Mahakama Yawapa Kinga Wabunge 19 wa CUF
Baada
ya wabunge wanane wa viti maalumu wa CUF, kuvuliwa uanachama wa chama
hicho na kisha kupoteza nyadhifa zao, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam imewapa kibali wabunge 19 wa majimbo wa chama hicho kuomba
kuwekewa kinga.
Mahakama
hiyo imetoa kibali hicho kwa wabunge hao baada ya kukubaliana na maombi
yao waliyofungua mahakamani hapo dhidi Bodi ya Wadhamini wa CUF,
mwenyekiti wa CUF na katibu mkuu wa chama hicho.
Katika
maombi hayo namba 69 ya mwaka 2017, wabunge hao wanaowakilishwa na
Wakili Mohamed Tibanyendela walikuwa wakiiomba mahakama iwaruhusu
kufungua maombi kuomba kinga ili wasiguswe kutokana na mgogoro wa
kiuongozi unaoendelea ndani ya chama hicho.
Wakiongozwa
na Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea, wabunge hao walifungua maombi
hayo ya kibali cha kuomba kinga Agosti 25 na yalisikilizwa upande mmoja
(waombaji pekee) Agosti 31 na kutolewa uamuzi huo juzi na Jaji Wilfred
Dyansobera.
Tibanyendela
alisema jana kwamba baada ya kupata kibali hicho, watafungua maombi
hayo mahakamani hapo baada ya kukamilisha taratibu zote.
“Ndio
nakamilishakamilisha hapa kuandaa maombi haya na baada ya hapo itabidi
kwanza wateja wangu wote wasaini. Kama unavyojua kwa sasa wote wako
Dodoma, bungeni, lakini tutafanya utaratibu ambao utawawezesha wote
kusaini kisha tutayapeleka mahakamani,” alisema.
Katika
maombi watakayofungua, wabunge hao wataomba kupewa kinga ili wasiguswe
kwa namna yoyote na wajibu maombi au watu wanaofanya kazi kwa maelekezo
yao, ili kutokuathiri haki na masilahi yao.
Pia,
wabunge hao wataiomba Mahakama iwalazimishe wajibu maombi hao kumaliza
tofauti zao kwa mujibu wa katiba ya chama na sheria za nchi.
Wabunge
hao wa majimbo wamestuka na kuchukua hatua hizo baada ya wenzao wanane
kupoteza nyadhifa zao kutokana na uamuzi wa chama hicho upande wa
Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa
kuwavua uanachama.
Chama
hicho kimekuwa katika mgogoro wa kiuongozi kwa muda mrefu tangu Profesa
Lipumba alipotangaza kujiuzulu mwaka 2015 na baadaye kubatilisha uamuzi
wake huo mwaka jana.
Kurejea
kwake kwa kuandika barua ya kutengua ile ya kujiuzulu, kulisabisha
kuibuka kwa makundi mawili ya wanachama wa chama hicho, moja likiongozwa
na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad linalompinga na jingine
linalomuunga mkono.
Katika
mwendelezo wa mgogoro huo, kambi inayoongozwa na Profesa Lipumba
ilitangaza kuwahoji na kuwachukulia hatua wanachama na viongozi
mbalimbali wakiwamo wabunge kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo kukihujumu
chama kwa kushirikiana na vyama vingine.
Kundi
la kwanza kuitwa kwa ajili ya kuhojiwa na Baraza Kuu la Uongozi ni
wabunge hao wa viti maalumu ambao wako kambi ya Maalim Seif.
Wabunge
hao wanane ni Severina Mwijage, Saumu Heri Sakala, Salma Mohamed
Mwassa, Riziki Shahari Ngwali, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji,
Hadija Salum Al-Qassmy na Halima Ali Mohamed ambao hata hivyo,
hawakuitikia wito huo na matokeo yake walivuliwa uanachama na kupoteza
ubunge.
Wabunge
19 wa majimbo ambao pia wako kambi ya Maalim Seif, kwa mujibu wa
taarifa hiyo lilikuwa ni kundi la pili kuitwa kuhojiwa na kisha
kufuatiwa na kundi la tatu ambalo ni viongozi wa ngazi za juu.
Mahakama Yawapa Kinga Wabunge 19 wa CUF
Reviewed by RICH VOICE
on
Septemba 06, 2017
Rating:
Hakuna maoni