EU yajitenga na Netanyahu na Trump kuhusu Jerusalem
Mkuu wa sera ya mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya (EU) amepuuzilia mbali wito wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuutaka umoja huo uutambue mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.
Bi Federica Mogherini amesema mataifa wanachama wa umoja huo hawataitambua Jerusalem kabla ya mwafaka wa mwisho kati ya Israel na Wapalestina kutiwa saini.
Amesema EU imeungana kwa pamoja kusisitiza kwamba Jerusalem inafaa kuwa mji mkuu wa Israel na pia taifa la Wapalestina litakapoundwa.
Alikuwa akihutubu baada ya mkutano ambapo Bw Netanyahu alitoa wito kwa EU kuifuata Marekani katika kuitambua Jerusalem.
Hatua ya Rais wa Marekani kutambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel imeshutumiwa vikali na Wapalestina na pia jamii ya kimataifa.
Aidha, imeyakera sana mataifa ya Kiarabu na Kiislamu.
Maandamano yameshuhudiwa katika maeneo ya Wapalestina Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, na pia katika balozi na Marekani mataifa mbalimbali duniani.
Bi Mogherini, aliyekuwa akihutubu katika kikao na wanahabari Brussels, Ubelgiji akiwa pamoja na Netanyahu, alisema EU itaendelea kukubali "maafikiano ya kimataifa" kuhusu Jerusalem.
"Kuna umoja kamili EU kuhusu hili, kwamba suluhu pekee kwa mzozo wa Israel na Wapalestina ni kuwepo kwa mataifa mawili ambapo Jerusalem itakuwa kwa pamoja mji mkuu wa Israel na mji mkuu wa taifa la Wapalestina.
"EU na nchi wanachama wataendelea kuheshimu maafikiano ya kimataifa kuhusu Jerusalem hadi hadhi kamili ya mji huo mtakatifu iamuliwe, kupitia mazungumzo ya moja kwa moja kati ya wadau wote."
Lakini Bw Netanyahu alisema hatua ya Marekani ilikuwa tu ni "kutambua uhalisia".
Alikuwa amefika Brussels kwa mashauriano na mawaziri wa mambo ya nje wa EU - mara ya kwanza kwa waziri mkuu wa Israel kuzuru mji huo katika kipindi cha zaidi ya miaka 20.
Maandamano yameendelea Mashariki ya Kati kupinga hatua ya Trump, ikiwa ni pamoja na Dahia, ngome ya Hezbollah mjini Beirut.
Akizungumza kutoka mafichoni, kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah alisema: "Trump alifikiria kwamba alipofanya tangazo lake … mataifa kote duniani nan chi za Kiarabu wamekimbia kumuunga mkono.
"Sasa anaonekana kutengwa, anaungwa mkono na Israel pekee. Huu msimamo ni muhimu sana na unafaa kuendelezwa."
Kuuhamisha ubalozi
Kando na kuitambua Jerusalem, Rais Trump alisema pia kwamba meagiza wizara ya mambo ya nje ya Marekani kujiandaa kuuhamisha ubalozi wa Marekani nchini Israel kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem.
Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa mara ya pili Jumatatu alishutumu uamuzi wa Trump wa kuhamisha ubalozi wa Marekani.
Akizungumza Ankara, Uturuki baada ya mazungumzo na mwenzake Recep Tayyip Erdogan, Bw Putin alisema:
"Urusi na Uturuki wanaamini uamuzi wa Marekani wa kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel na kuhamisha ubalozi wa Marekani huko hautasaidia kupatikana kwa suluhu ya mzozo Mashariki ya Kati."
"Kimsingi, hii inaweza kufuta matumaini ya shughuli ya kutafuta amani ya Wapalestina na Waisraeli."
Kwa nini Jerusalem inazozaniwa?
Mzozo kuhusu Jerusalem ni moja ya mzozo mkubwa kati ya Israel na Wapalestina ambao wanaungwa mkono na mataifa ya Kiarabu na Kiislamu.
Mji huo una maeneo matakatifu ya dini tatu zenye kufuata imani ya Ibrahim - Uyahudi, Ukristo na Uislamu - sana maeneo mengi yanapatikana Jerusalem Mashariki.
Israel ilitwaa eneo hilo kutoka Jordan wakati wa vita kati ya nchi za Kiarabu na Israel mwaka 1967 na imekuwa ikiuchukuliwa mji wote kuwa mji wake mkuu ambao hauwezi kugawanywa.
Kwa mujibu wa maafikiano wakati wa mazungumzo ya amani ya Wapalestina na Waisraeli ya 1993, hatima ya mji huo ilifaa kuamuliwa wakati wa hatua za mwisho za mazungumzo.
Hatua ya Israel kudhibiti Jerusalem yote haijawahi kutambuliwa kimataifa na nchi zote zina afisi za kibalozi Tel Aviv.
Tangu 1967, Israel imejenga makazi kadha ya Wayahudi na kuna takriban walowezi 200,000 wa Kiyahudi eneo hilo. Makazi haya yamekuwa yakishutumiwa na jamii ya kimataifa.
Hatua ya Marekani kuitambua Israel itaonekana na baadhi kama kutilia mkazo msimamo wa Israel kwamba makazi hayo ni halali.
EU yajitenga na Netanyahu na Trump kuhusu Jerusalem
Reviewed by RICH VOICE
on
Desemba 12, 2017
Rating:
Hakuna maoni