habari za jumanne hii
Tuesday, December 20, 2016
Taasisi zinazohamasisha ushoga kufutwa
WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ametaka apewe taarifa kuhusu
taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) wanaohamasisha au
kutangaza ndoa za jinsia moja nchini ili azifutie usajili mara moja.
Aidha
ametaka kutajwa kwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo ili
wachukuliwe hatua za kisheria kwa kujihusisha na vitendo hivyo ambavyo
vinapigwa vita dunia nzima.
Nchemba
aliyasema hayo jana mjini Kibaha alipokuwa akizungumza na taasisi za
Kijeshi za mkoa huo zikiwemo Uhamiaji, Polisi, Magereza na Zimamoto juu
ya kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Alisema
kuwa taasisi hizo hazifai kwani zinafanya kazi ya laana ambayo ni
kinyume cha maadili ya Kitanzania na hazistahili kuendelea kufanya kazi
kwa upotoshaji huo.
“Leteni
majina ya taasisi hizo ili tuzifute kwani hazistahili kuendelea kufanya
jambo hilo ambalo ni laana na halipaswi kufumbiwa macho ndani ya
jamii,” alisema Nchemba.
Kamanda
wa polisi mkoani Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa jeshi hilo
linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na upungufu wa
vitendea kazi, ikiwa ni pamoja na magari.
Mushongi
alisema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto hizo wamekuwa
wakikabiliana na uhalifu kwenye mkoa huo ambao umekuwa kimbilio la
wahalifu kutoka mikoa jirani ya Dar es Salaam.
Tuesday, December 20, 2016
Benki ya AfDB yaikopesha Tanzania Bilioni 360 kwa ajili ya bajeti ya 2016/2017
Na Benny Mwaipaja-WFM, Dar es salaam
Benki
ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, imeipatia Tanzania mkopo wenye masharti
nafuu wa dola Milioni 164, karibu Shilingi Bilioni 360, kwaajili ya
kuchangia Bajeti kuu ya Serikali katika kipindi cha Mwaka wa Fedha
2016/2017 pamoja na kuongeza mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo
nchini-TADB.
Mikataba
miwili imesainiwa jana Jijini Dar es salaam kati ya Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James kwa niaba ya Serikali na
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayeondoka Dkt. Tonia
Kandielo.
Mkataba
wa kwanza uliosainiwa ni kwa ajili ya kutunisha Mfuko Mkuu wa Serikali
ambapo Benki hiyo imetoa dola za kimarekani milioni 70 sawa na tsh 154
bilioni ambazo zitaelekezwa kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa Shirika
la Ugavi wa Umeme nchini-TANESCO.
Mkataba
wa pili ni kwaajili ya kuongezea mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo
nchini-TADB wenye thamani ya dola Milioni 94 sawa na shilingi Bilioni
204 kwa ajili ya kuiongezea uwezo Benki hiyo kutoa mikopo yenye riba
nafuu kwa wakulima ili kuongeza mnyonyoro wa thamani kuanzia uzalishaji,
uongezaji thamani na upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya
wakulima.
Uhai
wa mikopo yote miwili utakuwa ni miaka 40 ambapo serikali itaanza
kuilipa baada ya miaka kumi tangu kutolewa kwake, huku riba yake ikiwa
chini ya asilimia 1.
Akizungumza
baada ya kusainiwa kwa mkopo huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James, amesema mkopo huo umekuja wakati muafaka na
utasaidia kukuza na kuimarisha TANESCO na kuendeleza kilimo nchini.
“Tanzania
ni nchi iliyonufaika zaidi na mikopo yenye masharti nafuu kutoka Benki
ya Maendeleo ya Afrika-AFDB ikilinganishwa na nchi nyingine yoyote
iliyoko katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika,” alisema Bw. James.
Kwa
upande wake, Mwakilishi Mkazi wa AFDB anayeondoka Dkt. Tonia Kandielo
amesema kuwa hadi sasa Benki yake imeipatia Tanzania mkopo wenye thamani
ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 2, ambazo zimewekezwa kwenye
miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji,
nishati ya umeme, elimu na kilimo.
“Ninaamini
kuwa hatua ya kuongeza mtaji katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo-TADB
itachochea maendeleo ya kilimo nchini, na tunaahidi kuwa tutaendelea
kuiwezesha zaidi siku zijazo,” alisema Dkt. Kandielo.
Kuhusu
Sekta ya Nishati, Dkt. Kandielo amesema kuwa Benki yake imeona umuhimu
wa kuliwezesha shirika hilo ili liweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi
ili kuchochea uchumi wa Taifa.
“Mikopo
hii inahusiana na vipaumbele tulivyoviweka kama Benki ambavyo viko
katika malengo matano ambapo tunataka kuwekeza katika sekta ya nishati,
uzalishaji wa chakula, kuendeleza viwanda, kuiunganisha Afrika na
kuboresha maisha ya waafrika kwa ujumla,” aliongeza Dkt. Kandielo
Wakati
huo huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amemuaga rasmi
Dkt. Tonio Kandielo ambaye amehamishiwa nchini Afrika Kusini kuwa
Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo atakaye simamia Kanda ya Kusini mwa
Afrika.
Dkt.
Mpango, amesifu jitihada kubwa zilizofanywa na mwana mama huyo katika
kipindi cha miaka 6 aliyokuwepo hapa nchini ambapo ameweza kusimamia
vizuri maslahi ya Tanzania katika Benki hiyo.
Amesema
kuwa katika kipindi hicho Tanzania imeshuhudia maendeleo makubwa katika
sekta za ujenzi wa miundombinu ya barabara, kilimo, maji na umeme,
ambapo benki hiyo ilihakikisha kuwa miradi inatekelezwa kwa viwango
vinavyotakiwa.
Amemwomba
Mkurugenzi Mkuu huyo kuwezesha upatikanaji wa fedha kwaajili ya ujenzi
wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard gauge) inayohitaji
fedha nyingi, kusimamia utekelezaji wa mradi wa umeme wa kikanda
unaoanzia nchini Zambia, uboreshaji wa Bandari ya Itungi na Mbambabay.
Akijibu
hoja za Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Dkt. Tonia
Kandielo amesema kuwa anaamini mrithi wake ataendeleza mazuri
aliyoyafanya na kwamba yeye binafsi atahakikisha anafuatilia kwa karibu
miradi ambayo mikataba yake imesainiwa katika nyanja za maboresho ya
sekta ya umeme na kilimo.
Tuesday, December 20, 2016
Kiwango cha Pesa Kesi za Mafisadi Kushushwa Chini ili Kuwabana Wengi
WAZIRI
wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema serikali inatarajia
kujadili kushusha kiwango cha fedha kinachohusika katika makosa ya
rushwa na uhujumu uchumi kwenye mahakama ya mafisadi ili kukomesha
vitendo vya rushwa.
Mwakyembe alitoa kauli hiyo jana mara baada ya kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
“Nimeulizwa
sana na waandishi wa habari tangu Julai hadi sasa walitegemea kungekuwa
na kesi nyingi lakini kuna kesi moja katika Mahakama ya Mafisadi
tumekuja kubaini kwamba uchache wa kesi ndiyo mafanikio makubwa ya hatua
ya kisheria tuliyochukua,”amesema.
Aliongeza
kwa sasa waliozoea kupora mabilioni wamerudi nyuma ambapo wezi hao
wameonekana wakiiba fedha chini ya Sh bilioni moja iliyopo kisheria
hivyo wanategemea kujadili sheria hiyo ili iwalenge hata wanaochukua
kiasi kidogo.
“Sisi
kama serikali tukiona wizi sasa umenza kupungua na kuenea katika
viwango vya Sh milioni 400, 500, 700 tumeanza kujadiliana kuangalia
uwezekano wa kushusha kiwango cha fedha ili tuweze kukomesha kabisa
udokozi, ubadhilifu, wizi wa fedha au mali ya umma,”alisema.
Aidha
alifafanua uamuzi wa Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda kutafuta vijana
wanaojua sheria ili kusaidia wananchi kabla ya kwenda mahakamani ni
mzuri.
Aliongeza
kuwa tayari wamepeleka mswada wa msaada wa kisheria ambao utasaidia
wananchi hasa wa vijijini na wanawake ambao ndiyo wanaumizwa na desturi
zilizopitwa na muda ili kuwasaidia kupata haki na itakuwa na wasaidizi
wa kisheria nchi nzima wapatao 4,900.
Makonda
alisema wamejadili utoaji na upatikanaji wa haki kwa wakati kwani kuna
changamoto ya watu kuwa wengi na kuchelewa kupata haki zao.
Alisema
kwa kuona adha hiyo mkoa huo kwa kushirikiana na Wakuu wa wilaya
watajenga Mahakama za Mwanzo 20 ili kuongeza kasi za utoaji na
upatikanaji wa haki kwa wananchi endapo wanapopelekwa vituo vya polisi.
Tuesday, December 20, 2016
Polepole atangaza 'vua gamba' ya CCM kivingine
Mabadiliko
yaliyofanywa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yamekuja na mkakati
mpya wa kuwavua ‘gamba’ makada wa chama hicho wenye ukwasi waliovuna
kinyume na taratibu.
Katibu
wa Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey
Polepole amesema kuwa wako katika mkakati wa kukisafisha zaidi chama
hicho, akiwataka matajiri wenye ‘makandokando’ wajiondoe mapema.
“Kuwa
tajiri si dhambi na si kwamba CCM inafukuza matajiri, hapana. Tatizo
letu kama CCM katika mwelekeo mpya, mtazamo mpya na maegeuzi
yanayofanyika, hatuhitaji kuwa na aina ya matariji wanaojipatia utajiri
wao kwa hila, kwa rushwa na kwa dhuluma,” alisema Polepole katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini.
“Ukijiona
wewe ni tajiri na mikono yako ni michafu kwa maana ya kuwa na makando
ya kukosa uaminifu, hulipi kodi, ukae mbali na CCM,” aliongeza.
Alisema
watawachukulia hatua za kuwaondoa ndani ya chama hicho na kuwakabidhi
kwa vyombo vya dola ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Tangu alipochaguliwa, Polepole amekuwa akisisitiza kuwa chama hicho kitajikita katika msingi wake wa kuwatumikia wanyonge.
Mkakati
huo wa kuwang’oa matajiri wasiowaaminifu ndani ya chama hicho unafanana
na oparesheni iliyobatizwa jina la ‘Vua Gamba’ ndani ya chama hicho
miaka kadhaa iliyopita, iliyolenga kuwang’oa viongozi na vigogo ambao
walibainishwa kujipatia mali kinyume cha utaratibu na mafisadi.
Tuesday, December 20, 2016
Mahakama Kuu Yakubali Ombi la Godbless Lema Kuongezewa Muda wa Rufaa ya Dhamana Yake
Mahakama
Kuu Kanda ya Arusha, imelikubali ombi la Mbunge wa Arusha Mjini
Godbless Lema, la kuongezewa muda wa kuwasilisha Notisi ya nia ya
kukata rufaa ya dhamana yake.
Akitoa
uamuzi wake kuanzia saa 12:26 hadi saa saba mchana, Jaji Dk. Modesta
Opiyo wa Mahakama hiyo, alisema Mahakama hiyo imeruhusu maombi ya
kuwasilisha Notisi ya kuomba kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya
nia ya kukata rufaa ya dhamana yake.
Jaji
Opiyo amesema hoja za Upande wa serikali zilizowasilishwa na Wakili
Hashim Ngole za kudai waleta maombi hayo walikuwa wazembe na walichelewa
siku nne kuwasilisha Notisi baada ya rufaa yao kuondolewa na Jaji
Fatuma Masengi Desemba 2 hazina mashiko.
Alisema
kuondoa kesi mahakamani haimaanishi kuwanyima fursa ya kupigania nia ya
kukata rufaaa, bali milango inakuwa wazi haijafungwa.
Aidha
amesema siku nne zinazolalamikiwa kuwa walichelewa kutoa maombi hayo,
mahakama inaona hoja hizo hazina mashiko sababu siku mbili kati ya hizo
zilikuwa siku za mapumziko Jumamosi na Jumapili, hivyo walitumia siku
mbili kuandaa nyaraka na kuleta maombi hayo.
Pia alisema katika maombi hayo wametoa pia sababu za nia ya kutaka kukata rufaa na sababu hizo ziko wazi.
“Katika
hili hakuna uvunjifu wowote wa sheria uliofanywa na kutokana na hilo
Mahakama hii inatumia busara zake kuruhusu maombi haya ya kutoa Notisi
ya kuomba kuongezewa muda wa kukata rufaa juu ya dhamana yake Mbunge
huyu,” alisema Jaji Opiyo.
Amesema
Mahakama inatoa siku kumi pekee kuanzia uamuzi huo utolewa mleta maombi
(Lema) kuwasilisha Notisi yake ya kuomba kuongezewa muda wa kukata
rufaa hadi tarehe 30 shauri hili likakaposikilizwa tena.
Baada ya kutolewa kwa maamuzi hayo, tayari Wakili Sheck Mfinanga ameshakata Notisi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na kupokelewa.
Mfinganga amesema wanasubiri mahakama ili wapangiwe Jaji waendelee na kesi hiyo ya hatma ya dhamana ya Lema.
tuesday, December 20, 2016
Polisi yamnasa mtuhumiwa Sugu wa utapeli Tanzania
Jeshi
la Polisi nchini limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa utapeli
anayejulikana kwa jina la Wilfred Masawe (36) , mkazi wa Buza, Temeke
jijini Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi Mtuhumiwa huyo
alikuwa akitumia mbinu mbalimbali kutapeli zikiwemo kujitambulisha kama
kiongozi wa serikali kwa kutumia mtandao wa Whatsapp, huku akieleza
kuwa yupo nje ya nchi na kuna tatizo la msiba ambao umetokea nchini na
unamuhusu na hivyo alikua akitoa maelekezo kwa watendaji wa serikali
waweze kusaidia gharama za matibabu hospitalini, gharama za kusafirisha
mwili wa marehemu na gharama za mazishi.
Taarifa
hiyo pia imesema mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mbinu ya kujifanya
kiongozi mkubwa wa dini ya kikristo (Askofu) na kuwaambia waumini na
viongozi mbalimbali kuhusu maandalizi ya makongamano ya kidini kwa lengo
la kuwaomba michango kuweza kufanikisha makongamano hayo.
Baadhi
ya matukio aliyofanikiwa kutapeli ni pamoja na kuwatapeli viongozi wa
serikali, wafanyabiashara, mameneja na wakurugenzi wa taasisi za umma,
wanasiasa pamoja na waumini wa madhehebu ya dini.
Aidha,
matukio yote hayo alikuwa akiyafanya peke yake na alikuwa akiyaendesha
kwa mawasiliano ya njia ya ujumbe mfupi (SMS) bila kuzungumza kwa simu.
Jeshi la Polisi linakamilisha taratibu za kisheria ili mtuhumiwa huyo afikishwe mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
***
Tuesday, December 20, 2016
Mwenyekiti Wa CCM Taifa Rais Magufuli Akutana Na Viongozi Wapya Wa Chama Aliowateua Hivi Karibuni Na Dc Mteule Wa Ubungo
Mwenyekiti
wa CCM Taifa Rais Dkt John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkuu wa
Wilaya ya Ubungo Mteule Mhe. Kisare Makori akishuhudiwa na viongozi
wapya wa CCM aliowateua hivi karibuni. Kutoka kulia ni Katibu wa Itikadi
na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole, Katibu NEC Siasa na Uhusiano wa
Kimataifa Kanali Ngemela Eslom Lubinga na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara
Ndg. Rodrick Mpogolo walipoenda kujitambulisha Ikulu jijini Dar es
salaam leo Desemba 20, 2016.
Mwenyekiti
wa CCM Taifa Rais Dkt John Pombe Magufuli akiwa na Mkuu wa Wilaya ya
Ubungo Mteule Mhe. Kisare Makori (kushoto) pamoja na viongozi wapya wa
CCM aliowateua hivi karibuni. Kutoka kulia ni Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM Humphrey Polepole, Katibu NEC Siasa na Uhusiano wa
Kimataifa Kanali Ngemela Eslom Lubinga na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara
Ndg. Rodrick Mpogolo walipoenda kujitambulisha Ikulu jijini Dar es
salaam leo Desemba 20, 2016.
Mkuu
wa Wilaya ya Ubungo Mteule Mhe. Kisare Makori (kushoto) akibadilishana
mawasiliano na na viongozi wapya wa CCM walioteuliwa hivi karibuni.
Kutoka kulia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole,
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Ndg. Rodrick Mpogolo na Katibu NEC Siasa
na Uhusiano wa Kimataifa Kanali Ngemela Eslom Lubinga walipoenda
kujitambulisha kwa Mwenyekiti wa CCM Rais Dkt John Pombe Magufuli Ikulu
jijini Dar es salaam leo Desemba 20, 2016. PICHA NA IKULU
Tuesday, December 20, 2016
Serikali Haijazuia Watumishi Wa Umma Kukopa Benki
Kumekuwa
na taarifa inasambazwa katika mitandao ya kijamii, makundi ya
‘WhatsApp’, ‘Facebook’ na majukwaa mbalimbali ikieleza kuwa Serikali
imepiga marufuku watumishi wa umma kukopa Benki,SACCOS,VICOBA na Taasisi
mbalimbali za kifedha.
Taarifa
iliyotolewa leo tarehe 20 Desemba 2016 na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali imeeleza kuwa taarifa inayosambazwa, ambayo imetafsiri
mawasiliano ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni ya kupotosha,
hivyo watumishi wote wa umma wanaombwa kuipuuza.
Vilevile
watumishi wa umma wametakiwa kuzingatia kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali HAINA mamlaka ya kuzuia wala kuruhusu mtumishi yeyote wa
Serikali kukopa au kutokopa katika Taasisi yoyote ya Fedha nchini.
Watumishi
wa umma pia wamekumbushwa kuwa mikopo yote ya watumishi wa umma katika
Taasisi za Fedha hutolewa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu
zilizopo ili mradi mtumishi awe ametimiza vigezo.
Aidha,
watumishi wa umma wameaswa kuacha tabia ya kusambaza taarifa zisizo za
kweli na ambazo zina mamlaka husika ya kuzitoa ikiwa ni pamoja na
kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
***
Tuesday, December 20, 2016
Ajali yaua Watu Wanne wakiwemo Polisi Wawili
Watu
wanne wakiwamo polisi wawili, wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa
wakisafiria kuacha njia na kupindua katika kijiji cha Seruka kata ya
Chipogoro tarafa ya Rudi wilayani Mpwapwa mkoa wa Dodoma.
Ajali
hiyo ilitokea Desemba 19, mwaka huu, saa 11:30 jioni katika kijiji
hicho baada ya gari walilokuwa wakisafiria T517 CDL Toyota Alphat katika
barabara kuu ya Dodoma- Iringa, kuacha njia na kupinduka na kusababisha
vifo vya watu wanne na majeruhi tisa.
Kaimu
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ernest Kimola, amesema gari hiyo
iliyokuwa ikiendeshwa na Aggrey Lucas, baada ya kufika katika kijiji
hicho, liliacha njia na kupinduka na kusababisha vifo vya askari
Konstebo Mahende na Konstebo Sasi Mwita ambaye ni askari mkoa wa Songwe.
Kamanda Kimola amewataja wengine waliofariki katika ajali hiyo ni mke wa Konstebo Mwita, Pendo Mwita na Emaculata Nyangi.
Amewataja
majeruhi wa ajali hiyo ni Neema Mwita (8), Jenifa Mwita (4), Nyangi
Wambura (23), Konstebo Nashon (23) ambaye ni polisi kituo cha Tunduma na
Baraka Chacha (9).
Wengine
ni Juli Mwita (6), Pc Enock ambaye ni mmiliki wa gari lililopata ajali,
Makongoro Charles na Elizabeth Cosmas ambao wote wamelazwa katika
hospitali ya mkoa wa Dodoma.
Aidha,
kamanda Kimola amesema miili ya marehemu hao waliofariki katika ajali
hiyo, imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali
ya mkoa wa Dodoma.
habari za jumanne hii
Reviewed by RICH VOICE
on
Desemba 21, 2016
Rating:
Hakuna maoni