habari za leooo

Monday, October 10, 2016

Mahakama Kuu Yatoa Kibali Kwa CUF Kufungua Kesi Dhidi ya Msajili wa Vyama na Lipumba ....... Bodi Ya Wadhami wa Chama Hicho Yatoa Onyo Kali Kwa Mabenki Hapa Nchini

Wakati taariza zinazomtuhumu Profesa Ibrahim Lipumba kufungua akaunti benki kwa lengo la kuingiziwa fedha za ruzuku ya Chama cha Wananchi (CUF) kinyume cha sheria kwa ajili ya kukivuruga chama hicho zikienea.
Bodi ya Wadhamini ya CUF imetoa onyo pamoja na kuwatahadharisha watu wanaotumika kusaini nyaraka feki kwa lengo la kufungua akaunti hizo, pia imezitahadharisha benki zote nchini kutofungua akaunti yoyote kwa jina la CUF pasipo kupata muhtasari wa bodi halali ya chama hicho.

Katika hatua nyengine, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julias Mtatiro amefafanua kuwa wenye mamkaka halali ya kufungua akaunti ya chama hicho ni Bodi yake ya wadhamini pamoja na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamadi.

“Tunatoa onyo, kwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, kwamba tumeshafungua shauri na utaratibu wa kisheria umeshaanza kuchukua mkondo wake, tumesikitika kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, kinyume cha sheria namba tano 1992 ya vyama vya siasa na kinyume cha katiba, Msajili kwa mara ya kwanza anaziandikia benki zilizosajiliwa na BOT akizitaka kumfungulia akaunti Lipumba za kuwekea fedha,” amesema Mtatiro.

Mtatiro amedai kuwa ”Benki itakayomfungulia akaunti Lipumba ni makosa makubwa. Sababu huwezi fungua akaunti ya taasisi au chama bila ya bodi yake ya wadhamini kukaa kikao na kuandaa muhtasari kwa ajili ya kupeleka benki ili kufungua akaunti.Lipumba na watu wake wameandaa nyaraka feki pamoja na barua ya msajili kutaka kufungua akaunti. Tunajua amepeleka katika benki mbalimbali,

“NMB ilikataa sasa wanapeleka benki ya Exim na ilishapewa taarifa kuwa uhuni huu haukubaliki na masuala ya fedha yako chini ya katibu mkuu kwa mujibu wa katiba ya cuf,” amesema.

Sambamba na onyo lililotolewa na bodi hiyo, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam leo imekubali maombi yake ya kufungua shauri la kuitaka mahakama hiyo kutoa amri dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi ya kutoendesha shughuli zake za usimamizi wa vyama vya siasa kinyume cha sheria, pamoja na kutengua barua yake inayomtambua profesa Ibrahim Lipumba kama mwenyekiti halali wa chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasilisha maombi hayo, Wakili Juma Nassoro amesema kuwa Jaji wa mahakama hiyo Munisi, amekubali maombi yao na kwamba jopo la mawakili wa CUF linatarajia kuwasilisha maombi rasmi wiki hii.

“Jaji Munisi baada ya kutusikiliza vifungu vya sheria tulivyotumia, Mahakama imekubali ombi letu ili tuweze kufungua maombi ya kuomba mahakama itamke kufuta barua ya msajili inayomtambua Lipumba kama mwenyekiti halali wa CUF. Pia Itoe zuio rasmi kwa msajili kutofanya shughuli zake nje ya utaratibu ambao amepewa chini ya sheria ya vyama vya siasa,” amesema Nassoro.

Amesema baada ya mahakama kuridhia maombi yao, iliwataka kuwasilisha maombi rasmi ndani ya siku14 kuanzia leo.

“Tumeambiwa tuwasilishe maombi ndani ya siku 14, lakini tutayawasilisha ndani ya siku Saba na tutaiomba mahakakama iyasikilize kwa Hati ya dharula ili shughuli za chama ziendelee,” amesema.
 
 

Monday, October 10, 2016

Rais Magufuli Apokea Hati Za Utambulisho Kutoka Kwa Mabalozi Wa Nchi Mbalimbali Ikulu Jijini Dar Es Salaam 10th Oktoba 2016

SeeBait

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 10 Oktoba, 2016 amepokea hati za utambulisho za mabalozi wanne wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho Ikulu Jijini Dar es Salaam ni Balozi wa Jamhuri ya Sudan hapa nchini Mhe. Mahjoub Ahmed Abd Allah Sharfi, Balozi wa Jamhuri ya Slovakia hapa nchini Mhe. Frantisek Dlhopolcek, Balozi wa Ukraine hapa nchini Mhe. Yevheni Tsymbaliuk na Balozi wa Jamhuri ya Ghana Mhe. Kwame Asamoah Tenkorang.

Rais Magufuli amezungumza na Mabalozi hao kwa nyakati tofauti baada ya kupokea hati zao za utambulisho, ambapo wamesisitiza umuhimu wa kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hizo kwa kujikita zaidi katika biashara na uwekezaji.

"Mhe. Balozi najua nchi yenu ya Sudan ina utajiri wa mafuta na imefanikiwa kujenga uchumi wake kupitia mafuta, sisi pia hapa nchini tumebaini uwepo wa mafuta na gesi asilia katika baadhi ya maeneo, ningependa uhusiano na ushirikiano wetu sasa ujielekeza katika kubadilishana uzoefu na ujuzi wa namna tunavyoweza kunufaika na mafuta na gesi"  amesema Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na Balozi wa Sudani hapa nchini Mhe. Mahjoub Ahmed Abd Allah Sharfi.

Dkt. Magufuli pia ametoa wito kwa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi za Sudan, Slovakia, Ukraine na Ghana kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo Mafuta na gesi, Kilimo, Uvuvi, Mbuga za wanyama, Madini na ufugaji.

"Hivi sasa Tanzania ipo katika mpango wa ujenzi wa viwanda na pia tunatekeleza mpango wa pili wa maendeleo, hivyo nakuomba Mhe. Balozi uwahamasishe wafanyabiashara na wawekezaji wa Ukraine waje wawekeze katika viwanda kwani soko la uhakika la bidhaa lipo" amesisitiza Dkt. Magufuli alipokuwa akizungumza na Balozi wa Ukraine hapa nchini Mhe. Yevheni Tsymbaliuk.

Aidha, Rais Magufuli amewasihi Mabalozi wa Slovakia, Ukraine na Ghana ambao makazi yao ya Ubalozi yapo Mjini Nairobi nchini Kenya kuanzisha Ubalozi wao hapa nchini ili kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano katika masuala ya biashara na uwekezaji.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Oktoba, 2016.
 
 

Monday, October 10, 2016

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Yatupiwa Lawama Kwa Kuchelewa Kutoa Majina ya Wanufaika wa Mikopo

SeeBait
Wakati vyuo vikuu vikikaribia kufunguliwa, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imelaumiwa kwa kuchelewa kutoa majina ya wanufaika huku yenyewe ikisema itahakikisha majina yanatolewa sanjali na tarehe za vyuo kufunguliwa. 

Pia, HESLB imesema miongoni mwa vipaumbele vitakavyozingatiwa kwenye utoaji wa mikopo katika mwaka wa masomo 2016/2017 ni kwa wanafunzi wenye mahitaji makubwa, waliotoka kwenye kaya masikini, waliosoma shule za kata na waliotoka vijijini. 

Kauli hiyo imekuja baada ya bodi hiyo kutupiwa lawama kwa kuchelewa kutoa majina ya wanufaika wa mikopo kabla hawajaripoti vyuoni, hasa wanafunzi wa mwaka wa kwanza.

Mkurugenzi wa mtandao wa haki za wanafunzi (TSNP), Shitindi Venance alisema hadi sasa wanafunzi wanaojiunga na masomo ya elimu ya juu nchini kwa mwaka wa kwanza wa masomo 2016/2017, ambao wameomba mkopo bado hawajui ni kiasi gani wamepewa. 

Malalamiko ya Shitindi yamerejea kilichotokea mwaka jana baada ya wanafunzi kuripoti vyuoni, lakini majina yalipotolewa na bodi hiyo baadhi yao hawakuwa wanu- faika hali iliyosababisha usumbufu. 

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema miongozo ya utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka huu ni tofauti na mwaka jana. 

“Utaratibu wa mwaka huu ni tofauti kwa kuzingatia wanafunzi wanaoanza masomo na wale wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali,” alisema Badru. 

Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa majina ya wanufaika wa mikopo yataanza kutolewa kwa kuzingatia tarehe ambayo chuo husika kinafunguliwa.

 “Kila chuo kinafunguliwa kwa mujibu wa tarehe iliyopangwa kwa hiyo na sisi tunatoa majina kuendana na utaratibu wa chuo husika,” alisema. 

Hata hivyo, Badru alisema uta- ratibu wa kupanga viwango vya mikopo kwa wanafunzi na kisha kutoa orodha ya majina ya wanufaika haihusishi bodi ya mikopo peke yake. 

Alisema kabla ya kuidhinisha majina ya wanufaika na mikopo, lazima Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) iwe imeshatoa orodha ya majina wa wanafunzi ambao imewadahili kwa kuzingatia vigezo vyao, halafu majina hayo yatumwe vyuoni. 

Alisema mzunguko wote huo unahitaji muda na umakini wa hali ya juu ndiyo maana huchukua muda. 
 

Monday, October 10, 2016

Lipumba Afungua Akaunti Mpya ya Ruzuku CUF.......Benki ya NMB Yalaumiwa kwa Kuvujisha Siri

SeeBait
Siri kwamba Profesa Ibrahim Lipumba amefungua akaunti mpya yenye jina la chama cha Wananchi CUF imefichuka. Wanaolaumiwa kutokana na kufichuka kwa siri hiyo ni watumishi wa benki ya NMB tawi la Ilala.

Prof. Lipumba ni Mwenyekiti wa CUF, anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa huku chama chake kikiwa tayari kimemfukuza uanachama.

Abdul Kambaya, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma anayetambulika na Msajili wa Vyama Vya Siasa pia huku Baraza Kuu la Uongozi la CUF likiwa limemsimamisha uanachama, amenukuliwa na gazeti la Tanzania Daima, akilaani kitendo cha benki ya NMB kuvujisha taarifa za akaunti mpya ya Prof. Lipumba.

“Aulizwe Meneja wa NMB Ilala, kutoa siri za wateja, hayo ndiyo maadili ya kazi yake? Uko wapi usiri kati ya mteja na benki?” alihoji Kambaya.

Hata hivyo, alipotafutwa Kambaya  ili kufafanua uanzishwaji wa akaunti hiyo, matumizi yake na kama yamezingatia matakwa ya Katiba ya CUF na Sheria ya Vyama Vya Siasa, hakuwa tayari kufafanua akidai kuwa si wakati muafaka.

“Tutaeleza mambo hayo kwa wakati muafaka, kama kuna jambo tunakuwa accused (tunatuhumiwa), iulizeni ofisi ya msajili au benki husika, wao wana taarifa kamili,” alisema.

Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa kupitia Sisty Nyahoza imenukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari ikikiri kumtambulisha Prof. Lipumba kwa benki ya NMB ili aweze kufungua akaunti hiyo, hata hivyo amedai kuwa ofisi ya msajili haijui matumizi ya akaunti hiyo.

Taarifa za kufunguliwa kwa akaunti mpya yenye jina la CUF kwa malengo yanayodaiwa ni kuchukua ruzuku za chama hicho zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii Alhamis ya tarehe 06 Septemba mwaka huu.

Uongozi wa CUF taifa kupitia kwa Mbarara Maharagande, Naibu Mkurugezi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma umesema kuwa, utatoa taarifa rasmi juu ya suala hilo  leo Jumatatu, tarehe 10 Oktoba.
 
 

Monday, October 10, 2016

Spika wa Bunge Job Ndugai afumua Kamati ya Bunge na Kuisuka Upya

SeeBait
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amefanya mabadiliko makubwa kwenye Kamati ya Bunge ya masuala ya Ukimwi, akiwabadilisha wabunge ishirini na wanne waliokuwa wanaunda kamati hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Ofisi ya Bunge, Ndugai ameteua wajumbe wapya kumi na sita wa kamati hiyo ambao pia watakuwa wajumbe wa kamati nyingine.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Spika ametumia Mamlaka aliyonayo kikatiba kuunda Kamati za Bunge kadri anavyoona inafaa, na kwamba mabadiliko haya yamelenga katika kuboresha utekelezaji wa majukumu ya kibunge.

“Kanuni ya 116 (3) –(5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari 2016 inampa Spika mamlaka ya kuteua wajumbe ili wawe wajumbe katika kamati mbalimbali za Bunge ikiwa ni pamoja na mamlaka ya kuongeza, kubadilisha au hata kupunguza idadi ya wabunge katika kamati za kudumu za Bunge,” imeeleza taarifa hiyo.

Mabadiliko hayo yameanza mara moja kuanzia mwezi huu wa Oktoba na kwamba wajumbe wote wameshatumiwa barua tayari kwa maandalizi ya kukutana na kuwachagua viongozi wa kamati hiyo.

Hii ni orodha ya waliokuwa wajumbe wa kamati hiyo na kamati walizohamishiwa kufuatia mabadiliko hayo:

Monday, October 10, 2016

Mkutano wa ACT- Wazalendo Watoa Maazimio Mazito Dar

Chama cha ACT- Wazalendo kimemuomba Rais John Magufuli kuunda timu ya wataalamu kupitia upya rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba na kuitisha mkutano mkuu wa kikatiba ili kuipitisha. 
Chama hicho kilisema mchakato wa kura za maoni uanze upya ili kupata Katiba Mpya. 

Hayo ni miongoni mwa maazimio matatu yaliyotolewa na chama hicho kwenye mkutano wa siku moja wa kidemokrasia.

Akisoma maazimio hayo, Ofisa Habari wa chama hicho, Abdallah Khamis alisema, “chama kimeazimia mchakato wa kuandika Katiba Mpya uanze kwa kufanya marekebisho ya sheria ya kura ya maoni na Sheria ya mchakato wa Katiba.” 

Alisema, iwapo Serikali itaamua kwenda na Katiba Inayopendekezwa iliyopo sasa chama hicho kitaipinga kwa kufanya kampeni ya hapana kwenye kura ya maoni. 

Alisema wakati mchakato wa Katiba ukiwa umesimama, Baraza la Wawakilishi Zanzibar limepitisha sheria ya kutafuta mafuta na gesi kinyume na matakwa ya Katiba ya Muungano ambayo inatambua mafuta na gesi kuwa ni masuala ya muungano. 

“Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia umeshauri kuwa chama kimwelekeze mbunge wake kuwasilisha bungeni hoja binafsi ya kufanya mabadiliko, kwa kuondoa mafuta na gesi kama jambo la muungano ili kuiwezesha Zanzibar kutafuta mafuta na gesi asilia bila vikwazo,” alisema. 

Khamis alisema chama hicho kimeazimia kufanya maadhimisho ya miaka 50 ya Azimio la Arusha Februari, 2017. 

“Katika maadhimisho hayo chama kifanye mkutano mkuu wa Kidemokrasia jijini Arusha na kutanguliwa na Halmashauri Kuu ya chama kwenye ukumbi uleule ambao Tanu ilifanya na kuzaa Azimio la Arusha mwaka 1967,” alisema. 

Ofisa huyo alisema katika maadhimisho hayo chama kimeshauriwa kuwa wataalamu wa ndani na nje waalikwe kujadili mafanikio na changamoto za Azimio la Arusha katika miaka 25 iliyopita. 
Pia, wataalamu watajadili madhara ya kutelekezwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1992 huko Zanzibar.
 
 
habari za leooo habari za leooo Reviewed by RICH VOICE on Oktoba 10, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...