habari za leo hizi hapa
Saturday, December 17, 2016
Mbunge Sugu anusurika ajali, mtoto afariki kwenye ajali hiyo
Taarifa
zilizoripotiwa na kituo cha runinga cha ITV leo December 17 2016
zinasema kuwa mbunge wa Mbeya mjini ‘CHADEMA’, Joseph Mbilinyi
amenusurika kifo katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Iyunga jijini
Mbeya baada ya gari lake kufeli break na kumgonga mtoto ’15’ ambaye
amefariki wakati akipelekwa hospitali.
Aidha
taarifa hiyo inaeleza kuwa askari polisi wanne wamejeruhiwa baada ya
kupata ajali wakati wakielekea kwenye ajali hiyo aliyopata mbunge Joseph
Mbilinyi ‘sugu’
Gari hilo lilikuwa linaendeshwa na dereva wake, Gabriel Andrew (43) ambaye anashikiliwa na polisi.
Saturday, December 17, 2016
Dr Mwele Malechela(Aliyetumbuliwa) : Safari itasonga kwa msaada wa Mungu
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, NIMR, Dr Mwele Malechela, ametoa kauli yake baada ya uteuzi wake kutenguliwa na Rais Dkt John Magufuli, Ijumaa hii.
Kutenguliwa
kwake kumekuja siku moja tu baada ya kuzungumza na waandishi na kudai
kuwepo kwa virusi vya Zika nchini. Alisema kati ya watu 533 waliopimwa
wakati wa utafiti walioufanya, asilimia 15.6 waligunduliwa kuwa na
virusi hivyo. Taarifa yake, ilikuja kukanushwa na Waziri wa Afya, Ummy
Mwalimu.
Akijibu tweet iliyosema, ” Pole sana @mwelentuli safari yako na isonge mbele Dada,” Dr Mwele amesema, “Ahsante na itasonga kwa msaada wa Mungu.”
Tweet nyingine alijibu: Ahsante Mathew. Nilipewa dhamana nimetumikia ninamshukuru Mungu kwa nafasi ya kutumikia WaTanzania kupitia utafiti.”
Saturday, December 17, 2016
Waziri Simbachawene atoa agizo jipya kwa machinga
Waziri
wa TAMISEMI George Simbachawene amewataka wamachinga kutotafsiri vibaya
agizo la Rais Magufuli kuwa halikumaanisha wafanye biashara kiholela
mahala popote bila utaratibu bali wazingatie sheria zilizopo zikiwamo za
mipango miji na usafi.
Simbachawene
pia amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na mamlaka za serikali
za mitaa, kuhakikisha wanatekeleza agizo la Rais John Magufuli la
kuwatafutia maeneo ya kufanyia biashara wafanyabiashara hao na
kuwashirikisha kwenye mchakato mzima wa kubaini maeneo yenye wateja na
miundombinu rafiki.
Aidha, watendaji nao wametakiwa kutotumia tafsiri hiyo kususa na kuwaacha wamachinga wafanye biashara zao kiholela.
Amesema
endapo utaratibu huo utafuatwa pamoja na mambo mengine utaweza
kurasimisha shughuli za wamachinga hali itakayosaidia pia kundi hilo
kuchangia mapato ya halmashauri kwa kiasi kikubwa na kuondoa kabisa
tabia ya kufukuzana fukuzana kila kukicha.
Saturday, December 17, 2016
Mahakama yatupa pingamizi la serikali katika kesi ya mbunge Godbless Lema.
Uamuzi wa kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya nia ya kukata
rufaa dhidi ya dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless
Lema, unatarajiwa kutolewa Desemba 20, mwaka huu na Mahakama Kuu Kanda
ya Arusha.
Uamuzi huo utatolewa baada ya Lema jana kufanikiwa kuwasilisha maombi yake ya kuongezewa muda wa kuleta notisi hiyo ya rufaa dhidi ya dhamana yake baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali pingamizi mbili za mawakili wa Serikali waliokuwa wakitaka maombi hayo yasisikilizwe.
Mbele ya Jaji Dk. Modesta Opiyo wa mahakama hiyo, upande wa Jamhuri
ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili Hashim Ngole, Matenus Marandu, Elizabeth
Swai na Adelaide Kasala huku Lema akitetewa na Wakili Sheck Mfinanga na
Faraji Mangula.
Katika maombi hayo namba 69 ya mwaka huu, baada ya kusikiliza hoja za
pande zote mbili, Jaji Dk. Opiyo alisema kuwa atatoa uamuzi huo siku
hiyo saa sita mchana.
“Baada ya kusikiliza hoja za pande zote nitatoa uamuzi Jumanne ijayo
saa sita mchana, msije asubuhi ili nipate muda wa kupitia hoja zenu,”
alisema Jaji Dk. Opiyo.
Awali, akitoa uamuzi wa pingamizi mbili zilizotolewa Desemba 14,
mwaka huu na mawakili hao wa Jamhuri, Jaji Dk. Opiyo, aliyesoma uamuzi
huo kwa muda wa dakika 50 kuanzia saa 5:30 asubuhi hadi saa 6:20 mchana,
alisema ameamua kuzitupa pingamizi hizo baada ya kuziona hazina mashiko
ya kisheria.
Alisema kuwa hakuna maombi kama hayo yaliyoacha kusikilizwa
mahakamani kwa kushindwa kuonyesha kifungu namba 392 A cha sheria ya
uendeshaji wa mashauri ya jinai hivyo akalitupa pingamizi la kwanza la
mawakili wa Serikali waliodai maombi hayo hayakufuata utaratibu wa
kisheria ikiwemo kutoonyesha vifungu vya sheria waliyoitumia kuleta
maombi hayo.
“Baada ya kupitia hoja za pande zote, mahakama imeamua kutupa
pingamizi hizo za Jamhuri baada ya kuziona kuwa hazina mashiko kisheria
na hata upande wa Jamhuri ulishindwa kurejea shauri lolote ambalo
limewahi kufanyiwa uamuzi na mahakama za juu kuhusu suala hilo,” alisema
Jaji Dk. Opiyo.
Akizungumzia hoja ya pili ambayo Jamhuri ilidai ya kiapo kinachounga
mkono maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo kimekosewa hivyo hakifai
kwa sababu wamejumuisha mambo yasiyotakiwa kisheria ikiwemo maoni,
mabishano na hitimisho na kubeba hoja za rufaa alisema mahakama hiyo
imeondoa aya ya 11 na 12.
Alisema kuwa aya nyingine za 9, 10, 13 na ile ya 17 zitabaki katika
hati hiyo ya kiapo kwa sababu hazibebi hoja za rufaa, maoni, mabishano
wala hitimisho hivyo mahakama hiyo haiwezi kukataa hati hiyo ya kiapo
iliyoambatanishwa na maombi hayo.
Akiwasilisha hoja za maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi
hiyo ili rufaa hiyo iweze kusikilizwa, Wakili Mfinanga, alidai
mahakamani hapo kuwa maombi hayo yamewasilishwa mahakamani hapo chini ya
kifungu 361(2) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Alidai kuwa uamuzi wanaotarajia kukatia rufaa ni uliotolewa Novemba
11, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Desderi
Kamugisha, ambapo Lema anakabiliwa na kesi namba 440 na 441 za uchochezi
dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.
Alitaja sababu mbili za msingi za kukatia uamuzi huo rufaa kuwa ni
kuiomba mahakama hiyo ipitie makosa ya kisheria yaliyofanywa na mahakama
ya chini na kusema kuwa uamuzi huo ulimpa mleta maombi (Lema) dhamana
ila kabla hajapewa masharti ya dhamana upande wa Jamhuri ulitoa notisi
ya nia ya kukata rufaa.
“Kwa msingi huo mahakama ilisema imefungwa mkono na hawawezi
kuendelea na jambo lolote kuhusu suala hilo hata uamuzi wake wa kumpa
dhamana haukuwezwa kutimizwa na mahakama haikueleza upande wowote ambao
haujaridhika na uamuzi huo una haki ya kukata rufaa,” alidai Mfinanga na
kuongeza:
“Kuna vitu muhimu na vitasahihishwa iwapo tutaleta notisi ya nia ya
kukata rufaa na rufaa yenyewe kusikilizwa na mahakama yako ambayo ni
msimamizi wa haki na sheria ikatoa ruksa ili tuweze kusikilizwa na
rekodi ya mahakama ya chini iweze kurekebishwa, ni muhimu mahakama
kuzingatia maombi haya pasipo kuzingatia mambo mengine.”
Huku akirejea mashauri mbalimbali ya mahakama za juu, aliendelea
kueleza mahakama hiyo kuwa mahakama ikishasema imempa mtu haki ya
dhamana lazima itaje masharti ya dhamana.
“Tunaomba mahakama itupatie muda tena mfupi ambao hautazidi hata saa
1:30 kwa ajili ya kuleta notisi hiyo ili mahakama iweze kurekebisha
makosa hayo,” alisema.
Akiwasilisha hoja ya pili, Wakili Mangula, alidai mahakamani hapo
kuwa tangu kutolewa kwa uamuzi huo hawajapumzika na muda wote walikuwa
mahakamani.
Alidai kuwa walikuwa wanaenda mahakamani kwa njia tofauti ili kuiomba mahakama irekebishe makosa hayo ya kisheria.
Alidai kuwa baada ya uamuzi huo kutolewa muda wa kazi ulishaisha na
ilikuwa Ijumaa hivyo Novemba 14, mwaka huu walipeleka barua ya
malalamiko mahakamani hapo na walipoitwa pande zote mbili katika shauri
namba 6 lakini walikumbana na pingamizi zilizowasilishwa na mawakili wa
Serikali.
“Novemba 22, mahakama ilitoa uamuzi na kututaka waleta maombi tukate
rufaa na hapo mleta maombi alipata haki yake ya kukata rufaa ambayo
haikuelezwa mahakama ya chini na tulitoa notisi tukiamini tuko ndani ya
muda na hatimaye rufaa ililetwa mbele ya Jaji Mfawidhi Fatuma Masengi,”
alidai.
Alieleza mahakama hiyo kuwa katika rufaa hiyo namba 113, walikutana
tena na pingamizi la Serikali kuwa wametoa notisi ya rufaa hiyo nje ya
muda wa siku moja hivyo hizo ni jitihada walizokuwa wakifanya na si
wazembe, wajinga wa sheria kama ilivyodaiwa na wakili wa Serikali.
Akijibu hoja za waleta maombi hao, Wakili Ngole, alidai kuwa ni
wazembe, wajinga wa sheria na kuwa hata uamuzi wanaolalamikia mahakamani
hapo ambao awali ulimpa mleta maombi dhamana, lakini kabla hajapewa
masharti ya dhamana mahakama iliingiliwa mamlaka yake hawajawasilisha na
maombi hayo.
Wakili huyo alidai mahakamani hapo kuwa hakukuwa na makosa yoyote ya
kisheria kama inavyodaiwa na waleta maombi hao na kudai kuwa baada ya
hakimu kusema mahakama inampa mshtakiwa dhamana Jamhuri kwa haki yake
walisimama na kuifahamisha mahakama wana nia ya kukata rufaa.
“Ni utaratibu wa kisheria kuwa panapokuwa na notisi ya nia ya kukata
rufaa mahakama haiwezi kuendelea na jambo lolote kuhusiana na kesi hiyo,
hivyo hakimu asingeweza kuendelea na kesi na inafahamika notisi
inasimama badala ya rufaa,” alidai na kuongeza:
“Kwa mujibu wa kifungu 359(1) na 361(1) cha sheria ya mwenendo wa
makosa ya jinai, vinaeleza mtu ambaye hajaridhika na hatua yoyote au
uamuzi uliotolewa au kupitishwa anaweza kukata rufaa mahakama za juu.”
Lema anashikiliwa kwa zaidi ya mwezi mmoja katika mahabusu ya Gereza
Kuu la Kisongo baada ya kukamatwa Novemba 2, mwaka huu nje ya Viwanja
vya Bunge mjini Dodoma ambapo alifikishwa mahakamani Novemba 8, mwaka
huu akikabiliwa na mashtaka ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. Magufuli.
Saturday, December 17, 2016
Waziri Mkuu Amsimamisha Kazi Mwekahazina Wa Wilaya Ya Bahi.......Aagiza arudishwe Longido kujibu tuhuma zinazomkabili
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi aliyekuwa Mwekahazina wa
Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Issai Mbilu ambaye kwa sasa
amehamishiwa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma na kuagiza arudishwe haraka na
kuja kujibu tuhuma za ubadhilifu sh. milioni 642.4 za miradi
zinazomkabili.
“Tunaendelea
kudhibiti na kuweka nidhamu ndani ya Serikali. Ukiharibu Longido
usitegemee kuhamishiwa wilaya nyingine tunamalizana hapa hapa. Hatuwezi
kuhamisha ugonjwa hapa na kuupeleka wilaya nyingine hivyo Mwekahazina
huyu arudishwe haraka Longido,” amesisitiza.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana Ijumaa, Desemba 16, 2016 wakati akizungumza
na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwenye ukumbi wa
Halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Pia
amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw. Richard Kwitega
kumuandikia barua Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI) akimuomba amrudishe Mwekahazina huyo katika kituo
chake cha kazi cha zamani ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili.
Amesema
Serikali haitamvumilia mtumishi wa idara yoyote atakayeharibu jambo
halafu kuhamishwa sehemu nyingine, “hivyo naagiza kuanzia sasa
nimemsimamisha kazi Mwekahazina huyu na arudi hapa kujibu kwanini
ameleta hasara ya hizi fedha. Na nyie watumishi wengine hili liwe funzo
kwenu,” amesema.
Amesema
miradi mingi ya maendeleo inakwama kwa sababu ya baadhi ya watumishi
kuweka mbele maslahi binafsi badala ya kuzingatia maadili ya utumishi,
hivyo amewaagiza Wakuu wa Idara wafuatilie kwa makini miradi
inayotekelezwa katika maeneo yao kama inalingana na thamani halisi ya
fedha zilizotolewa.
Akizungumzia
kuhusu kushamiri kwa biashara haramu ya dawa za kulevya wilayani
Longido, Waziri Mkuu amewaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama
ya wilaya kufanya kufanya msako wa nyumba hadi nyumba na kuwakamata wote
watakaokutwa wanafanya biashara hiyo.
“Wilaya
hii ina sifa mbaya ya kuwa kitovu cha kusafirisha dawa ya kulevya
zikiwemo bangi na mirungi. Hivyo nawaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi
na Usalama waendeshe msako kwa kila nyumba na atakayekamatwa achukuliwe
hatua. Dawa za kulevya zinadhohofisha nguvu kazi ya Taifa,”.
“Ukivuta
bangi unapishana na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu kwani unakwenda kulala
jambo ambalo hatuwezi kulikubali. Watakaokutwa wanauza au kununua
mirungi na bangi wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa pamoja
na kutaifisha magari yanayotumika kubeba bidhaa hiyo haramu,” amesema.
Awali,
Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Daniel Chongolo akisoma Taarifa ya Wilaya
amesema Longido inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutumika
kama njia kuu ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi
kwenda nchi jirani ya Kenya ambako biashara hiyo imehalalishwa.
Changamoto
nyingine ni ukosefu wa hospitali ya wilaya hali inayofanya wananchi
kwenda kutibiwa Kenya, ambapo Waziri Mkuu alisema haiwezekani wakakosa
hospitali ya wilaya hivyo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo
kuhakikiusha anatenga fedha za ujenzi huo.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali ipo mbioni kujenga kiwanda
cha kuchakata madini ya magadi soda ili yawe na ubora na thamani kubwa.
Ametoa kauli hiyo aliposimamishwa na wananchi katika kijiji cha
Loonolwo kilichopo Kata ya Gelai Merugoi Wilayani Longido akitokea
wilayani Ngorongoro.
Amesema
lengo la kujenga kiwanda hicho ni kuwawezesha wananchi wa wilaya hiyo
hasa akinamama wanaoishi karibu na Ziwa Natron linalotoa magadi hayo
waweze kunufaika na uwepo wa ziwa hilo.
Waziri
Mkuu amesema ujenzi wa kiwanda hicho utawezesha vijana na akinamama hao
wanaouza magadi maeneo ya pembezoni mwa barabara katika ziwa Natron
kupata ajira kwa kuwa kitazalisha ajira zaidi ya 500 katika wilaya hizo
mbili za Longido na Ngorongoro.
Pia
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo kushirikiana na
wataalam wake kufanya tathimini ya uhaba wa chakula katika wilaya za
Longido na Ngorongoro ili Serikali ijue Mkoa wa Arusha una ukosefu wa
chakula kwa kiasi gani.
"Gambo
fanya tathimini ya hali ya njaa katika wilaya hizi mbili ili tuweze
kuwasaidia wananchi hawa. Hata hivyo nawaomba wananchi mtunze kiasi cha
chakula mlichonacho na marufuku tumia nafaka kwa ajili ya kupika pombe,”
amesema.
Awali,
wananchi hao waliokuwa na mabango mbalimbali walilalamikia kero ya
mipaka ya ardhi kati ya vijiji vya wilaya za Longido na Ngorongoro,
ambapo Waziri Mkuu alimuagiza Afisa Ardhi Mkoa wa Arusha, Bw. Hamdoun
Mansour kwenda katika vijiji hivyo vya mpakani na kukutana na viongozi
wa kimila ili kumaliza mgogoro huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Saturday, December 17, 2016
Waziri Mkuu: Waliouza Kiwanja Cha Shule Wachukuliwe Hatua
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw.
Rashid Taka na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Raphael Siumbo kufanya
uchunguzi na kuwachukulia hatua watendaji wote watakaobainika kuhusika
katika uuzwaji wa kiwanja cha shule ya msingi Waso.
Ametoa
agizo hilo Alhamisi, Desemba 15, 2016 wakati akihutubia wananchi katika
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Waso Wilaya ya Ngorongoro
akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Waziri
Mkuu alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona watendaji wachache
wasiokuwa waadilifu wanamega kiwanja cha shule na kukiuza kwa maslahi
yao, hivyo aliwataka viongozi hao kufuatilia na kumpa taarifa ya hatua
za kisheria walizochukua kwa wahusika.
“Mkuu
wa wilaya na Mkurugenzi hapa kuna malalamiko ya viwanja fuatilieni
viwanja hivyo vinavyolalamikiwa na wananchi ni viwanja gani je hiyo ya
kwamba mmeuza viwanja vya shule ameuziwa nani,” alisema.
Aidha, Waziri Mkuu amemtaka Bw. Taka ahakikishe Mkuu wa Idara ya
Ardhi,
Maliasili na Mzingira, Bw. Switbeth Byorushengo anatekeleza majukumu
yake ipasavyo. Ametoa agizo hilo baada ya wananchi kudai Ofisa huyo
ameshindwa kufanya kazi na kumuomba Waziri Mkuu aondoke naye.
Alisema
Bw. Byorushengo anatakiwa kuhakikisha halmashauri hiyo inapima viwanja
vya kutosha na kutoa hati kwa wananchi ili waweze kupata maeneo ya
kujenga makazi na shughuli zingine za kijamii.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo
Bw. Byorushengo kuhakikisha halmashauri hiyo inaanza ujenzi wa hospitali
ya wilaya na ifikapo Aprili, 2017 awe amepewa taarifa za ulipofikia
ujenzi huo.Kwa upande wake Mkurugenzi huyo alisema tayari wapo katika
mchakato wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ambapo wametenga sh. milioni
800 za kuanzia.
Akizungumzia
kuhusu mgogoro wa ardhi kati ya vijiji vya Tarafa ya Loliondo na
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Waziri Mkuu alitoa muda wa siku 30 kwa
uongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA) wawe
wamekamilisha uhakiki wa mpaka huo.
Naye
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro
Mheshimiwa William Ole Nasha alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia kutatua
mgogoro huo wa ardhi kwa kuwa ni wa muda mrefu na unakwamisha shughuli
za maendeleo.
Awali,
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo alisema Wilaya ya Ngorongoro
inachangamoto nyingi ikiwemo ya ardhi na sasa kuna mgogoro kati ya
Kampuni ya Thomson Safari na wananchi ambao wanadai kuwa ardhi hiyo
ilichukuliwa kinyemela na mwekezaji huyo bila ya wao kushirikishwa.
Alisema
baada ya ziara ya Waziri Mkuu kumalizika mkoani hapa atarudi wilayani
Ngorongoro kwa ajili ya kutatua kero mbalimbali ikiwemo ya ardhi na
matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na wawekezaji ambazo matumizi yake
hayajulikani.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Saturday, December 17, 2016
Taarifa ya Bodi ya Mikopo kwa wadaiwa sugu kuhusu mwisho wa kulipa kwa hiari
Hatua ya Bodi inafuatia mwitikio chanya kutoka kwa wadaiwa ndani ya siku 30 za awali ambazo zinakamilika leo Desemba 14, 2016.
Akitoa
taarifa ya kuongezwa kwa muda; Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi, Abdul_Razaq
Badru amesema kuwa wadau wameomba kuongezewa muda kutokana na baadhi
yao kukabiliana na changamoto za majukumu ya kazi na hivyo kushindwa
kujitokeza ndani ya siku 30 zilizokuwa zimetangazwa awali.
Katika
hatua nyingine, Bw. Badru amesema kuwa ndani ya siku za nyongeza Ofisi
za Bodi ya Mikopo zilizopo Mwenge, jijini Dar es Salaam zitaendelea kuwa
wazi kwa siku za Jumamosi, Disemba 17, 2016 na Jumapili, Disemba 18,
2016 kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri ili kutoa fursa
muhimu kwa wadaiwa wote wa mikopo ya elimu ya juu ambao hawajaanza
kurejesha mikopo yao kupata taarifa kuhusu madeni yao na kulipa.
Ili
kuharakisha utoaji wa muhtasari wa deni la mdaiwa; mhusika aje na
Majina yake kamili, Chuo alichosoma, Mwaka wa kuanza na wa kuhitimu,
anuani yake ya barua pepe (email), nambari ya simu ya kiganjani, mwajiri
wake na Check Number yake iwapo ameajiriwa serikalini.
‘Kuwa Mzalendo, Rejesha Mkopo wa Elimu ya Juu’
Kwa mawasiliano zaidi piga 0763 459165 au 0767 513208
Imetolewa na:
MKURUGENZI MTENDAJI
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
14/12/2016
Saturday, December 17, 2016
Serikali Yakanusha Kuwepo Kwa Ugonjwa wa ZIKA Nchini
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema hakuna uthibitisho wa kuwepo kwa ugonjwa wa Zika nchini.
Imeeleza kuwa utafiti uliofanyika ni wa kuangalia ubora wa kipimo cha ugonjwa huo.
Ufafanuzi
wa Wizara hiyo umekuja siku moja baada ya Taasisi ya Utafiti wa
Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kutoa ripoti ya utafiti uliofanywa na
taasisi hiyo kwa kushirikia na Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Bugando,
inayoeleza kuwepo wa maambukizi ya virusi vya Zika katika jamii ya
Watanzania.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
alitoa ufafanuzi huo kwa waandishi wa habari jana, ambapo alisema
wananchi wanapaswa kuondoa hofu kwa kuwa ugonjwa huo haujaingia nchini.
“Napenda
kuwatoa hofu wananchi kwa sasa haijathibitishwa kuwepo kwa ugonjwa wa
Zika nchini…wao walifanya utafiti nchini wa kuchunguza ubora wa kipimo
cha kupima magonjwa ya Zika na Chikungunya, hawakupima kama zika ipo
nchini au hakuna,” alisema Waziri Ummy.
Alisema wizara yake itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali, kutafiti ili kubaini kama ugonjwa wa Zika upo nchini au la.
Wizara hiyo pia imeshaanda mkakati wa Zika nchini, unaoelekeza kufuatilia ugonjwa huo.
Mganga
Mkuu wa Serikali, Mohammed Kambi alisema, NIMR walichokifanya ni
kufanya utafiti wa kutathmini ufanisi na ubora wa kipimo, ambacho
kinaweza kuja kutafiti magonjwa ya zika na mengine na kwamba kiutaratibu
hizo ni hatua za awali.
Alisema,
taarifa hiyo ya NIMR itafanyiwa tathmini ya kisanyasi ili wanasayansi
wajiridhishe kama ilifuata taratibu zote na matokeo hayo yanaweza
kuendelezwa mbele zaidi na baadae kuweka mikakati ya kuzidi kuthibisha
uwepo wa ugonjwa huo.
“Tuna
taratibu hizo za upande wa kitaalamu lakini kuna taratibu katika kutoa
tamko, kuhusu uwepo wa ugonjwa kama huu kwasababu ni aina ya uginjwa
unaotakiwa uripotiwe kimataifa…inabidi taarifa ije rasmi katika wizara,
kuna mganga mkuu na Shirika la Afya tuangalie hizo na tukijidhihirisha
taarifa rasmi inatolewa na mratibu wa magonjwa hayo,” alisema Dk
Mohammed.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NIMR, DK Mwele Malecela alisema
taarifa aliyoitoa juzi, ilikuwa ni matokeo ya utafiti wa kubainisha
uwezo wa kipimo hicho katika kuanisha virusi vya Zika, Dengue na
Chikungunya na matokeo ya awali yalionesha uwepo wa virusi vya Zika.
Alisema pamoja na matokeo hayo, hawakuona dalili wala madhara yoyote yanayosababishwa na Zika ikiwemo Kichwa kidogo na mengine.
“Hili
suala ni kwamba lilikuwa ni suala la kuainisha na katika uanishaji huo
tukajikuta tumeona virusi hivyo, lakini hiyo haimanishi kuna
uthibitishio, naomba nisisitize uthibitisho wa ugonjwa unatolewa na
wizara ya afya kwa kufuata uatartibu maalumu uliowekwa,” alisema.
Alisema
kuwa wataendelea kufanya utafiti hasa katika kuangalia magonjwa ya
Zika, Dengue na Chikungunya na kutoa matokeo kwa kile watakachokipata
katika utafiti huo.
Juzi
NIMR ilitoa matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi hiyo pamoja na
Chuo Kikuu cha Katoliki cha Bugando na utafiti kuanisha uwepo wa
maambukizi ya virusi vya zika katika jamii ya Watanzania na kuangalia
adhati ya maambukizi katika kusababisha watoto wanaozaliwa na ulemavu.
Sampuli
za damu kutoka kwa watu 533 zilipimwa. Kati yao, watoto wachanga 80
walizaliwa na ulemavu wa viungo mbalimbali. Kati ya waliopimwa 533, 83
(15.6%) waligundulika kuwa wameambukizwa virusi vya Zika.
Kati
ya wale watoto wachanga 80 waliozaliwa na ulemavu, 43.8% walikuwa
wameambukizwa virusi vya Zika, utafiti unaendelea kujua ukubwa wa tatizo
hili.
Saturday, December 17, 2016
Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumamosi ya Disemba 17
Jumamosi, 17 Desemba 2016
KUELEKEA MCHEZO WA AFRICAN LYON NA AZAM FC
Azam FC itaanza ngwe hiyo ikiwa na nguvu mpya kabisa baada ya kufanya usajili mzuri kwenye dirisha dogo la usajili, kwa kuongeza sura mpya tano pamoja na kumrejesha winga wake, Enock Atta Agyei, aliyekuwa kwa mkopo Medeama ya Ghana ilipomsajili, na sasa ataanza kuonekana katika mechi za ligi mara baada ya kutimiza miaka 18 Januari 5 mwakani.
Wachezaji wapya watano waliosajiliwa na Azam FC kwenye dirisha dogo ni beki Yakubu Mohammed (Aduana Stars, Ghana), kiungo mkabaji raia wa Cameroon, Stephan Kingue Mpondo (Coton Sports, Cameroon), winga Joseph Mahundi aliyerejea nyumbani (Mbeya City, huru) na washambuliaji Samuel Afful (Sekondi Hasaacas, Ghana), Yahaya Mohammed (Aduana Stars, Ghana).
Kikosi cha Azam FC kilichomaliza mzunguko wa kwanza wa ligi kikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 25 tofauti ya pointi 10 dhidi ya vinara Simba (35), kimeonekana kurejea na ari ya juu na morali kubwa kuelekea mzunguko wa pili kutokana na kiwango bora na hali ya kupambana wanayoonyesha kwenye maandalizi mazoezini.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, alisema wamejiandaa vema kuelekea mchezo huo pamoja na mzunguko wa pili wa ligi kiujumla kutokana na nguvu mpya walizoziongeza kikosini.
“Kiufupi raundi ya pili tumejiandaa na timu inanguvu mpya ya wachezaji tuliowasajili ambao hawakuwepo raundi ya kwanza hata mazoezi jinsi yanavyoendelea na jinsi wachezaji wanavyoonekana tunaamini kwa raundi ya pili tutaanza katika mazingira mazuri kuliko ambavyo tulikuwa tukifanya mzunguko wa kwanza,” alisema.
Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, alisema kuwa wanaingia kwenye raundi ya pili wakijua kuwa kutakuwa na ushindani mkubwa, lakini amekipanga kikosi chake kufanya vizuri huku akiwaambia mashabiki wa Azam FC waendelee kuisapoti timu hiyo.
“Mashabiki waendelee kutusapoti tunajua kwa namna tulivyokuwa tukicehza mzunguko wa kwanza ilikuwa ni ngumu kwao, lakini si kwa wao tu bali ilikuwa kwa watu wote, kwa kile ambacho naweza kuwaambia wajaribu kutuvumilia, mpira tutakaokuwa tunacheza na matokeo tutakayokuwa tunayapata mzunguko wa pili, wenyewe watakuwa wakiyapenda na hawatajutia kabisa kuchagua na kuisapoti Azam FC,” alimalizia.
Rekodi zao (Head To Head)
Agosti 21 mwaka huu, timu hizo zilikutana katika mchezo wa raundi ya kwanza, uliokuwa ni wa tano kihistoria kukutana kwenye ligi, ambapo uliisha kwa matokeo ya sare ya bao 1-1, Lyon ikitangulia kufunga kupitia kwa Hood Mayanja kwa mpira wa kona wa moja kwa moja kabla ya nahodha John Bocco ‘Adebayor’, kufunga bao zuri la kusawazisha mwishoni mwa mtanange huo.
Mpaka sasa katika mechi hizo tano walizokutana, Azam FC imeshinda mara tatu, Lyon mara moja huku mchezo mmoja wakienda sare.
Katika mechi zote hizo, Azam FC ndio iliyofunga mabao mengi zaidi ikitupia saba katika lango la wapinzani wao hao, huku Lyon yenyewe ikitingisha nyavu za matajiri hao mara nne tu.
HOFFENHEIM NA BORUSSIA DORTMUND ZATOSHANA NGUVU BUNDESLIGA
Timu ya Hoffenheim na Borussia
Dortmund zimegawana pointi katika mchezo mzuri wa Bundesliga
ulioishia kwa sare ya magoli 2-2 jana usiku.
Katika mchezo huo wenyeji Hoffenheim
walifunga goli la kwanza ndani ya dakika mbili kupitia kwa Mark Uth,
hata hivyo goli hilo lilisawazishwa na Mario Gotze.
Sandro Wagner aliongeza goli la pili
la Hoffenheim, lakini mshambuliaji nyota wa Dortmund- Pierre-Emerick
Aubameyang akasawazisha goli hilo.
Sandro Wanger akiwa ameupiga mpira uliomshinda kipa Roman wa Dortmund
Osumane Dembele akiwa amebebwa kwenye machela baada ya kuumia huku Aubameyang akiangalia
KATIBU TAWALA MKOANI MARA AHITIMISHA MAFUNZO KWA WADAU WA FILAMU MKOANI HUMO
Katibu
Tawala mkoa wa Mara, Adoh Mapunda (katikati) akizungumza hii leo kwenye
kilele cha mafunzo ya siku tatu kwa wadau wa filamu mkoani humo. Mafunzo
hayo yalianza juzi Disemba 14,2016 kwenye ukumbi wa shule ya Sekondari
Mara Mjini Msoma.
Yaliandaliwa na Bodi ya Filamu nchini kwa lengo la kuwajengea welezi wanatasinia wa filamu ili kuzalisha kazi zenye ubora na hivyo kukidhi ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi ambapo zaidi ya washiri 200 walionufaika na mafunzo hayo wamepatiwa vyeti. Tayari mafunzo ya aina hiyo yamefanyika mikoa ya Morogoro na Mwanza na yataendelea katika mikoa mingine. #BMGHabari Wanatasnia wa filamu mkoani Mara wakimsikiliza Katibu Tawala mkoani humo, Adoh Mapunda, wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kwa wanatasnia hao. Ameahidi kutoa fulana (Tshirt) 250 kwa ajili ya wanatasnia wa filamu mkoani Mara waliohudhuria mafunzo hayo ambapo zitawasaidia hususani kuwa na sare ya aina moja wakikutana kwa pamoja Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi.Nuru Millao, amesema sekta ya filamu ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wanatasnia wake na taifa kwa ujumla hivyo Bodi za filamu mikoani zihakikishe zinasimamia maendeleo ya tasnia hiyo. Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu nchini, Bi.Joyce Fisso, amebainisha kwamba wadau wa filamu wakiwemo watayarishaji, waongozaji, wahariri pamoja na waigizaji wamefundishwa vyema mafunzo hayo ili kuzalisha kazi bora. Mgeni rasmi, Katibu Tawala mkoani Mara, Adoh Mapunda (wa pili kulia), akipokea cheti cha utambuzi kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi.Nuru Millao
MAJALIWA AANZA ZIARA WILAYANI ARUMERU NA KUZUNGUMZA NA WATUMISHI
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na watumishi wa serikali na Halmashauri ya wilaya ya
Arumeru kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Arusha Desemba 17,
2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya watumishi wa halmashauri
ya wilaya ya Arumeru wakimsikiliza waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya
Arusha, Desemba 16, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipokea taarifa ya maendeleo ya wilaya ya Arumeru baada ya kusomewa
taarifa hiyo na Mkuu wa wilaya hiyo, Alexander Mnyeti kwenye
ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Arusha Desemba 17, 2016. (Picha
na Ofisi ya Wairi Mkuu)
:
UNHCR yasema watu wote lazima waondolewe Aleppo
habari za leo hizi hapa
Reviewed by RICH VOICE
on
Desemba 17, 2016
Rating:
Hakuna maoni