HABARI ZA ALHAMISI HII
Thursday, October 27, 2016
TFS Yanasa Lori Likisafirisha Mbao Kinyume cha Sheria
______________________
Kikosi cha Kufuatilia na Kuzuia Uharibifu wa Misitu cha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwa kushirikiana na Kikosi Dhidi ya Ujangili kanda ya Dar es Salaam kimefanikiwa kukamata lori lenye namba za usajili T 676 ANQ lililokuwa likisafirisha mbao kinyume cha sheria huku zikiwa zimefichwa kwa kufunikwa na bidhaa mbalimbali ikiwemo sabuni ili zisionekane kiurahisi kwenye vituo vya ukaguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo, Kaimu Afisa Habari wa Wakala huyo, Nurdin Chamuya alisema tukio hilo limetokea tarehe 14 Oktoba, 2016 majira ya saa kumi usiku maeneo ya Amana, Ilala Jijini Dar es Salaam baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema juu ya uwepo lori hilo katika maeneo hayo.
Chamuya alisema baada ya kupata taarifa hizo vikosi hivyo vilifika eneo la tukio na kufanya mahojiano na baadhi ya wananchi waliokuwa karibu na lori hilo ambapo mmoja kati ya wahudumu wa lori hilo alieleza kuwa lori hilo lilitokea Mkoani Kigoma na kwamba lilikuwa limepakia mzigo wa sabuni na chupa za maji zilizotumika. Dereva wa lori hilo hakuweza kupatikana.
“Wahudumu hao walipotakiwa kufungua mlango wa lori hilo kwa ajili ya upekuzi zaidi walisita kwa madai kuwa hawakuwa na funguo za lori hilo, Hatimaye waliwasiliana na mmlikiwa wa eneo ambaye alikuwa amekabidhiwa funguo kwa ajili ya ulinzi” alisema Chamuya.
Alieleza kuwa mmiliki huyo alipofika alisema, anamfahamu mwenye gari ambaye ndiye mpangaji wa eneo lilipokutwa gari na kwamba anazo taarifa za gari hilo, na ameombwa apokee mzigo na kuutunza hadi atakaporudi kutoka safari ya Mwanza kwa tatizo la msiba wa Baba yake.
Baada ya mmiliki wa eneo hilo kufanya mawasiliano na mwenye gari kuhusu mzigo uliokuwa kwenye gari hilo, mwenye gari alieleza kuwa kwa taarifa za dereva wake na ajenti aliyepakia mzigo Kigoma, gari lake lilikuwa na chupa chakavu na sabuni kutoka Kigoma na hakuna aina nyingine ya mzigo kwa ufahamu wake na akaruhusu gari hilo kufunguliwa mbele ya mwenye eneo.
“Baada ya gari hilo kufunguliwa, kilichoonekana kwa urahisi ni sabuni na mifuko michache inayosomeka kwa nje kuwa ni dawa ya kuku. Baada ya upekuzi ndipo zilionekana mbao zilizokuwa zimefichwa chini ya katoni za sabuni. Tumeshikilia Lori hilo kwa hatua zaidi za kisheria.
“Kufuatia tukio hili, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania tunatoa onyo kali kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo vya uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu kinyume cha sheria ya misitu namba 14 ya mwaka 2002 pamoja na kanuni zake za mwaka 2004 na kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria za nchi” alisema Chamuya.
Akizungumzia athari mbalimbali za vitendo hivyo vya uvunaji holela wa mazao ya misitu bila ya kufuata taratibu za kisheria za uvunaji endelevu alisema vitendo hivyo vinatishia nchi kuwa jangwa ambapo takwimu zinaonyesha jumla ya hekta 372,000 za misitu nchini hupotea kila mwaka kutokana na matumizi makubwa ya rasilimali hizo ambayo yanazidi uzalishaji wake kwa ujazo wa mita 19.5 milioni kwa mwaka.
Chamuya ametoa wito kwa wananchi wote nchini kushirikiana na Serikali katika uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za misitu na kuacha fikra potofu kuwa kazi hiyo ni ya Serikali pekee na taasisi zake kwakuwa faida zake hunufaisha jamii yote na vivyo hivyo kama athari zitajitokeza basi zitaikumba jamii yote bila kubagua.
Thursday, October 27, 2016
Serikali Yatangaza Matokeo ya Mtihani Darasa la 7......Bofya hapa Kuyaona
Serikali
imetangaza matokeo ya mtihani wa darasa la 7 kwa mwaka 2016
ambapo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 2.52 na shule iliyoongoza
kitaifa ni shule ya Msingi Kwema ya mkoani Shinyanga
AU
Thursday, October 27, 2016
Sakata la posho za madiwani Arusha laibukia bungeni
Sakata
la posho za madiwani wa Jiji la Arusha bado halijapoa, baada ya Mbunge
wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini kuliibulia katika Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), akisema linakwamisha ukusanyaji wa
mapato.
Sakata
hilo liliibuka jana wakati kamati hiyo ilipokuwa ikipitia na kuhoji
hesabu za halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Mbunge
huyo alisema halmashauri hiyo imekata posho kwa madiwani na watendaji
na kuzipeleka fedha hizo kwa walimu, jambo ambalo linawavunja moyo
wawakilishi hao wa wananchi kutimiza majukumu yao.
“Madiwani
ndiyo wanawasaidia kuwahamasisha wananchi katika ukusanyaji wa mapato
na hao mnawavunja moyo. Mkurugenzi hamuwezi kufikia malengo kama mtakuwa
watendaji peke yenu,” alisema Selasini.
Alisema
halmashauri hiyo ikimaliza mvutano huo inaweza kuongeza mapato kutoka
Sh12 bilioni hadi Sh18 bilioni na kujiendesha bila kutegemea ruzuku.
Mbunge
huyo alisema katika halmashauri zote nchini hakuna diwani anayelipwa
posho ya Sh10,000, kwa nini madiwani wa jiji hilo pekee walipwe kiasi
hicho.
Akijibu
hoja hiyo, mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Athuman Kihamia alisema
hakuna diwani anayelipwa kiasi hicho cha fedha na kwamba, madiwani wote
wanalipwa posho ya Sh40,000 kwa mwezi na nauli Sh10,000 kulingana na
kanuni walizokubaliana mwaka 2003.
Alisema madiwani hao walikuwa na posho zipatazo tano ambazo ni nauli, kujikimu, vikao, madaraka na mawasiliano.
Pia, Kihamia alisema walikuwa wakilipwa Sh150,000 za mafuta kinyume na kanuni walizokubali kuzitumia za mwaka huo.
Pia, Kihamia alisema walikuwa wakilipwa Sh150,000 za mafuta kinyume na kanuni walizokubali kuzitumia za mwaka huo.
“Siwezi kurudia makosa kwa kulipa fedha zisizofuata kanuni na utaratibu, maana mtakuja kunihoji hapa kwa nini nimezilipa,” alisema.
Mbunge
wa Kwela (CCM), Ignas Malocha alimpongeza mkurugenzi huyo kwa kufuata
misingi na utaratibu wa kanuni na sheria katika uendeshaji wa jiji hilo.
Akizungumza nje ya kamati hiyo, Meya wa jiji hilo, Calist Lazaro alitaka liachwe lijiendeshe lenyewe bila kuingiliwa.
Thursday, October 27, 2016
Madudu Kibao Yaibuliwa Mradi wa NSSF Kigamboni
Shirika
la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limekiri kuwapo ubadhirifu kwenye
mkataba wa ubia na Kampuni ya Azimio Housing Estates iliyotakiwa
kuendeleza ekari 20,000 za ardhi Kigamboni na kuna hatari ya kupoteza Sh
bilioni 270.
NSSF
pia imekiri ubadhirifu katika utoaji mikopo kwenye Saccos mbalimbali
nchini ikiwamo ya Bumbuli, inayoonekana kukopeshwa zaidi ya Sh bilioni
mbili, bila kuwa na sifa huku kukiwa pia hakuna kumbukumbu ya mwaka
mzima kama walirudisha mkopo wa awali.
Mwenyekiti
wa Bodi ya NSSF, Profesa Samuel Wangwe alieleza jana mbele ya Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwamba Bodi yake ilipoingia
madarakani iligundua ubovu wa mkataba huo na kusitisha kutoa fedha na
sasa inaangalia namna ya kujitoa bila kupoteza fedha zilizowekezwa.
Alisema
uwekezaji huo ambao ardhi ya mwekezaji ilipaswa kuwa ekari 20,000,
hatua ya awali ulipaswa kuanza na ekari 300, lakini uchunguzi
uliofanyika hivi karibuni ulionesha kuwa kuna ekari 3,500 pekee hali
inayoonesha udanganyifu uliofanyika tangu awali.
Pia
mwekezaji huyo alidanganya uhalisia wa bei ya ardhi hiyo, kwani
alionesha kuwa thamani ya ekari ya moja ni Sh milioni 800 wakati
kiuhalisia, ardhi hiyo thamani yake ni Sh milioni 25 peke yake.
Mwenyekiti
wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka alisema imekuwa vigumu kwa Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuthibitisha uwepo wa viwanja
hivyo kwa kukosekana hatimiliki, umiliki wa ekari 19,700 za ardhi ambazo
ni sehemu ya mtaji wa Azimio Housing Estates kwa asilimia 20, hivyo
fedha za NSSF zinakuwa kwenye hatari ya kupotea.
Alisema
NSSF ambayo inamiliki hisa ndogo kuliko Azimio, imewekeza fedha nyingi,
zaidi ya dola milioni 129 za Marekani wakati mbia huyo aliwekeza dola
milioni 5.5.
Akijibu
hoja za Mwenyekiti huyo, Profesa Wangwe alisema mradi huo ulisimama
tangu Februari kutokana na mbia kukosa fedha na kwamba hakopesheki kwani
NSSF inamdai.
Mbunge
wa Msalala, Ezekiel Maige alisema mradi huo wa Kigamboni ni mchafu na
katika mazingira hayo ambayo Bodi pia imeshituka kuwa mchafu hivyo ni
vema NSSF ingejitoa kuliko kuendelea na mkataba mbovu.
“Ni
vema ukishagundua kuwa unachezea kitenesi kichafu ambacho kilianza
kuchezewa na watu ambao wameshaondolewa, usiendelee kucheza na mtu yule
yule ili asije kukuingiza katika matatizo makubwa zaidi,” alisema Maige.
Profesa
Wangwe alisema ni vigumu kujitoa haraka kwenye mkataba huo, kutokana na
fedha nyingi waliyowekeza ambayo iko hatarini kupotea na kwamba ardhi
yote ni ya mwekezaji huyo hivyo wanatafuta namna ya kurudisha fedha
waliyowekeza hata kama haitakuwa na faida.
Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aesh Hilaly alihoji kama mkataba unaruhusu mwekezaji huyo kukopa ili kuendeleza mradi huo.
Mkurugenzi
wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema mwekezaji huyo alitaka kukopa
NSSF ili aendeleze mradi huo ambao umesimama lakini hakopesheki kwa
kuwa anadaiwa.
Hata
hivyo, baadhi ya wabunge walihoji uhalali wa Saccos kukopeshwa mara
mbili kwa mwaka, huku zingine zikikosa mikopo na vigezo vilivyotukia
katika kutoa mikopo hiyo.
Kuhusu
Saccos ya Bumbuli, Kaboyoka alisema mbunge wake anafahamika, hivyo
inashangaza ipewe fedha hizo kwa mwaka mmoja na kuhoji sifa zilizotumika
kuzitoa wakati Saccoss zingine hazijapata.
Alisema
ni vema ufanyike ukaguzi maalumu kwenye Saccos hiyo kwani fedha hizo ni
mafao ya wafanyakazi ingawa pia inatia shaka katika utoaji, kwani awali
Saccos hiyo ilipewa zaidi ya Sh bilioni moja na kwamba hesabu
hazioneshi, kwamba fedha hizo zilirejeshwa, lakini ndani ya mwaka mmoja
ikapewa fedha zingine.
NSSF
ilitoa mikopo kwa Saccos tisa kwa kiasi kinachozidi asilimia 50 ya
thamani ya mali za Saccos husika, kinyume na sera ya Shirika ya
kukopesha na ziliomba kiasi ambacho hazikustahili.
Katika
ripoti ya CAG mbali na Bumbuli, Saccos zingine zilizopewa fedha nyingi
ni Korongo Amcos, UMMA, SBC, Hekima, Ukombozi, Uzinza, Harbour na Umoja.
Akijibu
hoja hizo, Profesa Wangwe alisema Saccos zilizopewa fedha zaidi ya mara
mbili kwa mwaka ikiwamo ya Bumbuli iliyopewa Sh bilioni 2.473 kwa mwaka
2014/15, wakati anaingia kwenye nafasi hiyo, aliliona hilo kama tatizo
hivyo kuagiza kufanyike ukaguzi maalumu.
Alisema
waliokuwa wanasimamia Saccos hizo walisimamiswa kazi tangu Bodi mpya
ilipoingia na kwamba walisitisha kutoa mikopo ya aina yoyote katika
Saccos zote nchini, hadi uongozi wa Shirika utakapoanzisha utaratibu
mpya.
“Watu
wote waliohusika na ubadhirifu wameshaondolewa ofisini, tulishituka
kuona namna fedha hizo zilivyotolewa, si zote zilizofika kwa wahusika,
zingine ziliishia kwenye mikono ya watu, tuliona ni vema ufanyike
ukaguzi maalumu,” alisema Profesa Wangwe.
Thursday, October 27, 2016
Mchungaji Rwakatare Kuwatoa Wafungwa Wengiine 43 gerezani kwa Kuwalipia Faini Zao
Mchungaji
Kiongozi wa Kanisa la Assemblies of God (Mlima wa Moto), Getrude
Rwakatare amesema ataendelea na mpango wake wa kuwanusuru wafungwa
wanaotumikia adhabu magerezani kwa kuwalipia faini ili warejee uraiani.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, alisema katika awamu ya pili
ameamua kuwalipia wafungwa 43 waliopo katika magereza ya Mkoa wa
Dodoma.
“Kampeni
hii ya kuwalipia faini kati ya Sh 50,000 hadi 200,000 wafungwa waliopo
magerezani imetupa moyo na Watanzania wengi wameguswa na hata
kutupongeza. Kutokana na hali hii kanisa letu sasa limefanya hivyo tena
na safari hii tunaelekea mkoani Dodoma,” alisema.
Mchungaji
Rwakatare alisema kesho watawatoa wafungwa hao mkoani Dodoma ambapo
vigezo walivyoangalia ni wanawake wanaonyonyesha, wagonjwa na wazee.
“Nasi tunatimiza maandiko ya Mungu katika kufanya hivi na kuunga mkono juhudi za Mwenyekiti wa Parole, Augustino Mrema,” alisema Mchungaji Rwakatare.
Alisema
kutokana na makosa mbalimbali ya faini waliohukumiwa nayo wafungwa
hayo, kanisa lao limetoa Sh milioni 6.8 kwa ajili ya kulipia faini hizo.
Awali
Rwakatare kupitia kanisa lake, aliwalipia wafungwa 78 katika magereza
matatu ya Keko, Segerea na Ukonga ya jijini Dar es Salaam na kuachiwa
huru baada ya kulipa faini ya Sh milioni 25 zilizochangwa na waumini wa
kanisa hilo.
Thursday, October 27, 2016
Maagizo 10 ya Makamba kwa uongozi wa mkoa wa Katavi baada ya kukamilisha ziara
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe January
Makamba ameendelea na ziara yake katika Mkoa wa Katavi kwa kutembelea
kijiji cha Kabege ambapo aliangalia mradi Mkubwa wa Umwagiliaji wa
Mwamkulu katika Manispaa ya Mpanda ambao kwasasa umesitisha kutoa huduma
zake kwa kukosekana kwa maji ya kutosha katika Mto Katuma.
Katika
kikao cha Majumuisho ya Ziara yake ya siku mbili katika Mkoa wa Katavi,
Waziri Makamba ameutaka uongozi wa Mkoa huo kudhibiti yafuatayo:
1. Ongezeko la watu na mifugo ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia uharibifu wa mazingira.
2.
Kusitisha uchepushaji kwa Mto Katuma ambapo taarifa ya Mkoa ilieleza
kuna jumla yamabanio 40 ambayo yanatumiwa na watu kuchepusha maji kwa
ajili ya manufaa yao binafsi.
3. Uchimbaji hatari wa Madini usiofuata taratibu
4. Kuhuisha sheria ndogo ndogo za mazingira katika ngazi mbalimbali za Serikali za mitaa
5. Kuanisha maeneo maalumu ambayo yatatangazwa katika Gazeti la Serikali kama mazingiranyeti ili kuyapa ulinzi zaidi
6. Kusimamia uondoshwaji wa wavamizi katika Vyanzo vya maji
7.
Kufanyika kwa sensa ya mifugo ili kujua Mkoa una mifugo kiasi gani na
kubuni namna boraya kuhumudimia mifugo hiyo bila kuathiri mazingira
8. Ameahidi kuaanda andiko maalumu la Mradi wa Ziwa Katuma
9.
Mmiliki wa Jema Sitalike Project kutafutwa popote alipo, leseni yake ya
madini isitishwe,apigwe faini na kurekebisha eneo alilokuwa akitumia
awali kwa shughuli za uchenjuaji wadhahabu.
10.
Waziri Makamba meagiza Watendaji kata na Vijiji kutotoa vibali vya
uchimbaji wa madini bila kufuata utaratimu wa Wizara ya Nishati na
Madini.
Aidha
Waziri Makamba amewasili Katika Mkoa wa Kigoma na kutembelea kiwanda
cha Nyanza Mines nakuwapongeza kwa kuzalisha chumvi kwa kutumia nishati
ya jua ambapo awali kiwanda hicho kilifungiwa Baraza la Taifa la Hifadhi
na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutokana na uharibifu wa Mazingira kwa
kutumia magogo mengi mwaka 2015. Kiwanda hicho kwa sasa kinazalisha
tani 20,000-25,000 ndani ya miezi mitatu.
Thursday, October 27, 2016
Kigogo wa Jeshi la Polisi Ashushwa cheo....Mwingine Atimuliwa
Mkuu wa jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu Jeshi la Polisi limemvua cheo mkuu wake wa kituo cha Himo (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Zuhura Suleiman kwa tuhuma za kukutwa na gari la wizi aina ya Toyota Rav4.
Pia, jeshi hilo limemfukuza kazi kwa fedheha (kwa kutolipwa haki zozote) ofisa wake mwingine wa cheo cha koplo, Federika Shirima ambaye naye anatuhumiwa kukutwa na magari mawili yaliyoibwa jijini Dar es Salaam.
Hatua ya jeshi hilo dhidi ya askari wake imekuja siku chache baada ya kufichuka kwa tuhuma hizo ambazo zilionekana kulipaka matope.
Alipohojiwa na wanahabari Jumatatu iliyopita kuhusu tuhuma za kukutwa na gari hilo lililoibwa pia Dar es Salaam, ASP Zuhura alikanusha na kusisitiza kuwa hazijui.
“Hiyo taarifa (ya gari) mbona siijui. Hakuna taarifa kama hizo,” alikanusha taarifa hizo ambazo baadaye zilithibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa ambaye alikiri maofisa wake kukutwa na magari hayo, lakini akasema hawawezi kupewa adhabu kabla ya kuthibitika kuwa amefanya uhalifu.
“Makachero wetu wanashirikiana na kikosi kazi cha Dar es Salaam na watakapobainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisema.
Taarifa zilizopatikana jana zilisema, ofisa mwenye cheo cha koplo alisomewa barua ya kufukuzwa kazi juzi jioni na muda huohuo na ASP Zuhura naye akasomewa barua ya uhamisho.
“Kwa cheo cha ASP mamlaka yake ya nidhamu ni katibu mkuu kwa hiyo kilichofanyika ni kumuondoa kwenye wadhifa wa OCS akisubiri uamuzi mwingine kutoka juu,” kilidokeza chanzo chetu.
ASP Zuhura alipotafutwa kwa simu jana ili kuzungumzia suala hilo hakupokea, lakini Koplo Federika alipopigiwa alipokea na kukana kufukuzwa kazi kisha kukata simu.
Kamanda Mutafungwa alipopigiwa simu alitaka atumiwe ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) na alipotumiwa na kuulizwa kuhusu suala hilo, hakukanusha wala kuthibitisha zaidi ya kujibu atafutwe leo saa 5:00 asubuhi.
Kukamatwa kwa maofisa hao kulitokana na kutajwa na mtandao wa wizi wa magari jijini Dar es Salaam uliokuwa mikononi mwa polisi, ambao walisafiri hadi Himo na kuyakamata.
Akizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema mtandao huo umekuwa ukipeleka magari ya wizi Arusha na Moshi.
Credit: Mwananchi
Thursday, October 27, 2016
Aliyejifanya Usalama wa Taifa Ahukumiwa Miaka Miwili Jela
Mahakama
ya Wilaya ya Ilala imemhukumu Seleman Manoti, kifungo cha miaka miwili
jela kwa kupatikana na hatia ya kujifanya usalama wa Taifa.
Hata
hivyo, mahakama imetoa hukumu hiyo bila mshitakiwa kuwepo mahakamani
kutokana na kuruka dhamana kesi hiyo ilipokuwa inasikilizwa.
Akitoa
hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi, Flora Haule alisema kuwa upande wa
mashitaka, ulileta mashahidi wanne kwa ajili ya kuthibitisha tuhuma
hizo.
Alisema
kutokana na ushahidi uliotolewa, mahakama imeridhishwa na ushahidi huo
na kwamba mahakama inamtia hatiani mshitakiwa licha ya yeye kutokuwepo.
“Hati
ya kumkamata mshitakiwa itolewe na adhabu hii itaanza kutumika pindi
mshitakiwa atakapokamatwa kwani alitoroka akiwa na haki ya kusikilizwa,” alisema Hakimu Haule.
Wakili wa Serikali, Ester Kyara aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa iwe fundisho kwa wengine.
Inadaiwa
kuwa Novemba 19, 2014 maeneo ya Kariakoo Msimbazi wilayani Ilala,
mshitakiwa alijitambulisha kwa Issaya Odelo na Charles Odinga kuwa Ofisa
Usalama wa Taifa, kitu ambacho alijua si kweli.
Katika
hatua nyingine, kondakta Ally Salum (23), mkazi wa Mwananyamala,
amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia
ya kuiba daladala.
Mbali
na mshitakiwa huyo, Exavery Kaunga (44) ambaye ni mlinzi na mkazi wa
Kiwalani, Minazi Mirefu, aliachiwa baada ya ushahidi dhidi yake kuwa na
shaka.
Akitoa
hukumu hiyo jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Hakimu Mkazi
Mwandamizi, Juma Hassan, alisema kuwa upande wa mashitaka ulileta
mashahidi wanne kuthibitisha kosa hilo.
“Nimeridhika
na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka, nakutia hatiani
mshitakiwa kama ulivyoshitakiwa kwa kutumikia kifungo cha miaka mitano
jela,” alisema Hakimu Hassan.
Kabla
ya kutolewa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Grace Mwanga aliiomba
mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine.
Hata hivyo, mshitakiwa alipoulizwa ni kwa nini asipewe adhabu kali,
hakujibu chochote na mahakama kutoa adhabu hiyo.
Washitakiwa
hao walishitakiwa kwa makosa mawili ya kula njama kutenda kosa ambapo
inadaiwa kati ya Julai 5, mwaka jana, washitakiwa walikula njama kutenda
kosa.
Pia
inadaiwa Julai 5,2015 pembezoni mwa barabara ya Nyerere katika Kituo
cha Mafuta cha Victoria, washitakiwa waliiba gari lenye namba za usajili
T 624 CSH aina ya Eicher mali ya Kampuni ya White Swan.
HABARI ZA ALHAMISI HII
Reviewed by RICH VOICE
on
Oktoba 27, 2016
Rating:
Hakuna maoni