jumanne hii

...... PLAZA.jpgJEMBE1.jpg

 

Jumanne, 27 Desemba 2016

JOSE MOURINHO ASIFIA GOLI TAMU LA HENRIKH MKHITARYAN

Kocha wa Manchester United Jose Mourinho amepongeza goli zuri lililofungwa kwa mpira wa kisigino kwa nyuma na Henrikh Mkhitaryan katika mchezo walioibuka na ushindi dhidi ya Sunderland katika dimba la Old Trafford.

Mkhitaryan alifunga goli hilo lililozua utata kutokana na kuwa alikuwa ameotea akipokea pasi kutoka kwa Zlatan Ibrahimovic na kufanya matokeo ya mchezo huo kuwa Manchester 3-1 Sunderland.

Mkhitaryan mwenyewe amesema goli hilo ni goli zuri kuwahi kufunga katika maisha yake ya soko, na kuongeza kuwa hayo yalikuwa ni mazingaumbwe madogo ya kipindi cha Sikukuu ya Krismasi.

MANCHESTER CITY YAKWEA HADI KATIKA NAFASI YA PILI KATIKA LIGI KUU YA UINGEREZA

Timu ya Manchester City imekwea hadi nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 3-0 dhidi ya Hull City wakiwa ugenini katika dimba la KCOM.

Kikosi cha Pep Guardiola kilipata ushindi wake wa 12 katika msimu huu, na kuwa nyuma kwa pointi saba dhidi ya vinara timu ya Chelsea.

Yaya Toure alifunga goli la kwanza kwa mkwju wa penati katika kipindi cha pili, baada ya Raheem Sterling kuchezewa rafu, Kelechi Iheanacho akafunga la pili na Curtis Davies kujifunga la tatu.
                                                          Yaya Toure akifunga goli kwa mkwaju wa penati
                                       Kelechi Iheanacho akifunga goli la pili la Manchester City 
    Curtis Davies akijifunga wakati akijaribu kuokoa mpira uliopigwa na Raheem Sterling 
 

BALOZI SEIF AREJEA ZANZIBAR BAADA YA KUKAMILISHA ZIARA YA KIKAZI NCHINI CHINA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipokewa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar akitoa Nchini China baada ya kumaliza ziara ya siku Tano ya Kiserikali. Kulia ya Mh. Ayoub ni Meya wa Manispaa ya Mjini Mstahiki Khatib Abdulrahman Khatib na Waziri wa Kazi Uwezeshaji, Wazee, Vijhana na Watoto Mh. Maudlin Cyrus Castico.
Balozi Seif akisalimiana na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Joseph Abdulla Meza.
Balozi Seif akisalimiana na Timu ya Wazee waasisi wa Chama cha Mapinduzi.
Balozi Seif kulia akiwa makini kusikiliza Maswali mbali mbali aliyoiulizwa na Wana Habari mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar akitokea Nchini China. Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohamed aliyembatana naye katika ziara hiyo ya Kiserikali ya siku Tano. Picha na – OPMR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kukamilika kwa ujenzi wa miradi mitatu inayotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutafungua fursa pana ya ajira hasa kwa Vijana pamoja na kuimarika kwa ufanisi wa kazi katika Taasisi za Umma na hata zile Binafsi.

Akizungumza na Waandishi wa Vyombo mbali mbali vya Habari hapa Nchini mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar akitokea Nchini China kwa ziara ya siku Tano ya Kiserikali Balozi Seif aliitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa Bandari ya Mpiga Duri, kukamilika kwa eneo la maegesho ya ndege pamoja na Mawasialiano Serikalini { E. Government }.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kukamilisha taratibu zilizobakia katika hatua za mwisho kwa ajili ya kukamilisha mradi wa ujenzi wa eneo la maegesho ya Ndege kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema Zanzibar kupitia miradi hiyo itaongeza mapato yake kupitia Sekta ya Utalii, harakati za Kibiashara nah ii itatokana na ongezeko kubwa la idadi ya watalii na wageni watakaoamua kutumia huduma hizo za usafiri wa uhakika.

Akizungumzia Mradi wa Mawasiliano Serikalini { E - Government } Balozi Seif alisema kukamilika kwa mradi huo awamu ya Pili kwa hatua ya kuunganishwa na mfumo wa Mtandao wa Kisasa utawawezesha Wananchi kupata huduma kwa njia ya mawasiliano.

Alisema Wananchi watapata kuhudumiwa moja kwa moja kwa mfumo wa Internet kwenye sekta za Afya, Elimu pamoja na urahisishaji wa ukusanyaji wa Mapato ya Serikali Kuu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
 

Jumanne, 27 Desemba 2016

MAMIA YA WAOMBOLEZAJI WAJITOKEZA WA MPIGANAJI MPOKI BUKUKU JIJINI DAR ES SALAAM, KUZIKWA LEO NYUMBANI KWAO DODOMA


Mamia ya wadau pamoja na wale wa Tasnia ya Habari wamejitokeza kwa wingi katika uwanja wa shule ya Tabata, Wilayani Ilala Jijini Dar es Salaam kuaga mwili wa aliyekuwa mpiga picha Mwandamizi wa Magazeti ya The Guardian Limited yanayochapisha magazeti ya Nipashe, The Guardian, marehemu Mpoki Bukuku (44) aliyefariki dunia juzi baada ya kupata ajali ya gari.

Wadau mbalibali walipata kutoa salamu zao za rambirambi kwa familia ya marehemu ambapo pia Waziri mwenye dhamana, Mh. Nape Nnauye alipata kutoa salamu na kuungana na msiba huo. 

Pia Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Mh. Freeman Mbowe nae alipata kutoa salamu huku akitaka wanahabari kuyaendeleza yale aliyoacha Marehemu.

Pia viongozi mbalimbali wamepata kutoa salamu zao wakiwakilisha tasnia ya habari, vyama vya wanahabari na maeneo mengine wakiwemo ndugu na jamaa wa karibu.

Msemaji wa familia, ambaye ni kaka wa marehemu, Gwamaka Bukuku, aliwashukuru watu wote kwa kujitokeza ambapo amewaomba kuendeleza umoja wao kama walivyouonyesha kwa marehemu.

“Mwili wa marehemu baada ya kutoka hapa unapelekwa Dodoma kwa mazishi na huko ndipo utazikwa. baada ya taratibu hizi hapa mwili utasafirishwa na kupelekwa nyumbani kwa wazazi wake, Dodoma kwa ajili ya mazishi ambayo yatafanyika leo Dodoma” amesema. Habari picha na Mob Blog
Mwili wa Mpoki Bukuku ukiwasili nyumbani kwake Tabata ukitokea Muhimbili
                                                                            Mwili ukiwa ndani ya nyumba yake
Familia ya Mpoki Bukuku ikiwa na uzuni baada ya kuwasili kwa mwili wa mpendwa wao nyumbani
Mwili wa Mpoki Bukuku ukitoka nyumbani kwake kuelekea uwanja wa shule kwa ajili ya kuagwa
Mkurugenzi wa Redio One, Deo Rweyunga ( mwenye shati jeusi ) akisalimiana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akisalimiana na aliyewahi kuwa mkuu wa wilaya mbalimbali nchini, Baraka Konisaga











Tuesday, December 27, 2016

Mwanafunzi Ajeruhiwa Na Risasi Kichwani Na Walinzi Wa Kampuni Ya Kifaru Jijini Arusha

Mwanafunzi wa kidato cha pili wa shule ya sekondari Mringa, Vanessa Josephat [16] mkazi wa Sakina jijini hapa amejeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi kichwani na walinzi wa kampuni ya ulinzi ya kifaru waliokuwa wakiwatoa kwa nguvu kwenye nyumba yao yenye mgogoro .

Tukio hilo limethibitishwa na kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha Charles Mkumbo ambaye alisema kuwa polisi inamshikilia Fabian Charles mlinzi wa kampuni ya kifaru pamoja na silaha aina ya shoot gun iliyo tumika katika tukio hilo huku majeruhi amelazwa katika hospitali ya KCMC kutokana na hali yake kuwa mbaya .

Kamanda mkumbo alisema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa tatu asubuhi katika eneo la sakina jijini hapa, ambapo alisema walinzi watatu wa kampuni hiyo waliokuwa wakilinda nyumba hiyo inayomilikiwa na Josephat Nehemia walitumia silaha hiyo kuwafyatulia familia inayoishi hapo ili waondoke na ndipo silaha hiyo ilipomjeruhi mwanafunzi huyo .

Taarifa zinaeleza kuwa December 21 mwaka huu kampuni ya udalali ya Marc Recorders Limited wakiwa na mabaunsa na watu wengine walivamia nyumba hiyo na kuwatoa nje wamiliki wa nyumba hiyo na kuondoka na vyombo vyao vya ndani wakidai nyumba hiyo imeshauzwa kwa , Thobias Ludovick Senya baada ya mmiliki kushindwa kulipa deni la shilingi million 3.7 alilokuwa akidaiwa na taasiai ya fedha Heritage.

Baada ya tukio hilo familia hiyo yenye watu wapatao kumi wakiwemo watoto na kichanga walianza kulala nje kando ya geti la nyumba hiyo wakipigwa na baridi kali pasipo kuwa na msaada wowote

Mmiliki wa nyumba hiyo Josephat Nehemia Ogaga alisema baada ya familia yake kutolewa nje wakati yeye akiwa safarini walikuja walinzi hao wa kampuni ya kifaru na kuanza kulinda na baada ya yeye kurejea alifanikiwa kuwaondoa walinzi hao na kuirejesha ndani familia yake akidai taratibu za kuuza nyumba yake hazikufuatwa ila kilichofanyika ni uhuni .

“Nikweli nilikuwa nadaiwa na Heritage financial shilingi milioni 3 .7 na nililipa deni na kubaki shilingi million 1.8 hivyo hatua ya kuja kuuza nyumba yangu yenye thamani shilingi million 200 kwa deni hilo ni uhuni mtupu umefanyika” alisema Nehemia

Hata hivyo siku moja baadae walinzi hao walirejea tena wakiwa na silaha za moto na kuanza kufyatua risasi ovyo ndani ya nyumba hiyo kwa lengo la kuwatisha familia hiyo ili waondoke ndani ya nyumba hiyo ambapo moja ya risasi ilimjeruhi mwanafunzi huyo kichwani ambaye amelazwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC Mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya matibabu

Kamanda Mkumbo amezitaka kampuni za ulinzi kutoingilia migogoro bila kufuata utaratibu kwani vyombo vyenye mamlaka ya kushughulikia migogoro kama hiyo vipo na hivyo amezitaka kampuni za ulinzi kufuata taratibu zao za utendaji wa kazi na kuacha kukimbilia maslahi yao ya kupata fedha haraka,

Mkumbo alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.
 

Tuesday, December 27, 2016

Waziri Mahiga apokea Dola elf 50,000 kwa ajili ya Waathirika wa Kagera

Serikali ya Jamhuri ya Korea imetoa msaada wa Dola za Marekani elf 50,000 takribani milioni 108 kwa fedha za Tanzania kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi lilitokea mkoani Kagera mwezi Septemba 2016.

Msaada huo ulikabidhiwa leo jijini Dar es Salaam na Balozi wa Korea nchini Tanzania, Mhe. Song Geum Young na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb) kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb).

Baada ya kupokea msaada huo, Dkt. Mahiga aliishukuru Serikali ya Korea na kuahidi kuwa msaada huo ataukabidhi kwa Mhe. Waziri Mkuu ili uweze kutumika kama ulivyokusudiwa.

Mhe. Mahiga alisema kuwa Korea imekuwa mbia mkubwa wa Tanzania tokea nchi hiyo ilipoanzisha mahusiano ya kidiplomasia na Tanznaia miaka 25 iliyopita. Alieleza kuwa katika kipindi hicho Tanzania imekuwa ikipokea misaada mbalimbali ya kiuchumi, kijamii na ya kibinadamu ukiwemo huu wa leo ulioelekezwa kwa waathirika wa tetemeko la ardhi la mkoani Kagera.

Mhe. Waziri alitaja misaada ambayo Korea imeipatia Tanzania ni pamoja na ujenzi wa daraja la Malagarasi mkoani Kigoma, ujenzi wa hospitali ya kisasa ya Mloganzila na ujenzi wa hospitali ya uchunguzi wa afya ya Mama iliyopo Chanika. Aidha, Korea hivi karibuni itaanza ujenzi wa daraja la Selander ambalo linatarajiwa kuanzia ufukwe wa Coco, Oysterbay hadi maeneo ya hospitali ya Aga Khan, Upanga jijini Dar es Salaam.

Waziri Mahiga alibainisha pia kuwa Jamhuri ya Korea itatoa msaada mkubwa zaidi wa maendeleo kwa Tanzania kuliko nchi yeyote ya Afrika. Taarifa hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea, Mhe. Yun Byung-se alipofanya naye mazungumzo kando ya Mkutano wa nchi za Afrika na Korea uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia tarehe 06 na 07 Desemba 2016.

Kwa upande wake, Balozi wa Korea nchini aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania hususan kutoa atia misaada ya maendeleo ili iweze kutimiza azima ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
 

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 27 Desemba 2016.
 

Tuesday, December 27, 2016

Picha za Ray C akiwa ndani ya muonekano mpya wa kihindi

Huenda huu ukawa ndio ujio mpya wa msanii mkongwe wa muziki wa bongofleva Rehema Chalamika aka Ray C baada ya misukosuko ya hapa na pale katika maisha yake ya muziki.

Muimbaji huyo ambaye amedaiwa kuweza kuachana na matumizi ya Madawa ya kulevya baada ya kushindwa kwa muda mrefu,wiki chache zilizopita aliweka kambi ndani ya studio ya Wanene kwa ajili ya maandalizi ya ujio wake mpya.

Wiki hii amepiga picha zake mpya zinazomuonyesha akiwa na muonekano wa kihindi. Angalia picha.

Tuesday, December 27, 2016

Huddah Monroe aeleza sababu ya kuitosa Wasafi Beach Party ya Diamond

Wasafi Beach Party iliyofanyika Disemba 24, Jangwani Sea Breezy jijini Dar es Salaam, ilikuwa iwakutanishe mahasimu warembo Huddah Monroe na Vera Sidika jukwaani kama mahost.

Wengi tulikuwa tukisubiri kushuhudia drama ya kufungia mwaka kutoka kwa warembo hao wa Kenya, lakini bahati mbaya fahari mmoja hakutokea. 
Huddah Monroe ametumia Snapchat kuelezea sababu iliyomfanya ashindwe kuja kwenye party hiyo kuwa ni kushindwa kufikia makubaliano waliyokuwa wamejipangia na Diamond na hivyo ikamlazimu kukatisha kuja katika dakika za mwisho.
 
 

Tuesday, December 27, 2016

Majina ya waliokuwa wamefaulu katika usaili wa ajira serikalini, kufutwa.

Watu wote waliokuwa wamefanya usaili kwa ajili ya ajira serikalini kupitia Sekretarieti ya Ajira ya Utumishi wa Umma kabla ya ajira kusimamishwa, watafutwa ndani ya miezi 6 na kulazimika kuomba upya kipindi ajira hizo zitakapotangazwa tena.

Hilo limebainishwa na sekretarieti hiyo kupitia majibu kwa wadau mbalimbali kwa mwezi Desemba ambao wamekuwa wakiuliza maswali na kujibiwa kila mwezi kupitia tovuti yake, na kubainisha kuwa suala hilo litawahusu wale ambao walifaulu usaili lakini kabla hawajapangiwa vituo vya kazi au kupewa barua na waajiri wao, ajira zikasimamishwa ili kupisha uhakiki wa watumishi hewa.

Taarifa hiyo imesema kuwa huo ni utaratibu wa kawaida wa sekretarieti hiyo, kwamba majina ya waliofaulu huhifadhiwa kwenye kanzi data (Database) kwa muda usiozidi miezi sita, na baada ya hapo majina hayo hufutwa.

"Kwa mujibu wa Taratibu zetu za uendeshaji wa mchakato wa ajira majina ya waombaji kazi waliofaulu lakini hawakupangiwa vituo vya kazi kwa sasa huhifadhiwa kwenye kanzi data kwa muda usiozidi miezi sita" Imesema taarifa hiyo

Swali lingine kutoka kwa mdau na jibu lake liko kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa ajira zilisitishwa mwezi Juni, na sasa ni mwezi Desemba, utaratibu huo unamaanisha kuwa wasailiwa wote waliofaulu lakini hawakupangiwa kazi, watalazimika kusubiri upya matangazo ili waombe upya na kufanya usaili upya.

Aidha Sekretariet hiyo imebainisha kuwa zoezi ya uhakiki wa watumishi hewa 
 
bado linaendelea, na kwamba wakipewa ruhusa ya kutangaza ajira wakati wowote watatangaza.
 

Tuesday, December 27, 2016

Hili ni ombi la Rais Magufuli kwa Watanzania mwaka 2017

Rais wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amewaomba Watanzania wote kuutunza na kuudumisha umoja katika mwaka 2017 huku akiwataka kufanya kazi kwa bidii.

Rais Magufuli amendika maombi hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter ambapo pamoja na kuwaomba Watanzania kutekeleza mambo hayo amewatakiwa Watanzania heri ya mwaka mpya.

“Ombi langu kwa Watanzania wote tuulinde,tuutunze na kuudumisha umoja wetu ktk mwaka 2017 kwa kufanya kazi kwa bidii. MUNGU IBARIKI TANZANIA,” ameandika Rais Magufuli.

Tuesday, December 27, 2016

Mbunge Wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe Na Mkewe Wapata Mtoto Wa Kike.

July 14, 2016 Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe aliuacha  rasmi ukapera baada ya kufunga ndoa na mpenzi wake. Leo December 27 2016 Zitto Kabwe na mkewe wamepata mtoto wa kike ambaye wamempa jina la Josina – Umm Kulthum.

Zitto Kabwe amezitoa taarifa hizo kwenye mitandao ya kijamii.
 
Ameandika: ''Mimi na Mke wangu mpendwa tumebarikiwa na Allah kupata mtoto wa kike. Mtoto na mama yake wana afya njema kabisa, Mashaallah. Mtoto amezaliwa saa moja na dakika 45 asubuhi leo Disemba 27, 2016''''.
 
''Binti yetu ataitwa Josina - Umm Kulthum. Josina kwa heshima ya mwanamama mpigania Uhuru wa Kusini mwa Afrika, Josina Muthembi Machel wa FRELIMO. Umm Kulthum kwa heshima ya mama yangu mdogo na pia jina la binti wa Mtume Muhammad (SAW)''
 
''Tunamshukuru mungu kwa Baraka hizi za mtoto Josina - Umm Kulthum Zitto''

Tuesday, December 27, 2016

Moto wateketeza nyumba 50 wamiliki wake wakila Krismasi

MOTO mkubwa umezuka na kuteketeza nyumba zaidi ya 50 katika kisiwa cha Kasalazi kilichopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa mkoani Mwanza.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 3:00 usiku, linadaiwa kuwa ni la nne kutokea kisiwani humo katika miaka ya karibuni.

Imeelezwa kuwa moto huo ulizuka na kuteketeza nyumba hizo huku wamiliki wake wakiwa kwenye shamra shamra za Krismasi.

Nyumba zilizoteketea kwa moto ni zile zilizojengwa kwa kutumia mabanzi ya miti, mbao na kuezekwa kwa maturubai, nyasi na baadhi kwa bati.Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kasalazi, Andrew Mkama, amesema  kuwa wakati tukio hilo linatokea, wakazi wengi wa kisiwa hicho walikuwa kwenye kumbi mbalimbali za starehe kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2,000 iliyopita.

Mkama alisema alilazimika kupuliza filimbi kuashiria hatari na wananchi walijitokeza na kuanza jitihada za kuuzima moto huo licha ya kwamba tayari ulikuwa umeshasababisha madhara makubwa kwa kuunguza mali zote zilizokuwa ndani yake.
 
Hata hivyo alisema hakuna mtu aliyekufa wala kujeruhiwa kutokana na janga hilo.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema moto huo umesababisha hasara kubwa kwao.

Mmoja wa mashuhuda hao, Raphael Bituro, anayemiliki duka la vinywaji, alisema baada ya kupulizwa filimbi kuashiria hali ya hatari, baadhi ya wateja wake walikurupuka bila kulipia vinywaji vyao na hivyo kusababisha apate hasara.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole, alithibitisha kisiwa hicho kuungua kwa moto.

Kipole alisema ameagiza kufanyika kwa uchunguzi ili kubaini ukubwa wa madhara hayo na kuahidi kutoa taarifa zaidi atakapopewa ripoti hiyo.

Kisiwa hicho kinakadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya 2,400 ambao hujihusisha na shughuli za uvuvi na ni miongoni mwa visiwa vinane vilivyopo kwenye Kata ya Bulyaheke wilayani Sengerema.
 
 

Tuesday, December 27, 2016

Polisi Wapigwa Marufuku Kuvisha Mabango Madereva Walevi

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga amesema wamesitisha kuwatangaza watuhumiwa katika mitandao ya kijamii  baada ya kupata malalamiko ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Hata hivyo, amesema hadi wanasitisha walikuwa wamewakamata  madereva 20 wa Dar es Salaam, lengo likiwa ni kuonyesha jamii ili wengine wenye tabia hiyo wajifunze kupitia kwa wenzao na kuacha kuendesha wakiwa wamelewa.

“Kwa sababu watu wengi wapo mtandaoni ilikuwa rahisi ujumbe kuwafikia kwa wakati mmoja. Tulipata malalamiko ya haki za binadamu kuwa kufanya hivyo kunawasababishia kudhalilika katika familia zao, tukaona tusitishe,” amesema Mpinga.

Hata hivyo, amesema pamoja na kusitisha utaratibu huo, madereva wasijisahau kwa sababu vijana wapo kazini na wanaendelea kuwakamata wale wote watakaokiuka sheria za barabarani, ikiwamo hiyo ya kuendesha wakiwa wamelewa.

Awali, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imelitaka Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, kuacha kuziweka hadharani picha za madereva wanaotuhumiwa kukiuka sheria, badala yake liwafikishe mahakamani kwanza.

Kauli ya Tume hiyo imetokana na utaratibu ulioanzishwa na trafiki wa kuwavisha mabango madereva wanaotuhumiwa kukiuka sheria ambayo yameandikwa makosa yao na kurushwa kwenye mitandao ya kijamii kabla hawajafikishwa mahakamani.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Bahame Nyanduga amesema hayo wakati akifafanua kuhusu kusitisha kuwaanika katika mitandao ya kijamii madereva wanaokamatwa na trafiki kwa makosa ya usalama barabarani ikiwamo ulevi

Tuesday, December 27, 2016

Benki Kuu (BoT) yatolea ufafanuzi taarifa za kutotumika tena noti ya shilingi 500

Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuwafahamisha wananchi wote kuwa habari inayoenea katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwamba noti ya shilingi mia tano haitatumika tena baada ya Disemba 31, 2016 sio taarifa ya kweli na ni uvumi unaopaswa kupuuzwa.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za kibenki BoT, Marcian Kobello ambapo alifafanua kuwa noti ya shilingi 500 itaendelea kuwepo katika mzunguko sambamba na ile sarafu ya shilingi 500 hadi pale noti hiyo itakapotoweka mikononi mwa wananchi.

Aidha, Kobello amewataka wananchi kupuuza taarifa zinazoeleza vinginevyo kwani si za kweli.

Serikali iliamua kuleta sarafu ya TZS 500 baada ya kuwepo malalamiko kuwa noti ya TZS 500 ambayo ndiyo inazunguka zaidi inachakaa mapema sana.
 

Tuesday, December 27, 2016

Mkulima achomwa mkuki mdomoni, watokea shingoni

MKULIMA na mkazi wa kijiji cha Dodoma Isanga kata ya Masanze wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Augustino Mtitu,amechomwa mkuki mdomoni na kutokea shingoni.

Umemjeruhi hivyo kulazimika kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, kufanyiwa upasuaji kuondoa mkuki huo na kuokoa maisha yake.

Mtitu na wengine wanane walijeruhiwa katika vurugu zilizohusisha jamii ya wafugaji wa Kimasai na wakulima wa kijiji hicho kilichopo wilayani Kilosa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Alisema mpaka jana watu watatu walikuwa wanashikiliwa na Polisi, na msako unaendelea kuwasaka wale wote waliohusika katika kufanya vurugu hizo.

Tukio hilo ni la Desemba 25, mwaka huu, baada ya mtu huyo kujaribu kuzuia vurugu hizo, zilizokuwa zimetokea baada ya wafugaji hao kulisha mifugo yao katika shamba la maharage na mahindi katika kijiji hicho.

Mtitu akijaribu kuzuia vurugu hizo, aliishia kuchomwa mkuki na mmoja wa wafugaji wa jamii hiyo, ambao baada ya tukio hilo walikimbia kutoka eneo hilo.

Kutokana na tukio hilo, wananchi wenzake waliamua kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya matibabu.

Lakini, alihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji na matibabu zaidi ya kuokoa maisha yake.

Baada ya kutokea kwa tukio hilo, muda mfupi baadaye wafugaji hao walirudi tena kijijini hapo, kwa lengo la kuokoa mifugo yao iliyokuwa imekamatwa, na ndipo walipoanzisha tena vurugu kwa kuwashambulia watu wengi wanane akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji pamoja na wa Kitongoji.

Watu watano, kati ya waliojeruhiwa, walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kupatiwa matibabu. Diwani wa Kata ya Masanze, Bakari Pilo, akizungumza kwa njia ya simu, alisema hilo ni tukio la tatu kutokea kwenye kata yake katika kipindi kifupi.

Alisema vitendo hivyo vinaendelea kuhatarisha usalama wa wananchi, hasa wakulima, kufuatia mamlaka zinazohusika kushindwa kuwahamishia wafugaji katika eneo walilokuwa wametengewa, licha ya suala hilo kupitishwa kwenye vikao vya Baraza la Madiwani.

Stanley Andrea, ambaye ni ndugu wa Mtitu, yupo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro akimuunguza nduguye, alisema kuwa tukio hilo ni la Desemba 25, mwaka huu majira ya saa 5 asubuhi kwenye mashamba ya wakulima baada ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya mahindi na maharage ili kulisha mifugo.

Alisema, wakulima wenye mashamba hayo,waliamua kuifukuza mifugo hiyo, lakini wafugaji wa jamii ya Kimasai, waliingilia kati na kuanza kuwapiga kwa fimbo wakulima na kusababisha kutokea kwa vurugu baina ya pande mbili hizo.

Alisema, mfugaji mmoja wa Kimasai alichukua mkuki na kumchoma Mtitu sehemu ya mdomoni na kutokezea shingoni na kuwajeruhi wengine wanane, akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji na wa Kitongoji, ambao baadhi wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.

Alisema kuwa vurugu ziliongezeka, pale wafugaji hao waliporudi kijijini hapo kwa ajili ya kuikomboa mifugo yao iliyokuwa inashikiliwa, kabla ya kufika kwa askari polisi kutoka mjini Kilosa.

Muuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Sanifa Mdee, alisema walimpokea mgonjwa huyo akiwa na mkuki mdomoni, ulitokea upande wa shingoni na kuanza kumpatia matibabu na kumtoa mkuki huo, ambapo amelazwa wodi namba moja hospitalini hapo.

Hata hivyo, alisema kutokana na mkuki huo kuchomwa kwa nguvu, ulijeruhi baadhi ya meno yake na kuharibu fizi, hali iliyosababisha jana madaktari kumfanyia upasuaji wa kurekebisha fizi zake, ambapo baada ya kutolewa mkuki huo, hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.

Tuesday, December 27, 2016

Taarifa Kwa Umma Kuhusu Gharama Za Matibabu Ya Dawa Ya Sumu Ya Nyoka Nchini

Kama tunavyofahamu, nchi yetu ina aina mbalimbali za nyoka ambao pindi wakimuuma mtu huleta madhara mbalimbali ya kiafya. Aidha tunafahamu kwamba tatizo hili lipo zaidi katika maeneo ya vijijini ambako uwezo wa wananchi kumudu gharama za matibabu ni mdogo.

Dawa za kutibu sumu ya nyoka huagizwa kutoka nje ya nchi. Dawa hizo siyo tu hazipatikani kwa urahisi, bali pia zinapatikana kwa gharama kubwa. Bei ya kununulia dawa hizi ni kati ya dola za kimarekani 55 hadi 85 (yaani shilingi za kiTanzania 118,250 hadi 182,750) kwa kichupa kidogo (vial) kimoja. Kichupa hicho huweza kutumika kwa wagonjwa wanne, lakini mara tu baada ya kufunguliwa dawa hiyo huwa haifai tena kutumika ndani ya mwezi mmoja tu.
 
Pamoja na changamoto hizo, Serikali kupitia MSD kila mwaka huagiza dawa hizi kwa ajili ya mahitaji hayo ya kutibu wagonjwa walioumwa na nyoka, ambapo bei ya kuinunua kutoka MSD ni TZS 200,000/= kwa kichupa kimoja. Hospitali zetu mbalimbali zimekuwa zikiagiza dawa hizi kutoka MSD na kwa washitiri wengine kwa bei hii au zaidi na kuwatibu waathirika wanaohitaji dawa za sumu za nyoka mara zinapohitajika. 
 
Napenda kuwakumbusha kwamba kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, huduma za tiba hutolewa bure kwa makundi maalum, au kwa kuchangiwa kwa sehemu ya gharama, au kwa kupitia mfumo wa Bima mbalimbali za Afya kama vile CHF. Kwa wale wasio na uwezo na wanaothibitishwa kuwa hawana uwezo, utaratibu wa msamaha hutumika.
 
Katika kuhakikisha kwamba wananchi wanaohitaji dawa ya  sumu ya nyoka wanahudumiwa ipasavyo, Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anatoa maelekezo yafuatayo:-

Waganga Wakuu wa Mikoa na Viongozi wa Hospitali zote nchini wahakikishe kuwa Hospitali zote za umma zinaingiza dawa hii katika dawa za dharura ili iweze kununuliwa kama dawa zingine za dharura kupitia kifungu cha fedha za dawa za dharura.  
 
Kwa wagonjwa ambao watakuwa na Bima ya Afya, basi gharama za matibabu hayo zitalipwa kwa kupitia utaratibu huo wa Bima. Wananchi wanahimizwa kujiunga na Bima za Afya (CHF/NHIF) ili kupata unafuu wa matibabu haya na mengine. Mfano CHF - gharama ya kujiunga katika Halmashauri mbalimbali kwa kaya ni kati ya shilingi 5,000/= hadi shilingi 30,000/= kwa mwaka.
 
Kwa wagonjwa ambao watakuwa hawana Bima ya Afya, hao watatakiwa kuchangia gharama hiyo kwa nusu ya bei ya gharama ya dawa hizi au kwa kiwango kingine kitakachoamuliwa na Mganga Mkuu wa Serikali kadri itavyohitajika. 
Hii ni kutokana na ukweli kwamba kung'atwa na nyoka ni ajali na wananchi wengi wanaopatwa na ajali hii wapo maeneo ya vijijini ambao kimsingi uwezo wao wa kumudu gharama hizi kubwa za matibabu ya dawa ya sumu ya nyoka ni mdogo.
 
Wagonjwa watakaothibitika kuwa hawana fedha za kuchangia gharama hiyo, basi hospitali husika kwa kupitia mpango wa msamaha wa kulipia huduma za afya wahakikishe kwamba wanampatia mgonjwa huduma hizo kwa utaratibu wa msamaha wa gharama hizo.

Aidha, kwa kuwa nchi yetu ni kubwa na ina nyoka wengi, Mhe Waziri wa Afya anawaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kupitia kwa uangalifu takwimu za wagonjwa walioumwa na nyoka katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi 2016 na kuziwasilisha Wizarani kabla  ya tarehe 31 Januari 2017 ili  kupata takwimu za mahitaji halisi ya dawa ya sumu ya nyoka nchini. Hii itasaidia  kuboresha upangaji, uagizaji na upatikanaji wa dawa hizo nchini. 
 
Vile vile, Waziri wa Afya ameiagiza Bohari ya Dawa (MSD)  kuweka utaratibu wa haraka wa kununua dawa hizo moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ili kupata unafuu wa bei.

Imetolewa na:-
Nsachris Mwamwaja
Mkuu Kitengo cha Mawasiliano Serikalini  - Afya
26/12/2016
 

Tuesday, December 27, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne ya Disemba 27


 
jumanne hii jumanne hii Reviewed by RICH VOICE on Desemba 27, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...