SERIKALI YATUMIA BILIONI 85 KUPELEKA MAWASILIANO VIJIJINI
Serikali
imesema kuwa imetumia shilingi Bilioni 85 kupeleka mawasiliano vijijini
kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kuzipatia ruzuku
kampuni za simu za mkononi ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata
huduma za mawasiliano.
Hayo
yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng.
Edwin Ngonyani wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwenye Kamati ya Bunge ya Kudumu ya
Miundombinu mjini Dodoma.
“Mfuko
huu unaendelea kuhakikisha kuwa mawasiliano bora yanafika katika maeneo
mengi nchini hususan vijijini na kwenye maeneo ambayo hayana mvuto wa
kibiashara ambapo Takwimu zinabainisha kuwa, tayari
mawasiliano yamefikishwa kwenye kata 443, vijiji 1,939 kuanzia mwezi
Machi 2013 hadi Julai mwaka huu”, amefafanua Naibu Waziri Ngonyani.
Ameongeza
kuwa tayari Mfuko umetiliana saini mkataba na kampuni za simu za
mkononi mwezi Agosti mwaka huu kuhakikisha kuwa zinapeleka mawasiliano
kwenye kata nyingine 75 na vijiji 154.
Aidha,
ametanabaisha kuwa hadi hivi sasa asilimia 94 ya wananchi wanapata
huduma ya mawasiliano nchini na kuongeza kuwa, Serikali kupitia mkataba
wake na Kampuni ya Simu ya Halotel imefikisha mawasiliano kwenye jumla
ya vijiji 3,069 kati ya vijiji 4,000 tangu walipoanza utekelezaji wa
jukumu hilo mwezi Novemba, 2015 na wanatarajia kukamilisha kazi hiyo
ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Kwa
upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya
Miundombinu Mhe. Moshi Kakoso, amezitaka kampuni za simu za mkononi
zinazopeleka mawasiliano vijijini na maeneo yasiyokuwa na mvuto wa
kibiashara ambazo zinapatiwa ruzuku na Serikali kuhakikisha kuwa zinatoa
taarifa sahihi kwa Mfuko huo ikiwemo hatua zilizofikiwa za ujenzi na
usimikaji wa minara na uwepo wa mawasiliano kwenye vijiji husika.
Amewataka
UCSAF kujitangaza na kuweka mabango yao kwenye minara yote nchini
iliyojengwa kupitia ruzuku ya Serikali ili kuwawezesha wananchi kutambua
uwajibikaji wa Serikali katika kufikisha mawasiliano kwa wananchi wake.
Naye,
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta
ya Mawasiliano), Eng. Angelina Madete, amesema kuwa Wizara kupitia UCSAF
itahakikisha kuwa kila mwananchi anafikiwa na mawasiliano kuendana na
jukumu la msingi la Mfuko huo la kufikisha mawasiliano kwa wote.
Mtendaji
Mkuu wa Mfuko huo Eng. Peter Ulanga, amewahakakikishia wajumbe wa
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu kuwa Taasisi yake itashirikiana
na wataalam kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuhakiki kazi
zilizofanywa na kampuni za simu za mkononi za ujenzi na usimikaji wa
minara na uwepo wa mawasiliano kwenye vijiji mbalimbali nchini.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
SERIKALI YATUMIA BILIONI 85 KUPELEKA MAWASILIANO VIJIJINI
Reviewed by RICH VOICE
on
Agosti 31, 2017
Rating:
Hakuna maoni