Wednesday, November 9, 2016
Treni Yanusurika Kuchomwa Moto na Wananchi....Vioo 30 vya Mabehewa Vyapasuliwa, 17 Watiwa Mbaroni
TRENI ya abiria inayofanya safari zake kati ya Kituo Kikuu cha Reli na maeneo ya Pugu Dar es Salaam maarufu kama ‘Treni ya Mwakyembe’ nusura ichomwe moto juzi, baada ya wananchi kudai kuchoshwa na usumbufu wa shirika hilo.
Wananchi hao walitaka warudishiwe nauli zao kwa kile walichodai Shirika la Reli Tanzania (TRL) limeshindwa kuwa na ratiba inayoeleweka.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 3:00 usiku eneo la Majumbasita, baada ya treni hiyo kukaa kituoni hapo kwa muda mrefu bila kuambiwa kuambiwa chochote.
Hali hiyo iliwafanya abiria kuvamia kituo kidogo cha mawasiliano kilichopo eneo hilo wakitaka warejeshewe nauli zao vinginevyo wangekichoma moto pamoja na mabehewa ya treni hiyo.
Mwandishi aliwashuhudia abiria wakitaka kuingia ndani ya kituo hicho huku wakiwalazimisha wafanyakazi waliokuwapo wawarudishie fedha zao za nauli.
Purukushani hiyo iliyodumu kwa takribani saa mbili ilimalizika kwa abiria hao kuvunja vioo vya mabahewa ya treni vipatavyo 30.
Wafanyakazi kuona hivyo walijifungia ndani ya kituo hicho huku polisi waliokuwa wakisindikiza treni hiyo wakitimua mbio kunusuru maisha yao.
Baadhi ya abiria walisema tangu Ijumaa iliyopita wamekuwa wakipata usumbufu kwa kukatishiwa tiketi huku treni ikichelewa na wakati mwingine kutoonekana kabisa.
Walisema jambo hilo limekuwa likiwasababishia hasara na kuwalazimu kutafuta usafiri mwingine na kuchelewa kufika kwenye majukumu yao.
Kufuatia
kukithiri vitendo vya uharibifu wa miundombinu ya reli na treni
vinavyofanywa na baadhi ya wananchi, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL)
kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji , Masanja Kadogosa imetoa onyo kwa wananchi kutofanya vitendo hivyo.
“Tukio
hili si mara ya kwanza kujitokeza, lilijitokeza tarehe 24, 26 na 28
mwezi wa 10 na Novemba 7 Katika matukio hayo kulitokea uharibifu wa
miundombonu na kujeruhi baadhi ya wafanyakazi wa TRL akiwemo Mustapha
Omary ambaye ameshonwa nyuzi 8 katika hospitali ya mnazi mmoja,” amesema.
Amesema
kutokana na uharibifu huo, watuhumiwa 17 wanashikiliwa na jeshi la
polisi na kwamba upepelezi ukikamilika watachukuliwa hatua za kisheria.
Kadogosa
amedai kuwa, wahusika wa fujo na uharibifu huo ni makondakta wa dalala
kwa lengo la kutisha wananchi kutoutumia usafiri wa treni.
“Kuna
watu wa daladala wanafikiri wataendelea kufanya fujo ili wananchi waone
kuwa usafiri wa treni si salama wapande magari yao, sisi hatulazimishi
wananchi kuutumia usafiri wetu ila kutokana na ubora wa huduma zetu
wanakuja wenyewe. Pia hatusitishi kutoa huduma kwa sababu ya fujo zao
sababu tutawatesa abiria wetu zaidi ya 21,000,”
Naibu
Kamishna wa Polisi na Kamanda wa Reli, Simon Chillery amesema jeshi la
polisi linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini wengine waliohusika.
Wednesday, November 9, 2016
Rais Barack Obama ampongeza Rais Mteule, Donald Trump na kumualika Ikulu kujadiliana juu makabidhiano ya ofisi.
Rais Barack Obama wa Marekani amempongeza Rais Mteule wa taifa hilo, Donald Trump na kumualika Ikulu kujadiliana juu makabidhiano ya ofisi.
Wednesday, November 9, 2016
Msajili wa vyama vya siasa Tanzania, avifutia usajili Vyama Vitatu
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania Jaji Francis Mutungi ametangaza kuvifutia usajili vyama vitatu baada ya kubainika kukiuka sheria ya usajili wa vyama.
Vyama hivyo ni pamoja na CHAUSTA kilichopata usajili wa kudumu tarehe 5 Novemba 2001, The African Progressive Party of Tanzania ( APPT-Maendeleo) kilichopata usajili wa kudumu terehe 4 Machi 2003 na Chama cha Jahazi Asilia kilichopata usajili wa kudumu tarehe 17 Novemba 2004.
Jaji Mutungi amesema kuwa mchakato wa kufuta usajili wa vyama hivyo umetokana na zoezi la uhakiki wa utekelezaji wa masharti ya usajili na matakwa mengine ya sheria ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu lililofanyika kuanzia tarehe 26 Juni hadi 26 Julai 2016.
Amesema katika zoezi hilo uhakiki ulibaini kuwa vyama hivyo vimepoteza sifa za usajili wa kudumu kwa kukiuka masharti ya sheria ya vyama vya siasa, na kwamba kila chama kilipewa ya nia ya msajili kufuta usajili wake, lakini vikashindwa kutoa utetezi wa kuridhisha ili visifutiwe usajili.
Kufuatia uamuzi huo, Msajili amewataka waliokuwa wanachama wote wa vyama hivyo kutojiuhusisha na shughuli yoyote kwa majina ya vyama hivyo, na kwamba kufanya hivyo ni kuvunja sheria, huku akiviasa vyama vingine kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria.
Wednesday, November 9, 2016
Breaking News: Donald Trump Ndo Mshindi wa Kiti cha Urais wa Marekani
Mgombea wa Chama cha Republican, Donald Trump ameshinda uchaguzi mkuu wa Marekani baada ya kufikisha kura 276 huku Hillary Clinton akiwa na kura 218.
Hillary Clinton amempigia simu Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump na kumpongeza kufuatia ushindia huo alioupata.
Akizungumza
na wafuasi wake baada ya kutangazwa mshindi, Trump amewataka raia wote
wa Marekani, waliomchagua na ambao hawakumchagua kuungana na kuanza
kuijenga nchi yao kwani muda wa kampeni na siasa za kugawanyika
umekwisha.
Wednesday, November 9, 2016
Rais Magufuli Ampongeza Donald Trump Kwa Kushinda Kiti cha Urais Wa Marekani
Leo November 9, 2016 Marekani imeweka historia nyingine baada Donald Trump wa chama cha Republican kutangazwa mshindi wa kiti cha Urais, na tayari ameanza kupokea pongezi kutoka kwa viongozi wa nchi mbalimbali ikiwemo Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli.
Rais Magufuli ametoa pongezi zake kwa Rais Donald Trump kupitia ukurasa wake Twitter
Wednesday, November 9, 2016
Ratiba ya Mazishi ya Spika Mstaafu, Samwel John Sitta
Mwili wa aliyekuwa spika wa bunge, Samuel Sitta unatarajia kuwasili nchini siku ya Alhamis ukitokea nchini Ujerumani ambapo alipokuwa akipatiwa matibabu.
Taarifa hiyo imetolewa na Gerald Mongela ambaye ni msemaji wa familia.
Amesema mara baada ya mwili huo kuwasili nchini utapelekwa nyumbani kwa marehemu Masaki jijini Dar es Salaam na siku ya Ijumaa shughuli za kuaga zitafanyika katika viwanja vya Karimjee kisha kupelekwa bungeni mjini Dodoma.
“Mwili wa mpendwa wetu mheshimiwa Samuel Sitta utawasili na ndege ya Emirates siku ya Alhamis saa tisa na nusu alasiri na baada ya hapo mwili tutauleta hapa nyumbani kwaajili ya kukaa nao na kupumzika kusubiri ratiba ya Ijumaa,”alisema Mongela.
Mazishi ya Marehemu Samwel John Sitta yatafanyika siku ya Jumamosi Urambo mkoani Tabora.
Wednesday, November 9, 2016
Serikali: Ukosefu wa ajira kwa vijana umepungua
Serikali ya Tanzania imesema kwamba kulingana na takwimu inaonesha kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana nchini Tanzania umepungua kwa asilimia mbili, kutoka asilimia 13.7 mwaka 2012 mpaka asilimia 11.7 mwaka huu.
Akizungumza jana bungeni, mjini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali na majibu Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu Mhe. Anthony Mavunde, alisema licha ya kupungua huko kwa ukosefu wa ajira, serikali imeweka mipango ya kuwawezesha vijana kuwa na wigo mpana wa ajira nchini.
Mhe. Mavunde alisema kuwa kwa takwimu hizo Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kutoa ajira kwa vijana wengi zaidi kushinda baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya na Uganda.
Wednesday, November 9, 2016
TRA Yakusanya Shilingi Trilioni 1.15 Mwezi Oktoba
Na Ally Daud-MAELEZO.
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikia kukusanya shilingi trilioni 1.15 kwa mwezi Oktoba ikiwa ni kukamilisha malengo waliyojiwekea katika ukusanyaji wa mapato.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi Bw. Richard Kayombo wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu hali ya makusanyo na zoezi la uhakiki wa namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN)linaloendelea hivi sasa.
“Tumefanikiwa kukusanya shilingi Trilioni 1.15 kwa mwezi Oktoba mwaka huu ikiwa ni kufanikisha malengo ya ukusanyaji kodi nchini ili kukuza uchumi wa nchi pamoja kusaidia Serikali kuendeleza huduma za jamii nchini” alisema Bw. Kayombo.
Aidha Bw. Kayombo amesema kuwa mapato hayo yametokana na mikakati thabiti iliyowekwa na mamlaka hiyo katika ukusanyaji kodi hapa nchini ili kuweza kusaidia ongezeko la pato la Taifa .
Katika hatua nyingine TRA imefanikiwa kushinda kesi 9 kati ya 10 zilizokuwa zikiendelea katika mahakama mbalimbali nchini dhidi ya walipa kodi wake na kufanikiwa kupata kiasi cha takribani Bilioni 16.9 .
“Tumefanikiwa kushinda kesi 9 kati ya 10 ambazo zilifikishwa mahakamani dhidi ya walipa kodi na kupata kiasi cha shilingi bilioni 16.9 hivyo kufanya juhudi zetu za kukusanya mapato mengi zaidi” aliongeza Bw. Kayombo.
Mbali na hayo Bw. Kayombo amesema kuwa zoezi la uhakiki wa namba za utambulisho wa mlipa kodi ambalo limeanza hivi karibuni linaendelea na litafikia tamati Novemba 30 mwaka huu kwa mkoa Dar es salaam hivyo wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya uhakiki huo.
Aidha Bw. Kayombo ameongeza kuwa kila mwenye namba ya utambulisho wa mlipa kodi anatakiwa akahakiki kwa ajili ya kupata taarifa sahihi za mlipa kodi ili kuepuka kufutwa kwa namba yake ya utambulisho baada ya zoezi hilo kumalizika kwa mkoa husika.
HABARI ZA KIMATAIFAA
Habari | 09.11.2016 | 16:16
Obama amwalika Trump ikulu ya White House
Reviewed by RICH VOICE
on
Novemba 09, 2016
Rating:
Hakuna maoni