Serikali Yaunda Kikosi Maalumu Kudhibiti Mashambilizi Ya Risasi Nchini
Wiki
moja baada ya kujeruhiwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), Tundu Lissu Serikali imeunda kikosi kazi kushughulikia
uvunjifu wa amani nchini.
Kikosi
hicho kinachoshirikisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama pia
kinashughulika na kukusanya silaha za kivita ambazo zimekuwa zikitumika.
Lissu
alijeruhiwa kwa risasi Alhamisi Septemba 7 nyumbani kwake Area D mjini
Dodoma na sasa anaendelea na matibabu jijini Nairobi, Kenya.
Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi amesema hayo
bungeni leo Alhamisi akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Chambani
(CUF), Yusuf Salim Hussein.
Mbunge
huyo amesema hana wasiwasi na uimara, uwezo na weledi wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kusimamia majukumu yake ndiyo maana
nje ya mipaka ya nchi ni salama lakini ana wasi wasi kuhusiana na hali
ya usalama nchini.
“Lakini
ndani ya nchi yetu hali si salama na mifano miwili ya juzi ya mbunge
(Lissu) na Meja Jenerali mstaafu Vincent Mritaba inadhihirisha kwamba
ndani ya nchi yetu tuna matatizo, je ni kwa nini Jeshi la Wananchi
lisishiriki kikamilifu kuondosha matumizi ya silaha na mauaji ya raia
wasio na hatia ndani ya nchi yetu?” alihoji mbunge huyo.
Amesema anavyoona yeye silaha za kivita zinamilikiwa na JWTZ na matumizi yake yanatakiwa yawe ya chombo hicho.
Mbunge
huyo alihoji ni kwa nini wasitumike askari maalumu kuhakikisha silaha
za kivita zinazotumika vibaya kuua raia zinakamatwa.
Waziri
Mwinyi akijibu swali hilo amesema ni dhahiri kwamba kazi ya JWTZ ni
ulinzi wa mipaka lakini pale linapohitajika au kuombwa kusaidia mamlaka
zingine za kiraia au vyombo vingine vya ulinzi na usalama huwa tayari
kufanya hivyo.
“Tunavyozungumza
ni kwamba, mamlaka hizo ambazo ni vyombo vingine vya ulinzi na usalama
vikihitaji msaada wa jeshi mara zote tunakuwa tayari kutoa msaada huo,
kwa hali ilivyo sasa imeundwa task force (kikosi kazi) inayojumuisha
vyombo vyote vya ulinzi na usalama ili kulifanyia kazi tatizo hili la
uvunjivu wa amani ndani ya nchi,” amesema.
Amesema
hana shaka na kazi hiyo imeanza, hivyo kuwahakikishia wananchi kuwa
jukumu hilo litafanywa vyema ili hali ya usalama iwepo ndani ya nchi.
Dk
Mwinyi amesema ni kweli silaha za kivita zinadhibitiwa na JWTZ na kwa
kutumia kikosi kazi hicho, watakusanya silaha hizo kutoka kwa raia au
watu wengine wote ambao wanamiliki silaha hizo ambazo kwa kawaida,
utaratibu na kisheria hawapaswi kuwa nazo.
Amesema zitakapopatikana silaha hizo zitarudishwa katika mamlaka zinazohusika.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Mkoani (CUF), Twahir Awesu Mohamed alihoji Serikali imejipangaje kuimarisha amani nchini.
Waziri
Mwinyi amesema JWTZ imejipanga kikamilifu kuhakikisha mipaka ya nchi
inalindwa muda wote dhidi ya adui yeyote atakayejitokeza kuivamia.
“Jeshi
letu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, limeimarisha
ulinzi katika maeneo ya mipaka yenye wakimbizi ,” amesema.
Amesema
hatua hiyo imesaidia kuzuia na kukabiliana na vitendo vya kihalifu
vinavyowezwa kusababishwa na wakimbizi katika mipaka na katika makambi.
Serikali Yaunda Kikosi Maalumu Kudhibiti Mashambilizi Ya Risasi Nchini
Reviewed by RICH VOICE
on
Septemba 14, 2017
Rating:
Hakuna maoni