Thursday, September 8, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi ya Septemba 8



Thursday, September 8, 2016

Mahakimu 11 Wafukuzwa Kazi......Wengine 30 Kikaangoni

Watumishi 34 wa mahakama wakiwemo mahakimu 11, wamefukuzwa kazi kutokana na makosa mbalimbali ya kinidhamu.

Aidha, Tume ya Utumishi wa Mahakama inaendelea kujadili hatma ya mahakimu 30, waliokuwa wanatuhumiwa kuhusika na rushwa na kushinda zao mahakamani ili kuangalia kama walifanya makosa ya kinidhamu.

Jaji Mkuu, Mohammed Chande Othman alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea taarifa za ukaguzi wa mahakama pamoja na uendeshwaji wa mashauri.

Othman alisema watumishi hao, wamefukuzwa kutokana na uamuzi wa kikao cha Tume ya Mahakama, kilichofanyika Agosti 18, mwaka huu baada ya kushughulikia masuala mbalimbali ya kinidhamu.

“Tumewafukuza mahakimu wakazi wafawidhi, mahakimu wa mahakama za Mwanzo za Rombo, Temeke, Bahi na Chamwino na watumishi wengine 23. Hii ni idadi ndogo ambayo ni sawa na asilimia 0.005 ya wafanyakazi wote lakini kwa mahakama ni doa kubwa,” alisema Jaji Mkuu.

Alisema mahakimu hao wamefukuzwa kwa makosa mbalimbali ya kinidhamu, ikiwemo kutumia muhuri wa mahakama kinyume cha taratibu, kuathiri utendaji wa haki kwa kumsaidia mtu kufungua kesi moja katika mahakama mbili pamoja na kufungua kesi ya mirathi bila kuwa na hati ya kifo.

Aliongeza kuwa kuna makosa ya kisheria ambayo jaji au hakimu akikosea kutumia kifungu cha sheria hawajibishwi, lakini kuna makosa ya kinidhamu ambayo yanaondoa sifa ya kuwa hakimu au jaji.

Kuhusu mahakimu walioshinda kesi za rushwa mahakamani, Jaji Chande alisema mahakama inaweza isiwakute na hatia, lakini Tume itaangalia kama walifanya vitendo vya ukosefu wa nidhamu na kuwawajibisha.

Aidha, alisema mahakimu wengine 32 waliokuwa wanakabiliwa na kesi za jinai na kushinda kesi mahakamani, wanafunguliwa mashitaka ya kinidhamu katika Kamati ya Maadili ya Maofisa wa Mahakama kwa sababu inawezekana hawajapatikana na hatia ya kosa la jinai, lakini kama kuna vitendo vya ukosefu wa maadili watawawajibisha kimaadili.

Mahakama Maalumu ya Ufisadi
Katika hatua nyingine, Mahakama Maalumu ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi imeanza rasmi na wiki ijayo Kanuni za Uendeshaji wa mahakama hiyo, zinatarajiwa kuchapishwa. 
Jaji Mkuu Othman alisema mahakama hiyo, imeanza rasmi Julai 18 mwaka huu baada ya Rais John Magufuli kusaini sheria ya uanzishwaji wa mahakama hiyo.

“Wiki ijayo tutachapisha kanuni mbalimbali za uendeshwaji wa mahakama hiyo, ikiwemo jinsi ya kulinda mashahidi pamoja na taratibu za ufunguaji wa kesi,” alisema Othman.

Alisema mahakama hiyo itakuwa na majaji wa kutosha ili kufanya kazi kwa uadilifu na kumaliza kesi kwa wakati, pia haitakuwa ikiahirisha kesi mara kwa mara.

Kuhusu utendaji kazi wa mahakama, Jaji Mkuu alisema mahakama haiwezi kutoa haki kama itakuwa inajificha au kuendeshwa kwa siri, ndiyo maana kwenye maboresho ya mahakama, wameamua kuwapa fursa wananchi kutoa mapendekezo au kero zao kupitia namba za simu pamoja na barua pepe.

Kesi za uchaguzi 
Awali akiwasilisha taarifa za utendaji wa Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi, Wilaya na za Mwanzo, Msajili wa Mahakama Kuu, Ilvin Mugeta alisema baada ya uchaguzi, walipokea kesi 247 za uchaguzi, 53 za kupinga matokeo ya ubunge na 194 za udiwani.

Mugeta alisema tayari wameshamaliza kesi 234, zimebaki 13, lakini hadi kufikia Desemba mwaka huu kesi zote zitakuwa zimemalizika.

Aidha, alisema tathmini waliyoifanya inaonesha kesi zilizopo zinawiana na mahakimu, na kama watawezeshwa kwa vifaa vya kutendea kazi hadi Desemba mwaka huu watamaliza kesi zote zilizofunguliwa mwaka huu.

Mahakama ya Rufaa 
Kwa upande wake, Msajili wa Mahakama ya Rufaa, John Kahyoza alisema kiwango cha kumaliza mashauri katika Mahakama ya Rufaa kimeongezeka, pia wana lengo la kuhakikisha nakala za hukumu zinapatikana siku hukumu na ndani ya siku tatu zitapatikana kwenye tovuti ya Mahakama ya Tanzania.

Aidha, aliwaomba wananchi watoe ushirikiano ili rufaa zisikilizwe na kuisha mapema, kwa sababu kuna watu wanashindwa kufika mahakamani bila sababu za msingi au kutoa visingizio jambo linalosababisha rufaa zao kuchelewa.

Umuhimu wa mahakama
Katika hotuba yake kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria Februari 4, mwaka huu, Rais Magufuli alisema anaitegemea sana Mahakama na aliwaambia majaji na mahakimu nchini kuwa:

“Nawaomba waheshimiwa majaji na waheshimiwa mahakimu, muitangulize Tanzania kwanza. Mkiitanguliza Tanzania kwanza tutaweza kufika mbali na tutaweza kuwasaidia watanzania wengi. 
"Nimeamua nchi iende, na itaenda. Anayefikiri ataikwamisha, atakwama yeye kwa sababu Mungu yuko pamoja na mimi. Na watu ninaowategemea sana ni Mahakama. Mahakama unafunga kila mmoja. Hata Rais nikitaka kufungwa na Mahakama, nafungwa. Mbunge anafungwa, nani anafungwa, nyinyi ndio wenyewe”.
 
 

Thursday, September 8, 2016

Marais EAC Kukutana kwa Dharura Jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyeji wao Rais Magufuli

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mkutano wa 17 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanyika Jijini Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameitisha Mkutano wa 17 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi Wanachama Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Septemba, 2016.

Mkutano huo ambao ulitanguliwa na vikao vya maandalizi vya Makatibu Wakuu na Mawaziri vilivyofanyika Jijini Arusha utajadili agenda kuu nne ambazo ni:- Mahusiano ya kibiashara na uwekezaji kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara (EPA).

Agenda zingine ni Kupokea Taarifa ya Mwezeshaji wa mazungumzo ya Amani nchini Burundi, Mhe. Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Tanzania; Kupata taarifa ya hatua za kukamilisha uanachama wa Sudan Kusini kwenye EAC; na Kuapishwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Rwanda.

Akizungumzia mkutano huo kwa Waandishi wa Habari, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga amesema kuwa mkutano huu umeitishwa kwa dharura ili kuzungumzia agenda hizo muhimu hususan ile ya nchi wanachama kukubaliana kwa pamoja kusaini au kutosaini Mkataba wa EPA ifikapo tarehe 1 Oktoba, 2016.

Kuhusu Mkataba wa EPA, Mhe. Waziri Mahiga alisema kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilianza mazungumzo na Jumuiya ya Ulaya ya kushirikiana kibiashara kupitia EPA miaka 14 iliyopita na kuingia makubaliano ya awali mwaka 2014. 
Alieleza kuwa kwa mujibu wa makubaliano hayo ya awali EU na EAC zilikubaliana Mkataba huo usainiwe kwa pamoja na nchi zote za Jumuiya mwezi Julai 2016 kabla ya kuanza utekelezaji wake.

Hata hivyo Tanzania ilitangaza kutosaini makubaliano hayo kwa sababu mkataba huo unaweza kukwamisha juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania nchi ya Viwanda na Uchumi wa kati ifikapo 2025.

Aidha, Tanzania inahitaji kujadiliana zaidi na nchi wanachama ili kujiridhisha kuwa mkataba huo hautoathiri Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki hususan hatua ya mwanzo ya mkataba ambayo ni Umoja wa Forodha.

Kuhusu nchi nyingine wanachama Mhe. Mahiga alieleza kwamba, tayari Kenya na Rwanda zimesaini mkataba huo huku Uganda ikisubiri majadiliano ya nchi wanachama kabla ya kusaini na Burundi ikijitoa kusaini mkataba huo kwa vile tayari nchi za Ulaya zimeiwekea vikwazo vya kiuchumi.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 07 Septemba 2016.
 
 

Thursday, September 8, 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Akagua makazi yake mapya Dodoma.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa makazi mapya ya Waziri Mkuu katika eneo la Mlimwa na kuagiza umalizike kwa wakati ili aweze kuhamia kama alivyoahidi.

Katika ziara hiyo aliyoifanya jana mchana (Jumatano, Septemba 7, 2016) Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na namna kazi ya ujenzi inavyofanyika.

“Nimekuja kukagua makazi mapya na mahali pa kufanyia kazi. Kazi ya ujenzi inaendelea vizuri, nimejionea mwenyewe na naamini katika kipindi kifupi watakuwa wamekamilisha,” alisema.

Alisema kutokamilika kwa ujenzi huo hauwezi kukwamisha azma yake ya kuhamia Dodoma kwa sababu tayari inafahamika kuwa Makao Makuu ya Ofisi ya Waziri Mkuu yako Dodoma.

Alisema uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma hautokani na shinikizo la kisiasa bali ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko lake ni agizo lililotolewa Oktoba Mosi, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa chama cha TANU.

“Tangu wakati huo Serikali zote ziliendelea kufanya juhudi mbalimbali za kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa kiwango kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo,” alisema.

“Pia tukumbuke kauli ya Mheshimiwa Rais aliyotoa kwenye hotuba yake ya Julai 23, 2016 alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM, na akairudia tena Julai 25, kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa na mimi siku hiyo hiyo nikaweka msisitizo,” alisema.

Alisema uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano wa kuhamia Dodoma unakuja baada ya kuridhishwa na ujenzi wa miundombinu na maeneo ya kutolea huduma za kijamii kwa wageni na wenyeji ikiwemo Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) yenye uwezo wa kutibu magonjwa makubwa kama ya moyo na figo.

Waziri Mkuu alisema tayari Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ina mpango kamambe (master plan) na ina viwanja vya kutosha kujenga makazi na ofisi mbalimbali.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
,,,,,,,

Thursday, September 8, 2016

Wazee wa CHADEMA Wamtuhumu Msajili wa Vyama Kwa Kuandaa Mitego Haramu ya Kukifuta Chama Hicho

Baraza la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) limetoa pongezi kwa Kamati Kuu ya chama hicho kuahirisha maandamano na mikutano ya nchi nzima iliyopewa jina la Ukuta.

Maandamano hayo ambayo yalipangwa kufanyika kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu yaliahirishwa na Kamati Kuu ya chama hicho kwa madai ya kuombwa na viongozi wakuu wa madhehebu ya dini.

Akizungumza katika Makao Makuu ya chama hicho jana, Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Roderick Lutembeka alisema, hatua ya kamati hiyo kuahirisha maandamano hayo ni muhimu na inaonesha jinsi chama hicho kina viongozi wavumilivu.

“Kwa kutambua moyo wa kiuongozi waliouonesha na dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania wote, tunapenda kuwapongeza viongozi wetu wakuu kwa uamuzi huu wa busara ambao umeuthibitishia umma kuwa chama kina viongozi imara,” alisema Lutembeka

Katika hatua nyingine, baraza hilo limesema limebaini kuwepo kwa njama zinazopikwa dhidi ya chama hicho kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Baraza la Vyama vya Siasa nchini, kukifuta chama hicho.

“Taarifa zinaonesha njama hizo zinalenga kukihujumu Chadema kwa kuandaa mitego haramu ya kisiasa ili hatimaye yatolewe mapendekezo ya kukifuta katika orodha ya vyama vya siasa,” alisema Lutembeka  na kuongeza;

“Tarehe 15 Agosti mwaka huu Jaji Mtungi alitangaza kuwa, Baraza la Vyama vya Siasa lilikuwa limeitisha kikao ambacho kingefanyika tarehe 29-30 Agosti kujadili masuala ya hali ya kisiasa nchini. Siku mbili kabla ya kikao Mwenyekiti wa baraza akatangaza kukiahirisha hadi tarehe 3-4 mwezi huu.

“Jambo la kushangaza baada ya busara kutumika kupitia viongozi wa dini kushawishi Chadema kuahirisha kwa kutoa mwanya wa mazungumzo hadi tarehe 1 mwezi ujao, Kamati ya Uongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa ikaibuka tena na kutangaza kuahirisha kikao cha baraza hadi itakapotangazwa tena.

“Wakati taarifa zote hizo zikitolewa na viongozi wa baraza, ofisini hapa (Chadema) hakuna hata barua moja kutoka kwa msajili ya kutuita katika kikao chochote kati ya hivyo. Kuanzia kile cha tarehe 29-30 Agosti, tarehe 3-4 Septemba wala hiyo ya kuahirisha.

“Katika mazingira haya nani ambaye hatashawishika kuamini ofisi ya msajili inatii maagizo ya watawala,” 
 
 

Thursday, September 8, 2016

Profesa Lipumba Aendelea Kupingwa Kila Kona.


Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ameendelea kupingwa ndani ya chama hicho, na safari hii jumuiya ya wanawake wa chama hicho ikiibuka na kumtaka ajiweke kando ili kuepusha mpasuko zaidi.

Aidha, wamewataka wanawake wafuasi wa chama hicho kote nchini, kuunga mkono uongozi wa muda uliowekwa na Baraza Kuu la Uongozi wa CUF hivi karibuni, ambao ulimtangaza Julius Mtatiro kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Uongozi ndani ya chama hicho kilichowahi kuwa kikuu cha upinzani Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini Dodoma jana, Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wanawake wa CUF, Savelina Mwijage ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, alisema kauli yao imelenga kuunga mkono hatua iliyochukuliwa na Baraza la Uongozi dhidi ya wanaotajwa kukiuka Katiba.

Baraza hilo lilikutana Agosti 28, mwaka huu mjini Zanzibar ikiwa ni hatua ya kukabiliana na hali ya hewa iliyochafuka baada ya kundi la wanachama kuvamia Mkutano Mkuu Maalumu wa uchaguzi Agosti 21, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Mwijage aliyefuatana na wabunge wengine wanne wa viti maalumu, amesema wanawake ndani ya CUF wamefedheheshwa na wafuasi wa Profesa Lipumba kwa kufanya vurugu, kudhalilisha wanawake wakati wa mkutano wa Dar es Salaam na pia kukisababishia chama hasara ya Sh milioni 600 zilitozumika kugharamia mkutano huo.

“Tunalaani kwa nguvu zote vitendo vya baadhi ya watu wanaotaka kukivuruga chama, lakini pia kuiingiza nchi katika migogoro ya udini, ukabili, ubara na Uzanzibari. Mbinu hiyo imepitwa na wakati, tunawaomba Watanzania wote wapuuze siasa hizo za uchochezi,” alisema.

Akizungumza hatua ya kusimamishwa kwa baadhi ya viongozi 11 wa juu wa chama hicho, wanaodaiwa kushiriki kukivuruga chama, alisema ni hatua sahihi na kwamba hata Profesa Lipumba hapaswi kuwa nyuma ya vurugu hizo, kwani aliachia madaraka kwa hiyari yake wakati chama kikielekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Kauli ya wanawake hao wa CUF ilikuja saa chache baada ya Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya ambaye ni mbunge pekee wa kike mwenye jimbo kutoka chama hicho, kuliambia Bunge kuwa hajatikiswa na uamuzi wa kumsimamisha uanachama na kwamba anaendelea kutimiza majukumu yake ndani ya chama, ambacho kabla ya mpasuko wa hivi karibuni, ndiye aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara.

Mbali ya Lipumba na Sakaya, wengine waliositishiwa uanachama ni Abdul Kambaya ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Ashura Mustapha, Omar Mhina, Thomas Malima, Kapasha M. Kapasha, Mohamed Habib Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.

Ashura ni mjumbe wa Baraza Kuu na aliwahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma CUF wakati Mnyaa na Kombo, walikuwa wabunge kipindi cha 2010-2015; Mnyaa akiwakilisha Jimbo la Mkanyageni na Kombo Jimbo la Chake Chake, kisiwani Pemba.

Kutokana na kusimamishwa kwa viongozi hao, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alimtangaza Mtatiro aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara kuwa kiongozi wa kamati ya uongozi wa muda, inayowajumuisha pia Ahmed Katani na Mwijage ambao ni wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.

Katani ni Mbunge wa Tandahimba, Mtwara wakati Severina alikuwa mjumbe wa kamati kama hiyo ilipoteuliwa Agosti mwaka jana baada ya Profesa Lipumba kujiuzulu uenyekiti kwa barua ya Agosti 5, mwaka jana.

Baraza hilo lilimteua pia Joram Bashange kukaimu nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbaraka Maharagande kuwa Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma hadi hapo nafasi hizo zitakapojazwa rasmi kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya Chama hicho.
 

Thursday, September 8, 2016

Afariki Kisimani Akimuokoa mbuzi

MKAZI wa Kijiji cha Kazibizyo Kata ya Ng’anzo, Wilayani Bukombe, Sebastian Lumbe (36), amefariki dunia kisimani alimoingia   kumuokoa mbuzi kwa ujira wa Sh 6,000.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika Mtaa wa Misheni   baada ya mbuzi huyo kutumbukia kwenye kisima kinachodaiwa kuwa na urefu wa futi 30.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Misheni, Antony Kuya alithibitisha kutokea   tukio hilo.

Alisema baada ya mbuzi huyo kutumbukia kisimani, mmiliki wake, Marco Sylvester alitangaza ujira wa Sh 6,000 kwa mtu ambaye angefanikiwa kumtoa   na ndipo Lumbe alipojitolea kuingia kisimani humo.

Alisema kabla ya Lumbe kuingia kisimani humo na kukutwa na mauti, walijitokeza watu wawili tofauti lakini kila walipoingia waligundua kisima hicho kilikuwa kirefu.

Kwa sababu hiyo  walighairi  hadi alipofika yeye na kujitosa.

“Baada ya kuingia kisimani alianza kupiga kelele za kuomba msaada.

“Watu waliokuwa karibu na kisima hicho walimtupia kamba lakini wakati anajaribu kuivuta kupanda ilikatika na akaanguka kurudi kisimani.

“Baadaye kijana mmoja, Leonard Mathayo aliingia kujaribu kumuokoa lakini wakati akiwa humo ndani alisema baada ya kukaribia kufika mwisho wa shimo alimkuta akitupa miguu.

“Alipoanza kumfunga kamba ili wamvute  aliishiwa nguvu na kukosa hewa na hivyo ilimlazimu kuomba msaada kutoka nje,” alisema Kuya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo aliwaonya wananchi kuwa waangalifu na visima virefu kama hivyo kwa sababu  ni hatari.
 
 

Thursday, September 8, 2016

Profesa Lipumba Asema Hana mpango wa kuhama CUF wala kuanzisha chama Kingine ........Ataja Sababu Zilizomfanya Amkatae Lowassa

Aliyekuwa mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema hana mpango wa kuhamia chama chochote.
Aidha amesema hana mpango wa kuanzisha chama chake kwa kuwa yeye bado ni Mwenyekiti halali wa CUF kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho.

Akiongea katika kipindi cha Powerbreakfast cha Clouds FM Alhamisi hii, Profesa Lipumba amesema Katibu Mkuu wa CUF anataka kukiua chama cha CUF Tanzania bara.

“Mimi nipo CUF bado, na ni Mwenyekiti halali kwa mujibu wa Katiba na sina mpango wa kuhamia chama kingine,”

“Katibu Mkuu wetu anataka chama hiki upande wa bara kife kabisa na ibaki CHADEMA pekee yake ndio maana anafukuza wabunge.,”

Pia Lipumba amesema Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif alikosea kumnyima mkono Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein kwa kuwa unapoenda kwenye msiba jambo la msiba lilipaswa kutawala.

“Hata mimi nilipokutana na Maalim baada ya kunikatalia kurudi kwenye uenyekiti tulisalimiana.” Alisema Lipumba.

Katika hatua nyingine Lipumba alizungumzia sababu ya kutomkubali Mh. Edward Lowassa kuingia UKAWA.

“Sababu za msingi za kutomkubali Mh. Edward Lowassa kuingia UKAWA, ni kwamba ukiwa katika siasa unahitaji uongozwe na misingi na ‘principals’ na hoja kwamba mnagombea kitu gani, na sisi tulianzisha UKAWA kwa kusema kwamba tutafute nchi, serikali na dola inayowajibika ambayo inatengeneza mambo vizuri, inatumia rasilimali vizuri itapambana na ufisadi na itajenga demokrasia ya kweli katika nchi yetu, ukiwa na misingi hiyo kwamba utataka kiongozi ambaye anaunga mkono misingi hiyo na tulikuwa wote kwenye bunge la katiba na Mh. Edward Lowassa alikuwepo kwenye bunge hilo hakuwa mmoja ya wabunge aliyeunga mkono rasimu ya Katiba,” alisema Lipumba.

Alioongeza, “Kwahiyo ilikuwa ni kinyume kabisa na ile misingi iliyotuunganisha kwamba utataka kiongozi ambaye anaunga mkono misingi hiyo na ukumbuke Mh. Edward Lowassa alikuwepo katika bunge la katiba ya rasimu ya Jaji Warioba na hakuunga mkono rasimu hiyo kwahiyo ilikuwa ni kinyume kabisa na ile misingi iliyotuunganisha na kuanzisha UKAWA kuja kumchukua Edward Lowassa ndiye awe mgombea urais wa watu wanaounga mkono rasimu ya Jaji Warioba,
 
 

Thursday, September 8, 2016

Ray C aonyesha muonekano wake mpya.........Mashabiki Wampa Ushauri Mzito

Msanii wa muziki Rehema Chalamila ‘Ray C’ ameonyesha picha yake ya kwanza toka asaidiwe na jeshi la polisi miezi michache iliyopita baada ya kudaiwa kuzidiwa na matumizi ya Madawa ya kulevya

Jumatano muimbaji huyo aliwaonyesha mashabiki wake muonekano wake mpya hali ambayo imewafanya mashabiki kumtaka kuachana na matumizi ya Madawa ya kulevya kwa kuwa amekuwa akisaidiwa mara kadhaa kuachana na matumizi ya Madawa ya kulevya lakini yeye amekuwa akirudia.

Haya ni baadhi ya maoni ya mashabiki wake.
 
 
 

Thursday, September 8, 2016

Majibu ya Waziri mkuu Majaliwa Leo Bungeni kuhusu wahusika wa mauaji ya askari na Swala la Uchumi wa Nchi

Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania inaendelea kukutana na wadau tofauti wanaohusika na masuala ya uchumi katika kuhakikisha uchumi wa nchi unaendelea kukua.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Hai Mhe. Freeman Mbowe mijini Dodoma aliyetaka kujua hali ya uchumi ilivyo kwa sasa hapa nchini.

Waziri Mkuu  amesema kuwa lengo kuu la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha uchumi wa nchi unaongezeka kupitia nyanja tofauti kwa kushirikiana na taasisi za fedha zilizopo ili kufikia uchumi wa kati kama ilivyoanishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Akizungumza kuhusu suala la midororo wa upokeaji wa mizigo katika bandari nchini, Waziri Mkuu amesema kuwa mdororo huo umetokana na kupungua kwa kiasi cha mizigo na  kushuka kwa uchumi duniani.

Katika suala ya mauaji yaliyotokea Tanga, Mwanza na Vikindu, Waziri Mkuu amesema kuwa usalama wa wananchi utaendelea kuimarishwa huku serikali ikiahidi kupambana vitendo vya mauaji kwa raia na askari katika maeneo mbali mbali nchini.

“Serikali imesikitika sana na jambo hili la mauaji hivyo itahakikisha wauaji hao wanawekwa katika mikono ya Sheria na kuongeza ulinzi kwa maeneo yote nchini kwa kuanzia ngazi ya vitongoji” alifafanua Waziri Mkuu.

Mbali na hayo Waziri Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya dola katika kuthibiti matukio hayo.

Kuhusu suala la uwepo wa tozo katika zao la korosho swali limeibuliwa na Mbunge wa viti maalumu Mhe.Riziki Lulida (CUF), Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Serikali imeshatoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia uondoaji wa Tozo zisizo na maana katika zao la korosho.
,,,,,,,,,,,,,,
 

Thursday, September 8, 2016

Waziri Mkuu: Serikali Haijashindwa Kuongoza Nchi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo macho, haijalala na haijashindwa kuongoza nchi bali imejipanga  kuliongoza Taifa kwa mafanikio makubwa.
 
"Serikali haijashindwa kuongoza nchi. Nataka niwahakikishie waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwamba tutaongoza nchi hii kwa mafanikio makubwa na kazi hiyo imeanza kwa marekebisho makubwa kwa maeneo ambayo tunadhani yatafanya Taifa hili liweze kupata mafanikio makubwa,” amesema.
 
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Septemba 8, 2016) Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali lililoulizwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Bw. Freeman Mbowe, ambaye alitaka kufahamu Serikali ina mkakati gani wa kunusuru mdororo wa uchumi uliopo nchini.
 
Bw. Mbowe alidai kwamba hali ya uchumi imeshuka na kwa mujibu wa taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BOT) uagizaji wa bidhaa kutoka nje umepungua, uuzaji wa bidhaa nje ya nchi na sekta ya ujenzi imesimama hali inayoashiria kudorora kwa uchumi.
 
Kuhusu suala la kupungua kwa mizigo katika bandari na vituo vya forodha, Waziri Mkuu amesema usafirishaji wa mizigo kwa njia ya bahari umeshuka duniani kote kwa sababu ya kushuka kwa hali ya uchumi kutokana na kuporomoka kwa bei ya mafuta na gesi.
 
Hata hivyo Waziri Mkuu amesema tayari wafanyabiashara wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wameihakikishia Serikali kwamba mizigo yao yote itakuwa inapitia Bandari ya Dar es Salaam hasa kwa mkakati wa pamoja wa ujenzi wa reli ya standard gauge inayoanzia Dar es Salaam-Tabora - Isaka.
 
Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema Serikali itahakikisha inaendelea kuimarisha amani na ulinzi kwenye maeneo yote nchini na kwamba vyombo vya dola viko macho. “Watu wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu yakiwemo mauaji watakamatwa popote walipo na kuchukuliwa hatua za kisheria,; amesema.

Amesema hatua hiyo inatokana na matukio ya mauaji yaliyotokea hivi karibuni ambapo raia wasiokuwa na hatia na askari waliuawa katika maeneo ya Vikindu mkoani Pwani, Tanga na Mwanza. Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani

Katika swali lake, Bw. Ngonyani alitaka kujua ya Serikali kuhusu  kukomesha mauaji hayo, yanayotokea kwa watu wasio na hatia pamoja na askari, ambapo Waziri Mkuu, alitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa wananchi na familia, ambazo ndugu zao walipoteza maisha katika mauaji hayo.

Pia ametoa wito kwa Watanzania wote kuhakikisha wanawafichua watu ambao wanawatilia shaka na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ili waweze kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua

Habari na Ofisi ya Waziri Mkuu 
 

Thursday, September 8, 2016

Jeshi La Polisi Latolea Ufafanuzi Taarifa Inayosambazwa Kwenye Mitandao Juu Ya Kukamatwa Watu Wanaokuwa Kwenye Nyumba Za Wageni Mchana

Kamishna wa Polisi Kanda Maalum Dar Es Salaam anatoa rai kwa wakazi wa Jiji la Dar Es salaam na wageni wanaoingia jijini wakitokea mikoani  kupuuza  taarifa za sauti  zinazozagaa katika mitandao ya kijamii kuwa Polisi wanawakamata ovyo watu wanaolala kwenye nyumba za kulala wageni.

Taarifa hizo za uvumi  zinazoendelea kuzagaa  kwenye mitandao ya Kijamii kama WHATSAPP, TELEGRAM na pia zimechapishwa kwenye baadhi ya magazeti kwamba Askari Polisi wanawakamata watu  ovyo mchana wakiwa kwenye nyumba za kulala wageni  kwa madai ya kukamata kwa makosa ya uzembe na uzururaji na pia kutimiza kauli ya Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ‘HAPA NI KAZI TU’.

Kimsingi niwatoe hofu raia wema kuwa tunaendelea na oparesheni za kuwasaka watuhumiwa wa makosa mbalimbali yakiwemo wanaofanya biashara ya nyumba za kulala wageni kinyume cha sheria (guest bubu), majambazi na wahalifu wengine wa makosa mbalimbali.

Aidha taarifa za kuaminika zimebaini kuwa baadhi ya nyumba za kulala wageni zimekuwa zikitumika kuhifadhi magenge ya wahalifu, dada poa na kaka poa, hivyo Jeshi la Polisi tunawajibika kufuatilia na kuwakamata wahalifu.
 
Niwajibu wa Polisi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye nyumba za kulala wageni, Hoteli, migahawa, Vilabu vya vileo,  kumbi za starehe zinazokesha na zisizokesha na watakaobainika kuvunja sheria, hatua kali za kisheria dhidi yao zitachukuliwa. 
Sheria ya Mwenendo ya makosa ya jinai kifungu cha 60(1) (sura ya 77 iliyofanyiwa marekebisho 2002) kinampa nguvu askari kufanya ukaguzi wa maeneo yote yaliyotajwa hapo juu na kumkamata mtu yeyote anayetiliwa shaka akienda kinyume na utaratibu wa biashara hizo.

Sambamba na hayo nawatahadharisha wafanyabiashara wote wa nyumba za kulala wageni wafuate taratibu za kupokea wageni kwa kuandika kwenye vitabu, kuandika namba za vitambulisho vyao na sehemu wanayotoka, na pale watakapomtilia mashaka mteja yeyote watoe taarifa kituo chochote cha polisi.

Pia wenyeviti wa serikali za mitaa na wajumbe wa nyumba kumi wanawajibika kuwatambua wageni wote wanaoingia kwenye himaya zao na kuwachukulia hatua stahiki ili kuimarisha usalama katika jiji letu la  Dar Es salaam.

DAR ES SALAAM BILA UHALIFU INAWEZEKANA, TUSHIRIKIANE KUISAFISHA JIJI LETU

S.N.SIRRO - CP
 KAMISHNA WA POLISI
KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM
 
 

Thursday, September 8, 2016

Makamu wa Rais: Viongozi Na Watumishi Wa Umma Kuchukuliwa Hatua Kali Iwapo Watabainika Kukiuka Taratibu Za Kazi

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameiagiza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Nchi kuchunguza na kuwachukulia hatua kisheria na za kinidhamu viongozi na watumishi wa umma ambao wanakiuka taratibu za kazi kwa ajili ya maslahi yao binafsi.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo 8-Sep-2016 mjini Mtwara wakati anafungua jengo la sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma Kanda ya Kusini ambalo ujenzi wake umegharimu takribani shilingi bilioni MBILI.

Makamu wa Rais amesema iwapo kama hatua hizo zitachukuliwa haraka zitakomesha na kupunguza kasi ya mmomonyoko wa maadili kwa viongozi na watumishi wa umma hali ambayo itaongeza uwajibikaji katika utendaji wa kazi miongoni watendaji hao.

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuiimarisha sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma nchini kwa kuijengea uwezo wa rasilimali watu na fedha kwa kadri hali ya uchumi itakavyo ruhusu ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Makamu wa Rais amewahimiza viongozi na watumishi wa umma kuthamini na wahakikishe walinda maslahi ya umma wakati wote wa utendaji wao wa kazi ili kuondoa malalamiko kwa wananchi.

Makamu wa Rais amesema ni jambo la muhimu kwa sekretarieti hiyo kufutilia mienendo ya viongozi wa umma na kuwabaini wale wanaokwenda kinyume na misingi ya uadilifu na wachukuliwe hatua ipasavyo kabla hawaleta madhara kwa serikali na jamii kwa ujumla.

Makamu wa Rais pia ametoa rai maalum kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara kuitumia ofisi hiyo mpya ya sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma Kanda ya Kusini kwa kutoa taarifa kuhusu mienendo ya viongozi wanaokiuka maadili ya umma katika utendaji wao wa kazi ili waweze kuchukuliwa hatua.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Angela Kairuki amesisitiza kuwa kazi ya kuhakiki mali na madeni ya viongozi wa umma itaendelea kwa kasi nchini na mwaka huu sekretarieti hiyo itahakiki mali za viongozi wapatao 500 kote nchini.

Naye Jaji Mstaafu na Kamishna wa Maadili Nchini Salome Kaganda akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa jengo hilo ameiomba serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kufanikisha zoezi la uhakiki wa mali na madeni ya viongozi kwa nchi nzima.

Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Mtwara.
8-Sep-2016.
 
 

LA LIGA: RONALDO KUREJEA REAL JUMAMOSI BERNABEU NA OSASUNA!

RONALDO-ZOEZICristiano Ronaldo hajacheza Mechi yeyote tangu Julai 10 alipoumia kwenye Fainali ya EURO 2016 huko Paris awakati Nchi yake Portugal ikiifunga France 1-0 na kutwaa Ubingwa wa Ulaya na yeye kucheza Dakika chache za mwanzo na kuumizwa lakini Jumamosi hii huenda akarejea tena Uwanjani kwa mara ya kwanza baada ya kupona.
Msimu huu mpya Ronaldo, ambae ndie Mchezaji Bora Barani Ulaya, hajacheza hata Mechi moja ya Klabu yake Real Madrid na alirejea Mazoezini baada ya Real kutwaa UEFA SUPER CUP walipoibwaga Sevilla mapema Agosti na pia kuzikosa Mechi mbili za La Liga ambazo zote Real walishinda.
Mechi inayofuata kwa Real ni Jumamosi Uwanjani kwao Santiago Bernabeu kwenye La Liga watakapocheza na Osasuna lakini Kocha wa Real Zinedine Zidane huenda akapanga Kikosi mchanganyiko huku akiwa na jicho moja kwenye Mechi inayofuata ya UEFA CHAMPIONZ LIGI watakapocheza Jumatano Septemba 14 tena wakiwa Nyumbani Santiago Bernabeu na Sporting Lisbon ikiwa ni Mechi yao ya kwanza kabisa ya Kundi lao ya Mashindano hayo makubwa kabisa kwa Klabu Barani Ulaya ambayo wao ndio Mabingwa Watetezi.
Huenda Zidane akampa muda Ronaldo Uwanjani ili kumjenga polepole baada ya hivi karibuni kuzidisha kasi ya Mazoezi baada ya kupona Goti lake.
Kwenye La Liga, Real, Barca na Las Palmas ndizo Timu pekee zenye Pointi 6 baada ya kushinda Mechi zao zote 2 za kwanza za Msimu mpya na Ligi hiyo kusimama kwa Wiki 2 kupisha Mechi za Kimataifa.
LA LIGA
Ratiba:
**Saa za Bongo
Ijumaa Septemba 9
2145 Real Sociedad v RCD Espanyol
Jumamosi Septemba 10
1400 Celta de Vigo  v Atletico de Madrid
1700 Real Madrid CF v Osasuna
1915 Malaga CF v Villarreal CF
1915 Sevilla FC v Las Palmas
2130 FC Barcelona   v Deportivo Alaves
Jumapili Septemba 11
1300 Sporting Gijon v CD Leganes
1700 Valencia C.F v Real Betis
1915 Granada CF v SD Eibar
2130 Deportivo La Coruna v Athletic de Bilbao


ULAYA U-21: MARCUS RASHFORD AICHEZEA ENGLAND U-21 KWA MARA YA KWANZA, AFUMUA HETITRIKI!

ENGLAND-U21-RASHFORDENGLAND U-21, Kikosi cha Vijana wa chini ya Miaka 21, sasa wanahitaji ushindi wa Mechi 1 tu ili kutinga Fainali za Mashindano ya Ulaya kwa Vijana wa U-21 baada ya Leo kuinyuka Norway 6-1 huko Colchester kwenye Mechi ya Kundi la 9 huku Marcus Rashford akipiga Bao 3.
England, wakiwa chini ya Meneja Gareth Southgate, Leo walimtumia Marcus Rashford, Kijana wa Man United mwenye Miaka 18, kwa mara ya kwanza kwenye Kikosi hicho baada ya Meneja wa England Sam Allardyce kuridhia aende huko badala ya Kikosi cha Kwanza.
Leo hii Rashford alijibu hilo kwa kupiga Bao 3 moja likiwa la Penati walipoishindilia Norway 6-1 licha ya wapinzani hao kuwa na Kijana Staa wa Real Madrid Martin Odegaard.
++++++++++++++++++++
JE WAJUA?
-MARCUS RASHFORD:
-HUPIGA BAO KILA MECHI YAKE YA KWANZA AKICHEZEA TIMU KWA MARA YA KWANZA!
-Mechi zake za kwanza kwa Man United kwenye Ligi Kuu England na EUROPA LIGI alifunga.
-Mechi yake ya kwanza kwa Kikosi cha Kwanza cha England alifunga.
-Hii Mechi yake ya kwanza kwa England U-21 amefunga.
++++++++++++++++++++
Bao nyingine za England zilifungwa na Lewis Baker, Ruben Loftus-Cheek na Nathaniel Chalobah.
Bao pekee la Norway lilifungwa na Ghayas Zahid.
Sasa England wamebakisha Mechi 2 kwenye Kundi la 9 na wanahitaji Pointi 3 tu kutinga Fainali Mwakani huko Poland.
VIKOSI VILIVYOANZA:
England: Gunn, Iorfa, Targett, Chalobah, Chambers, Hause, Baker, Ward-Prowse, Rashford, Loftus-Cheek, Redmond.
Akiba: Wildsmith, Holding, Hayden, Galloway, Gray, Watmore, Akpom.
Norway: Rossbach, Haraldseid, Jenssen, Grogaard, Fossum, Sorloth, Odegaard, Berge, Daehli, El Younoussi, Selnaes.
Akiba: Dyngeland, Trondsen, Zahid, Rosted, Thorsby, Meling, Espejord.


 

KOMBE LA DUNIA 2018: ARGENTINA BILA MESSI YANASA, NEYMAR AIPAISHA BRAZIL, CAVANI, SUAREZ WAIRUSHA URUGUAY!

CONMEBOL
Kombe la Dunia – Russia 2018
Mechi za Makundi
Matokeo:
Jumatano Septemba 7
Uruguay 4 Paraguay 0
Venezuela 2 Argentina 2   
Chile 0 Bolivia 0     
Brazil 2 Colombia 2 
Peru 2 Ecuador 1       
++++++++++++++++++++++++
NEYMAR-ECUARDOMechi 5 za Kanda ya Nchi za Marekani ya Kusini chini ya Mwamvuli wa Shirikisho lao CONMEBOL kusaka Nchi 4 zitakazotinga moja kwa moja huko Russia Mwaka 2018 kwenye Fainali za Kombe la Dunia zimepigwa Alfajiri ya Leo.
Brazil, wakicheza kwao huko Arena Amazonia, Manaus, waliichapa Colombia 2-1 kwa Bao za Miranda, Dakika ya Pili, na Neymar, Dakika ya 74, huku Bao la Colombia likifungwa na Marquinhos aliejifiunga mwenyewe Dakika ya 36.
Argentina, wakicheza Ugenini na bila ya Kepteni wao Lionel Messi, walitoka Sare 2-2 na Venezuela ambao waliongoza 2-0 kwa Bao za Dakika za 35 na 53 za Anor na Martinez na Argentina kusawazisha Dakika za 58 na 83 kupitia Prattor na Otamendi.
Uruguay, wakiwa kwao, waliishindilia Paraguay 4-0 huku Wafungaji wao wakiwa Edinson Cavani, Bao 2, Rodriguez na Luis Suarez.
++++++++++++++++++++++++
JE WAJUA?
-CONMEBOL itatoa Nchi 4 kutinga Fainali za Kombe la Dunia huko Russia Mwaka 2018.
-Nchi hizo zinaweza kuwa 5 ikiwa Timu itakayomaliza Nafasi ya 5 kwenye Kundi lao itashinda Mechi ya Mchujo dhidi ya Timu nyingine toka Bara jingine ambayo itakuwa ni moja toka Kanda ya Oceania yenye Nchi za Visiwani ambazo ni New Zealand, New Caledonia, Fiji, Papua New Guinea, Solomon Islands na Tahiti.
++++++++++++++++++++++++
Hii ni Raundi ya 8 ya Mechi za Kanda hii na sasa Uruguay wapo kileleni wakifuatia Brazil, Argentina na Ecuador.
MSIMAMO:
SAMERICA-TEBO-SEP7
CONMEBOL
Kombe la Dunia – Russia 2018
Mechi za Makundi
Ratiba/Matokeo:
**Saa za Bongo
Alhamisi Septemba 1
Bolivia 2 Peru 0      
Ijumaa Septemba 2
Colombia 2 Venezuela 0   
Ecuador 0 Brazil 3  
Argentina 1 Uruguay 0     
Paraguay 2 Chile 1  


BAADA VAKESHENI, LIGI KUU ENGLAND DIMBANI JUMAMOSI, YA KWANZA DABI YA MANCHESTER, MAN UNITED-MAN CITY!

MANUNITED-CITY-10SEPBAADA kupumzika kwa Wiki 2 kupisha Mechi za Kimataifa, LIGI KUU ENGLAND, EPL, itarejea tena kilingeni Jumamosi Septemba 10 na Mechi ya kwanza kabisa ni Dabi ya Manchester kati ya Mahasimu Manchester United na Manchester City.
Mechi hii itachezwa Uwanjani Old Trafford na kuzikutanisha Timu ambazo, pamoja na Chelsea, ndizo pekee zilizocheza Mechi zao 3 na kushinda zote na hivyo kuwa kileleni.
Mechi hii, ambayo itachezwa Saa 8 na Nusu Mchana na kusimamiwa na Refa Mark Clattenburg, inawakutanisha Mameneja wapya kwa Klabu zao ambao ni Mahasimu tangu huko Spain walipozioongoza Real Madrid na Barcelona.
++++++++++++++++++++++++++
JE WAJUA?
-Safari hii Ligi hii ya England haina tena Jina la Mdhamini na itajulikana rasmi kama Ligi Kuu tofauti na Msimu uliopita ilipoitwa Barclays Premier League kutokana na udhamini wa Barclays.
+++++++++++++++++++++++++++
Hivi sasa Jose Mourinho, aliekuwa Real Madrid, ni Meneja wa Man United na Pep Guardiola, aliekuwa Barcelona ni Meneja wa Man City.
Mara baada ya mtanange huo wa Dabi, Saa 11 Jioni, zipo Mechi nyingine 6 za EPL ikiwemo ile ya Arsenal kucheza Nyumbani na Southampton na Tottenham kuwa Ugenini kucheza na Stoke City.
Jumamosi itafungwa na Mechi ya Saa 1 na Nusu Usiku huko Anfield ambako Liverpool watacheza na Mabingwa Watetezi Leicester City.
Jumapili ipo Mechi 1 kati ya Swansea City na Chelsea na Jumatatu Usiku pia ipo Mechi moja huko Stadium of Light kati ya Sunderland na Everton.
LIGI KUU ENGLAND
Ratiba:
**Saa za Bongo
Jumamosi Septemba 10
1430 Man United v Man City               
1700 Arsenal v Southampton            
1700 Bournemouth v West Brom          
1700 Burnley v Hull         
1700 Middlesbrough v Crystal Palace              
1700 Stoke v Tottenham            
1700 West Ham v Watford         
1930 Liverpool v Leicester         
Jumapili Septemba 11
1800 Swansea v Chelsea  
Jumatatu Septemba 12
2200 Sunderland v Everton

KUELEKEA DABI YA MANCHESTER: IBRA AMTIA MCHECHETO BRAVO!

IMG-20160908-WA0001Zlatan Ibrahimovic amechochea moto wa Dabi ya Manchester itakayochezwa Jumamosi Uwanjani Old Trafford kwa kumpelekea onyo Kipa mpya wa Manchester City Claudio Bravo kupitia Mtandao wa Jamii wa Facebook.
Bravo, mwenye Miaka 33 na ambae ni Nahodha wa Nchi yake Chile, alijiunga na Man City hivi karibuni kutoka Barcelona na Jumamosi anatarajiwa kukaa Golini kwa mara ya kwanza wakati City ikitua Old Trafford kuwavaa Mahasimu wao Manchester United.
Ibrahimovic, aliejiunga na Man United Msimu huu akitokea PSG na ambae ndie Mfungaji Bora wa Man United kwa sasa, aliposti Video kwenye Facebook ikiwa na kauli ya 'kumtisha' Bravo huku akionekana akifungasha Boksi lenye vifaa vya Mazoezi ili alitume kama Paseli liende Uwanja wa Etihad kwa Bravo.
Bango la Video hiyo lilikuwa na maneno: "Karibu Manchester! Hivi ni vifaa vya Mazoezi, utavihitaji. Ntakuona Jumamosi."
IMG-20160908-WA0000
 

Shirika la Marekani Liberty Media kununua Formula 1

  • Saa 3 zilizopita
Image copyright EPA
Image caption Kampuni ya Liberty Media italipa $4.4bn
Shirika la habari la Liberty limesema litanunua biashara ya mashindano ya magari ya langalanga ya Formula 1, katika mkataba wa thamani ya dola bilioni nne unusu za kimarekani.
Liberty, ambayo inamilikiwa na bilionea John Malone, katika hatua za kwanza itanunua hisa chache katika kampuni hiyo kutoka kwa muungano wa wawekezaji wanaouza hisa.
Baadaye, itachukua udhibiti kamili iwapo maafisa wasimamizi wa mashindano wataidhinisha ununuzi.
Liberty imesema Bernie Ecclestone, ambaye amedhibiti mashindano hayo kwa muda mrefu, ataendelea kuwa afisa mkuu mtendaji wa Formula One.
Image copyright Getty Images
Image caption Bernie Ecclestone (kulia) akiwa na mkuu wa timu ya Red Bull Christian Horner.
Chase Carey, naibu mwenyekiti wa 21st Century Fox, atakuwa mwenyekiti mpya.


Mathieu Flamini: Crystal Palace wamchukua kiungo wa zamani Arsenal

  • Saa moja iliyopita
Image copyright Getty Images
Image caption Mathieu Flamini alishinda Kombe la FA mara tatu akiwa na Arsenal
Crystal Palace wamemchukua kiungo wa kati wa zamani wa Arsenal Mathieu Flamini, ambaye alikuwa amesalia kuwa ajenti huru baada ya kuruhusiwa kuondoka na klabu ya Arsenal majira ya joto.
Flamini, 32, amepewa mkataba wa hadi mwisho wa msimu.
Mchezaji huyo aliondoka kwa Gunners baada ya kucheza mechi 246 vipindi viwili na kushinda vikombe vya FA mara tatu.
Mfaransa huyo pia alishinda Serie A mwaka 2011 miaka mitano aliyokaa AC Milan.
Ndiye mchezaji wa tano kununuliwa na Palace kwa mkataba wa kudumu majira ya sasa.
Flamini alihamia Italia baada ya kukaa miaka minne Arsenal kisha akarejea Emirates mwaka 2013.
Palace wamewanunua pia Andros Townsend, Steve Mandanda, James Tomkins, na Christian Benteke.
Wamempokea pia Loic Remy kwa mkopo kutoka Chelsea.
SHUKRANI ZANGU NI KWA BBC SWAHILI ,MPEKUZI PAMOJA NA SOKA IN BONGO

 
 
 
Reviewed by RICH VOICE on Septemba 08, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...