Wabunge Wahoji Ahadi ya Milioni 50 Kwa Kila Kijiji Iliyotolewa Na Rais Magufuli
Ahadi
ya Chama Cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 ya kutoa Sh. milioni 50
kwa kila kijiji na kila mtaa kwa sehemu za mijini, ambayo
haijatekelezwa kwa miaka miwili mfululizo huenda ikaanza kutekelezwa
baada ya jana Bunge kuitaka serikali kutoa taarifa bungeni kuhusu
utekelezaji wake.
Akiwasilisha
bungeni jijini Dodoma jana taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Bajeti kuhusu makadirio ya bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa
mwaka ujao wa fedha, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Jitu Soni, alisema
pamoja na kwamba serikali iliahidi kutoa Sh. milioni 50 kwa kila
kijiji, hadi sasa hakuna fedha yoyote iliyotolewa.
Alisema
kuwa katika mwaka wa fedha 2016/17, serikali ilitenga Sh. bilioni 60
(Fungu 21) na katika mwaka huu wa fedha ilitenga kiasi hicho cha fedha
kwa ajili ya kufanya utafiti wa majaribio kwa baadhi ya mitaa, vijiji,
kata na shehia kutekeleza mradi huo.
"Hata
hivyo, fedha hizo zilizotengwa katika miaka yote, hakuna fedha yoyote
iliyotolewa licha ya serikali kuahidi na kuweka utaratibu maalum kuhusu
utoaji wa Sh. milioni 50 kwa kila kijiji kupitia Tamisemi," alisema.
"Kamati
ingependa Bunge lako tukufu lipewe taarifa ya utekelezaji wa mradi huu
ikiwamo 'Pilot Study' (utafiti wa majaribio) iliyofanyika," alisema.
Kiongozi
huyo wa kamati pia alisema tathmini ya jumla ya mwenendo wa utoaji wa
fedha za utekelezaji bajeti ya mwaka 2017/18 si wa kuridhisha kwa baadhi
ya mafungu.
"Hadi
kufikia Machi, mwaka huu, kati ya mafungu nane yaliyo chini ya wizara,
ni miwili tu yaliyokuwa yamepokea fedha zaidi ya asilimia 60 ya bajeti
zilizoidhinishwa na Bunge," alisema na kueleza zaidi:
"Kati
ya mafungu 47 ya wizara mbalimbali yanayostahili kupata fedha za
maendeleo ni mafungu 16 tu yamepata fedha zaidi ya asilimia 50."
Pia
alisema mapato yatokanayo na ushuru wa usafirishaji wa fedha na bidhaa
zinazotozwa ushuru wa bidhaa kama pombe kali yameshuka kwa asilimia 30.
"Kamati
inaendelea kuishauri serikali kuhakikisha kwamba sera zake za kikodi
kwa sekta zinazokua ziwe zina lengo la kulea na kuendeleza sekta hizo na
si kukusanya kodi kiasi ambacho kinaathiri hata ukuaji wa sekta
husika,"alisema.
Jitu
pia alisema pamoja na michezo ya kubahatisha kukua kwa kasi na kuipatia
serikali mapato, kamati yake inashauri kupanda kwa ada, tozo na kodi
mbalimbali kwa kuwa kimsingi michezo hiyo si ya kiuzalishaji na imekuwa
na madhara makubwa kwa jamii.
"Katika
nchi za Afrika Mashariki, Tanzania inaongoza kwa kutoza kiwango cha
chini kwenye mapato ghafi ya michezo ya kubahatisha kuliko nchi
nyingine," alisema.
Alitolea mfano Kenya kuwa inatoza asilimia 35, Rwanda asilimia 13 na Uganda inatoza asilimia 20 ya mapato ghafi.
Alisema
kamati inaitaka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT) kusimamia
kikamilifu sheria ili kuhakikisha kwamba wanaoshiriki katika michezo
hiyo wawe wanafikia umri wa miaka 18.
Jitu
pia alisema kamati yake inaishauri serikali kuhakikisha inalipa madeni
yote ya watumishi, makandarasi na wazabuni yaliyohakikiwa.
Wabunge Wahoji Ahadi ya Milioni 50 Kwa Kila Kijiji Iliyotolewa Na Rais Magufuli
Reviewed by RICH VOICE
on
Juni 05, 2018
Rating:
Hakuna maoni