Uchaguzi 2017: Mkutano wa wagombea urais na IEBC Kenya waahirishwa
Tume ya Uchaguzi Kenya imeahirisha mkutano ambao ulikuwa umepangwa kufanyika leo kati ya mwenyekiti wa tume hiyo na wagombea wa urais.
Mkutano huo ulikuwa umepangiwa kufanyika saa nane unusu adhuhuri lakini tume hiyo imetoa taarifa na kusema umeahirishwa.
Uchaguzi mpya umepangiwa kufanyika Alhamisi wiki ijayo.
Hata hivyo, ingawa Rais Uhuru Kenyatta amesisitiza yuko tayari kwa uchaguzi huo na utaendelea, mgombea wa upinzani Raila Odinga alijiondoa wiki iliyopita.
Jana, Bw Odinga, ambaye ni mgombea wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) alitangaza kwamba siku hiyo badala ya kushiriki uchaguzi, wafuasi wake watafanya maandamano makubwa kote nchini.
Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati siku ya Jumatano alikuwa amewalaumu wanasiasa wa kusababisha kuwepo kwa mazingira yanayoifanya vigumu kuandaa uchaguzi huru na wa haki.
Alisema alikuwa anawapa "kadi ya manjano".
Bw Chebukati alikuwa ameahidi kuhudumu kama mpatanishi kati ya wanasiasa hao.
Tume hiyo Jumatano ilipata pigo baada ya mmoja wa makamishna Dkt Roselyn Akombe kutangaza kujiuzulu akiwa Marekani na kusema hana mipango yoyote ya kurejea Kenya hivi karibuni.
Kenyatta kupinga mazungumzo
Rais Kenyatta today alionekana kupinga mkutano Jumatano alipotangaza kwamba hatafanya mazungumzo yoyote na upinzani.
Akihutubu Saboti, Trans Nzoia magharibi mwa nchi hiyo, alisema wale ambao hawataki kushiriki uchaguzi wa 26 Oktoba hawafai kuwazuia watakaotaka kushiriki uchaguzi huo kupiga kura.
"Vile hakuna anayelazimisha mtu kushiriki uchaguzi wa 26 Oktoba, vile vile hakuna aliye na haki ya kuzuia wengine kushiriki," alisema.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi IEBC ilimtangaza Rais Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, akiwa mbele ya mpinzani wake Raila Odinga wa muungano wa upinzani Nasa kwa zaidi ya kura 1.4 milioni.
Bw Odinga alipinga matokeo hayo mahakamani na Mahakama Kuu ikaamua ulijaa kasoro nyingi na kuagiza uchaguzi mpya ufanyike katika kipindi cha siku sitini.
Tume ya uchaguzi ilitangaza tarehe mpya ya uchaguzi kuwa 26 Oktoba lakini Bw Odinga alijiondoa wiki iliyopita akisema mageuzi ambayo yalifaa kutekelezwa kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki hayajatekelezwa.
Uchaguzi 2017: Mkutano wa wagombea urais na IEBC Kenya waahirishwa
Reviewed by RICH VOICE
on
Oktoba 19, 2017
Rating:
Hakuna maoni