Kamati ya Bunge yashindwa kumhoji Kubenea, alazwa kliniki ya Bunge
Kamati
ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, imeahirisha kumuhoji
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea kutokana na kufika mbele yake akiwa
mgonjwa.
Kubenea
amefika mbele ya kamati leo Jumatano saa nne asubuhi akiwa katika
baiskeli ya wagonjwa (Wheel chair) chini ya ulinzi wa askari wa Jeshi la
Polisi.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Kapteni mstaafu George Mkuchika amesema walikutana
kutokana na kupelekewa shauri na Spika la kumuita Kubenea akidaiwa
kudharau mamlaka ya Spika kwa kauli alizozitoa katika kanisa moja jijini
Dar es Salaam.
“Kamati
ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inakutana pale inapoletewa shauri
na Spika, tumeletwa mashauri ya Kubenea ya kudharau mamlaka ya Spika
kwa kauli ambazo amezitoa katika kanisa huko Dar es Salaam,” amekaririwa
Mkuchika katika taarifa iliyotolewa na Bunge.
Amesema utaratibu unamtaka mtu anayetakiwa kufika mbele ya kamati hiyo kupelekewa hati ya kuitwa na kwamba alishapelekewa.
Mkuchika
amesema Kubenea amepelekwa akiwa katika baiskeli ya wagonjwa na kuiomba
kamati impangie siku nyingine kwa hiyo wameridhia ombi lake.
“Kamati
baada ya kumsikiliza Kubenea imeridhia ombi lake la kumpangia tarehe
nyingine kwa kumpa muda wa kuangalia afya yake mpaka atakapopona,”
amesema.
Mkuchika aliagiza Kubenea apelekwe katika Zahanati ya Bunge ili apewe huduma ya kwanza.
Awali,
Kubenea baada ya kuhojiwa na kamati kama ataweza kuzungumza katika
kikao hicho aliiomba kamati kumpangia siku nyingine kwa kuwa asingeweza
kuzungumza kwa wakati huo kutokana na kuwa katika maumivu makali.
Septemba
12, Spika wa Bunge, Job Ndugai aliagiza mbunge huyo kufika mbele ya
kamati hiyo kuhojiwa kuhusu tuhuma alizozitoa wakati wa ibada Septemba
10 kwamba Spika alisema uongo bungeni wakati akitangaza idadi ya risasi
zilizopigwa kwenye gari la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Kamati ya Bunge yashindwa kumhoji Kubenea, alazwa kliniki ya Bunge
Reviewed by RICH VOICE
on
Septemba 20, 2017
Rating:
Hakuna maoni