Rais Magufuli amtumia ujumbe mfalme wa Oman
Rais John Magufuli leo Oktoba 18, 2017 amemtumia ujumbe Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said na wawekezaji wengine wa Oman kuwa atafurahi kuona wanakuja kuwezeka nchini tena kwa haraka na kudai serikali itatoa ushirikiano.
Rais ametuma ujumbe huo kwa mfalme wa Oman kupitia kwa Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman Mhe. Dkt. Mohammed Hamad Al Rumhy aliyeongozana na Waziri wa Uwekezaji wa Oman Mhe. Salem Ben Nasser Al Ismaily na Naibu Waziri wa Utalii Mhe. Maitha Saif Majid, ambao walikua Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuwa nchi hiyo ipo tayari kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuongeza uwekezaji katika viwanda, uzalishaji wa nishati, kuongeza thamani ya madini, kuendeleza sekta ya gesi na mafuta na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo ili kukuza uchumi kwa kasi zaidi.
“Mhe. Dkt. Mohamed naomba ukamwambie Mfalme kuwa namshukuru kwa ujumbe huu na namkaribisha sana Tanzania, nimefurahi kuona mpo tayari kushirikiana nasi kujenga viwanda, kuzalisha mazao na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, sisi tupo tayari hata leo, njooni tushirikiane kwa sababu nyinyi ni ndugu zetu na tutafanya uwekezaji kwa faida yetu sote” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametaka Oman iongeze ushirikiano na Tanzania katika masuala ya utalii na usafiri wa anga, kuwekeza katika usindikaji wa nyama na uvuvi na ushirikiano katika kubadilishana wataalamu wa nyanja mbalimbali wakiwemo walimu wa lugha ya Kiswahili na Kiarabu.
Mbali na hilo Rais Magufuli amemshukuru Mfalme wa Oman kwa msaada kujenga visima vya maji 100 hapa nchini na amemuomba kuungana na Serikali katika safari yake ya kuhamia Dodoma kwa kujenga miundombinu itakayoweka kumbukumbu ya ushirikiano wa kidugu na kihistoria kati ya nchi hizi mbili.
Rais Magufuli amtumia ujumbe mfalme wa Oman
Reviewed by RICH VOICE
on
Oktoba 19, 2017
Rating:
Hakuna maoni