habari za leo hizi hapa

Saturday, December 17, 2016

Mbunge Sugu anusurika ajali, mtoto afariki kwenye ajali hiyo

Taarifa zilizoripotiwa na kituo cha runinga cha ITV leo December 17 2016 zinasema kuwa mbunge wa Mbeya mjini ‘CHADEMA’, Joseph Mbilinyi amenusurika kifo katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Iyunga jijini Mbeya baada ya gari lake kufeli break na kumgonga mtoto  ’15’ ambaye amefariki wakati akipelekwa hospitali.

Aidha taarifa hiyo inaeleza kuwa askari polisi wanne wamejeruhiwa baada ya kupata ajali wakati wakielekea kwenye ajali hiyo aliyopata mbunge Joseph Mbilinyi  ‘sugu’
Gari hilo lilikuwa  linaendeshwa na dereva wake, Gabriel Andrew (43) ambaye anashikiliwa na polisi.
 
 

Saturday, December 17, 2016

Dr Mwele Malechela(Aliyetumbuliwa) : Safari itasonga kwa msaada wa Mungu


Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, NIMR, Dr Mwele Malechela, ametoa kauli yake baada ya uteuzi wake kutenguliwa na Rais Dkt John Magufuli, Ijumaa hii.

Kutenguliwa kwake kumekuja siku moja tu baada ya kuzungumza na waandishi na kudai kuwepo kwa virusi vya Zika nchini. Alisema kati ya watu 533 waliopimwa wakati wa utafiti walioufanya, asilimia 15.6 waligunduliwa kuwa na virusi hivyo. Taarifa yake, ilikuja kukanushwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

Akijibu tweet iliyosema, ” Pole sana @mwelentuli safari yako na isonge mbele Dada,” Dr Mwele amesema, “Ahsante na itasonga kwa msaada wa Mungu.”

Tweet nyingine alijibu: Ahsante Mathew. Nilipewa dhamana nimetumikia ninamshukuru Mungu kwa nafasi ya kutumikia WaTanzania kupitia utafiti.”


Saturday, December 17, 2016

Waziri Simbachawene atoa agizo jipya kwa machinga

Waziri wa TAMISEMI George Simbachawene amewataka wamachinga kutotafsiri vibaya agizo la Rais Magufuli kuwa halikumaanisha wafanye biashara kiholela mahala popote bila utaratibu bali wazingatie sheria zilizopo zikiwamo za mipango miji na usafi.

Simbachawene pia amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na mamlaka za serikali za mitaa, kuhakikisha wanatekeleza agizo la Rais John Magufuli la kuwatafutia maeneo ya kufanyia biashara wafanyabiashara hao na kuwashirikisha kwenye mchakato mzima wa kubaini maeneo yenye wateja na miundombinu rafiki.

Aidha, watendaji nao wametakiwa kutotumia tafsiri hiyo kususa na kuwaacha wamachinga wafanye biashara zao kiholela.

Amesema endapo utaratibu huo utafuatwa pamoja na mambo mengine utaweza kurasimisha shughuli za wamachinga hali itakayosaidia pia kundi hilo kuchangia mapato ya halmashauri kwa kiasi kikubwa na kuondoa kabisa tabia ya kufukuzana fukuzana kila kukicha.
 
 

Saturday, December 17, 2016

Mahakama yatupa pingamizi la serikali katika kesi ya mbunge Godbless Lema.

Uamuzi wa kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya nia ya kukata rufaa dhidi ya dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, unatarajiwa kutolewa Desemba 20, mwaka huu na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Uamuzi huo utatolewa baada ya Lema jana kufanikiwa kuwasilisha maombi yake ya kuongezewa muda wa kuleta notisi hiyo ya rufaa dhidi ya dhamana yake baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali pingamizi mbili za mawakili wa Serikali waliokuwa wakitaka maombi hayo yasisikilizwe.
 
Mbele ya Jaji Dk. Modesta Opiyo wa mahakama hiyo, upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili Hashim Ngole, Matenus Marandu, Elizabeth Swai na Adelaide Kasala huku Lema akitetewa na Wakili Sheck Mfinanga na Faraji Mangula.
 
Katika maombi hayo namba 69 ya mwaka huu, baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Dk. Opiyo alisema kuwa atatoa uamuzi huo siku hiyo saa sita mchana.
 
“Baada ya kusikiliza hoja za pande zote nitatoa uamuzi Jumanne ijayo saa sita mchana, msije asubuhi ili nipate muda wa kupitia hoja zenu,” alisema Jaji Dk. Opiyo.
 
Awali, akitoa uamuzi wa pingamizi mbili zilizotolewa Desemba 14, mwaka huu na mawakili hao wa Jamhuri, Jaji Dk. Opiyo, aliyesoma uamuzi huo kwa muda wa dakika 50 kuanzia saa 5:30 asubuhi hadi saa 6:20 mchana, alisema ameamua kuzitupa pingamizi hizo baada ya kuziona hazina mashiko ya kisheria.
 
Alisema kuwa hakuna maombi kama hayo yaliyoacha kusikilizwa mahakamani kwa kushindwa kuonyesha kifungu namba 392 A cha sheria ya uendeshaji wa mashauri ya jinai hivyo akalitupa pingamizi la kwanza la mawakili wa Serikali waliodai maombi hayo hayakufuata utaratibu wa kisheria ikiwemo kutoonyesha vifungu vya sheria waliyoitumia kuleta maombi hayo.
 
“Baada ya kupitia hoja za pande zote, mahakama imeamua kutupa pingamizi hizo za Jamhuri baada ya kuziona kuwa hazina mashiko kisheria na hata upande wa Jamhuri ulishindwa kurejea shauri lolote ambalo limewahi kufanyiwa uamuzi na mahakama za juu kuhusu suala hilo,” alisema Jaji Dk. Opiyo.
 
Akizungumzia hoja ya pili ambayo Jamhuri ilidai ya kiapo kinachounga mkono maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo kimekosewa hivyo hakifai kwa sababu wamejumuisha mambo yasiyotakiwa kisheria ikiwemo maoni, mabishano na hitimisho na kubeba hoja za rufaa alisema mahakama hiyo imeondoa aya ya 11 na 12.
 
Alisema kuwa aya nyingine za 9, 10, 13 na ile ya 17 zitabaki katika hati hiyo ya kiapo kwa sababu hazibebi hoja za rufaa, maoni, mabishano wala hitimisho hivyo mahakama hiyo haiwezi kukataa hati hiyo ya kiapo iliyoambatanishwa na maombi hayo.
 
Akiwasilisha hoja za maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi hiyo ili rufaa hiyo iweze kusikilizwa, Wakili Mfinanga, alidai mahakamani hapo kuwa maombi hayo yamewasilishwa mahakamani hapo chini ya kifungu 361(2) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
 
Alidai kuwa uamuzi wanaotarajia kukatia rufaa ni uliotolewa Novemba 11, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Desderi Kamugisha, ambapo Lema anakabiliwa na kesi namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.
 
Alitaja sababu mbili za msingi za kukatia uamuzi huo rufaa kuwa ni kuiomba mahakama hiyo ipitie makosa ya kisheria yaliyofanywa na mahakama ya chini na kusema kuwa uamuzi huo ulimpa mleta maombi (Lema) dhamana ila kabla hajapewa masharti ya dhamana upande wa Jamhuri ulitoa notisi ya nia ya kukata rufaa.
 
“Kwa msingi huo mahakama ilisema imefungwa mkono na hawawezi kuendelea na jambo lolote kuhusu suala hilo hata uamuzi wake wa kumpa dhamana haukuwezwa kutimizwa na mahakama haikueleza upande wowote ambao haujaridhika na uamuzi huo una haki ya kukata rufaa,” alidai Mfinanga na kuongeza:
 
“Kuna vitu muhimu na vitasahihishwa iwapo tutaleta notisi ya nia ya kukata rufaa na rufaa yenyewe kusikilizwa na mahakama yako ambayo ni msimamizi wa haki na sheria ikatoa ruksa ili tuweze kusikilizwa na rekodi ya mahakama ya chini iweze kurekebishwa, ni muhimu mahakama kuzingatia maombi haya pasipo kuzingatia mambo mengine.”
 
Huku akirejea mashauri mbalimbali ya mahakama za juu, aliendelea kueleza mahakama hiyo kuwa mahakama ikishasema imempa mtu haki ya dhamana lazima itaje masharti ya dhamana.
 
“Tunaomba mahakama itupatie muda tena mfupi ambao hautazidi hata saa 1:30 kwa ajili ya kuleta notisi hiyo ili mahakama iweze kurekebisha makosa hayo,” alisema.
 
Akiwasilisha hoja ya pili, Wakili Mangula, alidai mahakamani hapo kuwa tangu kutolewa kwa uamuzi huo hawajapumzika na muda wote walikuwa mahakamani.
 
Alidai kuwa walikuwa wanaenda mahakamani kwa njia tofauti ili kuiomba mahakama irekebishe makosa hayo ya kisheria.
 
Alidai kuwa baada ya uamuzi huo kutolewa muda wa kazi ulishaisha na ilikuwa Ijumaa hivyo Novemba 14, mwaka huu walipeleka barua ya malalamiko mahakamani hapo na walipoitwa pande zote mbili katika shauri namba 6 lakini walikumbana na pingamizi zilizowasilishwa na mawakili wa Serikali.
 
“Novemba 22, mahakama ilitoa uamuzi na kututaka waleta maombi tukate rufaa na hapo mleta maombi alipata haki yake ya kukata rufaa ambayo haikuelezwa mahakama ya chini na tulitoa notisi tukiamini tuko ndani ya muda na hatimaye rufaa ililetwa mbele ya Jaji Mfawidhi Fatuma Masengi,” alidai.
 
Alieleza mahakama hiyo kuwa katika rufaa hiyo namba 113, walikutana tena na pingamizi la Serikali kuwa wametoa notisi ya rufaa hiyo nje ya muda wa siku moja hivyo hizo ni jitihada walizokuwa wakifanya na si wazembe, wajinga wa sheria kama ilivyodaiwa na wakili wa Serikali.
 
Akijibu hoja za waleta maombi hao, Wakili Ngole, alidai kuwa ni wazembe, wajinga wa sheria na kuwa hata uamuzi wanaolalamikia mahakamani hapo ambao awali ulimpa mleta maombi dhamana, lakini kabla hajapewa masharti ya dhamana mahakama iliingiliwa mamlaka yake hawajawasilisha na maombi hayo.
 
Wakili huyo alidai mahakamani hapo kuwa hakukuwa na makosa yoyote ya kisheria kama inavyodaiwa na waleta maombi hao na kudai kuwa baada ya hakimu kusema mahakama inampa mshtakiwa dhamana Jamhuri kwa haki yake walisimama na kuifahamisha mahakama wana nia ya kukata rufaa.
 
“Ni utaratibu wa kisheria kuwa panapokuwa na notisi ya nia ya kukata rufaa mahakama haiwezi kuendelea na jambo lolote kuhusiana na kesi hiyo, hivyo hakimu asingeweza kuendelea na kesi na inafahamika notisi inasimama badala ya rufaa,” alidai na kuongeza:
 
“Kwa mujibu wa kifungu 359(1) na 361(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, vinaeleza mtu ambaye hajaridhika na hatua yoyote au uamuzi uliotolewa au kupitishwa anaweza kukata rufaa mahakama za juu.”
 
Lema anashikiliwa kwa zaidi ya mwezi mmoja katika mahabusu ya Gereza Kuu  la Kisongo baada ya kukamatwa Novemba 2, mwaka huu nje ya Viwanja vya Bunge mjini Dodoma ambapo alifikishwa mahakamani Novemba 8, mwaka huu akikabiliwa na mashtaka ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. Magufuli.
 
 
 
 

Saturday, December 17, 2016

Waziri Mkuu Amsimamisha Kazi Mwekahazina Wa Wilaya Ya Bahi.......Aagiza arudishwe Longido kujibu tuhuma zinazomkabili

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi aliyekuwa Mwekahazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Issai Mbilu ambaye kwa sasa amehamishiwa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma na kuagiza arudishwe haraka na kuja kujibu tuhuma za ubadhilifu sh. milioni 642.4 za miradi zinazomkabili.

“Tunaendelea kudhibiti na kuweka nidhamu ndani ya Serikali. Ukiharibu Longido usitegemee kuhamishiwa wilaya nyingine tunamalizana hapa hapa. Hatuwezi kuhamisha ugonjwa hapa na kuupeleka wilaya nyingine hivyo Mwekahazina huyu arudishwe haraka Longido,” amesisitiza.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana Ijumaa, Desemba 16, 2016 wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.

Pia amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw. Richard Kwitega kumuandikia barua Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) akimuomba amrudishe Mwekahazina huyo katika kituo chake cha kazi cha zamani ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili.

Amesema Serikali haitamvumilia mtumishi wa idara yoyote atakayeharibu jambo halafu kuhamishwa sehemu nyingine, “hivyo naagiza kuanzia sasa nimemsimamisha kazi Mwekahazina huyu na arudi hapa kujibu kwanini ameleta hasara ya hizi fedha. Na nyie watumishi wengine hili liwe funzo kwenu,” amesema.

Amesema miradi mingi ya maendeleo inakwama kwa sababu ya baadhi ya watumishi kuweka mbele maslahi binafsi badala ya kuzingatia maadili ya utumishi, hivyo amewaagiza Wakuu wa Idara wafuatilie kwa makini miradi inayotekelezwa katika maeneo yao kama inalingana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa.

Akizungumzia kuhusu kushamiri kwa biashara haramu ya dawa za kulevya wilayani Longido, Waziri Mkuu amewaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya kufanya kufanya msako wa nyumba hadi nyumba na kuwakamata wote watakaokutwa wanafanya biashara hiyo.

“Wilaya hii ina sifa mbaya ya kuwa kitovu cha kusafirisha dawa ya kulevya zikiwemo bangi na mirungi. Hivyo nawaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama waendeshe msako kwa kila nyumba na atakayekamatwa achukuliwe hatua. Dawa za kulevya zinadhohofisha nguvu kazi ya Taifa,”.

“Ukivuta bangi unapishana na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu kwani unakwenda kulala jambo ambalo hatuwezi kulikubali. Watakaokutwa wanauza au kununua mirungi na bangi wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa pamoja na kutaifisha magari yanayotumika kubeba bidhaa hiyo haramu,” amesema.

Awali, Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Daniel Chongolo akisoma Taarifa ya Wilaya amesema Longido inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutumika kama njia kuu ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi kwenda nchi jirani ya Kenya ambako biashara hiyo imehalalishwa.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa hospitali ya wilaya hali inayofanya wananchi kwenda kutibiwa Kenya, ambapo Waziri Mkuu alisema haiwezekani wakakosa hospitali ya wilaya hivyo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikiusha anatenga fedha za ujenzi huo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali ipo mbioni kujenga kiwanda cha kuchakata madini ya magadi soda ili yawe na ubora na thamani kubwa. Ametoa kauli hiyo aliposimamishwa na wananchi katika kijiji cha Loonolwo kilichopo Kata ya Gelai Merugoi Wilayani Longido akitokea wilayani Ngorongoro.

Amesema lengo la kujenga kiwanda hicho ni kuwawezesha wananchi wa wilaya hiyo hasa akinamama wanaoishi karibu na Ziwa Natron linalotoa magadi hayo waweze kunufaika na uwepo wa ziwa hilo.

Waziri Mkuu amesema ujenzi wa kiwanda hicho utawezesha vijana na akinamama hao wanaouza magadi maeneo ya pembezoni mwa barabara katika ziwa Natron kupata ajira kwa kuwa kitazalisha ajira zaidi ya 500 katika wilaya hizo mbili za Longido na Ngorongoro.

Pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo kushirikiana na wataalam wake kufanya tathimini ya uhaba wa chakula katika wilaya za Longido na Ngorongoro ili Serikali ijue Mkoa wa Arusha una ukosefu wa chakula kwa kiasi gani.

"Gambo fanya tathimini ya hali ya njaa katika wilaya hizi mbili ili tuweze kuwasaidia wananchi hawa. Hata hivyo nawaomba wananchi mtunze kiasi cha chakula mlichonacho na marufuku tumia nafaka kwa ajili ya kupika pombe,” amesema.

Awali, wananchi hao waliokuwa na mabango mbalimbali walilalamikia kero ya mipaka ya ardhi kati ya vijiji vya wilaya za Longido na Ngorongoro, ambapo Waziri Mkuu alimuagiza Afisa Ardhi Mkoa wa Arusha, Bw. Hamdoun Mansour kwenda katika vijiji hivyo vya mpakani na kukutana na viongozi wa kimila ili kumaliza mgogoro huo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
 

Saturday, December 17, 2016

Waziri Mkuu: Waliouza Kiwanja Cha Shule Wachukuliwe Hatua

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Rashid Taka na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Raphael Siumbo kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua watendaji wote watakaobainika kuhusika katika uuzwaji wa kiwanja cha shule ya msingi Waso.

Ametoa agizo hilo Alhamisi, Desemba 15, 2016 wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Waso Wilaya ya Ngorongoro akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.

Waziri Mkuu alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona watendaji wachache wasiokuwa waadilifu  wanamega kiwanja cha shule na kukiuza kwa maslahi yao, hivyo aliwataka viongozi hao kufuatilia na kumpa taarifa ya hatua za kisheria walizochukua kwa wahusika.

“Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi hapa kuna malalamiko ya viwanja fuatilieni viwanja hivyo vinavyolalamikiwa na wananchi ni viwanja gani je hiyo ya kwamba mmeuza viwanja vya shule ameuziwa nani,” alisema.

Aidha, Waziri Mkuu amemtaka Bw. Taka ahakikishe Mkuu wa Idara ya
Ardhi, Maliasili na Mzingira, Bw. Switbeth Byorushengo anatekeleza majukumu yake ipasavyo. Ametoa agizo hilo baada ya wananchi kudai Ofisa huyo ameshindwa kufanya kazi na kumuomba Waziri Mkuu aondoke naye.
Alisema Bw. Byorushengo anatakiwa kuhakikisha halmashauri hiyo inapima viwanja vya kutosha na kutoa hati kwa wananchi ili waweze kupata maeneo ya kujenga makazi na shughuli zingine za kijamii.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw. Byorushengo kuhakikisha halmashauri hiyo inaanza ujenzi wa hospitali ya wilaya na ifikapo Aprili, 2017 awe amepewa taarifa za ulipofikia ujenzi huo.Kwa upande wake Mkurugenzi huyo alisema tayari wapo katika mchakato wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ambapo wametenga sh. milioni 800 za kuanzia.

Akizungumzia kuhusu mgogoro wa ardhi kati ya vijiji vya Tarafa ya Loliondo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Waziri Mkuu alitoa muda wa siku 30 kwa uongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA) wawe wamekamilisha uhakiki wa mpaka huo.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro Mheshimiwa William Ole Nasha alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia kutatua mgogoro huo wa ardhi kwa kuwa ni wa muda mrefu na unakwamisha shughuli za maendeleo.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo alisema Wilaya ya Ngorongoro inachangamoto nyingi ikiwemo ya ardhi na sasa kuna mgogoro kati ya Kampuni ya Thomson Safari na wananchi ambao wanadai kuwa ardhi hiyo ilichukuliwa kinyemela na mwekezaji huyo bila ya wao kushirikishwa.

Alisema baada ya ziara ya Waziri Mkuu kumalizika mkoani hapa atarudi wilayani Ngorongoro kwa ajili ya kutatua kero mbalimbali ikiwemo ya ardhi na matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na wawekezaji ambazo matumizi yake hayajulikani.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Saturday, December 17, 2016

Taarifa ya Bodi ya Mikopo kwa wadaiwa sugu kuhusu mwisho wa kulipa kwa hiari

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imeongeza muda kwa wadaiwa sugu kulipa madeni yao hadi Desemba 30, 2016.

Hatua ya Bodi inafuatia mwitikio chanya kutoka kwa wadaiwa ndani ya siku 30 za awali ambazo zinakamilika leo Desemba 14, 2016.

Akitoa taarifa ya kuongezwa kwa muda; Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi, Abdul_Razaq Badru amesema kuwa wadau wameomba kuongezewa muda kutokana na baadhi yao kukabiliana na changamoto za majukumu ya kazi na hivyo kushindwa kujitokeza ndani ya siku 30 zilizokuwa zimetangazwa awali.

Katika hatua nyingine, Bw. Badru amesema kuwa ndani ya siku za nyongeza Ofisi za Bodi ya Mikopo zilizopo Mwenge, jijini Dar es Salaam zitaendelea kuwa wazi kwa siku za Jumamosi, Disemba 17, 2016 na Jumapili, Disemba 18, 2016 kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri ili kutoa fursa muhimu kwa wadaiwa wote wa mikopo ya elimu ya juu ambao hawajaanza kurejesha mikopo yao kupata taarifa kuhusu madeni yao na kulipa.

Ili kuharakisha utoaji wa muhtasari wa deni la mdaiwa; mhusika aje na Majina yake kamili, Chuo alichosoma, Mwaka wa kuanza na wa kuhitimu, anuani yake ya barua pepe (email), nambari ya simu ya kiganjani, mwajiri wake na Check Number yake iwapo ameajiriwa serikalini.
‘Kuwa Mzalendo, Rejesha Mkopo wa Elimu ya Juu’

Kwa mawasiliano zaidi piga 0763 459165 au 0767 513208

Imetolewa na:
MKURUGENZI MTENDAJI
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
14/12/2016
 
 

Saturday, December 17, 2016

Serikali Yakanusha Kuwepo Kwa Ugonjwa wa ZIKA Nchini

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema hakuna uthibitisho wa kuwepo kwa ugonjwa wa Zika nchini.

Imeeleza kuwa utafiti uliofanyika ni wa kuangalia ubora wa kipimo cha ugonjwa huo.

Ufafanuzi wa Wizara hiyo umekuja siku moja baada ya Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kutoa ripoti ya utafiti uliofanywa na taasisi hiyo kwa kushirikia na Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Bugando, inayoeleza kuwepo wa maambukizi ya virusi vya Zika katika jamii ya Watanzania.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alitoa ufafanuzi huo kwa waandishi wa habari jana, ambapo alisema wananchi wanapaswa kuondoa hofu kwa kuwa ugonjwa huo haujaingia nchini.

“Napenda kuwatoa hofu wananchi kwa sasa haijathibitishwa kuwepo kwa ugonjwa wa Zika nchini…wao walifanya utafiti nchini wa kuchunguza ubora wa kipimo cha kupima magonjwa ya Zika na Chikungunya, hawakupima kama zika ipo nchini au hakuna,” alisema Waziri Ummy.

Alisema wizara yake itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali, kutafiti ili kubaini kama ugonjwa wa Zika upo nchini au la.

Wizara hiyo pia imeshaanda mkakati wa Zika nchini, unaoelekeza kufuatilia ugonjwa huo.

Mganga Mkuu wa Serikali, Mohammed Kambi alisema, NIMR walichokifanya ni kufanya utafiti wa kutathmini ufanisi na ubora wa kipimo, ambacho kinaweza kuja kutafiti magonjwa ya zika na mengine na kwamba kiutaratibu hizo ni hatua za awali.

Alisema, taarifa hiyo ya NIMR itafanyiwa tathmini ya kisanyasi ili wanasayansi wajiridhishe kama ilifuata taratibu zote na matokeo hayo yanaweza kuendelezwa mbele zaidi na baadae kuweka mikakati ya kuzidi kuthibisha uwepo wa ugonjwa huo.

“Tuna taratibu hizo za upande wa kitaalamu lakini kuna taratibu katika kutoa tamko, kuhusu uwepo wa ugonjwa kama huu kwasababu ni aina ya uginjwa unaotakiwa uripotiwe kimataifa…inabidi taarifa ije rasmi katika wizara, kuna mganga mkuu na Shirika la Afya tuangalie hizo na tukijidhihirisha taarifa rasmi inatolewa na mratibu wa magonjwa hayo,” alisema Dk Mohammed.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NIMR, DK Mwele Malecela alisema taarifa aliyoitoa juzi, ilikuwa ni matokeo ya utafiti wa kubainisha uwezo wa kipimo hicho katika kuanisha virusi vya Zika, Dengue na Chikungunya na matokeo ya awali yalionesha uwepo wa virusi vya Zika.

Alisema pamoja na matokeo hayo, hawakuona dalili wala madhara yoyote yanayosababishwa na Zika ikiwemo Kichwa kidogo na mengine.

“Hili suala ni kwamba lilikuwa ni suala la kuainisha na katika uanishaji huo tukajikuta tumeona virusi hivyo, lakini hiyo haimanishi kuna uthibitishio, naomba nisisitize uthibitisho wa ugonjwa unatolewa na wizara ya afya kwa kufuata uatartibu maalumu uliowekwa,” alisema.

Alisema kuwa wataendelea kufanya utafiti hasa katika kuangalia magonjwa ya Zika, Dengue na Chikungunya na kutoa matokeo kwa kile watakachokipata katika utafiti huo.

Juzi NIMR ilitoa matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi hiyo pamoja na Chuo Kikuu cha Katoliki cha Bugando na utafiti kuanisha uwepo wa maambukizi ya virusi vya zika katika jamii ya Watanzania na kuangalia adhati ya maambukizi katika kusababisha watoto wanaozaliwa na ulemavu.

Sampuli za damu kutoka kwa watu 533 zilipimwa. Kati yao, watoto wachanga 80 walizaliwa na ulemavu wa viungo mbalimbali. Kati ya waliopimwa 533, 83 (15.6%) waligundulika kuwa wameambukizwa virusi vya Zika.

Kati ya wale watoto wachanga 80 waliozaliwa na ulemavu, 43.8% walikuwa wameambukizwa virusi vya Zika, utafiti unaendelea kujua ukubwa wa tatizo hili.

Saturday, December 17, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumamosi ya Disemba 17



Jumamosi, 17 Desemba 2016

KUELEKEA MCHEZO WA AFRICAN LYON NA AZAM FC

BAADA ya maandalizi ya takribani wiki tatu, hatimaye Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kesho inatarajia kufungua pazia la mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kukipiga dhidi ya African Lyon, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam saa 10.00 jioni.

Azam FC itaanza ngwe hiyo ikiwa na nguvu mpya kabisa baada ya kufanya usajili mzuri kwenye dirisha dogo la usajili, kwa kuongeza sura mpya tano pamoja na kumrejesha winga wake, Enock Atta Agyei, aliyekuwa kwa mkopo Medeama ya Ghana ilipomsajili, na sasa ataanza kuonekana katika mechi za ligi mara baada ya kutimiza miaka 18 Januari 5 mwakani.

Wachezaji wapya watano waliosajiliwa na Azam FC kwenye dirisha dogo ni beki Yakubu Mohammed (Aduana Stars, Ghana), kiungo mkabaji raia wa Cameroon, Stephan Kingue Mpondo (Coton Sports, Cameroon), winga Joseph Mahundi aliyerejea nyumbani (Mbeya City, huru) na washambuliaji Samuel Afful (Sekondi Hasaacas, Ghana), Yahaya Mohammed (Aduana Stars, Ghana).

Kikosi cha Azam FC kilichomaliza mzunguko wa kwanza wa ligi kikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 25 tofauti ya pointi 10 dhidi ya vinara Simba (35), kimeonekana kurejea na ari ya juu na morali kubwa kuelekea mzunguko wa pili kutokana na kiwango bora na hali ya kupambana wanayoonyesha kwenye maandalizi mazoezini.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, alisema wamejiandaa vema kuelekea mchezo huo pamoja na mzunguko wa pili wa ligi kiujumla kutokana na nguvu mpya walizoziongeza kikosini.

“Kiufupi raundi ya pili tumejiandaa na timu inanguvu mpya ya wachezaji tuliowasajili ambao hawakuwepo raundi ya kwanza hata mazoezi jinsi yanavyoendelea na jinsi wachezaji wanavyoonekana tunaamini kwa raundi ya pili tutaanza katika mazingira mazuri kuliko ambavyo tulikuwa tukifanya mzunguko wa kwanza,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, alisema kuwa wanaingia kwenye raundi ya pili wakijua kuwa kutakuwa na ushindani mkubwa, lakini amekipanga kikosi chake kufanya vizuri huku akiwaambia mashabiki wa Azam FC waendelee kuisapoti timu hiyo.

“Mashabiki waendelee kutusapoti tunajua kwa namna tulivyokuwa tukicehza mzunguko wa kwanza ilikuwa ni ngumu kwao, lakini si kwa wao tu bali ilikuwa kwa watu wote, kwa kile ambacho naweza kuwaambia wajaribu kutuvumilia, mpira tutakaokuwa tunacheza na matokeo tutakayokuwa tunayapata mzunguko wa pili, wenyewe watakuwa wakiyapenda na hawatajutia kabisa kuchagua na kuisapoti Azam FC,” alimalizia.

Rekodi zao (Head To Head)

Agosti 21 mwaka huu, timu hizo zilikutana katika mchezo wa raundi ya kwanza, uliokuwa ni wa tano kihistoria kukutana kwenye ligi, ambapo uliisha kwa matokeo ya sare ya bao 1-1, Lyon ikitangulia kufunga kupitia kwa Hood Mayanja kwa mpira wa kona wa moja kwa moja kabla ya nahodha John Bocco ‘Adebayor’, kufunga bao zuri la kusawazisha mwishoni mwa mtanange huo.

Mpaka sasa katika mechi hizo tano walizokutana, Azam FC imeshinda mara tatu, Lyon mara moja huku mchezo mmoja wakienda sare.

Katika mechi zote hizo, Azam FC ndio iliyofunga mabao mengi zaidi ikitupia saba katika lango la wapinzani wao hao, huku Lyon yenyewe ikitingisha nyavu za matajiri hao mara nne tu.
 

HOFFENHEIM NA BORUSSIA DORTMUND ZATOSHANA NGUVU BUNDESLIGA

Timu ya Hoffenheim na Borussia Dortmund zimegawana pointi katika mchezo mzuri wa Bundesliga ulioishia kwa sare ya magoli 2-2 jana usiku.

Katika mchezo huo wenyeji Hoffenheim walifunga goli la kwanza ndani ya dakika mbili kupitia kwa Mark Uth, hata hivyo goli hilo lilisawazishwa na Mario Gotze.
Sandro Wagner aliongeza goli la pili la Hoffenheim, lakini mshambuliaji nyota wa Dortmund- Pierre-Emerick Aubameyang akasawazisha goli hilo.
                    Sandro Wanger akiwa ameupiga mpira uliomshinda kipa Roman wa Dortmund
Osumane Dembele akiwa amebebwa kwenye machela baada ya kuumia huku Aubameyang akiangalia
 

KATIBU TAWALA MKOANI MARA AHITIMISHA MAFUNZO KWA WADAU WA FILAMU MKOANI HUMO

Katibu Tawala mkoa wa Mara, Adoh Mapunda (katikati) akizungumza hii leo kwenye kilele cha mafunzo ya siku tatu kwa wadau wa filamu mkoani humo. Mafunzo hayo yalianza juzi Disemba 14,2016 kwenye ukumbi wa shule ya Sekondari Mara Mjini Msoma.

Yaliandaliwa na Bodi ya Filamu nchini kwa lengo la kuwajengea welezi wanatasinia wa filamu ili kuzalisha kazi zenye ubora na hivyo kukidhi ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi ambapo zaidi ya washiri 200 walionufaika na mafunzo hayo wamepatiwa vyeti. Tayari mafunzo ya aina hiyo yamefanyika mikoa ya Morogoro na Mwanza na yataendelea katika mikoa mingine. #BMGHabari
Wanatasnia wa filamu mkoani Mara wakimsikiliza Katibu Tawala mkoani humo, Adoh Mapunda, wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kwa wanatasnia hao. Ameahidi kutoa fulana (Tshirt) 250 kwa ajili ya wanatasnia wa filamu mkoani Mara waliohudhuria mafunzo hayo ambapo zitawasaidia hususani kuwa na sare ya aina moja wakikutana kwa pamoja
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi.Nuru Millao, amesema sekta ya filamu ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wanatasnia wake na taifa kwa ujumla hivyo Bodi za filamu mikoani zihakikishe zinasimamia maendeleo ya tasnia hiyo.
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu nchini, Bi.Joyce Fisso, amebainisha kwamba wadau wa filamu wakiwemo watayarishaji, waongozaji, wahariri pamoja na waigizaji wamefundishwa vyema mafunzo hayo ili kuzalisha kazi bora.
Mgeni rasmi, Katibu Tawala mkoani Mara, Adoh Mapunda (wa pili kulia), akipokea cheti cha utambuzi kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi.Nuru Millao

KIMBUNGA CHAKATISHA HOTUBA YA ZUMA BAADA YA HEMA KUANGUKA

MAJALIWA AANZA ZIARA WILAYANI ARUMERU NA KUZUNGUMZA NA WATUMISHI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa serikali na Halmashauri ya wilaya ya Arumeru kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Arusha Desemba 17, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Arumeru wakimsikiliza waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Arusha, Desemba 16, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea taarifa ya maendeleo ya wilaya ya Arumeru baada ya kusomewa taarifa hiyo na Mkuu wa wilaya hiyo, Alexander Mnyeti kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Arusha Desemba 17, 2016. (Picha na Ofisi ya Wairi Mkuu)
:
Kamishna wa Umoja wa Mataifa anaeshughulikia wakimbizi Filippo Grandi amesema raia wote wa Syria lazima waruhusiwe kuondoka katika eneo la mashariki mwa Aleppo na serikali lazima idhibiti mateso na ugumu wa maisha kujitokeza tena katika maeneo mengine. Katika taarifa yake ya leo Grandi amesema kuna hatari kubwa kwamba hali ya watu kupoteza makazi yao na mateso wanayopitia haiwezi kwisha, lakini pia inaweza kujitokeza tena katika vita vingine. Aidha afisa huyo ya ngazi ya juu ya Umoja wa Mataifa ameongeza kusema kuwa, kwa umuhimu wa kuwalinda raia katika kila eneo la mgogoro, vita vya Syria lazima vimalizwe sasa na pasipo kuchelewa.



Makao makuu ya Kanisa Katoliki Duniani yamesema kiongozi wa kanisa hilo Papa Francis amepokea takribani barua pepe 50,000 za pongezi ya kutimiza miaka 80 ya kuzaliwa kupitia anauni iliyofunguliwa maalumu kwa kazi hiyo. Ujumbe unaweza kutumwa kwa Kilatini, Kihispania, Kireno, Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani na Kipoland. Lakini katika ujumbe uliotumwa kwa wingi ni kwa lugha ya Kiingereza, Kihispania na Kiitaliani, ingawa kulikuwepo zaidi ya ujumbe 1,000 uliotumwa kwa lugha ya Kilatini. Vatican vilevile imesema Papa Francis amepata kifungua kinywa na watu wanane wasio na makazi, wanaoishi katika maeneo ya karibu na eneo la St. Peter, na alipokea mafungu matatu ya maua kutoka kwao, ambayo ameyaweka katika makazi yake ya Santa Marta.



Waziri wa Mambo ya Ndani wa Poland Mariusz Blaszczak amevituhumu vyama vya upinzani kwa kutaka kujinyakulia madaraka kinyume cha sheria. Mapema asubuhi, polisi walitumia nguvu kuwaondoa waandamanaji waliokuwa wamelizingira jengo la bunge katikati ya Warsaw, waliokuwa wanadai wabunge wa chama tawala wamekiuka katiba kwa kupitisha sheria ya bajeti ya mwaka 2017 hapo jana. Msemaji wa chama kiitwacho Jukwaa la Raia, amesema kundi kubwa la upinzani katika bunge, likiwa na wabunge kati ya 20-30 limepokezana kukaa katika ukumbi wa bunge. Na kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters kiasi ya waandamanaji 30 bado wameendelea kusalia katika eneo la mbele la ukumbi wa bunge. Mgogoro ulianza Ijumaa baada ya upinzani kupinga mipango ya chama tawala cha Sheria na Haki kudhibiti vyombo vya habari bungeni kushiriki vikao vya awali kabla ya zoezi la kupigia kura bajeti.




Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imewafukuza waandishi habari watano wa mashirika ya habari ya Ubelgiji, huku kukiwa na ripoti zinazosema walikuwa na lengo la kuripoti maandamano ya kumpinga Rais Joseph Kabila. Televisheni moja ya Kifaransa ilisema waandishi hao kutoka televisheni za VRT na VTM waliwasili Kinshasa Ijumaa, lakini walikataliwa kupewa kibali na serikali na walikamatwa. Msemaji wa serikali Lambert Mende alinukuu dura za uhamiaji akisema waandishi walikiuka kanuni za kuingia nchini humo katika kutekeleza majukumu yao na kwamba wamerejea mjini Brussel jana jioni. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Didier Reyndre amekilaani kitendo hicho, akisema uhuru wa habari ni haki ya msingi kwa taifa lake na kwamba atawasilisha jambo hilo kwa serikali ya Congo.


Mkutano mkuu wa chama tawala nchini Zimbabwe ZANU-PF umemuidhinisha Rais Robert Mugabe kuwa mgombea wake katika uchaguzi wa 2018, ambapo kama ataibuka mshindi katika uchaguzi huo utaongeza miaka yake 36 madarakani. Kiongozi huyo amepitishwa na miundo yote ya chama hicho, katika mkutano uliofanyika eneo la Masvingo, umbali wa kilometa 300, kusini mashariki mwa mji mkuu, Harare.

 
habari za leo hizi hapa habari za leo hizi hapa Reviewed by RICH VOICE on Desemba 17, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...