JUMAMOSI HII

 

 

 JEMBE1.jpg

 

 MKEKA.jpg

 

Saturday, December 24, 2016


Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumamosi Ya Disemba 24



Saturday, December 24, 2016


Mbowe Aeleza kwa nini Amekuwa Kimya Kupotea kwa Ben Saanane


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema amekuwa kimya muda mrefu kuhusiana na kupotea katika mazingira ya kutatanisha, msaidizi wake Ben Saanane kwa kuwa suala hilo lipo kwenye uchunguzi. 

Mbowe alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya wakati wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho Kanda ya Nyasa inayojumuisha mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe na Rukwa. 

Alisema yeye pia ameathiriwa na tukio hilo kama ilivyo kwa wazazi wake na ndugu wengine kwa kuwa ni mtu muhimu kwake katika kutekeleza majukumu yake. 

“Ndugu zangu Watanzania msione nipo kimya, nimefanya hivi kutokana na kuwa suala hili lipo kwenye uchunguzi kwani tukizidisha kuongea ongea wale ambao wamemteka wanaweza kupoteza uhai wake kisa maneno,” alisema Mbowe. 

Alisema, “Chadema ni taasisi ambayo ina vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vinaendelea kuchunguza tukio hili la aina yake.” 

Katika hatua nyingine, Mbowe aliishitumu Serikali akidai kwamba imeendelea kuwafunga wanachama wake na kwamba mpaka sasa 180 wapo mahabusu. Alisema hizo ni jitihada za kuua nguvu za upinzani. 

Akijibu madai hayo, Kamishna wa Polisi (Operesheni na Mafunzo), Nsato Marijani alisema jeshi hilo linawashikilia watu wengi kwa makosa mbalimbali vituoni na wengine mahabusu katika magereza. Alisema polisi haimkamati mfuasi wa chama cha siasa bali mtu anayekwenda kinyume cha sheria. 

“Hayo yanayosemwa siyo ya kweli, waache kulipaka tope jeshi la polisi. Tutaendelea kuwakamata watu wote wanaovunja sheria. Hata kama akiwa mjomba wangu tutamkamata.” 

Msigwa kidedea 
Katika uchaguzi huo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa aliibuka kidedea baada ya kushinda kwa kupata kura za ndiyo 62 sawa na asilimia 58.49 kati ya kura 106 zilizopigwa. 

Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema nafasi ya makamu mwenyekiti imechukuliwa na Sadrick Malila ambaye alipata kura za ndiyo 93 sawa na asilimia 88 ya kura zilizopigwa 106 huku kura tatu zikiharibika. 
Mnyika alisema kuwa nafasi ya  mweka hazina imechukuliwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Sophia Mwakagenda ambaye alishinda kwa kupata kura 91 ambayo ni sawa na asilimia 86 kura zote 106 zilizopigwa. 

Mnyika alisema katika uchaguzi huo wajumbe walipiga kura za ndiyo au hapana kwa lengo la kufanya uchaguzi wa maridhiano kwani uchaguzi wa kuweka wagombea wawili husababisha makundi na kuleta migogoro ndani ya chama. 

“Hivyo Kamati Kuu Taifa baada ya kuliona hilo tukaamua kuwaita wagombea wote na kuwaeleza nia yetu ya kufanya hivyo na hatujafanya huku tu, hata kanda nyingine tulizopita tumefanya hivyo" Alisema Mnyika

Saturday, December 24, 2016


Basata yaonya disko toto, maonesho machafu


BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata), linalosimamia sanaa na burudani nchini, limeonya wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani, kuepuka kuruhusu disko toto na kujaza watu kwenye kumbi hizo.

Aidha, Baraza hilo pia limesisitiza kuwa halitafumbia macho ukumbi utakaokiuka maelekezo yake, ikiwa ni pamoja na kuruhusu maonesho machafu yenye kudhalilisha utu hasa yanayoonesha maungo ya ndani, kwa kuwa yameshapigwa marufuku.

Hayo yamo kwenye taarifa ya Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, kwa lengo la  kuwatakia wasanii na wadau wote wa sanaa heri ya Krismasi na Mwaka mpya.

Huku ikisisitiza kauli mbihu yake kuwa ‘Sanaa ni kazi tuikuze, tuilinde na kuithamini’, Basata iliwataka wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani, kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizo kwenye vibali vyao vya uendeshaji kumbi.

“Wanaelekezwa kuhakikisha wanakuwa na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda wa matumizi wa kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalumu hasa makazi ya watu na kuhakikisha ulinzi na usalama wa maisha ya watu na mali zao,” ilieleza taarifa hiyo.

Basata pia iliwakumbusha wamiliki wa kumbi za sherehe na burudani, kuwa inakatazwa kukusanya watoto kwenye kumbi hizo kupitia ‘Disko Toto’ katika msimu huu wa Sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya, ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.

“Uzoefu unaonesha, kwamba nyakati za sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi hujisahau na kuandaa madisko toto hali mbayo imekuwa ikisababisha maafa ambayo yangeepukika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.

“Aidha, baadhi ya wamiliki na waendeshaji kumbi wamekuwa wakijisahau na kuendekeza faida bila kujali maelekezo ya vibali vyao, wamekuwa wakijaza watu kupita viwango vya madaraja waliyopangiwa na Basata,” ilieleza taarifa hiyo na kuonya kuwa hatua kali na za kisheria zitachukuliwa kwa atakayekiuka maagizo hayo.

 

RAIS DKT. MAGUFULI AKUTANA NA BALOZI WA UTURUKI NCHINI MHE YASEMIN ERALP


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiwa na Balozi wa Uturuki nchini Mhe. Yassemin Eralp walipokutana kwa mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Desemba 23, 2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika picha ya kumbukumbu na Balozi wa Uturuki nchini Mhe. Yasemin Eralp walipokutana kwa mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Desemba 23, 2016. Wengine kutoka kushoto ni Balozi zuhura Bundala, Balozi Joseph Sokoine na Bw. Hassan Mwamweta wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiwa na Balozi wa Uturuki nchini Mhe. Yassemin Eralp walipokutana kwa mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Desemba 23, 2016

 

Ijumaa, 23 Desemba 2016

EXIM BENKI YA CHINA YAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kushoto pamoja na Makamu wa Rais wa Benki ya Kimataifa ya Exim ya Nchini China Bwana Sun Ping wakiingia ndani ya Ukumbi kwa ajili ya mazungumzo ya pamoja ya ushirikiano kati nya pande hizo mbili. Nyuma ya Balozi Seif Kushoto ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Mh. Mohamed Ahmed Salum.
Makamu wa Rais wa Benki ya Kimataifa ya Exim ya Nchini China Bwana Sun Ping akisalimiana na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar Nd. Khamis Mussa.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Nd. Asha Ali Abdulla akisalimiana na Bwana Sun Ping kabla ya kuanza Mkutano wao.
Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akizunguma na Makamu wa Rais wa Benki ya Kimataifa ya Exim ya Nchini China Bwana Sun Ping Makao Makuu ya Benki hiyo Mjini Beijing Nchini China.

Bwana Sun Ping kulia akibadilishana mawazo na Mgeni wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara bnaada ya kumaliza mkutano wao Mjini Beijing China.

 

 
Benki ya Kimataifa ya Exim ya Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China imeahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusaidia Maendeleo ya Wananchi wake kupitia miradi tofauti inayoanzishwa.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Benki hiyo Bwana Sun Ping wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anayeuongoza Ujumbe wa Viongozi Wanne wa Serikali akimalizia ziara yake ya Kiserikali ya Siku Tano Nchini China.

Bwana Sun Ping alisema Taasisi hiyo ya Fedha ya China imeridhika na hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa na Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake kiasi kwamba Benki hiyo itaangalia namna za kusaidia nguvu katika kuona miradi inayoanzishwa inatekelezwa.

Makamu wa Rais wa Benki hiyo ya Exim alimueleza Balozi Seif na Ujumbe wake kwamba Tanzania ndio nchi pekee iliyopewa kipaumbele na benki hiyo katika kupatiwa mikopo na misaada ikilinganishwa na Nchi nyengine Barani Afrika.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Benki hiyo ya Exim kwa ukarimu wake wa kuunga mkono miradi ya Maendeleo inatotekelezwa na Zanzibar kwa njia ya misaada na hata mikopo.

Balozi Seif alisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana miongoni mwa Wanachi waliowengi Zanzibar kufuatia kuibuka kwa miradi kadhaa ya Kiuchumi na maendeleo iliyopata msukumo kupitia Benki hiyo ya Kimataifa ya Exim.

Othman Khamis Ame 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar 23/11/2016.


Saturday, December 24, 2016

Kingunge Asema Bila tume huru Wapinzani Wasahau Kuingia Ikulu .......Lowassa Akubali Yaliyopita Si Ndwele

Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru amesema bila ya kuwa na tume huru ya uchaguzi na Katiba Mpya, vyama vya upinzani visahau kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Kauli ya Kingunge imekuja siku moja baada Rais John Magufuli kumteua Jaji Themistocles Kaijage kuwa mwenyekiti mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) baada ya Jaji Damian Lubuva kufikia muda wake wa kustaafu.

Kwa muda mrefu, NEC imekuwa ikilalamikiwa na vyama vya upinzani kwa kutokuwa huru kwa sababu ya uongozi wake wote huteuliwa na Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, huku sheria zikikataza matokeo ya nafasi ya urais kupingwa mahakamani.

Mbali na mwenyekiti kuteuliwa na Rais, wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo ni wakurugenzi wa wilaya ambao pia huteuliwa na Rais kwa kuwa NEC haina wafanyakazi wake kote nchini.

Akizungumza katika mkutano wa kuwafariji vijana waliokamatwa na Jeshi la Polisi na kushtakiwa kwa makosa yaliyohusu Uchaguzi Mkuu uliopita, uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Kingunge aliwatia moyo vijana hao, akisema hakuna ushindi unaopatikana bila kupambana.

Kingunge, aliyetumia muda mrefu kueleza historia ya maisha yake katika siasa na jinsi alivyopambana katika harakati za kudai uhuru, alisema hali ya sasa ni mbaya kuliko wakati wa wakoloni wa Kiingereza ambao walikujwa wakali, kwa sababu CCM haifuati Katiba wala sheria.

“Yako mambo ambayo itabidi tujitahidi yaamuliwe sasa kabla ya 2020. Mambo hayo makubwa kwanza ni tume huru (ya uchaguzi). Suala hilo lazima lizungumzwe sasa, hatuwezi kwenda 2020 na tume ya sasa na Katiba ya mwaka 1977. Tukienda hivyo sahau habari ya upinzani kushinda uchaguzi,” alisema.

Kingunge ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo ya waziri anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na mkuu wa mkoa alisema, “(Pia) Sheria inayohusu matokeo ya uchaguzi wa Rais kuhojiwa. Hivi sasa sheria inasema matokeo ya uchaguzi wa Rais hayahojiwi mahakamani. Lazima hilo suala lipate jibu sasa. Kwa hiyo Katiba na sheria iseme, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanaweza kuhojiwa mahakamani. Tusipokuwa na hilo, tutakuwa na matatizo makubwa sana.”

Alisema pamoja na kwamba Chadema inapendwa na wananchi wengi na Edward Lowasa aliyegombea urais kwa tiketi chama hicho, anapendwa, bado ni vigumu kushinda kwa sababu mfumo uliopo sasa.

“Tufanye yoyote, lakini tuhakikishe, ama tunapata Katiba Mpya au vipengele hivi vya sheria vinafanyiwa marekebisho. Kwa maoni yangu, kundi hili lililo madarakani bila shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi, halitataka mabadiliko,” alisema.

Alisema enzi zao walifanikiwa kupata uhuru kwa sababu walijitolea kwa nguvu na wengine, na yeye akiwamo, waliacha kazi za mishahara mikubwa na kujiunga na Tanu kupigania uhuru.

“Tulifanikiwa kupata uhuru kwa sababu walijitoa mhanga. Wengi tu waliacha kazi, mtu anamaliza chuo kikuu anasema sitaki kazi anaingia Tanu kusaidia. Kwa hiyo tukawa na jeshi kubwa la vijana waliohakikisha nchi inapata uhuru,” alisema.

“Ninyi mnapambana katika mazingira magumu na wazee wenzenu walipambana katika mazingira hayo. Haikuwa rahisi. Wapo wengi walitusaliti, wengine hawakufanya lolote. Baba yangu tuligombana, nilipoacha kazi kwenda kuitumikia Tanu. Miezi sita hatukuzungumza.”

Akizungumza mkutano huo, Lowassa, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliwatia moyo vijana walioshtakiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, akisema bado jeshi kubwa la vijana linahitajika.

“Yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo. Si haki kusema unakwenda mahali pengine, mwenzako amepasafisha, safisha pa kwako. Nimefurahia moyo huo. Kama alivyosema Ngombale, tunataka jeshi kubwa zaidi, watu wengi zaidi,” alisema Lowassa.  

Saturday, December 24, 2016

Penzi la Bibi wa Miaka 60 Laua Kijana wa Miaka 23

KIJANA mwenye umri wa 23 na mpenzi wake, bibi mwenye umri wa miaka 60 , wakazi wa kijiji cha Tentula, Kata ya Ikozi wilayani Sumbawanga, wanashikiliwa na polisi wakihutumiwa kumshambulia na kumuua kikatili jirani yao aitwae Desder Justino (23) kwa kile kinachoelezwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Inaelezwa kuwa, Justino pia alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na bibi huyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, George Kyando alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa mauaji hayo yalitokea Desemba 21 mwaka huu saa nne asubuhi katika nyumba ya mwanamke huyo iliyopo kijijini Tentula.

Taarifa kutoka kijijini humo zinadai kuwa, mwanamke huyo licha ya umri wake kuwa mkubwa, alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na vijana hao wawili wa rika moja.

Kamanda Kyando hakuwa tayari kutaja majina ya wapenzi hao ambao ni watuhumiwa wa mauaji kwa sababu za uchunguzi.

Lakini alisema mwanaume ana umri wa miaka 23 huku mpenzi wake ana umri wa miaka 60. Akielezea zaidi, Kamanda Kyando alisema siku ya tukio Justino alikwenda nyumbani kwa mwanamke huyo ambaye anadaiwa kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi na kumkuta kijana mwingine (mtuhumiwa), na hapo ndipo ugomvi ukaibuka baina ya vijana hao.Alisema Justino alijeruwa kichwani.

“Wawili hao yaani wapenzi hao (mwanamke na mwanaume) walimshambulia Justino (Desder) kwa kumpiga kichwani na kitu chenye ncha kali na kumjeruhi vibaya na alikufa akiwa anatibiwa hospitalini,” alisema Kamanda Kyando na kuongeza  kuwa, watuhumiwa hao wanashikiliwa na watafikishwa mahakamani uchunguzi wa awali utakapokamilika.

Saturday, December 24, 2016

Makamu wa Rais ataka wazazi na walezi kuacha kuwaoza watoto wakiwa wadogo

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka wazazi na walezi wa visiwani Zanzibar, kuacha tabia ya kuwaoza wasichana wakiwa na umri mdogo, bali wawasomeshe kwa ajili ya manufaa yao ya jamii kwa ujumla.

Samia alisema hayo kwa nyakati tofauti, wakati akizindua madarasa ya kisasa iliyojengwa kwenye eneo la Kilimani na kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa na ujenzi wa msikiti mkubwa kuliko yote nchini Tanzania unaojengwa katika eneo la Ijitimai Kidoti mkoani Kaskazini Unguja.

Ujenzi huo unafanywa kwa michango ya wananchi. Alisema hayo katika siku yake ya kwanza ya ziara ya Kikazi Unguja.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, Zanzibar, ilieleza kuwa makamu huyo wa Rais yupo katika ziara visiwani Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Samia alisema kama wazazi na walezi watasomesha watoto wa kike, elimu watakayopata itasaidia kwa kiasi kikubwa wasichana hao, kufanya maamuzi sahihi na yenye tija katika jamii.

Alisisitiza kuwa elimu ni haki ya msingi kwa mtoto wa kike, hivyo ni muhimu kwa jamii ya Zanzibar ihakikishe watoto wa kike wote wanapata elimu, kwani watakuwa na uwezo wa kuchagua na kuandaa mustakbali wa maisha yao ya baadaye, ikilinganishwa na hali ilivyo sasa kwenye baadhi ya maeneo.

Kuhusu elimu ya dini, aliwahimiza wazazi na walezi, kuwalea watoto katika maadili mema kwa kuzingatia maandiko matakatifu ya Mtume Mohammad (S.A.W).

Saturday, December 24, 2016


Jaji Magimbi kusikiliza rufaa ya Godbless Lema Desemba 28


JAJI Salma Magimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ndiye atakayesikiliza rufaa ya kutaka dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Desemba 28 mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Wakili wa Lema, Sheck Mfinanga alisema rufaa hiyo namba 126 ya mwaka 2016, imepangiwa kusikilizwa na Jaji huyo. Alisema kimsingi wanalalamikia uamuzi wa Mahakama kutomwachia huru, licha ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kumpatia dhamana.

Awali, uamuzi uliotolewa Novemba 11 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Desderi Kamugisha, ambapo Lema anakabiliwa na kesi namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli, uliweka wazi dhamana.

Hakimu Kamugisha alikubali kutoa dhamana kwa madai kuwa sheria haizuii kumpa dhamana mtu kwa kesi ya uchochezi, ila kabla ya kutoa masharti ya dhamana licha ya kutamka dhamana ipo wazi, mawakili wa serikali walipinga kumpatia dhamana Lema, kwa madai wameonesha nia ya kukata rufaa.

Kutokana na mawakili hao kusema hivyo, Hakimu aliamua kesi hiyo ibaki kama ilivyo na mtuhumiwa asubiri maamuzi ya Mahakama Kuu.

Lema alilazimika kwenda mahabusu hadi sasa katika Gereza Kuu la Kisongo. Baada ya hatua hiyo, mawakili wa Lema wakiongozwa na Sheck Mfinanga, walianza kutafuta suluhisho la mteja wao kupata dhamana na walianza na kuandika maombi na kuitaka Mahakama Kuu kufanya marejeo kwa kuitisha faili la kesi hiyo kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Lakini, ombi lilitupwa na Kaimu Jaji Mfawidhi, Sekela Moshi, Novemba 11 mwaka huu kwa madai kuwa walikosea, badala ya kufanya marejeo walitakiwa kukata rufaa. Mawakili hao walilazimika kukata rufaa siku hiyo hiyo na Desemba 2 mwaka huu, ilitupwa na Jaji Fatuma Masengi kwa madai kuwa ilikuwa nje ya muda.

Baada ya hatua hiyo, mawakili hao walipeleka ombi Mahakama Kuu, kuomba kuongezewa muda wa kupeleka notisi ya kukata rufaa yao juu ya dhamana na hatimaye Desemba 20, Jaji Dk Modesta Opiyo, alikubali na kumwongezea muda Lema wa siku 10.

Siku hiyo ya kuongezewa muda, mawakili wa Lema walifanikiwa kukata rufaa hiyo. Lema anashikiliwa kwa zaidi ya mwezi katika mahabusu ya Gereza Kuu Kisongo.

Alikamatwa Novemba 2 mwaka huu nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma na alifikishwa mahakamani Novemba nane mwaka huu, akikabiliwa na mashitaka ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.

Saturday, December 24, 2016


Polisi Yanasa 200 Kwa Ujambazi Dar


JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa 200 wanaohusishwa na makosa mbalimbali.

Wanne kati ya hao, wanatuhumiwa kukutwa na gari lililoibwa hivi karibuni katika eneo la ofisi za Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (TIRA) zilizopo Manispaa ya Ilala.

Mkuu wa Operesheni Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, alitaja watu hao wanne wanaotuhumiwa kukutwa na gari hilo kuwa ni Leonard Said, Omary Said, Shomaly Kilobo na Adam Unemba.

Alisema katika uchunguzi wa awali, watuhumiwa wote wamekiri kuhusika katika wizi wa gari hilo, aina ya Toyota Spacio lenye namba za usajili T 398 CAE, boksi la chuma la kutunzia fedha na televisheni ya ukubwa wa inchi 32.

Alisema Desemba 5, mwaka huu alipokea taarifa kutoka kwa Mhasibu Mkuu wa TIRA, Egnance Edward (53) kuwa wamekuta ofisi za mamlaka hiyo, zimevunjwa na kuibwa baadhi ya vifaa ikiwemo gari hilo.

 
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amemwambia rais wa Tunisia Beji Essebsi kwamba serikali ya Ujerumani inataka kuharakisha hatua za kuwarudisha wakimbizi waliokataliwa hifadhi. Merkel amezungumza hayo baada ya polisi wa Italia kumpiga risasi na kumuua Anis Amri kijana wa Kitunisia aliyetuhumiwa kuhusika na mashambulio katika soko la Krismasi mjini Berlin ambapo watu 12 waliuwawa baada ya yeye kulitosa Lori katika umati wa watu. Amri alinyimwa hifadhi ya ukimbizi hapa Ujerumani. Kansela Merkel amesema kwamba mkasa huo umezua maswali mengi na ameahidi kwamba serikali yake itachukua hatua ili kuimarisha usalama. Wakati huo huo waziri wa sheria Heiko Maas na mwenzake wa mambo ya ndani Thomas de Maizière wametangaza kufanyika mazungumzo juu ya kuchukua hatua za haraka za kuwarudisha wakimbizi waliokataliwa hifadhi sambamba na kuwafwatilia kwa karibu wale wanaodhaniwa kuwa ni hatari.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kuitaka Israel isimamishe ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi kwenye Ukingo wa Magharibi. Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Samantha Power ametetea uamuzi wa nchi yake wa kutoshiriki kupiga kura baada ya miaka mingi ya kutumia kura ya turufu kuyapinga maazimio yaliyokuwa yanailaumu Israel. Kwa upande wake Israel imemlaumu rais Barack Obama kwa hatua hiyo na imeapa kwamba haita litekeleza azimio hilo la Umoja wa Mataifa. Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa amesema uamuzi wa nchi yake kwa namna yoyote ile hautapunguza msimamo thabiti wa Marekani wa kuunga mkono usalama wa Israel akitolea mfano msaada uliotolewa na Marekani wa dola bilioni 38 kwa ajili ya kununulia silaha. Kwa upande wake mamlaka ya Palestina yamelipongeza Baraza la Usalama kwa kupitisha azimio hilo huku yakiilaumu Israel kwa sera yake ya ujenzi wa makaazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi. 

Rais Barack Obama wa Marekani ametia saini sheria juu ya sera ya ulinzi itakayoruhusu kiasi cha dola bilioni 611 kwa ajili ya jeshi la Marekani kwa mwaka ujao wa 2017. Sheria hiyo ina vipengele vyenye lengo la kuendeleza kasi ya kupambana na kundi la magaidi wanaojiita Dola la Kiislamu IS lakini wakati huo huo rais Obama amelilaumu bunge kwa msimamo wake wa kushikilia kuiendeleza jela ya Guantanamo katika kisiwa cha Cuba. Asilimia 2.1 ya fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kuongeza mishahara ya wanajeshi.

Serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wapinzani nchini humo wamefikia makubaliano ya muda ambapo sasa rais Joseph Kabila ataachia madaraka ifikapo mwisho wa mwaka ujao wa 2017. Baraza la maaskofu wa kanisa Katoliki ambalo lilisimamia mazungumzo ya kutafuta suluhisho katika mgogoro wa kisiasa nchini Kongo limetoa taarifa kwamba makubaliano hayo yatatiwa saini baada ya sherehe za Krismasi. Kulingana na makubaliano hayo, uchaguzi wa rais utafanyika kabla ya kumalizika mwaka ujao wa 2017 wakati huo huo serikali ya umoja itaundwa katika kipindi cha mpito. Rais Joseph Kabila alipaswa kuondoka madarakani tangu tarehe 19 mwezi huu wa Desemba baada ya muhula wake kumalizika lakini hakufanya hivyo huku uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi Novemba umeahirishwa hadi Aprili mwaka 2018. Wapinzani wengi wanaitathmini hatua hiyo kuwa ni njama za kumwezesha rais Kabila kuendelea kubakia madarakani baada ya mihula miwili inayoruhisiwa kikatiba. 

Majeshi ya Syria yameimarisha udhibiti wa mji wa Aleppo baada ya kuuteka kabisa. Wenyeji waliokuwa na shauku ya kurudi majumbani mwao walirejea katika mji huo ulio haribiwa sana. Jeshi la Syria limetangaza kuiteka Aleppo mashariki mji uliokuwa ngome ya waasi baada ya kufikiwa makubaliano juu ya kuondolewa maalfu ya wapiganaji wa upinzani na raia. makubaliano hayo yalifikiwa baada ya juhudi za Uturuki na Urusi ambayo ni mshirika mkuu wa rais Bashar al Assad. Makubaliano hayo yamemaliza vita vikali vya zaidi ya miaka minne ambapo mji huo wa Aleppo uligawanyika katika sehemu mbili upande wa magharibi uliokuwa unadhibitiwa na serikali na wa mashariki uliokuwa chini ya waasi. 

michezoooo
 


Seebait.com 2016

KIONGOZI WA ZAMANI WA 'MABAUNSA' AFARIKI DUNIA

 
  ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wanyanyua Tanzania (TWLA), Mpoki Bukuku amefariki dunia leo. Bukuku, aliyekuwa mpiga picha wa kampuni ya The Guardian, wachapishaji wa magazeti la Nipashe, The Guardian na Lete raha, amefariki dunia leo katika Taasisi ya Mifupa (MOI), alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu. Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa Umma (MOI) Almas Jumaa. "Ni kweli Mpoki amefariki dunia mchana huu, alipokelewa jana usiku baada ya kupata ajali ya gari maeneo ya Mwenge  (ITV), taarifa zaidi tutazitoa baadaye," alisema Almas.
Mpoki Bukuku (kushoto) akiwa na Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete
Bukuku (kushoto) akiwa na Mwandishi nguli wa habari za michezo nchini, Masoud Saanan
Mpoki Bukuku amewahi pia kufanya kazi kampuni za Business Times Limited (BTL) na Mwananchi Communication Limited (MCL) kabla ya kujiunga na Guardian. Marehemu ameacha mke na watoto. 

YANGA 'MIGOMO' WALAZIMISHWA SARE 1-1 NA AFRICAN LYON


YANGA imevuna faida ya mgomo baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na African Lyon katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam. Matokeo hayo yanaifanya Yanga iendelee kukamata nafasi ya pili kwa pointi zake 37 baada ya kucheza mechi 17 sawa na Simba iliyo kileleni kwa pointi zake 38.  Simba inaweza kuongeza gepu la pointi hadi nne iwapo itashinda dhidi ya JKT Ruvu leo Uwanja wa Uhuru.  Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao na African Lyon walicheza kwa kujihami zaidi kipindi cha kwanza wakifanya mashambulizi ya kushitukiza. Mashambulizi ya Yanga leo hayakuwa na nguvu kutokana na kocha Mzambia, George Lwandamina kulundika viungo watano, Haruna Niyonzima, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Said Juma na Deus Kaseke akitumia mshambuliaji mmoja tu, Amissi Tambwe.
Kiungo wa Yanga, Mzimbabwe Thabani Kamusoko akikosa bao la wazi leo 
Kiungo wa Yanga, Deus Kaseke (kulia) akitafuta maarifa ya kumpira beki wa Lyon, Miraj Adam 
Winga wa Yanga, Simon Msuva akimiliki mpira mbele ya beki wa African Lyon
Hata hivyo, ililitia misuokosuko lango la Lyon kuanzia dakika ya tatu baada ya Tambwe kupiga kichwa vizuri akimalizia krosi ya Msuva, lakini mpira ukaenda juu kidogo na dakika ya 33 Niyonzima akapiga juu ya kuikosesha timu yake bao la wazi. Lyon nayo ilikaribia kupata bao dakika ya 30 kama si mpira wa kichwa wa Thomas Maurice kwenda nje baada ya krosi ya Abdallah Mguhi ‘Messi’. Kipindi cha pili, timu zote ziliingia kwa malengo ya kutafuta mabao na kuanza kushambuliana moja kwa moja hali iliyonogesha mchezo.  Walikuwa Lyon waliofanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 67 kupitia kwa Ludovic Venance aliyemalizia pasi ya mchezaji wa zamani wa Yanga, Abdallah Mguhi ‘Messi’. Venance aliyesajiliwa dirisha dogo kutoka Mbao FC ya Mwanza, alifunga bao hilo baada kuingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Awadh Juma. Hata hivyo, bao hilo halikudumu sana, kwani Yanga walifanikiwa kusawazisha dakika ya 74 kupitia kwa mkali wake mabao, Amissi Tambwe akimalizia krosi nzuri ya beki wa kulia Juma Abdul. Yanga wakaongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Lyon kusaka bao la ushindi, huku wachezaji walioingia kipindi cha pili, Emmanuel Martin na Geoffrey Mwashiuya wakiupasua vizuri ukuta mgumu wa wenyeji wao, lakini bahati mbaya hawakupata bao.  Wachezaji wa Yanga walicheza chini ya kiwango chao na dhahiri walionekana kuathiriwa na maandalizi hafifu kabla ya mechi hiyo – hususan kutokana na mgomo wa mazoezi kwa siku mbili, Jumatatu na Jumanne wakishinikzia kulipwa mishahahra yao ya Novemba. Mashabiki wa Yanga waliwatukana wachezaji kwa kitendo cha kugoma na hawakufanikiwa kuwafanyia fujo kutokana na ulinzi wa askari. Kikosi cha African Lyon kilikuwa; Youthe Jehu, Baraka Jaffary, Miraji Adam, Halfan Twenye, Hamad Wazir, Hamad Manzi, Hassan Isihaka,Omary Abdallah/Peter Mwalyanzi dk80, Awadhi Juma/ Ludovic Venance dk46, Thomas Maurice/Cossmas Lewis dk82. na Abdallah Mguhi. Yajnga SC; Deogratias Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Haruna Niyonzima, Mwinyi Hajji Mngwali/ Geoffrey Mwashiuya dk74, Kelvin Yondan, Vincent Bossou, Simon Msuva, Thabani Kamusoko/ Obren Chirwa dk56, Amissi Tambwe, Said Juma na Deus Kaseke/ Emanuel Martin dk65.

CHANZO CHA HABARI MPEKUZI, DW ,BIN ZUBERY
JUMAMOSI HII JUMAMOSI HII Reviewed by RICH VOICE on Desemba 23, 2016 Rating: 5

Hakuna maoni

Chapisho Lililoangaziwa

Thursday, September 15, 2016 Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya Septemba 15 ...