habari za leooo.

Friday, December 2, 2016

Aliyetishia kumuua Trump mitandaoni aonja joto la jiwe

Maafisa Usalama wa Rais mteule wa Marekani, Donald Trump wamemtembelea mtu mmoja aliyetishia kumuua kiongozi huyo kwa ujumbe alioweka kwenye mitandao ya kijamii.

Vyanzo vya vyombo vya dola viliuambia mtandao wa TMZ kuwa kikosi maalum cha mashushu wa usalama cha Trump pamoja na Mkuu wa Polisi msaidizi wa Ohio, Jumatatu ya wiki hii walifika nyumbani kwa mtuhumiwa huyo aliyeweka ujumbe wake kwenye mitandao Novemba 14 mwaka huu, ukisioma “Kill Trump” (Muue Trump).

Ilielezwa kuwa kikao kati ya maafisa hao wa usalama nyumbani kwa mtu huyo anayetumia jina la ‘Micah’, kilienda vizuri ambapo aliwaeleza kuwa alikuwa anatania tu huku akisisitza kuwa huenda akapata wazo hilo pale ambapo Trump ataanza kutekeleza ahadi zake tata.

Micah pia alithibitisha kutembelewa na maafisa hao wa usalama na kueleza kuwa waliridhika na maelezo yake kuwa alikuwa anafanya utani tu, hivyo waliondoka.

Trump amekuwa akipata vitisho vya kushambuliwa tangu alipokuwa akiendesha kampeni zake. Mara kadhaa maafisa usalama walimuondoa ghafla jukwaani baada ya kuhisi jaribio la kutaka kumdhuru kutoka kwa wahudhuriaji.
 
 

Friday, December 2, 2016

Godbless Lema Anyimwa Dhamana Kwa Mara Nyingine Tena

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imemnyima dhamana Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA) Godbless Lema. Mahakama hiyo imeeleza kuwa mawakili wamtuhumiwa huyo walipaswa kuonesha kusudio la kukata rufaa ndani ya siku10 kabla ya kukata rufaa.

Hii ni mara ya tano mbunge huyo anakosa dhamana mahakamani tangu alipokamatwa Novemba 3 mwaka huu akiwa mjini Dodoma na kusafirishwa hadi Arusha katika kesi ya uchochezi inayomkabili.

Katika kesi ya msingi lema anatuhumiwa kutoa maneno ya kichochezi dhidi ya Rais Magufuli kwa madai kuwa Mungu ndiye aliyemwambia maneno hayo wakati akiwa anaomba.
 
 

Friday, December 2, 2016

Mahakama Yawaachia Huru Wafuasi wa CHADEMA Waliokuwa Wakikusanya na Kusambaza Matokeo ya Uchaguzi Mkuu

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru wanachama watano wa Chadema pamoja na watu wengine watatu wasio raia wa Tanzania waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhalifu wa kimtandao.

Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage aliwaachia huru washtakiwa hao jana chini ya Kifungu cha 91(1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kusema hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.

Waliachiwa huru, baada ya Wakili wa Serikali, Elia Athanas kuomba kufutwa kesi hiyo chini ya kifungu hicho na Mahakama kuridhia.

Kesi hiyo, imefutwa ikiwa katika hatua ya kuanza kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka baada ya kukamilisha upelelezi wao na washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Oktoba 27, 2015 na kusomewa mashtaka ya makosa ya uhalifu wa kimtandao, wakidaiwa kukusanya na kusambaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015.

Washtakiwa hao ni Mashinda Edwin Mtei, Julius Mwita, Fredrick Eddie Fussi, Meshack Carlos Mlawa na Anisa Nicholaus Rulanyaga.

Mbali na wanachama hao wa Chadema, washtakiwa wengine ambao ni raia wa kigeni ni Julius Mwonga Matei (Kenya), Jose Mavinga Nimi ambaye kwa sasa ni marehemu (Angola) na Kim Hyunwook (Korea) kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo kinyume cha Kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Uhalifu wa Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Kwa pamoja, walidaiwa kuwa kati ya Oktoba 25 na 26, 2015 kwenye maeneo tofauti ndani ya Jiji la Dar es Salaam, walichapisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2015 yasiyo sahihi na ambayo hayakuthibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kwa lengo la kuipotosha jamii.

Walidaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, walichapisha na kusambaza matokeo hayo kupitia mfumo wa uratibu wa uchaguzi uitwao ‘M4C Election Results Management’ na kupitia mitandao mingine ya kijamii, kama vile Facebook na Twitter.

Washtakiwa Matei, Mavinga na Hyunwook wanadaiwa kujihusisha na ajira nchini bila ya kuwa na kibali, kinyume cha Sheria ya Uhamiaji. Wanadaiwa kuwa Oktoba 26, 2015 katika Hoteli ya King D, iliyoko wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, wageni hao walijihusisha katika ajira ya kukusanya na kusambaza matokeo ya uchaguzi wa urais nchini kwa Chadema bila kibali.

Pia wageni hao walidaiwa kujihusisha na shughuli za biashara nchini kwa niaba ya Wanama Saccos, bila ya kuwa na kibali kinyume cha Sheria ya Uhamiaji.
 
 

Friday, December 2, 2016

Tundu Lissu : Tunakuja na staili mpya kumkabili Magufuli

Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema kuwa vyama vya  upinzani vimejipanga vizuri kwaajili ya kukabiliana na Rais Dkt. John Magufuli .

Amesema hayo katika Semina iliyowashirikisha viongozi wa vyama vya upinzani kutoka Mataifa 16 iliyofanyika  Makao Makuu ya Chama hicho Kinondoni Jijini Dar es salaam, amesema  wanapambana kuhakikisha  uwanja wa siasa unakuwa sawa lazima wabadili staili ya kumkabili Rais Magufuli.

Lissu amesema watafanya siasa  ikiwa Magufuli anataka ama hataki, ama wanavunja Sheria ama hawavunji” Akipiga marufuku shughuli za kisiasa, hatuwezi kwenda kanisani kuomba, hapana lazima kazi ziendelee katika aina nyingine”amesema Lissu.

Aidha, Lissu ameongeza kuwa katika Uchaguzi uliopita haukuwa wa haki na huru ambapo mawakala waliokuwa wakihesabu kura walikamatwa  na kupelekwa polisi.

Hata hivyo ameongeza kuwa hali ya kisiasa ilivyo kwa sasa kiongozi yeyote atakayefanya siasa anaonekana kama mhalifu na hukamatwa na kupelekwa mahakamani, hivyo hakuna Demokrasia bali kuna udikteta mkubwa.

riday, December 2, 2016

Waziri Mkuu Majaliwa aiagiza Bodi ya Taifa ya Wahasibu Kuwaanika na Kuwachukulia Hatua Kali Wahasibu Wezi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameiagiza Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu nchini (NBAA) kuwachukulia hatua wale wote wanaoitia doa taaluma hiyo kwa kufanya ubadhilifu wa fedha za umma.

Maagizo hayo yametolewa kwa niaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mpango, wakati wa Uzinduzi wa Kituo cha Taaluma ya Uhasibu (APC) uliokwenda sambamba na ufunguzi wa Mkutano wa mwaka wa wahasibu unaojumuisha wadau kutoka nchi za Afrika Mashariki, katika eneo la Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Amesema kuwa Idadi ya Wahasibu wenye sifa inazidi kuongezeka na hivyo kuisaidia Serikali, japo kuwa Serikali hairidhiki kuona wanataaluma wa Uhasibu na Ukaguzi wa hesabu (CPA) wanaongezeka huku vitendo vya ubadhilifu wa fedha za Umma na ufisadi vikiendelea kuripotiwa.

“Wapo hata wahasibu wanaotumia taaluma yao vibaya, wanaowawezesha wafanyabiashara kukwepa kodi, wanachakachua vitabu vya taarifa za fedha na kufanya ufisadi kwa njia ya kalamu na kompyuta jambo ambalo halikubaliki hata kidogo” Aliongeza Dkt. Mpango

Alisema kuwa machozi ya masikini wa Tanzania yatawafuata mafisadi hadi kaburini lakini serikali ya Awamu ya Tano haitasubiri hao mafisadi wafe, itawatumbua na wala hakuna mzaha na kwamba tayari mahakama ya mafisadi imeanza kazi na itawashughulikia.

Aidha, Waziri huyo wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amewaasa wanataaluma wa uhasibu na ukaguzi wa hesabu kuitumia taaluma yao kuisaidia Serikali katika hatua yake ya kuelekea katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda kwa kuwa taaluma hiyo ina umuhimu mkubwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu, Bw. Pius Maneno alisema kuwa, Kituo hicho kilichozinduliwa cha APC hadi kumalizika, kitagharimu Sh. Bilioni 35 ambapo mpaka sasa fedha zilizotumika ni takribani Sh. Bilioni 31.5.

“Gharama halisi za ujenzi wa kituo hicho zilikuwa Bilioni 14 lakini kutokana na mzabuni wa ujenzi kuchelewesha ujenzi ndio maana kumekuwa na Ongezeko la kiasi hicho cha fedha” aliongeza Bw. Maneno.

Ujenzi wa kituo hicho ambao uko katika eneo lenye ukubwa wa takribani ekari 14 umehusisha ujenzi wa Kumbi za mikutano zinazochukua zaidi ya watu 1600, viwanja vya michezo na vyumba vya kisasa 108 vya kulala wageni.
 
Bw. Maneno alisema kuwa kujengwa kwa kituo hicho kutaifanya Bodi hiyo kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kilichokuwa kikitumika kukodi kumbi za kufanyia na kusahisha mitihani ya Bodi (NBAA).

Alizitaja faida zingine kuwa ni kuboreshwa kwa mazingira ya kitaaluma na wanataaluma wa uhasibu pamoja na kuimarika kwa utawala bora na kuwa chachu ya uchumi wa viwanda, kwa kuwa Kituo hicho, kinatoa elimu bora itakayowawezesha wahitimu kuingia kwenye ushindani ndani ya nchi za Afrika Mashariki na Duniani kwa ujumla.

Ujenzi wa Kituo hicho umedhaminiwa na serikali kupitia mkopo kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii-NSSF, Bodi ya Uhasibu-NBAA na Mbia mwenza wa kituo hicho, Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Serikali-GEPF.

Friday, December 2, 2016

Taarifa kutoka Ikulu: Rais Magufuli amtumia salamu za rambirambi kufutia kifo cha SACP Peter Kakamba

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Ernest Mangu kufuatia kifo cha Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Peter Kakamba kilichotokea tarehe 30 Novemba, 2016 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Katika salamu hizo Rais Magufuli amesema anaungana na askari wote wa Jeshi la Polisi, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na kifo cha SACP Peter Kakamba katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

“Natambua mchango mkubwa alioutoa Marehemu (SACP) Peter Kakamba katika Jeshi la Polisi na katika jukumu kuu la ulinzi wa raia na mali zao, kwa hakika tumempoteza kiongozi aliyekuwa akifanya kazi zake vizuri” amesema Rais Magufuli.

“Nakuomba IGP Ernest Mangu unifikishie salamu nyingi za pole kwa familia ya marehemu, askari na wote walioguswa na msiba huu na sote tumuombee Marehemu (SACP) Peter Kakamba apumzishwe mahali pema peponi, Amina” Amemalizia Rais Magufuli.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

Friday, December 2, 2016

Waziri wa Mambo ya Nje kuongoza ujumbe wa Tanzania Mkutano wa Mawaziri wa Afrika na Korea

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Afrika na Korea unaotarajiwa kufanyika nchini Ethiopia tarehe 06 na 07 Desemba, 2016 mjini Addis Ababa, Ethiopia.
 
Mkutano huu ambao umeandaliwa na Serikali ya Korea kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika una lenga kukuza ushirikiano pamoja na kuandaa maeneo mapya ya ushirikiano baina ya Korea na mataifa ya Afrika katika miaka mitatu ijayo.
 
Tanzania ni moja ya nchi nne (4) za Afrika ambazo Korea imezichagua kuanzisha mahusiano ya kimkakati “strategic partnership” yatakayozifanya nchi hizo kupewa kipaumbele katika kupokea misaada na mikopo nafuu kutoka Korea katika kipindi cha miaka mitano ijayo kati ya 2016 hadi 2020.
 
Katika kipindi hicho Tanzania itapokea kiasi cha dola za Kimarekani milioni 300 ikiwa ni asilimia 17.1 ya msaada utakaotolewa Barani Afrika, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi inayoongoza Barani humo kupata msaada wa Jamhuri ya Korea.
 
Pamoja na ushiriki kwenye Mkutano huo, imependekezwa ufanyike mkutano baina ya Tanzania na Serikali ya Korea kuzungumzia masuala ya ushirikiano baina ya nchi zetu mbili. 

Aidha, ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano wa Afrika na Korea ni fursa muhimu ya kukuza mahusiano baina ya nchi zetu mbili hususan katika Nyanja ya uchumi. Serikali ya Korea ilitoa ahadi ya kuongeza uwekezaji Barani Afrika hususan katikasekta za nishati, miundombinu na viwanda.
 
Itakumbukwa kuwa, tayari Jamhuri ya Korea inashirikiana na Tanzania katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Mradi wa kuendeleza kilimo cha Mwani Zanzibar wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 3.6 na Awamu ya Pili ya Mradi wa kuboresha Uchunguzi wa Afya ya Uzazi Jijini Dar es Salaam wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni nne (4).
 
Miradi mingine ambayo Jamhuri ya Korea inashirikiana na Tanzania ni ujenzi wa Daraja la Selander Jijini Dar es Salaam, Mradi wa Daraja la Kikwete kwenye Mto Malagarasi Mkoani Kigoma na Ujenzi wa Hospitali ya Kimataifa iliyopo eneo la Mloganzila Jijini Dar es Salaam.
 
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 01Desemba, 2016.
 

Friday, December 2, 2016

Askofu Gwajima akutwa na kesi ya kujibu.......Mahakama Yamtaka Ajieleze Disemba 13

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemuona Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima anayekabiliwa na kesi ya kushindwa kuhifadhi silaha, ana kesi ya kujibu.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha alitoa uamuzi huo jana baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wa upande wa Jamhuri pamoja na vielelezo.

Alisema kutokana na ushahidi huo, ameona upande wa Jamhuri umejenga kesi hivyo Gwajima na wenzake watatu, wana haki ya kujitetea, kuita mashahidi au kukaa kimya.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alidai kuwa washtakiwa watajitetea kwa njia ya kiapo na watakuwa na mashahidi watatu.

Hakimu Mkeha alisema Desemba 13, mwaka huu, washtakiwa watajitetea na siku hiyo atasikiliza utetezi wa washtakiwa wote wanne pamoja na mashahidi wao.

Mbali na Gwajima, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni msaidizi wa askofu huyo, Yekonia Bihagaze (39), mfanyabiashara George Mnzava (43) na mkazi wa Kimara Baruti, Geoffrey Milulu (31).

Inadaiwa kuwa, Machi 29 mwaka jana, katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A, washitakiwa walikutwa wakimiliki bastola aina ya Baretta yenye namba CAT 8802 bila kuwa na kibali kutoka mamlaka inayohusika na silaha na milipuko.

Aidha, inadaiwa washtakiwa hao walikuwa wakimiliki isivyo halali risasi tatu za bastola pamoja na risasi 17 za bunduki aina ya shotgun. Gwajima anadaiwa kushindwa kuhifadhi silaha katika hali ya usalama.
 

iday, December 2, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Ijumaa ya Disemba 2





habari za leooo. habari za leooo. Reviewed by RICH VOICE on Desemba 02, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...