Rais Magufuli Kawapa Siku 7 Mawaziri Wake
Rais
Dkt. John Magufuli ametoa wiki moja kwa Mawaziri kufanyia kazi
changamoto na maoni yaliyotolewa na wafanyabiashara katika mkutano wa 11
wa Baraza la Taifa la Biashara ili kuweza kutatua kero zao.
Amewataka
Mawaziri kuandika maelezo yenye majibu ya changamoto na maoni hayo na
kuwasilisha kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili serikali ifanyie kazi
na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini.
Rais
Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa baraza hilo ametoa maagizo hayo jana
wakati akihitimisha mkutano huo ambao wafanyabiashara na wawekezaji
kutoka sekta mbalimbali walipata nafasi ya kueleza maendeleo ya shughuli
zao, changamoto zinazowakabili na mapendekezo ya kuimarisha biashara na
uwekezaji hapa nchini.
Miongoni
mwa changamoto zilizoweza kuwasilishwa katika mkutano huo ni pamoja na
utozaji wa kodi unaoathiri biashara na uwekezaji, urasimu wa taasisi za
serikali, udhibiti wa bidhaa za kutoka nje ya nchi zinazoathiri
uzalishaji wa bidhaa za ndani, uwepo wa sheria na kanuni kandamizi kwa
biashara na uwekezaji na utendaji usioridhisha kwa baadhi ya maafisa wa
Serikali.
“Nataka
kuwaambia kwa dhati kabisa, serikali ninayoiongoza haiwachukii
wafanyabiashara, inawapenda na itawaunga mkono, kama nilivyowaambia huko
nyuma huu ndio wakati wenu wa kufanya biashara, fanyeni biashara zenu
na lipeni kodi, hizi changamoto tumezipokea na tutazifanyia kazi”,
alisema Dkt. Magufuli.
Kwa
upande mwingine, Rais Magufuli ametoa wito kwa wafanyabiashara hao
kuhakikisha wanashiriki katika miradi mikubwa anayotekelezwa na serikali
ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge),
mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge),
mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima – Uganda hadi bandari
ya Tanga – Tanzania, na amewataka wafanyabiashara wanaofanya vitendo
vya udanganyifu katika kodi na uingizaji wa bidhaa wabadilike.
Rais Magufuli Kawapa Siku 7 Mawaziri Wake
Reviewed by RICH VOICE
on
Machi 20, 2018
Rating:
Hakuna maoni