Mapacha walioungana kuzikwa kaburi moja


Marehemu mapacha Maria na Consolata Mwakikuti (20) waliofariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita mjini hapa watazikwa katika kaburi moja kesho.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mapacha hao watazikwa pamoja japo kunatengenezwa majeneza mawili.

Alisema kwa kuwa wakati wa uhai wao mapacha hao walishakataa kutenganishwa, uongozi wa mkoa unatengeneza majeneza mawili kwa sababu ni watu wawili, lakini watazikwa kwenye jeneza moja lenye miili miwili.

Hata hivyo, misalaba itakuwa miwili kwa sababu ni watu wawili tofauti, alisema Kasesela.

Alisema familia za baba na mama wa mapacha hao kutoka Tukuyu, Mbeya na Bukoba, Kagera pamoja na waliokuwa walezi wa mapacha hao, Masista wa Consolata wa hapa Iringa wamekubaliana makaburi ya kuzikwa pia.

“Kwa pamoja tumekubaliana watoto hawa wazikwe katika makaburi ya viongozi wa dini Tosamaganga Iringa," alisema Kasesela. "Sista aliongea nao kabla ya kufariki wakampa nafasi na jukumu la kuhakikisha kwamba wanazikwa hapo.”

Aidha, kaimu mkuu wa mkoa huo alisema wameamua mazishi yafanyike kesho, ili kumsubiri Askofu Mkuu wa Jimbo la Njombe, na Rais wa Baraza la Maaskofu (Tec), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo la Iringa aliye jijini Dar es Salaam kikazi.

Alisema shughuli za kuaga miili hiyo zitaanza saa mbili asubuhi katika Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu).

Baada ya zoezi la kuaga msafara wa mazishi utapita barabara kuu kuelekea Tosamaganga, ili wananchi waweze kutoa heshima zao za mwisho kama watashindwa kufika Rucu.

Mapacha walioungana kuzikwa kaburi moja Mapacha walioungana kuzikwa kaburi moja Reviewed by RICH VOICE on Juni 05, 2018 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...