Friday, October 28, 2016

Kauli ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kwa wanaotumia picha zake mitandaoni na kupotosha aliyoyasema

SeeBait

Rais mstaafu kutoka kwenye awamu ya nne ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ameamua kujibu kile kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii katika siku za karibuni.
 
Usiku wa kuamkia leo, kupitia akaunti yake ya Twitter, Rais Mstaafu wa Tanzania,Dkt. Jakaya Kikwete aliandika masikitiko yake juu ya namna watu wanavyotumia picha zake na kupotosha yale aliyoyasema juzi akiwa chuo kikuu cha Dar es Salaam  ili kufanikisha matwaka yao ya kisiasa.
Aidha, Rais Kikwete aliwataka watu hao kumuacha kwani ameshamaliza muda wake wa uongozi hivyo ni wakati wake sasa kupumzika. 

Rais Kikwete pia alikanusha tuhuma za kuwa  anatofauti na Rais wa sasa Dkt John Pombe Magufuli na kusema kuwa anamuunga mkono Rais Magufuli pamoja na serikali yake.
Kauli ya Rais Mstaafu Kikwete ambayo imekuwa ikipotoshwa mtandaoni ni ile aliyoitoa kwenye  maadhimisho ya miaka 55 ya chuo kikuu cha Dar es Salaam ambapo aliwataka  viongozi wapya kuenzi mazuri ya nyuma akimaanisha kwamba hivi sasa yeye ndo Mkuu wa Chuo hicho(Chancellor), hivyo  akaahidi kuyaenzi mazuri aliyoyakuta toka kwa watangulizi wake

“Ukiwa mpya lazima watu waone una mambo mapya, lakini mapya ya maendeleo," alisema Rais Mstaafu Kikwete na kuongeza; “Sio mapya ya kubomoa ya kule tulikotoka,” 
 

Friday, October 28, 2016

Sumaye kunyang’anywa shamba na serikali, apewa notisi ya siku 90

SeeBait

Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema hati ya shamba lililopo maeneo ya Bunju la aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Fredrick Sumaye liko katika hatua ya kufutwa na kwamba Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Kinondoni Rehema Mwinuka ameshatoa barua ya notisi ya siku 90.

Lukuvi ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wandishi wa habari.

“Shamba la Sumaye hati yake iko katika hatua za kufutiwa,
Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ambaye anajukumu la kutoa notisi, ameshatoa notisi kwamba hajaendeleza eneo hilo kwa muda mrefu hivyo kwa mujibu wa sheria hati yake inatakiwa kufutwa,” alisema.

Alisema serikali haitofumbia macho wamiliki wa ardhi na mashamba ambao hawajayaendeleza kwa muda mrefu.

Pia, kufuatia ongezeko la matapeli wanaotumia nyaraka za kughushi za barua za toleo (ofa) zinazodaiwa kutolewa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Lukuvi alitoa agizo hususani kwa wakazi wa jiji hilo wanaomiliki ardhi pasipo kuwa na hati miliki, kujisalimisha kwa kupeleka barua zao za ofa kwa Kamishna wa Ardhi ili wapatiwe hati halali.

“Wamiliki wote wanaomiliki ardhi kwa karatasi za ofa halali wazibadilishie ili wapewe hati halali, na atakaegundulika kumiliki ofa feki polisi watawakamata na kupelekwa mahakamani,” alisema.

Alisema asilimia 60 ya watu wanaopeleka kesi za migogoro ya ardhi wizarani, chanzo cha migogoro hiyo ni karatasi za ofa zinazotoka katika halamshauri za jiji na manispaa.

“Natoa miezi mitatu ili karatasi hizi zisitokee tena kila mtu alete barua ya ofa watapewa hati zao ndani ya mwezi mmoja ,wazilete kwa kamishna wa ardhi wa mkoa, baada ya hapo sitasikiliza malalamiko ya watu walioibiwa ardhi wakiwa na ofa ya namna hii.

“Tumieni miezi mitatu vizuri kubadilisha ofa,” amesema.

Hali kadhalika, Lukuvi alipiga marufuku vitendo vya uvamizi wa ardhi na mashamba vinavyofanywa na baadhi ya wananchi, na kuwataka wananchi kutoa taarifa pindi watakapobaini kuwa kuna shamba au ardhi isiyoendelezwa.

“Serikali ina laani uvamizi wa ardhi na mashamba unaofanywa na baadhi ya wananchi sababu baadhi yao yanamilikiwa kihalali na yana hati, serikali ipo na sheria zipo zitafanya kazi yake,” alisema.
 
 

Friday, October 28, 2016

Bia Ya Kopo Ya Safari Lager 500ml Yaendelea Kubamba Kitaa



Bila shaka umeshaliona tangazo hili matata kabisa la Safari Lager ukipita Barabara ya Kawawa jijini Dar, wajanja wanakwambia utaalamu uliotumia kutengeneza bango hilo la 3D ni wa hali ya juu sana.

Tangazo hili limekuwa likiwavutia wapita njia katika barabarani hiyo na kuwateka hisia zao, “Dah yaani hili tangazo tu lilivyo linakufanya uitafute bia yenyewe uishushe kinywani” alisikika mmoja wa muenda kwa miguu.

Sasa si tu kwamba tangazo linateka hisia na kuwa kivutio, bia yenyewe ina ladha nzuri ya aina yake na inaleta urahisi na unafuu kwa mtumiaji yeyote wa Safari Lager. Kampuni ya Bia ya TBL ilizindua bia hii ya kopo ya kwanza yenye ujazo wa mililita 500 kwa bia ya Kitanzania mwishoni mwa mwezi wa 8 mwaka huu na hadi sasa imeonekana kuwa kipenzi cha watumiaji katika maeneo mbalimbali nchini.

“Bia mpya ya kopo ya Safari ni dhahiri kwamba imetengezwa kumpa umahiri Mtanzania katika safari ya maisha yake. Inapatikana kwa urahisi na kwa wakati muafaka hata wakati mtu anakwenda kwenye mihangaiko yake au kubeba akiwa anakwenda kwenye matembezi au safarini” alisema Meneja Bidhaa wa Safari Lager, Edith Bebwa

Meneja Bidhaa wa Safari Lager, Edith Bebwa alipokuwa akitambulisha bia mpya ya Safari Lager kwenye kopo la mililita 500 ambayo inapatikana Tanzania nzima.

Baadhi ya wateja wakiwa na nyuso za furaha baada ya kujipatia bia mpya ya Safari Lager katika kopo lenye ujazo wa 500ml
 
 

Friday, October 28, 2016

Basi la Hood lagongana na lori na kupinduka kwenye mlima Kitonga

SeeBait
Basi la kampuni ya Hood linalofanya safari zake kati ya Mbeya na Arusha jana  mchana lilipata ajali na kupinduka katika mlima Kitonga mkoani Iringa baada ya kugongana na lori la mafuta.
 
Katika ajali hiyo mtu mmoja amepoteza maisha na wengine 43 wamejeruhiwa. Kati ya majeruhi hao 25 wapo Hospitali ya Itunda Ilula na 18 wapo katika Hospitali ya Mkoa.

 
 

Friday, October 28, 2016

Bia ya Serengeti yasherehekea kutimiza miaka 20

SeeBait
  •     SBL yaizindua bia hiyo katika muonekano mpya
  •     Yashinda zaidi ya medali 10 za ubora wa kimataifa
Dar es Salaam  Oktoba 28, 2016- Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) leo  imetangaza kuanza kwa sherehe maalumu kuadhimisha miaka 20  tangu kuanzishwa kwa bia ya Serengeti Premium Lager (SPL)  mwaka 1996. Sherehe hizo zinaambatana na uzinduzi upya wa bia hiyo ikiwa katika muonekano mpya.

Akizungumza  jana jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa SBL Helene Weesie, alisema mbali na kuonesha mafanikio ya bia ya Serengeti kwa kipindi cha miongo miwilil iliyopita, kampuni ya SBL itatumia kipindi hiki kuwashukuru wateja  wake na umma wa Watanzania  kwa kuikubali bia ya Serengeti kama chaguo lao la hivyo kuifanya kuwa mingoni mwa bia zinazoongoza hapa nchini.

 “Tunawashukuru  wateja wetu, wafanya biashara, wasambazaji, mashirika ya sekta binafsi, serikali na wadau wote  ambao kimsingi wametusaidia  na kuwa nasi  katika safari yetu hii ya mafaniko,” alisema Weesie.

Bia ya Serengeti Premium Lager ni ya kwanza kutengenezwa kwa kimea kwa asilimia 100hapa nchini ikiwa ni ubunifu wa Mpishi Mkuu mtanzania aitwaye Winston Kagusa  ambaye alichanganya mbinu ya utengenezaji wa bia za kijerumani na  vionjo vya hapa nchinikupata kupata kinwaji hiki kinacopendwa na wengi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu, bia ya Serengeti ilizalishwa kwa mara ya kwanza ikilenga kufikia sehemu ndogo maalumu ya soko lakini azma hii ilibadilishwa na kuzalishwa kwa wingi kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji ya bidhaa hiyo jambo ambalo lilisababisha kuanzishwa uzalishaji zaidi katika viwanda vya SBL vilivyoko Moshi na Mwanza.

Aidha Mkurugenzi huyo aliendelea kusema kwamba katika kipindi chote cha miongo miwili bia ya Serengeti imekuwa na vifungashio vya muonekano tofauti tofauti vinavyoakisi mabadiliko ya kinyakati na mahitaji ya wateja wake. “muonekano mpya tunaouzindua leo hii ni muendelezo wa kielelezo hiki kwamba daima SBL tunajali mahitaji ya wateja wetu na tuko karibu nao, amesema Weesie.

“Tunaona fahari kuzalisha Bia ya Serengeti Premium Lager  katika  ubora uleule wa hali ya juu katika viwanda vyote vitatu, na huu ni uthibitisho halisi kutokana na kutambuliwa  na wateja wetu wa ndani  pamoja na medali  zaidi ya 10  za kutambulika kimataifa  ambazo bia hii imeshinda. Tunaahidi wateja wetu kwamba tutaendeleakuzalisha Serengeti Premium Lager  katika ubora wa hali ya juu  kwa kuzingatia vigezo vya ubora vilivyoanishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO),” alisema Weesie.

Uzinduzi wa muonekano mpya wa  bia ya Serengeti pia umekuja na kauli mbiu mpya wa kinywaji hicho cha “Taifa Letu. Fahari Yetu. Bia Yetu.” Aidha kampuni hiyo imewakaribisha wateja wake na wadau mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi katika hafla ya maadhimisho ya miaka 20 ya bia ya Serengeti yatakayofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Mkurungezi wa Masoko wa SBL , Cesear Mloka akifafanua jambo kwa waandishi wa habari mara baada ya kutangazwa kwa maadhimisho ya miaka 20  tangu kuanzishwa kwa bia ya Serengeti Premium Lager (SPL)  mwaka 1996.Anayefuatia katikati ni Meneja Masoko wa SBL Anitha Msangi na mwishoni kulia ni Mkurungezi mkuu wa SBL  Helene Weesie.Mkutano huu umefanyika mapema jana katika Hyatt Regency Hotel Jijini Dar es salaam.

Mpishi Mkuu mtanzania  Winston Kagusa aliyefanikiwa kuchanganya mbinu ya utengenezaji wa bia za kijerumani na  vionjo vya hapa nchini kupata  kinywaji hiki  cha Serengeti Premium Lager kinachopendwa na wengi.

 Mkurugenzi Mkuu wa SBL Helene Weesie akiongoza katika kuzindua chapa mpya ya Serengeti Premium Lager sherehe ambazo zinaambatana na maadhimisho ya miaka 20 ya bia hiyo kulia kwake ni Meneja Masoko wa SBL Anitha na kushoto kwake wa kwanza ni Mpishi Mkuu wa kwanza wa Serengeti Premium Lager Winston kagusa na mwishoni ni Mkurungezi wa Masoko  Cesear Mloka.Hafla hii ilifanyika katika hotel ya Hyatt Regency Jijini Dar es salaam.

Mkurugenzi wa Mawasiliano, SBL John Wanyacha akifafanua jambo kwa waandishi wa habari katika Mkutano wa waandishi wa habari ambapo Bia ya serengeti premium lager inatimiza miaka 20 toka kuanzishwa kwake na pia kuzinduliwa kwa chapa yenye muonekano mpya.Mkutano huu ulifanyika mapema jana katika hotel ya Hyatt Regency

Waandishi wa habari wakichukua matukio katika mkutano huo 
 
 

Friday, October 28, 2016

Sumaye: Sirudi CCM hata waninyang’anye Mashamba Yangu Yote

Siku moja baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kutangaza nia ya Serikali kumnyang’anya shamba Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, mwanasiasa huyo mkongwe amedai hilo halimtikisi.

Sumaye ambaye tayari ameshakabidhiwa notisi ya siku 90 kutokana na kutoliendeleza, amesema kuwa tayari suala hilo ameshaliwasilisha mahakamani na kwamba mwanasheria wake ndiye anayefahamu tarehe iliyopangiwa kesi hiyo.

“Nilienda mahakamani na ikaamuriwa kusiwe na shughuli yoyote, nasubiri tarehe ya kesi ambayo mwanasheria wangu ndiyo anaijua,” Sumaye anakaririwana MwanahalisiOnline.

Mwanasiasa huyo aliyehamia Chadema miezi michache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka jana, amesema kuwa kama CCM wanataka kumdhoofisha kwa kumnyang’anya mashamba ili arejee haitawezekana.

“Kama walidhani kwa kunifanyia hivi nitarudi Chama Cha Mapinduzi (CCM) wasahau, hata kama nilikuwa na nia hiyo sirudi,” amesema Sumaye.

Serikali imetangaza kuanza mchakato wa kumnyang’anya Sumaye shamba lake lililoko Mwabwepande jijini Dar es Salaam kwa madai kuwa ameshindwa kuliendeleza kwa muda mrefu, kinyume na matakwa ya sheria.
 
 

Friday, October 28, 2016

Matokeo darasa la saba: Majina ya watahiniwa 10 waliofanya vizuri na shule 10 bora na Ambazo Hazikufanya Vizuri

Ufaulu kwa watahiniwa wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi 2016 umepanda kwa asilimia 2.52 kutoka asilimia 67.84 mwaka jana hadi asilimia 70.36, huku wavulana waking’ara katika matokeo hayo ambao wengi wametoka shule za Kanda ya Ziwa.
 
Matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk Charles Msonde ambaye alisema kati ya wanafunzi 10 bora waliofanya vizuri katika mtihani huo, msichana ni mmoja tu, Justina Gerald wa Shule ya Msingi ya Tusiime ya jijini Dar es Salaam.
 
Kati ya wanafunzi hao 10, watahiniwa saba wanatoka Shule ya Msingi Kwema iliyopo mkoani Shinyanga, wawili Tusiime na mmoja kutoka Kaizirege ya Bukoba mkoani Kagera. 

Dk Msonde alisema jumla ya watahiniwa 555,291 kati ya 789,479 waliofanya mtihani huo wamefaulu kwa kupata jumla ya alama 100 na zaidi kati ya alama 250.
 
“Idadi hii ya watahiniwa waliofaulu ni sawa na asilimia 70.36, kati ya hao wasichana ni 283,751 na wavulana 271,540. Mwaka 2015 ufaulu ulikuwa ni asilimia 67.84 kuwapo ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.52,” alisema Dk Msonde.
 
Watahiniwa 16,929 wamepata daraja A, watahiniwa 141,616 wamepata Daraja B, watahiniwa 396,746 wamepata daraja C, watahiniwa 212,072 wakipata daraja D na 21,872 wakipata daraja E . 

Dk Msonde alisema ufaulu katika masomo ya Sayansi na Maarifa ya Jamii umepanda kwa asilimia kati ya 4.06 na 14.76 ikilinganishwa na mwaka 2015 huku masomo ya Kiswahili, Hisabati na Kiingereza ufaulu umeshuka kwa asilimia kati ya 0.39 na 12.51 ukilinganisha na mwaka jana.
 
“Watahiniwa wamefaulu zaidi katika somo la Kiswahili ambalo ufaulu wake ni asilimia 76.81 na somo walilofaulu kwa kiwango cha chini ni Kiingereza lenye ufaulu wa asilimia 36.05,” alifafanua Dk Msonde.
 
Dk Msonde aliwataja watahiniwa waliofanya vizuri na shule zao kwenye mabano kuwa ni:
  • Japhet Stephano, Jamal Athuman na Enock Bundala (Kwema),
  • Justina na Shabani Mavunde (Tusiime),
  • Jacob Wagine, Isaac Isaac, Daniel Kitundu na Benjamin Benevenuto (Kwema)
  •  Azad Ayatullah (Kaizirege).
Wasichana 10 bora:
  1. Justina Gerald (Tusiime)
  2.  Danielle Onditi (Tusiime)
  3. Linda Mtapima (Kaizirege),
  4. Cecilia Kenene (Mugini),
  5. Magdalena Deogratias (Rocken Hill),
  6. Asnath Lemanya (Tusiime),
  7. Fatuma Singili (Rocken Hill),
  8. Ashura Makoba (Kaizirege),
  9. Rachel Ntitu (Fountain of Joy),
  10. Irene Mwijage (Atlas)
Wanafunzi wavulana 10 bora kitaifa,
  1. Japhet Stephano (Kwema),
  2. Jamal Athuman (Kwema),
  3.  Enock Bundala (Kwema),
  4. Shabani Mavunde (Tusiime),
  5. Jacob Wagine (Kwema),
  6. Isaac Isaac (Kwema),
  7. Daniel Kitundu (Kwema),
  8. Benjamin Benevenuto (Kwema),
  9. Azad Ayatullah (Kaizirege)
  10. Benezeth Hango (Kwema).
Shule 10 bora ni:-
  1. Kwema (Shinyanga),
  2. Rocken Hill (Shinyanga),
  3. Mugini (Mwanza),
  4. Fountain of Joy (Dar es Salaam),
  5.  Tusiime (Dar es Salaam),
  6. Mudio Islamic (Kilimanjaro),
  7. Atlas (Dar),
  8. St Achileus (Kagera),
  9. Giftskillfull (Dar),
  10. Carmel (Morogoro).
Shule 10 ambazo hazikufanya vizuri ni:-
  1. Mgata (Morogoro)
  2. Kitengu (Morogoro)
  3. Lumba Chini (Morogoro),
  4. Zege  (Tanga),
  5.  Kikole (Tanga),
  6. Magunga ya Morogoro,
  7. Nchinila (Manyara),
  8. Mwabalebi (Simiyu)
  9. Ilorienito (Arusha)
  10. Chohero (Morogoro)
Mikoa 10 iliyoongoza kitaifa ni Geita, Katavi, Iringa, Dar es Salaam, Kagera, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Njombe na Tabora wakati Halmashauri 10 bora ni Mpanda Manispaa, Geita Mji, Arusha Mji, Mafinga Mji, Chato, Mwanza Jiji, Moshi Mji, Mji Makambako, Ilemela na Hai.

 
 

Friday, October 28, 2016

Yanga Wamrejesha Kazini Kocha Wao Hans Van Pluijm Leo .......Wakataa Ombi Lake la Kujiuzulu

SeeBait

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwanachama wa Klabu ya Yanga, Mwigulu Nchemba akiwa katika Mazungumzo na Kocha wa Yanga aliyetangaza kujiuzulu kuitumikia klabu hiyo hivi karibuni, Hans Van Pluijm na kumtaka ajeree kwenye kibarua chake cha kuendelea kukinoa kikosi cha Yanga kinachoshikilia Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit.
 
 

Friday, October 28, 2016

Tamko: CCM yawajibu Lowassa na Zitto Kabwe ..... Pia yakana kushiriki kwenye kuivuruga CUF

SeeBait

Ikiwa imepita siku mbili tangu aliyekuwa mgombea wa kiti cha Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa mwamvuli wa UKAWA, Edward Lowassa kueleza tathimni ya utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano chini Rais John Magufuli, ambapo alidai kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi huo, kumekuwepo na ukiukwaji wa misingi ya demokrasia na utumishi wa umma kuwa kaa la moto.
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimevunja ukimya na kumjibu kwa kusema kuwa katika kipindi cha uchaguzi mkuu uliopita alikuwa wa kwanza kukiuka misingi ya demokrasia. Kuhusu utumishi wa umma kuwa kaa la moto, imemjibu kuwa wanao lalamika hivyo ni wale wanaotumiwa kuficha mafisadi na wakwepa kodi.
Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka amewaambia waandishi wa habari kuwa Lowassa hastahili kuituhumu serikali ya Rais Magufuli kuwa inakiuka misingi ya demokrasia.

“Demokrasia ya kweli lazima ianze ndani ya chama, ni demokrasia ipi iliyotoa mamlaka kwa vyama vinavyounda UKAWA kuwanyima wanachama wao haki ya kuomba kupeperusha bendera za vyama walivyoviasisi, kuvitetea kuvigharamia kwa kuamua kumteua mgombea mtunguo ambaye hajapimwa wala hajawahi kuvipigania?,” amehoji.

Ole Sendeka ameongeza kuwa “Kitendo hicho cha kutowashirikisha wanachama na kuwanyima haki yao kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kulidhihirisha usaliti wa hali ya juu wa misingi ya demokrasia.”

Amesema CCM haigopeshwi na matamko ya Lowassa anayotoa katika vyombo vya habari kwa kuwa havitaiathiri na kwamba imemamua kumjibu kwa madai kuwa anapotosha umma kwa kueleza mambo yasiyo na ukweli.

Ametoa wito kwa vyama vya siasa nchini kutochukulia kwa wepesi masuala ya demokrasia na mabadiliko.

“Wanasayansi wa masuala ya siasa waiangalie demokrasia ya CHADEMA na UKAWA inavyofanya kazi maana ni kihoja, watuambie njia iliyotumika kuwapata wabunge viti maalumu. Kila kiongozi aliteua maswahiba zake na wengine kwa ugeni wao ndani ya CHADEMA,” amesema.

Pia Sendeka amemtaka kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo kutoichukia serikali ya Rais Magufuli kwa kuwa inatekeleza yale aliyokuwa anayapigania.

“Chuki ya Zitto ya kuendelea kunyooshea kidole serikali ya CCM haina tija, sababu inatekeleza yote aliyokuwa akiyapigania,” amesema.

Katika hatua nyingine, Sendeka amedai kuwa CCM haijashiriki kukihujumu chama cha Wananchi (CUF) kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa kuwa kinawachonganisha viongozi wa chama hicho ili kigawanyike.

“Hatuna haja ya kuhangaika na CUF na wapanga siasa za uongozi CHADEMA, hatujashiriki kukivuruga na hatuna muda huo,” amesema.

=======
Ndugu wanahabari,

Kwa muda sasa kumekuwepo na usambazaji wa taairifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa wakishirikiana na baadhi ya vyombo vya habari zinazolenga kukejeri, kudhihaki, kukatisha tama, kubeza na kudhoofisha jitihada zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi na Seikali zake katika kuleta maendeleo kwa Watanzania

Kumekuwepo na makala zinazoandikwa na magazeti mawili ya nje ambazo hutolewa kila baada ya miezi miwili na ambazo zinapotosha na kuandika habari zisizo za kweli kuhusu Tanzania

Pia, yapo magazeti mawili ya ndani ambayo yamekuwa yakitoa makala mfululizo kwa kila wiki zinazolenga kumchafua Mheshimiwa Rais na kuichafua taswira ya nchi yetu.

Tumesikitishwa na waandishi wa makala hizo walioamua kujivua uzalendo na kushiriki mpango wa kuiharibu heshima na taswira ya nchi yetu kwa maslahi ya maadui zetu wa nje na baadhi ya wanasiasa. Tunafuatilia kujua nini kinawasukuma kufanya hivyo na kwa maslahi ya nani ilhali sote ni watanzania. Je ni tama ya madaraka tu au mengine?. Hakuna anayepinga ukosoaji bali unapaswa uwe ukosoaji wenye nia njema

Ndugu wanahabari,

Mtakumbuka hivi karibuni aliyewahi kuwa Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa tuhuma za ufisadi ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa, alisambaza taarifa kwa vyombo vya habari aliyoiita tathimini ya mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu wa octoba 25,2015

Katika taairifa yake, alidai kuwa alileta msisimko mpya katika siasa za Tanzania, kwamba ameshirikiana na wenzake kuionyesha nchi yetu maana ya demokrasia na kukosoa juhudi za serikali na wateule wa Rais.

Demokrasia kimsingi ni dhana inayohusisha ushiriki na kuheshimu mawazo ya wengi katika kufikia uamuzi. Ikiwa maana halisi ni hii, tunajiuliza ni ipi demokrasia aliyoionyesha Lowassa ambayo leo anajisifu kuwa nayo?

- Tulishuhudia akiwa mgombea Urais wa chama ambacho hakijui, hakushiriki kukijenga wala kutoa mchango wowote unaompa hadhi ya kupeperusha bendela huku katiba na kanuni ya chama hicho ikivunjwa. Kidemokrasia anayepewa fursa ya kupeperusha bendela ya chama chochote makini duniani ni kiongozi au mwanachama aliyethibitika kwa imani na matendo, kuzielewa, kuzitekeleza, kuzitetea falsafa, itikadi na malengo ya msingi ya chamahicho. Mgombea ni taswira halisi na alama muhimu inayoakisi dhamira ya chama husika machoni kwa wananchi.

- Demokrasia ya kweli lazima ianzie ndani ya chama, ni demokrasia ipi inayotoa mamlaka kwa vyama vinavyounda UKAWA kuwanyima wanachama wao haki ya kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera za vyama walivyoviasisi, kuvitetea, kuvigharamia na walivyovitumikia kwa kuamua kumteua mgombea “MTUNGUO” (ambaye hajapimwa wala hajawahi kuvipigania). Kitendo hicho cha kutowashirikisha wanachama na kuwanyima haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kilidhihirisha usaliti wa hali ya juu wa misingi ya demokrasia

- CHADEMA watuambie njia iliyotumika kuwapata wabunge wa viti maalumu. Ni demokrasia gani inayotoa fursa kwa baadhi tu ya viongozi kuteua wabunge ambao wanakiwakilisha chama chote. Ambapo kila kiongozi aliteua maswahiba zake na wengine kwa ugeni wao ndani ya CHADEMA walikosa watu wanaowafahamu na kuamua kuwateua wanawake maswahiba wao ndani ya CCM. Msingi wa kawaida wa kupata wabunge wa viti maalumu ukiacha kura za maoni, kigezo kingine muhimu ni mchango wa mgombea / mwanachamahuyo katika kukijenga na kukitumikia chama chake. Yaliyotokea kwa CHADEMA kwenye wabunge wake wa viti maalumu ni mapya kwenye ulimwengu wa demokrasia. Inahitaji wataalamu wa sayansi ya siasa kufanya utafiti wa aina hii mpya ya demokrasia

Tulidhani baada ya mwaka mmoja kupita, wenzetu hawa wangelikuwa wamejifanyia tathimini, kujikosoa, kujisahihisha, na hata kufanya uungwana wa kuwaomba radhi wanachama wao kwa uvunjifu mkubwa wa misingi ya demokrasia, katiba na kanuni za vyama vyao

Tunatoa wito kwa vyama vya siasa nchini kutokuchukulia kwa wepesi masuala ya demokrasia na mabadiliko, yasiwe ni nyimbo za kuburudisha au kutoa matumaini hewaq kwa wanachama na wananchi. Kanuni mojawapo ya demokrasia ndani ya vyama ni lazima ionekane katika muundo wake na katika utekelezaji wa muundo huo

Umefika wakati vyama vya siasa vinapaswa kujifunza kuuza sera ili kujenga na sio kusubiri matukio kwa ajili ya kupata huruma ya wananchi. Tunasubiri kushuhudia na kusikia demokrasia demokrasia itakavyoendeshwa katika uchaguzi wa ndani wa vyama hivyo ambapo kuna taarifa mmoja wa vigogo amefanikiwa kupata kiasi cha dola milioni 15 zitakazomsaidia kupanga safu yake ya uongozi

Katika kutimiza mpango huo, tayari yapo mawasiliano ya mara kwa mara ya baadhi ya viongozi wakitoka Zanzibar na sehemu zingine za nchi kuja Dar es Salaaam, na imeonekana dhahiri mazungumzo yao kutowashirikisha viongozi wenzao waandamizi kwani yanalenga kafanikisha mpango huo.

Mheshimiwa Rais Dk John Pombe Magufuli, ameendelea kufanya juhudi kubwa katika kujenga nchi kwa kuimarisha utendaji na nidhamu ya utumishi serikalini, kukusanya mapato na kusimamia matumizi sahihi ya fedha, kupambana na kuzuia mianya ya rushwa pamoja na kusimamia haki, usawa na wajibu kwa raia. Mwenzetu anayaona haya kuwa ni kuufanya utumishi wa umma kaa la moto.

Juhudi hizi na nyinginezo ikiwemo ununuzi wa ndege mpya, ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, afya na kununua vitanda vya wazazi, kutoa elimu burekuanzia shule ya msingi mpaka sekondari na nyinginezo hazipaswi kukatishwa tama kwa maslahi ya wachache ni vyema kuziunga mkono kwa maslahi ya taifa letu

Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Rais Dk. Magufuli madarakani, CCM inawaomba wananchi kuendelea kummunga mkono katika dhamira yake safi yakuwaondolea kero, kuboresha huduma za jamii na kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Imetolewa na;-
CHRISTOPHER OLE SENDEKA
MJUMBE WA NEC NA MSEMAJI WA CCM
28/10/2016 
 

Friday, October 28, 2016

CHADEMA yapinga kununuliwa na Lowassa, yashindwa kuzungumzia tuhuma za ufisadi.


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema ni uongo na ni propaganda za wapinzani wao kwamba Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa alimhonga Mwenyekiti Freeman Mbowe ili kupata nafasi ya kugombea urais mwaka 2015.

Dkt.  Mashinji ameyasema hayo katika kipindi cha Kikaangoni  kinachorushwa na kituo cha EATV kupitia ukurasa wa facebook ambapo wananchi walikuwa wakimuuliza maswali ya papo kwa papo naye anayajibu.

“Si kweli kwamba Mwenyekiti Freeman Mbowe alimhonga Lowassa ili agombee urais kupitia CHADEMA , ni propaganda zinazoenezwa na wapinzani wetu ili kuwadanganya wananchi” Amesema Dkt. Mashinji.

Amesema Lowassa alijiunga na CHADEMA kwa njia halali kwa mujibu wa taratibu za chama, na maamuzi ya kumteua kugombea urais yalifanywa na vikao halali kuanzia ngazi ya Kamati Kuu hadi Mkutano Mkuu.

Kuhusu sababu za CHADEMA kumkaribisha Lowassa licha ya kumtaja miaka mingi kuwa alihusika na ufisadi, Dkt Mashinji, hakutaka kulifafanua kwa undani, lakini aliishia kusema kuwa wao walijiridhisha kuwa hakuwa na hatia yoyote na kwamba kama kweli alikuwa ni fisadi, basi vyombo vya dola vingemchukulia hatua.

"Kama mtu kweli alikuwa ni fisadi, kwanini hakuwahi kuchukuliwa hatua, hata kufikishwa mahakamani?, nadhani hilo tuliache" Alisema kwa ufupi Dkt Mashinji.

Aidha Dkt. Mashinji amewataka watanzania na wapenzi wa CHADEMA kufahamu kwamba chama hicho hakipo kimya bali kinaendelea na mikakati ya kuhakikisha kwamba kinawafikia watanzania kwa kuwatetea kwa kila hali kutokana na mambo yanayoendelea nchini.

 

Friday, October 28, 2016

Haijalishi Mtandao Wako Uko Vipi…TECNO Phantom 6 Plus Inatereza Tu

SeeBait
Ukiachilia mbali Tecno Phantom 6 Plus kuwa simu iliyotengenezwa na betri inayodumu kwa muda mrefu zaidi, nikufahamishe kwamba simu hiyo pia ina uwezo mkubwa kwa upande wa intaneti.
Tecno Phantom 6 Plus ina kasi ya hatari unapoitumia kupata mambo mbalimbali au kutazama video mtandaoni. 

Sasa ukiunganisha hili la spidi na uwezo wa kukaa na chaji kwa muda mrefu (Ikiwemo kuchaji kwa haraka) inakuwezesha kuitumia kwa muda wote bila mushkeri wala wasiwasi wa aina yoyote wa kuzimikiwa au kutoweza kuangalia video zako kwa wakati. 
Picha hii inaonesha ni kwa jinsi gani Tecno Phantom 6/+ ilivyo na uwezo wa kuchaji betri kwa haraka ndani ya muda mfupi ikitumia USD Type C

Angalia uchambuzi mfupi kuhusu spidi ya Tecno Phantom 6 Plus kwenye upande wa intaneti na tupe maoni yako kwenye kisanduku cha ujumbe.


Unaweza kutembelea kurasa za mitandao ya kijamii ya Tecno kufahamu zaidi kuhusiana na Tecno Phantom 6 na Phantom 6 Plus.
 
  
 

Friday, October 28, 2016

Maalim Seif afanya ziara Wilaya zote za Unguja na kuzungumza na viongozi wa CUF......Atoa Maneno Mazito Akiikumbuka Octoba 28 Jecha Alipofuta Matokeo Zanzibar

Wakati leo ni mwaka mmoja tangu matokeo ya Uchaguzi Mkuu Zanzibar yafutwe Oktoba 28, 2015, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amemtuhumu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kuwa ndiye aliikwamisha nchi kwa kupindua maamuzi ya wananchi.

Maalim Seif alisema kutokana na uamuzi huo, ndiyo maana mpaka sasa mwenyekiti huyo ameshindwa kuibuka hadharani akielewa alibeba dhima ya Wazanzibari na Watanzania wote wapenda amani. 

Maalim Seif aliyasema hayo jana alipofanya ziara ya siku moja katika wilaya zote saba za Unguja katika kumbukumbu ya mwaka mmoja, tangu Jecha alipofuta uchaguzi huo.

Maalim Seif aliita siku hii ‘black October’ akisema ndiyo siku Jecha alitekeleza kwa makusudi kufuta ndoto ya Wazanzibari ya kupata viongozi wanaowataka.

“Jecha ndiye aliyesitisha ndoto yetu ya kuwa Singapore, alipindua demokrasia na kufuta matokeo bila ya kuwapo kifungu chochote cha Katiba kinachotoa mamlaka hiyo,” alisema Maalim Seif.

Makamu huyo wa kwanza wa Rais mstaafu, alisema kuwa kabla ya Jecha hajatekeleza azma hiyo ovu, waangalizi wote wa uchaguzi kutoka ndani na nje ya nchi na ZEC wenyewe walijiridhisha na kutoa tamko kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.

Waangalizi hao ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Bara la Afrika (SADC), Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU). 

“Nasema alichotekeleza Jecha ni dhuluma na mapinduzi ambayo yalilenga kupindua maamuzi halali ya wananchi wa Zanzibar,” alisisitiza Maalim Seif akiwahutubia viongozi na watendaji wa CUF wa wilaya za Unguja.

Alisema yeye na viongozi wenzake wamekuwa wakiwatuliza wananchi na kwenda nao bega kwa bega, wakielewa hakuna popote umma ulipodai haki yao duniani kwa njia za kistaarabu na za kidemokrasia wakashindwa.

“Hivyo tambueni kuwa kimya kingi kina mshindo na haki yetu iliyoporwa haipo mbali kuipata kwani baada ya dhiki ni faraja,” alisema Maalim Seif.

“Jueni kuwa katika kutekeleza hayo zipo njama za waziwazi za kutaka kuipitisha Katiba ambayo haikupendekezwa na Watanzania kupitia maoni yaliwasilishwa kwa Tume ya Jaji Joseph Warioba,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif alisema miongoni mwa njama hizo ni mazungumzo yanayoendelea sasa kujaribu kuibua utaratibu wa kura ya maoni ili kuipitisha Katiba hiyo, chini ya usimamizi wa ZEC na NEC.

Alisema miongoni mwa njama za kuififisha Zanzibar ni mpango wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi na kuwakosesha wananchi fursa ya kufaidi raslimali zao.

Jecha hakupatikana jana kuzungunzia madai hayo, lakini Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alipoulizwa alisema kwa sasa wapo katika mkakati wa kuimarisha chama katika ngazi zote yakiwamo matawi yao.

“Unajua sisi hatuzungumzii tena hayo, uchaguzi ulikwishafanyika na Serikali ikaundwa na sasa inafanya kazi, la msingi tunaimarisha chetu,” alisema Vuai aliyeko katika ziara ya kichama kisiwani Pemba.

Akizungumza katika ofisi za CUF Wilaya ya Kati Unguja, Maalim Seif alisema, “Nataka nikwambieni kilichotendeka kupitia Baraza la Wawakilishi la Zanzibar hivi karibuni wakidai kujadili sheria ya uchimbaji mafuta, ni kiini macho tu, maana hatujaona mabadiliko yoyote katika Katiba ya Jamhuri tukielewa kwamba jambo hilo bado ni suala la Muungano.”

Maalim Seif alihoji pia uhalali wa tamko la SMZ wa kumzuia asiongee na wananchi misikitini, akisema hiyo ni katika njama za kumnyamazisha asiyaeleze hayo.

Hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi za Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed alipiga marufuku hatua ya Maalim Seif kutembelea na kuongea na wananchi misikitini.

Kufuatia hatua hiyo Maalim Seif alihoji akisema, “Je, Mohamed Aboud haelewi wajibu wake, mbona hatujamsikia akikemea uvunjwaji wa Katiba na pia ukiukwaji wa Sheria Na. 5 ya Vyama Vingi vya Siasa ya Mwaka 1992, inayotoa ruhusa kufanya mikutano na maandamano, hayaoni hayo, hajui kuwa yamepigwa marufuku kinyume na Katiba?” 

Friday, October 28, 2016

Mfanyabiashara Arusha kizimbani kwa kunajisi mwanawe

SeeBait

Mfanyabiashara maarufu jijini Arusha na mkazi wa kata ya Sakina, Alistalius Silayo (45) amefikishwa mahakamani akituhumiwa kumnajisi mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 11.

Akisomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Pennina Joackim ilidai kuwa mfanyabiashara huyo alitenda kosa hilo katika vipindi tofauti kati ya Januari na Septemba mwaka huu.

Mwendesha Mashitaka alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Patricia Kisinda kuwa mshtakiwa alikuwa akifanya kosa hilo mara kwa mara katika miezi hiyo eneo la Sakina kwa Iddy yaliko makazi yake.

Alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha Kifungu cha 158 Kifungu kidogo cha 1(a) cha Sheria na Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 na kufanyiwa marekebisho 2002.

Baada ya kusomewa mashitaka, mshitakiwa alikana shitaka hilo na hakimu alisema dhamana iko wazi ya wadhamini wawili wanaotambulika kisheria. 

Mbali ya hilo, pia wadhamini hao lazima wawe na mali isiyohamishika yenye thamani ya zaidi Sh milioni 10 na wadhamini hawaruhusiwi kutoka nje ya Mkoa wa Arusha bila ya kibali cha Mahakama.

Hata hivyo, wadhamini hao walishindwa kukamilisha taratibu za dhamana mahakamani hapo na hakimu aliwapa muda kukamilisha taratibu katika saa za kazi na kuamuru mshtakiwa kurudishwa rumande hadi taratibu zitakapokamilika. 

Kesi hiyo itatajwa tena Novemba 10, mwaka huu kwani Mwanasheria wa Serikali alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.



 
Reviewed by RICH VOICE on Oktoba 28, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...