Rais Magufuli aagiza ukuta mkubwa kujengwa migodi ya Tanzanite
Rais
John Magufuli ameagiza kujengwa uzio katika eneo linalozunguka machimbo
ya Tanzanite liliko Simanjiro ikiwa ni hatua yake ya kutaka kukabiliana
na utoroshwaji wa rasilimali hiyo.
Amelisisitiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuanza kazi hiyo haraka iwezekanavyo.
Rais
Magufuli ambaye yuko ziarani mkoani Manyara amesema vikosi vya ulinzi
na usalama vinapaswa kushirikiana kujenga ukuta huo ambao utaanzia eneo
la block A hadi D la machimbo hayo.
Baada
ya ujenzi huo kukamilika ametaka kufungwa mitambo maalumu ikiwamo
kamera zitakazokuwa na uwezo kutambua na kubaini matukio yoyote
yanayotendeka katika eneo hilo.
“Nataka
ukuta huu uanze mara moja tena JWTZ kupitia Suma JKT waanze kazi hii
mara moja na baada ya kukamilika eneo hili liwe na mlango mmoja tu ambao
utaweka mtambo wa ukaguzi... wewe ukiweka Tanzanite tumboni
tutakubaini, ukiweka kwenye kiatu uonekane pia,” amesema Rais Magufuli.
Amesema
lengo la Serikali kufanya hivyo ni kuhakikisha inapata sehemu ya mapato
yake na wawekezaji waondoke na haki yao bila kupunjwa upande wowote.
Amesema
hataki kuona rasilimali za Taifa zinatoroshwa kienyeji na kwenda
kuwafaidisha wajanja wachache walioko nje ya nchi hivyo ili kudhibiti
hali hiyo ameamua kuchukua hatua madhubuti.
“Hapa
adui yetu siyo CCM au Chadema ama mwingine yeyote, adui yetu ni yule
anayopora mali zetu, hatupaswi kugombana sisi wenyewe na kumuacha adui
yetu yuko pembeni, naomba tushikamane katika hili maana hii vita ya
uchumi siyo lelemama lazima tuwe wamoja,” amesema.
Pia,
amesema ndoto yake ni kuona soko la Tanzanite linakuwa Simanjiro ili
wafanyabiashara kutoka ng’ambo kama Marekani, India na Ulaya wanafika
kwenye eneo hilo kufanya biashara.
“Tunataka
soko la Tanzanite linakuwa hapa Simanjiro ili hawa wafanyabiashara
wafunge safari waje kununulia hapa na hiyo itakuwa na manufaa pia kwa
wafanyabiashara wa eneo hilo maana hata yule mchinja mbuzi ama mwenye
gesti atafaidika na ujio huo,” amesema.
Rais
Magufuli amesema hayo leo Jumatano wakati akizindua barabara ya kiwango
cha lami ya Mererani yenye urefu wa kilometa 26 ambayo imegharimu kiasi
cha Sh 32.5 bilioni. Rais ameahidi kuendelea na kipande kilichobakia
ili lami hiyo ifike makao makuu ya Mkoa wa Manyara ambayo ni Babati.
Rais Magufuli aagiza ukuta mkubwa kujengwa migodi ya Tanzanite
Reviewed by RICH VOICE
on
Septemba 20, 2017
Rating:
Hakuna maoni