo kwa mazishi   Jumamosi.

Sitta alifariki Novemba 07 mwaka huu katika Hospitali ya Technal University alipokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya saratani ya tezi dume.
 

Thursday, November 10, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi ya Novemba 10



Thursday, November 10, 2016

Ushindi wa Trump Waacha Kilio Bungeni Dodoma



Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson amesema wabunge wanawake wamesikitishwa na kushindwa kwa mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Chama cha Democrat, Hillary Clinton.

Dk. Tulia alitoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma jana, baada ya kutambulisha wageni mbalimbali.

Alisema walitarajia mambo yangekuwa mazuri upande wao  akiwa mama (wanawake), lakini haikuwezekana.

“Safari hii haikuwezekana, asikate tamaa maana baada ya miaka minne mambo yanaweza kuwa mazuri zaidi kuliko ilivyokuwa sasa. Nampa pole mama Clinton kwa kuwa safari hii haikuwezakana,” alisema Dk Tulia huku akishangiliwa na wabunge wanawake na kuongeza:

“Nasikia kuna watu hapa wanasema tungempeleka mheshimiwa fulani… katika maeneo yale mama Clinton angeshinda,” alisema.

Kutokana na kile kilichoonekana kupigwa butwaa na uchaguzi huo, kabla ya kuuliza swali la nyongeza jana asubuhi, Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema), alisema ana masikitiko makubwa kwa sababu Hillary Clinton ameshindwa uchaguzi.

“Kwa niaba ya wanawake wenzangu, nampa pole mama Clinton kwa kushindwa uchaguzi, tumeumia sana na tumerudi nyuma,” alisema.

Kauli hiyo ilimfanya Dk. Tulia kumtaka aeleze amepata wapi taarifa wakati bado wabunge wanawake wana faraja  Hillary angeweza kushinda.

Hata hivyo, akijibu swali la Suzan, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Khamis Kigwangala,  alimpa pole Hillary kwa kushindwa kwenye uchaguzi huo.
Reviewed by RICH VOICE on Novemba 10, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...