jumatano ya leooooo

Wednesday, December 14, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumatano ya Disemba 14

Wednesday, December 14, 2016

Rais Dkt Magufuli ateua Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, jana tarehe 13 Desemba, 2016 amemteua Dkt. Khatib M. Kazungu kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Dkt. Khatib M. Kazungu anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Doto James ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Kabla ya Uteuzi huo Dkt. Khatib M. Kazungu alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, iliyopo katika Mkoa wa Mtwara.

Uteuzi huu unaanza mara moja.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
 

Wednesday, December 14, 2016

Hashim Rungwe kumtetea ‘Ndama mtoto wa ng’ombe’....Kesi yake Yaahirishwa Hadi Disemba 27


Wakili wa kujitegemea, Hashimu Rungwe amejitokeza kumtetea mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam, Ndama Shabani Hussein maarufu kama ‘Pedeshee Ndama mtoto wa Ng’ombe’. 

Rungwe aliyekuwa mgombea urais kupitia Chaumma katika Uchaguzi Mkuu uliopita, alijitokeza jana na kujitambulisha mahakamani kuwa ndiye atamtetea mshitakiwa huyo. 

Ndama mtoto wa ng’ombe (44) anakabiliwa na mashtaka ya kughushi, kutakatisha fedha na kujipatia dola za Marekani 540,390 kwa njia ya udanganyifu. 

Baada ya kujitambulisha mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa, Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa alisema kesi hiyo imepangwa kutajwa, upelelezi bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine. Hakimu Nongwa aliiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 27,2016. 

Mshtakiwa huyo alipelekwa rumande kwa sababu miongoni mwa mashtaka yanayomkabili limo shtaka la kutakatisha fedha ambalo halina dhamana. 

Katika kesi hiyo, Ndama anadaiwa kuwa Februari 20,2014 jijini Dar es Salaam, alighushi kibali cha kusafirisha madini kuonyesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha kilo 207 za dhahabu yenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000 kwenda Australia wakati akijua si kweli. 

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa Machi 6, 2014 jijini Dar es Salaam alitengeneza kibali cha Umoja wa Mataifa ofisi ya Dar es Salaam akijaribu kuonyesha dhahabu hiyo kutoka Congo inatarajiwa kusafirishwa kwenda Australia. 

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 2014 katika jiji la Dar es Salaam alitakatisha fedha kwa kufanya muhamala wa dola za Marekani 540,390 kwa kuelekeza ziwekwe katika akaunti namba 9120000085152 iliyopo katika benki ya Stanbic yenye jina la Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited na kuanza kuzitoa taslimu wakati akijua fedha hizo zinatokana na zao la uhalifu.

Wednesday, December 14, 2016

Lowassa adai T.B Joshua ameitabiria Chadema ushindi


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amesema ataingia Ikulu baada ya miaka minne ijayo na rafiki yake T.B Joshua amemtabiria kuwa Serikali ijayo itaongozwa na Chadema. 

Lowassa, ambaye alishika nafasi ya pili katika kinyang’anyiro cha urais mwaka jana, ameshaonyesha nia ya kuingia tena kwenye mpambano huo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. 

Akizungumza na viongozi na wanachama wa Chadema mkoani Tabora, waziri huyo mkuu wa zamani alisema ana uhakika wa kuingia Ikulu bila ya umwagaji wa damu. 

Huku akishangiliwa, Lowassa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliwashukuru wana Tabora na Watanzania kwa ujumla kwa kura walizompa katika uchaguzi mkuu uliopita. 

Lowassa aliwaeleza wanachama na viongozi wa chama hicho kuhusu utabiri wa T.B.Joshua na angalizo alilompa. 

Alisema muhubiri huyo maarufu barani Afrika anayefanya shughuli zake nchini Nigeria na ambaye alikuja nchini mara baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita, alimpa angalizo kuwa ili washinde ni lazima wawe wamoja, washikamane na kuwa majasiri.

 “Najua waandishi wa habari wataandika, lakini sijali rafiki yangu Joshua ametabiri Serikali ijayo ya Tanzania itaongozwa na Chadema,” alisema. 

Lowassa amekuwa akienda Lagos, Nigeria kuhudhuria ibada za T.B Joshua anayeongoza kanisa la The Synagogue Church of All Nations na ambaye amekuwa akitabiri matukio makubwa kutokea sehemu mbalimbali duniani. 

Katika kudhihirisha urafiki wake na T.B Joshua, Lowassa alisema katika mahafali ya wanafunzi wa vyuo vikuu ambao ni wanachama wa Chadema yaliyofanyika jijini Dar es Salaam katikati ya mwaka, kuwa CCM ilimuita nabii huyo nchini baada ya uchaguzi ili amshawishi akubali matokeo. 

Lowassa aliwaambia wanafunzi hao kuwa alimweleza T.B Joshua matukio yote yaliyotokea wakati wa uchaguzi na hivyo kumfanya nabii huyo aamue kutohudhuria sherehe za kuapishwa.

 Hata hivyo mwenyewe T.B Joshua hajathibitisha kauli hiyo ya Lowassa. Kuhusu Tabora, Lowassa alisema ni mkoa wa kihistoria na ndio kitovu cha siasa nchini kwa kuwa ndiko kulikoanza vuguvugu la mapambano ya kudai uhuru na kwamba una heshima yake kisiasa. 

Aliwataka viongozi na wanachama wa Chadema kuhakikisha wanalinda heshima hiyo kwa kuifanya Chadema kuongoza nchi. 

Lowassa, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu, aliwaeleza wanachama na viongozi kuwa ruzuku ni fimbo ya kuwagombanisha wanachama katika vyama vya siasa. 

Aliwataka wanachama na viongozi kuhakikisha hawagawanywi na ruzuku na kwamba waulinde Ukawa na wakatae kuvurugwa. 

“Vyama vingi nchi za Afrika hugawanywa kwa fedha za Serikali zilizopo madarakani, jambo ambalo sisi tulikatae,” alisema. 

Aliwaleza wanachama hao ruzuku inatolewa ili wanachama wabaki wakigombana na kushindwa kufanya mambo ya msingi. 

Akiizungumzia elimu, Lowassa alisema CCM inapata ushindi katika maeneo ambayo yapo nyuma kielimu na kuitaja mikoa ya Singida, Mtwara, Lindi, Dodoma na Tabora. 

Alieleza kuwa mikoa iliyo nyuma kielimu ndio ngome ya chama tawala na kwamba ndio maana anaposisitiza elimu itolewe bure, anajua anachomaanisha. 

Mbunge huyo wa zamani wa Monduli aliambatana na mjumbe mwingine wa Kamati Kuu ya Chadema, Mwita Waitara, ambaye katika hotuba yake alisisitizia suala la tume huru ya uchaguzi. 

Waitara, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Ukonga aliwataka wanachama wa Chadema kusimama imara kudai tume huru. 

Awali, mratibu wa Chadema wa Kanda ya Magharibi, General Kaduma alisema watu watakaojaribu kuwagawa wanachama, watawekwa pembeni ili wawaache wengine waendelee kuongoza chama. 

Alisema madhumuni ya mikutano ya ndani ya chama hicho inayoendelea nchi nzima ni kupanga mambo yanayohusu ujenzi wa chama chao na kuwakumbusha viongozi mambo ya msingi ya chama.
  

Wednesday, December 14, 2016

Serikali Yamwaga Ajira za Walimu wa Sayansi na Hisabati

SERIKALI imetangaza kuajiri walimu wa masomo ya sayansi na hisabati katika shule za sekondari ambao wametakiwa kupeleka nakala za vyeti vyao vya elimu ya sekondari, vya taaluma ya ualimu (stashahada na shahada) kwa ajili ya uhakiki.

Tangazo kwa Umma lililotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Maimuna Tarish lilisema vyeti vya sekondari vinavyotakiwa kuhakikiwa ni vya kidato cha sita.

Alisema ajira hizo ni kwa walimu wa Stashahada na Shahada za Mafunzo ya Ualimu wa Masomo ya Hisabati na Sayansi waliohitimu mwaka 2015.

Alisema nakala hizo ziwasilishwe kupitia barua pepe ya wizara kuanzia jana hadi Ijumaa ya Desemba 16 mwaka huu na yeyote ambaye vyeti vyake havitahakikiwa hatafikiriwa katika uajiri.

 

Wednesday, December 14, 2016

Kamanda Sirro: Aliyetishwa na kauli ya Mzee wa Upako afungue kesi

Polisi  Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imemtaka yeyote anayeona kuwa kauli iliyotolewa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo maarufu Mzee wa Upako imetishia maisha yake, afungue kesi.

Kamanda wa kanda hiyo, Simon Sirro aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua hatua polisi waliyoichukua kutokana na kauli aliyoitoa Mchungaji huyo kwamba waandishi waliomwandika vibaya watakufa kabla ya Machi mwakani.

“Kama kuna mtu anaona katishika na kauli hiyo aje afungue kesi milango iko wazi. Kama kuna mwandishi yeyote anayeona ametishika na kauli hiyo aje, kesi ikifunguliwa tutaifanyia kazi kwa sababu hadi sasa hakuna aliyelalamika,” alisema.

Kauli ya Mzee wa Upako aliitoa katika mahubiri yake ya Jumapili ikiwa ni mwendelezo wa majibu yake kutokana na tuhuma zilizoandikwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kwamba alimfanyia fujo jirani yake.

Wakati huo huo, Sirro alisema kuwa wanaendelea na uchunguzi wa madai ya kupotea kwa Bernard Saanane ambaye ni kiongozi wa Chadema. Kiongozi huyo anadaiwa kupotea tangu Novemba 18.

“Kuna watu wanasema wanataka ile miili ichunguzwe… lile ni tukio la Pwani na mwenye wasiwasi anaruhusiwa kuwasiliana na uongozi wa kule kwa sababu ule ni mkoa mwingine,” alisema. 

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forum, Maxence Melo alisema atazungumzia suala hilo Ijumaa.

Wednesday, December 14, 2016

Polisi Dar yawatia mbaroni watu 22 kwa kosa la uporaji katika magari

Kikosi  maalumu cha kupambana na wizi wa kutumia silaha na wizi wa kutumia nguvu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kimewakamata watuhumiwa 22 kwa makosa ya kuwapora wenye magari na wapitanjia kwenye mataa ya kuongozea magari.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema watuhumiwa hao, wamekuwa wakijiunda kwenye vikundi na kuwanyang’anya watu wenye magari na watembea kwa miguu mali zao kama simu za mikononi, kompyuta, saa na fedha.

Alisema ufuatiliaji ulifanyika na kuwakamata watuhumiwa hao kwa nyakati tofauti, ambapo Desemba 11 mwaka huu huko Temeke maeneo ya Keko Magurumbasi na mataa ya Veta na Chang’ombe walikamatwa watuhumiwa 10 kwa makosa ya wizi kutoka maungoni na wizi kutoka kwenye magari.

Aliwataja baadhi ya watuhumiwa hao kuwa ni Ayubu Amiri (19), mkazi wa Mtoni Mtongani, Shabani Fadhili(18) mkazi wa Keko, Herman Francis (26), mkazi wa Keko Magurumbasi na wenzao saba.

“Katika mahojiano watuhumiwa wamekiri kujihusisha na makosa mbalimbali yakiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha na kutumia nguvu,” alisema.

Aidha alisema uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa Herman Francis anakabiliwa na tuhuma za mauaji, ambapo Machi 20 mwaka huu alimchoma mtu kisu na kutoroka kusikojulikana. 

Wakati huo huo, Desemba 12 mwaka huu askari waliwakamata watuhumiwa wengine 12 kwa makosa ya wizi kutoka kwenye magari.

Watuhumiwa hao wametajwa kuwa ni Sande Kassim (18), mkazi wa Keko, Emmanuel Abeli (21), Paulo Abeli(18), Jafari Nyerere (22), Hamis Salum (22), Hemed Idrisa(22) wote wakazi wa Keko na wenzao sita.

Katika tukio lingine, polisi wamewakamata watuhumiwa wanne wanaojihusisha na wizi kwa kuwarubuni watu kwa kukodi magari yao na baadaye hutumia nguvu  kuwapora.

Watuhumiwa hao wametajwa kuwa ni Juma Kajeni (35), mkazi wa Tabata, Hamadi Kaganda (38), mkazi wa Mbagala, Mashaka Ally(62), mkazi wa Yombo na Mshamu Ally (32), mkazi wa Mtongani. 

Alisema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika watapelekwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.

Pia aliwatahadharisha wananchi na wamiliki wa magari kuwa makini kwa watu hao ambao huja kwa nia ya kuwalipa fedha nyingi au kukodi gari kwa kiwango kikubwa na kisha wanatokomea na gari.

Wakati huo huo, polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kupitia kikosi kazi chake cha kupambana na wizi wa magari kimekamata magari matatu ya wizi katika mikoa mbalimbali. 

Sirro alilitaja gari lenye namba T 386 CGY aina ya Verosa rangi nyeusi, mali ya Abraham Robert wa jijini Dar es Salaam na gari hilo lilikamatwa mkoani Mbeya likiwa limetelekezwa.

Gari jingine ni lenye namba T 946 DGH aina ya IST rangi ya fedha ikiwa inaendeshwa na mtuhumiwa aitwaye Hamadi Saidi (27) mkazi wa Kimara Dar es Salaam ambalo lilikamatwa huko mkoani Morogoro, gari hilo liliibiwa maeneo ya Kawe Beach jijini Dar es Salaam.

Alilitaja gari lingine kuwa ni Mitsubishi Canter lenye namba T 753 CVZ ambazo ni namba bandia huku namba zake halisi zikiwa ni T.815 DJF mali ya Magreth iliibiwa maeneo ya Kimara Suka jijini Dar es Salaam.

Alisema mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa anaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika atapelekwa mahakamani. 

Pia alisema  watuhumiwa wengine waliohusika na wizi wa magari hayo wanaendelea kutafutwa ili kubaini mtandao mzima wa wizi wa magari na watuhumiwa wengine wanaotafutwa kwa wizi wa magari hapo nyuma ambao walikimbia. 
 

Wednesday, December 14, 2016

Waziri Ummy azindua Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto

Kwa mara ya kwanza mawaziri 11 wamekutana kwa ajili ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia, huku Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikiweka wazi mpango wake wa kuanzisha madawati ya kuwalinda watoto katika shule za msingi na sekondari.

Aidha, ina mpango wa kuanzisha kamati za ulinzi na usalama wa mtoto katika kila mtaa na kijiji nchi nzima, lengo likiwa ni kutokomeza vitendo vya ukatili na unyanyasaji kwa watoto.

Mawaziri hao walikutana jana katika uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto wa miaka mitano 2017/18 hadi 2021/22 uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hatua hiyo inatokana na kuwepo vitendo vya ubakaji pamoja na vitendo vya watoto wa kiume kulawitiana.

Aliongeza kuwa licha ya kuwepo walimu wa nidhamu lakini wamekuwa wakiogopwa hivyo madawati hayo yatakuwa ni rafiki pindi mtoto anapokutana na vitendo hivyo anakimbilia katika dawati hilo.

Alifafanua kuwa kamati za ulinzi na usalama wa mtoto kwa kila mtaa na kijiji pamoja na kuanzisha mtandao wa wanaume katika kila kata ambao watakuwa wakitetea na kulinda vitendo vya ukatili.

“Ukatili mashuleni tunazungumzia ubakaji wa wakubwa, kinachosikitisha watoto wa kiume wanalawitiana katika mazingira ya shule, sisi kama wizara tumeona tuanzishe dawati la kuwalinda watoto katika shule zetu zote za msingi na sekondari,” alisema.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini, Alvaro Rodriguez alisema dhamira ya serikali imechangia katika kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika Bara la Afrika chini ya mpango mpya wa ushirikiano wa kimataifa katika kukomesha ukatili dhidi ya watoto.

Rodriguez alisema malengo ya dunia yanataka kumaliza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto na badala yake kuwekeza katika kuwawezesha na kuwalinda.

Alisema UN itaendelea kushirikiana na serikali katika kuzuia ukatili wa aina yoyote kwa wanawake na watoto.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliagiza wizara, taasisi za serikali, mikoa, wilaya pamoja na mamlaka za mitaa, kuhakikisha zinazingatia mpango kazi huo kwa kutenga fedha katika bajeti zao kuanzia mwaka wa fedha 2017/18 ili kukidhi utekelezaji wa mpango huo.

Alisema utekelezaji wa mpango huo utagharimu Sh bilioni 267.4 kwa miaka mitano, ambapo unatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wake, waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama alisema mpango huo ni muhimu kwa taifa hasa kwa wakati huu, kwa kuwa vitendo vya unyanyasaji vimekuwa vikiongezeka.

Alisema imefika mahali ambapo vitendo hivyo vinatakiwa vikome na kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu itasimamia mpango kazi huo ili kuhakikisha unatekelezeka na kuendana na gharama halisi ili kufikia malengo.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alisema serikali inataka kupitia sheria ya mtoto ya mwaka 2009 ili kubaini mapungufu ambyo wadau wameyaona na kuyafanyia marekebisho.

Alisema pia wanaangalia namna ya kupanua wigo wa fursa kwa wanawake na watoto katika kutafuta haki na hatua mojawapo ya kufanikisha suala hilo ni kuanzisha mfumo wa msaada wa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya alisema kuwa katika kutekeleza mpango huo, wizara hiyo itahakikisha inasimamia ipasavyo katika maeoneo yote inayohusika.

Naye Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alisema, lengo la serikali ni kuhakikisha wanapeleka umeme katika vijiji vyote kupitia REA awamu ya tatu hasa katika zahanati ili kuwasaidia akinamama kujifungua katika mazingira salama.

Aidha, pia alisema shule nyingi zinaungua kutokana na matumizi ya vibatari hivyo wamekusudia kufikisha umeme katika shule zote. Dk Kalemani pia aliwaonya wamiliki wa migodi ambao wamekuwa hawawashirikishi wanawake katika shughuli za kiuchumi.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura alisema wizara yake itatumia idara za sanaa na utamaduni ili kuhakikisha wanatokomeza vitendo vya ukatili.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi alimwakilisha waziri wa wizara hiyo, Mwigulu Nchemba alisema matukio ya ukatili yamekuwa ni mengi, na kuahidi kuwa wizara itaendelea kuhakikisha wanatumiwa wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Mawaziri wengine waliozungumza katika mkutano huo ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage. Wizara nyingine zinazoshiriki ni Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii. Jinsia na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akizungumza na wadau (hawapo pichani) kwa niaba ya Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kabla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto  jijini Dar es Salaam .
Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mh. Jenista Joakim Mhagama akiongea na  wadau (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto  jijini Dar es Salaam
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mh. Charles Mwijage akiongea na wadau (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto  jijini Dar es Salaam
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe akiongea na wadau (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto  jijini Dar es Salaam
Mratibu Mkazi wa  Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akiongea na  wadau (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto  jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mh. Anastazia Wambura akiongea na  wadau (hawapo pichani) kabla ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mh. Anastazia Wambura (Kulia) akifurahia jambo na  kwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Injinia Stella Manyanya baada ya uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto  jijini Dar es Salaam . (Picha zote na Benjamin Sawe-Maelezo)
 
 

Wednesday, December 14, 2016

CUF Yakubali Kushiriki Uchaguzi wa Mbunge Dimani.......Mwaka jana Walisusa Baada ya Jecha Kufuta Matokeo


Kamati ya Utendaji ya CUF imepitisha majina matatu ya wanaowania kuteuliwa kugombea ubunge katika Jimbo la Dimani, Mkoa wa Mjini Mgharibi kisiwani Unguja. 
Wakati CUF imepitisha majina hayo yatakayokwenda kwenye mchujo wa kura ya maoni ndani ya chama hicho kupata jina moja, CCM nao wamepitisha majina matatu ambayo ni Juma Ali Juma, Hussein Migoda Mataka na Abdalla Sheria yatakayopitia mkondo huohuo. 
Uchaguzi huo utakaofanyika Januari 22, mwakani umetangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), kujaza nafasi ya Hafidh Ali Tahir aliyefariki dunia ghafla mkoani Dodoma hivi karibuni wakati akihudhuria vikao vya Bunge. 
 CUF itakuwa ikishiriki uchaguzi huo kwa mara ya kwanza baada ya kususa ule wa marudio uliofanyika Machi 20, kutokana na kitendo cha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana. 
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alitaja majina hayo kuwa ni Abdulrazak Khatib Ramadhan, Asha Hamad Makungu na Ahmed Abass Haji, ambao watapigiwa kura jimboni huko ili kumpata mmoja atakayeiwakilisha CUF. 
Akizungumza baada ya kikao hicho kilichoongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, Mazrui alisisitiza kuwa chama hicho hakitazikubali hujuma zote, yakiwamo masharti hayo ya NEC aliyoyaita ya mfukoni. 
Katika hatua nyingine, CUF imesema inaendelea na mazungumzo na vyama vinavyounda Ukawa kuona namna bora ya kushiriki uchaguzi mdogo ujao jimboni humo ili kuhakikisha wanaibwaga CCM. 
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Joram Bashange alisema chama hicho bado ni sehemu ya Ukawa na hakuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kutengua uamuzi huo. 
“Suala hilo lilipitishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa uliofanyika tarehe 23 mpaka 27 Juni, 2014 na mkutano mkuu ndicho chombo cha juu kabisa na chenye maamuzi ya mwisho katika chama,” alisema. 
Kikao hicho kilikuwa na ajenda moja ya maandalizi ya uchaguzi mdogo wa madiwani 22 Tanzania Bara na ubunge wa Dimani. 
Kamati ya Utendaji ilipitisha ratiba ya uchaguzi wa ndani ya chama kwa ajili ya kuwapata wagombea wa CUF katika nafasi hizo. 
Wakati huo huo, Bashange amesema Kamati ya Utendaji ya Taifa imeshangazwa na kauli ya Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima kwamba wagombea wa CUF lazima fomu zao za uteuzi zithibitishwe na kutiwa saini na pande mbili zinazohasimiana. 
“Kailima amekitoa wapi kifungu cha sheria au kanuni, alichokitumia kuweka sharti hilo la ajabu tena kwa chama kimoja tu,” alisema na kuongeza:“Huwezi kuwa na sharti linalokihusu chama kimoja tu katika kuthibitisha uteuzi wa wagombea.” 
Alisema fomu za uteuzi wa wagombea kutoka NEC huthibitishwa na katibu wa chama wa ngazi inayohusika na kwa ubunge na madiwani ni katibu wa wilaya.

Wednesday, December 14, 2016

Kada wa CCM Aliyetuhumiwa Kughushi Kitambulisho cha Usalama wa Taifa Aachiwa huru baada ya Jamhuri kusema hawana nia kuendelea na kesi

Miezi kadhaa iliyopita aliyekuwa mwenyekiti wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi ‘UVCCM’ Arusha, Lengai Ole Sabaya alishtakiwa kwa kosa la kujifanya ofisa usalama wa Taifa na kughushi kitambulisho cha usalama wa taifa.

Kesi hiyo imetolewa maaamuzi na mahakama ya hakimu mkazi Arusha leo December 14 2016 ambapo imemuachia huru Lengai Ole Sabaya baada ya upande wa Jamhuri kusema hawana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
  
 
 
KIMATAIFAAA
Karibu raia 6,000, miongoni mwao watoto 2,000 wameondolewa kutoka wilaya iliyokuwa inadhibitiwa na waasi mjini Aleppo katika muda wa masaa 24 yaliyopita. Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema leo kwamba katika kipindi hicho waasi 366 wameweka chini silaha zao na kuondoka kutoka katika maeneo hayo yaliyokuwa yakishikiliwa na waasi katika mji huo. Jana, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Syria , Staffan de Mistura, alitoa wito wa kupata uwezekano wa kufikiwa eneo hilo la zamani la waasi na kuthibitisha mwisho wa operesheni ya kijeshi na kushughulikia kuondolewa kwa mamia kwa maelfu ya raia na wapiganaji wa upinzani kutoka mashariki mwa Aleppo baada ya kubanwa na majeshi ya serikali. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba Syria na washirika wake wanahusika na vifo na uharibifu mjini Aleppo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa, majeshi yanayoiunga mkono serikali yanaripotiwa kuwauwa raia 82, ikiwa ni pamoja na wanawake 11 na watoto 13 tangu yalipoingia katika mji huo.
 
Marekani itaendelea kuipa changamoto China https://www.blogger.com/blogger.g?blogID=5562888949021030863#editor/target=post;postID=6506052512291544860kwa tabia yake ya kimabavu katika bahari ya kusini mwa China, amesema kamanda wa majeshi ya Marekani katika eneo la bahari ya Pacific leo, wakati hali ya wasi wasi kati ya mataifa hayo yenye nguvu duniani ikiongezeka kuhusiana na matamshi ya rais mteule Donald Trump. Admirali Harry Harris, mkuu wa kikosi cha jeshi la Marekani katika bahari ya pacific, alionya kwamba Marekani haitakubali udhibiti wa China wa kanda hiyo, licha ya maendeleo ya haraka ya China kujenga visiwa ambavyo vina uwezo wa kuweka ndege za kijeshi. Matamshi yake yamekuja wakati Beijing imeonesha hali ya kukasirika baada ya Trump, kuzungumza moja kwa moja na kiongozi wa Taiwan Tsai Ing-wen, na kushauri kwamba huenda Marekani ikapuuza sera yake ya miongo kadhaa ya kukubali sera ya China moja.Wakati huo huo waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Jean - Marc Ayrault ameshutumu matamshi ya kibabe ya rais mteule wa Marekani Donald Trump dhidi ya mshirika mkubwa wa kibiashara China baada ya kutishia kutupilia mbali sera ya China moja ya Marekani.
 
Kiongozi wa Gambia Yahya Jammeh amewasilisha pingamizi katika mahakamani kuu ya nchi hiyo kutaka kubatilishwa matokeo ya hivi karibuni ya uchaguzi wa rais. Jammeh hapo kabla alikubali kushindwa na mpizani wake Adama Barrow, lakini baadaye alibadilisha mawazo. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 51, ambaye ameitawala nchi hiyo ya Afrika Magharibi kwa miaka 22, pia aliwaamuru wanajeshi na polisi kuingia mitaani katika mji mkuu Banjul kuzuwia maandamano na upinzani.Wakati huo huo, ujumbe wa Umoja wa Afrika umewasili mjini Banjul kumshawishi Jammeh kukubali kushindwa na kukabidhi madaraka kwa Barrow. Kubalidika kwa Jammeh kumesababisha shutuma kali kutoka Umoja wa mataifa, Umoja wa Ulaya na Marekani pamoja na viongozi wa kikanda.
 
 
Bunge la Ufaransa limekubali kurefusha amri ya hali ya hatari nchini humo kwa miezi sita. Sheria hiyo iliwekwa kufuatia mashambulizi ya kigaidi mjini Paris Novemba mwaka 2015, ambapo watu 130 waliuwawa. Hatua hiyo sasa imerefushwa kwa mara ya tano katika muda wa miezi 13, ambapo wakosoaji wanasema sheria hiyo ya hali ya hatari inawapa maafisa madaraka makubwa ya kuingilia maisha ya faragha ya raia.Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Bernard Cazeneuve hata hivyo ameitetea hatua hiyo kwa kusema, kwamba changamoto ya kiusalama kwanza ni kupambana na kitisho cha ugaidi wa wanajihadi. Kuwashinda wenye itikadi kali ya Kiislamu kuna maana kwamba inahitajika kutumia kila uwezo uliopo katika mapambano kuilinda jamhuri na kuwaunganisha watu wote wakati wote kwa ajili ya maadili haya.

Wiki saba baada ya kufungwa kwa kile kinachoitwa kambi ya wahamiaji ya porini katika mji wa pwani wa Calais nchini Ufaransa, umejengwa ukuta sasa kuzuwia wahamiaji wengine hapo baadaye kuingia katika eneo hilo. Ukuta huo uligharamiwa na serikali ya Uingereza kama sehemu ya mpango wa pamoja wa usalama kati ya Ufaransa na Uingereza.Ukuta huo una lengo la kuzuwia watu kusafiri kwa kujificha katika malori na vyombo vingine vya usafiri kutoka upande wa Ufaransa katika juhudi za kuingia Uingereza. Makundi ya haki za binadamu yameshutumu kile kinachoitwa, "Ukuta mkuu wa Calais ", na kusema ni ukatili na hatari.

katika michezooo
 
jumatano ya leooooo jumatano ya leooooo Reviewed by RICH VOICE on Desemba 14, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...