ijumaa hii ya leooo

Friday, September 30, 2016

Taarifa Ya Kanusho Kuhusu Tangazo La Ajira Serikalini


SeeBait

Kuna tangazo ambalo linasambazwa kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii lenye kichwa cha habari ‘’Sekretarieti ya Ajira yatangaza zaidi ya nafasi za kazi 1,000’’. Likionyesha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inawatangazia watanzania wenye sifa na uwezo kujaza jumla ya nafasi wazi za kazi 1,101 kwa niaba ya waajiri mbalimbali Serikalini.

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira anapenda kuwataafu wadau na wananchi wote kwa ujumla kuwa taarifa hiyo haina ukweli wowote na inalenga kuupotosha Umma, hivyo wananchi wote wanapaswa kuzipuuza. 

Matangazo yote ambayo hutolewa na Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni lazima yaonekane kwenye Tovuti ya Sekretarieti ya Ajira www.ajira.go.tz au portal ya Ajira ambayo ni portal.ajira.go.tz.

Kama mnavyofahamu hivi karibuni Serikali ilitoa taarifa ya kusitisha Ajira mpya Serikalini kwa ajili ya zoezi la uhakiki wa Watumishi hewa kama ambavyo taarifa ilivyotolewa hapo awali, kwa kuwa zoezi hilo bado halijakamilika tunaomba wananchi wote na wadau wa Sekretarieti ya Ajira waendelee kuvuta subira hadi pale zoezi hilo litakapokamilika na taarifa rasmi itatolewa na Mamlaka husika.

Sekretarieti ya Ajira inapenda kuomba radhi kwa wale wote waliopata usumbufu kutokana na tangazo hilo lenye nia ya kupotosha Umma. 

Aidha,tunaendelea kuwasisitiza wadau wetu wote kuwa, wanapoona matangazo ya kazi yanayodaiwa kutolewa na Sekretarieti ya Ajira katika baadhi ya mitandao ya kijamii wasiyokuwa na uhakika nayo wajiridhishe kwa kuangalia katika tovuti na portal ya Sekretarieti ya Ajira kabla ya kuyafanyia kazi.

Aidha, Sekretarieti ya Ajira inapenda kutoa taarifa kuwa haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wenye nia ya kuupotosha umma kupitia taarifa zinazosambazwa ambazo hazina ukweli.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Tarehe 30 Septemba, 2016

Friday, September 30, 2016

Chadema Waahirisha Tena Maandamano ya Oparesheni UKUTA


SeeBait


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe ametangaza kuwa Operesheni UKUTA iliyokuwa ifanyike Oktoba Mosi haitofanyika tena.

Mbowe amesema hayo leo baada ya kimya cha muda mrefu tangu kuahirishwa kwa maandamano Septemba Mosi. Aidha, Mbowe amesema kuwa hawatataja tarehe ya kufanya maandamano ili kutompa adui nafasi ya kujipanga. Amesisitiza kuwa maandamano yapo, ila tarehe hawataweka hadharani.

Operesheni hii ilikuwa ifanyike Septemba Mosi mwaka huu lakini iliahirishwa ili kuwapa nafasi viongozi wa dini kuweza kukutana na kujadiliana na Rais Dkt Magufuli juu ya mustakabali wa hali ya kisiasa nchini kufuatia kuzuiwa kwa shughuli mbalimbali za kisiasa.

Hadi leo viongozi wa dini bado hawajakutana na Rais Magufuli licha ya wao kueleza kuwa Rais Magufuli hajakataa kukutana nao kama inavyoelezwa na baadhi ya vyombo vya habari

Friday, September 30, 2016

Mapokezi ya Maalim Seif Buguruni yaota mbawa


SeeBait

Mapokezi makubwa yaliyopangwa kufanyika leo  jijini Dar es salaam ya kuwapokea Wajumbe wa Baraza Kuu la CUF na  Kamati ya Uongozi ya chama na Katibu Mkuu Maalim Seif yameota mbawa kufuatia kusitishwa  kwa hofu ya kutokuwepo usalama.

Mapema jana, ilitangazwa kwamba Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, wajumbe wa baraza kuu la CUF na kamati ya uongozi ya chama wangefanyiwa mapokezi makubwa katika ofisi hizo lakini yaliahirishwa ghafla baadaye usiku kwa kuhofia kuwapo vurugu.

Kiongozi wa wabunge wa CUF waliokuwa wameandaa mapokezi hayo, Riziki Shahari alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa wameahirisha mapokezi hayo baada ya kujiridhisha kuwa hali ya usalama siyo nzuri.

“Tunazo taarifa kuwa yapo makundi hatari ya watu yanayoishi ndani ya ofisi huku yakilindwa na vyombo vya dola tangu ofisi hiyo iporwe na aliyewahi kuwa mwanachama na kiongozi wa juu wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akishirikiana na watu wanaomuunga mkono.

 “Tunajipa muda wa kushauriana na viongozi wa juu wa chama chetu huku tukiwaomba wanachama wote walioko Dar, mikoani na Zanzibar wawe watulivu kwani chama kina viongozi makini na hawawezi kuwa tayari kuona maisha ya wanachana na viongozi yanahatarishwa kwa kuigeuza ofisi kuu kuwa uwanja wa mapambano,” alisema Shahari.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alisema wabunge 41 kati ya 43 wa CUF walioandaa mapokezi hayo walikuwa wamekwishafika Dar es Salaam, lakini wamechunguza na kubaini kuwa yangeleta maafa.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF – Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema pamoja na hayo, chama hicho kimeshamalizana na Profesa Lipumba na kusisitiza kuwa si mwanachama tena.

Friday, September 30, 2016

Utafiti Twaweza: Nchi Haiongozwi Kidikteta


SeeBait

Asilimia 58 ya Watanzania wamepinga kauli za baadhi ya wanasiasa kuwa Rais John Magufuli anaendesha nchi kidikteta huku asilimia 31 imesema haina uhakika na jambo hilo.

Aidha, imeelezwa kuwa asilimia 80 ya wananchi wanaona kwamba baada ya uchaguzi juhudi za kimaendeleo zipewe kipaumbele na vyama vya siasa.

Akitoa taarifa za utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti ya Twaweza jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Aidan Eyakuze alisema ni asilimia 11 pekee ya Watanzania ndiyo waliosema nchi hii inaongozwa kidikteta.

“Baadhi ya wanasiasa na wasomi walitafsiri uongozi wa Rais Magufuli kama udikteta na neno hilo likawa mojawapo ya mambo yaliyounda Ukuta, asilimia 11 wanakubaliana na wazo hilo lakini asilimia 58 wanalipinga huku asilimia 31 wanasema hawana uhakika,” alisema Eyakuze.

Alisema kundi kubwa ambalo limejibu kuwa Rais Magufuli ni dikteta ni la vijana na watu matajiri na wenye uwezo wa juu kiuchumi kuliko masikini, wazee na watu wenye elimu ya chini; huku alisema asilimia 29 ya wananchi walio karibu ya vyama vya upinzani wanamuona Rais kuwa ni dikteta na asilimia tano ni wa chama tawala yaani CCM.

Aidha, alisema wananchi wana uelewa tofauti tofauti kuhusu neno udikteta, asilimia 32 walitafsiri kama kutawala kimabavu, asilimia 15 walitafsiri kuwa mtu mmoja ndiye mwenye maamuzi ya nchi nzima, huku asilimia 34 ya watu waliohojiwa hawaelewi maana ya neno hilo.

Katika demokrasia, Eyakuze alisema asilimia 51 ya Watanzania walisema mikutano inasaidia kuiwajibisha serikali huku asilimia 49 ikisema mikutano huvuruga umakini wa serikali na wananchi kudhoofisha shughuli za kimaendeleo.

Katika suala la maandamano, asilimia 50 walisema hawawezi kushiriki maandamano yoyote, asilimia 29 wanaweza kushiriki na asilimia 20 walijibu kuwa hawajui.

“Kati ya takwimu hizo, vijana waliosema wako tayari kushiriki maandamano yoyote na siyo lazima ya ukuta ni asilimia 35, watu wazima ni asilimia 15, wafuasi wa CCM asilimia 27 na wa vyama vya upinzani ni asilimia 43,” alisema Eyakuze.

Aidha alisema kuwa miongoni mwa waliosema kuwa hawatajiunga na maandamano asilimia 45 walisema ni kwa sababu wana wasiwasi itatokea vurugu na asilimia 29 walisema kwa sababu siyo njia sahihi za kutatua matatizo.

Alisema wananchi sita kati ya kumi waliunga mkono kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa wakiwemo wale wa vyama vya upinzani waliunga mkono suala hilo.

“Asilimia 60 waliunga mkono maamuzi ya Rais kuzuia mikutano ya kisiasa huku wazee wengi zaidi ndio walioonekana kuunga mkono zaidi uamuzi huo ambao ni asilimia 70 na vijana asilimia 55 na asilimia 31 ya wafuasi wa vyama vya upinzani wanakubaliana na kuzuiwa kwa maandamano ya Ukuta."

Asilimia 16 wananchi wanafahamu harakati za ukuta na asilimia 79 hawafahamu harakati hizo na miongoni mwa wanaofahamu uelewa wao kuhusu harakati hizo ni asilimia 48. Na kwamba kati ya wanaofahamu ukuta asilimia 50 walijibu wanaunga mkono ukuta na asilimia hamsini hawaungi mkono.

“Asilimia tisa kati ya wanaounga mkono ukuta katika maandamano ya Septemba mosi walipanga kushiriki ambapo ni pamoja na asilimia tatu ya wale wa chama tawala,” alisema.

Katika utafiti huo umeonesha kuwa wananchi hawakubaliani na mbinu zinazotumiwa na baadhi ya vyama vya upinzani katika kuhakikisha demokrasia inalindwa. 


Friday, September 30, 2016

Zanziar Yapitisha Marekebisho ya Katiba Yanayomzuia Rais wa Zanzibar Kushauriana na Kiongozi wa Upinzani


SeeBait

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imewasilisha marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ya 11 ya mwaka 1984, ambayo yatatoa nafasi na kumpa uwezo Rais wa Zanzibar, kuchagua wajumbe wa Baraza la Wawakilishi bila ya kushauriana na Kiongozi wa Upinzani ambaye kwa sasa hayupo katika baraza hilo.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, katika marekebisho hayo vifungu viwili vinahitaji kufanyiwa marekebisho kikiwemo cha 66 kwa kufanya marekebisho na kufuta maneno ya vyama na kiongozi wa upinzani.

Akifafanua katika kifungu hicho, alisema lengo lake ni kutoa nafasi kwa Rais wa Zanzibar kuchagua nafasi mbili za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi bila ya kushauriana na Kiongozi wa Upinzani katika Baraza ambaye kwa sasa hayupo, baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kususia Uchaguzi Mkuu wa marudio mwaka huu, na hivyo kutopata mwakilishi yeyote na hivyo kufutika kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Haroun alisema katika mazingira ya sasa katika Baraza la Wawakilishi, hakuna kiongozi katika Baraza hilo pamoja na vyama vilivyopata wingi wa kura, hatua ambayo imemfanya Rais kushindwa kuteua wajumbe wawili katika Baraza la Wawakilishi.

‘Katika Baraza la Wawakilishi la sasa Rais ameshindwa kuteua wajumbe wawili katika nafasi kumi ambapo anatakiwa ashauriane na kiongozi wa upinzani ambaye hayupo kwa sasa,” alifafanua na kuongeza kuwa Kifungu cha 77(2) kinafuta neno la upinzani lenye uwakilishi ndani ya Baraza la Wawakilishi.

Akifafanua, alisema marekebisho ya Katiba yanayopendekezwa mbele ya Baraza la Wawakilishi, lengo lake kubwa kuimarisha demokrasia na kumpa nafasi Rais kuchagua wajumbe wa Baraza watakaofanya kazi kwa maslahi ya taifa. 

Katiba ya Zanzibar imempa mamlaka Rais wa Zanzibar kuchagua wajumbe 10 katika Baraza la Wawakilishi, ambapo nafasi mbili kwa kushauriana na kiongozi wa upinzani ambaye hayupo kwa sasa.

Wajumbe watatu wa Baraza la Wawakilishi walioteuliwa kutoka katika vyama vya upinzani, wanatokana na nafasi 10 kwa mujibu wa uwezo aliopewa Rais na Katiba. Wajumbe hao watatu kutoka vyama vya upinzani ni Hamad Rashid Mohamed, Juma Ally Khatib na Said Soud Said.

ijumaa hii ya leooo ijumaa hii ya leooo Reviewed by RICH VOICE on Septemba 10, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...