HABARI ZA JUMAMOSI NZURI YA LEO 07/01/2017
Saturday, January 7, 2017
Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumamosi Ya January 7
Magari yenye taa za mwanga mkali yapigwa marufuku
POLISI
Kikosi cha Usalama Barabarani kimesema kitaanza kukamata magari yote
ambayo yamewekwa taa zenye mwanga mkali (spotlights) kwa kuwa uwekaji wa
taa hizo, ni kinyume na sheria ya usalama barabarani.
Uwekaji
wa taa hizo zenye mwanga mkali, umezuka kwa kasi katika maeneo
mbalimbali nchini, jambo ambalo limetajwa linaweza kusababisha ajali kwa
dereva atakayemulikwa na taa hizo.
Kauli
hiyo imetolewa na Kamanda wa Kikosi hicho, Naibu Kamisha Mohammed
Mpinga ofisi kwake jijini Dar es Salaam, ambapo alisema ukamataji wa
magari hayo utaanza rasmi wiki ijayo.
Mpinga
alisema wameshatoa maelekezo kwa askari wa usalama barabarani,
kuhakikisha wanakamata magari, pikipiki na malori makubwa ambayo
yamewekwa taa hizo.
“Ziko
taa za aina fulani zinazowekwa kwenye magari na hata ukitembea usiku
utaona mwingine ameweka taa moja mwingine anaweka nyingi sana, kiasi
ambacho zimeleta matatizo kwa madereva wengine,” alisema Kamanda Mpinga.
Aidha,
alisema kwenye barabara kuu kuna mtindo wa madereva wa magari makubwa,
kuweka taa kubwa ambazo zinawekwa juu na kumulika mwanga mkali, kiasi
ambacho dereva anayemulikwa anapata upofu wa muda na kushindwa kudhibiti
chombo chake.
Kamanda
Mpinga alisema kuwa walishatoa muda wa kutosha kwa wamiliki wote wa
magari, walioweka taa hizo kuziondoa, hivyo kwa sasa wataanza
kuwachukulia hatua wote ambao watakuwa hawajaziondoa.
Alifafanua
kuwa uwekaji wa taa hizo ni kinyume cha Sheria ya Usalama Barabarani
Kifungu cha 39 Sura ya 168, ambacho kinaeleza matumizi ya taa. Mpinga
pia alisema magari yatakayokamatwa ni yale ambayo yameongezewa taa hizo.
Alisema magari ambayo yametoka kiwandani yakiwa na taa hizo, hayatahusika.
“Hapa
nazungumzia taa za kuongeza. Lakini pia kuna magari kwa ajili ya
uwindaji huwa yanawekwa taa, lakini wanachotakiwa kufanya waweke kava,
wakati wote ziwe na kava,” alisema.
Alisema
wamiliki wa magari hayo ya kuwindia, wanatakiwa kuondoa kava hizo
wanapokuwa porini tu na kuongeza kuwa mtindo wa wamiliki wa magari
makubwa kuweka taa nyuma ya magari ambayo inamulika, matokeo yake mtu
anayemfuata anafikiri gari anakuja kumbe inakwenda mbele.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Atembelea Mgodi Wa Makaa Ya Mawe Ya Ngaka.....Anusa Madudu, Aahidi kutuma Gavana, CAG, Msajili wa Hazina kufanya ukaguzi
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa atamtuma mara moja Msajili wa Hazina aende kufanya
uchunguzi wa kina na wa kijinai (forensic investigation) ili
kijiridhisha kama mapato na matumizi ya kampuni ya TANCOAL ni halali.
Ametoa kauli hiyo jana mchana (Ijumaa, Januari 6, 2017) mara baada ya kupokea taarifa na kutembelea mgodi huo ili kuona shughuli za uzalishaji zikoje.
Waziri
Mkuu amesema atamwagiza pia mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali ili apitie mahesabu ya kampuni tangu mwaka 2011 walipoanza
uzalishaji.
“Mbali na CAG, itabidi Gavana wa Benki Kuu naye aangalie utumaji wa fedha uliokuwa ukifanywa kama ulifanyika kwa halali,” alisema.
“Mbali na CAG, itabidi Gavana wa Benki Kuu naye aangalie utumaji wa fedha uliokuwa ukifanywa kama ulifanyika kwa halali,” alisema.
Katika
maswali aliyoyauliza Waziri Mkuu, alitaka kujua ni kwa nini kampuni
hiyo haijalipa gawio kwa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ambao ni
mbia (asilimia 30) na kampuni ya Intra Energy Limited (asilimia 70)
licha ya kuwa imekuwa ikifanya uzalishaji wa makaa ya mawe na
kuyasafirisha kwenye viwanda hapa nchini na nje ya nchi.
“Taarifa
zenu zinaonyesha kuwa mmepata kila mwaka lakini rekodi nilizonazo
zinanionyesha kuwa mwaka 2013 mlipanga kuzalisha tani 50,000 na mkauza
zaidi ya hapo. Mkaguzi wa hesabu anasema kampuni imepata hasara, hii
itawezekanaje?” alisema wakati akimhoji Mkurugenzi Mtendaji wa NDC, Bw. Mlingi Mkucha.
“Desemba
2013 mliuza tani 39,000 kwa wamiliki wa viwanda vya nguo, pia mliuza
tani 2,000 kwa kampuni ya saruji ya Zambia, Novemba 2013 mliingia
makubaliano ya kuuza tani 165,000 kwa kampuni ya saruji ya Kitanzania na
ziliuzwa. Mbona financial statement zenu zinasema mwaka huo nao mlipata
hasara?”
“Mnasema gawio (dividend) hutolewa baada ya mtu kutangaza faida. Mbona mlivuka lengo lakini mkatangaza kuwa kampuni imepata hasara katika mwaka huo wa fedha?”
Waziri
Mkuu alimbana Bw. Mkucha aeleze ni kwa nini akiwa mwanasheria wa NDC
aliruhusu kuwepo kwa mkataba unaotoa mwanya kwa kampuni ya TANCOAL
kulipia gharama za menejimenti kwa wakurugenzi ambao wako Australia
wakati hawahusiki na utendaji wa kila siku wa TANCOAL hapa nchini.
Pia
alihoji ni kwa nini aliyekuwa Mkurugenzi wa NDC, Bw. Gideon Nassari
alikuwa ni mjumbe wa Bodi ya TANCOAL na mjumbe wa Bodi ya Intra Energy
Corporation ya Australia huku akiwa ni Mtendaji Mkuu wa NDC.
“Wewe
ulikuwa mwanasheria wa NDC na ulilijua hilo lakini hukuona taabu ya
kiutendaji katika hilo? Au ulishindwa kusema kwa sababu alikuwa ni bosi
wako?”
Waziri Mkuu amemtaka Bw. Mkucha aupeleke mikataba huo kwa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali ili aupitie upya na hasa kipengele cha kufungua
akaunti za NDC kwa kutumia kanuni za Australia na suala la utaratibu wa
gawio kwa wanahisa ambapo kifungu kilichopo kinaipa Bodi ya TANCOAL
mamlaka ya kuamua kutoa au kutokutoa kwa wanahisa.
“Kipengele
kama hiki kwenye mikataba kinazuia ninyi kupata gawio, na ndiyo maana
hesabu zao kila mwaka zimekuwa zinasoma hasara na ninyi mnaona sawa tu
huku Serikali ikiendelea kukosa mapato yake,” alisema.
Waziri
Mkuu ameutaka uongozi wa kampuni ya TANCOAL uongeze uzalishaji ili
iweze kukidhi mahitaji ya ndani kwani makampuni mengi yamebaini gharama
kubwa iliyopo kwenye matumizi ya mafuta ya dizeli na sasa yanahitaji
makaa ya mawe kwa uzalishaji.
“Nimetembelea
mgodi na kujiridhisha kuwa makaa ya mawe yapo ya kutosha. Uongozi wa
kampuni mmesema mashine ziko bandarini Mtwara, lipieni mkamilishe
taratibu ili mashine na mitambo yenu vije kusaidia kuongeza uzalishaji,” alisema.
“Nirudie
wito wa Serikali kuwa hatutaruhusu uagizaji wa makaa ya mawe kutoka nje
ya nchi na kwa maana nyingine tumewaongezea wigo wa soko lakini ninyi
mnakosa teknolojia ya uchimbaji makaa kwa wingi. Fanyeni haraka kuleta
hivyo vifaa vilivyoko bandarini,” alisisitiza.
Akiwa
kwenye mgodi huo, Waziri Mkuu alielezwa kuwa kampuni hiyo imepanga
kuongeza uzalishaji na kufikia tani 60,000 kutoka tani 2,500 za sasa.
Hivi sasa, uchimbaji kwenye mgodi wa Ngaka unafanyika kwenye eneo la
Mbalawala na Mbuyura ambayo yana mashapo (deposits) ya tani milioni 423.
IMETOLEWA NA
Tanzania Yapata Fursa Kubwa ya Biashara....Yaingizwa Katika Mpango Mkubwa wa Biashara na China
Jitihada
za Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan za kuiingiza Tanzania katika
mpango mkubwa wa biashara kwenye Bara la Asia, Mashariki ya Kati, Ulaya
na Afrika, umefanikiwa.
Ni baada ya Tanzania kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi saba zilizoingizwa katika mpango, unaojulikana kama ‘China One Belt, One Road Stratergy’. Nchi nyingine ambazo zimechaguliwa na kuingizwa kwenye mpango huo ni Malaysia, Sri Lanka, Nepal, Bangladesh, Pakistan na Thailand.
Taarifa
iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, jana, ilisema baada ya Tanzania
kuingizwa rasmi katika mpango huo, Makamu wa Rais, Samia ambaye pia
mjumbe katika jopo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa la Kumuwezesha
Mwanamke Kiuchumi, akiwakilisha nchi za Ukanda wa Kusini na Mashariki
mwa Afrika, alikutana na watendaji kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi
Tanzania (TPSF), Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Biashara
(TCCIA) na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), kuwaeleza kuhusu muhimu
wa Tanzania kuingizwa kwenye mpango huo.
Makamu
wa Rais alisema Tanzania imepata uanachama ndani ya mpango huo, baada
ya kukutana na kufanya mazungumzo na mfanyabiashara wa madini na vito
kutoka China, Dk Helen Lau kuhusu manufaa ya mpango huo.
Alisema
alimuomba mfanyabiashara huyo, kuisaidia Tanzania kuingia kwenye mpango
wa China One Belt, One Road Stratergy, jambo ambalo limefanikiwa.
Taarifa
hiyo iliendelea kusema kuwa mwezi Septemba mwaka 2016, ulifanyika
mkutano Guangdong nchini China kujadili maombi ya kujiunga na mpango
huo, ambapo Makamu wa Rais alimuomba Dk Helen, kwa niaba ya Tanzania,
awasilishe maombi ya kutaka kujiunga.
Kwa
bahati nzuri, ombi la Tanzania lilikubaliwa na kupata uanachama katika
mpango huo mkubwa wa China One Belt, One Road Stratergy.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, Makamu wa Rais alisema kuwa moja ya fursa
zinazotolewa na Serikali ya China katika mpango huo, kila nchi
mwanachama hupewa vyumba vya ofisi katika jengo linaloitwa 21st Century
Maritime Silk Road Expo bila kulipa kodi ya pango kwa miaka mitatu.
Baadhi
ya vyumba vya jengo hilo, vitatumiwa na nchi husika kuonesha na
kutangaza bidhaa zao. Kufutia Tanzania kuingizwa kwenye mpango huo,
Samia aliwaagiza watendaji wa sekta binafsi aliokutana nao Ikulu jijini
Dar es Salaam, wajipange na kuweka mikakati ya namna ya kunufaika na
mpango huo haraka iwezekanavyo.
Alibainisha
kuwa mpango huo wa China One Belt, One Road Stratergy, ulibuniwa na
serikali ya China kwa dhamira ya kuzikutanisha jumuiya za
wafanyabiashara za Mashariki mwa Bara Asia, Mashariki ya Kati, Ulaya na
Afrika ili wabadilishane mawazo, kuonesha njia na kupeana ushauri wa
jinsi ya kukuza biashara kati ya nchi wanachama wa mpango huo ili
kuiwezesha sekta ya biashara, kuchangia vyema kwenye uchumi wa mataifa
yao.
Makamu
wa Rais alisema baada ya Tanzania kuingia kwenye mpango huo, itanufaika
na fedha za mfuko kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu, ambazo
zinatolewa kwa nchi zilizojiunga na mpango huo.
OFISI YA WAZIRI MKUU
Zitto Kabwe Aitaka Serikali Itangaze Balaa la Njaa
Kiongozi
wa Chama cha ACT –Wazalendo, Zitto Kabwe ameitaka Serikali kutangaza
rasmi baa la njaa kwa mujibu wa sheria kutokana na hali ya chakula kuwa
mbaya nchini.
Kauli
ya Zitto imetolewa wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisisitiza
utunzaji wa chakula baada ya kukagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Kanda ya Songea.
Agizo
la Majaliwa pia limetolewa siku mbili baada ya Waziri wa Kilimo, Dk
Charles Tizeba kutofautiana na Zitto kuhusu hali ya chakula ambapo
Waziri huyo alisema hali ya chakula nchini ni shwari huku Mbunge huyo wa
Kigoma Mjini akisema ni mbaya.
Jana,
mbunge huyo akihutubia mkutano wa kampeni ya kumnadi mgombea udiwani
Kata ya Nkome, Geita aliendelea kupigilia msumari kauli yake akisema,
“Hali ya chakula ni mbaya, ni mbaya, ni mbaya.”
Alisema
baada ya ziara ya Waziri Mkuu kwenye maghala ya Taifa na kujionea hali
ya chakula nchini, ni vyema Serikali ikachukua hatua.
“Ninapendekeza
Serikali ichukue hatua muhimu ya kisheria ya kutangaza baa la njaa
nchini. Tamko la baa la njaa litaisaidia Serikali kupata bajeti ya
dharura ya kununua chakula na kutoa uhuru kwa wakuu wa wilaya kutangaza
bila woga kuwa maeneo yao yana njaa,” alisema Zitto huku akimpongeza Majaliwa kwa ziara hiyo.
Lowassa, Maalim Seif Kutikisa Zanzibar Kesho
Wanasiasa
wakongwe nchini, Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar na Edward Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika, kesho wanatarajia kuungana kwa mara ya
kwanza jukwaani tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Vigogo
hao wa vyama vya CUF (Maalim Seif) na Chadema (Lowassa) wataunguruma
katika viwanja vya Skuli ya Fuoni visiwani Zanzibar kumnadi mgombea
ubunge wa jimbo la Dimani kwa tiketi ya CUF, Abdulrazaq Khatib
Ramadhani, katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Januri 22 kuziba nafasi
ya aliyekua mbunge wa jimbo hilo, Hafidh Ally Tahir aliyefariki dunia
Novemba 11 mwaka jana.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu amesema kuwa chama chake kimemua
kuungana na CUF katika uchaguzi huo ili kuhakikisha mshirika wake huyo
wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) anamshinda mgombea wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Aidha,
Mwalimu aliongeza kuwa baada ya Lowassa kushiriki uzinduzi wa kampeni
hizo kesho, viongozi wengine wa Chadema watafuata kwa kufanya mikutano
mbalimbali jimboni humo. Alisema kuwa baada ya Lowassa atafuata
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe pamoja Tundu Lissu kwa nyakati
tofauti, kisha wengine wataendelea hadi mwisho wa kampeni hizo.
Akizungumzia
uamuzi huo wa Chadema, Mkurugenzi wa Habari,Uenezi na Mawasiliano kwa
Umma, Salim Bimani alieleza kufurahishwa na uamuzi huo wa Chadema na
kueleza kuwa hatua ya Lowassa kuhudhuria uzinduzi huo itaongeza hamasa
kubwa kwa wapenzi wa chama hicho.
“Umenambia
hadi Lowassa atakuwepo? Ni furaha iliyoje, Wanzibari wana shauku
kumuona. Siku ya kampeni patakuwa hapatoshi Skuli ya Fuoni, hapa Simba
(Maalim Seif) kule Lowassa kipenzi kingine cha Wazanzibar,” Bimani
anakaririwa na Mwananchi.
Aliongeza
kuwa kama Lowassa atahudhuria mkutano huo atakuwa na mambo mawili
makubwa ya kufanya, la kwanza likiwa kuwashukuru Wazanzibar kwa kura
walizompa katika uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Na la pili litakuwa
kumpigia kampeni mgombea wa CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhani.
Lowassa
ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Maalim Seif ambaye ni
Katibu Mkuu wa CUF, wataingia katika jimbo hilo ikiwa ni siku chache
baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kufanya uzinduzi wa
kampeni hizo akiambatana na viongozi wengine wa kitaifa wa chama hicho.
\ ..............
Wafugaji 50 Wala Kinyesi, Damu na Mkojo Kunusuru Maisha Yao
Watu
50 wakiwa na watoto wadogo wamenusurika kufa, baada ya kupotea ndani ya
Pori la Akiba la Selous kwa siku saba; huku wakikosa chakula na maji na
kulazimika kula kinyesi cha ng’ombe, damu na mikojo ya binadamu.
Watu
hao ambao ni wafugaji, walikuwa wakihama na mifugo yao inayokadiriwa
kufikia 1,780 kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Rufiji mkoani Pwani,
yakiwemo Chumvi na Muhoro waliekea Morogoro, ambako walidai ndiko
yalipo makazi yao.
Tukio
hilo ambalo si la kawaida kutokea katika pori hilo, lilianzia Jumatano
iliyopita wakati wafugaji hao, walipoanza safari ya kuelekea Malinyi
mkoani Morogoro, wakiongozwa na mwenyeji wao, waliyemtaja kwa jina la
Mzee Mzigua, ambaye hata hivyo wanadai aliwalaghai na kuwatelekeza.
Wafugaji
hao walisema walitembea kwa siku tano ndani ya pori hilo, wakitarajia
kufika Malinyi, yaliko makazi yao. Lakini hali ilikuwa tofauti, baada ya
mwenyeji wao huyo, kuwalaghai kwa kuwapitisha njia sisizo sahihi.
Walisema
waliishiwa chakula na maji ya akiba na mwisho walijikuta wanatokea
ndani ya Pori la Akiba la Selous; huku hali zao zikiwa zimedhoofu
kutokana na njaa na kiu cha maji. Wakiwa safarini, mwenyeji wao huyo,
aliwataka kila mmoja alipe fedha ikiwa ni ujira wake kwa kuwaonyesha
njia. Walidai kuwa walimlipa fedha nyingi.
Wengine
walimlipa Sh milioni mbili, Sh milioni moja na wengine Sh 500,000,
wakitarajia angewasaidia. Walitembea usiku na mchana ndani ya pori hilo,
wakipishana na wanyama wakali kama simba na nyati, hivyo kuhatarisha
usalama wa maisha yao na watoto wao.
Hali
ilizidi kuwa mbaya zaidi, baada ya kutimia siku ya tano wakiwa ndani ya
pori hilo, pale walipoishiwa chakula na maji, hivyo kuwalazimu kuanza
kuchinja ng’ombe na kunywa damu kwaajili ya kukata kiu. Pia walikula
kinyesi chao ili kupunguza njaa. Yule mwenyeji wao aliwatelekeza baada
ya kuona hali zao zimekuwa mbaya.
Alitokomea
kusikojulikana, akiwaacha wasijue pa kwenda, hivyo kulazimika
kutelekeza mifugo yao ili kunusuru kwanza maisha yao. Halikadhalika,
wengine walilazimika kunywa mikojo yao na mingine kuwanywesha watoto wao
kunusuru maisha yao, hali iliyowafanya kuathirika kiafya na kushindwa
kuendelea na safari.
Wengine walianguka na kupoteza fahamu. “Sisi
tulikuwa tunataka turudi nyumbani kwetu Morogoro. Huku tulikuja wakati
wa operesheni ya Morogoro, huku tulikuja kununua ng’ombe lakini miji
yetu ipo kule Morogoro. Tukaambatana na huyo mwenyeji wetu
aliyejitambulisha kwa jina la Mzee Mzigua na mtoto wake.Lakini tunajua
mpaka nyumbani kwake”alisema Kiongozi wa msafara wa wafugaji hao, aliyejitambulisha kwa jina la Lisesi Cherahani Bela na kuendelea;
“Zilitimia
kama siku nne tukiwa hatujanywa maji, jua lilikuwa linawaka, tukaanza
kuanguka, tukaanza kuchinja ng’ombe na kunywa damu, tulijaribisha kula
kinyesi cha ng’ombe, tulikuwa tunakojoa mkojo tunanywesha hata watoto.
Mimi nilikunywa mkojo lita moja, ikaniathiri hapa kifuani, kumbe mkojo
ni kitu kibaya.”
Akizungumza
na waandishi wa habari waliofika katika eneo hilo, kiongozi huyo
alisema baada ya kuona hali inakuwa mbaya zaidi, alitafuta eneo ambalo
lina mtandao wa simu na kufanya mawasiliano na watu mbalimbali, ambapo
alifanikiwa kuwasiliana na watu wa Kigoma na kuomba msaada wao.
Alisema
kuwa watu hao, waliwasiliana na wahifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi
na kuwasiliana na wahifadhi wa Pori hilo la Selous, ambao walianza kazi
ya kuwasaka na hatimaye kuwakuta katika eneo la Mlima Luhombelo,
lililopo katikati ya Pori hilo wakiwa tayari wameshadhoofika kiafya.
Askari
hao wa wanyamapori wa Pori hilo, waliwapatia uji na maji na kuwapa
huduma ya kwanza wale wengine ambao walikuwa na hali mbaya.
Baada
ya taarifa hizo za kupotea kwa wafugaji hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maliasili na Utalii, Gaudence Milanzi alifika katika eneo hilo juzi,
akiambatana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania
(TAWA), Martin Leibooki, Meneja wa Pori la Akiba la Selous, Henock
Msocha na maofisa wengine wa wizara na pori hilo.
Milanzi
alisema Serikali inaangalia namna ya kuwasaidia wafugaji hao, kurejea
katika hali zao kiafya pamoja na kuwasaidia kutafuta mifugo yao ili
waweze kurejea katika makazi yao na kuendelea na shughuli zao.
“Kwa
upande wa Serikali kama Wizara hatuchukulii kama hawa wameingia kwenye
hifadhi hapana, muhimu kwanza ni kuokoa maisha ya binadamu, na hicho
ndicho tunategemea kukifanya sasa hivi, na baada ya hapo kutakuwa na
masuala ya kutafuta hiyo mifugo, kwa sababu wamepata hasara kubwa”alisema Katibu Mkuu huyo.
Aliutaka
uongozi wa wilaya ya Rufiji, kutoa ushirikiano na wizara ili kuwabaini
waliowadanganya wafugaji hao, kwa kuwaingiza kwenye pori hilo na
kuwatapeli kiasi hicho kikubwa cha fedha.
“Hawa
waliowadanganya na kupita huko ndani ya pori kwa kweli tutaendelea
kuwatafuta na tutaomba tuwe na ushirikiano na uongozi wa Wilaya kwa
sababu inaelekea kuna watu kazi yao ndo hiyo, ukiangalia pesa walizowapa
ni nyingi sana, sasa watu wamechukua pesa zote na wamewaacha katika
hali kama hii, wengine wana watoto wadogo, kwa hiyo tutahakikisha
tunashirikiana kuwatafuta ili tukomeshe hili tatizo moja kwa moja”alisema.
Katibu
Mkuu huyo alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TAWA na Mhifadhi Selous kwa
juhudi za haraka walizochukua. Alisema wizara yake itaendelea
kushirikiana na Mamlaka mbalimbali, kutoa misaada ya haraka, endapo
yatatokea tena matukio ya aina hiyo.
Kwa
upande wake, Leibooki alisema TAWA ambao ndiyo wamiliki wa hifadhi zote
za wanyamapori nchini, haitawachukulia hatua za kisheria wafugaji hao,
kwa kuwa waliingia ndani ya pori kwa kudanganywa na watu wenye nia
mbaya.
Lakini,
alisisitiza kuwa mamlaka yake, itawashughulikia kisheria wawindaji
haramu na wafugaji wanaoingiza mifugo yao ndani ya hifadhi zilizo chini
ya Mamlaka yake.
Pia
alisema Mamlaka yake, inaendelea na utaratibu wa kushirikiana na
wananchi waishio pembezeni mwa hifadhi zote, kwa kuwapa elimu ya ufugaji
bora kwa kushirikiana na wizara zinazohusika na kuendeleza miradi ya
maendeleo, ikiwemo miundombinu ya maji.
Katibu
Mkuu wa Chama cha Wafugaji chini (CCWT), Magembe Makoye aliwataka
viongozi wa Halmashauri mbalimbali nchini, kutatua migogoro ya wakulima
na wafugaji mahali walipo, bila ya kuondoa watu wengine.
Alisema
kuwa wao kama chama, wamesikitishwa na tukio la kuondolewa kwa wafugaji
hao katika bonde hilo la Rufiji, kwa kuwaambia warudi walipotoka.
Alisema tamko hilo lilitolewa na uongozi wa Halmashauri hiyo na ndilo
lililosababisha matatizo hayo.
Makoye
alisema kufanya hivyo, hakuondoi migogoro ya wafugaji na wakulima,
badala yake ni kuendelea kuzalisha migogoro hiyo katika maeneo mengine,
ambayo wafugaji watahamia.
“Tunalaani
kweli vitendo hivi vya viongozi na watendaji wengine wa Halmashauri
kuwafukuza wafugaji, tena wakati mwingine kwa kuwatisha na matokeo yake
wananchi hawa 50 wangepoteza maisha, kama isingekuwa bahati ya mtu mmoja
kuwa na simu kati yao” alisema Katibu Mkuu huyo.
“Kwa
kweli kwa niaba ya wafugaji wote wa Tanzania naishukuru sana Wizara ya
Maliasili kupitia kwa Katibu Mkuu, Gaudence Milanzi.” alisema Katibu huyo.
Alisema
kuwa kungeweza kutokea majanga makubwa zaidi kwa kuwa kuwa wafugaji hao
walikuwa wakisafiri na watoto wao wadogo katika mazingira hatarishi
katikati ya pori hilo, ambalo lina wanyama wakali.
“Kwa
kweli ni mazingira ya kusikitisha. Lakini niishukuru sana Serikali kwa
maana ya Wizara ya Maliasili na Utalii, wamefanya kazi yao kwa namna
ambavyo mimi ninawiwa kuwashukuru. Tangu jana tumewasiliana na Katibu
Mkuu wa Wizara, leo watu wote wameweza kupatikana, kumefanyika doria ya
ndege, doria za magari, doria kwa miguu, wamewatafuta hawa watu,
wamewaokoa, wamewaleta kwenye huduma za afya, wamewapa chakula,
wamewahifadhi, hawajawadhuru” alisema.
Baadhi
ya Mzoga wa ngombe uliopatikana ndani ya Pori la Akiba la Selous,
Kanda ya Kaskazini Mashariki Kingupira baada ya Wafugaji 50
waliotelekezwa kwa muda wa siku tano na mtu mmoja waliyemtaja kwa jina
maarufu la Mzigua aliyewarubuni kwa kuwaonyesha njia za mkato ndani ya
Pori hilo na kisha kuwakimbia( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya
Maliasili na Utalii)
Mmoja
wa wafugaji aliyepotea na kutelekezwa ndani ya Pori la Akiba la
Selous, Bw. Lisesi Cherehani aliyekuwa na ng’ombe 180 na punda mmoja
akiangalia mmoja wa ng'ombe wake aliyekufa kwa kukosa maji ya kunywa
kwa muda wa siku tano kwenye Kanda ya Kaskazini Mashariki katika Pori
la Akiba la Selous ( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na
Utalii)
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi
(katikati) akipata taarifa kutoka kwa Meneja wa Mradi wa Pori la Akiba
la Selous Bw. Enock Msocha (wa tatu kushoto) mara baada ya kuwasili
kwa ajili ya kuwatembelea Wafugaji 50 waliokolewa na Askari
wanyamapori baada ya kutelekezwa na mtu mmoja waliyemtaja kwa jina
maarufu la Mzigua aliyewarubuni kwa kuwaonyesha njia ya mkato ndani ya
Pori hilo na kisha kuwakimbia ( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya
Maliasili na Utalii)
Uzinduzi wa Kampeni: Kinana Arusha Kombora Zito Kwa Maalim Seif na CUF
Katibu
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amerusha kombora
zito kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif
Hamad, huku akimwita mgombea wa urais wa kudumu aliyekata tamaa.
Pamoja
na hayo, Kinana amewataka Wazanzibari kuachana na maneno ya mitaani
kwani Uchaguzi Mkuu ulishamalizika na Dk. Ali Mohamed Shein
ameshaapishwa kuwa rais kwa mujibu wa sheria.
Kauli
hiyo aliitoa jana katika uzinduzi wa kampeni za chama hicho za uchaguzi
mdogo wa ubunge Jimbo la Dimani zilizofanyika Maungani, nje kidogo ya
mji wa Unguja.
Alisema
CCM itaendelea kuchaguliwa na wananchi kwa sababu inatimiza wajibu wa
kuwatumikia wananchi, kutimiza matakwa na sera kwa mujibu wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM.
Kinana
alishangazwa na CUF kushindwa kutanua wigo wa demokrasia ndani ya chama
hicho na kuendelea kumshikilia mgombea urais mmoja wa kudumu kwa zaidi
ya miongo minne.
“Kuna
mgombea mmoja hapa Zanzibar ameanza kugombea urais tokea akiwa na miaka
30 na sasa ana miaka 80, toka akiwa bado kijana mbichi, sasa amekuwa
kikongwe na kupinda mgongo ila bado ana tamaa ya kuwania urais.
“Demokrasia
ndani ya chama chetu ni ya aina yake na kwamba kukubalika kwetu mbele
ya wananchi kunatokana na misimamo yetu inayotetea masilahi ya umma.
Hata demokrasia yetu ndani ya CCM kamwe haifanani na vyama vingine,” alisema Kinana huku akishangiliwa.
Kinana
alisema CCM ina umoja imara na katu hazuiwi mwanachama kuwania nafasi
ya uongozi na haina sifa ya kuwa na wagombea wa kudumu kama ilivyo CUF
ambayo tangu ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 hadi sasa,
Katibu Mkuu wake Maalim Seif amekuwa mgombea wa kudumu.
Alisema
ushiriki wa wana CCM 25 ndani ya chama kuwania nafasi ya uteuzi wa
ubunge Jimbo la Dimani ni kielelezo tosha cha kuimarika kwa demkorasi,
na mgombea aliyepatikana anaungwa mkono na wanachama wote.
Alieleza
kuwa vikao vya CCM vya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati Kuu
(CC) vilikutana na kupitisha jina la mgombea aliyeshinda kura za maoni,
huku CUF ikiwa kimya, ikishindwa hata kufanya vikao vyake kwa mujibu wa
katiba ya chama chao.
Akizumgumzia
kupwaya kwa dhana na misingi ya demokrasia ndani ya CUF, Kinana alisema
hivi sasa chama hicho kina wenyeviti watatu, ambao mmoja ni wa muda,
mwingine wa mpito na aliyebaki ni wa zamani
Aidha
Kinana aliwashangaa wanachama wa CUF ambao wanakubali kudanganywa
kirahisi kila siku na kuaminishwa ipo siku mgombea wao wa urais
aliyeshindwa uchaguzi atatangazwa na Umoja wa Mataifa (UN) kuwa Rais wa
Zanzibar.
“Tuliambiwa
hapa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar utafutwa, watakuja watu toka UN, mara
tukaelezwa wangekuja Jumuiya ya Ulaya, wakaambiwa washone nguo mpya
kusherehekea ushindi, huku siku zikitaradadi hakuna kinachotokea,” alisema.
Kinana
alisema viongozi wa CUF hawana uwezo wowote wa kuwatumikia wananchi na
kuwaletea maendeleo kwani walibahatika kuingia katika Serikali ya Umoja
wa Kitaifa, lakini bado hakuna walichofanya.
“Kama
ni mkate CUF walipata nusu na CCM nusu, wakashika wizara makini za
Biashara na Viwanda, Katiba na Sheria, Habari na Utamaduni, Mawasiliano
na Miundombinu, lakini kutokana na wao kuwa dhaifu, hawakumudu hata
kujenga kiwanda kidogo,” alisema.
Kinana
aliwaomba wananchi wa Dimani kumchagua mgombea ubunge wa CCM, Juma Ali
Juma kwa sababu ni makini, mchapakazi na mwepesi wa kuwatumikia
wananchi.
Akihutubia
katika mkutamo huo wa uzinduzi wa kampeni, mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM,
Balozi Seif Ali Idd, aliwaeleza wananchi wa Dimani kuwa si sifa ya
wagombea wa CUF kuwatumikia wananchi na mfano mzuri ni katika majimbo ya
Pemba.
Vigogo Wengine Kutumbuliwa TANESCO.....Lengo ni kuimarisha utendaji wa Shirika Hilo
Siku
moja baada ya vigogo watatu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
kushushwa vyeo, uongozi wa shirika hilo umesema utaendelea na fagio hilo
kama njia ya kuongeza ufanisi kwenye utendaji.
Vigogo
hao wa ngazi za juu ambao ni wakurugenzi, wamehamishiwa Chuo cha
Mafunzo cha Tanesco (TSS) kwa madai kuwa shirika linaboresha ufanisi
wake.
Walioshushwa vyeo ni pamoja na Declan Mhaiki aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji anayeshughulikia usambazaji wa umeme.
Wengine
ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji na Huduma kwa Mteja, Mhandisi
Sophia Mgonja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji Umeme, Nazir
Kachwamba.
Wakati
hao wakipitiwa na panga hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali Watu,
Watson Mwakyusa, aliamua kuandika barua kuacha kazi mwenyewe.
Juzi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka, alisema jana wangetoa taarifa kuhusu hamisha hamisha hiyo.
Jana
mchana Idara ya Kitengo cha Mahusiano cha Shirika hilo, kilitoa taarifa
na kusema kuwa wataendelea na hatua mbalimbali za mabadiliko ya uongozi
kwa lengo la kuongeza ufanisi zaidi wa kiutendaji.
Taarifa
hiyo ilieleza kuwa mabadiliko yanayoendelea ndani ya Tanesco yatawekwa
wazi wakati mwafaka kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za shirika
kupitia vyombo vya habari.
Kitengo hicho kilieleza kuwa kwa sasa bado wanaendelea na panga pangua na endapo watakamilisha watatoa taarifa kwa umma.
“Tunaomba
vyombo vya habari vitoe fursa kwa mamlaka husika kuendelea kukamilisha
zoezi hili muhimu kwa maendeleo ya Shirika na Taifa kwa ujumla na
taarifa rasmi itatolewa baada ya zoezi kukamilika,’’ ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Januari
Mosi, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli alimteua Dk. Mwinuka kuwa Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, baada ya kumng’oa aliyekuwa mkurugenzi
wa shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Mramba
alitenguliwa uteuzi wake siku mbili baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa
Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kutangaza kuridhia ombi la Tanesco la
kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 kutoka 18 waliyoomba.
Kabla ya uteuzi huo, Dk. Mwinuka alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Akiwa
mjini Bukoba kwenye ibada ya Mwaka Mpya, Rais Magufuli alisema amekerwa
na kusikitishwa na vitendo vya baadhi ya watumishi wa umma kujitokeza
hadharani na kutangaza au kuzungumzia mambo ya kitaifa kama uamuzi wa
Serikali bila kushirikisha viongozi wao wa ngazi za juu.
Kutokana na hali hiyo, alisema watendaji hao ni miongoni mwa majipu yanayostahili kutumbuliwa.
Waziri Nchemba: Hatutamhukumu mtu kwa kazi anayoifanya, tutamhukumu kwa kosa analolifanya
Ikiwa
imepita siku moja tangu waziri wa mambo ya ndani ya Nchi Mwigulu
Nchemba kusema kuwa watakaofanya unyama wa kuua au kuchinja watu au
wanyama kwa mapanga na sime wataona chamoto, bado kauli hiyo imekaidiwa
kwa baadhi ya watu wanaosadikika kuwa ni wa jamii ya kifugaji baada ya
kumjeruhia kichwani kwa sime Rajabu Ayub (36) mkazi wa kijiji cha
Mbigiri wilayani kilosa, akiwa shambani kwake na kumsababishia maumivu.
Polisi
mkoani Morogoro mpaka sasa inawashikilia watu 24 kwa mahojiano zaidi
kuhusu tukio hilo. Waziri Mwigulu Nchemba ameagiza nguvu zaidi ya dola
iongozwe katika maeneo hayo mpaka mhusika wa tukio hilo atakapopatikana.
Marekani kumsaka mtoto wa Osama Bin Laden Aliyeapa Kulipa Kisasi
Marekani
imesema kuwa imemuorodhesha mtoto wa mwisho wa Osama Bin Laden, Hamza,
katika orodha ya magaidi wanaosakwa na taifa hilo.
Wizara
ya mambo ya nje ya Marekani imesema kuwa Hamza Bin Laden ameanza
kushiriki katika maswala ya kundi la al Qaeda, kundi la jihad
lililofadhiliwa na babake.
Hamza
amesema kuwa atalipiza kisasi mauaji ya babake yaliotekelezwa na kikosi
maalum cha Marekani kwa kutekeleza mashambulizi dhidi ya Wamarekani.
Hamza amepigwa marufuku kufanya biashara na raia wa Marekani huku mali zake zikizuiliwa pia.
Mamake
Hamza ni Khairiah Sabar, mmoja wa wake za Osama aliyekamatwa wakati wa
shambulio la wanajeshi wa Marekani kwenye maficho ya Osama mjini
Abbotabad nchini Pakistan mwaka 2011.
Mkuu wa kitengo cha usalama cha kundi la al-Qaeda Ibrahim al-Banna pia ameongezwa katika orodha hiyo .
Marekani imetoa kitita cha dola milioni 5 kwa mtu yeyote atakayemkamata al-Banna.
Hamza
bin Laden alitambuliwa kuwa mmoja wa viongozi wa al-Qaeda mwaka 2015 na
baadaye akaapa kulipiza kisasi mauaji ya babake mwezi Julai mwaka
uliopita.
Katika
ujumbe wa sauti wa dakika 21 wenye kichwa "We Are All Osama," (Sote ni
Osama), na uliochapishwa katika mitandao, aliapa lazima angelipiza
kisasi mauaji ya babake mwaka 2011 nchini Pakistan.
''Tutaendelea
kuwasaka na kuwapiga popote pale mtakapokuwa mmejificha ati nyuma ya
pazia za usalama kwa maovu mnayoyaendeleza ,Palestina, Afghanistan,
Syria, Iraq, Yemen, Somalia na kote kwenye ardhi ya waislamu
mnayokalia,'' shirika la habari la Reuters lilimnukuu.
''Na
kwa wale wanaodhania kuwa tutakuwa tukilipiza kisasi mauaji ya Osama
ole wenu, kwanini sisi tutakuwa tukilinda dini ya kiislamu'' alisema Hamza.
Hamza,
kulingana na wachanganuzi, alitambulishwa na kiongozi wa kidini wa
kundi la al-Qaeda Ayman al-Zawahiri katika ujumbe huo uliolenga
kuwavutia vijana ambao kwa sasa wamejiunga kwa wingi na kundi la Islamic
state.
Hamza sasa anaungana na nduguye wa kambo, Saad, kuwa miongoni mwa watu wa jamii ya Osama walioorodheshwa kuwa magaidi.
Chanzo: BBC
Chanzo: BBC
Serikali yapiga marufuku ununuzi wa sare za jeshi la zima moto na uhamiaji toka taasisi binafsi
Naibu
waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mhandisi Hamad Yusuph Masaun amepiga
marufuku ununuzi wa sare za jeshi la zima moto na uhamiaji kwa taasisi
binafsi na badala yake ameagiza sare hizo zizalishwe katika viwanda vya
jeshi la magereza nchini.
Mhandisi
Masauni ameyasema hayo baada ya kutembelea kiwanda cha jeshi la
magereza kilichopo Ukonga kinachoendeshwa kwa nguvu kazi ya wafungwa
ikiwa ni ufuatiliaji, utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania la kulitaka jeshi hilo liwasimamie wafungwa katika
uzalishaji wa sare.
“Kuanzia
leo uhamiaji,zima moto wote washone nguo, kama ambavyo magereza
wanashona katika kile kiwanda, kwamba dhamira ya mheshimiwa rais ya
kutoa maelekezo ambayo yamefuatilia utendaji kazi wake nimeridhika,
kwamba ni marufuku kama alivyosema mheshimiwa rais kwa askari Magereza
na askari wote wa vyombo vya usalama nchini kununua uniform kwa raia,
jeshi la magereza linatengeza furniture zenye ubora wa hali ya juu,”
alisema Mhandisi Masauni.
Lowassa Atajwa Kusababisha Deni la Milioni 1
Jina
la waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa limetajwa na mkaazi mmoja wa
Mbeya mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla kuwa sababu ya deni la
shilingi milioni moja kutokana na mapenzi ya wafuasi wake.
Mkaazi
huyo wa kata ya Ruanda Nzovwe aliyejitambulisha kwa jina la Amos
Mwakyambiki alidai kuwa wafuasi wa Chadema waliharibu paa la nyumba yake
walipopanda kwa lengo la kufuatilia mkutano wa Lowassa wakati wa
uchaguzi mkuu wa mwaka jana, na kwamba chama hicho kilimuahidi kumlipa
fidia ya shilingi milioni moja lakini hadi sasa ahadi hiyo
haijatekelezwa.
Alimueleza
mkuu wa mkoa huo kuwa kutokana na uharibifu huo mkubwa uliofanyika,
wapangaji wake waliamua kuhama nyumba yake hivyo kukosa kipato.
“Naomba
Serikali ya Mkoa inisaidie kuzungumza na meya (wa Chadema) ili niweze
kulipwa stahiki zangu kwani sasa sijui hatma yangu. Kuku niliokuwa nauza
kwa ajili ya kupata nauli kwenda ofisi za jiji wamekwisha,” Mkaazi huyo
anakaririwa.
Kutokana
na madai hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya alimuagiza Mkuu wa Wilaya
kufuatilia suala hilo huku akitahadharisha wananchi kuhusu matumizi ya
nyumba zao wakati wa kampeni.
“Lakini na nyie wananchi msikubali nyumba zenu zibadilishwe kuwa viwanja vya siasa,” alisema Makalla.
Akizungumzia
taarifa hizo, Mkuu wa Idara ya Habari ya Chadema, Tumaini Makele
alisema kuwa chama hicho kitafuatilia kuona ni nani aliyetoa ahadi hiyo
kwa mwananchi huyo na ilikuwa katika mazingira gani ili walifanyie kazi
ipasavyo.
Picha 8: Muonekano wa sasa wa Jennifer na Patrick walioibuliwa na marehemu Steven Kanumba
Watu
wengi watawakumbuka Jennifer na Patrick kwa jinsi walivyoweza kutikisa
tansia ya filamu Tanzania kipindi cha nyuma walipoibuliwa na marehemu
Steven Kanumba.
Watoto hawa wawili walicheza kwa ustadi mkubwa katika filamu za Uncle JJ na This is It zote za marehemu Kanumba.
Kwa
sasa Hanifa Daud ‘Jennifer’ na Othman Njaidi ‘Patrick’ si watoto tena.
Wawili hawa hawajaonekana sana kwenye filamu baada ya Steven Kanumba
aliyewatoa kufariki.
Jennifer
ambaye amehitimu kidato cha nne mwaka jana mara ya mwisho alionekana
kwenye filamu ya Zena na Betina ya Salma Jabu a.k.a Nisha mwaka 2014.
Kwa upande wake Patrick, yeye alisema kuwa hana shauku ya kuigiza tena
kama ilivyokuwa awali.
Credit: Bongo5
Saturday, January 7, 2017
Picha: Billicanas Ya Mbowe Yabomolewa Rasmi
Shirika
la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza kubomoa jengo la iliyokuwa Klabu
Bilicanas na ofisi za Free Media inayomiliki gazeti la Tanzania Daima
zinazomilikiwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe, lililopo makutano ya barabara
ya Mkwepu na Indira Gandhi lenye kitalu namba 725-726/24 na hati namba
C. T No. 186018/15 and C. T No. 186018/10.
Ubomoaji huo ulioanza jana unafanyika wakati Mbowe ameingia katika mgogoro na NHC baada ya kampuni ya udalali ya Poster and General Traders kumtolea vyombo nje mwanzoni mwa Septemba, mwaka jana kwa kudaiwa Sh bilioni 1.2 ambayo ni deni la pango ya miaka 20.
Mwanzoni
mwa Septemba, mwaka jana NHC kwa kushirikiana na Kampuni ya Poster and
General Traders, ilifika katika jengo hilo kwa maelekezo ya kutoa
thamani mbalimbali zilizokuwa katika ofisi za jengo hilo na kumpa Mbowe
siku 14 kulipa deni analodaiwa na kuweza kugomboa mali hizo.
Mpango
huo ulisimamiwa na Meneja wa Ukusanyaji Madeni wa NHC, Japhet
Mwanasenga na alisema Mbowe alikuwa na muda wa wiki mbili kwa wakati huo
kulipa fedha hizo kabla ya vifaa vyake kupigwa mnada.
Mwanasenga
alisema taratibu zote zilifuatwa kabla ya kumwondoa mteja huyo ikiwamo
notisi na kwamba vifaa hivyo vitashikiliwa kwa muda huo na endapo
akishindwa kulipa jengo hilo atapangishwa mtu mwingine.
Alisema
shirika hilo linahitaji fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa
majengo yake hivyo mteja anayedaiwa ajiandae kuondolewa wakati wowote
huku baadhi ya watu wakilihusisha tukio la Mbowe kuondolewa katika ofisi
hizo na masuala ya siasa.
Hata hivyo, Mwanasenga, alisema uamuzi wa kumwondoa katika ofisi hizo hauna uhusiano na masuala ya siasa.
Kutokana
na hali hiyo, Mbowe kupitia Mawakili wake, John Malya na Peter
Kibatala, walifungua shauri la kupinga kuondolewa katika jengo hilo
Mahakama Kuu ya Tanzania na kutaka kurudishwa katika jengo hilo.
Hata
hivyo, maombi hayo yalitupiliwa mbali Oktoba 17, mwaka jana na Jaji
Sivangilwa Mwangesi na kusema kuwa mahakama hiyo imechukua uamuzi huo
baada ya kujiridhisha na hoja kuu tatu kuwa hakuna mkataba wa ubia
uliopo baina ya NHC na Mbowe Hotels Limited na kuwa uhusiano pekee
uliosalia ni wa mpangaji na mpangishaji.
Pia
Jaji Mwangesi alisema mahakama imejiridhisha kuwa NHC imefuata taratibu
zote katika kuiondoa Mbowe Hotels Limited kwa kutoa ilani ya siku 30 na
baadaye siku 14 kabla ya kumtoa mteja wao huyo.
Kuhusu
kusajiliwa au kutosajiliwa kama dalali rasmi wa mahakama wa kuendesha
mchakato wa kumhamisha Mbowe katika jengo hilo, alisema hiyo nayo
haikuwa hoja yenye mashiko na kwamba waombaji walitakiwa kuwasiliana na
Msajili wa Mabaraza ya Ardhi.
Katika
shauri hilo, NHC iliongozwa na Wakili Kiongozi, Aloyce Sekule na
Ipilinga Panya na mawakili wake wengine waliojikita katika kujibu hoja
zilizokuwa zikitolewa na wateja wao.
HABARI ZA JUMAMOSI NZURI YA LEO 07/01/2017
Reviewed by RICH VOICE
on
Januari 07, 2017
Rating:
Hakuna maoni