Thursday, December 1, 2016

Idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2017


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene amesema kuwa wanafunzi 526,653 kati ya 555,291 waliofaulu mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka huu wamechaguliwa kujiunga Kidato cha Kwanza mwakani katika shule za sekondari za Serikali.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi hiyo ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika awamu ya kwanza ni sawa na asilimia 94.85 ya wanafunzi wote waliofaulu.

Akizungumza na Waandishi wa habari tarehe 28 Novemba 2016 mjini Dodoma Waziri Simbachawene ameeleza kuwa wanafunzi 28,638 wakiwemo wavulana 12,937 na wasichana 15,701 hawakuchaguliwa katika awamu ya kwanza ya uchaguzi.

Aidha Waziri Simbachawene aliitaja mikoa ambayo wanafunzi wake walifaulu lakini hawakuchaguliwa katika awamu ya kwanza kuwa ni pamoja na Dar Es Salaam (18,820), Arusha (4,752), Songwe (1,465), Kigoma (1,208), Manyara (1,141), Lindi (608), Mbeya (406) na Katavi (238).

Kuhusu wanafunzi waliochaguliwa Waziri Simbachawene amesema kuwa, wasichana ni 268,052 sawa na asilimia 94.5 na wavulana ni 258,601 sawa na asilimila 95.2.

Aidha, Waziri wa Nchi amesema kuwa wanafunzi wote wenye ulemavu waliofaulu wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2017.

Kwa mujibu wa Waziri Simbachawene mchanganuo wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za serikali umegawanyika katika makundi manne ambapo kundi la kwanza limehusisha wanafunzi 900 wakiwemo Wavulana 480 na Wasichana 420 ambao wamepelekwa katika shule za Bweni kwa wenye ufaulu mzuri zaidi.

Ameongeza kuwa kundi la pili limehusisha wanafunzi 1005 ikiwa ni Wavulana 915 na Wasichana 90 ambao wamepelekwa katika shule za Bweni mahsusi kusomea Ufundi.

Pia amesema kuwa kundi la tatu limewahusisha Wanafunzi 780 wakijumuishwa Wavulana 430 na Wasichana 350 ambao wamechaguliwa kujiunga na Shule za Bweni Kawaida na kundi la nne limewahusisha wanafunzi 723 wakiwemo wavulana 405 na wasichana 318 wa shule za bweni kwa ajili ya wanafunzi walio na Ulemavu.

Kulingana na takwimu hizo, Waziri Simbachawene amesema kuwa jumla ya wanafunzi 3,407 wamechaguliwa kujiunga na shule za bweni kidato cha kwanza ambapo wavulana ni 2,230 sawa na asilimia 65.4 na wasichana 1,178 sawa na asilimia 34.6, pia watahiniwa wapatao 6,260 sawa na asilimia 0.78 ya waliosajiliwa hawakufanya mtihani.

Aidha Waziri Simbachawene amesema kuwa wanafunzi 523,245 wakiwemo wavulana 256,371 na wasichana 266,874 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za kutwa.

Wakati huo huo Mhe. Simbachawene amesema hatasita kuzichukulia hatua, shule zilizohusika na udanganyifu wa mitihani kwani wanarudisha nyuma maendeleo ya taaluma nchini yanayofanywa na Serikali.

“Serikali imeanza kuwachukulia hatua kwa mujibu wa taratibu wale wote waliohusika na udanganyifu huu� hatua hizo ni pamoja na kuwavua madaraka waliokuwa Waratibu Elimu Kata na Walimu Wakuu, kuwashtaki mahakamani na kupeleka mashauri yao Tume ya utumishi ya Walimu (TSC),” amesema Mheshimiwa Waziri.

Pia ametoa agizo kwa Wakuu wa Mikoa kubainisha sababu za wanafunzi walioingia darasa la kwanza kutomaliza masomo yao kama ilivyotarajiwa.

“Naagiza Wakuu wa Mikoa kubainisha sababu za wanafunzi hao kutomaliza na hatua stahiki za kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaoandikishwa darasa la kwanza wanamaliza mzunguko wa masomo kwa mujibu wa Sera ya Elimu,” amesisitiza Mhe. Simbachawene na kutaka Wakuu wa mikoa kuchukua hatua stahiki zilizoelekezwa.
 
 

Thursday, December 1, 2016

Warioba: Maadili yameporomoka kwa viongozi na jamii

Jaji Mstaafu, Joseph Sinde Warioba amevishauri vyombo vinavyo simamia maadili kubadilika kiutendaji na kuachana na masuala ya kisiasa na amependekeza kuwa Taasisi  ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali kupewa nguvu ili zifanye kazi zake kiurahisi.

Aliyasema hayo Jijini Dar es salaam alipokuwa akichangia kwenye mdahalo  wa wadau ulioandaliwa na TAKUKURU kuhusu kujenga na kukuza maadili, haki za binadamu, uwajibikaji, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa.

Warioba alisema ni jambo lisilofichika kuporomoka kwa maadili si kwa jamii pekee, bali hata kwa baadhi ya viongozi.

“Lazima kuwe na misingi ya uongozi,maadili yameporomoka sana na ni ngumu kuyarudisha”alisema Warioba.

Aidha, Warioba alisema maadili hayajengwi na sheria wala hayasimamiwi na taasisi bali yanajengwa na kusimamiwa na jamii.
 
 

Thursday, December 1, 2016

Wadaiwa Sugu NHC Washitakiwa kwa Rais Magufuli

Shirika  la Nyumba la Taifa (NHC), limewasilisha ripoti ya wadaiwa sugu wa shirika hilo, zikiwamo wizara, taasisi za Serikali na watu binafsi kwa Rais Dk. John Magufuli, huku wizara mbili zikiwa na deni kubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mikoa na Utawala wa NHC, Raymond Mndolwa, alisema uamuzi huo umekuja baada ya Rais Magufuli kuwataka kukusanya madeni hayo na kuwasilisha taarifa hiyo ofisini kwake ili aweze kuipitia.

Mndolwa alisema NHC ilitoa notisi ya siku 90 ambayo ilianza  Septemba, mwaka huu, huku wadaiwa hao wakitakiwa kulipa madeni  ndani ya muda uliopangwa.

Alisema kuwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo bado zinadaiwa kiasi kikubwa cha fedha, licha ya kuwapo kwa mazungumzo ya kulipa madeni yao.

“Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto inadaiwa Sh bilioni 1.4, huku wakilipa Sh milioni 300, wakati Wizara ya Habari, inadaiwa Sh bilioni 1.14, lakini imelipa Sh milioni 700,” alisema Mndolwa.

Mndolwa alisema shirika hilo hadi sasa limekusanya Sh bilioni 5.9 kati ya Sh bilioni 9.3 ambalo ni deni la Serikali kupitia wizara na taasisi mbalimbali, huku Sh bilioni 2.5 zikikusanywa kutoka kwa wadaiwa binafsi ambao awali walikuwa wanadaiwa Sh bilioni 4.

Alisema lengo la shirika hilo ni kuhakikisha madeni yanalipwa ili fedha hizo ziweze kutumika kwenye shughuli nyingine za maendeleo, ikiwamo ujenzi wa nyumba za kisasa 300 mkoani Dodoma.

Alizitaja wizara zinazodaiwa ni Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Fedha na Uchumi, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na iliyokuwa Wizara ya Ujenzi.

Wadaiwa wengine ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
 
 

Thursday, December 1, 2016

Wafanyabiashara Wawili wa Madini Wafikishwa Mahakamani kwa Tuhuma za Kulawiti na Kubaka Watoto


Wafanyabiashara wawili mashuhuri wa madini katika miji ya Mererani na jiji la Arusha jana walifikishwa mahakamani mjini Moshi kwa wakikabiliwa na makosa ya ulawiti na ubakaji watoto. 
Mmoja wao, Welaufoo Munisi (38) anashtakiwa kwa kosa la kumlawiti mtoto wa kiume wa mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), mwenye umri wa miaka 16. 
Mtoto anayedaiwa kufanyiwa kitendo hicho ni mwanafunzi wa shule moja ya sekondari wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, baba yake ni mchungaji katika usharika ambao tunauhifadhi kwa sababu za kimaadili. 
Akimsomea mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa Kilimanjaro, Joachim Tiganga, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tamari Mndeme alidai kuwa Munisi alitenda kosa hilo Novemba 21, 2016. 
Wakili huyo alidai kuwa siku hiyo katika nyumba za wafanyakazi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), mshtakiwa alimlawiti kijana huyo mwenye umri wa miaka 16. 

Kabla ya kufikishwa kortini jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Koka Moita alidai kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo baada ya kumnyeshwa kijana huyo dawa za kulevya. 
Hata hivyo, Munisi alikana mashtaka hayo na kesi hiyo imepangwa kutajwa Desemba 14 mwaka huu baada ya wakili Mndeme kuiambia Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo ulikuwa haujakamilika. 

Dhamana yake ilikuwa wazi na alitakiwa kuwa na wadhamini wawili na hadi saa 8:00 mchana alikuwa hajatimiza masharti hayo.
Wakati Munisi akikabiliwa na shtaka hilo, mfanyabiashara mwingine wa Mererani, Benedict Kimario (42) jana alipandishwa kizimbani mjini Moshi, akikabiliwa na mashtaka ya kumlawiti na kumbaka mtoto wa miaka minane. 

Wakili Mndeme alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Idan Mwilapo kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo Mei 10 mwaka huu katika Kijiji cha Mrau, Wilaya ya Rombo, Kilimanjaro.

Mshtakiwa huyo anayetetewa na wakili wa kujitegemea, Joseph Peter, alikana tuhuma hizo na kesi hiyo imepangwa kutajwa kesho ili kuangalia kama ametimiza masharti ya dhamana au la baada ya jana kukwama. 
Alikwama baada ya Hakimu Mwilapo kumtaka kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja angesaini hati ya dhamana ya Sh5 milioni, lakini wakajitokeza wadhamini ambao si wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro. 
Wadhamini hao walikuwa na barua kutoka Mererani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, ambazo kiutaratibu zilipaswa kwanza kuidhinishwa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro.
 

Thursday, December 1, 2016

Mganga wa Kienyeji Auawa Akitaka Kumbaka Mgonjwa

Mganga wa kienyeji aliyejulikana kwa jina la Kashinje Kashinje (55), mkazi wa kijiji cha Singita kilichopo Kata ya Usanda wilayani Shinyanga ameuawa kwa kupigwa na wananchi ikielezwa alijaribu kutaka kumbaka mteja wake.

Mteja huyo ambaye ni mwanamke mwenye umri wa miaka 20 (jina linahifadhiwa) alikwenda kutibiwa kwa lengo la kupata mtoto.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Muliro Jumanne, tukio hilo ni la Novemba 29 mwaka huu, akisema lilitokea majira ya saa tano asubuhi.

Alisema Kashinje alifariki dunia alipokuwa anakimbizwa hospitali baada ya kujeruhiwa kwa kitu chenye ncha kali katika jicho la kulia na kupigwa kwa fimbo mgongoni na watu waliojichukulia sheria mkononi.

“Watu hao walijichukulia sheria mkononi baada ya mganga huyo kujaribu kumbaka mwanamke (jina linahifadhiwa), mkazi wa kijiji cha Ishinabulandi wilaya ya Shinyanga ambaye alikuwa akimtibu kwa tiba za asili ili aweze kupata mtoto”, alieleza kamanda Muliro.

Alisema tatizo lililompeleka mwanamke huyo kwa mganga ni kupata tiba ili aweze kupata mtoto.

Kamanda Muliro alibainisha kuwa chanzo cha tukio hilo ni tamaa za kimwili na uongo wa kimatibabu wa kutaka kumuingilia kimwili mgonjwa wake baada ya kumlewesha kwa dawa za kienyeji, lakini alifanikiwa kupiga kelele na ndipo wananchi walipomvamia mganga huyo.
Reviewed by RICH VOICE on Desemba 01, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...