habari za leo jumatanoooo.

Wednesday, October 26, 2016


Baba aua mwanawe kisa kufungua redio kwa Sauti Kubwa


SeeBait
BABA mmoja mkazi wa Kijiji cha Maji ya Moto, Wilaya ya Arumeru mkoani hapa, Wilfred Kivuyo amemuua mtoto wake baada ya kumchoma kisu tumboni, kwa kosa la kufungulia redio kwa sauti ya juu.

Kabla ya tukio hilo inadaiwa yalitokea mabishano ya kugombea kupunguza sauti ya redio kati ya baba na mtoto, ambapo baba aliamua kumchoma kisu tumboni mtoto wake na utumbo kutoka nje.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema, tukio hilo lilitokea Oktoba 23, mwaka huu saa tatu usiku katika Kijiji cha Maji Moto na kumtaja marehemu kuwa ni Abraham Wilfred (22), ambaye kabla ya mauti alikuwa nyumbani akiendelea na shughuli zake huku akiwa amefungulia redio.

Alisema siku ya tukio mtuhumiwa huyo alifika nyumbani akiwa amelewa na kumkuta mtoto wake amefungulia redio kwa sauti ya juu, ambapo alimtaka kupunguza sauti hiyo lakini mtoto huyo aligoma.

“Baada ya hapo mabishano na kutoelewana kulijitokeza baina yao wakaanza kupigana, baba alipozidiwa nguvu na mtoto wake alichomoa kisu cha kukunja kwenye mfuko wa suruali kisha akamchoma tumboni na kumsababisha utumbo kutoka nje.

“Mara baada ya tukio hilo mtoto huyo alichukuliwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu, lakini hata hivyo alifariki wakati madaktari wakiendelea kuokoa maisha yake,” alisema Kamanda Mkumbo.

Kamanda Mkumbo alisema Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka mtuhumiwa huyo ambaye baada ya tukio alikimbia ili hatua zaidi za kisheria zisichukuliwe dhidi yake


Wednesday, October 26, 2016


Wachina wawili mbaroni kwa kosa la utekaji nyara, Polisi latoa tahadhari kwa wananchi


SeeBait

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata raia wawili wa China kwa makosa ya utekaji nyara mfanyakazi wa kasino ya Le Grande iliyopo maeneo ya Upanga, ambaye pia ni mchina aliyefahamika kwa jina la Liu Hong (48).

Kamishna wa Kanda hiyo, Kamanda Simon Sirro leo amewaambia waandishi wa habari kuwa, wachina hao walimteka Hong na kumfanyia vitendo vya ukatili ambapo walitoa masharti ya kupatiwa dola za kimarekani 19,000 ili wamuache huru.

Kamanda Sirro amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Wang Young Jing (37) na Chen Chung Bao (35).Amesema watuhumiwa hao baada ya kufanyiwa upekuzi katika chumba walichomficha Hong walikuta bomba la sindano, kamba za plastiki ambavyo vinasadikika kutumika kumjeruhi raia huyo wa china.

Amesema baada ya askari polisi kufanikiwa kumuokoa Hong walimpeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu.

Aidha, Kamanda Sirro ametoa taadhari kwa wakazi wa Dar es Salaam kuwa makini na raia wa kigeni waishio nchini kwa kuwa baadhi yao hushughulika na uhalifu ikiwemo utekaji nyara.

Amewataka wananchi kutoa taarifa pindi watakapobaini kuwa kuna raia wa kigeni wanaonyanyasa wazawa na kufanya vitendo vya kihalifu.

Wednesday, October 26, 2016

Kesi ya uchaguzi meya Kinondoni yapata hakimu

SeeBait

Kesi ya  kupinga uchaguzi wa Umeya na Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni iliyofunguliwa na Chadema katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepangwa  mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage na imepewa namba 304 ya 2016.

Katika kesi hiyo Chadema kupitia wakili wake, John Malya wanaiomba  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itengue uchaguzi huo.

Pia wanaomba mahakama iamuru uchaguzi huo uitishwe upya na walipe gharama za kesi.

Walalamikaji katika kesi hiyo ni Mustafa Abdul Muro na Jumanne Mbunju dhidi ya Benjamin Sitta, Manyama Mangaru, Mwenyekiti wa Uchaguzi wa Kinondoni, Msimamizi wa mkutano  huo na Meya na Naibu Meya wa Kinondoni.

Mwanasheria wa chama hicho, John Malya alisema wamefika mahakamani hapo ili kueleza walichokifanya si sahihi na kwamba wamekwenda mahakamani hapo kwa ajili ya kutafuta haki.

Wednesday, October 26, 2016

Mawaziri Uganda Na Tanzania Watembelea Eneo Litakapojengwa Gati Itakayotumika Kupakia Mafuta Kutoka Uganda Kwenye Meli

SeeBait



Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Mhandisi Irene Muloni wametembelea eneo la Chongoleani mkoani Tanga ambako kutajengwa hifadhi ya mafuta pamoja na gati itakayotumika kupakia mafuta kwenye Meli mbalimbali ili kusafirishwa.

Mafuta hayo yatapakiwa kwenye Meli hizo baada ya kusafirishwa na Bomba kutoka Hoima nchini Uganda kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi.

Akiwa katika eneo hilo Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda aliwaeleza wananchi wa eneo hilo kuwa nchi ya Uganda inaishukuru Tanzania kwa kukubali Bomba hilo lipite katika ardhi ya Tanzania suala ambalo litakuwa na faida mbalimbali kwa Wananchi ikiwemo mabadiliko ya kiuchumi.

Alisema kuwa lengo ni kuona kuwa mradi huwa huo unaanza kazi mwaka 2020 na ndiyo maagizo ambayo Marais wa nchi mbili wameyatoa kwa watendaji wanaosimamia Mradi huo wa Bomba la Mafuta.

Mhandisi Muloni alitumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kujiandaa kikamilifu kwa fursa za kiuchumi kwani watekelezaji wa mradi watahitaji huduma mbalimbali kama za chakula, malazi na usafiri hivyo kupitia utoaji wa huduma hizo wananchi nao watapata kipato.

Pia alizishukuru Sekta Binafsi za Uganda na Tanzania kwa kuwa tayari kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha kuwa mradi huo unafanikiwa akitolea mfano kampuni ya GBP ya Tanzania ambayo imeonesha nia ya kununua hisa katika kampuni itakayoanzishwa kwa ajili ya usimamizi wa Bomba hilo la Mafuta.

Pia alizishukuru kampuni za TULLOW ya Uingereza, CNOOC ya China na TOTAL ya Ufaransa kwa kuamua kutekeleza mradi huo ambao utawezesha jumla ya mapipa laki mbili ya mafuta kusafirishwa kwa siku kupitia Bomba hilo la Mafuta lenye urefu wa kilomita 1443.

Kwa upande Profesa Muhongo alisema kuwa Bomba hilo pia litatumika kusafirisha mafuta kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya nchi hiyo kugundua mafuta.

Alisema kuwa Waziri kutoka DRC anayesimamia Nishati hiyo amefika nchini ili kufanya mazungumzo na Tanzania juu ya kutekeleza suala hilo ambapo inakadiriwa kuwa nchi hiyo itakuwa ikisafirisha mapipa 30,000 hadi 100,000 kwa siku kupitia Bomba hilo la Mafuta.

Alisema kuwa Gati hiyo ya Chongoleani ina uwezo wa kupakua mafuta kwa muda wa mwaka mzima kutokana na kutokumbwa na mawimbi makubwa ya bahari ambayo hupeleka shughuli hiyo kusuasua.

“ Ndugu zangu shughuli ya upakiaji wa mafuta katika Bandari hii itafanyika kwa muda wa mwaka mzima kwani Bandari hii haina mawimbi makubwa yatakayozuia shughuli hii kufanyika, na ndiyo moja ya vigezo vilivyotumika katika kuchagua Bandari hii kupokea mafuta kutoka Uganda,”alisemaProfesa Muhongo.

Kwa upande wa Wananchi, baadhi ya Wananchi hao walisema kuwa wamepokea mradi huo kwa matumaini makubwa ambapo wamesema kuwa wana imani kuwa mara mradi utakapoanza wataweza kupata huduma mbalimbali ikiwemo Elimu, Afya, Miundombinu ya barabara n.k.

Naye Profesa Muhongo aliwaasa wananchi hao kuwa na subira wakati Serikali ikiwa inafanya mipango mbalimbali ili kuhakikisha kuwa mradi huo unafanyika kwa ufanisi.

Wednesday, October 26, 2016

Waraka wa Lowassa: Uchambuzi wa Serikali ya Magufuli mwaka mmoja baada ya Uchaguzi

SeeBait
Tarehe Kama ya leo mwaka Jana, ilikuwa siku muhimu sana kwa watanzania na Mimi binafsi.Niliwaongoza watanzania kupiga kura nikiwa mgombea wa upinzani.

Naamini nilileta sura na msisimko mpya katika siasa za Tanzania.Nilishirikiana na wenzangu kuionesha nchi yetu Demokrasia maana yake ni nini.

Napogeuka nyuma kuingalia siku ile, nasikia faraja kubwa sana hasa kwa jinsi watanzania walivyotuunga mkono na kuonyesha matumaini makubwa kwetu.Ujasiri na ushapavu wa hali ya juu aliyouonesha Mke wangu Regina wakati wa kampeni,ulinipa nguvu kubwa.

Chini ya Mwenyekiti wetu Freeman Mbowe,tuliendesha kampeni za kiungwana kama tulivyoahidi.Upepo ule ulivuma kwa kasi mpaka visiwani ambako Maalim Seif aliporwa dhahiri ushindi.

Kwa mujibu wa Tume isiyo huru ya uchaguzi, tulishindwa uchaguzi ule.Hatutaki kuendelea kuyalilia maziwa yaliyokwisha mwagika ambayo hayazoleki, lakini kile ambacho tulikisema wakati ule kwanini tunataka mabadiliko,hivi sasa kila mtu anakiona.

Pamoja na mafanikio machache katika baadhi ya maeneo lakini maisha yamezidi kuwa magumu, ajira imeendelea kuwa bomu linalosubiri kulipuka,Elimu bure iliyoahidiwa siyo inayotekelezwa,utumishi wa umma umekuwa kaa la moto,.Nasononeka sana nikiona viongozi wanavyoshindana kuwasweka ndani madiwani na viongozi wengine wa kuchaguliwa hasa wa UKAWA.

Nawashukuru sana wananchi kwa imani kubwa waliyoionesha kwangu na UKAWA kwa ujumla.Kumalizika kwa uchaguzi ndiyo mwanzo wa uchaguzi mwengine, kwahiyo mapambano ndiyo kwanza yameanza.Kasi,nguvu, ari na hamasa niliyonayo ni kubwa zaidi kuliko wakati mwengine wowote.

Wednesday, October 26, 2016

Wazanzibari 40,000 Wafungua kesi Mahakamani Kuupinga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

SeeBait
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeingia kwenye jaribio jingine, baada ya Wazanzibari 40,000 kufungua kesi mahakamani kupinga uhalali wake. 

Kesi hiyo ilifunguliwa jana katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) na Rashid Salum Adiy kwa niaba ya wenzake 39,999, katika Masijala ndogo ya mahakama hiyo iliyoko jijini Dar es Salaam. 

Wadaiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Adiy anasema kuwa msingi wa kesi hiyo ni kwamba Muungano huo haukuanzishwa kisheria. 

“Sisi tunadai Muungano huu hauko kwa misingi ya kisheria na kutokana na ushahidi tulionao, uko kisiasa tu na jambo hili linahitaji mfumo na mwenendo wa kisheria kwa kuwa wenye mamlaka ya nchi ni wananchi,” alisema Adiy. 

Alisema kutokana na nyaraka walizonazo wanapinga hati ya Muungano inayodaiwa ilisainiwa Aprili 22, 1964 na wanapinga uamuzi wa Baraza la Mapinduzi kuridhia Muungano huo. 

Wanapinga barua ya Mei 6, 1964, iliyopelekwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), kuelezea kutambuliwa kwa Muungano huo. 

Pia, wanapinga uhalali wa barua ya Novemba 2, 1964 iliyopelekwa UN ikielezea matumizi ya jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria iliyopitishwa na Bunge Desemba 10, 1964 ikielezea matumizi ya jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Adiy na wenzake wanadai kwa kuwa Muungano ni wa kisiasa, ndiyo maana hauwezi kuleta manufaa kwa pande zote mbili hususani uwiano wa kiuchumi na kielimu. 

Baada ya kuwasilisha nyaraka zao wanasubiri kesi hiyo isajiliwe kwa kupewa namba katika Mahakama hiyo na kupangiwa taratibu za usikilizwaji wake. 

Mbali na Wazanzibari 40,000, pia alisema wanayo majina mengine ambayo watayawasilisha mahakamani baadaye, kesi itakapokuwa imeanza

Wednesday, October 26, 2016

Asilimia 90 ya Wanafunzi kupata Fedha zao za Mikopo Kesho

SeeBait

Wakati baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu wakiendelea kusubiri kupata mikopo yao, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia kesho, asilimia 90 ya wanufaika watakuwa wameshapata fedha zao. 
Majaliwa alisema hayo jana wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). 
“Taarifa niliyonayo ambayo nimepata asubuhi hii (jana), wachache sana wameanza kulipwa jana (juzi), lakini ulipaji utaendelea mpaka keshokutwa (kesho), tunatarajia kufikia asilimia 90 ya wanaostahili kulipwa watakuwa wameshalipwa,” alisema. 
Majaliwa ambaye ni mhitimu wa UDSM, aliwataka waombaji wa mikopo washirikiane na Wizara ya Elimu kwa kutoa taarifa sahihi ili kurahisisha ulipaji.
“Serikali haitavumilia tena ucheleweshwaji wa makusudi  wa malipo ya fedha za mikopo ya chuo. Kama kuna tatizo, taarifa zitolewe haraka ili kuzuia migogoro kati ya wanafunzi na Serikali yao,” alisema.
Alisema upungufu wa wahadhiri waandamizi umesababishwa na masharti ya ajira za mkataba, unaowataka kuwa miaka 65 na maprofesa kuwa miaka 70.
“Hii inaathiri hali ya utoaji wa taaluma kwa fani za ‘Post-Graduates’. Serikali itaendelea kuweka kipaumbele cha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo,” alisema Majaliwa. 
Alisema licha ya juhudi hizo za Serikali, vyuo pia vinatakiwa kuwa na utaratibu wa kurithishana kazi ili kusiwe na pengo katika utoaji wa taaluma pale baadhi ya wahadhiri wanapostaafu.

Majaliwa ambaye pia alizindua kitabu kilichopewa jina la ‘From Lumumba Street to The Upper Hill and Beyond’, alisema Serikali itatoa ushirikiano katika utekelezaji wa mipango ya chuo hicho. 
Akizungumzia kuhusu masilahi  ya watumishi wa vyuo vikuu, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuondoa malimbikizo ya madai kwa watumishi wote wa umma na sasa inakamilisha uhakiki wa taarifa za kiutumishi ili kubaini watumishi hewa.
 “Serikali inaendelea na maboresho na kuimarisha masilahi kwa watumishi wote wa umma kupitia bodi ya mishahara na mara tutakapokamilisha, tutapanga upya mishahara na motisha kwa watumishi,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Dk Leonard Akwilapo alisema wizara hiyo imetenga Sh9 bilioni kwa ajili ya kufanya ukarabati wa miundombinu kwenye chuo hicho zikiwamo maabara. 
Awali, katika hotuba yake, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala aliishukuru Serikali kwa kuanza kufanyia kazi baadhi ya changamoto zanazokikabili chuo hicho ikiwamo upungufu wa hosteli za wanafunzi. 

Wednesday, October 26, 2016

Umeya Kinondoni: CHADEMA Wafungua Kesi Mahakamani, Wadai Uchaguzi Haukuwa Halali

SeeBait

Viongozi  wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wamekimbilia mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi wa umeya na naibu meya wa Manispaa ya Kinondoni katika Jiji la Dar es Salaam uliompa ushindi Diwani wa Msasani, Benjamin Sitta wa CCM kuwa Meya.

Ukawa kupitia kwa Wakili wao, John Mallya wamewasilisha kesi hiyo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 23 mwaka huu, kwa kuwa ulikuwa batili na ulikiuka taratibu za kisheria.

Mallya alisema kesi hiyo ambayo walalamikaji ni aliyekuwa Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Jumanne Mbunju na aliyekuwa mgombea wa umeya, Diwani wa Kata ya Kinondoni, Mustafa Muro, imepokelewa lakini haijafunguliwa.
 
Mbali na Sitta, walalamikiwa wengine katika kesi hiyo ni Naibu Meya, Manyama Mangaru, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli na Ofisa Tawala wa Halmashauri hiyo.

Akizungumza baada ya kesi hiyo kupokelewa, Wakili Mallya alisema wamefungua kesi hiyo kupinga kile wanachoita uchaguzi ambao CCM walikaa wenyewe na kupigiana kura.

Alisema: “Katika kesi hiyo tunaiomba Mahakama itengue uamuzi uliomchagua meya huyo, iamuru manispaa iitishe uchaguzi wa umeya mara moja pia imuamuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa na wasimamizi wa uchaguzi wafuate taratibu za kisheria.”

Katibu wa Chadema mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kileo alisema wamefika mahakamani kutafuta haki kwa sababu wanaamini wamenyang’anywa haki yao.

Alisema kilichosababisha uchaguzi wa Ubungo kuahirishwa ni kukiukwa kwa taratibu hivyo Mkurugenzi na Ofisa Tawala wa Ubungo walipoona taratibu zimekiukwa Kinondoni, waliamua kuahirisha uchaguzi.

“Kilichofanyika siku ile ilikuwa ni kuchagua Mwenyekiti wa CCM, lakini siyo uchaguzi wa kumchagua meya wa Kinondoni kwa sababu hata kisheria, uchaguzi unatakiwa kuwa robo tatu ya wajumbe ambao walitakiwa kuwa 23, lakini walikuwa 18, ndiyo maana hata matokeo yalikuwa kura 18,” alisema.

Alidai madiwani wao walinyimwa fursa ya kuingia manispaa na kuwasilisha malalamiko yao hivyo hawamtambui Meya wa Kinondoni na kwa sasa hakuna Meya wa Manispaa hiyo.

Wednesday, October 26, 2016

Rais Magufuli Ateuliwa kuwania tuzo ya Forbes kwa watu maarufu barani Afrika

SeeBait

Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameingia katika listi ya watu ambao wametajwa kuwania tuzo ya Person Of The Year 2016 ambayo hutolewa na Jarida la Forbes Africa.

Rais Magufuli ameingia katika kinyang’anyio hicho, akiwania tuzo hiyo pamoja na Mwanzilishi wa Capitec Bank, Michiel le Roux, Thuli Madonsela, Ameenah Gurib na watu wa Rwanda.

Kama Rais Magufuli atafanikiwa kushinda tuzo hiyo, basi Tanzania itakuwa imepata tuzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo kwani mwaka jana 2015, mshindi wa tuzo hiyo alikuwa Mkurugenzi Mtendaji na Rais wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group), Mohammed Dewji.

Utaratibu wa jinsi ya kupiga kura kwa mwaka huu ni kutumia tovuti ya http://poy2016.com/ ambapo baada ya kuingia hapo, unaweza kugusa jina la mtu ambaye unapendekeza ashinde tuzo na hapo kura itakuwa imehesabiwa.


Wednesday, October 26, 2016

Tanzania Yapata Mkopo Wenye Masharti Nafuu Wa Zaidi Ya Shilingi Bilioni 300 Kutoka Benki Ya Maendeleo Ya Afrika (Afdb) Na Serikali Ya Korea

SeeBait

Benny Mwaipaja, WFM, Seoul, Korea
TANZANIA, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Korea ya Kusini zimetiliana saini makubaliano ya pamoja kutekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya umeme gridi ya Kaskazini Magharibi inayoanzia mkoani Mbeya, Nyakanazi hadi Kigoma, yenye msongo wa kV 400 mbapo Serikali ya Korea imeahidi kutoa Dola za Marekani milioni 50 sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 100.18, kwa ajili ya kugharamia mradi huo.
 
Hali kadhalika, Tanzania na Benki ya Exim ya Korea, zimesaini  Mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za marekani milioni 90.092 sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 194 za Tanzania, kwa ajili ya mradi wa Upanuzi wa Miundombinu ya mfumo wa maji taka Jijini Dar es salaam.
 
Kwa upande wa Tanzania, Makubaliano pamoja na Mkataba vimesainiwa na Mhe. Dkt. Philip Mpango (MB) Waziri wa Fedha na Mipango kwa niaba ya Serikali, Oktoba 25, 2016 Jijini Seoul nchini Korea Kusini huku upande wa AfDB, aliye saini ni Rais wa Benki hiyo Adesina Akinwumi, na kwa upande wa Benki ya Exim, mkataba huo umesainiwa na Mwenyekiti ambaye pia ni Rais wa Benki hiyo Lee Duk-Hoon.
 
Akizungumza mara baada ya kutia saini makubaliano na mkataba huo, Dkt. Mpango amesema makubaliano na mkataba vilivyosainiwa vina manufaa makubwa kwa wananchi wa Tanzania.
 
“Wananchi wa Upande ule waanze kufurahia kwamba maendeleo yanakuja na hasa tunaposema maendeleo ya viwanda ambavyo ni lazima vitumie umeme, na kwamba mradi huu unatarajia kupelekwa hadi Mbeya” Amesisitiza Dkt. Mpango.
 
Dkt. Mpango, amesema kuwa mradi huo una umuhimu mkubwa pia kwa kuwa serikali imedhamiria kuufungua ukanda wa Magharibi mwa Tanzania, kwa upande wa viwanda vya aina mbalimbali.
 
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Uwekezaji) wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini Tanzania-TANESCO, Decklan Mhaiki, amesema mradi wa umeme wa Nyakanazi hadi Kigoma utakuwa na urefu wa kilometa 280 na utakapo kamilika utaondoa changamoto ya shirika hilo kuzalisha umeme unatumika katika ukanda huo wa Magharibi hususan Kigoma, kwa kutumia majenereta ambayo uendeshaji wake ni ghali na umeme wake si wa uhakika.
 
“Kuleta laini kama hii, kwanza itapunguza gharama kubwa, na umeme wa ziada utakao zalishwa tunaweza kuuza nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, upande wa pili wa Ziwa Tanganyika, lakini kikubwa ni kuwahakikishia wananchi wa mkoa wa Kigoma kuwa na umeme wa uhakika” ameongeza Bw. Mhaiki.
 
Akizungumzia mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya maji taka Jijini Dar es salaam, Dkt. Philip Mpango, amebainisha kuwa mradi huo unatarajia kuwa na tija kwakuwa utatatua changamoto ya majitaka kutuama mitaani hasa wakati wa mvua na kusababisha magonjwa ya mlipuko kikiwemo kipindupindu.
 
Akifafanua kuhusu mradi huo, Mchumi ambaye pia ni  Afisa anayeshughulika na utafutaji wa Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Melckzedek Mbise, amesema kuwa mradi wa maji wa Ruvu  unatarajia kuongeza wingi wa maji Jijini Dar es salaam, utakaosababisha uzalishaji wa maji taka pia kuongezeka, hivyo mradi huo wa kuondoa maji taka umekuja  wakati muafaka.
 
“Mradi huu umekuja wakati muhimu na mkopo una masharti nafuu sana” Amesisitiza Bw. Mbise.
 
Naye Afisa Mkuu wa utafutaji rasilimali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Sabra Issa Machano, amesema kuwa  kati ya nchi 54 za Kiafrika zinazohudhuria mkutano wa Tano wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na Afrika, Mjini Seoul Korea, ni nchi nne tu zilizopewa mkopo na ufadhili ambazo ni Kenya, Uganda na Ethiopia, huku Tanzania ikipewa kiasi kikubwa zaidi cha fedha jambo linaloonesha kuwa Tanzania inakubalika Kimataifa.

Wednesday, October 26, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano ya Octoba 26

SeeBait


habari za leo jumatanoooo. habari za leo jumatanoooo. Reviewed by RICH VOICE on Oktoba 26, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...