Monday, November 14, 2016
Wadaiwa Sugu Bodi ya Mikopo wapewa siku 30
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa
bodi hiyo Abdul-Razaq Badru amesema kuwa hadi sasa kuna jumla ya
wadaiwa sugu 142,470 wenye mikopo ya shilingi 239,353,750,170.27
iliyokwishaiva hawajajitokeza wala kuanza kulipa mikopo yao.
Akitolea
ufafanuzi wa maana ya neo "Wadaiwa Sugu", Badru amesema kuwa ni
wanufaika waliokopeshwa, muda wa matarajio ukapita bila kuwasilisha
taarifa zao na kulipa madeni ya mikopo waliyokopeshwa tangu mwaka wa
masomo 1994/1995.
Kuhusu
hatua zinazochukuliwa na bodi hiyo, Badru amesema mbali na kutoa siku
30, bodi hiyo inakamilisha taratibu za kuwafikisha mahakamani kwa
kuvunja sheria ya bodi ya mikopo kifungu cha 19A(1).
Hatua
nyingine ni pamoja na kuyawasilisha majina hayo katika taasisi za
mikopo, kuwasiliana na wadhamini wao pamoja na kuyatangaza hadharani
majina ya wadaiwa sugu wote ili waajiri, wadhamini na wadau wengine
wayajue na kutoa taarifa katika bodi hiyo.
Kuhusu
takwimu za mikopo iliyotolewa, amesema tangu 1994/95 hadi 2015/16 jumla
ya shilingi 2,595,932,575.56 zimekopeshwa kwa jumla ya wanufaika
379,179.
Amesema
kati ya mikopo yote iliyokopeshwa, mikopo iliyoiva ni shilingi
1,425,708,285,046.48 kwa wanufaika 238,430 ambao tayari wamemaliza
kipindi chao cha matazamio.
Badru
amesema kuwa jumla ya wanufaika wa mikopo 93,500 wamebainika na
kupelekewa ankara za madeni yao, ambapo kati yao wanufaika 81,055
wanaendelea kulipa.
Monday, November 14, 2016
ACT-Wazalendo walaani kauli ya Serikali kutowajengea wananchi......Wadai kauli hiyo ni fedheha kwa waathirika na Wadau.
Watanzania
wanakumbuka kuwa mnamo tarehe 10 Septemba, 2016 lilitokea tetemeko la
ardhi katika eneo la Kanda ya Ziwa na hususan Mkoa wa Kagera.
Tetemeko
hilo lilisababisha athari mbalimbali zikiwemo vifo, majeruhi, uharibifu
wa makazi na miundombinu ya umma na watu binafsi. Jumla ya Watu 117,721
wameathirika kwa kupoteza makazi yao, mali na athari za kisaikolojia
katika Wilaya za Bukoba, Missenyi, Muleba, Karagwe na Kyerwa.
Aidha,
jumla ya watu 17 walipoteza maisha na 560 walijeruhiwa. Vilevile,
nyumba 2,072 za makazi zilianguka kabisa na nyumba 14,595 za makazi
zilibomoka, baadhi zina kuta au kupata nyufa kubwa na hivyo kuzifanya
kuwa hatarishi kwa makazi ya binadamu. Vilevile, maafa haya
yalisababisha uharibifu mbalimbali wa miundombinu ya barabara na majengo
ya watu na taasisi mbalimbali, ikiwemo shule na Hospitali.
Kufuatia
maafa hayo, wananchi na taasisi mbalimbali, pamoja na nchi marafiki,
waliitikia wito wa kuwasaidia wahanga wa maafa na kukarabati miundo
mbinu iliyoharibika. Hadi kufikia mwezi Oktoba, Fedha, Vyakula na Vifaa
mbalimbali vya Ujenzi vilikuwa vimepatikana kwa njia ya michango
mbalimbali.
Chama
chetu kimeshtushwa na kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwamba Wananchi
walioathirika wajitegemee wenyewe na kwamba misaada yote iliyotolewa Ni
ya Serikali na Taasisi zake tu. Kauli hii ya Mkuu wa Mkoa haikubaliki
kwani inadhalilisha waathirika na watu wote waliojitoa kuwasaidia
waathirika hao.
Tunachukulia
kauli hii kama tangazo la wizi wa uaminifu wa wananchi waliochanga. Ni
busara ya kawaida kuwa hatua ya kwanza katika kushughulikia maafa ni
kurudisha hali ya maisha ya watu katika hali ya kawaida sambamba na
ukarabati wa miundombinu. Aidha, suala la ujenzi wa miundo mbinu ya
taasisi za umma ni jukumu la msingi la serikali. Kwa sababu hii:
•
ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuu kujitenga na kufuta kauli ya mkuu
wa mkoa wa Kagera kwa sababu inaigombanisha serikali na wananchi
inaowaongoza.
•
ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuelekeza ni misaada iliyopatikana kwa
michango ya wananchi, taasisi na nchi rafiki katika kusaidia wananchi
walioathirika kurudi katika maisha ya kawaida, ikiwemo ukarabati na
ujenzi wa nyumba za kuishi.
•
ACT Wazalendo tunatoa wito kwa taasisi za kiraia nchini kuchukua nafasi
yake katika kuendelea kuikumbusha serikali wajibu wake wa msingi wa
kuboresha maisha ya watu.
Janeth Rithe
Katibu wa Taifa ACT Wazalendo, Kamati ya Maendeleo ya Jamii
13/11/2016, Dar Es salaam.
Monday, November 14, 2016
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS ) amtaka Rais Shein asisaini muswada wa mafuta na gesi
Rais
wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS ), Omar Said Shaaban amemshauri
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein asiusaini Muswada wa sheria ya
mafuta na gesi uliopitishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi hivi
karibuni kwa madai kuwa unavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Omari
ameeleza msimamo huo katika barua yake ya maneno 1,293 aliyomwandikia
Dk Shein akifafanua jinsi gani muswada huo unavunja sheria na Rais huyo
anavyoingizwa kwenye mtego wa kuvunja Katiba.
Katika barua hiyo, mwanasheria hiyo anasema, “Mheshimiwa
Rais, zipo taarifa kuwa unajiandaa kuweka saini kwenye muswada huo
uliopitishwa na Baraza la Wawakilishi ili hatimaye iwe sheria. Naomba
nikunasihi uachane na mpango huo ili kujiepusha na mtego wa jaribio la
kuvunja Katiba.”
Anasisitiza,
“Kwa heshima naomba nikueleze kuwa jaribio la Serikali yako na Baraza
la Wawakilishi la Zanzibar na hatua yako ya kuweka saini muswada huo ili
uwe sheria, ni uvunjaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambayo wewe umeapa kuilinda, lakini pia ni kinyume na maelekezo
ya sheria inayorejewa kama ndiyo chanzo cha mamlaka ya Zanzibar kutunga
sheria yake.”
Mwanasheria
huyo anabainisha kuwa kama kweli nia ya dhati ipo ya kuondoa mafuta na
gesi kwenye Muungano, hatua pekee na salama kwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ni kusukuma kumalizika kwa mchakato wa Katiba Mpya au
kupelekwa mabadiliko ya Katiba Bungeni kuliondoa jambo hilo kwenye
Nyongeza ya Kwanza ya Katiba.
Omari
alisema akiwa mwanasheria tena kiongozi kwenye kada hiyo, ana wajibu wa
kikatiba, kimamlaka na kitaaluma kusimamia ulindwaji na usimamizi wa
Katiba na sheria za nchi na akiwa mwenye uchungu na Zanzibar, anapenda
kuona ikisimamia rasilimali zake yenyewe bila ya kukiuka masharti ya
Katiba.
Alibainisha
kuwa katika Katiba ya Muungano kwenye nyongeza ya kwanza, suala la
mafuta na gesi ni jambo la Muungano hivyo usimamizi wake na utungiwaji
sheria kwa mujibu wa Katiba zote mbili upo chini ya Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
“Hakuna
mahali duniani kote ambapo suala lenye misingi yake kikatiba
linaondolewa kwa “makubaliano ya viongozi wa wakuu wa Serikali,” anasema.
Monday, November 14, 2016
Donald Trump Akataa Kulipwa Mshahara wa Urais
Rais mteule wa Marekani, bilionea Donald Trump amesema hatakubali kupokea mshahara wa urais pindi atakapokuwa madarakani.
Trump
ameweka msimamo huo jana katika mahojiano maalum na mtangazaji maarufu,
Lesley Stahl katika kipindi cha 60 Minutes, aliyetaka kufahamu kuhusu
uamuzi wake juu ya mshahara wake akiwa ni mfanyabiashara mkubwa.
“Sijawahi
kuzungumzia hili, lakini jibu langu ni hapana,” alisema. “Nafikiri
inanibidi kupokea kwa mujibu wa sheria $1, kwahiyo ntachukua $1 (Sawa na
shilingi 2,200 za Tanzania) kwa mwaka. Lakini hata sijui ni nini,”
aliongeza.
Ingawa
mtangazaji huyo alimkumbusha Trump kuwa anaiacha $400,000 kwa mwaka,
rais huyo mteule alisisitiza, “sitachukua mshahara. Sitapokea.”
Wakati
wa kampeni, Trump aliahidi kuwa atajiweka kando na biashara zake endapo
atachaguliwa kuwa Rais wa Marekani, na kwamba atajikita zaidi katika
kutimiza ahadi zake kwa Wamarekani. Alisema kuwa biashara zake ataziacha
mikononi mwa watoto wake.
Monday, November 14, 2016
Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatatu ya Novemba 14
Monday, November 14, 2016
Vyoo 100 kujengwa barabara ya Mwanza Kwenda Dar Es Salaam
Taasisi
ya The Desk & Chair Foundation (TD& CF), inatarajia kujenga
vyoo 100 katika Barabara Kuu ya Mwanza-Shinyanga-Dar es Salaam
unaokadiriwa kutumia Sh. milioni 500.
Mwenyekiti
wa TD & CF, Alhaji Sibtain Meghjee alisema hivi karibuni mjini
Mwanza kwamba mradi huo ni sehemu ya miradi mitatu mikubwa ambayo
taasisi yake inatekeleza nchini.
Alisema
baada ya kukamilisha mradi mkubwa wa jengo la kupumzikia wananchi
wanaokwenda kutibiwa na kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure wanatarajia kujenga
vyoo 100 kwenye barabara ya kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam kwa basi.
Meghjee
alieleza kuwa maandalizi ya awali ya mradi huo yameshaanza na kwamba
watashirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu
(SUMATRA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ili kupata taarifa
sahihi kabla ya mradi kuanza.
“Penye
nia pana njia, baada ya kukamilisha ndoto yetu, leo ya mradi huu mkubwa
wa ujenzi wa jengo la kupumzikia hapa Sekou Toure, tunatarajiwa
kutekeleza miradi mitatu mikubwa ukiwemo wa vyoo kwa ajili ya abiria
wanaosafiri kati ya Mwanza na Dar es Salaam:
“Tunataka
msamiati wa kuchimba dawa wakati wa safari ubaki kuwa historia kwa hiyo
tunatarajia kufanya jaribio moja la kujenga matundu 100 ya vyoo katika
njia na barabara kuu ya Mwanza hadi Dar es salaam ambavyo vitagharimu
shilingi milioni 500.Tutashirikiana na mamlaka husika, ofisi yako na
idara ya afya,”alisema Meghjee.
Meghjee
alieleza kuwa taasisi hiyo pia ina mpango wa kutekeleza mradi wa
kutengeneza viungo bandia kwa kushirikiana na kitengo cha Jairpur
Foot/Knee and Limb Project cha India ambao unahitaji Dola 200,000 za
Marekani (sh. milioni 44), zitakazowezesha kuanzisha huduma ya viungo
hivyo bandia vya miguu, mikono, fimbo na baiskeli.
Alisema
wanaendelea kuwasiliana na wafadhili watakaoshirikiana nao kwenye mradi
huo na kuwahakikishia walengwa kuwa viungo hivyo vitapatikana kwa
gharama nafuu mara utakapokamilika mradi huo.
Meghjee
aliongeza kuwa wakati wakiendesha ujenzi wa jengo la mapumziko katika
Hospitali ya Sekou Toure,walipata wazo la kujenga mabanda yatakayotumiwa
na madereva wa pikipiki (boda boda) kuegesha vyombo vyao kivulini na
kupata huduma ya vyoo na mabafu.
Mwenyekiti
huyo wa TD & CF aliongeza zaidi kuwa endapo Halmashauri ya Jiji
itaridhia na kuwapa eneo maalumu na mahususi la ujenzi wa huduma hiyo
watafanya jaribio hilo moja ili kuweza kuona matunda yake.
Monday, November 14, 2016
Kesi ya Akina Zombe: Mrakibu wa Polisi (SP) Bageni Apinga Hukumu ya Kunyongwa Hadi Kufa
Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni, Mrakibu wa Polisi (SP),Christopher Bageni amewasilisha maombi Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kupinga adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
SP
Bageni alihukumiwa adhabu hiyo baada ya mahakama hiyo kujiridhisha
kwamba aliwaua kwa kukusudia wafanyabiashara wanne wa madini kutoka
Mahenge mkoani Morogoro na dereva teksi mkazi wa Manzese, Dar es
Salaam, katika Msitu wa Pande.
Bageni
kupitia Wakili wake, Gaudioz Ishengoma, aliwasilisha maombi hayo
mwishoni mwa wiki yaliyoambatana na hati ya kiapo iliyoapwa na wakili
huyo.
Muwasilisha
maombi anaomba mahakama hiyo kuifanyia marejeo hukumu dhidi yake
iliyotolewa Septemba 13 na kusomwa Septemba 16 mwaka huu na Msajili wa
Mahakama hiyo, John Kahyoza.
Akitoa
sababu kuomba marejeo, anadai alinyimwa haki sawa ya kusikilizwa
wakati wa kutathmini ushahidi ulioko kwenye kumbukumbu za mahakama kwa
kuegemea kwenye ushahidi wa upande wa mashtaka.
Alidai
katika kuchanganua ushahidi ambao uamuzi wa mahakama uliegemea,
mahakama ilishughulika na ushahidi wa msingi (Exam in Chief) wa upande
wa mashtaka na iliangalia kwa juu juu tu ushahidi wa utetezi hususan wa
Bageni au haikuutazama kabisa.
“Kuna
kukinzana kwa haki kwa maana ya kwamba mtoa maombi alinyimwa haki sawa
ya kusikilizwa, kwa mahakama kuchagua na kuegemea upande wa mashtaka
pekee na kushindwa kuzingatia ushahidi wa upande wa utetezi, hasa wa
mtoa maombi.
“Uamuzi
wa mahakama umetolewa katika msingi wa makosa ya dhahiri kwenye
kumbukumbu za mahakama, hivyo kusababisha upotoshaji wa haki, kushindwa
kuzingatia mwongozo wa kanuni katika asili, thamani na matumizi ya
ushahidi wa kuungwa mkono,” ilisema sehemu ya maombi hayo.
Alidai
kuwa kwa kushindwa kuchanganua na kutathmini ushahidi kwa umakini
kwenye kumbukumbu, mahakama ilishindwa kuainisha ushahidi wa mjibu rufaa
wa nne (Bageni) kimazingira kama ilivyo ni dhahiri unakosa thamani ya
kuhitaji ushahidi wa kuunga mkono na hivyo si salama kuegemea katika
kumtia hatiani.
“Kwa
kushindwa kuona na kuzingatia ushahidi uliokusudiwa kuwa na ushahidi wa
kuunga mkono, siyo ushahidi huru na hauna mashiko kuthibitishwa (PW27)
na haupo (PW36).
“Kwa
kushindwa kufanya uchambuzi wa ushahidi kwenye kumbukumbu kwa umakini
wenye manufaa, vinginevyo mahakama ilipaswa kuona wajibu wa kuthibitisha
shtaka kwenye jinai haukufikiwa,”anasema Wakili Ishengoma.
Anadai
mahakama katika kuamua, kama ilivyofanya katika uhalisia wake, kuhusu
ushiriki wa mtoa maombi katika eneo la tukio la uhalifu, ilishindwa
kubaini katika ujumla wake ushahidi wa upande wa mashtaka ambao
haukuweza kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.
Ishengoma
alidai mahakama haikuuchukulia ushahidi kwenye kumbukumbu katika ujumla
wake hivyo kutengua uamuzi wa kuachiwa huru kwa mtoa maombi na kumtia
hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa kusimamia ushahidi ambao haupo
na uvumi pamoja na ushahidi wa mashaka makubwa.
Alidai
kutokana na hukumu ya mahakama, haikuwa bayana ni kwa ushahidi wa nani
ulithibisha mtoa maombi Bageni alimwezesha au kumsaidia nani katika
mauaji ya marehemu hao.
Katika
hati ya kiapo iliyoapwa na Wakili Ishengoma, Bageni anadai yeye na
wengine wanane ambao hawako katika maombi hayo walishtakiwa Mahakama Kuu
Kanda ya Dar es Salaam kwa makosa ya mauaji ya watu wanne katika Kesi
ya jinai namba 26 ya mwaka 2006.
Bageni
alikuwa mshtakiwa wa pili na katika hukumu iliyotolewa na Jaji Salum
Massati, amnayo wote waliachiwa huru, lakini Mkurugenzi wa Mashtaka
(DPP) hakuridhishwa na uamuzi huo hivyo alikata rufaa namba 358 ya mwaka
2013.
Kabla
ya usikilizwaji wa rufaa hiyo, DPP aliwaondolea rufaa wajibu rufaa
watano na kubaki wajibu rufani wanne ambao waliachiwa huru pia Septemba
16, mwaka huu.
Walioachiwa
huru ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO)
Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe na maofisa wengine wawili
baada ya mahakama kuona hakuna ushahidi wa wazi ama mazingira kuwatia
hatiani.
Katika
kesi ya msingi, Bageni alidaiwa kuwaua kwa kukusudia wafanyabiashara
Sabinus Chigumbi, maarufu Jongo na ndugu yake, Ephrahim Chigumbi,
Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, aliyekuwa dereva wa teksi wa Manzese ,
Januari 14, mwaka 2006, katika Msitu wa Pande, Mbezi Luis, Dar es
Salaam.
Monday, November 14, 2016
Kidato cha Pili Waanza Mitihani leo
Wanafunzi
wa kidato cha pili nchini wameanza kufanya mitihani yao ya upimaji leo
katika shule za sekondari 4,669 zilizopo Tanzania Bara.
Jumla ya wanafunzi 435,221 wamesajiliwa kufanya mitihani hiyo wakiwamo 67 wasioona na 306 wenye uoni hafifu.
Mbali
na mitihani hiyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa
(Necta), Dk Charles Msonde amesema mtihani wa Taifa wa darasa la nne
utafanyika Novemba 23 na 24, mwaka huu.
"Mitihani
hii inafanyika katikati ya mafunzo ili kubaini changamoto zilizopo na
kutafuta namna ya kuboresha mafunzo hayo," amesema Dk
Msonde.
Wakati
huo huo, Dk Msonde amefafanua kuwa mafunzo ya ualimu wa shule ya msingi
ngazi ya stashahada yamefutwa lakini wanafunzi waliopo vyuoni
watamalizia masomo yao kwa muda uliobaki.
Dk Msonde amesema mafunzo hayo ya walimu yataendelea kwa utaratibu wa zamani ambao ulikuwa ngazi ya cheti.
Amesema usimamizi wa mitihani hiyo itakuwa chini ya Necta kama ilivyokuwa zamani badala ya Nacte.
Reviewed by RICH VOICE
on
Novemba 14, 2016
Rating:
Hakuna maoni