habari za jumanne hii




Tuesday, December 20, 2016

Taasisi zinazohamasisha ushoga kufutwa


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ametaka apewe taarifa kuhusu taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) wanaohamasisha au kutangaza ndoa za jinsia moja nchini ili azifutie usajili mara moja.

Aidha ametaka kutajwa kwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua za kisheria kwa kujihusisha na vitendo hivyo ambavyo vinapigwa vita dunia nzima.

Nchemba aliyasema hayo jana mjini Kibaha alipokuwa akizungumza na taasisi za Kijeshi za mkoa huo zikiwemo Uhamiaji, Polisi, Magereza na Zimamoto juu ya kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Alisema kuwa taasisi hizo hazifai kwani zinafanya kazi ya laana ambayo ni kinyume cha maadili ya Kitanzania na hazistahili kuendelea kufanya kazi kwa upotoshaji huo.

“Leteni majina ya taasisi hizo ili tuzifute kwani hazistahili kuendelea kufanya jambo hilo ambalo ni laana na halipaswi kufumbiwa macho ndani ya jamii,” alisema Nchemba.

Kamanda wa polisi mkoani Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa jeshi hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na upungufu wa vitendea kazi, ikiwa ni pamoja na magari.

Mushongi alisema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto hizo wamekuwa wakikabiliana na uhalifu kwenye mkoa huo ambao umekuwa kimbilio la wahalifu kutoka mikoa jirani ya Dar es Salaam.
 
 

Tuesday, December 20, 2016

Benki ya AfDB yaikopesha Tanzania Bilioni 360 kwa ajili ya bajeti ya 2016/2017

Na Benny Mwaipaja-WFM, Dar es salaam
Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, imeipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola Milioni 164, karibu Shilingi Bilioni 360, kwaajili ya kuchangia Bajeti kuu ya Serikali katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2016/2017 pamoja na kuongeza mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini-TADB.

Mikataba miwili imesainiwa jana Jijini Dar es salaam kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James kwa niaba ya Serikali na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayeondoka Dkt. Tonia Kandielo.

Mkataba wa kwanza uliosainiwa ni kwa ajili ya kutunisha Mfuko Mkuu wa Serikali ambapo Benki hiyo imetoa dola za kimarekani milioni 70 sawa na tsh 154 bilioni ambazo zitaelekezwa kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini-TANESCO.

Mkataba wa pili ni kwaajili ya kuongezea mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini-TADB wenye thamani ya dola Milioni 94 sawa na shilingi Bilioni 204 kwa ajili ya kuiongezea uwezo Benki hiyo kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima ili kuongeza mnyonyoro wa thamani kuanzia uzalishaji, uongezaji thamani na upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima.

Uhai wa mikopo yote miwili utakuwa ni miaka 40 ambapo serikali itaanza kuilipa baada ya miaka kumi tangu kutolewa kwake, huku riba yake ikiwa chini ya asilimia 1.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mkopo huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, amesema mkopo huo umekuja wakati muafaka na utasaidia kukuza na kuimarisha TANESCO na kuendeleza kilimo nchini.

“Tanzania ni nchi iliyonufaika zaidi na mikopo yenye masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika-AFDB ikilinganishwa na nchi nyingine yoyote iliyoko katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika,” alisema Bw. James.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa AFDB anayeondoka Dkt. Tonia Kandielo amesema kuwa hadi sasa Benki yake imeipatia Tanzania mkopo wenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 2, ambazo zimewekezwa kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, nishati ya umeme, elimu na kilimo.

“Ninaamini kuwa hatua ya kuongeza mtaji katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo-TADB itachochea maendeleo ya kilimo nchini, na tunaahidi kuwa tutaendelea kuiwezesha zaidi siku zijazo,” alisema Dkt. Kandielo.

Kuhusu Sekta ya Nishati, Dkt. Kandielo amesema kuwa Benki yake imeona umuhimu wa kuliwezesha shirika hilo ili liweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi ili kuchochea uchumi wa Taifa.

“Mikopo hii inahusiana na vipaumbele tulivyoviweka kama Benki ambavyo viko katika malengo matano ambapo tunataka kuwekeza katika sekta ya nishati, uzalishaji wa chakula, kuendeleza viwanda, kuiunganisha Afrika na kuboresha maisha ya waafrika kwa ujumla,” aliongeza Dkt. Kandielo

Wakati huo huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amemuaga rasmi Dkt. Tonio Kandielo ambaye amehamishiwa nchini Afrika Kusini kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo atakaye simamia Kanda ya Kusini mwa Afrika.

Dkt. Mpango, amesifu jitihada kubwa zilizofanywa na mwana mama huyo katika kipindi cha miaka 6 aliyokuwepo hapa nchini ambapo ameweza kusimamia vizuri maslahi ya Tanzania katika Benki hiyo.

Amesema kuwa katika kipindi hicho Tanzania imeshuhudia maendeleo makubwa katika sekta za ujenzi wa miundombinu ya barabara, kilimo, maji na umeme, ambapo benki hiyo ilihakikisha kuwa miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa.

Amemwomba Mkurugenzi Mkuu huyo kuwezesha upatikanaji wa fedha kwaajili ya ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard gauge) inayohitaji fedha nyingi, kusimamia utekelezaji wa mradi wa umeme wa kikanda unaoanzia nchini Zambia, uboreshaji wa Bandari ya Itungi na Mbambabay.

Akijibu hoja za Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Dkt. Tonia Kandielo amesema kuwa anaamini mrithi wake ataendeleza mazuri aliyoyafanya na kwamba yeye binafsi atahakikisha anafuatilia kwa karibu miradi ambayo mikataba yake imesainiwa katika nyanja za maboresho ya sekta ya umeme na kilimo.
 
 

Tuesday, December 20, 2016

Kiwango cha Pesa Kesi za Mafisadi Kushushwa Chini ili Kuwabana Wengi

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema serikali inatarajia kujadili kushusha kiwango cha fedha kinachohusika katika makosa ya rushwa na uhujumu uchumi kwenye mahakama ya mafisadi ili kukomesha vitendo vya rushwa.

Mwakyembe alitoa kauli hiyo jana mara baada ya kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

“Nimeulizwa sana na waandishi wa habari tangu Julai hadi sasa walitegemea kungekuwa na kesi nyingi lakini kuna kesi moja katika Mahakama ya Mafisadi tumekuja kubaini kwamba uchache wa kesi ndiyo mafanikio makubwa ya hatua ya kisheria tuliyochukua,”amesema.

Aliongeza kwa sasa waliozoea kupora mabilioni wamerudi nyuma ambapo wezi hao wameonekana wakiiba fedha chini ya Sh bilioni moja iliyopo kisheria hivyo wanategemea kujadili sheria hiyo ili iwalenge hata wanaochukua kiasi kidogo.

“Sisi kama serikali tukiona wizi sasa umenza kupungua na kuenea katika viwango vya Sh milioni 400, 500, 700 tumeanza kujadiliana kuangalia uwezekano wa kushusha kiwango cha fedha ili tuweze kukomesha kabisa udokozi, ubadhilifu, wizi wa fedha au mali ya umma,”alisema.

Aidha alifafanua uamuzi wa Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda kutafuta vijana wanaojua sheria ili kusaidia wananchi kabla ya kwenda mahakamani ni mzuri.

Aliongeza kuwa tayari wamepeleka mswada wa msaada wa kisheria ambao utasaidia wananchi hasa wa vijijini na wanawake ambao ndiyo wanaumizwa na desturi zilizopitwa na muda ili kuwasaidia kupata haki na itakuwa na wasaidizi wa kisheria nchi nzima wapatao 4,900.

Makonda alisema wamejadili utoaji na upatikanaji wa haki kwa wakati kwani kuna changamoto ya watu kuwa wengi na kuchelewa kupata haki zao.

Alisema kwa kuona adha hiyo mkoa huo kwa kushirikiana na Wakuu wa wilaya watajenga Mahakama za Mwanzo 20 ili kuongeza kasi za utoaji na upatikanaji wa haki kwa wananchi endapo wanapopelekwa vituo vya polisi.
 
 

Tuesday, December 20, 2016

Polepole atangaza 'vua gamba' ya CCM kivingine

Mabadiliko yaliyofanywa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yamekuja na mkakati mpya wa kuwavua ‘gamba’ makada wa chama hicho wenye ukwasi waliovuna kinyume na taratibu.

Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole amesema kuwa wako katika mkakati wa kukisafisha zaidi chama hicho, akiwataka matajiri wenye ‘makandokando’ wajiondoe mapema.

“Kuwa tajiri si dhambi na si kwamba CCM inafukuza matajiri, hapana. Tatizo letu kama CCM katika mwelekeo mpya, mtazamo mpya na maegeuzi yanayofanyika, hatuhitaji kuwa na aina ya matariji wanaojipatia utajiri wao kwa hila, kwa rushwa na kwa dhuluma,” alisema Polepole katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini.

“Ukijiona wewe ni tajiri na mikono yako ni michafu kwa maana ya kuwa na makando ya kukosa uaminifu, hulipi kodi, ukae mbali na CCM,” aliongeza.

Alisema watawachukulia hatua za kuwaondoa ndani ya chama hicho na kuwakabidhi kwa vyombo vya dola ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Tangu alipochaguliwa, Polepole amekuwa akisisitiza kuwa chama hicho kitajikita katika msingi wake wa kuwatumikia wanyonge.

Mkakati huo wa kuwang’oa matajiri wasiowaaminifu ndani ya chama hicho unafanana na oparesheni iliyobatizwa jina la ‘Vua Gamba’ ndani ya chama hicho miaka kadhaa iliyopita, iliyolenga kuwang’oa viongozi na vigogo ambao walibainishwa kujipatia mali kinyume cha utaratibu na mafisadi.
 
 

Tuesday, December 20, 2016

Mahakama Kuu Yakubali Ombi la Godbless Lema Kuongezewa Muda wa Rufaa ya Dhamana Yake

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, imelikubali ombi la  Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema,  la kuongezewa muda wa kuwasilisha Notisi ya nia ya kukata rufaa ya dhamana yake.

Akitoa uamuzi wake kuanzia saa 12:26 hadi saa saba mchana, Jaji Dk. Modesta Opiyo wa Mahakama hiyo, alisema Mahakama hiyo imeruhusu maombi ya kuwasilisha Notisi ya kuomba kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya nia ya kukata rufaa ya dhamana yake.

Jaji Opiyo amesema hoja za Upande wa serikali zilizowasilishwa na Wakili Hashim Ngole za kudai waleta maombi hayo walikuwa wazembe na walichelewa siku nne kuwasilisha Notisi baada ya rufaa yao kuondolewa na Jaji Fatuma Masengi Desemba 2 hazina mashiko.

Alisema kuondoa kesi mahakamani haimaanishi kuwanyima fursa ya kupigania nia ya kukata rufaaa, bali milango inakuwa wazi haijafungwa.

Aidha amesema siku nne zinazolalamikiwa kuwa walichelewa kutoa maombi hayo, mahakama inaona hoja hizo hazina mashiko sababu siku mbili kati ya hizo zilikuwa siku za mapumziko Jumamosi na Jumapili, hivyo walitumia siku mbili kuandaa nyaraka na kuleta maombi hayo.

Pia alisema katika maombi hayo wametoa pia sababu za nia ya kutaka kukata rufaa na sababu hizo ziko wazi. 
“Katika hili hakuna uvunjifu wowote wa sheria uliofanywa na kutokana na hilo Mahakama hii inatumia busara zake kuruhusu maombi haya ya kutoa Notisi ya kuomba kuongezewa muda wa kukata rufaa juu ya dhamana yake Mbunge huyu,” alisema Jaji Opiyo.

Amesema Mahakama inatoa siku kumi pekee kuanzia uamuzi huo utolewa mleta maombi (Lema) kuwasilisha Notisi yake ya kuomba kuongezewa muda wa kukata rufaa hadi tarehe 30 shauri hili likakaposikilizwa tena.

Baada ya kutolewa kwa maamuzi hayo, tayari Wakili Sheck Mfinanga ameshakata Notisi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na kupokelewa.

Mfinganga amesema wanasubiri mahakama ili wapangiwe Jaji waendelee na kesi hiyo ya hatma ya dhamana ya Lema.
 

tuesday, December 20, 2016

Polisi yamnasa mtuhumiwa Sugu wa utapeli Tanzania

Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa  kumkamata mtuhumiwa wa utapeli anayejulikana kwa jina la  Wilfred Masawe (36) ,  mkazi wa  Buza, Temeke jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi Mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mbinu mbalimbali kutapeli zikiwemo kujitambulisha kama kiongozi wa serikali kwa kutumia mtandao wa Whatsapp,  huku akieleza kuwa yupo nje ya nchi na kuna tatizo la msiba ambao umetokea nchini na unamuhusu na hivyo alikua akitoa maelekezo kwa watendaji wa serikali waweze kusaidia gharama za matibabu hospitalini, gharama za kusafirisha mwili wa marehemu na gharama za mazishi.

Taarifa hiyo pia imesema mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mbinu ya kujifanya kiongozi mkubwa wa dini ya kikristo (Askofu) na kuwaambia waumini na viongozi mbalimbali kuhusu maandalizi ya makongamano ya kidini kwa lengo la kuwaomba michango kuweza kufanikisha makongamano hayo.

Baadhi ya matukio aliyofanikiwa kutapeli ni pamoja na kuwatapeli viongozi wa serikali, wafanyabiashara, mameneja na wakurugenzi wa taasisi za umma, wanasiasa pamoja na waumini wa madhehebu ya dini.

Aidha, matukio yote hayo alikuwa akiyafanya peke yake na alikuwa akiyaendesha kwa mawasiliano ya njia ya ujumbe mfupi (SMS) bila kuzungumza kwa simu.

Jeshi la Polisi linakamilisha taratibu za kisheria ili mtuhumiwa huyo afikishwe mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
***
 

Tuesday, December 20, 2016

Mwenyekiti Wa CCM Taifa Rais Magufuli Akutana Na Viongozi Wapya Wa Chama Aliowateua Hivi Karibuni Na Dc Mteule Wa Ubungo

Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Dkt John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mteule Mhe. Kisare Makori akishuhudiwa na viongozi wapya wa CCM aliowateua hivi karibuni. Kutoka kulia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole, Katibu NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Kanali Ngemela Eslom Lubinga na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Ndg. Rodrick Mpogolo walipoenda kujitambulisha Ikulu jijini Dar es salaam leo Desemba 20, 2016.


Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Dkt John Pombe Magufuli akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mteule Mhe. Kisare Makori (kushoto) pamoja na viongozi wapya wa CCM aliowateua hivi karibuni. Kutoka kulia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole, Katibu NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Kanali Ngemela Eslom Lubinga na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Ndg. Rodrick Mpogolo walipoenda kujitambulisha Ikulu jijini Dar es salaam leo Desemba 20, 2016.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mteule Mhe. Kisare Makori (kushoto) akibadilishana mawasiliano na na viongozi wapya wa CCM walioteuliwa hivi karibuni. Kutoka kulia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Ndg. Rodrick Mpogolo na Katibu NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Kanali Ngemela Eslom Lubinga walipoenda kujitambulisha kwa Mwenyekiti wa CCM Rais Dkt John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam leo Desemba 20, 2016. PICHA NA IKULU
 
 

Tuesday, December 20, 2016

Serikali Haijazuia Watumishi Wa Umma Kukopa Benki

Kumekuwa na taarifa inasambazwa katika mitandao ya kijamii, makundi ya ‘WhatsApp’, ‘Facebook’ na majukwaa mbalimbali ikieleza kuwa Serikali imepiga marufuku watumishi wa umma kukopa Benki,SACCOS,VICOBA na Taasisi mbalimbali za kifedha.

Taarifa iliyotolewa leo tarehe 20 Desemba 2016 na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeeleza kuwa taarifa inayosambazwa, ambayo imetafsiri mawasiliano ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni ya kupotosha, hivyo watumishi wote wa umma wanaombwa kuipuuza.

Vilevile watumishi wa umma wametakiwa kuzingatia kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali HAINA mamlaka ya kuzuia wala kuruhusu mtumishi yeyote wa Serikali kukopa au kutokopa katika Taasisi yoyote ya Fedha nchini.

Watumishi wa umma pia wamekumbushwa kuwa mikopo yote ya watumishi wa umma katika Taasisi za Fedha hutolewa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu zilizopo ili mradi mtumishi awe ametimiza vigezo.

Aidha, watumishi wa umma wameaswa kuacha tabia ya kusambaza taarifa zisizo za kweli na ambazo zina mamlaka husika ya kuzitoa ikiwa ni pamoja na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
***
 

Tuesday, December 20, 2016

Ajali yaua Watu Wanne wakiwemo Polisi Wawili

Watu wanne wakiwamo polisi wawili, wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupindua katika kijiji cha Seruka kata ya Chipogoro tarafa ya Rudi wilayani Mpwapwa mkoa wa Dodoma.

Ajali hiyo ilitokea Desemba 19, mwaka huu, saa 11:30 jioni katika kijiji hicho baada ya gari walilokuwa wakisafiria T517 CDL Toyota Alphat katika barabara kuu ya Dodoma- Iringa, kuacha njia na kupinduka na kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi tisa.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ernest Kimola, amesema gari hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na Aggrey Lucas, baada ya kufika katika kijiji hicho, liliacha njia na kupinduka na kusababisha vifo vya askari Konstebo Mahende na Konstebo Sasi Mwita ambaye ni askari mkoa wa Songwe.

Kamanda Kimola amewataja wengine waliofariki katika ajali hiyo ni mke wa Konstebo Mwita, Pendo Mwita na Emaculata Nyangi.

Amewataja majeruhi wa ajali hiyo ni Neema Mwita (8), Jenifa Mwita (4), Nyangi Wambura (23), Konstebo Nashon (23) ambaye ni polisi kituo cha Tunduma na Baraka Chacha (9).

Wengine ni Juli Mwita (6), Pc Enock ambaye ni mmiliki wa gari lililopata ajali, Makongoro Charles na Elizabeth Cosmas ambao wote wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Dodoma.

Aidha, kamanda Kimola amesema miili ya marehemu hao waliofariki katika ajali hiyo, imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya mkoa wa Dodoma.
 
habari za jumanne hii habari za jumanne hii Reviewed by RICH VOICE on Desemba 21, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...