BEKI AZAM FC KUPELEKWA SAUZI KWA MATIBABU
BEKI wa kati wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Daniel Amoah, anatarajia kwenda jijini Cape Town, Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu ya goti Jumatatu ijayo.
Amoah ameshindwa kupona majeraha hayo tokea ayapate Desemba 19, mwaka jana, wakati Azam FC ikicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Polisi Tanzania na kuichapa mabao 3-1.
Februari 7 alirejea tena uwanjani na kucheza mechi dhidi ya Simba, Azam FC ikipoteza kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, ambapo alijikuta akijitonesha tena hali iliyomfanya kukaa nje ya dimba hadi sasa.
Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, amesema kuwa beki huyo ataenda kutibiwa katika Hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo nchini humo na akiangaliwa kwa undani tatizo lake kwa muda wa siku nne.
“Daniel Amoah analalamika au ana tatizo la maumivu makali katikati ya goti kwa hiyo timu ya Azam inampeleka Afrika Kusini kwa matibabu na uchunguzi zaidi na atakwenda Cape Town Jumatatu ijayo katika Hospitali ya Vincent Pallotti kuonana na Daktari bingwa wa mifupa Dr. Nickolas na atakaa huko kwa muda wa siku nne na itategemeana kama tatizo litakuwa ni kubwa basi ataongezewa muda wa kukaa huko,” alisema.
Beki huyo wa zamani wa Medeama ya Ghana aliyesajiliwa na Azam FC msimu uliopita, anakuwa mchezaji wa nne wa timu hiyo msimu huu kupelekwa Afrika Kusini kwa matibabu, awali mwaka jana walipelekwa Josepha Kimwaga, Shaaban Idd kufanyiwa upasuaji kabla ya wiki nne zilizopita nahodha Himid Mao ‘Ninja’ naye kupelekwa kwa uchunguzi wa goti lake na sasa akiwa fiti kabisa.
BEKI AZAM FC KUPELEKWA SAUZI KWA MATIBABU
Reviewed by RICH VOICE
on
Machi 21, 2018
Rating:
Hakuna maoni