HABARI ZA JUMATAU YA TAREHE 09/01/2017




 .

 ..

 .

WILFRIED ZAHA ATOKEA BENCHI NA KUISAIDIA IVORY COAST KUPATA USHINDI

Wilfried Zaha ametokea benchi na kuisaidia Ivory Coast, kupata ushindi kwa kuifunga Sweden magoli 2-1 katika mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na Kombe la Mataifa ya Afrika.

Baada ya kutoswa na makocha Roy Hodgson na Sam Allardyce, pamoja na Gareth Southgate, katika timu ya taifa ya Uingereza Zaha ameamua kuichezea nchi yake aliyozaliwa ya Ivory Coast.

Akicheza kwa mara ya kwanza na Ivory Coast mchezaji huyo wa kimataifa aliingia dimbani baada ya mapumziko Zaha, alitoa pande kwa Giovanni Sio aliyefunga goli la pili.
                                       Wilfried Zaha akielekea kupiga krosi iliyozaa goli la ushindi

 

Monday, January 9, 2017

Zitto Kabwe Amvaa JPM Kuzuia Mikutano ya Siasa.......Awataka Marais Wastaafu Waingilie Kati

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amewataka marais wastaafu kutokaa kimya, badala yake wajitokeze kumshauri rais Magufuli wanapoona mambo hayaendi sawa ili kunusuru nchi na uchumi.

Ameyasema hayo kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Isagehe, Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.

“Hii nchi inaongozwa kwa misingi ya kidemokrasia, nawaomba marais wastaafu wasikae kimya kuhusu kunusuru nchi, wamshauri rais kuhusu mambo mbalimbali likiwemo la vyama vya siasa kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara,”amesema Zitto.

Aidha, Zitto amemuomba rais Magufuli kufanya mabadiliko katika sekta ya madini kwa kuweka wazi mikataba ya wawekezaji na kwamba jambo hilo litasaidia wananchi kuwa na uelewa wa mikataba hiyo.

Hata hivyo, Zitto ameshangazwa kuona barabara inayounganisha migodi mitatu ya  dhahabu ya Buzwagi, Bulyanhulu na Geita Gold Mine kuwa barabara hiyo haina kiwango cha lami.
 
 

Monday, January 9, 2017

Video Mpya: Matonya – Hakijaeleweka

Msanii kutoka Tanga, Seif Shaaban maarufu kama Matonya  ametuletea video yake mpya wimbo unaitwa ‘Hakijaeleweka‘, humo ndani ameonekana mrembo Gigy Money, Video imeongozwa na Tone Blaze.

Monday, January 9, 2017

TPSF: Serikali Yatakiwa Kujipanga Katika Ujio Wa Viwanda

Mfuko wa Sekta Binafsi nchini (TPSF) umesema ujio wa viwanda 200 kutoka nchini China,Serikali inatakiwa kujipanga kupokea viwanda hivyo kwani vitachangia kukua kwa uchumi pamoja na ajira nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye amesema China kwa sasa ni nchi yenye mitaji mikubwa kuliko nyingine duniani hivyo lazima kuongeza mahusiano zaidi ili kuweza kunemeeka  nao katika kuelekea uchumi wa kati wa viwanda kufikia 2025.

Simbeye amesema viwanda vingi vya China vimefikia hatua ya kuweza kuhamishwa katika sehemu mbalimbali katika Bara la Afrika na kuendelea na uzalishaji kutokana na uhakika wa rasilimali watu pamoja na malighafi.

Amesema  kutokana na uwekezaji wa viwanda hivyo suala la maeneo tengefu  liangaliwe kimkakati   katika kufanya maandalizi  ya viwanda hivyo pamoja na vingine vitakavyojengwa.Simbeye amesema nchi ya China ina uwezo mkubwa wa mitaji kuliko maeneo mengine duniani na Tanzania inaelekea katika uchumi wa viwanda  zilizowawezesha  kufanya mapinduzi ya viwanda.

Aidha amesema ujio wa Waziri wa Mambo ya Nchi wa China nchini  ni sehemu ya kuchangamkia fursa kwa karibu kwa kuongeza uhusiano uzidi kudumu ambao wenye maendeleo baina ya nchi mbili.
 

Monday, January 9, 2017

Picha: Rais Magufuli awasalimia wakazi wa Chato Mjini......Pia atembelea Shule ya Msingi aliyosoma Chato



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika benchi la kibanda cha kupigia kiwi (Shoe Shine) pamoja na wakazi wengine wa Chato katika eneo maarufu kama Stendi za zamani Chato mkoani Geita. Kibanda hicho cha Kiwi ndicho Rais Dkt. Magufuli alichokuwa akisafishiwa viatu  vyake kabla ya kuwa Rais, pia ni sehemu ambayo alikuwa akipenda kukaa na  kubadilishana mawazo na wakazi wa Chato wakati akiwa mapumzikoni kipindi cha Nyuma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Chato mkoani Geita. Shule hiyo ya Msingi Chato ndiyo Rais Dkt. Magufuli alisoma kuanzia darasa la kwanza mpaka Darasa la Saba. Rais Dkt. Magufuli amewaasa Wanafunzi hao kusoma kwa bidii kwasababu yeye pia alisoma shuleni hapo. Picha na Mpigapicha Maalum
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Chato mkoani Geita. Shule hiyo ya Msingi Chato ndiyo Rais Dkt. Magufuli alisoma kuanzia darasa la kwanza mpaka Darasa la Saba. Rais Dkt. Magufuli amewaasa Wanafunzi hao kusoma kwa bidii kwasababu yeye pia alisoma shuleni hapo. Picha na Mpigapicha Maalum.


Monday, January 9, 2017

Rais magufuli atoa ahadi kujenga vyumba Vitatu vya madarasa Shule Ya Msingi Chato Ambako Alisoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 9 Januari, 2017 amefanya ziara ya kushtukiza katika Shule ya Msingi Chato,ambapo ndipo aliposoma kuanzia darasa la kwanza hadi la saba na kuzungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo.

Rais Dkt Magufuli ameahidi kujenga madarasa matatu na ofisi moja ya walimu katika Shule hiyo kufuatia ombi la Walimu kuwa shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi wanaosoma shuleni hapo.

Aidha Dkt.Magufuli amewaasa wanafunzi kutilia mkazo masomo ili waweze kufaulu na kuwataka walimu kuhakikisha wanatumia vyema fedha zinazotolewa na Serikali kila mwezi katika kutoa elimu bila malipo na pasiwe na wanafunzi hewa kama ilivyo kwa baadhi ya shule ambazo zimegundulika kuwa na wanafunzi hewa katika uhakiki uliofanywa na serikali.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chato, Bwana Mwita Chacha amemshukuru Rais Dkt.Magufuli kwa msaada aliowapatia katika kukabiliana na uhaba wa madarasa uliokuwa unaikumba shule hiyo, pia kuitembelea Shule yao jambo ambalo limewatia moyo walimu na wanafunzi shuleni hapo.

Rais Magufuli pia ametembelea eneo la Stand ya zamani na kuzungumza na baadhi ya wananchi waliokuwepo eneo hilo na kutoa msaada kwa kikundi cha wasafisha viatu ili kuongeza mtaji wa biashara yao.

Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato, Geita.
9 Januari, 2017

Waziri Mkuu Majaliwa Akutana Na Waziri Wa Mambo Ya Nje Wa China

Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China,   Wang Yi   (kulia kwake) kwenye makazi yake, Oysterbay jijini Dar es salaam Januri 19, 2017.  Kushoto kwake ni Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,  Augustine Mahiga na wanne kulia ni Balozi wa China nchini, Lu Youqing. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
******* WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania itaendeleza ushirikiano na Serikali ya China katika nyanja mbalimbali kupitia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, nishati na miundombinu.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Januari 9, 2017) alipokutana na  Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mheshimiwa Wang Yi, kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema ushirikiano wa Tanzania na China ni wa kihistoria, hivyo ameihakikishia Serikali ya China kwamba utaendelezwa kwa manufaa ya wananchi wa Mataifa yote mawili.

Aidha, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini China kuja kuwekeza  katika sekta mbalimbali nchini zikiwemo za miundombinu, viwanda, kilimo na nishati.

 “Tanzania iko tayari kupokea kampuni zaidi za China kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali nchini.Tupo tayari kupokea viwanda kati ya 200 hadi 700 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo,” amesema.

Kwa upande wake Mheshimiwa Wang Yi amepongeza utendaji kazi wa Mheshimiwa Rais Dk. Magufuli pamoja na viongozi wengine hususan katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi na tayari matunda yameanza kuoneka.

“Serikali ya China kwa sasa iko katitka mkakati wa kuhamishia viwanda vyake vingi Barani Afrika. Iliamua kuichagua Tanzania kuwa moja katika ya nchi watakayohamishia viwanda hivyo kutokana na kuridhishwa na dhamira inayoonyeshwa na Serikali katika kuleta maendeleo,” amesema.

 IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
 

Waziri Mkuu Aagiza Maafisa Wanne Wakamatwe .........Ni kwa tuhuma za uzembe na upotevu korosho zaidi ya tani 2,000

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Zuberi Mwombeji awakamate maafisa wanne na kuhakikisha wanapelekwa Masasi chini ya ulinzi ili wajibu tuhuma za upotevu wa tani 2, 138 za korosho.

Maafisa hao ni Kaimu Meneja Mkuu Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi (MAMCU), Bw. Kelvin Rajab na Meneja Tawi wa MAMCU, Bw. Lawrence Njozi. Wengine ni wakurugenzi wa kampuni ya YURAP ya Masasi inayohusika na uhifadhi wa mazao kwenye maghala, Bw. Yusuph Namkukula na Bw. Ramadhani Namakweto.

Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo kwenye kikao alichokiitisha Songea mjini Jumamosi, Januari 7, 2017 baina ya watendaji kutoka Bodi ya Korosho Tanzania, MAMCU, wamiliki wa ghala la BUCO - Masasi na kikundi cha wakulima sita waliowawakilisha wenzao kutoka vyama vya msingi (AMCOS) za wilaya za Mtwara na Masasi.

Katika kikao hicho, Waziri Mkuu alitaka apatiwe maelezo ya kina ni wapi zilipo hizo tani 2,138 za korosho wakati taarifa waliyompatia viongozi hao jana inaonyesha kuwa waliuza korosho zote na hakuna hata kilo moja ambayo haijanunuliwa katika mnada wa tano uliofanyika Novemba 10, mwaka jana.

Kaimu Meneja Mkuu wa MAMCU, Bw. Kelvin Rajab alikiri mbele ya Waziri Mkuu kwamba korosho zote ziliuzwa na zilishalipwa na wanunuzi wa mnada wa tano lakini akadai hakupewa taarifa ya kukosekana kwa kiasi hicho cha korosho. Naye mmiliki wa ghala la BUCO, Bw.  Ramadhan Namakweto alikiri kupokelewa kwa korosho hizo ghalani kwake lakini akashindwa kutoa maelezo ni kwa nini hazionekani zilipo.

“Tangu mnada wa tano, mmekwishafanya minada mingine mitano hadi kufikia mnada wa 10. Kama kweli hizo korosho zipo ghalani, ni kwa nini korosho za hawa wakulima hazijatolewa ghalani na kuuzwa katika minada iliyofuata huku taarifa yenu ya fedha kuwa mlishazipokea na kuziuza?” alihoji Waziri Mkuu bila kupata majibu ya kueleweka.

Tuhuma zinazowakabili maafisa hao wanne ni kuwalipa kilo pungufu ya zile zilizowasilishwa ghalani, wakulima wa korosho katika wilaya ya Masasi na kutowapa maelezo yoyote juu ya upungufu huo. Mfano ni kufanya makato ya unyaufu kwa wakulima wa chama cha msingi CHAMALI kinyume na maagizo ya Serikali.

Nyingine ni kutowalipa fedha kwa wakati wakulima waliouza korosho kwenye mnada wa tano wa tarehe 10 Novemba 2016 na kutokutoa maelezo yoyote licha ya kuwa MAMCU ilishauza korosho hizo kwenye minada iliyofuatia na kupokea malipo.

Nyingine ni kutopelekwa mnadani kwa makusudi kwa tani 2,138 za korosho zilizokuwa katika maghala ya Mtandi na BUCO tangu Novemba 11, mwka jana; kutokutolewa taarifa ya kuwepo korosho hizo kwa mamlaka husika na kuwasababishia hasara wananchi.

Tuhuma nyingine ni kushindwa kufuatilia malipo ya korosho ya tani 1,156,262 ambazo ziliuzwa kwenye mnada wa 10 uliofanyika Desemba 21, 2016. Korosho hizo zilinunuliwa na Maviga East Africa (tani 503,297); Machinga Transport (tani 104,200); Tastey (319,576) na Saweya Impex (tani (229,189).

Kutokana na mapungufu hayo, Waziri Mkuu aliagiza watu hao wapelekwe Masasi chini ya ulinzi ili uchunguzi ufanyike na pia amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa hesabu za MAMCU na kujiridhisha kiasi cha korosho kilichonunuliwa; fedha zilizolipwa na kuingia akaunti za MAMCU; kiasi cha fedha zilizolipwa kwa vyama vya msingi na wananchi kwa ulinganifu na bei ya korosho kwa kila mnada husika.

Mapema, wakisoma risala yao kwa Waziri Mkuu, wakulima hao walisema wana kero nyingi sana kama vile kutolipwa fedha zao kwa wakati; kutoeleweka mahali zilipo korosho ambazo walishaziuza kwa MAMCU, kukatwa makato ya unyaufu ambayo Serikali ilikwishapiga marufuku na kutosikilizwa malalamiko yao na viongozi wa MAMCU pamoja na viongozi wa mkoa na wilaya.

“Makubaliano yalikuwa ni kwamba mkulima atapewa fedha yake siku sita baada ya mnada kufanyika lakini hivi sasa baadhi yetu tumeuza korosho tangu Oktoba, mwaka jana lakini hadi imefika Januari hii bado hatujalipwa. Pia kuna makato yaliyoondolewa kwenye mfumo, kwa mfano unyaufu lakini wao wameyaacha na unapoenda kuuza wanahesabu na kukukata kuwa utalipia gharama za unyaufu,” alisema msoma risala Bw. Sylvester Mtimbe ambaye pia ni mkulima kutoka AMCOS ya Chiungutwa.

Wakulima hao wa korosho kutoka Masasi mkoani Mtwara walikutana Januari 3, 2017 katika kijiji cha Chiungutwa na kuazimia kuwa wangeandamana hadi Dar es Salaam ili wawasilishe kilio chao kwa Waziri Mkuu au kwa Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli.

Kwa kutambua umbali uliopo kutoka Masasi hadi Dar es Salaam na kwamba yeye hakuwepo katika siku waliyopanga kwenda huko, Waziri Mkuu aliamua kuwaita wakulima hao wamfuate Songea ambako alikuwa na ziara ya kikazi ya siku nne.

Lowassa, Maalim Seif Watema Cheche Zanzibar

Katibu  Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad,  amesema kukaa kwake kimya kuna kishindo kikubwa kinakuja visiwani Zanzibar.

Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo, alisema kamwe hatorudi nyuma, kwani hajashindwa na wala haitotokea kushindwa katika maisha yake.

Kauli hiyo aliitoa jana mjini Unguja, alipokuwa akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani, ambapo pamoja na mambo mengine alisema umaskini sasa umekuwa ukiwatesa wananchi katika kila eneo.

Katika uchaguzi huo CUF inawakilishwa na mgombea wake Abdulrazak Khatib Ramadhan ambaye anapambana vikali na mgombea wa CCM, Juma Ali Juma.

Maalim Seif ni kama alikuwa akijibu mapigo ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdurhamn Kinana ambaye mwishoni mwa wiki alisema kuwa kiongozi huyo anazungumza hali ya kuwa hajui lolote kinachoendelea katika nchi wala katika chama chake.

“Sasa nawaambieni musinione kimya, kimya kikuu kina mshindo mkubwa wala usidhani kuwa tumeshaachia hapana bado kabisa tunaendelea kupigania haki yenu na haki Inshallah haipo mbali na mimi niwaambieni vijana sijashindwa na sitoshindwa.

“…na kama itatokea bahati mbaya nishindwe nitawataarifuni mchukue uamuzi wenu lakini sitegemei kufika huko kwani mambo haya yana miiko yake,’’ alisema Maalim Seif.

Akizungumzia hali ya umaskini nchini alisema tangu uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, ulipoingia madarakani kwa kile alichodai kwa kutumia mabavu hali ya umaskini imeendelea kuwatesa wananchi.

Alisema hali hiyo inachangiwa na uongozi kufanya mambo yasiyokuwa na tija ambapo kwa kushirikiana na kiongozi mstaafu wa Serikali iliyopita walifanya mapinduzi na kubatilisha matokeo ya  uchaguzi yaliyofanywa na Wazanzibari waliyoyafanya Oktoba 25, mwaka 2015.

“Lakini  kilichotokea mwaka juzi sasa Serikali imekuwa ya dhulma wale wenye ajira wanapokonywaa ajira zao  ikiwemo kuwaondosha wafanyabiashara darajani, Kijangwani na sasa wanakwenda Michenzani jambo ambalo ni hatari kwa Taifa hili,’’ alisema Maalim Seif.

Katibu Mkuu huyo wa CUF ambaye alikuwa mgombea urais katika uchaguzi uliopita, alisema pamoja na hali hiyo lakini bado suala la mafuta na gesi limekuwa na upungufu hasa kupitia sheria yake ambapo sasa kunaifanya Zanzibar kuwa kama manispaa.

Naye aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliyeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) Edward Lowassa,  alimpongeza Maalim Seif kwa kumwalika na jinsi alivyokuwa mvumilivu katika mambo yote wanayomfanyia.

Alisema Maalim Seif alimshinda aliyekuwa mgombea urais wa CCM, Rais Dk. Ali Mohamed Shein  kwa wastani wa kura 16,000.

Kutokana na hilo aliwashukuru vijana waliosikia wito wake wa kutofanya vurugu baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo kwani kama wangefanya hivyo kulikuwa na hatari ya kupoteza maisha.

Akizungumzia suala la njaa  alisema ni ajabu kwa Rais aliyepo madarakani kubeza suala hilo.

Lowassa alisema kuwa wakati wa utawala wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, hasa pale nchi ilipokubwa na baa la njaa, alisema yupo tayari kuzungumza na makaburu  ili kuweza kukabiliana na baa hilo lililoikumba nchi kwa wakati huo.

Alisema ni lazima kuhakikisha katika uchaguzi mbalimbali kunakuwa na ushindi na kila mmoja akatae azuie wizi wa kura kama uliotokea 2015.

“Lazima kukataa kuibiwa kura ni lazima kukataa kutiwa hofu na kutishwa hii ni nchi yetu sote tufuate sheria na uchaguzi ujao ni lazima kushinda na viongozi wanaopambana ni lazima kuungwa mkono kama ilivyokuwa kwa Maalim Seif ni mfano wa kuigwa,’’ alisema Lowassa.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar,  Nassor  Mazrui alisema wanaingia katika uchaguzi huo bila kuwa na ruzuku lakini hadi sasa tayari Sh milioni 20.4 zimepatikana kutoka kwa wanachama wenyewe.

Aliyashukuru majimbo yaliyochanga ikiwa ni pamoja na Nungwi, Makunduchi, Mtoni, Magomeni, Kikwajuni, Konde, Chambani, Chakechake, Chonga, Bububu na Ole.

Naye Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Zanzibar,  alisema wataendesha kampeni kistaarabu tofauti na wa upande wa pili ambao ni CCM wanaorusha maneno badala kueleza sera.

Alitoa ratiba za kampeni hiyo ambapo Januari 11 atakuwepo Mbunge wa Singida Tundu Lisu na Januari 15 Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro atakuwa mgeni rasmi.
 

Anglicana Kwafukuta.......Chimeledya Amtimua Askofu Mokiwa, Lakini Kagoma Kutoka

Mashitaka  10 yaliyofunguliwa na walei 32 wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam yakiwemo ya ufisadi wa mali za kanisa, yamesababisha Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dk Jacob Chimeledya kumvua uaskofu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam Dk Valentine Mokiwa.

Hata hivyo Dk Mokiwa amegomea uamuzi huo kwa maelezokuwa mwajiri wake ni Sinodi ya Dar es Saalam ambayo ndiyo yenye uamuzi wa kumfuta kazi na sio askofu mkuu au askofu mwingine yeyote wa kanisa la Anglikana Tanzania.

Uamuzi wa kumvua uskofu ulichukuliwa juzi na Askofu Chimeledya baada ya Askofu Mokiwa kugoma kujiuzulu kama ilivyoshauriwa na nyumba ya maaskofu ambayo ilimkuta na hatia ya kufuja mali za kanisa hilo na kukiuka maadili ya kichungaji ambayo yalibainishwa kwenye ripoti ya uchunguzi iliyoundwa na kiongozi mkuu wa kanisa hilo nchini.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kanisa hilo zilieleza kuwa katika kikao kilichofanyika juzi kanisani Ilala, askofu Chimeledya na ujumbe wake walihudhuria kikao cha halmashauri ya kudumu ya dayosisi ya Dar es Salaam akatangaza uamuzi wa kumvua uaskofu Dk Mokiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Licha ya uamuzi wa kumvua uaskofu, Dk Chimeledya pia aliagiza waraka unaoagiza askofu huyo kuondolewa madarakani, usambazwe kwenye makanisa yote yaliyoko chini ya dayosisi ya Dar es Salaam na usomwe jana kwenye ibada mbele ya waumini.

“Ni kweli kikao hicho kilifanyika jana, Dk Chimeledya alikuja na katibu mkuu na msajili wa kanisa kwenye kikao, lakini tulishangaa kwamba walikuja na askari polisi kinyume na utaratibu wa kanisa, alisoma maamuzi hayo aliyodai yametolewa na nyumba ya maaskofu,”alisema msemaji wa Dayosisi ya Dar es Salaam Yohana Sanga.

Dk Mokiwa agoma kung’oka
Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam Padri Jonathan Senyagwa jana alisema habari hizo sio za kweli na barua ambazo zimesomwa katika baadhi ya makanisa jijini Dar es Salaam zilisomwa kwa makosa.

“Mwenye mamlaka ya kumfukuza kazi ni yule aliyemwajiri, na mwajiri wa Dk Mokiwa ni Sinodi ya Dar es Salaam...tutatoa tamko hivi karibuni kuthibitisha kwamba askofu wa jimbo bado hajafukuzwa,” alisema Padri Senyagwa.

Alisema waraka ambao umesambazwa na askofu mkuu wa Tanzania haujapitia kwenye halmashauri ya kudumu ya dayosisi ili kupata baraka zake na wala hauna baraka kutoka kwa sinodi ya dayosisi jambo ambalo linaufanya waraka huo ukose sifa za kutekelezeka.

“Ninachokwambia ni kwamba askofu wa dayosisi ya Dar es Salaam bado ni Mokiwa, hatuzitambui barua zilizosomwa katika baadhi ya makanisa,” alisisitiza katibu mkuu huyo wa Dayosisi.

Mgomo huo pia ulithibitishwa na Sanga, ambaye alifafanua kuwa juzi kulifanyika kikao kati ya viongozi wakuu wa kanisa na halmashauri ya kudumu ya dayosisi ya Dar es Salaam na kuelezwa na askofu mkuu wa Tanzania Dk Chimeledya hatua ya kumvua uaskofu Dk Mokiwa jambo ambalo halmashauri iligoma.

“Tulifanyia kikao chetu pale kanisa la Ilala, viongozi wetu wakuu walikuja na polisi wakatusomea huo waraka na kutangaza maamuzi hayo mbele ya halmashauri, lakini maamuzi hayo yaligomewa na wajumbe wa halmashauri ya Dayosisi ya Dar es Salaam,” alisema Sanga.

Alisema halmashauri iligoma kubariki uamuzi huo kwa sababu kanisa la Anglikana Tanzania lina kanuni na taratibu zake. 

Alifafanua kuwa waraka wa kumwondoa madarakani Dk Mokiwa lazima upate baraka za halmashauri ya kudumu ya dayosisi na sinodi ya dayosisi.

“Ule waraka tuliupitia na kubaini kuwa hauna baraza za nyumba ya maakofu, wala hauna baraka za halmashauri ya kudumu na Sinodi ya dayosisi ndio maana tuliwakatalia,” alisema Sanga na kuongeza kuwa maamuzi ya kumvua uaskofu Dk Mokiwa yamefanywa na askofu mkuu wa Tanzania, katibu mkuu na msajili wa kanisa na sio vikao vya kanisa.

“Ninachosisitiza hapa ni kwamba askofu wa dayosisi ya Dar es Salaam bado ni Dk Mokiwa, huo waraka uliotangazwa ni ushawishi wa watu wachache wanaotaka kumchafua kiongozi wetu wa Dayosisi,” alisema.

Aombwa ajiuzulu uaskofu 
Awali tume hiyo iliyoundwa kuchunguza tuhuma dhidi yake, baada ya kubaini makosa mengi yaliyofanywa na askofu huyo ilimshauri ajiuzulu wadhifa wake na awe tayari kufanya huduma nyingine ya kumtumikia Mungu.

“Hatua tunayoichukua ni kwa nia njema kabisa ya kulinusu kanisa letu ambalo limekuwa naheshima kubwa hapa nchini na duniani kote,” unasema waraka uliosaniwa na Dk Chimeledya.

Tume hiyo ilichukua uamuzi huo katika kutatua mgogoro uliopo ndani ya dayosisi ya Dar es Salaam:

“Nia yetu ni njema kabisa na hatuna chuki, uhasama wala upendeleo katika jambo hili, ifahamike kuwa vyombo vyote ndani ya kanisa ikiwemo nyumba ya maaskofu vinalifahamu jambo hili vyema, hivyo tulitarajia tutaungwa mkono ili kuisaidia dayosisi yetu ya Dar es Salaam kwenda mbele.”

Pia waraka huo unaeleza kuwa hiyo sio mara ya kwanza kanisa hilo kufanya maamuzi ya namna hiyo na kutoa mfano kuwa hata enzi za askofu Mokiwa akiwa askofu mkuu wa Tanzania alichukua hatua za kulinusuru kanisa lisipotee katika migogoro mbalimbali ikiwemo mgogoro wa dayosisi ya Tanga ambako alimtaka askofu wa dayosisi hiyo ajiuzulu kwa hiyari na alikubali.

Baada ya kutenguliwa uaskofu wa Mokiwa, Dayosisi ya Dar es Salaam itakuwa chini ya uangalizi wa uongozi wa askofu mkuu mpaka taratibu nyingine za kikanuni zitakapokamilika.

“Nina wasii Wakristo wote kwa nieaba ya Bwana Yesu Kristo tuendelee kuwa watulivu katika kuijenga dayosisi yetu na kanisa la Mungu kwa ujumla.”

Mashitaka 10 ya Mokiwa 
Askofu Mokiwa Machi 2015 alifunguliwa mashitaka 10 ambayo ni kuizuia dayosisi ya Dar es Salaam kupeleka michango pasipo maelekezo ya sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam, kuhamasisha dayosisi kujitoa katika udhamini wa kanisa Anglikana Tanzania (KAT) kwa lengo la kuifarakanisha dayosisi na jimbo kinyume na katiba ya dayosisi.

Mashitaka mengine ni kufuja mali za kanisa na kuingia mikataba kiholela yenye viashiria vya rushwa katika eneo la kanisa la mtoni Buza na miradi mingine, kushindwa kutatua migogoro inayohusu uwekezaji na maadili baina ya dayosisi na mitaa ya Magomeni ambao kuna mgogoro na Benki ya DCB, kanisa la Kurasini na mengine.

Askofu huyo pia anadaiwa kushindwa kutatua migogoro baina ya mapadiri na waumini na kutunza mali za kanisa katika mtaa wa Watakatifu wote Temeke na kutelekeza nyumba ya askofu iliyopo Oysterbay ambako imegeuzwa kuwa yadi ya kuuza magari.

Pia alilalamikiwa kushitakiwa mahakamani na Marehemu Christopher Mtikila na watu wengine watatu kwa kosa la kuwatishia silaha ya moto na kuwapapasa maungoni mwao bila ridhaa yao kinyume na maadili ya kikanisa.

Askofu Mokiwa pia analalamikiwa kuanzisha taasisi ya MEA Foundation iliyomwezesha kupokea fedha nyingi za wafadhili kwa ajili ya maendeleo ya dayosisi, lakini fedha zimefujwa na hesabu za chombo hazikuwahi kukaguliwa.

Tuhuma zingine ni kurejea kwa mchakato wa mapitio ya katiba mpya na kuvuruga mchakato wa awali wa maandalizi ya katiba mpya ya dayosisi kwa kutumia fedha za dayosisi na kutekelezwa askofu msaidizi dayososi ya Katanga Kalemi .

 

Rais Shein Awajibu wanaofikiri ataondolewa madarakani na UN

Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein amewataka wananchi wa Zanzibar kufanya kazi na kutodanganyika kuwa ataondolewa madarakani na mtu yeyote.

Akizungumza jana visiwani humo mbele ya wananchi, Dk. Shein alieleza kuwa hakuna mtu au taasisi yoyote itakayotawala Zanzibar wakati yeye bado yuko madarakani.

“Hakuna atakayeweza kuingilia masuala ya Zanzibar, hakuna atakeyongoza Serikali hii wakati mimi bado ni ko madarakani. Msidanganywe,” alisema Dk. Shein.

“Hakuna cha Umoja wa Mataifa wala Katibu Mkuu gani atakayekuja kuiongoza Serikali hii wakati mimi niko madarakani,” alisisitiza.

Rais Shein ameyasema hayo wakati ambapo Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amekuwa katika harakati anazoziita kuishtaki Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Umoja wa Mataifa akidai kupokonywa ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

CUF inashiriki uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Dimani, ikiwa ni miezi takribani tisa tangu chama hicho kisusie uchaguzi wa marudio uliofanyika mwaka jana baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25 akieleza kuwa ulikubwa na kasoro nyingi.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatatu ya January 9

 
HABARI ZA JUMATAU YA TAREHE 09/01/2017 HABARI ZA JUMATAU YA TAREHE 09/01/2017 Reviewed by RICH VOICE on Januari 09, 2017 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...