Friday, December 16, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Ijumaa ya Disemba 16


Friday, December 16, 2016

Mahakama Kuu Yaamuru Mwanafunzi wa UDOM Aliyefukuzwa Chuo kwa Kuongoza Mgomo Arudishwe Masomoni

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dodoma imetengua uamuzi wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ya kumfukuza mwanachuo Phillip Mwakibinga na kuamuru arudishwe ili kumalizia masomo yake.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, John Chaba kwa niaba ya Jaji Awadhi Mohamed aliyekuwa akisikiliza shauri hilo.

Mwakibinga alikuwa akisoma Shahada ya Kiswahili mwaka wa tatu wakati akisimamishwa na alikuwa Waziri Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii. Katika uamuzi huo, mahakama ilisema mlalamikaji hakupewa nafasi ya kusikilizwa na hivyo kukiuka haki ya asili ya mlalamikaji. Pia mlalamikaji hakupewa haki ya kusikilizwa na hakuandikiwa mashtaka rasmi.

“Baraza liliegemea upande moja bila kumhoji wala nafasi ya kusikilizwa na kujitetea,” alisema. 

Mwakibinga alifukuzwa Udom Januari 14, mwaka jana, kwa madai ya kuongoza mgomo ambapo siku hiyo baraza la chuo lilikaa na kumfukuza bila kupewa nafasi ya kusikilizwa.

Alifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kutaka mahakama kutengua uamuzi huo. Kwa mujibu wa wakili wa Mwakibinga, Elias Machibya alisema awali waliomba ruhusa ya kufungua kesi na wakapewa Februari 5, mwaka jana wakiomba kutengua maombi ya baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma.

“Tulipata kibali cha kufungua kuomba kutengua maamuzi ya Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kumfukuza,” alisema.

Alizitaja sababu kuu tatu za kupinga mwanafunzi huyo kufukuzwa chuo kuwa ni pamoja na kutopewa nafasi ya kusikilizwa, hakuna hatua za nidhamu zilizochukuliwa, walimfukuza wakidai aliwahi kuhusika na migomo ya nyuma.

 Alidai barua ya kumfukuza ilisainiwa na Profesa Shaban Mlacha.

Januari 14, mwaka jana uongozi wa Udom ulimfukuza Mwakibinga ambaye wakati huo alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya wanafunzi, Kitivo cha Sayansi ya Elimu ya Jamii, na kupewa barua ya kusimamishwa kutokana na kosa la kuhamasisha mgomo.

Uongozi huo ulisema Mwakibinga amefukuzwa kabisa kwa kuwa alishawahi kujihusisha na mgomo wa mwaka 2010/2011 akafukuzwa lakini akakata rufaa na kuomba msamaha kwenye Kamati nidhamu.

“Baada ya kukata rufaa Kamati ikamuonea huruma ikamrudisha kabla ya kurudi alitakiwa aje na kiapo kutoka kwa mwanasheria kwamba hatajihusisha na mgomo tena lakini akarudia tena kosa hilo."

Mwakibinga amesema amefurahia uamuzi huo kwani ndio sababu ya msingi ya kufungua kesi na mahakama imetenda haki. Alisema anasubiri barua ya hukumu ambayo itatoka kesho ndipo taratibu zake za kurudi chuo zitakapoanza.
 
 

Friday, December 16, 2016

Mkuu Brigedi ya Nyuki JWTZ afariki dunia

KAMANDA wa Brigedi ya Nyuki ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Brigedia Jenerali Cyril Mhaiki, amefariki dunia katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.

Katika salamu zake za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania, Davis Mwamunyange, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, alisema jana kuwa, amepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha Brigedia Jenerali Mhaiki aliyefikwa na mauti juzi.

Dk Shein kwa niaba yake na ya wananchi wote Zanzibar, alisema wamepokea kwa mshtuko, taarifa ya kifo cha Kamanda huyo hodari aliyetoa mchango mkubwa katika shughuli za ulinzi na usalama na maendeleo ya nchi.

Aidha, salamu hizo za rambirambi zilieleza kuwa Brigedia Jenerali Mhaiki ameacha pengo kubwa, si tu kwa familia yake, bali kwa Brigedi ya Nyuki, JWTZ na nchi kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa mchango wake hautosahaulika.

Alimuomba Mwamunyange kuzifikisha salamu hizo za rambirambi kwa wanafamilia, maofisa na wapiganaji wa vikosi vyote vya ulinzi na usalama.

Pamoja na hayo, salamu hizo zilimuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huku akimuomba Mwenyezi Mungu kumlaza mahala pema Kamanda huyo.
 
 

Friday, December 16, 2016

Waziri Mkuu Acharuka....Asema NGO Chonganishi Zitafutwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa miezi sita ya kujitathimini mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yanayofanya kazi zake wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, kama yanafanya kazi kwa misingi ya sheria na maadili.

Baadaye, yatahakikiwa na kama yatabainika yanachochea migogoro, yatafutwa.

Pia, Majaliwa amezicharukia NGOs nyingine zinazoitangaza vibaya Tanzania kimataifa kwa kupiga picha za kudhalilisha watoto wakiwa wanatembea kwenye mawe huku wamevaa kandambili kubwa, kuonesha nchi ni masikini. Ametaka NGOs hizo kuondoka nchini, la sivyo serikali itazishughulikia.

“Hizi NGOs zingine si muondoke, nendeni kwingine mkafanye kazi. Halafu nyie mnaotuma picha za kudhalilisha watoto wakiwa wamevaa kandambili kubwa, kudai nchi za nje eti Tanzania ni masikini, tutawashughulikia,” alisema Majaliwa alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro jana.

Aidha alisema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atakuja wilayani hapo kukagua kazi walizozifanya, wanazozifanya na miradi wanaosaidia jamii.

Majaliwa aliwaambia watumishi hao wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo wakurugenzi wa mashirika yasiyo ya serikali, yanayofanya shughuli zake wilayani hapo, kuwa serikali haitaki mashirika chochezi wa migogoro na itayafuta.

Alisema serikali haitasita kuyafuta mashirika yanayofanya kazi wilayani humo, ambayo yapo kwa nia ya uchochezi na kuacha kufanya kazi katika malengo yaliyokusudiwa.

Waziri Mkuu alisema wilaya hiyo, ina mashirika yasiyo ya serikali 30 ambayo yamesajiliwa, lakini yanayofanya kazi ni 19 tu.

Alisisitiza kuwa haiwezekani serikali isajili mashirika hayo, lakini utendaji kazi wake uwe hafifu.

Alisema ukifuatilia, mashirika hayo utagundua kuwa yanapokea fedha nyingi, lakini hakuna cha maana wanachokifanya kwa wananchi. Alisema serikali ina taarifa ya NGOs hizo zinazopewa fedha na wafadhili.

“Najua taarifa zenu mnapokea kiasi gani cha fedha na mnazifanyia nini, lakini namleta Mkaguzi wa serikali ili akague mnatumiaje fedha zenu, nawapa miezi sita tu halafu ukaguzi utaanza, maana kuna mashirika mengi lakini kazi mnazofanya hazionekani,” alisema Majaliwa.

Alisema baadhi ya mashirika, yana akaunti nchi jirani ya Kenya na mengine kama PWC anapewa Sh bilioni 2.5 kwa mwaka na shirika la UCRT linapokea Sh bilioni 1.5 kwa mwaka, lakini hajui yanafanya nini.

“Nina taarifa zenu mnapata hela nyingi, lakini mnahudumia vipi jamii hakuna, sasa ngojeni ukaguzi ufanyike halafu nitachukua maamuzi maana kila siku Loliondo kuna nini hapa mnasajiliwa halafu hakuna cha maana,” alisema.

“Kuna nini Loliondo, kwani kila mara Loliondo nina taarifa za kila NGOs zinazofanya kazi hapa, najua mnachokifanya, sasa nawaambia serikali haitawafumbia macho kuona hiki ninachokifanya hapa na ikigundulika mnafanya kinyume na matakwa ya usajili tutazifuta”.

Alisema serikali itazifuta NGOs zote, ambazo zitabainika ni kiini cha migogoro Loliondo. Alitoa hadhari kwa kampuni zinazofanya kazi zake bila usajili, kuwa zikigundulika, zitachukuliwa hatua.

Aliwageukia watumishi wa umma na kuwatahadharisha wale wanaotoa taarifa za migogoro ya ndani kwa wahusika wa NGOs na kisha kuzituma nje ya nchi kwenye mitandao ya kijamii na barua pepe.

Alisema kuwa nao watashugulikiwa, kwa kuwa wanapaswa kuwa majibu ya migogoro na si wasambazaji wa habari mbaya za nchi.

Alisisitiza watekeleze kikamilifu kauli ya ‘Hapa Kazi Tu’ ; na si kutumia NGOs kwa ajili ya kudai kuwasaidia wananchi, huku wakijua kuwa wananchi hawanufaiki na fedha hizo wanazopewa na wafadhili Awali akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Wilaya hiyo, Majaliwa alitoa tahadhari kwa madiwani kuacha kushirikiana na watu wa Uhasibu wanaotoa hela kwaajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema baadhi ya madiwani, wanakwamisha miradi ya maendeleo kwa kula fedha kwa sababu ya ukaribu walionao.

Akizungumzia nidhamu ya fedha, Majaliwa alisisitiza kila mtumishi lazima afanye kazi kwa bidii, ikiwemo kutoa huduma bila kuwabagua wananchi kwa itikadi zao za vyama.

Friday, December 16, 2016

Afande Sele aanika sababu za kuitosa ACT Wazalendo

Mwanamuziki mkongwe, Selemani Msindi maarufu kama Afande Sele ameeleza sababu zilizopelekea jana kutangaza kung’atuka ndani ya Chama Cha ACT – Wazalendo mwaka mmoja baada ya harakati za uchaguzi Mkuu ambao aliutumia kugombea ubunge wa Morogoro Mjini.

Afande Sele ameeleza kuwa moja kati ya sababu zilizopelekea yeye kung’atuka ni kutofikia malengo yake ya kuingia ndani ya chama hicho ya kupata ubunge.

“Nimejitoa ACT- Wazalendo kwa makusudi kabisa na hili lilikuwa ni jambo tarajiwa, kitu cha kwanza moja ya matarajio yalikuwa baada ya mimi kuingia ACT nakuwa Mbunge ila sasa sikupata Ubunge na kama ningeupata Ubunge basi nisingejitoa ndani ya chama,” Anasema Afande Sele .

Jana, kupitia ukurasa wake wa Facebook, mwanamuziki huyo alieleza kuwa amechukua uamuzi huo sio kwa bahati mbaya hivyo uamuzi wake uheshimiwe. Alisisitiza kuwa hatajiunga na chama chochote cha siasa hadi pale ambapo ataamua vinginevyo.

Mei mwaka jana, Afande Sele alitangaza kugombea ubunge wa Morogoro mjini kupitia ACT-Wazalendo lakini hakufanikiwa kuupata ubunge wa jimbo hilo kupitia sanduku la kura, Oktoba 25 mwaka jana.
 
 

Friday, December 16, 2016

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Lataka Mmiliki wa Jamii Forums Aachiwe Mara Moja

Kwa muda wa siku tatu sasa Jeshi la Polisi Tanzania linamshikilia Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jamii Media Limited, Maxence Melo katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Dar es Salaam.

Hadi sasa, si Melo, familia yake au wanasheria wake walioelezwa kosa linalomfanya ashikiliwe. Wanasheria wa Melo wameweka kambi katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, lakini hakuna majibu ya maana wanayopewa na wala Melo hafikishwi mahakamani.

Taarifa wanazotoa askari waliopo kituoni hapo, ambazo si taarifa rasmi, ni kwamba Melo anashikiliwa kwa nia ya kumtaka awape polisi majina wanayoyahitaji ya wachangiaji wa masuala mbalimbali katika mtandao wa Jamii Forums kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandaoni huku wakidai ni maelekezo kutoka “juu”.

Siku ya Jumatano, Desemba 14, 2016 polisi wamefika ofisini na nyumbani kwa Melo wakapekua sehemu zote. Taarifa kutoka ofisini kwa Melo zinaonyesha polisi wamechukua nyaraka mbalimbali ikiwamo hati ya kusajili kampuni, leseni ya biashara na nyingine.

Pia polisi wameondoka na wafanyakazi wawili wa Kampuni ya Jamii Forums kwa mahojiano zaidi.

Taarifa nyingine zinaonyesha kuwa polisi wanaomshikilia Melo wanajiapiza kuwa hata kama mawakili wake watakwenda mahakamani hawatamwachia hadi atekeleze wakitakacho.

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) linafuatilia kwa karibu mwenendo na utendaji wa Jeshi la Polisi juu ya suala la uhuru wa kujieleza na kutoa maoni unaotolewa na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977).

Katika siku za karibuni, TEF na Watanzania kwa ujumla wanashuhudia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na Jeshi la Polisi linaloelekea kuacha kuheshimu misingi ya utawala wa Sheria na Katiba ya Tanzania.

Melo kama mtuhumiwa anayo haki ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma katika muda usiozidi saa 24. Kitendo cha polisi kumshikilia kwa siku tatu, ambapo hatujui kama anateswa au la, ni uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu.

Tamko la Haki za Binadamu la Mwaka 1948 linavitaka vyombo vya dola kuheshimu utawala wa sheria ambao pamoja na mambo mengine msingi wake ni kuheshimu mgawanyo wa madaraka (separation of power). Kitendo cha Polisi kuanza kuchukua sheria mkononi kwa kukamatakamata watu, kuwatisha waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu hakikubaliki.

TEF inalitaka Jeshi la Polisi kumwachia mara moja Melo bila masharti au kumfikisha mahakamani na kumfungulia mashitaka kwa mujibu wa sheria ikiwa ana kosa. 

Tunamwomba Rais John Magufuli aingilie kati mzozo huu na kuwafahamisha polisi kuwa wanayoyatenda wanapalilia mbegu ya chuki katika nchi jambo ambalo si jema waliache mara moja.

TEF inaungana na Watanzania kulaani kitendo cha polisi kumkamata Melo kwa kutumia sheria mbaya isiyokubalika ya Makosa ya Mtandaoni. 

TEF inatetea haki ya uhuru wa kutoa mawazo na kukataa ukandamizaji huu wa polisi wanaodai wana maelekezo kutoka juu chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano. Mungu ibariki Tanzania.


Theophil Makunga,
Mwenyekiti,
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Dar es Salaam, Desemba 15, 2016
 
 

Friday, December 16, 2016

Ndalichako Asitisha Ajira za Walimu Wa Masomo ya Sanaa

WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, ametoa masharti mapya ya ajira za ualimu nchini, huku akisema Serikali haitaajiri walimu wa masomo ya sanaa (arts) kwa kuwa wapo wa kutosha.

Akizungumza mjini Dodoma jana wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), Profesa Ndalichako, alisema Serikali kwa sasa haiwezi kuajiri walimu wa masomo hayo kwa kuwa inataka kuajiri walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ambao idadi yao ni ndogo.

“Pamoja na uamuzi huo mpya, ajira za walimu wapya wa masomo ya sayansi nazo zimebadilika kwani wale wote waliohitimu ualimu wa sayansi na hisabati, wanatakiwa watume vyeti vyao kabla ya kupangiwa kituo cha kazi.

“Kuhusu wale walimu wa ‘arts’, kule tuna walimu wa ziada ambao tutajaribu kuwapanga kutokana na shule, kwani wengi walikuwa wamepangwa shule moja. Kwahiyo, tutaangalia utaratibu wa kuwapanga kulingana na mahitaji,’’ alisema Profesa Ndalichako.

Akizungumzia suala la ubora wa elimu nchini, Profesa Ndalichako aliwataka walimu wakuu hao kuhakikisha wanasimamia ubora wa elimu kwa kuwa wao ndio wanaowaandaa wanafunzi kabla hawajaenda vyuoni.

“Vilevile pelekeni takwimu sahihi za wanafunzi waliopo katika shule zenu kuisaidia Serikali katika kupanga bajeti ili iweze kutoa fedha sahihi.

“Hapa kuna kimbembe, yaani wakati mwingine huwa najifanya nimepoteza takwimu ya shule fulani, nikiziomba na kutumiwa, zinakuwa ni tofauti na zile za mwanzo.

“Hili nawaomba mkalisimamie ili iwe rahisi kwetu kupanga bajeti yenye tija,’’ alisema.

Kuhusu ujenzi wa maabara katika shule za sekondari, waziri huyo alisema kwamba kutokana na nyingi kukamilika, Serikali itatoa vifaa vya maabara kuanzia Januari mwakani baada ya kuwa vimeingia nchini kutoka vilikoagizwa.

Awali, akisoma risala ya walimu hao, Rais wa TAHOSSA, Bonus Nyimbo, aliiomba Serikali itoe waraka wa kupiga marufuku matumizi ya simu kwa wanafunzi shuleni kwa kuwa zimekuwa zikichangia kushuka kwa ufaulu kwa baadhi ya wanafunzi.

“Ili kuboresha elimu, tunaiomba Serikali itoe waraka wa kupiga marufuku matumizi ya simu kwa wanafunzi kwani simu nyingi tunazozikamata tunakuta mule hakuna taaluma,’’ alisema Nyimbo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Global Education Link, Abdulmalik Molel, ambaye pia kampuni yake ilipewa tuzo ya heshima katika kuendeleza elimu nchini, alisema ni jukumu la kila mmoja kutimiza wajibu wake ili kuiendeleza elimu ya Tanzania.

“Kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu, wazazi, walezi na walimu, waambieni wanafunzi wasiwe na ‘expectation’ (matarajio) makubwa kwani wanapokuwa na matarajio hayo, wakienda vyuo vikuu wanakuwa wasumbufu,” alisema.

Wakati hayo yakiendelea, juzi taarifa ilitolewa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Maimuna Tarishi, ikisema kwamba, walimu wahitimu wa masomo ya sayansi na hisabati waliohitimu shahada na astashahada mwaka 2015, wanatakiwa kuwasilisha nakala za vyeti vya elimu ya sekondari vya kidato cha nne na sita na taaluma ya ualimu kwa uhakiki.

Pamoja na hayo, hivi karibuni Serikali ilitangaza kusitisha ajira zote nchini ili kukabiliana na wimbi la watumishi hewa.

Sambamba na uamuzi huo, nyongeza za mishahara kwa watumishi wa Serikali nazo zilisimamishwa ili kukabiliana na watumishi hao hewa ambao walikuwa wakiingizia hasara Serikali.
 

Friday, December 16, 2016

Utafiti wa NIMR Wagundua watu 83 waliougua ugonjwa wa zika Hapa Nchini


Watu 83 hapa chini wamegundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa zika kati ya watu 533 waliochukuliwa sampuli za damu.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini (NIMR) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Bugando, umeonyesha kuwa watu hao walipata maambukizi hayo kati ya mwaka 2015 na 2016.

Wakati NIMR ikitoa ripoti yake ya utafiti kuhusu kugundulika watu waliokuwa na virusi vya zika nchini, Januari 31 Serikali ilitoa taarifa kukanusha kuwapo kwa ugonjwa huo nchini.

Taarifa hiyo iliyotolewa kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitaarifu: “Kumekuwepo na taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya kitaifa na kimataifa kuhusu Homa ya Zika ambao ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi kijulikanacho kama “Zika Virus”.

“Ugonjwa wa Homa ya Zika bado haujaingia Tanzania. Wananchi waondoe hofu juu ya uwepo wa ugonjwa huu. Hata hivyo, ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya zika, dengue na malaria ambayo huenezwa kwa namna inayofanana.”

Jana, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk Mwele Malecela alikutana na waandishi wa habari kueleza ripoti ya utafiti wao ikionyesha zika ipo Tanzania na wanaendelea na utafiti kujua ukubwa wa tatizo.

“Utafiti huu ulifanyika kuanzia mwaka 2015 hadi 2016 katika mikoa nane, ambapo jumla ya sampuli 533 za damu zilipimwa na kati yao, watoto wachanga 80 walizaliwa na ulemavu wa viungo mbalimbali ambapo baada ya kufanya utafiti tulibaini asilimia 43.8 ya watoto hao wachanga walikuwa wameambukizwa virusi vya ugonjwa wa zika katika mikoa hiyo,” alisema Dk Malecela.

Aliitaja mikoa iliyofanyiwa utafiti huo kuwa ni Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita, Kigoma, Tabora, Singida na Morogoro na kwamba bado taasisi hiyo na Chuo Kikuu cha Bugando wanaendelea na utafiti huo ili kujua ukubwa wa tatizo hilo katika mikoa hiyo.

Dk Malecela alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo alisema kati ya watu 533 waliopimwa, watu 83 sawa na asilimia 15.6 waligundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa zika na hivyo kupatiwa matibabu ya haraka.

“Kwa wale watoto wachanga 80 waliozaliwa na ulemavu, asilimia 43.8 walikuwa wameambukizwa virusi vya zika na mpaka sasa bado tunaendelea na utafiti kubaini ukubwa wa tatizo hili na kuchukua hatua za haraka,” alisema Dk Malecela.

Alisema kwa sasa wanaendelea na utafiti katika mikoa hiyo kwa wanawake waliopata matatizo ya kuharibika kwa mimba ili kujua ukubwa wa tatizo hilo.

Dk Salvatory Florence kutoka Idara ya Magonjwa ya Watoto ya Hospitali ya Hubert Kairuki alisema ugonjwa huo hauna tiba ni kama ugonjwa wa dengue ulivyo ambapo mgonjwa anapaswa kunywa maji mengi.

Dk Florence ambaye pia ni Mhadhiri Chuo cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki, alisema wajawazito wa miezi mitatu wapo katika hatari ya kuzaa watoto wenye matatizo ya mtindio wa ubongo na watoto wenye vichwa vidogo (microcephalus) endapo wataambukizwa virusi hivyo kupitia kwa mama zao.

“Zika ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi kijulikanacho kama “Zika Virus na unaenezwa na mbu aina ya Aedes ambaye huwa ana tabia ya kuuma asubuhi na pia nyakati za mchana na wakati mwingine jioni,” alisema Dk Florence.

Pia, utafiti wa Nimr ulionyesha kuwa waendesha bodaboda katika mkoa wa Dar es Salaam, wapo hatarini kupata virusi vya Ukimwi.

Utafiti huo uliofanyika katika jiji hilo Agosti mwaka huu, umeonyesha kuwa licha ya madereva hao wa pikipiki kuwa na maambukizi madogo ya VVU kwa asilimia 2.5, bado wapo hatarini kutokana na kuwa na wapenzi wengi huku wengi wao wakigoma kutumia kinga.
 

Friday, December 16, 2016

Kafulila ahama NCCR, ahamia Chadema


Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kigoma Kusini kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila leo ametangaza kukihama chama hicho na kusema kuwa atajiunga na Chama cha Demokrasia na Manendeleo (CHADEMA).

Kafulila ambaye alijizolea umaarufu mkubwa katika bunge la kumi kwa kufichua hoja mbalimbali za ufisadi amesema kuwa ameshawasilisha barua ya kujiuzulu kwa uongozi wa chama hicho.

Akieleza sababu iliyomsukuma kujiunga na CHADEMA, Kafulila alinukuliwa akisema kuwa kikubwa ni kuhakikia wanaleta mabadiliko nchini Tanzania. 

"Ili kufanya safari kuwa fupi, kuondoa vikwazo vya huyu yuko chama hiki mwingine kile nimemamua kujiunga na CHADEMA ili kurahisisha uletaji mabadiliko katika nchi yetu sababu nimeona uhitaji huo," alisema Kafulila.

Katika uchaguzi uliopita Kafulila alipoteza jimbo la Kigoma Kusini ambalo lilikwenda wa Hasna Sudi Katunda Mwilima aliyekuwa akigombea kupitia Chama cha Mapinduzi.
 CHANZO NI MPEKUZI
 
 
 
 
 
Reviewed by RICH VOICE on Desemba 16, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...