NEC yathibitisha mgombea wa Chadema kujitoa kwa Nyalandu

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imethibitisha kumtoa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge Singida Kaskazini mgombea kwa tiketi ya Chadema, David Djumbe.

Mgombea huyo ameondolewa kwenye orodha baada ya kutimiza masharti ya kujitoa katika uchaguzi kwa mujibu wa sheria.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima alisema jana kuwa Djumbe alifuata maelekezo kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi.

“Kama Sheria inavyosema Kifungu cha 49(1)(2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 mgombea anaweza kujitoa kwa kuandika barua na kuisaini yeye mwenyewe pamoja na ahadi ya kiapo cha sheria alichoapa mbele ya hakimu.

“Tume haimkubalii wala haimkatalii sababu ni hiari yake. Amewasilisha taarifa hizo na Tume imemfuta katika orodha ya wagombea,” alisema Kailima alipoulizwa jana kuhusu hatima ya mgombea huyo.

Desemba 20, Djumbe aliwasilisha nyaraka za kujitoa katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Januari 13 mwakani akieleza kuwa jina lake lilipelekwa kimakosa.

Mkanganyiko ndani ya Chadema ndiyo uliosababisha jina la Djumbe kupelekwa NEC na kupitishwa kuwa mgombea ubunge Singida Kaskazini.

Wakati Chadema ngazi ya Taifa ikisema haitashiriki katika uchaguzi huo mpaka NEC itakapokutana na wadau kujadili changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi wa udiwani katika kata 43, uongozi wa chama hicho mkoani Singida ulipeleka Tume jina la Djumbe kuwa mgombea.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Singida, Shaban Limu alisema Djumbe aliteuliwa kugombea na kamati ya utendaji ya wilaya.

Alisema wakati anateuliwa uongozi wilaya na mkoa ulikuwa haujawasiliana na makao makuu kujua msimamo juu ya uchaguzi huo.

Jimbo la Singida Kaskazini liko wazi baada ya aliyekuwa mbunge kwa tiketi ya CCM, Lazaro Nyalandu kujivua uanachama wa chama hicho hivyo kupoteza nyadhifa zote ukiwamo ubunge. Alijiunga na Chadema.

Uchaguzi pia unafanyika katika majimbo ya Longido ambako matokeo ya uchaguzi wa ubunge ya mwaka 2015 yalibatilishwa na Mahakama; na Songea Mjini ambako aliyekuwa mbunge kwa tiketi ya CCM, Leonidas Gama alifariki dunia.
NEC yathibitisha mgombea wa Chadema kujitoa kwa Nyalandu NEC yathibitisha mgombea wa Chadema kujitoa kwa Nyalandu Reviewed by RICH VOICE on Desemba 27, 2017 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...