Waziri wa Afya Atoa Ufafanuzi Mwingine Sakata la Tundu Lissu
Waziri Ummy Mwalimu amejibu tuhumu zinazotolewa na baadhi ya watu dhidi ya serikali baada ya kutaka kuombwa kugharamia matibabu ya Lissu, na kusema kwamba serikali imelazimika kufanya hivyo kwa sababu mgonjwa alijitoa kwenye utaratibu wa serikali.
Ummy Mwalimu ambaye ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ametoa maelezo hayo leo kwenye ukurasa wake wa twitter, na kusema kwamba serikali isingeweza kuingilia kati bila kuombwa na familia ya Tundu Lissu, kwani mgonjwa alishatolewa kwenye utaratibu wa serikali kwa kupelekwa Nairobi, na hiyo sio mara ya kwanza kwa serikali kufanya hivyo.
"Mgonjwa alitolewa kwenye utaratibu wa serikali alipopelekwa Nairobi, sasa gharama/tiba zaid yahitajika, serikali inaingiaje bila ridhaa ya familia? Na hii sio mara ya 1 kutokea. Mzee wetu S.Sitta (RIP), alikwenda matibabu London kwa utaratibu binafsi kisha alileta maombi serikali ishiriki", ameandika Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy Mwalimu ameendelea kwa kuandika akisema kwamba mgonjwa ni Mbunge anayehitaji matibabu zaidi, lakini kwa kuwa sasa hivi yupo nje ya utaratibu wa serikali, ili serikali iweze kushiriki ni lazima yawepo maombi ya kufanya hivyo.
Hapo juzi serikali ilitoa tamko ikisema kwamba watakubali kusimamia matibabu ya Tundu Lissu popote duniani iwapo familia yake itaomba kufanya hivyo, na sio vinginevyo, kitendo ambacho kimeibua sintofahamu nyingi kwa baadhi ya wananchi wakiilaumu serikali kwa kutojali matatizo ya Tundu Lissu.
Waziri wa Afya Atoa Ufafanuzi Mwingine Sakata la Tundu Lissu
Reviewed by RICH VOICE
on
Septemba 24, 2017
Rating:
Hakuna maoni