ijumaa hii ya leooo
Friday, September 30, 2016
Taarifa Ya Kanusho Kuhusu Tangazo La Ajira Serikalini
Kuna
tangazo ambalo linasambazwa kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii lenye
kichwa cha habari ‘’Sekretarieti ya Ajira yatangaza zaidi ya nafasi za
kazi 1,000’’. Likionyesha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inawatangazia watanzania
wenye sifa na uwezo kujaza jumla ya nafasi wazi za kazi 1,101 kwa niaba
ya waajiri mbalimbali Serikalini.
Katibu
wa Sekretarieti ya Ajira anapenda kuwataafu wadau na wananchi wote kwa
ujumla kuwa taarifa hiyo haina ukweli wowote na inalenga kuupotosha
Umma, hivyo wananchi wote wanapaswa kuzipuuza.
Matangazo
yote ambayo hutolewa na Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika
Utumishi wa Umma ni lazima yaonekane kwenye Tovuti ya Sekretarieti ya
Ajira www.ajira.go.tz au portal ya Ajira ambayo ni portal.ajira.go.tz.
Kama
mnavyofahamu hivi karibuni Serikali ilitoa taarifa ya kusitisha Ajira
mpya Serikalini kwa ajili ya zoezi la uhakiki wa Watumishi hewa kama
ambavyo taarifa ilivyotolewa hapo awali, kwa kuwa zoezi hilo bado
halijakamilika tunaomba wananchi wote na wadau wa Sekretarieti ya Ajira
waendelee kuvuta subira hadi pale zoezi hilo litakapokamilika na taarifa
rasmi itatolewa na Mamlaka husika.
Sekretarieti
ya Ajira inapenda kuomba radhi kwa wale wote waliopata usumbufu
kutokana na tangazo hilo lenye nia ya kupotosha Umma.
Aidha,tunaendelea
kuwasisitiza wadau wetu wote kuwa, wanapoona matangazo ya kazi
yanayodaiwa kutolewa na Sekretarieti ya Ajira katika baadhi ya mitandao
ya kijamii wasiyokuwa na uhakika nayo wajiridhishe kwa kuangalia katika
tovuti na portal ya Sekretarieti ya Ajira kabla ya kuyafanyia kazi.
Aidha,
Sekretarieti ya Ajira inapenda kutoa taarifa kuwa haitasita
kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wenye nia ya kuupotosha
umma kupitia taarifa zinazosambazwa ambazo hazina ukweli.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.
Tarehe 30 Septemba, 2016
Friday, September 30, 2016
Chadema Waahirisha Tena Maandamano ya Oparesheni UKUTA
Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe
ametangaza kuwa Operesheni UKUTA iliyokuwa ifanyike Oktoba Mosi
haitofanyika tena.
Mbowe
amesema hayo leo baada ya kimya cha muda mrefu tangu kuahirishwa kwa
maandamano Septemba Mosi. Aidha, Mbowe amesema kuwa hawatataja tarehe ya
kufanya maandamano ili kutompa adui nafasi ya kujipanga. Amesisitiza
kuwa maandamano yapo, ila tarehe hawataweka hadharani.
Operesheni
hii ilikuwa ifanyike Septemba Mosi mwaka huu lakini iliahirishwa ili
kuwapa nafasi viongozi wa dini kuweza kukutana na kujadiliana na Rais
Dkt Magufuli juu ya mustakabali wa hali ya kisiasa nchini kufuatia
kuzuiwa kwa shughuli mbalimbali za kisiasa.
Hadi
leo viongozi wa dini bado hawajakutana na Rais Magufuli licha ya wao
kueleza kuwa Rais Magufuli hajakataa kukutana nao kama inavyoelezwa na
baadhi ya vyombo vya habari
Friday, September 30, 2016
Mapokezi ya Maalim Seif Buguruni yaota mbawa
Mapokezi makubwa yaliyopangwa kufanyika leo jijini Dar es salaam ya
kuwapokea Wajumbe wa Baraza Kuu la CUF na Kamati ya Uongozi ya chama na
Katibu Mkuu Maalim Seif yameota mbawa kufuatia kusitishwa kwa hofu ya kutokuwepo usalama.
Mapema
jana, ilitangazwa kwamba Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif
Hamad, wajumbe wa baraza kuu la CUF na kamati ya uongozi ya chama
wangefanyiwa mapokezi makubwa katika ofisi hizo lakini yaliahirishwa
ghafla baadaye usiku kwa kuhofia kuwapo vurugu.
Kiongozi
wa wabunge wa CUF waliokuwa wameandaa mapokezi hayo, Riziki Shahari
alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa wameahirisha
mapokezi hayo baada ya kujiridhisha kuwa hali ya usalama siyo nzuri.
“Tunazo
taarifa kuwa yapo makundi hatari ya watu yanayoishi ndani ya ofisi huku
yakilindwa na vyombo vya dola tangu ofisi hiyo iporwe na aliyewahi kuwa
mwanachama na kiongozi wa juu wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
akishirikiana na watu wanaomuunga mkono.
“Tunajipa
muda wa kushauriana na viongozi wa juu wa chama chetu huku tukiwaomba
wanachama wote walioko Dar, mikoani na Zanzibar wawe watulivu kwani
chama kina viongozi makini na hawawezi kuwa tayari kuona maisha ya
wanachana na viongozi yanahatarishwa kwa kuigeuza ofisi kuu kuwa uwanja
wa mapambano,” alisema Shahari.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alisema wabunge 41 kati ya
43 wa CUF walioandaa mapokezi hayo walikuwa wamekwishafika Dar es
Salaam, lakini wamechunguza na kubaini kuwa yangeleta maafa.
Hata
hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF – Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema
pamoja na hayo, chama hicho kimeshamalizana na Profesa Lipumba na
kusisitiza kuwa si mwanachama tena.
Friday, September 30, 2016
Utafiti Twaweza: Nchi Haiongozwi Kidikteta
Asilimia
58 ya Watanzania wamepinga kauli za baadhi ya wanasiasa kuwa Rais John
Magufuli anaendesha nchi kidikteta huku asilimia 31 imesema haina
uhakika na jambo hilo.
Aidha,
imeelezwa kuwa asilimia 80 ya wananchi wanaona kwamba baada ya uchaguzi
juhudi za kimaendeleo zipewe kipaumbele na vyama vya siasa.
Akitoa
taarifa za utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti ya Twaweza jana Dar
es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Aidan Eyakuze alisema
ni asilimia 11 pekee ya Watanzania ndiyo waliosema nchi hii inaongozwa
kidikteta.
“Baadhi
ya wanasiasa na wasomi walitafsiri uongozi wa Rais Magufuli kama
udikteta na neno hilo likawa mojawapo ya mambo yaliyounda Ukuta,
asilimia 11 wanakubaliana na wazo hilo lakini asilimia 58 wanalipinga
huku asilimia 31 wanasema hawana uhakika,” alisema Eyakuze.
Alisema
kundi kubwa ambalo limejibu kuwa Rais Magufuli ni dikteta ni la vijana
na watu matajiri na wenye uwezo wa juu kiuchumi kuliko masikini, wazee
na watu wenye elimu ya chini; huku alisema asilimia 29 ya wananchi walio
karibu ya vyama vya upinzani wanamuona Rais kuwa ni dikteta na asilimia
tano ni wa chama tawala yaani CCM.
Aidha,
alisema wananchi wana uelewa tofauti tofauti kuhusu neno udikteta,
asilimia 32 walitafsiri kama kutawala kimabavu, asilimia 15 walitafsiri
kuwa mtu mmoja ndiye mwenye maamuzi ya nchi nzima, huku asilimia 34 ya
watu waliohojiwa hawaelewi maana ya neno hilo.
Katika
demokrasia, Eyakuze alisema asilimia 51 ya Watanzania walisema mikutano
inasaidia kuiwajibisha serikali huku asilimia 49 ikisema mikutano
huvuruga umakini wa serikali na wananchi kudhoofisha shughuli za
kimaendeleo.
Katika
suala la maandamano, asilimia 50 walisema hawawezi kushiriki maandamano
yoyote, asilimia 29 wanaweza kushiriki na asilimia 20 walijibu kuwa
hawajui.
“Kati
ya takwimu hizo, vijana waliosema wako tayari kushiriki maandamano
yoyote na siyo lazima ya ukuta ni asilimia 35, watu wazima ni asilimia
15, wafuasi wa CCM asilimia 27 na wa vyama vya upinzani ni asilimia 43,”
alisema Eyakuze.
Aidha
alisema kuwa miongoni mwa waliosema kuwa hawatajiunga na maandamano
asilimia 45 walisema ni kwa sababu wana wasiwasi itatokea vurugu na
asilimia 29 walisema kwa sababu siyo njia sahihi za kutatua matatizo.
Alisema
wananchi sita kati ya kumi waliunga mkono kuzuiwa kwa mikutano ya
kisiasa wakiwemo wale wa vyama vya upinzani waliunga mkono suala hilo.
“Asilimia
60 waliunga mkono maamuzi ya Rais kuzuia mikutano ya kisiasa huku wazee
wengi zaidi ndio walioonekana kuunga mkono zaidi uamuzi huo ambao ni
asilimia 70 na vijana asilimia 55 na asilimia 31 ya wafuasi wa vyama vya
upinzani wanakubaliana na kuzuiwa kwa maandamano ya Ukuta."
Asilimia
16 wananchi wanafahamu harakati za ukuta na asilimia 79 hawafahamu
harakati hizo na miongoni mwa wanaofahamu uelewa wao kuhusu harakati
hizo ni asilimia 48. Na kwamba kati ya wanaofahamu ukuta asilimia 50
walijibu wanaunga mkono ukuta na asilimia hamsini hawaungi mkono.
“Asilimia
tisa kati ya wanaounga mkono ukuta katika maandamano ya Septemba mosi
walipanga kushiriki ambapo ni pamoja na asilimia tatu ya wale wa chama
tawala,” alisema.
Katika
utafiti huo umeonesha kuwa wananchi hawakubaliani na mbinu zinazotumiwa
na baadhi ya vyama vya upinzani katika kuhakikisha demokrasia
inalindwa.
Friday, September 30, 2016
Zanziar Yapitisha Marekebisho ya Katiba Yanayomzuia Rais wa Zanzibar Kushauriana na Kiongozi wa Upinzani
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imewasilisha marekebisho ya Katiba ya
Zanzibar ya 11 ya mwaka 1984, ambayo yatatoa nafasi na kumpa uwezo Rais
wa Zanzibar, kuchagua wajumbe wa Baraza la Wawakilishi bila ya
kushauriana na Kiongozi wa Upinzani ambaye kwa sasa hayupo katika baraza
hilo.
Kwa
mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, katika marekebisho hayo
vifungu viwili vinahitaji kufanyiwa marekebisho kikiwemo cha 66 kwa
kufanya marekebisho na kufuta maneno ya vyama na kiongozi wa upinzani.
Akifafanua
katika kifungu hicho, alisema lengo lake ni kutoa nafasi kwa Rais wa
Zanzibar kuchagua nafasi mbili za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi bila
ya kushauriana na Kiongozi wa Upinzani katika Baraza ambaye kwa sasa
hayupo, baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kususia Uchaguzi Mkuu wa
marudio mwaka huu, na hivyo kutopata mwakilishi yeyote na hivyo kufutika
kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif
Shariff Hamad alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Haroun
alisema katika mazingira ya sasa katika Baraza la Wawakilishi, hakuna
kiongozi katika Baraza hilo pamoja na vyama vilivyopata wingi wa kura,
hatua ambayo imemfanya Rais kushindwa kuteua wajumbe wawili katika
Baraza la Wawakilishi.
‘Katika
Baraza la Wawakilishi la sasa Rais ameshindwa kuteua wajumbe wawili
katika nafasi kumi ambapo anatakiwa ashauriane na kiongozi wa upinzani
ambaye hayupo kwa sasa,” alifafanua na kuongeza kuwa Kifungu cha 77(2)
kinafuta neno la upinzani lenye uwakilishi ndani ya Baraza la
Wawakilishi.
Akifafanua,
alisema marekebisho ya Katiba yanayopendekezwa mbele ya Baraza la
Wawakilishi, lengo lake kubwa kuimarisha demokrasia na kumpa nafasi Rais
kuchagua wajumbe wa Baraza watakaofanya kazi kwa maslahi ya taifa.
Katiba
ya Zanzibar imempa mamlaka Rais wa Zanzibar kuchagua wajumbe 10 katika
Baraza la Wawakilishi, ambapo nafasi mbili kwa kushauriana na kiongozi
wa upinzani ambaye hayupo kwa sasa.
Wajumbe
watatu wa Baraza la Wawakilishi walioteuliwa kutoka katika vyama vya
upinzani, wanatokana na nafasi 10 kwa mujibu wa uwezo aliopewa Rais na
Katiba. Wajumbe hao watatu kutoka vyama vya upinzani ni Hamad Rashid
Mohamed, Juma Ally Khatib na Said Soud Said.
ijumaa hii ya leooo
Reviewed by RICH VOICE
on
Septemba 10, 2016
Rating:
Hakuna maoni