Friday, December 16, 2016
Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Ijumaa ya Disemba 16
Friday, December 16, 2016
Mahakama Kuu Yaamuru Mwanafunzi wa UDOM Aliyefukuzwa Chuo kwa Kuongoza Mgomo Arudishwe Masomoni
MAHAKAMA
Kuu Kanda ya Dodoma imetengua uamuzi wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma
(Udom) ya kumfukuza mwanachuo Phillip Mwakibinga na kuamuru arudishwe
ili kumalizia masomo yake.
Uamuzi
huo ulitolewa jana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, John Chaba kwa
niaba ya Jaji Awadhi Mohamed aliyekuwa akisikiliza shauri hilo.
Mwakibinga
alikuwa akisoma Shahada ya Kiswahili mwaka wa tatu wakati akisimamishwa
na alikuwa Waziri Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii. Katika uamuzi
huo, mahakama ilisema mlalamikaji hakupewa nafasi ya kusikilizwa na
hivyo kukiuka haki ya asili ya mlalamikaji. Pia mlalamikaji hakupewa
haki ya kusikilizwa na hakuandikiwa mashtaka rasmi.
“Baraza liliegemea upande moja bila kumhoji wala nafasi ya kusikilizwa na kujitetea,” alisema.
Mwakibinga
alifukuzwa Udom Januari 14, mwaka jana, kwa madai ya kuongoza mgomo
ambapo siku hiyo baraza la chuo lilikaa na kumfukuza bila kupewa nafasi
ya kusikilizwa.
Alifungua
kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kutaka mahakama kutengua uamuzi huo.
Kwa mujibu wa wakili wa Mwakibinga, Elias Machibya alisema awali
waliomba ruhusa ya kufungua kesi na wakapewa Februari 5, mwaka jana
wakiomba kutengua maombi ya baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma.
“Tulipata kibali cha kufungua kuomba kutengua maamuzi ya Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kumfukuza,” alisema.
Alizitaja
sababu kuu tatu za kupinga mwanafunzi huyo kufukuzwa chuo kuwa ni
pamoja na kutopewa nafasi ya kusikilizwa, hakuna hatua za nidhamu
zilizochukuliwa, walimfukuza wakidai aliwahi kuhusika na migomo ya
nyuma.
Alidai barua ya kumfukuza ilisainiwa na Profesa Shaban Mlacha.
Januari
14, mwaka jana uongozi wa Udom ulimfukuza Mwakibinga ambaye wakati huo
alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya wanafunzi, Kitivo cha Sayansi ya
Elimu ya Jamii, na kupewa barua ya kusimamishwa kutokana na kosa la
kuhamasisha mgomo.
Uongozi
huo ulisema Mwakibinga amefukuzwa kabisa kwa kuwa alishawahi
kujihusisha na mgomo wa mwaka 2010/2011 akafukuzwa lakini akakata rufaa
na kuomba msamaha kwenye Kamati nidhamu.
“Baada
ya kukata rufaa Kamati ikamuonea huruma ikamrudisha kabla ya kurudi
alitakiwa aje na kiapo kutoka kwa mwanasheria kwamba hatajihusisha na
mgomo tena lakini akarudia tena kosa hilo."
Mwakibinga
amesema amefurahia uamuzi huo kwani ndio sababu ya msingi ya kufungua
kesi na mahakama imetenda haki. Alisema anasubiri barua ya hukumu ambayo
itatoka kesho ndipo taratibu zake za kurudi chuo zitakapoanza.
Friday, December 16, 2016
Mkuu Brigedi ya Nyuki JWTZ afariki dunia
KAMANDA
wa Brigedi ya Nyuki ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
Brigedia Jenerali Cyril Mhaiki, amefariki dunia katika Hospitali ya
Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.
Katika
salamu zake za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama
Tanzania, Davis Mwamunyange, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, alisema jana kuwa, amepokea kwa huzuni
kubwa taarifa za kifo cha Brigedia Jenerali Mhaiki aliyefikwa na mauti
juzi.
Dk
Shein kwa niaba yake na ya wananchi wote Zanzibar, alisema wamepokea
kwa mshtuko, taarifa ya kifo cha Kamanda huyo hodari aliyetoa mchango
mkubwa katika shughuli za ulinzi na usalama na maendeleo ya nchi.
Aidha,
salamu hizo za rambirambi zilieleza kuwa Brigedia Jenerali Mhaiki
ameacha pengo kubwa, si tu kwa familia yake, bali kwa Brigedi ya Nyuki,
JWTZ na nchi kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa mchango wake
hautosahaulika.
Alimuomba
Mwamunyange kuzifikisha salamu hizo za rambirambi kwa wanafamilia,
maofisa na wapiganaji wa vikosi vyote vya ulinzi na usalama.
Pamoja
na hayo, salamu hizo zilimuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira
ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu katika kipindi hiki kigumu cha
msiba huku akimuomba Mwenyezi Mungu kumlaza mahala pema Kamanda huyo.
Friday, December 16, 2016
Waziri Mkuu Acharuka....Asema NGO Chonganishi Zitafutwa
WAZIRI
Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa miezi sita ya kujitathimini mashirika
yasiyo ya kiserikali (NGOs) yanayofanya kazi zake wilayani Ngorongoro
mkoani Arusha, kama yanafanya kazi kwa misingi ya sheria na maadili.
Baadaye, yatahakikiwa na kama yatabainika yanachochea migogoro, yatafutwa.
Pia,
Majaliwa amezicharukia NGOs nyingine zinazoitangaza vibaya Tanzania
kimataifa kwa kupiga picha za kudhalilisha watoto wakiwa wanatembea
kwenye mawe huku wamevaa kandambili kubwa, kuonesha nchi ni masikini.
Ametaka NGOs hizo kuondoka nchini, la sivyo serikali itazishughulikia.
“Hizi
NGOs zingine si muondoke, nendeni kwingine mkafanye kazi. Halafu nyie
mnaotuma picha za kudhalilisha watoto wakiwa wamevaa kandambili kubwa,
kudai nchi za nje eti Tanzania ni masikini, tutawashughulikia,” alisema
Majaliwa alipozungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ngorongoro jana.
Aidha
alisema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atakuja
wilayani hapo kukagua kazi walizozifanya, wanazozifanya na miradi
wanaosaidia jamii.
Majaliwa
aliwaambia watumishi hao wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro pamoja
na wadau mbalimbali wakiwemo wakurugenzi wa mashirika yasiyo ya
serikali, yanayofanya shughuli zake wilayani hapo, kuwa serikali haitaki
mashirika chochezi wa migogoro na itayafuta.
Alisema
serikali haitasita kuyafuta mashirika yanayofanya kazi wilayani humo,
ambayo yapo kwa nia ya uchochezi na kuacha kufanya kazi katika malengo
yaliyokusudiwa.
Waziri Mkuu alisema wilaya hiyo, ina mashirika yasiyo ya serikali 30 ambayo yamesajiliwa, lakini yanayofanya kazi ni 19 tu.
Alisisitiza kuwa haiwezekani serikali isajili mashirika hayo, lakini utendaji kazi wake uwe hafifu.
Alisema
ukifuatilia, mashirika hayo utagundua kuwa yanapokea fedha nyingi,
lakini hakuna cha maana wanachokifanya kwa wananchi. Alisema serikali
ina taarifa ya NGOs hizo zinazopewa fedha na wafadhili.
“Najua
taarifa zenu mnapokea kiasi gani cha fedha na mnazifanyia nini, lakini
namleta Mkaguzi wa serikali ili akague mnatumiaje fedha zenu, nawapa
miezi sita tu halafu ukaguzi utaanza, maana kuna mashirika mengi lakini
kazi mnazofanya hazionekani,” alisema Majaliwa.
Alisema
baadhi ya mashirika, yana akaunti nchi jirani ya Kenya na mengine kama
PWC anapewa Sh bilioni 2.5 kwa mwaka na shirika la UCRT linapokea Sh
bilioni 1.5 kwa mwaka, lakini hajui yanafanya nini.
“Nina
taarifa zenu mnapata hela nyingi, lakini mnahudumia vipi jamii hakuna,
sasa ngojeni ukaguzi ufanyike halafu nitachukua maamuzi maana kila siku
Loliondo kuna nini hapa mnasajiliwa halafu hakuna cha maana,” alisema.
“Kuna
nini Loliondo, kwani kila mara Loliondo nina taarifa za kila NGOs
zinazofanya kazi hapa, najua mnachokifanya, sasa nawaambia serikali
haitawafumbia macho kuona hiki ninachokifanya hapa na ikigundulika
mnafanya kinyume na matakwa ya usajili tutazifuta”.
Alisema
serikali itazifuta NGOs zote, ambazo zitabainika ni kiini cha migogoro
Loliondo. Alitoa hadhari kwa kampuni zinazofanya kazi zake bila usajili,
kuwa zikigundulika, zitachukuliwa hatua.
Aliwageukia
watumishi wa umma na kuwatahadharisha wale wanaotoa taarifa za migogoro
ya ndani kwa wahusika wa NGOs na kisha kuzituma nje ya nchi kwenye
mitandao ya kijamii na barua pepe.
Alisema kuwa nao watashugulikiwa, kwa kuwa wanapaswa kuwa majibu ya migogoro na si wasambazaji wa habari mbaya za nchi.
Alisisitiza
watekeleze kikamilifu kauli ya ‘Hapa Kazi Tu’ ; na si kutumia NGOs kwa
ajili ya kudai kuwasaidia wananchi, huku wakijua kuwa wananchi
hawanufaiki na fedha hizo wanazopewa na wafadhili Awali akizungumza na
watumishi wa halmashauri ya Wilaya hiyo, Majaliwa alitoa tahadhari kwa
madiwani kuacha kushirikiana na watu wa Uhasibu wanaotoa hela kwaajili
ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema baadhi ya madiwani, wanakwamisha miradi ya maendeleo kwa kula fedha kwa sababu ya ukaribu walionao.
Akizungumzia
nidhamu ya fedha, Majaliwa alisisitiza kila mtumishi lazima afanye kazi
kwa bidii, ikiwemo kutoa huduma bila kuwabagua wananchi kwa itikadi zao
za vyama.
Friday, December 16, 2016
Afande Sele aanika sababu za kuitosa ACT Wazalendo
Mwanamuziki
mkongwe, Selemani Msindi maarufu kama Afande Sele ameeleza sababu
zilizopelekea jana kutangaza kung’atuka ndani ya Chama Cha ACT –
Wazalendo mwaka mmoja baada ya harakati za uchaguzi Mkuu ambao aliutumia
kugombea ubunge wa Morogoro Mjini.
Afande
Sele ameeleza kuwa moja kati ya sababu zilizopelekea yeye kung’atuka ni
kutofikia malengo yake ya kuingia ndani ya chama hicho ya kupata
ubunge.
“Nimejitoa
ACT- Wazalendo kwa makusudi kabisa na hili lilikuwa ni jambo tarajiwa,
kitu cha kwanza moja ya matarajio yalikuwa baada ya mimi kuingia ACT
nakuwa Mbunge ila sasa sikupata Ubunge na kama ningeupata Ubunge basi
nisingejitoa ndani ya chama,” Anasema Afande Sele .
Jana,
kupitia ukurasa wake wa Facebook, mwanamuziki huyo alieleza kuwa
amechukua uamuzi huo sio kwa bahati mbaya hivyo uamuzi wake uheshimiwe.
Alisisitiza kuwa hatajiunga na chama chochote cha siasa hadi pale ambapo
ataamua vinginevyo.
Mei
mwaka jana, Afande Sele alitangaza kugombea ubunge wa Morogoro mjini
kupitia ACT-Wazalendo lakini hakufanikiwa kuupata ubunge wa jimbo hilo
kupitia sanduku la kura, Oktoba 25 mwaka jana.
Friday, December 16, 2016
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Lataka Mmiliki wa Jamii Forums Aachiwe Mara Moja
Kwa
muda wa siku tatu sasa Jeshi la Polisi Tanzania linamshikilia
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jamii Media Limited, Maxence Melo
katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Dar es Salaam.
Hadi
sasa, si Melo, familia yake au wanasheria wake walioelezwa kosa
linalomfanya ashikiliwe. Wanasheria wa Melo wameweka kambi katika Kituo
Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, lakini hakuna majibu ya maana wanayopewa
na wala Melo hafikishwi mahakamani.
Taarifa
wanazotoa askari waliopo kituoni hapo, ambazo si taarifa rasmi, ni
kwamba Melo anashikiliwa kwa nia ya kumtaka awape polisi majina
wanayoyahitaji ya wachangiaji wa masuala mbalimbali katika mtandao wa
Jamii Forums kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandaoni huku wakidai ni
maelekezo kutoka “juu”.
Siku
ya Jumatano, Desemba 14, 2016 polisi wamefika ofisini na nyumbani kwa
Melo wakapekua sehemu zote. Taarifa kutoka ofisini kwa Melo zinaonyesha
polisi wamechukua nyaraka mbalimbali ikiwamo hati ya kusajili kampuni,
leseni ya biashara na nyingine.
Pia polisi wameondoka na wafanyakazi wawili wa Kampuni ya Jamii Forums kwa mahojiano zaidi.
Taarifa
nyingine zinaonyesha kuwa polisi wanaomshikilia Melo wanajiapiza kuwa
hata kama mawakili wake watakwenda mahakamani hawatamwachia hadi
atekeleze wakitakacho.
Jukwaa
la Wahariri Tanzania (TEF) linafuatilia kwa karibu mwenendo na utendaji
wa Jeshi la Polisi juu ya suala la uhuru wa kujieleza na kutoa maoni
unaotolewa na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(1977).
Katika
siku za karibuni, TEF na Watanzania kwa ujumla wanashuhudia ukiukwaji
mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na Jeshi la Polisi linaloelekea
kuacha kuheshimu misingi ya utawala wa Sheria na Katiba ya Tanzania.
Melo
kama mtuhumiwa anayo haki ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma katika
muda usiozidi saa 24. Kitendo cha polisi kumshikilia kwa siku tatu,
ambapo hatujui kama anateswa au la, ni uvunjaji mkubwa wa haki za
binadamu.
Tamko
la Haki za Binadamu la Mwaka 1948 linavitaka vyombo vya dola kuheshimu
utawala wa sheria ambao pamoja na mambo mengine msingi wake ni kuheshimu
mgawanyo wa madaraka (separation of power). Kitendo cha Polisi kuanza
kuchukua sheria mkononi kwa kukamatakamata watu, kuwatisha waandishi wa
habari na watetezi wa haki za binadamu hakikubaliki.
TEF
inalitaka Jeshi la Polisi kumwachia mara moja Melo bila masharti au
kumfikisha mahakamani na kumfungulia mashitaka kwa mujibu wa sheria
ikiwa ana kosa.
Tunamwomba
Rais John Magufuli aingilie kati mzozo huu na kuwafahamisha polisi kuwa
wanayoyatenda wanapalilia mbegu ya chuki katika nchi jambo ambalo si
jema waliache mara moja.
TEF
inaungana na Watanzania kulaani kitendo cha polisi kumkamata Melo kwa
kutumia sheria mbaya isiyokubalika ya Makosa ya Mtandaoni.
TEF
inatetea haki ya uhuru wa kutoa mawazo na kukataa ukandamizaji huu wa
polisi wanaodai wana maelekezo kutoka juu chini ya uongozi wa Serikali
ya Awamu ya Tano. Mungu ibariki Tanzania.
Theophil Makunga,
Mwenyekiti,
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Dar es Salaam, Desemba 15, 2016
Friday, December 16, 2016
Ndalichako Asitisha Ajira za Walimu Wa Masomo ya Sanaa
WAZIRI
wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako,
ametoa masharti mapya ya ajira za ualimu nchini, huku akisema Serikali
haitaajiri walimu wa masomo ya sanaa (arts) kwa kuwa wapo wa kutosha.
Akizungumza
mjini Dodoma jana wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Wakuu wa
Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), Profesa Ndalichako, alisema
Serikali kwa sasa haiwezi kuajiri walimu wa masomo hayo kwa kuwa inataka
kuajiri walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ambao idadi yao ni
ndogo.
“Pamoja
na uamuzi huo mpya, ajira za walimu wapya wa masomo ya sayansi nazo
zimebadilika kwani wale wote waliohitimu ualimu wa sayansi na hisabati,
wanatakiwa watume vyeti vyao kabla ya kupangiwa kituo cha kazi.
“Kuhusu
wale walimu wa ‘arts’, kule tuna walimu wa ziada ambao tutajaribu
kuwapanga kutokana na shule, kwani wengi walikuwa wamepangwa shule moja.
Kwahiyo, tutaangalia utaratibu wa kuwapanga kulingana na mahitaji,’’ alisema Profesa Ndalichako.
Akizungumzia
suala la ubora wa elimu nchini, Profesa Ndalichako aliwataka walimu
wakuu hao kuhakikisha wanasimamia ubora wa elimu kwa kuwa wao ndio
wanaowaandaa wanafunzi kabla hawajaenda vyuoni.
“Vilevile
pelekeni takwimu sahihi za wanafunzi waliopo katika shule zenu
kuisaidia Serikali katika kupanga bajeti ili iweze kutoa fedha sahihi.
“Hapa
kuna kimbembe, yaani wakati mwingine huwa najifanya nimepoteza takwimu
ya shule fulani, nikiziomba na kutumiwa, zinakuwa ni tofauti na zile za
mwanzo.
“Hili nawaomba mkalisimamie ili iwe rahisi kwetu kupanga bajeti yenye tija,’’ alisema.
Kuhusu
ujenzi wa maabara katika shule za sekondari, waziri huyo alisema kwamba
kutokana na nyingi kukamilika, Serikali itatoa vifaa vya maabara
kuanzia Januari mwakani baada ya kuwa vimeingia nchini kutoka
vilikoagizwa.
Awali,
akisoma risala ya walimu hao, Rais wa TAHOSSA, Bonus Nyimbo, aliiomba
Serikali itoe waraka wa kupiga marufuku matumizi ya simu kwa wanafunzi
shuleni kwa kuwa zimekuwa zikichangia kushuka kwa ufaulu kwa baadhi ya
wanafunzi.
“Ili
kuboresha elimu, tunaiomba Serikali itoe waraka wa kupiga marufuku
matumizi ya simu kwa wanafunzi kwani simu nyingi tunazozikamata tunakuta
mule hakuna taaluma,’’ alisema Nyimbo.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Global Education Link, Abdulmalik Molel,
ambaye pia kampuni yake ilipewa tuzo ya heshima katika kuendeleza elimu
nchini, alisema ni jukumu la kila mmoja kutimiza wajibu wake ili
kuiendeleza elimu ya Tanzania.
“Kila
mmoja anapaswa kutimiza wajibu, wazazi, walezi na walimu, waambieni
wanafunzi wasiwe na ‘expectation’ (matarajio) makubwa kwani wanapokuwa
na matarajio hayo, wakienda vyuo vikuu wanakuwa wasumbufu,” alisema.
Wakati
hayo yakiendelea, juzi taarifa ilitolewa jijini Dar es Salaam na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Maimuna
Tarishi, ikisema kwamba, walimu wahitimu wa masomo ya sayansi na
hisabati waliohitimu shahada na astashahada mwaka 2015, wanatakiwa
kuwasilisha nakala za vyeti vya elimu ya sekondari vya kidato cha nne na
sita na taaluma ya ualimu kwa uhakiki.
Pamoja na hayo, hivi karibuni Serikali ilitangaza kusitisha ajira zote nchini ili kukabiliana na wimbi la watumishi hewa.
Sambamba
na uamuzi huo, nyongeza za mishahara kwa watumishi wa Serikali nazo
zilisimamishwa ili kukabiliana na watumishi hao hewa ambao walikuwa
wakiingizia hasara Serikali.
Friday, December 16, 2016
Utafiti wa NIMR Wagundua watu 83 waliougua ugonjwa wa zika Hapa Nchini
Watu 83 hapa chini wamegundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa zika kati ya watu 533 waliochukuliwa sampuli za damu.
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini (NIMR) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Bugando, umeonyesha kuwa watu hao walipata maambukizi hayo kati ya mwaka 2015 na 2016.
Wakati
NIMR ikitoa ripoti yake ya utafiti kuhusu kugundulika watu waliokuwa na
virusi vya zika nchini, Januari 31 Serikali ilitoa taarifa kukanusha
kuwapo kwa ugonjwa huo nchini.
Taarifa
hiyo iliyotolewa kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto ilitaarifu: “Kumekuwepo na taarifa kupitia vyombo
mbalimbali vya habari vya kitaifa na kimataifa kuhusu Homa ya Zika ambao
ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi kijulikanacho kama “Zika Virus”.
“Ugonjwa
wa Homa ya Zika bado haujaingia Tanzania. Wananchi waondoe hofu juu ya
uwepo wa ugonjwa huu. Hata hivyo, ni muhimu kwa kila mmoja wetu
kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya zika, dengue na
malaria ambayo huenezwa kwa namna inayofanana.”
Jana,
Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk Mwele Malecela alikutana na waandishi wa
habari kueleza ripoti ya utafiti wao ikionyesha zika ipo Tanzania na
wanaendelea na utafiti kujua ukubwa wa tatizo.
“Utafiti
huu ulifanyika kuanzia mwaka 2015 hadi 2016 katika mikoa nane, ambapo
jumla ya sampuli 533 za damu zilipimwa na kati yao, watoto wachanga 80
walizaliwa na ulemavu wa viungo mbalimbali ambapo baada ya kufanya
utafiti tulibaini asilimia 43.8 ya watoto hao wachanga walikuwa
wameambukizwa virusi vya ugonjwa wa zika katika mikoa hiyo,” alisema Dk Malecela.
Aliitaja
mikoa iliyofanyiwa utafiti huo kuwa ni Mwanza, Simiyu, Shinyanga,
Geita, Kigoma, Tabora, Singida na Morogoro na kwamba bado taasisi hiyo
na Chuo Kikuu cha Bugando wanaendelea na utafiti huo ili kujua ukubwa wa
tatizo hilo katika mikoa hiyo.
Dk
Malecela alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya
taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo alisema kati ya watu
533 waliopimwa, watu 83 sawa na asilimia 15.6 waligundulika kuwa na
maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa zika na hivyo kupatiwa matibabu ya
haraka.
“Kwa
wale watoto wachanga 80 waliozaliwa na ulemavu, asilimia 43.8 walikuwa
wameambukizwa virusi vya zika na mpaka sasa bado tunaendelea na utafiti
kubaini ukubwa wa tatizo hili na kuchukua hatua za haraka,” alisema Dk Malecela.
Alisema
kwa sasa wanaendelea na utafiti katika mikoa hiyo kwa wanawake
waliopata matatizo ya kuharibika kwa mimba ili kujua ukubwa wa tatizo
hilo.
Dk
Salvatory Florence kutoka Idara ya Magonjwa ya Watoto ya Hospitali ya
Hubert Kairuki alisema ugonjwa huo hauna tiba ni kama ugonjwa wa dengue
ulivyo ambapo mgonjwa anapaswa kunywa maji mengi.
Dk
Florence ambaye pia ni Mhadhiri Chuo cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki,
alisema wajawazito wa miezi mitatu wapo katika hatari ya kuzaa watoto
wenye matatizo ya mtindio wa ubongo na watoto wenye vichwa vidogo
(microcephalus) endapo wataambukizwa virusi hivyo kupitia kwa mama zao.
“Zika
ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi kijulikanacho kama “Zika Virus na
unaenezwa na mbu aina ya Aedes ambaye huwa ana tabia ya kuuma asubuhi na
pia nyakati za mchana na wakati mwingine jioni,” alisema Dk Florence.
Pia, utafiti wa Nimr ulionyesha kuwa waendesha bodaboda katika mkoa wa Dar es Salaam, wapo hatarini kupata virusi vya Ukimwi.
Utafiti
huo uliofanyika katika jiji hilo Agosti mwaka huu, umeonyesha kuwa
licha ya madereva hao wa pikipiki kuwa na maambukizi madogo ya VVU kwa
asilimia 2.5, bado wapo hatarini kutokana na kuwa na wapenzi wengi huku
wengi wao wakigoma kutumia kinga.
Friday, December 16, 2016
Kafulila ahama NCCR, ahamia Chadema
Mbunge
wa zamani wa Jimbo la Kigoma Kusini kwa tiketi ya Chama cha
NCCR-Mageuzi, David Kafulila leo ametangaza kukihama chama hicho na
kusema kuwa atajiunga na Chama cha Demokrasia na Manendeleo (CHADEMA).
Kafulila
ambaye alijizolea umaarufu mkubwa katika bunge la kumi kwa kufichua
hoja mbalimbali za ufisadi amesema kuwa ameshawasilisha barua ya
kujiuzulu kwa uongozi wa chama hicho.
Akieleza
sababu iliyomsukuma kujiunga na CHADEMA, Kafulila alinukuliwa akisema
kuwa kikubwa ni kuhakikia wanaleta mabadiliko nchini Tanzania.
"Ili
kufanya safari kuwa fupi, kuondoa vikwazo vya huyu yuko chama hiki
mwingine kile nimemamua kujiunga na CHADEMA ili kurahisisha uletaji
mabadiliko katika nchi yetu sababu nimeona uhitaji huo," alisema Kafulila.
Katika
uchaguzi uliopita Kafulila alipoteza jimbo la Kigoma Kusini ambalo
lilikwenda wa Hasna Sudi Katunda Mwilima aliyekuwa akigombea kupitia
Chama cha Mapinduzi.
CHANZO NI MPEKUZI
Reviewed by RICH VOICE
on
Desemba 16, 2016
Rating:
Hakuna maoni